“Mr. Kaird, usiwe na wasiwasi, hata kama Regina ana koneksheni kubwa, lakini nikuhakikishie tutafanya kazi nzuri tuki…”
Zuberi alitaka kumfariji Kaird lakini kabla ya kumaliza sentensi yake, Kaird aliingilia;
“Haina haja, Mr. Zuberi, hatuna mpango tena wa kufanya kazi pamoja. Makubaliano yetu tuliokubaliana mwanzo nayafuta kuanzia sasa,” aliongea Kaird huku aking’ata meno kwa hasira.
“Nini! Kwanini unaenda kinyume na maneno yako?” Wote Hamisa na Zuberi walijikuta sura zikiwafubaa na kushindwa hata kujua nini waongee.
“Hatukusaini mkataba wowote baina yetu, haiwezi kuhesabika kama ahadi. Sitaki kushirikiana na nyie, sio kwasababu hamna vigezo bali sitaki kumkasirisha Bosi Leibsoni.” Mara baada ya kuongea hivyo haraka haraka alisogelea upande aliokuwepo Regina.
Akiwa na sura iliyojaa soni, alimsogelea Regina na kumuomba ushirikiano upya.
“Miss Regina, nitazingatia ombi lako kwa umakini, naona hali ya kampuni yako ni nzuri zaidi kwa sisi kushirikiana.”
Regina muda huo alikuwa bize kudili na watu waliokuwa wakimsalimia na wengi wao walikuwa ni mabosi wa makampuni makubwa. Mara baada ya kusikia kauli hiyo kutoka kwa Kaird, aliishia kukunja sura kidogo.
“Sorry, Mr. Kaird. I am no longer interested in cooperating with you guys,” aliongea akimaanisha havutiwi tena kushirikiana nao.
Ijapokuwa alitarajia jibu hilo, lakini bado alishikwa na mawazo. Mara baada ya Zuberi na Hamisa kuona hilo, walijikuta wakishikwa na hasira mno kiasi cha kutaka kutapika damu. Yaani Kaird alikuwa radhi kuachana nao na aende kuomba kwa Regina ambako alijua angekataliwa?
Walijihisi takataka muda huo; hakuamini kuungana kwake na Multimedia hakukuwa na ushawishi mkubwa kwa tajiri kama Kaird.
Kutokana na jambo hilo, Zuberi na mpenzi wake hawakuwa na hamu tena ya kuendelea kukaa katika sherehe hiyo, hivyo haraka haraka walitembea kinyonge, wasithubutu hata kumwangalia Regina usoni.
Ukweli ni kwamba Regina tokea mwanzo hakuwachukulia kama washindani. Malengo yake ilikuwa ni kudili na matajiri wakubwa wa biashara, na Brewer na Kaird ilikuwa ni mwanzo tu.
Henry na baadhi ya watu wachache waliokuwa wakimfahamu Hamza walisimama nae huku wakiongea.
“Sir, sio kwamba tunamsaidia Madam, ni kutokana na ushawishi wa Leibsoni ndiyo maana,” aliongea Henry huku akicheka.
“Na hili ni swala ambalo siwezi kuamua tu, mnaweza pia kujumuika na nyie. Nina uhakika mke wangu hawezi kukasirika,” aliongea Hamza akimwangalia mke wake aliyekuwa bize akiongea na wazungu.
Mpaka sherehe inakuja kutamatika, Regina alikuwa amepata mwaliko kutoka kwa zaidi ya makampuni ishirini na wote walitaka kushirikiana naye kibiashara.
Kama Henry na yeye angeonyesha kufahamiana na Regina, pengine mialiko ingekuwa mingi zaidi.
Mwanzoni Regina alitaka kujihusisha na kampuni ambazo alipendezwa kufanya nazo kazi, lakini mwishowe kampuni yake ni kama imegeuka na kuwa keki na kila mtu aliitaka.
Wakati wakiwa njiani kwenye gari kurudi hotelini, Regina alikuwa amefumba macho yake akionekana kupumzika, hakuongea neno lolote na Hamza.
Baada ya kufika hotelini, Regina alihisi kuchoka sana. Alikaa kitandani huku akivuta pumzi kwa nguvu. Kulikuwa na hali ya jasho kwenye paji la uso wake.
Hamza aliangalia mwonekano wa mwanamke huyo na pale pale alionekana kugundua, ijapokuwa Regina alionekana kutulia kidogo lakini kiuhalisia ilikuwa stress kuongea na watu wengi namna ile ambao hakuwa akiwajua.
Hamza aliishia kutoa tabasamu hafifu na kisha alikaa kitandani na kunyoosha mkono wake akitaka kumtuliza Regina, lakini mwanamke huyo alimkwepa kwa kusogea mbali.
“Wife, nini tatizo? Una hasira na mimi kwa kilichotokea? Haikuwa makusudi pale, sikujua yule Leibsoni angekuja kunitafuta, mimi mwenyewe hata sikuwahi kumfahamu. Si unaona Henry na wengine ambao nilifahamiana nao hawakuthubutu kukusogelea kwa sababu ya kuheshimu maamuzi yako,” Hamza aliona ajitetee na Regina aligeuza kichwa chake na kumwangalia.
“Nani kasema nimekasirika?”
“Kama sio hivyo…”
“Niambie, wewe ni nani kwanza?” aliongea Regina na kumfanya Hamza kushangaa kwani katika macho ya Regina ni kama vile ndio kwanza wanaanza kufahamiana.
“Nataka kujua Mameni ni nani, Vita Takatifu ni nini, kwa nini wanakuita Lucifer, na Prince mrithi wa utawala wa kuzimu ni jambo gani. Leo ni siku ya kuniambia, sidhani kama kuna haja ya kuendelea kunificha,” aliongea Regina kwa uzito, akimfanya Hamza kuvuta pumzi nyingi na kuzitoa.
“Mameni ni mshikaji wangu, zaidi ya ndugu, ni mfanyabiashara mkubwa wa kuuza na kusambaza silaha duniani. Ana mtandao mzuri wa usafirishaji, na kwa sababu Leibsoni pia ni mfanyabiashara, wamekuwa marafiki. Kuhusu mimi, niliwahi kuwa kiongozi wa juu wa jumii ya siri ya Inferno, inayojulikana pia kama Hellfire Club. Kutokana na nafasi yangu, nilipachikwa majina ya utani kama Selafi, Lucifer, mfalme wa kuzimu, na Prince. Kuhusu jina Lucifer, ni kutokana na chimbuko lenyewe la jumuia hii; ukifuatilia historia, utaelewa ninachomaanisha. Kuhusu Vita Takatifu, hiyo ni hadithi ndefu yenye mfululizo wa maswali mengi. Wife, nitamtafuta mtu atakayeandaa taarifa kwa mtiririko mzuri ili uelewe. Siwezi kuelezea yote usiku huu,” aliongea Hamza, akimfanya Regina kupatwa na mshtuko na moyo wake kuenda mbio baada ya kusikia hayo.
“Na vipi kuhusu jina la ‘Gwiji Mtaalamu wa Juu’? Kwa nini wanakuita hivyo?” aliuliza Regina.
“Hayo pia ni majina ya sifa walizonipa. Ukweli ni kwamba sijali sana; kama ningekuwa najali kuhusu majina na vyeo, nisingerudi Tanzania na kuwa msaidizi katika kampuni yako,” alijibu Hamza, na Regina alimwangalia huku akitabasamu kwa dhihaka.
Hamza alikuwa bado ni yuleyule. Ingawa kulikuwa na mambo ya kushangaza kuhusu maisha yake, lakini angalau alikuwa mkweli. Mara baada ya kufikiria kwa muda, uso wake ulitulia, kisha akavimbisha mashavu.
“Nilisema nitajitahidi mwenyewe kupata ubia wa kibiashara, lakini umeharibu kila kitu.”
“Wife! Ningejua vipi kama Leibsoni atakuja na kuvuruga kila kitu?” alijibu Hamza kwa kujitetea.
“Sijali, yote ni kwa sababu yako. Kwa macho yao, wanaona kama mimi ni mwanamke ninayefanikiwa kupitia uhusiano wetu. Hili linanikasirisha, sitaki tena kwenda na wewe kwenye hafla kama ile. Mimi ndio ninakulipa mshahara, lakini wanadhani unanisaidia,” aliongea Regina kwa hasira, kisha akaelekea mezani na kujimiminia glasi ya maji akanywa yote kutuliza hasira.Hamza hakujua acheke au alie; aliguna tu muda huo.
“Ni kweli kabisa. Mshahara wangu napata kutoka kwako, wao wanakusingizia tu. Na kuanzia sasa, nitawatangazia wasifanye biashara na wewe kwa kutanguliza jina langu,” aliongea Hamza huku akiongeza utani, jambo lililomfanya Regina kumwangalia kwa uzito.
“Lazima unanicheka moyoni, ukidhani siwezi kufanya lolote bila msaada wako, hasa ukizingatia namna Hamisa na Zuberi walivyokuwa wakinicheka mbele ya wale matajiri.”
“Hamna, wife, sijawahi kufikiria hivyo. Niliweza kuona jinsi ulivyomjibu Brewer pale. Ulikuwa na ujasiri, na nilifurahi sana kukuona vile,” aliongea Hamza.
“Kweli!” Aliuliza Regina kimashaka.
“Kweli kabisa, kama nakudanganya mke wangu, nipasuliwe na radi.” Ile anamaliza kuongea kauli hiyo tu, ngurumo nzito ilisikika nje kiasi cha kufanya jiji hilo la Paris kuwa kama vile anga lake linataka kudondoka.
Regina macho yalimtoka kutokana na tukio hilo. Upande wa Hamza alizubaa, na kama hakuamini, haraka sana alisimama na kwenda kuchungulia dirishani kwa kuvuta pazia, na hapo ndipo alipoweza kuona wingu zito likiwa limetanda angani. Ilikuwa ni usiku sana, na ilionyesha mvua muda wowote itaanza kunyesha.
Hamza aliishia kukuna kichwa chake kwa wasiwasi huku akilaani ngurumo hiyo, ijapokuwa mara nyingi mvua inayoambatana na ngurumo ilinyesha kipindi cha masika, lakini kulikuwa na dalili mvua hiyo itakuwa kubwa.
Hamza mara baada ya kugeuka aliweza kumuona Regina akimwangalia huku anamcheka. Mrembo huyo alionekana kufurahia kuumbuka kwake, lakini alifurahishwa na tabasamu lake.
“Wife, hii ngurumo haihusiani kabisa na kuapia kwangu, nazungumzia radi kama radi na sio ngurumo,” aliongea Hamza akijielezea.
“Huna haja ya kuongea, kwa sababu Mungu tayari ashanipatia jibu ninalotaka. Wewe endelea tu kunidharau, isitoshe ni kweli nakutegemea, na mpaka sasa mambo yamebadilika, hivyo siwezi kufanya chochote.”
Baada ya kuongea hivyo, alijilaza kitandani huku akijiwekea mto na na kufumba macho .
“Nimechoka, nataka kulala. Unaweza kwenda kuendelea kucheza huko nje mwenyewe.”
Hamza akiwa na tabasamu lililojaa uchungu alijirusha na yeye kitandani pembeni ya Regina.
“Mke wangu, usiwe hivyo basi. Wengine wanaweza kuona unanitegemea, lakini mimi najua ukweli unajitegemea mwenyewe. Usiwe na hasira basi.”
“Mimi sina hasira,” aliongea Regina huku akiwa amefumba macho yake.
“Mimi siamini kama huna hasira. Sikutegemea kabisa yule mshenzi Leibsoni angetokea namna ile.”
“Nishasema tayari sina hasira sawa. Kwanza sina haki ya kuwa na hasira kwa mtu kama wewe mwenye cheo cha Lucifer, mfalme kutoka kuzimu. Mfanyabiashara yoyote mdogo kama mimi siwezi kuzuia kufaidika kwa uwezo wako. Nikikukasirikia si nitaonekana kama mtu mwenye uwezo mdogo wa kufikiri?”
“Wife, usiendelee basi kuongea hivyo. Kadri ninavyokusikia ndivyo ninavyozidi kupaniki. Hebu fumbua kwanza macho yako na uniangalie. Macho yangu yanaongea ukweli kuliko mdomo wangu, angalia utaona mwenyewe.”
Regina aliishia kufumbua macho yake na kisha aligeuza uso wake na kumwangalia Hamza usoni.
Waliishia kuangaliana, na Regina alinyoosha mkono wake na kuuweka katika sura ya Hamza na kumfanya bwana huyo mapigo yake kudunda kwa nguvu. Ilikuwa ni adimu sana kwa mrembo kama huyo kuchukua hatua kama hiyo.
“Nishakuambia sina hasira, kwanini bado huniamini? Unadhani sikuamini au ni kweli unanidharau kwenye moyo wako? Ukweli, muda mwingine najihisi labda nina maringo na ukiburi ila najua unanijali mno. Lakini hata hivyo, nataka kufanya kitu ambacho nitajivunia uwezo wangu. Sio jambo baya kwanza kumtegemea mwanaume. Ukiangalia kuna wanawake wengi sana ambao wanategemea waume zao kufanya kila kitu na wanaishi vizuri tu kwa furaha. Najua pia mimi ni mwanamke na napaswa kukutegemea, lakini siwezi kuigiza uhalisia kwani tayari mimi ni tajiri. Kulinganisha na hao wanawake wengine, sidhani kama kutaka kujifanyia kitu kwa uwezo wangu kunaniondolea kigezo cha kuwa mke mwema. Wewe unaonaje?” aliuliza Regina.
Hamza alijikuta akivuta pumzi nyingi na kuzishusha, na pale pale alishika mkono wa Regina.
“Mke wangu, kama huu ndio mtazamo wako basi nimefarijika. Lakini pia jua tu, siku moja ukiamua kutaka kunitegemea na kutaka kukaa tu nyumbani na kuwa kama wanawake wengine, siwezi kukudharau. Ninayekupenda ni wewe; kwangu mimi haijalishi una utajiri kiasi gani au cheo kipi katika kampuni.”
“Ndio, naelewa. Ukweli baada ya kukutana na wewe na pia kufahamiana na watu unaojuana nao kama ilivyo kwa Mr. Leibsoni, leo nimejikuta nikifikiria sana. Kwako wewe urithi nilioachiwa ni mdogo sana, na linaweza kuwa swala ambalo hata hujali. Lakini ndio urithi ambao babu na bibi wameniachia. Nataka kuiendeleza kampuni kwa sababu ya kuheshimu juhudi zao. Lakini vilevile kuna wafanyakazi kibao ambao wanategemea kuendesha maisha yao kupitia kampuni. Hivyo haiwezekani nikawa mwanamke ambaye ninachojua ni kununua na kula tu. Tukiwa kama hivi nichukulie mimi kama mimi na usijali sana kuhusu kazi yangu, sawa,” aliongea Regina na kauli yake ilimfurahisha Hamza moyoni.
Kwa namna walivyokuwa wakiangaliana usoni, urembo wa Regina ulivutia sana macho katika angle hiyo. Kilichomfurahisha zaidi ni haiba ya upole aliokuwa nayo.
Muda huo wakati akiwa amejilaza kitandani akimsikiliza mke wake, alijihisi kuwa mwanaume mwenye bahati dunia nzima na mke wake ni mrembo kuliko wanawake wote.
“Wife, nataka kusikia ukiniita mume wangu au Hubby. Mimi nimekuwa nikikuita mke kwa muda mrefu,” Hamza alijiambia ni wakati wa kugongelea chuma kikiwa bado ni cha moto. Regina mara baada ya kusikia hivyo, alijirembulisha.
“Sitaki, hujanichumbia bado nikakubali kuwa mke wako kihisia.”
“Ah! Basi kama ni hivyo, kuanzia sasa nitafikiria namna ya kukuchumbia,” aliongea Hamza na kumfanya Regina kuvimbisha mashavu.
“Hamza, unataka kweli kuoa mwanamke kama mimi? Hujali kubadilika badilika kwangu na hasira za karibu?”
“Wife, muda kama huu kwanini unauliza swali kama hilo? Tumefahamiana kwa muda mrefu sasa na kufanya mambo mengi, kuna siku uliwahi kuona nikionyesha dalili ya kutokukupenda?”
“Basi niambie umenipendea nini? Si una wanawake wengi tena warembo tu. Hata kama nimewazidi kidogo uzuri, lakini wamenizidi kwenye vitu vingine?” aliuliza Regina akiwa na shauku.
Hamza alipitisha mkono na kuvutia kichwa cha Regina na kukiweka kifuani kwake. Jambo hilo lilimfanya Regina kutetemeka maana ni mara yake ya kwanza, na kwa wasiwasi aliuliza.
“Unafanya nini?”
“Shiii! Sikiliza kwanza,” aliongea Hamza huku akilengesha sikio la Regina karibu na moyo wake.
“Unasikia mapigo yangu ya moyo?”
“Mh! Mbona yapo mbio sana?”
“Ndio. Kabla sijakutana na wewe, sijawahi kuwa na mwanamke ambaye ananifanya mapigo yangu kunienda mbio kama wewe. Kwangu mimi sijali unabadilika badilika wala una hasira za karibu,” aliongea Hamza na Regina mara baada ya kusikia sauti hiyo ya besi alishindwa kujizuia na kutega vizuri sikio lake.
Lakini ni muda ule ngurumo kubwa ilisikika kwa mara nyingine na mvua kubwa ilianza kunyesha.
Regina aliyekuwa ndani ya chumba hicho alichoweza kusikia ni sauti za matone ya mvua na upepo akiwa amemlalia Hamza kifuani.
Endelea kusoma kwenye jukwaa la fasihinet , kwanzia hiki kipande kwenda mbele ni bure:
- SEHEMU YA 192