STORY: DOCUMENT NUMBER 72
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
EPISODE 6
Saa mbili ya usiku ilimkutia Calvinjr njiani akiwa anaelekea Mbande, huko alikuwa anaenda kukutana na mke wa mzee Balezi ambaye alimuahidi kwamba kuna kitu alikuwa anahitaji kumwambia. Mwanaume alitumia dakika 40 tu pekee kufika Azam Complex, huo ni uwanja wa timu ya mpira wa miguu wa Azam.
Aliongeza spidi maana ilibakia muda mchache sana mpaka kufika hapo Mbande. Dakika chache sana zilizo fuatia alikuwa ndani ya hilo eneo, alisimamisha gari yake na kugeuka sehemu zote mpaka alipo iona nyumba yenye rangi ya blue, alitabasamu maana alielekezwa eneo hilo na hiyo ndiyo ilikuwa nyumba pekee yenye bati la blue ndani ya hilo eneo.
Alisogea mpaka ulipokuwa mlango wa getini ila alihisi upo wazi, alichungulia kwa ndani, hakuona kitu zaidi ya taa za ndani ya nyumba hiyo ambazo zilikuwa bado zinawaka. Baada ya kuingia tu alisimama kwanza, mwili ulimsisimka mno ndipo alipogeuka upande wake wa kushoto, alishangaa sana baada ya kuona mwili wa mlinzi ukiwa upo chini.
Alisogea kwenye eneo hilo kisha akamgusa pua mlinzi huyo ili kujua kama alikuwa hai au amekufa lakini kitu cha ajabu mlinzi huyo alikuwa amezimishwa tu. Alishangaa sana, ni mvamizi gani ambaye amekuja na anaonekana kabisa hakuwa na lengo la kumuua mtu huyo? Sasa kilicho mleta ni kipi? Hakuelewa.
Akiwa bado ameinama hapo alihisi kama kuna kivuli kinakuja upande ambao yeye alikuwepo. Aliinuka ghafla sana kisha akarudi nyuma, alipishana na buti ambalo kama lingempata huenda angetumia kama wiki moja hivi kuweza kuzinduka na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
"Kaa mbali na hii familia utailetea matatizo makubwa sana. Endelea kuishi maisha yako ya kawaida kama unavyo ishi siku zote na usitake kujifanya unaanza kukuza kuza mambo utawaletea matatizo watu wanao kuzunguka bure" sauti yenye mamalaka ilipenya vizuri kwenye masikio yake. Ina maana huyo mtu alikuwa anamfahamu vizuri ndiyo maana alimpa huo ushauri.
"Kwa maana hiyo wewe unanifahamu mimi vizuri sio? Kwahiyo wewe ni nani?" Mwanaume huyo aliyekuwa amejifunika na shuka jeusi kwenye mwili wake hakujibu kitu zaidi ya kukimbilia ulipo mlango wa geti ili atoke. Nani wa kumruhusu? Alikutanishwa na viganja kwenye kifua chake.
Alirudi nyuma kwa hatua kadhaa huku akionyesha mshtuko mkubwa wa kijana huyo kuwa na uwezo wa namna hiyo, Calvinjr alitabasamu na kuikunja suti yake kwenye mkono. Mwanaume huyo alitakiwa kutoa maelezo yeye ni nani na anamjuaje Calvinjr.
"Kitu cha ajabu kilitokea, mwanaume yule alivua shuka lake kwa kasi na kulirushia upande ambao alikuwepo Calvin, lilimfunika mwenye mwili wake wakati anahangaika kulitoa, mwanaume yule alijibinua na buti lake na kujizungusha kwa double kick nzito ambapo mateke yote yalitua kwenye kifua cha Calvinjr na kumuachia maumivu.
Kasi ya yale mateke ilimfanya yeye mwenyewe kuachia lile shuka huku akijibamiza ukutani. Alidondoka chini akiwa na maumivu ya kutosha. Alijigonga kwa nguvu kwenye mguu wake wa kulia kwa kutumia mkono wake, alijigeuza na kusimama kwa sarakasi lakini alikutana na hewa tu na utulivu wa humo ndani, mwanaume huyo alikuwa ametoweka zamani.
Aliinama na kumgusa yule mlinzi kwenye mshipa wa shingoni kwa nguvu na kumfanya ashtuke kama ametoka usingizini.
"Kuna nini! Kuna nini kwani?" aliongea mlinzi huyo akiwa kama mtu aliyetoka usingizini.
"Aliyekuwa hapa ni nani?" Calvinjr aliuliza baada ya kugundua kijana huyo alimtambua vizuri maana alikuwa bosi wa bosi wake.
"Sikumbuki chochote kile, maana kwa mara ya mwisho nakumbuka kuna mtu aligonga mlango lakini nilivyo fungua sikuona mtu, sijaelewa tena kilicho endelea mpaka saivi nilivyo shtuka hapa" ilionekana kwamba mtu aliyekuwa kwenye hilo eneo alikuwa akifanya mambo yake kwa kasi mno na kwa ufanisi mkubwa.
Calvinjr aliamua kumuacha mlinzi huyo na kuelekea ndani ambako hakuwa na uhakika kama familia hiyo ilikuwa kwenye usalama ila kitu ambacho kilimshangaza sana ni baada ya kukuta mlango umefungwa kumaanisha kwamba hakuna mtu aliyekuwa ameingia hapo ndani kabisa.
Ina maana hata yule mgeni aliyepishana naye hakuingia ndani, sasa alikuwa amekuja kufanya nini? Hata yeye hakuelewa ila alikuwa akiikumbuka sana ile kauli ya kwamba kaa mbali na hii familia maana utailetea matatizo makubwa sana.
Calvinjr aligonga mlango huo ambao ulienda kufunguliwa na mama huyo moja kwa moja. Sebuleni palikuwa kimya sana ni wao wawili tu ndio ambao walikuwa hapo.
"Poleni sana kwa matatizo makubwa ambayo yameweza kuwatokea"
"Tunashukuru sana kwa hilo na samahani sana kwa kukusumbua maana hata mchana nimepata taarifa kwamba ulikuja kule, niseme tu asante kwa sababu mume wangu alibahatika sana kupata bosi mwenye moyo kama wako maana kwa majukumu uliyo nayo sikudhani kama unaweza kukubali kupoteza muda wako kwa sababu ya familia yetu"
"Huu msiba ni wetu sote, yule aliyekufa kwangu hakuwa mfanyakazi tu bali kwangu nilikuwa namuona kama baba. Amekuwa mwema kwangu siku zote na kutimiza majukumu yake kwa asili miamoja, hivyo mazishi yake kampuni itasimamia lakini pia mtalipwa stahiki zenu zote mpaka kesho asubuhi malipo yatakuwa tayari"
"Ahsante! sana mwanangu, MUNGU aendelee kukupigania siku zote. Mume wangu amekufa lakini kuna mambo ambayo siyo ya kawaida na siyaelewi, sijamwambia mtu yeyoye hata polisi nimewaambia sijui lolote maana siwaamini sana hivyo nikahitaji kukufikishia wewe ili uone ni sehemu gani unaweza kutusaidia" mama huyo aliweka kituo kidogo kabla ya kuendelea kumsimulia mwanaume huyo kwamba ni kipi hasa kilikuwa kinamtatiza au ni siri ipi ambayo alikuwa nayo kwenye moyo wake.
"Jana baada ya mume wangu kurudi nyumbani, kuna watu walifika hapa nyumbani..."
"Samahani unasema watu?"
"Ndiyo"
"Ikawaje?"
"Hawa watu walifika kule tulipokuwa tunaishi wakidai kwamba ni wageni wa mume wangu hivyo walihitaji kuongea naye na kufanya mazungumzo ya siri hivyo walitoka na kwenda upenuni mwa nyumba ambako huko walikaa kwa dakika thelatini tu kisha wakatoka. Baada ya kutoka kule mume wangu alikuja kuniaga kwamba anatoka mara moja na hao watu na angerudi baada ya muda fulani"
"Wakati anakuja kuniaga alirudi akiwa tofauti sana, maana hata hali yake ilionekana kubadilika na kuwa kama mtu aliye na wasiwasi isivyokuwa kawaida. Alinipa ishara ya kukataa jambo ila sikumuelewa maana watu wale walikuwa wamefika tulipokuwa tumesimama hivyo wakaongozana naye na kutoka wakiwa pamoja"
"Baada ya hapo mume wangu hakurudi tena mpaka asubuhi ambapo tulikesha kumsubiri, zimetoka taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna miili miwili imepatikana kwenye mtaro ikiwa imekufa, nilipata wasiwasi mkubwa kwa maana mume wangu alikuwa bado hajarudi tangu jana yake na simu yake alikuwa ameiacha nyumbani.
Baada ya kuona miili ile ndipo nikagundua kwamba alikuwa ni yeye na kijana ambaye alikuwa anafanya naye kazi kwenye kampuni yako" mama huyo alimaliza maelezo yake ambayo Calvinjr alikuwa akiyahitaji sana na ndiyo sababu kubwa ambayo alikuwa anaisubiri kwa hamu kubwa.
"Ulifanikiwa kuwaona hao watu?"
"Hapana sikufanikiwa kuwaona sura zao maana walikuwa wamejifunika na mashuka meusi kwenye miili yao mpaka usoni"
"Unasema walijifunika mashuka meusi?" Calvinjr aliuliza kwa mshangao kwa sababu dakika chache tu alitoka kupambana na mtu ambaye alikuwa ndani ya mavazi meusi kama ambayo alikuwa anayazungumzia mama huyo.
"Ndiyo"
"Je kuna ishara zozote kwa mumeo ambazo labda uliziona siku kadhaa kutoka kwake kabla ya kifo chake ambazo ulikuwa huzielewi?"
"Hapana mume wangu alikuwa muwazi sana hivyo kama kungekuwa na kitu cha tofauti basi mimi ni lazima angeniambia kwa namna yoyote ile, ila.....!" mama huyo akiwa anaendelea kueleza ni kama alikumbuka kuhusu jambo fulani ambalo lilimfanya agande akiwa kama anavuta kumbukumbu fulani za nyuma, Calvinjr alikuwa makini sana kumsikiliza.
"Nakumbuka siku chache kabla hajafa, aliniambia kwamba kuna jambo anahisi kwamba halipo sawa. Alidai kuna kitu kinamkumbusha sana maisha ya huko nyuma ambapo kuna mambo yaliwahi kufanyika kwenye nchi hii na huenda yakajirudia kwa mara nyingine tena. Aliniambia kwamba kuna mtu amemuona, anamkumbusha sana maisha yaliyopita japo hana uhakika sana ila atakapokuwa ana uhakika ataniambia"
"Hivyo nilikuwa nasubiri kwa hamu kubwa sana aweze kuniambia ni kitu gani hicho ila kwa bahati mbaya sana hajanambia chochote mpaka anafariki" mama huyo aliongea akiwa ameinama chini kwa maskitiko makubwa.
"Kuna mtu yeyote yule ambaye umeongea nae kuhusu hizi taarifa?"
"Hapana wewe ndiye mtu wa kwanza"
"Sasa kwa sasa cha kufanya, inatakiwa siri zote ambazo unazo kumhusu mumeo inabidi uzizike kwenye moyo wako na kifua chako, yaani usije ukathubutu kumwambia mtu yeyote mwingine kwa gharama yoyote ile.
Kama kuna mtu atakutafuta na kuhitaji kujua mwambie kwamba hakuna unalo lijua lolote lile, na kwa sasa usije ukanipigia simu kwa namna yoyote labda tu pale ambapo unahisi kwamba upo kwenye hatari ndipo nipigie simu haraka sana.
Nimefanya hivyo kwa sababu nahisi huenda kuna watu wanatufuatulia hivyo huu muda mimi nitautumia kufanya uchunguzi ili nijue tatizo liko wapi"
"Pesa zenu zote nawaingizia kwenye akaunti zenu asubuhi na kwa sasa najua mtakuwa chini ya jeshi la polisi hivyo jiangalie sana na uyazingatie niliyo kwambia kwa ajili ya usalama wa familia yako" Calvinjr alimaliza maongezi na mama huyo huku akiwa anaaga na kuondoka hilo eneo kichwani akiwa na mambo mengi sana ambayo alikuwa anajiuliza kuhusu hao watu wanaovaa hayo mashuka meusi na mambo ambayo yapo nyuma yao.
Episode ya 6 inafika mwisho.
Kalamu ni yangu mwenyewe,
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app