Simulizi ya kipelelezi: Document number 72 (Nyaraka namba 72)

Simulizi ya kipelelezi: Document number 72 (Nyaraka namba 72)

STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 7.

Mita chache kutoka eneo lilipokuwepo bunge la nchi ya Tanzania, mji ulio fahamika kama DOGMA TULIPO, kwenye chumba kimoja cha mapumziko walionekana vijana wawili wakiwa ndani ya suti huku wakiwa wanabadilishana mazungumzo ambayo yalionekana kutokuwa na maelewano makubwa.

"Ndugu yangu ujue mimi sikuelewi mpaka sasa lengo lako kubwa hasa ni lipi mpaka unataka kuyafanya haya yote?"

"Hauwezi kunielewa kwa sababu unaishi kama bendera fuata upepo tu hujui hata kesho kipi kinatakiwa kufanyika ndani ya nchi yako mwenyewe, sasa sijui huo ubunge wananchi wako walikupa vipi mwanaume muoga kama wewe ambaye huwezi hata kuwasemea kabisa changamoto zao zikatatuliwa" mwanaume aliye Julikana kama Isaya Ndango, aliongea kwa jeuri kwa mbunge mwenzake huku yeye akijinasibu kwamba alikuwa shababi hivyo hakuwa akiogopa chochote kile.

"Muda mwingine kukurupuka kwa mtu kuropoka huwa hakutoi maana ya moja kwa moja kwamba yeye ni mpenda haki na anatumia akili kwa kile anacho kifanya. Jambo ambalo unalifanya linaenda kuigawanyisha nchi kabisa na kufanya watu waanze kuichukia serikali yao, sasa huoni kama unaiingiza nchi kwenye machafuko makubwa?

Tumia akili ndugu yangu sio kuhitaji kutafuta umaarufu na sifa za muda mfupi ambazo zinaweza kukuletea matatizo na kuiweka nchi kwenye machafuko yasiyo na ulazima kwa tamaa za watu wachache" mbunge huyo alimsihi sana Isaya ndango kusitisha hicho alichokuwa anahitaji kukifanya.

Isaya alicheka kwa muda kwanza akiwa anamwangalia mwenzake huyo usoni kwake huku akifunga vizuri kifungo cha juu kwenye koti la suti.

"Nina uhakika mpaka hapo ulipo wewe mwenyewe haujui unataka nini ndiyo maana unakosa misimamo kwa kuhisi mimi natafuta sifa. Nakukumbusha jambo moja tu, unahisi ni kwanini mimi ndiye mwanasiasa pendwa zaidi nchini kwa sasa? Unahisi ni mwanini wananchi kila siku wanaliimba jina langu kwamba siku moja natakiwa kuingia Ikulu? vipi unahisi haya mambo yanakuja kwa bahati mbaya?" Isaya Ndango alimuuliza mbunge mwenza huyo kisha akaendelea;

"Mambo siyo rahisi kama unavyo yaona wewe kwenye macho yako yanafanyika, kila ambacho unakiona kwenye macho yako basi ujue walikaa watu wenye akili wakakipanga na namna ya kukimaliza wanajua. Sasa ukija na uoga wako hapa na kuanza kuhubiri kwamba natafuta sifa basi wewe ndiye utakuwa hauna akili kabisa na unategemea akili za watu wachache ili uweze kufanya mambo yako" alitulia na kuendelea tena;

"Hii nchi, ni nchi iliyo barikiwa sana kwa kila kitu, kuanzia rasilimali zake, watu wenye uwezo mkubwa kiakili na kiuongozi ambao kwa tamaa za watu wachache wenye nia ovu hawapewi nafasi kwa sababu watu hao wanaogopa kwamba nafasi zao zitabebwa na hao watu"

"Hawa watu wenye uwezo mkubwa ndio ambao wanapaswa kuiongoza serikali hii ambayo imejaa udhalimu, ukatili wa kila namna, watu wanauawa kila siku, watu wanalia ajira kila kuitwapo leo huku viongozi wakubwa wakiwa wanawaajiri ndugu zao ambao hawafai hata kuwa viongozi sehemu yoyote ile"

"Nchi inapelekwa mputa kwa maslahi ya watu wachache, hivyo mtu kama mimi siwezi kukubali kuona nchi yangu inateketea kwa kumuogopa mtu yeyote yule na ndiyo sababu ambayo imefanya nimepigania hili mpaka leo bunge limeitishwa rasmi ili tuweze kuzungumza kwa kina kuhusu hili jambo na mwafaka wake utakuwaje mbeleni.

Hivyo kwa leo wabunge na viongozi wengine ambao watafika leo nitajua ndio hao ambao tupo nao pamoja kwenye safari hii ya kwenda kupata nchi mpya yenye kila lililo jema" alimaliza kuongea huku akiwa anaangalia saa yake. Mbunge mwenzake ni kama hakumuelewa ilimlazimu kumuuliza.

"Usiniambie kwamba ulipita kwa kila mbunge kuweza kumshawishi kuhakikisha unatekeleza mipango yako?" Aliuliza kwa mshangao lakini Isaya Ndango alitabasamu tu,
"Nisikilize rafiki yangu, mimi na wewe tumeanza siasa pamoja tukiwa sekondari lakini wewe ni muoga sana, kwa sasa mimi ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini hivyo kuwashawishi watu kwangu ni kazi ndogo sana na ndicho nilicho anza nacho, najua kwamba kama wabunge wengi wakiwa upande wangu basi kazi inaenda kuwa rahisi sana kwa upande wangu"

"Isaya unamaanisha nini kusema hivyo?"
"Hili ni jaribio langu la kwanza kwenda kuharibu kila kitu ambacho unakiona, na baada ya hapa nadhani karibia kila mbunge atakuwa upande wangu pale ambapo watasikia kile ambacho nitakiongea bungeni"
"Hey! hey! Suburi kidogo, unaamisha kwamba unataka......!?" mwenzake huyo akiwa anaongea kwa kigugumizi, mbunge Isaya alimsaidia kulisema hilo jambo.

"Tunataka kuipindua serikali madarakani"
"No, no, no Isaya. Umepatwa na nini ndugu yangu mpaka unawaza mambo mazito ya kigaidi namna hiyo? Ni tamaa ya madaraka au ni kipi kimekufanya ghafla sana umebadilika namna hiyo" rafiki yake alishangazwa sana na namna mwenzake huyo alivyokuwa anawaza mambo mazito sana namna hiyo.

"Haupaswi kuniuliza mimi hilo swali bali unatakiwa kuwauliza hao viongozi wako kwamba wanafeli wapi? Mpaka mbunge wa kawaida kama mimi nataka kuwatoa madarakani!"

"Hili jambo haliwezekani Isaya"
"Unajua kwanini sikutaka hata kukushirikisha?"
"Hapana"

"Sababu ndiyo hiyo, wewe ni mbinafsi sana kwa sababu huwa unajiwazia wewe tu na sio vinginevyo, mimi nina watu wengi ambao wapo upande wangu hivyo usije ukahisi kwamba nafanya haya mambo kwa kukurupuka kama unavyohisi wewe. Yule raisi hafai kuiongoza nchi hii tena kuanzia sasa, ana mambo mengi sana ya kutisha nyuma ya pazia ambayo wananchi wakiyajua basi siku hiyo hiyo watahitaji wamtoe hata kwa nguvu pale Ikulu"

"Ndo uwaze kumtoa raisi madarakani ndugu yangu? Kipi kinakupa hiyo jeuri namna hiyo?" Mbunge huyo baada ya kuuliza, Isaya alitabasamu tu na kuangalia saa yake na ghafla mlango wa hicho chumba walicho kuwepo ukawa unafunguliwa.

Mtu aliye ingia humo ndani alimuacha mdomo wazi mbunge huyo lakini kwa Isaya Ndango ilikuwa ni tofauti maana hata kauli ambayo aliitamka ilizidi kumchanganya mwenzake huyo.

"Mr President karibu sana" mbunge huyo alishangazwa na mambo makubwa mawili. Aliyekuwa ameingia hapo alikuwa ni waziri mkuu wa nchi ya Tanzania, wakati akiwa anajiuliza kwamba vipi waziri mkuu naye anahusika? Ndipo aliposhangazwa zaidi na maneno ya Isaya ndango baada ya kumuita waziri mkuu huyo, Mr president.

Kichwa chake kwa haraka sana kiliweza kuelewa kwamba ina maana kama huo mpango wa kumpindua mheshimiwa raisi pamoja na serikali yake ukikamiloka basi waziri mkuu ndiye ambaye alikuwa anategemewa kukalia kiti hicho, sasa alielewa kwamba ni kwanini Isaya Ndango alikuwa na jeuri ya kusema kwamba ana watu wazito sana upande wake.

Kama mpaka mtendaji mkuu huyo wa serikali alikuwa yupo upande wake basi ilionyesha walikuwa na mengi makubwa ambayo walitaka kuyafanya hata hivyo aliona kwamba ni jambo la hatari sana ambalo walikuwa wanalifanya vipi kama ingejulikana moja kwa moja na alisema siku hiyo anaenda kumwaga mboga mbele ya bunge ambalo huwa linarushwa moja kwa moja mubashara kabisa na watu wanaangalia kinacho endelea?.

Moyoni mwake alikiri kwamba hakuwa tayari kabisa kushiriki kwenye hilo jambo, kwa maana hakuelewa raisi huyo alikosea wapi kwa maana alikuwa anamuona kama mtu safi ambaye alikuwa anaiendesha nchi kwenye misingi safi kabisa na demokrasia ya wazi ambayo kila mwananchi alikuwa anaifurahia, vipi leo aambiwe kwamba kiongozi huyo alikuwa ana mambo ya ajabu ambayo kama wananchi wakiyajua wanaweza kumtoa madarakani hata siku hiyo hiyo, alichoka maana hakuwa na majibu ya moja kwa moja.

Swali la mwisho ambalo alishindwa kulipatia majibu yake, ni kuhusu huyo rafiki yake, ni kwanini alikuwa amemficha kwa kipindi chote hicho? Alikuwa hamuamini? na kama anataka kumtoa raisi madarakani maana yake yeye ndiye anaye itaka hiyo nafasi kwa sababu wananchi wanamkubali sana kwa siasa zake zenye mitazamo ya mbali mno, iweje aweze kumpatia hiyo nafasi waziri mkuu ndiye aingie Ikulu?

Kama waziri mkuu akiingia Ikulu, yeye atakuwa nani? na ana mpango upi hasa wa siri ambao unamfanya azisukume kete zake kwa kujiamini sana namna hiyo mpaka kuwaza mambo makubwa kiasi hicho?. Akiwa kwenye hayo mawazo ndipo waziri mkuu alipo msogelea.

"Heshima yako mheshimiwa!" alimsalimia kiongozi huyo mkubwa kwa heshima. Jina lake alikuwa anajulikana kama William Ivan Msoka, hilo ndilo lilikuwa jina la kisheria la mheshimiwa waziri mkuu huyo wa nchi ya Tanzania.

Alimpa mkono mbunge huyo ambaye alikuwa ana wasiwasi mno, macho yake yakiwa yanamuangalia Isaya na kumuuliza.

"Mbona huyu kijana ana wasiwasi sana, hauoni hatari kuingiza watu waoga kama hawa kwenye mpango kama huu?" waziri mkuu aliuliza huku akigeukia upande wa mbunge yule na kumkazia macho
"Hapana mheshimiwa, huyo ni kijana wangu tangu tunakua ndiyo maana hata safari yetu inafanana kwa kila kitu hata majimbo yetu ni jirani ila nadhani kwamba hakutegemea kukuona hapa ndiyo maana ana wasiwasi sana kiasi hicho maana sikumwambia kwamba unakuja" Isaya Ndango ilimbidi amtetee mwenzake maana hakuwa na namna nyingine huenda angeingia kwenye matatizo.

Waziri huyo alimuangalia vizuri sana huyo mbunge na kutamka;
"Nadhani ni muda mwafaka tuelekee kulutekeleza jambo letu maana ni dakika ishirini tu zijazo bunge linaanza ila kuna kitu kimoja naona kama hakipo sawa!" alimgeukia mbunge Isaya akiwa amehamaki kwa mshtuko,
"Spika wa bunge hatakuwepo leo"
"Whaaat? Kivipi?" Isaya Ndango alishtukizwa na hayo maelezo ya ghafla ambayo hakuyategemea kabisa.
"Ameitwa na raisi muda sio mrefu na kudai kwamba wana kikao cha dharura"
"Unamaanisha kwamba mheshimiwa raisi anajua juu ya huu mpango wetu?"

"Sina uhakika sana na hilo ila kahakikishe unaongea kila kitu mle, hivyo hata kama atakuwa amejua, atashtuka akiwa amesha chelewa, hivyo kwa leo bunge litaongozwa na naibu spika. Ni muda wa kwenda kuanza rasmi mapinduzi kwa kuwafahamisha wananchi yale ambayo hawayajui" Mr William Msoka aliongea kwa kujiamini na kutoka humo ndani kwani hakutakiwa kuongozana na vijana hao.

Isaya alimsogelea mbunge mwenzake na kumpiga piga mgongoni
"Ninayo karata yangu ya mhimu sana ambayo ipo mahali nimeiweka, sina wasiwasi ile nitaitumia kama plan B pale mambo yatakapokukuwa mabaya kwangu, usijali huu mchezo nauchezesha mimi" aliongea kwa tabasamu huku akitaka mwenzake huyo amfuate nyuma. Mbunge huyo hakumfuata kama Isaya alivyo hitaji bali alichepuka na kutokea mlango mwingine, aliondoka kahisa eneo hilo, yeye hakutaka kuwa mmoja wa waasi wa nchi yake mwenyewe.

Unahisi kuna mapinduzi ya nini? Raisi kweli ana mambo yake ya siri au ni tamaa zao za madaraka? Hiyo karata ambayo inampa kiburi zaidi ni ipi? Watafanikiwa mipango yao?

Episode ya 7 inafika tamati.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 8.

Bunge ndani ya mji mkuu wa DOGMA TULIPO, lilikuwa likienda mubashara kabisa na watu walikuwa wanaliona moja kwa moja bunge hilo la 17 kufanyika ndani ya nchi ya Tanzania. Watu wengi walikuwa wanapenda sana kushuhudia moja kwa moja ili kuweza kuona ni kwa namna gani wabunge wao walikuwa wanawawakilisha pamoja na kuwasilisha changamoto zao ambazo wanazipitia mtaani.

Watu wote walitoa heshima kwa naibu spika wa bunge ambaye alitoa taarifa kwamba siku hiyo mheshimiwa spika asingeweza kufika hapo kwani alikuwa kutekeleza majikumu mengine ya nchi hivyo bunge angeliongoza yeye siku hiyo.

Naibu spika wa bunge, alitoa taarifa kwamba siku hiyo bunge lilikuwa limehudhuriwa na wabunge 180, wageni waalikwa 10, mawaziri 7 pamoja na mheshimiwa waziri mkuu wa nchi ya Tanzania. Hivyo kwa ujumla wake walikuwa wanafika 198 lakini ukijumlisha na yeye walikuwa wanafika watu 199 ambao walikuwa ndani ya bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya kuweza kushiriki kwa hilo bunge.

Naibu spika wa bunge aliongea kwa sauti na kudai kwamba mijadala inafunguliwa rasmi na mchangiaji wa kwanza angekuwa ni mbunge Isaya Ndango ambaye alitakiwa kueleza mambo yake haraka kwa muda ambao alikuwa amepewa. Mwanaume huyo alisimama na kuiweka suti yake vyema, huku akimkonyeza waziri mkuu ambaye alimpa ishara ya kuendelea na hicho alichokuwa anataka kukisema.

Dakika chache nyuma kabla ya bunge kuanza.
Kwenye ofisi moja kubwa ndani ya jengo la ghorofa hapo ndani ya mji wa DOGMA TULIPO, alionekana mwanaume mmoja mwenye upara akiwa anaingia ndani ya lifti ambayo bila shaka ilikuwa inampeleka juu ya jengo hilo kubwa. Alishukia kwenye gorofa ya saba ambapo alipitiliza moja kwa moja kwenye ofisi kubwa ambayo hakuna mtu hata mmoja aliye mzuia kwa sababu taarifa zake zilikuwepo za ujio wake.

Ndani ya ofisi hiyo alikuwepo mwanaume ambaye alikuwa na mwili mkubwa akiwa amekaa kwenye meza yake, alimuangalia mwanaume aliyekuwa amefika hapo kama ishara ya kumsikiliza kwamba alikuwa anataka kusemaje.

"Bosi una uhakika na hiki tunacho hitaji kukifanya?" mwanaume huyo aliuliza huku akiwa anamwangalia bosi wake ili kupata uhakika wa jibu lake.

"You just do it Derrick (Wewe fanya tu Derick)" bosi huyo alijibu kwa sauti nzito, akiwa anampa taarifa kijana wake huyo ambaye alijulikana kama Derick kwamba afanye, hakutakiwa kuwa na maswali mengi kwa sababu maamuzi yalikuwa yameshafanyika.

Derick, aliichukua rimoti mezani na kuwasha runinga ambayo ilikuwa ukutani, ndio muda ambao bunge lilikuwa linaanza rasmi ndani ya mji wa DOGMA TULIPO. Wakiwa wanaangalia hapo ndio muda ambao mbunge Isaya Ndango alipewa ruhusa ya kuweza kuwasilisha mapendekezo yake au maoni yake mbele ya Bunge. Derick aliinyanyua simu yake na kuipiga mahali, simu hiyo iliita kwa sekunde mbili tu ikapokelewa.

"Do it" ndiyo amri ambayo aliitoa upande wa pili na kuikata simu hiyo kisha macho yake akayageuzia tena kwenye runinga kumuangalia kijana huyo mbunge akiwa anataka kutafuta umaarufu kupitia makosa ya wenzake.

Wakati huo mbunge Isaya Ndango, alikuwa ameanza kutoa heshima kwa viongozi wakubwa ili aanze kutoa mapendekezo yake, ndio muda ambao kilisikika kishindo kikubwa sana na runinga ikaanza kuonyesha kiza humo ndani na chengachenga. Haikuwa ni ndani ya ofisi hiyo tu pekee bali ni nchi nzima kwa kila ambaye alikuwa anaangalia moja kwa moja alikutana na hali ya aina hiyo, hakukuwa na kilicho kuwa kinaonekana mbele zaidi ya kiza tu hatimaye kukawa hakuna kitu na signals zikagoma kabisa kusoma.

Ndani ya ofisi hiyo kubwa, Derick alimgeukia bosi wake ambaye alikuwa amejawa na tabasamu la kutosha kwenye uso wake.

"Kazi nzuri Derick, sikukosea kukuweka kwenye hiyo nafasi. Unajua vijana mna kasumba kubwa moja; mnapenda sana umaarufu na umaridadi hata kwa mambo ambayo mnaona kabisa kwamba hamna uwezo nayo. Sasa angalia kijana mdogo kama huyo anajingiza kwenye mambo kama haya ambayo tulimpa mpaka nafasi ya kuweza kukaa nayo mbali lakini akaona kwake inamfaa zaidi kupata umaarufu na uhodari mbele za watu. Madhara yake ndo hayo kaenda akiwa na ndoto zake kichwani, hii inasikitisha sana kwa sababu kawaponza na wenzake, haya mambo hayapaswi kuzungumzwa popote pale hata kwa kutania tu ni kosa kubwa sana"

"Kipi kinafuata bosi?"

"Sasa kazi yako kubwa kwa sasa, kwanza hakikisha unamtafuta mkewe na kumuua, kwa maana kama alikuwa na taarifa nyingi basi lazima hata mkewe kuna mambo ya siri atakuwa anayajua hata kama sio sana ila inaweza kuwa hatari. Huu ni msiba mkubwa sana kwenye historia ya nchi hii hususani kufiwa na mtu mkubwa kama yule waziri mkuu"

"Hivyo kipindi hiki najua serikali haitaweza kutoa ulinzi kwa familia zote, ni wakati mwafaka kabisa wa wewe kukamilisha kila kitu na kufuatilia kwa umakini kama kuna mtu ana taarifa au anaonekana kuyafuatilia haya mambo kumpoteza haraka sana. Hakikisha hakuna kosa hata moja ambalo linafanyika kwenye hili jambo maana athari zake zitakuwa mbaya sana" mwanaume huyo aliongea akiwa amemkazia macho kijana wake Derick.

"Sawa bosi, utekelezaji unaanza hivi navyotoka hapa"

"Utekelezaji mwema" mwanaume huyo aliyekuwa na mwili wa haja, alitoka nje baada ya kumalizana na bosi wake hapo ofisini.

Jambo ambalo lilifanyika, liliwaacha wananchi midomo wazi wasielewe ni jambo gani ambalo lilikuwa limetokea ndani ya bunge kwa sababu ilikuwa ni ghafla sana. Watu walianza kupiga kelele kwenye mitandao ya kijamii na kudai kwamba nchi imevamiwa na magaidi huenda kuna jambo la hatari ambalo watu hao wamelifanya kama sio kuleta milipuko basi wamewateka viongozi hao wa nchi lakini kutokana na taarifa za watu wa karibu na eneo hilo pamoja na baadhi ya waandishi wa habari ambao walikuwa wapo nje kabisa ya jengo hilo la kisasa wakiwasubiri wanasiasa watoke ili waweze kuwahoji.

Walitoa taarifa pamoja na video fupi na kudai kwamba jengo hilo lilikuwa limeteketea lote kwa moto mkubwa ambao umesabaabishwa na mlipuko mzito mno. Watu walikuwa wanapiga makelele huku kila mtu akizungumza yake ambayo aliyaona sahihi kwa wakati huo.

Watu wengi walistaajabu, inawezekanaje eneo la mhimu ambalo linalindwa sana kama hilo kusababisha mlipuko mkubwa namna hiyo? Ni mtu gani ambaye alifanikiwa kuingia na bomu kubwa la kulitelekeza jengo hilo pasipo kukulikana? Lawama zote zikaangukia kwenye vyombo vya usalama.

Watu walitukana sana na kudai kwamba hakuna maana ya kuwa na vyombo vya usalama ambavyo haviwezi hata kunusa hatari kubwa kama hizo kwenye maeneo ya nchi kama hayo. Viongozi wa kisiasa wasiopungua 180 pamoja na wageni waalikwa wakiwemo wafanya biashara walikuwa wamepoteza maisha kirahisi sana namna hiyo? Kivipi yaani? Wananchi walibaki wameduwaa huku kila mtu akilia na lake wengine wakianza kujutia kuzaliwa ndani ya Tanzania.

Wanasiasa wa upinzani na chama tawala waliutumia mwanya huo kama uwanja wa nyumbani kwao kuweza kutamba na kudai kwamba wao ni wajuvi wa mambo ndiyo maana kila siku wamekuwa wakilia kwamba serikali iliyopo madarakani haiwafai na watu waiondoe kisha wawaweke wao lakini wananchi wakawa hawawaelewi sasa hayo ndiyo madhara yake na huo ulikuwa ni mwanzo tu maana mengi ya kutisha yalikuwa yanafuatia.

Msiba mzito sana ulikuwa umelitokea taifa la Tanzania, msiba ambao hawakuelewa watatumia nini kuweza kuusahau kwenye maisha ya watanzania walio wengi hususani wale ambao walikuwa wana mahusiano ya karibu na wapendwa wao ambao walikuwa wamekufa. Jambo la kisikitisha zaidi kilikuwa ni kifo cha mheshimiwa waziri mkuu wa nchi, ni kitu ambacho kiliongeza msisimko wa msiba huo baada ya watu kupotelewa na moja ya watu ambao waliwapenda sana.

Vikawa vilio visivyokuwa na majibu, nani alitakiwa kutoa majibu yake? hapo ndipo lawama zote zilipo sogezwa kwa mamlaka za ulinzi na usalama wa nchi. Watu walitukana na kudai kwamba jeshi la polisi hakuna kazi linafanya zaidi ya kula rushwa tu za watu wanyonge mtaani, jeshi la nchi lilikuwa likila mapato ya wananchi tu kwa kula pesa za bure huku wakiwa wamelala tu na kuwaza ngono, hata mkuu wa majeshi hakuonekana kuwa na umuhimu wowote ndani ya nchi kwa wakati huo.

Wengi walilaumu zaidi kuhusu taasisi nyeti ya usalama wa taifa kwamba wao ndio ambao walitakiwa kuona viashiria vyote vya hatari ambavyo vinaweza kujitokeza ndani ya nchi, sasa kama hawana huo uwezo wanafanya kazi ipi? Mbona walikuwa wamejazana wengi sana ndani ya huo mji mkuu wa DOGMA TULIPO? hapo ndipo baadhi ya watu wakajumlisha kwamba watu hao hawakuwa wakifanya kazi yao kama inavyotakiwa bali walikuwa hapo kwa kulinda maslahi ya viongozi tu pekee na hiyo ndiyo ilikuwa kazi yao.

Watu waliitukana sana taasisi hiyo nyeti na kuomba ivunjwe rasmi maana hawana uwezo wa kutenda kazi, wanaendekeza kupeana kazi kindugu na ndiyo maana taasisi haina weledi wowote ule juu ya kazi hiyo. Kila mtu aliongea alilo liona linamfaa, mengine yalikuwa ya kweli ila mengine watu waliongea tu kwa sababu ya hisia za uchungu ambazo walikuwa nazo kwenye mioyo yao ila haikuondoa ukweli kwamba Tanzania ilikuwa imeingia kwenye majonzi makubwa na vilio visivyokuwa na majibu.

Nusu saa kabla ya bunge kuanza. Ndani ya jiji la Dar es salaam, Calvinjr alikuea ndani ya ofisi yake asubuhi na mapema sana, akiwa na mawazo mengi sana ambayo yaliusumbua ubongo wake vilivyo. Alikuwa anakumbuka namna alivyokutana na mke wa mzee Balezi jana yake na kumwambia yale mambo kwamba mzee huyo alikuwa na mengi moyoni ambayo alitakiwa kuyaongea lakini hakupata nafasi ya kuyawasilisha baada ya kuuawa na watu ambao hawakuwa wakijulikana wanatoka wapi na walikuwa wakifanya kazi na nani.

Akiwa kwenye hayo mawazo simu ya mezani iliita kwa fujo sana, aliipokea taratibu bila wasiwasi
"Bosi kuna mgeni wako anahitaji kukuona saivi" ilisikika sauti ya binti wa mapokezi

"Mwambie kwamba nipo busy aje siku nyingine"

"Ni Mrs William bosi"

"Whaaat? Mlete haraka sana" alishtuka baada ya kusikia ni Mrs William, mwanamke ambaye aliahidi kumpatia mkataba wa tenda za ujenzi ambazo zilikuwa na mabilioni ya pesa, japo alishangaa sana mwanamke huyo kuja hapo kwa maana yeye ndiye aliyekuwa anatakiwa kwenda ofisini kwa mwanamke huyo.

Mrs William aliingia na kuanza mazungumzo na mwanaume huyo ambapo walikubaliana kila kitu na kusaini mkataba huo. Mrs William alitabasamu baada ya kukamilisha kila kitu kisha akamuuliza Calvinjr;
"Ulisema kuna kitu utaniandalia kwa msaada niliokupatia ndiyo maana nimekuja mwenyewe kuichukua hiyo zawadi yangu" mwanaume alishangazwa na maneno ya mwanamke huyo ambaye alikuwa ndiye mkandarasi mkuu wa serikali aliyekuwa akifanya kazi kwa karibu sana na waziri wa ujenzi.

Calvinjr kabla hajajibu chochote, aligeuza macho yake kwenye runinga baada ya kuona bunge hilo linaanza na viongozi wanatambulishwa na mhesimiwa naibu spika, ni kama kuna kitu kilimshangaza hata yeye baada ya kusikia kwamba spika wa bunge hatakuwepo siku hiyo, kutokuwepo sio shida sana ila hiyo taarifa ilitakiwa kutolewa mapema.

Utambulisho wa waziri mkuu ndio ulio mfanya Mrs William naye awe makini sana kwenye hiyo runinga, wakasahau hata hiyo zawadi ambayo walikuwa wanaiongelea muda mfupi uliopita hapo. Hazikupita hata dakika mbili ndipo uliposikika mlipuko mkubwa na runinga hiyo ikaacha kuonyesha kabisa.

Mwanamke huyo alidondoka chini na kuzimia, Calvinjr aliwa anashangazwa na lile tukio, alipagawa na tulio lingine la mwanamke huyo kuweza kuzimia asijue nini tatizo mpaka mrembo huyo awe kwenye hiyo hali.

Nini kinafuata? Bunge limelipuliwa? Kivipi? na nani? Na kwa sababu gani? Hata mimi nina maswali mengi sana.

Episode ya 8 inafika mwisho.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 9.

Calvinjr akiwa kwenye hali hiyo ya mshangao ya kushangaa ni kwa namna gani mkandarasi huyo aliweza kupata hilo tatizo ghafla sana namna hiyo, aliamua kuchukua uamuzi wa kumbeba na kutoka naye ili awahi hospitali.

Wafanyakazi wake wote ambao walikuwa wanamuona anapita na mwanamke huyo walihisi labda huenda watu hao ni wapenzi ila hawakujali sana kwa maana kila mtu alikuwa kwenye majonzi makubwa juu ya lile jambo ambalo lilikuwa linaendelea.

Calvinjr aliendesha gari haraka, kwa dakika ishirini tu akawa amefika kwenye malango ya hospitali ambapo madaktari walimpokea mgonjwa na kumtaka yeye abaki nje maana huko ndani hakuwa akiruhusiwa kuweza kuingia. Daktari mmoja wa kike ilimwangalia mwanaume huyo na kumkonyeza huku akiwa anamminyia jicho moja.

Calvinjr almpuuza mrembo huyo maana hakumuona kama yupo siriasi, watu wapo kwenye majonzi yeye anawaza mapenzi, sema alitabasamu tu kama kumfariji na kumwambia kwamba wapo pamoja asijue kwamba mwenzake analichukuliaje hilo tabasamu.

Alikaa kwa muda wa dakika kumi mpaka pale simu yake ya mfukoni ilipoanza kuita kwa fujo, aliitoa na kuiangalia. Ilikuwa ni namba binafsi ambayo ilianzia na sifuri tatu mwanzoni. Aligeuka na kuangalia kila upande kisha akakimbilia chooni na kuhakikisha kwamba hakuna mtu, akafunga mlango.

"Nakusikiliza bosi"

"Nakuhitaji haraka sana"

"Nipo njiani nakuja" alijibu na kuikata simu hiyo kwa haraka kisha kutoka ndani na hicho choo akihitaji kuwahi eneo ambalo mtu aliyesadikika kuwa bosi wake alikuwa anamhitaji.

Aliwaza kuhusu mgonjwa wake lakini hakuwa na namna alikuwa nje ya muda kabisa, basi akamuaga daktari mmoja na kumpa maagizo kwamba kama daktari wanao mtibu mgonjwa wake kwenye chumba ambacho alielekeza wakimhitaji, awaambie kwamba kaenda kuchukua mahitaji na angerudi kwa muda mchache ambao ulikuwa unakuja.

Alitoka nje kabisa na kupanda kwenye gari yake ila kabla hajaondoka, akiwa anajiandaa kupandisha kioo cha gari, alisita kwanza. Kusita kwake kulisababishwa na yeye kuona msafara wa magari. Hivyo alitulia ili kujua ni mtu gani alikuwa anaingia pale muda ule, kitu ambacho kilimchanganya na hakuelewa ni baada ya kumuona mke wa waziri mkuu akiwa amevimba macho kwa machozi ambayo alionekana kuyatoa kwa muda mrefu bila kupumzika akiwa anaelekea ndani ya hospitali hiyo.

Hakukuwa na tatizo kwa yeye kulia kwa sababu muda mchache uliokuwa umepita mumewe alikuwa ameuawa kwenye ule mlipuko ambao hata yeye mpaka muda huo hakuwa anaelewa ulitokeaje tokeaje, ila kitu ambacho kilimchanganya sana ni mke wa mheshimiwa kuwepo hilo eneo kwa huo muda.

Kama mwili wa mumeme haukuwa bado umepatikana kusema kwamba ulikuwa umeletwa hapo hospitalini ndiyo maana alikuwa amefika, sasa kama hata mwili wa mumewe hukuwepo yeye alifuata nini? Hakuelewa, alitamani sana kama angeweza kupata jibu ila kwa bahati mbaya sana alikuwa yupo nje ya muda.

Alitoka hapo hospitali na kuanza kuitafuta njia ya magomeni ambako alinyoosha na njia ya Urafiki na kwenda kuishia zilipo nyumba za utumishi maeneo ya Shekilango karibu na Ubungo. Alisimamisha gari yake karibu na kituo cha mwendokasi na kuelekea ndani mpaka mwenye mlango mmoja uliokuwa umefungwa kwa ndani huku mbele yake akiwa anawaona watoto wanacheza, bado ilikuwa mapema sana.

Baada ya kugonga mlango ukafunguliwa, akaingia ndani. Alishtuka baada ya kumkuta dada yake Tina yupo hapo tayari hakuongea lolote bali alipotezea tu.

"Nadhani umeona kilicho tokea" Mzee mwenye kitambi kikubwa kilicho kubali pesa alimuuliza akiwa anageukia upande wa dirisha lililokuwa limewekewa vitambaa vyeusi kiasi kwamba hakukuwa na uwezekano wa mtu wa nje kuona ndani au wa ndani kuona nje.

"Ndiyo nimeona mara moja tu ila mpaka sasa sielewi kwa maana kuna mteja nilikuwa naye baada ya kushuhudia yale matukio amezimia ghafla hivyo ikabidi nimuwahishe hospitali, ndipo ukawa unanipigia simu"

"Bunge limelipuliwa lote, hakuna kitu kilicho baki kwenye lile jengo. Hakuna mfupa wala dalili ya uwepo wa kitu chochote hapo kabla kwenye lile eneo. Kila kitu kimebaki majivu tu" Mzee huyo aliongea akiwa anamsogezea Calvinjr laptop ambayo ilichukuliwa na kamera za siri za usalama ambazo zilikuwa mbali na hilo eneo.

Video hiyo ilikuwa inaonyesha namna jengo hilo lilivyoshuka ndani ya dakika moja tu na kugeuka kuwa majivu. Usingeweza kuamini kwamba sehemu hiyo iliwahi kuwa hata na tofali, palibaki tambalale kabisa, wakati kabla palikuwa na majengo ya gharama isivyokuwa kawaida.

"Watu wangapi walikuwa ndani?"

"Kwa watu ambao tuna hesabu yao kwenye mifumo yetu, yaani viongozi pamoja na wageni waalikwa, jumla ni watu 199 ndio wamefia mle ndani ila bado hatujajua idadi kamili ya wafanyakazi wa lile jengo ambao lazima walikuwepo pale ni wangapi mpaka sasa" Mzee huyo alimjibu kijana wake, huku Tina akiwa ametulia tu ni wazi yeye hizo taarifa alikuwa nazo mapema.

"Inawezekanaje jambo kama hilo kutokea kirahisi sana sehemu kama hiyo? Yaani mtu anaingia na kutega bomu kubwa kiasi hicho na sisi hatujui? Kwamba tunalala sana au tumefeli wapi?" Calvinjr aliongea kwa hasira sana huku akigonga meza kwa nguvu.

Mwanaume huyu alikuwa ni jasusi wa taifa la Tanzania, haya maisha alikuwa anayaishi nyuma kabisa ya pazia ambapo waliokuwa wanamjua kwamba anaifanya hiyo kazi walikuwa ni watu wachache sana akiwemo dada yake wa damu pamoja na bosi wake.

Mr Gulamu Leopard, aliikunja suti yake vyema. Huyu ndiye alikuwa kiongozi wa shirika hilo la kijasusi ambalo lilifahamika kama Tanzania Beuracratic Security and Intelligence Services yaani (TBSIS), alimgeukia Calvinjr na kumwambia;

"Kwa hili hatuna namna zaidi ya kuzibeba lawama za nchi nzima kwa huu uzembe wetu mkubwa ambao sidhani kama kuna mtu atakuwa tayari kuweza kutusamehe kwa hili. Ila wakati tunazipokea hizi lawama hatutakiwi kupata hata dakika moja ya kuweza kulala, inatakiwa tuhakikishe kwamba kwa gharama yoyote tunajua ni nani yupo nyuma ya hili" alitulia kidogo na kuendelea.

"Hakuna mtu wa kawaida ndani ya nchi hii anaweza kuingia kwenye geti la bunge au sehemu yoyote ya bunge akafanikiwa kupita akiwa hata na risasi tu kwa ulinzi ambao tuliuweka pale"

"Unataka kumaanisha nini mkuu?" Calvinjr aliingilia kati ili aelewe kwamba mzee huyo alikuwa amelenga kumaanisha nini.

"Inamaanisha kwamba aliyefanya hili jambo ni moja ya kiongozi mkubwa wa serikali"
"Whaaaaat?" Calvinjr na Tina walijikuta wote wakiwa wanauliza kwa pamoja wakiwa wamepigwa na butwaa isivyokuwa kawaida.

"Kama ile sehemu hawezi mtu wa kawaida kupita na kitu chochote hatarishi kwa sababu ya ukaguzi mkali ambao huwa tunaufanya kuanzi kwa mtu husika anaye ingia pamoja na gari yake kwa ujumla tena kwa kutumia mitambo mikubwa ya kisasa, sasa mnahisi inawezekana vipi mtu wa kawaida aweze kupitisha huo mzigo? Jibu ni kwamba haiwezekani"

"Hii inamaanisha kwamba mtu ambaye amehusika kuingiza hili bomu mle ndani ni kiongozi mkubwa kwa sababu viongozi wengi wakubwa huwa hawakaguliwi kabisa na hata magari yao hayakaguliwi kwenye geti la bunge, ndivyo itifaki ya nchi ilivyo. Kwa maana hiyo Mtu ambaye aliingia na hilo bomu ambalo limeleta maafa, alitumia gari ambayo alijua kabisa haiwezi kukaguliwa kwenye mageti yote ambayo magari yanapita" Mr Gulamu Leopard, aliwaelekeza vijana wake kwamba ni kwanini yeye alikuwa ana uhakika na kile ambacho alikuwa anakisema.

Calvinjr alichoka mpaka akalazimika kukaa chini, nafsi yake ilikuwa inaenda kwa nguvu sana kila akiwaza kwamba hawahawa viongozi ambao walipaswa kuwalinda wananchi ndio ambao wanafanya mambo ya ajabu namna hiyo?

"Bosi, vipi kama kuna mtu labda kwa mahesabu yake akaamua kutumia gari ya kiongozi wa nchi kutekeleza hilo ili kujiweka mbali na hatia pale ambapo sheria itaamua kuchukua mkondo wake?" Tina aliuliza akiwa anairudia rudia tena video hiyo ambayo ilitaka moyo kuweza kuiangalia mara mbili mbili.

"Hilo jambo haliwezekani, kwa sababu gari zote za waheshimiwa kabla hawajapanda huwa zinakaguliwa na mamlaka za ulinzi kila sehemu hivyo kila gari lazima ihakikiwe kama ipo salama ndipo kiongozi apande. Gari hizo huwa zinafungwa vioo na hazisimami popote mpaka zinafika, sasa huyo mtu atawekaje bomu kubwa lenye uwezo mkubwa sana namna hiyo" Mr Gulamu alimjibu Tina akimaanisha kwamba mawazo ya binti huyo hayakuwa sahihi hata kidogo.

"Kuna kiongozi aliingia na hilo bomu likiwa kwenye begi lake kiasi kwamba hata walivyokuwa wanayakagua hayo magari wasingeona chochote na kwa bahati iliyokuwa mbaya huwezi kukagua begi ya kiongozi mkubwa labda mpaka kuwe na ruhusa maalumu kutoka kwa bosi hapo" Calvinjr aliongezea maelezo huku akisimama ili dada yake aelewe. Alipunguza koti kwenye mwili wake, hawakuwa na muda wa kupoteza wala kulala kwa sasa, ilitakiwa mhusika ajulikane ni nani hasa.

"Natakiwa kwenda huko" Calvinjr aliongea akiwa anamuangalia kiongozi wake usoni
"Hapana" alikataliwa, kitu ambacho hata yeye kilimshtua sana
"Kwanini"

"DOGMA TULIPO anaenda Tina, wewe kuna kazi mbili ambazo nataka nikupe"

"Bosi anaendaje Tina sehemu hiyo na mimi nipo? huko ni hatari sana hatujui mpaka sasa watu hawa wana mahesabu ya kufanya nini na wapi, sasa unamtuma vipi Tina" Calvinjr aliongea kwa kulalamika huku akiwa anamuangalia dada yake kwa hasira, hakutaka dada yake aingie kwenye hatari ambayo mpaka wakati huo hawakujua inatokea wapi.

"Tina nahitaji ripoti haraka sana, unaweza kwenda" Bosi huyo alimpa maagizo Tina kwamba amri yake haitabadilishwa, Tina alimkonyeza mdogo wake huku akimcheka na kumsanifu, dada mtu aliona kwamba mdogo wake bado hajawa imara sana, yeye ndiye alitakiwa kujijali na siyo kumjali dada yake mwenye uwezo. Ndiyo sababu alifurahi baada ya kiongozi wao kufanya maamuzi hayo ya mwisho.

"Kazi yako ya kwanza ni kumlinda mtoto wa waziri mkuu ila kabla haujaanza haya majukumu inatakiwa leo usiku uwe umefika ndani ya jimbo la DAMU INAYO ISHI huko Lindi ambako alikuwa anaongoza mbunge Isaya Ndango" Mzee huyo aliongea huku akiwa anaiweka picha chini ya mwanamke ambaye Calvinjr alitakiwi kumlinda kwa nguvu zake zote.

Kitu cha kushangaza, ilikuwa picha ya mrs William, yule mkandarasi mkuu wa serikali ambaye yeye mwenyewe alitoka kumpeleka hospitali muda sio mrefu. Alibaki na mshangao ambapo macho yake ni kama yalikuwa yanauliza maswali kwamba hiki ni nini mkuu?

"Huyo ndiye mtoto wa mheshimiwa waziri mkuu na ndiye mtoto wa pekee kabisa kwenye hiyo familia. Jina lake anaitwa Sarafina William ila jina maarufu ni mrs William na kwa bahati iliyo mbaya watu wengi hawajui kama huyo ni mtoto wa waziri mkuu hivyo msiba wa baba yake utamfanya ajulikane kitu ambacho kitakuwa hatari sana kwa maisha yake" maelezo ya Gulamu Leopard sasa yalimpa jibu kwamba ndiyo maana alimuona mke wa waziri mkuu pale hospitali, kumbe alikuwa anamuwahi mwanae wa pekee? Alichoka.

Episode ya 9 inafika tamati.

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 10.

Calvinjr akiwa ndani ya huo mshangao kwa kustaajabu mwanamke huyo kuwa mtoto wa waziri mkuu, Gulamu Leopard alimshtua kidogo baada ya kuguna kwa sauti, ikamfanya akae sawa kwa mara nyingine ili kumsikiliza bosi wake.

"Calvinjr inatakiwi uelewe kitu kimoja, kwa sasa mimi nakuamini sana wewe pamoja na dada yako tu basi hakuna mtu mwingine yeyote ambaye mimi namwamini zaidi ndiyo maana nimewamua kuwaita kwa siri na kuwapatia hii kazi nyie hapo" Mzee Gulamu aliongea kitu ambacho kidogo kilimshangaza Calvin.

"Bosi sijakuelewa, unamaanisha nini kusema kwamba unatuamini sisi tu? Inamaana vijana wako wengine huwaamini ingali wewe ndiye kiongozi wa shirika hili? Huoni kama unafanya vibaya kutowaamini vijana wengine ambao inatakiwa tushirikiane kudumisha ulinzi wa taifa hili?"

"Nisikilize kwa umakini sana bwanamdogo. Una miaka ishirini na mitano tu pekee, unatakiwa kujiuliza sana kwamba ni kwanini nasema nakuamini wewe na dada yako tu pekee. Mimi ni kiongozi wa juu zaidi ambaye natakiwa kila kitu kukiamua mimi kuhusu shirika hili lakini pia mimi ndiye ambaye ninatakiwa kujua kwamba ni nani na nani wananifaa kwa kazi fulani"

"Hili jambo limeharibiwa na kitu kinaitwa siasa, siasa imeua kabisa misingi ya kazi hii na kuifanya ianze kufanyika kisela kuliko weledi. Hii nafasi yangu kwa walio nje wengi wanaitamani sana kwa sababu kitu cha kwanza wanacho kiwaza ni pesa, ni kweli unakuwa na pesa lakini majukumu yaliyopo ni magumu kuliko hata hiyo pesa hususani kwa mtu ambaye una misimamo na kazi yako na unataka kuitekeleza kwa weledi mkubwa"

"Hata ikija kutokea siku sipo kwa bahati mbaya unatakiwa kuyaelewa haya mambo. Viongozi wengi wakubwa ndio wanaovunja utaratibu wa kazi kwa sababu ya kutaka ndugu zao waajiriwe bila kujali kama taasisi inahitaji watu makini na sio ndugu hapo ndipo tunaanza kupata watu wa hovyo ndani ya taasisi ambao wengine wanakuja kama vibaraka wa kulinda maslahi ya watu wao na sio kingine, hiyo ndiyo sababu nasema simuamini mtu yeyote mwingine zaidi yako na dada yako"

"Hivi kwa mfano wewe hapo raisi anakupigia simu kwamba ana ndugu yake anaona kabisa kwamba anafaa kwenye idara na anataka umchukue, utaogoma? Ukigoma anatishia kukufuta kazi na kukubambikizia kesi au kuidhuru familia yako. Hivyo inafika hatua unakuwa hauna namna zaidi ya kukubaliana naye kwa kile anacho kitaka, je hao ndio watu ambao unaweza ukawaamini na kufanya nao kazi hata kama umewafunza? Jibu ni hapana"

"Sio kila jasusi ni mtu makini kufanya kazi hizi, huwa tunaangalia vitu vingi sana hasa pale ambapo inahitajika apatikane mtu wa kwenda kufanya kazi za mhimu kama hizi. Kuna watu nyie mnafanya kazi mkidhani mpo pamoja huku yeye akiwarudisha hatua kumi nyuma kwenye kila kazi ili kulinda maslahi yake"

"Lakini licha ya mimi kuwaamini sana nyie wawili ila pia unatakiwa kuelewa kwamba wewe ndiye silaha yangu ambayo naitegemea sana kwenye kila jambo gumu kama hili linapotokea hapa nchini" Gulamu Leopard alitulia kwanza huku kijana huyo akiwa ametulia kwa umakini sana anamsikiliza. Alikohoa kidogo na kuendelea.

"Miaka ambayo nilikuiba kwa mama yako na kudanganya kwamba unaenda kusoma Kenya, ni miaka ambayo niliitumia vyema kukutafutia watu makini sana kukufunza kuliko ilivyo kwa vijana wengine"

"Watu wachache wanao kujua ikiwemo dada yako, hawana imani na wewe kabisa kwenye uwezo wako ndiyo maana hata dada yako ukisema kwamba unataka kumlinda huwa anaishia kukucheka tu kwa sababu anajua una uwezo mdogo hata mbele yake. Sasa hiyo ndiyo silaha yangu mimi ya mhimu sana kwani wengi wanajua wewe hauna madhara na hautakiwi kuwaonyesha sana namna ulivyo maana wanaweza wakaanza na wewe kukupunguza ili usije kuwa kikwazo hapo mbele"

"Hata dada yako, aendelee kuamini kwamba wewe ni moja ya wapelelezi wa kawaida tu hivyo hivyo mpaka siku ambayo itakuja kukulazimu na yeye akakufahamu vyema maana hizi kazi hamtakiwi kuaminiana sana hata kama mmezaliwa kwenye tumbo moja na kuna siri za mhimu hata dada yako hatakiwi kabisa kuzijua wala kuzisikia kutoka kwenye mdomo wako"

"Halafu nataka nikupe somo dogo ambalo unatakiwa kuishi nalo moyoni siku zote. Najua haujapenda mimi kumpeleka dada yako huko DOGMA TULIPO kwa sababu ya usalama wake. Kwenye maisha yako haya ambayo umeamua kuyaishi ogopa sana kitu kinaitwa hisia, zitakufanya upoteze kila kilicho karibu yako kwa uzembe mdogo sana"

"Kwenye maisha yako njia bora ya kuwalinda wale uwapendao ni kukaa nao mbali, ukikaa nao mbali wanakuwa salama zaidi kutoka kwenye upande wa maadui zako kwa sababu kwanza hawatapata nafasi ya kuwajua kabisa. Lakini pili hata wakiwajua hawatakuwa na cha kuwafanya kwa sababu watajua hata wakiwafanya kitu chochote kile wewe haitakuuma hivyo watakuwa hawajakukomoa kabisa"

"Watu huwa wanawaumiza watu kupitia udhaifu wao, hivyo kama wakigundua kwamba udhaifu wako upo kwa mtu fulani, basi mtu huyo ndiye ambaye anageuka kuwa silaha ya kukufanyia wewe maangamizi. Kaa mbali na dada yako, usiruhusu watu wengi wajue kwamba nyie ni ndugu na mna ukaribu ipo siku utakuja kujuta" Mzee huyo alimaliza hayo maelezo akiwa anampiga piga mgongoni kijana wake huyo baada ya kumpa elimu ya kutosha juu ya nafasi aliyokuwa nayo.

"Nimekuelewa mzee"

"Halafu kumbuka kitu kimoja, hili jambo nataka likae kwako na kwa dada yako tu, kwa sasa najua tunaingia sehemu mbaya ya kuwachunguza vigogo hivyo kwa namna yoyote ile watahitaji kufuta kila aina ya ushahidi ambao unajitokeza na kuwabambikizi kesi watu ambao hawahusiki kabisa na hayo mambo. Hivyo hili jambo linatakiwa kukaa baina yetu sisi tu hata dada yako nimemwambia juu ya hili, kuna vijana wengine nitawapa kazi ila najua hakuna la maana watakalo lifanya sana kwani ndo hawa hawa wengi wapo kuwalinda hawa viongozi"

"Tina ameenda huko kwa sababu ni mwanamke mrembo sana na anaweza kuingia sehemu yoyote ile kirahisi tofauti na kama ungeenda wewe hapo, kuna maeneo ambayo ulitakiwa kutumia nguvu zaidi kitu ambacho kingetuhatarisha sana kuharibu kazi mapema na kujulikana mapema kabla hatujapiga hatua yoyote ile. Nahitaji taarifa kesho usiku ya huko Lindi uwe umerudi" Gulamu Laopard alimaliza na kuanza kukusanya vifaa vyake ili aondoke, lakini Calvinjr alimzuia mzee huyo.

"Bosi, umenipa tu kazi ya kwenda huko Lindi kufuatilia familia ya Isaya Ndango ila haujanipa sababu maalumu kwamba ni kwanini natakiwa kuiwahi familia hiyo kama ipo salama hususani mkewe, unahisi kwanini wanaweza kuigusa familia hiyo?" Mzee huyo alitua laptop yake chini baada ya kusikia hilo swali kisha akamgeukia Calvinjr.

"Siasa ni mchezo mchafu kuliko watu wa nje wanavyo uona na kuhisi kwamba upo hivyo lakini siasa ni mchezo wa watu wachache ambao wanaumudu na kuishi vyema huko bila kupata matatizo ya aina yoyote ile?"

"Siasa inahitaji uwe na vitu viwili vikubwa ili uweze kuishi huko na kuwa na uhakika na maisha yako. Kwanza inatakiwa kuwa na nguvu, hapa kwenye nguvu watu wengi huwa wanawaza kitu kimoja ambacho ni pesa tu pekee. Ni kweli nazungumzia nguvu ya pesa ambayo inaweza hata kununua watu ila ukiwa na pesa pekee haijitoshelezi kwenye siasa kama endapo utakuwa unataka kushindana na wenye pesa wenzako hapo utajikuta unafeli hivyo pesa zinatakiwa kuambatana na nguvu kubwa ya ushawishi. Lakini ukiacha nguvu hiyo ya pesa na ushawishi, kitu cha pili ambacho unapaswa kuwa nacho kwenye siasa ni akili"

"Hili kundi lina watu wachache ambao kwa asilimia kubwa ndio ambao wanaendesha nchi nyingi hapa duniani. Madarakani wanakaa watu wenye nguvu ya pesa muda mwingine au watu wenye pesa wanawaweka watu wao wenye ushawishi mkubwa madarakani huku wao wakinufaika na matunda hayo lakini watu wenye akili ndio ambao huwa wanategemewa zaidi na watu wenye pesa kwani ndio ambao huwa wanaandaa mipango yote ya namna ya kufika Ikulu au kupata kitu chochote ndani ya nchi husika kwa wakati ambao wanautaka wao"

"Na mara nyingi watu wa namna hii huwa hawajulikani sana kwa manufaa ya watu wachache, hivyo akijulikana maana yake watu wengi watamtaka na wenye nguvu ya pesa na ushawishi ndio wanaweza kufanikiwa kufanya naye kazi"

"Sasa huyo mtoto kuna sehemu alikosea sana kwenye kuzifanya hesabu zake na ndiye ambaye amewaponza viongozi wenzake kuweza kuuawa leo hii" akiwa anatoa elimu kwa kijana wake alimshtua Calvinjr na hayo maneno yake.

"Bosi unamaanisha nini kusema kwamba yeye ndiye aliyewaponza wenzake? Maana nilikuwa namuona kama mwanasiasa machachari ambaye alikuwa na nguvu kubwa ya kuhitaji mabadiliko ya kweli? No way! kwamba hili ndilo limefanya wamemuua? ooooh shiiiit!" Calvinjr aliuliza na kujijibu mwenyewe maana alikumbuka na kuelewa kila kitu.

"Na hiyo ndiyo sababu ambayo imefanya wampoteze haraka sana kabla ya bunge kuanza kwa sababu angetapika kila kitu. Huyo bwana mdogo yeye amebahatika kuwa na kitu kimoja, ana nguvu kubwa ya ushawishi ila alikosa vitu viwili vya mhimu, pesa na akili ya mbali. Kupitia ushawishi wake akahisi kwamba anaweza kufanya kila ambacho anakitaka yeye kitu ambacho hakiwezi kufanyika hata siku moja"

"Nafasi yake ya nguvu ya ushawishi alifanikiwa kumuweka kwenye upande wake mheshimiwa waziri mkuu wa nchi ambaye sikujua kwamba walikuwa wana mpango gani wa siri mpaka kufikia hatua ya kuwa na hamu sana na bunge la leo. Inaonekana kwamba kati kati yao kuna wasaliti ambao wamezitoa siri zao hivyo wakawa wanajua kila hatua ambayo walikuwa wanaipiga"

"Hii ni kwa sababu inaonekana kabisa kwamba kuna mtu alijua kwamba yule bwana mdogo kuna siri anazo anataka kuziongea leo hii ndiyo maana wakaamua kumuwahi na kuua watu wote kwani waliamini kwamba watu wote ambao wamefika leo huenda wapo upande wake tayari hivyo wanaweza kuwa tatizo kwa baadae"

"Sasa hapa swali la msingi ni kutaka kujua kwamba alikiwa na siri zipi ambazo alitaka kuzisema leo mbele ya bunge na zilikuwa zinamhusu nani kiasi kwamba mtu akubali kuleta msiba mzito sana namna hii ndani ya taifa? Wanajua kwamba huenda mkewe akawa anajua baadhi ya mambo kwani ndiye mtu ambaye alikuwa naye karibu sana, huenda wakawaza kumuua. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyo nifanya nitake wewe uende huko Lindi na hiyo ndiyo inaweza kuwa sehemu ya mhimu zaidi ya kuweza kuanzia" Gulamu alimaliza na kubeba vitu vyake kisha akatoka humo ndani maana kila mtu alitakiwa kuondoka kimpango wake ndani ya chumba hicho.

Calvinjr sasa alielewa kwamba ni kwanini alitakiwa kuwepo huko, mzee huyo alikuwa anatumia sana akili, kumbe huko ndiko kulikokuwa kwa mhimu zaidi kuliko hata DOGMA TULIPO ambako ndiko lilikuwepo bunge la nchi kabla ya kulipuliwa.

Episode ya 10 inafika tamati

Febiani Babuya.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Naulizwa sana maswali kuhusu hii simulizi kama imekamilika.

Jibu lake[emoji116]

Ndiyo imekamilika na ipo yote full pdf[emoji996]
FB_IMG_1694584148778.jpg


Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom