Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA AROBAINI NA NANE
SONGA NAYO................

“Mwanangu dunia ina mambo mengi mazuri, dunia ina kila kitu cha kupendeza lakini vitu vyote ni bure kama hauna watu wa kufurahia nao na watu pekee wa kufurahia nao ni familia na kwa sasa sisi tuna familia ndogo, nimebaki na wewe tu mwenye maisha yangu natamani kupata mtu wa kuishi naye, natamani mjukuu nicheze naye, natamani nikae na mkwe wangu karibu. Umri wangu unazidi kwenda, najihisi upweke kila iitwapo leo na nimechoka kukaa hivyo hivyo lengo la kukuita hapa ni kwamba leo mimi na wewe tunaongozana Singida kwenda kukutana na familia yako” mama huyo aliongea mambo mengi tena kwa uchungu mkubwa akiwa anazipanga na kuzifuta futa zile picha huku akitokwa machozi.

Gavin alikuwa pembeni akisikiliza kwa umakini kile kilichokuwa kinazungumzwa, mama huyo kwenye moyo wake alikuwa anapitia maumivu makali mno. Alikuwa na kila kitu lakini alikosa familia kubwa kwa wakati huo kwa sababu familia yake kuna watu ambao waliichukua. Alikuwa akijisikia vibaya sana kumuona mama huyo kwenye hali kama hiyo ndiyo maana watu wake alikuwa anawaua kikatili sana.
“Sawa mama, Sio muda Othman anaandaa helikopter tuende huko ukamuone mkweo na mjukuu wako” kauli hiyo ilimfanya mama huyo kurejesha tabasamu dogo ambalo lilififia kwenye uso wake. Tangu Gavin awe na familia, hakuwahi kabisa kukutana na familia hiyo na familia ya Gavin ilikuwa inajua bwana huyo alikuwa mwenyewe kwenye maisha yake yote tena mkewe akimjua kwa jina la Mike Tores.

“Ni jambo ambalo litanipa furaha sana, nimpikie mjukuu wangu, nicheze naye ili hata siku nikifa nife nikiwa na amani moyoni. Jambo ambalo unatakiwa kulifanya kwa sasa Gavin, nahitaji baada ya hapa hawa watu wote wafe, wameleta upweke kwenye maisha yangu nataka wote wafe, kila aliye husika na hili sihitaji kumuona tena kwenye maisha yangu” aliongea kwa hasira akiwa anamwangalia mwanae usoni, Gavin alimkumbatia mama yake na kumbusu kwenye paji la uso kisha akamuacha mama huyo aondoke kwenye hicho chumba akabaki mwenyewe.

Alikaa humo ndani kwa dakika kumi akatoka na kwenda kwenye chumba kingine, ndani ya chumba hicho walikuwepo wanaume watatu akiwepo Othman pamoja na mwanamke mmoja mrembo isivyokuwa kawaida ambaye alikuwa amekaa mbele ya komputa nyingi za gharama ambazo zilikuwa ndani ya chumba hicho.
“Boss kuna kitu tumekipata hapa” Othman aliongea akiwa anaigusa tablet yake na kumkonyeza yule mrembo kwa sababu kazi yote hiyo yeye ndiye ambaye aliifanya.
“Nakusikiliza” Othman hakuongea zaidi ya kuonyesha video kwenye skrini kubwa ambazo zilikuwa mbele yao. Kwenye skrini hizo zilionyesha ugeni kwenye nyumba ya Sarah, ni ile siku ambayo alitembelewa na Bashir, halikuonekana kuwa jambo la kawaida kwa sababu hata baada ya kulitafuta jina la yule bwana kwenye mfumo halikuwepo.
“Ni nani huyo mtu?” Gavin aliuliza
“Tumejaribu kuangalia kwa umakini jina lake linaonyesha kwamba aliwahi kuwa komando lakini baadae akaja kuondoshwa, hakuna taarifa zake zingine ambazo zipo” Gavin alisogea karibu kumtazama vizuri bwana huyo ambaye naye hakuonekana kuwa mtu wa kawaida.
“Mbona hamkunipa hizi taarifa mapema?”
“Mwanzoni tulihisi kwamba ni wapelelezi wa kawaida ambao walikuwa wanaenda kwake kwa sababu ya kutaka kujua yale ambayo yalitokea ndani ya ule msitu mpaka pale tulipogundua kwamba huyu alikuwa ni wa tofauti” Othman wakati anaeleza aliiruhusu ile video iendelee mpaka sehemu ambayo walikuwa wanapigana Sarah na mtu huyo na maneno ambayo alimwambia mwanamke huyo yalikuwa ni ya vitisho maana yake hakuwa salama.
“Huyu mtu ni muuaji kwa aina ya mapigo ambayo alikuwa anatembea nayo, kama ni muuaji kwa nini hakumuua? Maana yake kuna mtu alimuagiza pale kwa lengo maalumu” Gavin alitamka kwa sauti huku akitaka video zingine ziwekwe hapo za kwenye nyumba ya Sarah. Waliangalia kwa umakini mpaka wakati Sarah anaondoka ndani ya nyumba hiyo na hawakujua anaelekea wapi na usiku mzito namna hiyo.

Kulipokucha kuna wanaume waliingia ndani ya hiyo nyumba wakambeba mama yake na kuondoka naye. Baada ya Sarah kufika alionekana kupaniki na kuondoka akiwa anakimbia kuelekea kwenye gari yake baada ya hapo hakuonekana tena mpaka familia inarudishwa na watu wa aina ile ile. Jambo hilo lilimshtua Gavin.
“Hii familia ilirejeshwa ni kabla au baada ya kifo cha mke wa raisi?”
“Ni muda mfupi tu baada ya mke wa raisi kuuawa”
“Na Sarah hakuwepo nyumbani sio?”
“Ndiyo bosi”
“Oooooh shiiiit!” vijana wake wote waligeuka kumwangalia yeye baada ya kutamka hivyo.
“Kuna nini bosi?” ilisikika sauti laini ya yule mtoto wa kike
“Sarah ndiye ambaye ametumika kumuua mke wa raisi”
“Kivipi?”
“Kwa sababu yule ni moja kati ya wadunguaji hatari sana ambao jeshi limewazalisha kwa miaka ya hivi karibuni na hakuna mwingine ambaye angeweza kuifanya ile kazi kwa usahihi zaidi yake. Kuna siri ambayo mama hataki kuniambia ila ni yeye alikutana na mkuu wa majeshi kwa siri na kumpatia kazi hiyo ya kumuua mke wa raisi sasa hapa natakiwa kujua kwamba kuna kitu gani kati ya mama na mkuu wa majeshi mpaka amsikilize na kumfanyia kazi yake. Kwenye kuifanya kazi hiyo mkuu wa majeshi hakutaka kuhusika moja kwa moja ndiyo maana akamtumia Sarah kama karata yake ili amuuzie kesi. Kwa sasa maisha ya Sarah hayapo salama kabisa kwa sababu muda wowote anaweza kuuawa na kutupiwa hiyo kesi ili hata uchunguzi ukifanyika akutwe ni marehemu ndiye mhusika. Othman andaa helikopta naenda Singida na mama saivi ila wewe unatakiwa kwenda kuichukua familia ya Sarah na kuipeleka mahali salama kwa sababu kwa sasa anahitaji msaada wetu” Gavin aliligundua hilo baada ya kuunganisha matukio hayo.
“Roger that”
“Nikirudi nadhani ni muda mwafaka wa mimi kufahamiana na mkuu wa majeshi kiundani zaidi” alitamka akiwa anatoka kwenye hicho chumba ili aondoke na mama yake kama ambavyo alikuwa anataka.

*************
Norah alikuwa nyumbani kwake akiwa na mwanae, tangu mumewe aweze kuondoka kumwambia kwamba anaenda Botswana hakuwa amemtafuta hali ambayo ilimtia mashaka mengi juu ya safari hizo za mumewe. Alikuwa kama anapoteza imani kabisa na mumewe wa ndoa kwa sababu alikuwa anaona kama kuna mambo mengi hakuwa anayajua kwa baba wa mwanae lakini hakuelewa angeanzia wapi kulifuatilia hilo kwa sababu lingempotezeshea uaminifu kwa namna kubwa.
Akiwa ndani kwake wakati huo na mwanae akiwa anairudia rudia ile habari ya mauaji ndani ya jiji la Jozi alijikuta anahema na kuzidi kuwa na hofu kwenye moyo wake. Alipiga goti na mwanae na kuanza kusali ili kama kulikuwa na jambo ambalo halikuwa sawa Mungu aweze kuwaepushia mbali. Akiwa analifanya zoezi hilo aliisikia sauti ambayo ilimshtua na haikuwa kawaida ndani ya eneo hilo ila baada ya kutuliza akili vizuri aligundua kwamba haukuwa mlio wa sauti ya ndege bali helicopter.

Alikuwa ni askari hivyo kwake haikuwa kazi ngumu kuweza kulitambua jambo hilo, moyo ulipiga kite akiwa mwingi wa wasiwasi. Ni kwa muda mrefu tangu wahamie ndani ya eneo hilo hakuwahi kushuhudia mlio kama huo hata kwa bahati mbaya lakini siku hiyo alikuwa anausikia tena ukionekana kabisa kwamba ulikuwa unatua ndani ya uzio mkubwa wa nyumba yake. Alisogea kwenye dirisha na mwanae huku mtoto wake akiwa anaifurahia hali ile lakini yeye wala hakuwa na hamu, hakuona kama kuna mambo yalikuwa sawa, nani ambaye alimtembelea na ule usafiri? Hakuamini kama kulikuwa kwema hivyo aliibeba silaha yake na kufunua dirisha hilo kwa mbali ili kuweza kutazama kile ambacho kingefuata kwa wahusika wa ule usafiri.
Asalaleee!! Alishangaa anamuona mumewe akifunguliwa mlango na kushuka huku watu ambao waliufungua mlango huo wakiwa wanainama kutoa heshima wakiwa ndani ya mavazi meusi. Moyo wake ulikuwa unaenda mbio kana kwamba kuna mtu alikuwa anaukimbiza nyuma. Wote walisimama wakati anashuka mwanamke ambaye alikuwa na umri wa kiutu uzima, hakujua kama yule mwanamke ni nani hivyo akabaki ameduwaa huku mwanae akiita kwa nguvu na kukimbilia nje kumlaki baba yake ambaye alimpenda mno naye akawa hana namna zaidi ya kumfuata mwanae huko nje.
Mtoto alienda kumkumbatia baba yake, baada ya hapo baba yake alimtaka mtoto huyo kumsalimia kwa heshima mwanamke ambaye alikuwa pembeni akimwangalia mtoto huyo kwa furaha huku chozi likiwa linashuka taratibu kwenye mashavu yake. Alimbeba mtoto huyo wakati ambao mama yake pia alikuwa anatokezea kwa nje kuwaona watu hao, alimkimbilia mumewe na kumkumbatia huku mama huyo akimtua mtoto chini akimtaka mwanamke huyo ambaye ni kama alikuwa amepigwa na bumbuwazi akiwa bado haelewi jambo lolote ambalo lilikuwa linatokea ndani ya hilo eneo aweze kumsalimia.
“Tuna mengi ya kuongea mke wangu ndiyo maana leo nimekuja na mama”
“Mama?”
“Ndiyo”
“Sijakuelewa ulisema hauna wazazi kabisa”
“Jibu linaweza kuwa kweli au si kweli, naomba twende ndani, leo nataka uujue ukweli kwamba mimi ni nani” mkewe alibaki ameduwaa, ni kama alikuwa anasimuliwa hadithi za kwenye riwaya lakini haikuwa hivyo, mbele yake ambaye alikuwa anaongea alikuwa ni mumewe halali wa ndoa na kwa pamoja walifanikiwa kupata mtoto wa kike.

Mama yake wakati wote alikuwa amembeba mjukuu, nyumba hiyo kwa nje walikaa wanaume kadhaa ambao walikuja na mumewe lakini kuna watu alihisi wameongezeka na hawakueleweka wametokea wapi muda mfupi tangu mumewe aje na huo ugeni hapo. Walikaa kwenye sebule kubwa kwa ajili ya kufanya mazungumzo.

Sehemu ya arobaini na nane inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA AROBAINI NA TISA
SONGA NAYO................

“Umsamehe mumeo kama nimevamia hapa bila ridhaa yako lakini ni mimi ambaye nilitaka kuwafahamu, imeniuma sana kuishi bila kupata hata muda wa kuwa na mjukuu wangu lakini nilikosa japo muda kidogo wa kuweza kukufahamu wewe, jambo hili niliona kama linanitesa kwenye moyo wangu ndiyo maana leo nipo hapa”
“Wewe ni nani?”
“Kuwa mpole binti yangu, leo nipo hapa mimi mwenyewe nitakuelekeza kila kitu ambacho unapaswa kukifahamu” maneno ya mama huyo yalimuacha mdomo wazi Norah, aligeuka kumwangalia mumewe lakini mwanaume huyo alikuwa amekaa dirishani akiwa anatazama nje kana kwamba hakuwepo humo ndani. Mama huyo alitulia kidogo na kuanza kumfungukia mkwewe sasa ili amjue mumewe.
“Kwanza umsamehe mumeo na mimi kwa ujumla kwa sababu hakuna kitu unacho kijua kutoka kwake, kila ambacho unahisi unakifahamu ni uongo. Haujui lolote kuhusu maisha yake, haulijui hata jina lake tu hivyo kiufupi ni kwamba hakuna kitu unakifahamu kutoka kwake ila kuanzia leo unaweza ukafahamu kila ambalo limejificha”
“Kwanza mumeo jina lake sio Mike Tores kama ambavyo unamfahamu wewe, mumeo jina lake halisi anaitwa Gavin Luca, ni mt……..” mama huyo alikatishwa na mkwewe ambaye alianza kwenda sawa na zile wasiwasi zake za tangu mwanzo.
“Samahani umesema anaitwa?”
“Gavin Luca”
“Unataka kuniambia baba wa mtoto wangu ndiye muuaji ambaye anatafutwa sana na kudaiwa kufanya mauaji ya kikatili kwa viongozi wakubwa wa taifa hili?”
“Ndiyo”
“Hapana, hapana, why?”
“Ndiyo maana nimekwambia uwe mpole unisikilize binti yangu kwa sababu kila kitu utakifahamu leo”
“Kwanini aishi na mimi kwenye maisha ya uongo? Why Mike?”
“Kwa sababu kama mngejulikana na ungeujua ukweli wake basi wewe na mtoto maisha yenu yangekuwa kwenye hatari kubwa. Alifanya haya ili kuwalinda wewe na mtoto na kwa leo kwa sababu unaenda kujua kila kitu basi hata kazi yako ndio utakuwa mwisho wako kuifanya”
“Hahahaha bado unataka kuniamulia maamuzi baada ya haya maisha ya maigizo ambayo nimeyaishi kwa hii miaka?”
“Sidhani kama una chaguo lingine Norah”
“Unataka kuniambia natakiwa kufuata kile ambacho unakitaka?”
“Kwa ajili ya mjukuu wangu! Jibu ni ndiyo”
“Mjukuu wako? Mjukuu wako ambaye hata haujui anakula nini, haujui amekuaje mpaka kufika hapo, leo hauoni hata aibu kumuita mjukuu wako kwa maisha yote ya maigizo ambayo nimekuwa nayaishi kwa muda wote huu na mtu ambaye silijui hata jina lake?”
“Una uhakika kwamba sijui mjukuu wangu anakula nini? Una uhakika kwamba sijui mjukuu wangu huwa anaishije? Huyu ndiye mtoto ambaye analindwa zaidi ndani ya taifa hili leo unaniuliza kama najua kakuaje? Unahisi nimejuaje kama Gavin ana familia? Kitu pekee ambacho nilikuwa nakikosa ni kuwa karibu na mjukuu wangu hivyo haijalishi unahitaji kunisikiliza au hauhitaji ila hisia zako haziwezi kufanya nikamuingiza mjukuu wangu kwenye hatari ya kifo nikaishia kumpoteza”
“Mwanangu ndiye mtoto ambaye analindwa zaidi ndani ya taifa hili? Unahisi tupo kwenye maigizo hapa?”

“Binti yangu nisikilize, Gavin asingeruhusu wewe na mtoto muishi kwenye mazingira hatari. Wewe hapo kuna watu ambao huwa wanakulinda kwa masaa ishirini na manne ya siku ndiyo maana wakati tunaingia hapa umeona kuna watu wanaongezeka lakini hata mtoto analindwa kila mahali ambapo anakuwepo ila watu ambao wanamlinda wewe huwezi kuwafahamu. Huyu ndiye future ya hii familia hivyo tusingeruhusu aishi maisha ya pekeyake bila ulinzi ingekuwa ni hatari kama kuna siku angefahamika”
“Kwahiyo mwanao muuaji, na wewe ndiye ambaye ulikuwa unaibariki kazi yake, leo unakuja hapa kuanza kunitongoza ili na mimi niwabariki kwa huo ushenzi ambao mnaufanya. Kumbuka unaongea na askari hapa na hili jambo nilitakiwa kulifikisha kwenye mamlaka husika lakini kwa heshima yake kama baba wa mwanangu naombeni sana muondoke kwenye maisha yangu na mhesabie kama hatukuwahi kuonana kabla. Siwezi kuishi na watu ambao ni wauaji” Norah aliongea kwa jazba akiwa anaanza kutoka ndani ya hilo eneo.
“Siku mwanao akiuawa mbele ya macho yako bado utakuwa na misimamo ya kipuuzi namna hiyo?” Norah aligeuka baada ya kuisikia kauli nzito hiyo kutoka kwa mama mkwe wake.
“Hakuna mtu ambaye anaweza kumuua mwanangu nikiwa hai”
“Kafa mke wa raisi ambaye analindwa kuliko mwanamke yeyote hapa nchini halafu wewe hapo ndo unaamini kwamba utamlinda Lionela? Mjukuu wangu haendi popote na siwezi kuruhusu kuipoteza familia yangu kama nilivyo wapoteza huko nyuma. Unahisi kwamba Gavin alipenda kuwa muuaji? Unahisi sisi tunayapenda haya maisha ambayo tunaishi bibie? Huyo hapo alipo aliwapoteza watu wote kwenye maisha yake na kubakiwa na watu wa kuhesabu tu, hawakupotezwa na Mungu bali ni wanadamu kadhaa ambao waliamua kuyabeba maisha yao. Unahisi kwamba wewe ndiye pekee mwenye uchungu? Hujui hata maumivu ya kumpoteza mtoto ambaye umemzaa mwenyewe tena kwa uchungu ila maamuzi yako ya kipuuzi ndiyo yatafanya umpoteze Lionela jambo ambalo siwezi kuliruhusu kufanyika. Kaa unisikilize umjue mumeo halafu baada ya hapo kama utaamua kuondoka basi mimi nitakuruhusu na hakuna mtu atakuja kukusogelea kwenye maisha yako yote kutoka kwenye familia yangu” mama huyo alioongea kwa ukali na kufoka baada ya kuona binti huyo ni kama anataka kubembelezwa sana na jambo hilo hakuwa tayari kuweza kulifanya.

Norah akiwa anajivuta alirudi na kukaa tena kwa mara nyingine, alikuwa mpole kwa sababu hakuwa anajua anadili na watu wa namna gani na maneno ambayo aliambiwa yalikuwa ni maelezo tosha kwamba watu hao walikuwa wamepitia mambo mengi kwenye maisha yao.
“Najua mpaka wakati huu huwa unatamani kujua kazi rasmi za mumeo ambazo anazifanya kumuingizia kipato kikubwa kwa sababu nina uhakika tangu uolewe naye haujawahi kupata shida ya kitu unacho kihitaji, hata kama utahitaji nini basi lazima utapatiwa kwa muda mwafaka, licha ya kukudanganya na baadhi ya kazi ambazo sizo za kweli lakini hilo halihalalishi kwamba alikuwa anakwambia ukweli”
“Mpaka hivi ninavyo ongea na wewe, baba mtoto wako ndiye mtu tajiri zaidi ndani ya bara zima la Afrika. Ana utajiri ambao hata akiamua kulilisha taifa zima watu wanaweza kula kwa miaka zaidi ya kumi na bado pesa zisiishe ukizingia na bajeti ya watanzania ilivyo ndogo kwenye matumizi yao ya kila siku. Najua utakuwa unajiuliza kwamba huo utajiri kaupatia wapi. Nakurudisha miaka ya huko nyuma ili uweze kunielewa vyema”
“Tanzania ilipata kuwa na mtu mmoja ambaye alivuma sana miaka ya huko nyuma, vitabu vya historia vimeliandika jina lake, nyaraka za serikali zimeliandika jina lake tena kwa kulichafua isivyokuwa kawaida, mtu huyo jina lake kamili alipata kuitwa Lucas Antony. Mpaka hapo huenda umesha likumbuka jina lake kwamba huyo alikuwa ni mfanya biashara maarufu ambaye mara kadhaa aliwahi kuhusishwa na biashara ya madawa ya kulevya, ni huyo huyo ambaye najua uliwahi kusikia kwamba amejenga mji wake kwa ajili ya familia yake na watu wake”
“Usisahau ndiye mtu ambaye aliikomboa nchi ikiwa kwenye hali mbaya ya kufilisika kwa kutoa zaidi ya dola za kimarekani bilioni kumi ili kuhakikisha taifa linarudi kwenye hali yake, ni huyo huyo ambaye amewasaidia zaidi ya watanzania milioni thelathini kabla ya kufa kwake na kuondoka hapa duniani. Huyo mwanaume ambaye mimi namzungumzia hapa ndiye baba mzazi wa baba wa mwanao yaani babu wa LIONELA”

“Mwanaume huyo alizaliwa kwenye maisha ya kifukara mno, maisha ya hali ya chini sana ambayo yalimfanya kukosa kila alichokuwa anakihitaji. Aliwapoteza wazazi wake kwa kukosa pesa ndogo kwa ajili ya matibabu yao lakini pia alimkosa mtu ampendae kwa sababu alishindwa kuendana na gharama za maisha. Jambo hilo lilimpa hasira dhidi ya umaskini na ndiyo sababu ambayo ilimsukuma na kumfanya kujiapia kuutafuta utajiri kwa namna yoyote ile, ndipo safari yake ya kuingia kwenye viunga vya mitaa ya PEENUGA ilipo anzia hapo”

Sehemu ya 49 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI
SONGA NAYO................

“Alienda kwenye hiyo mitaa kwa sababu kuishi huko hakukumhitaji mtu awe na elimu bali akili na maarifa ya mtaani, kulikuwa kunawafaa watu ambao hawakuzoea kudeka na huko ndiko alienda kujifunza mambo yote hayo mpaka kuja kuibukia kuwa mtu maarufu zaidi ndani ya Tanzania. Alikutana na mfanya biashara wa dawa za kulevya na bwana huyo ndiye alimfungulia milango ya maisha na kumbadilisha kwa kila kitu. Baada ya kuwa mwanaume ambaye alisimama kwa kila kitu ndipo aliamua kuja na mji wake ambao umebaki kuwa historia kubwa baina ya sisi wana familia.

Ile mitaa mipya kwake ambayo ilimpa umaarufu pia ilimsaidia yeye kupata mke, mke ambaye ndiye mama mzazi wa hawa watoto. Nasema watoto kwa sababu Gavin au Mike kama ambavyo unamjua wewe hakuzaliwa mwenyewe bali walizaliwa wawili wakiwa mapacha. Kuzaliwa kwa hawa watoto wawili lilikuwa jambo la furaha mno kwa yule tajiri lakini ilikuwa ni hatari pia kwake kama watoto hao wangefahamika kwa baadhi ya watu, kulikuwa na hatari kubwa ya kuja kuwakosa kwa baadae ndipo yakafanyika maamuzi magumu.
Maamuzi ambayo yalifanyika ni kwamba ilitakiwa mtoto mmoja atolewe yaani asilelewe na wao bali alelewe nje ili iwe rahisi kuwalinda ikitokea siku watu wakija kuujua ukweli kuhusu watoto hao, sasa hapo ndipo nilipo ingia mimi na kwenda kuwa mama wa Gavin. Mimi nilikuwa kanali wa jeshi ila mume wangu alikuwa mfanya biashara ambaye alikuwa na ukaribu mkubwa na baba yake Gavin hivyo walimshawishi yeye wakati najifungua ilidaiwa kwamba nimejifungua mapacha hivyo mimi nikajua kwamba nina watoto wawili mpaka baada ya mwaka mmoja ndipo nilikuja kuujua ukweli.

Ukweli ambao mimi niliujua kwa mara ya kwanza nilipingana nao kabisa mpaka alipokuja daktari kuthibitisha hilo ndipo nikakubali, nilielekezwa sababu za msingi za wao kufanya jambo lile. Moja kati ya sababu za msingi ambazo ziliwafanya wanitumie mimi nikiwa kanali ni kwa sababu walijua kwangu ni ngumu mtu yeyote wa nje kuweza kunishtukia hivyo jambo hilo likawa rahisi mno mpaka pale ambapo Gavin alitakiwa kusafiri kwenda nje ya nchi akiwa bado mdogo kabisa. Hakuna mtu ambaye alifuatilia ukweli wa wanangu tena kwa baadae kwa sababu baada ya Gavin kutoka nje tulitengeneza tukio ionekane kwamba mwanangu mmoja alikuwa amekufa.

Huko nje mimi ndiye ambaye nilikuwa nasafiri mara kwa mara kwa siri kuwa karibu naye kwa sababu wazazi wake walikuwa wanaonana naye kwa manati sana ukizingatia baba yake alijua kabisa kuna watu wanamfuatilia yeye ili kumdondosha na kama wangekuja kujua ukweli wa hao watoto basi wangeutumia kumdondosha. Ameishi kwenye nchi ishirini na tano hapa duniani ila taifa ambalo liliyabadilisha maisha yake na kumfanya kuwa binadamu hatari kama ambavyo wewe unamuona kwa sasa alivyo ni China.

Baba yake hakutaka siku yakija kutokea matatizo kwa mtoto huyu aje akosekane wa kumlinda kwani alikuwa naye mbali, mmoja ambaye alikuwa naye karibu ilikuwa ni rahisi kumlinda hivyo wakati huo ndipo alitengenezwa mtu aliyekuwa anazunguka naye kila pembe ya dunia kubadilisha mazingira ili wasije kueleweka kwamba waliwahi kuishi wapi na waliwahi kufanya nini na huyo mtu ndiye ambaye alitutengenezea huyu kijana ambaye yupo mbele yako. Gavin ameitumia robo tatu ya maisha yake kufanya mazoezi hatari, mazoezi ambayo ilikuwa ni amri kutoka kwa baba yake akiamini kwamba ingefika siku moja mtoto huyu angekuja kuwa msaada kwa kuilinda familia yake baadae.

Safari yao hiyo ya kumtengeneza ilienda kuishia china ndani ya kijiji kimoja kilichokuwa pembezoni, ndani ya kijiji hicho inaaminiwa zaidi miungu, watu wana imani ambazo zimevuka mipaka kiasi kwamba wewe ukiona lazima utahisi ni uchawi ila wao wanaamini kwamba hizo ni imani tu na kupitia imani jambo lolote lile ambalo unalitaka linaweza kuwa. Huko Gavin alipikwa kwenye mapigano ya hatari ya kila aina lakini wakati anamaliza mafunzo ambayo yalimchukua miaka mitano kuweza kuyakamilisha, alikuwa mwanafunzo bora kwa mwalimu wake hivyo kuna kitu alimpatia ambacho kinamfanya kuwa binadamu hatari zaidi kuwahi kuishi duniani.

The Fengdu Ghost city, china.
Huu ni mji wa mizimu ambao unapatikana huko mashariki mwa Han, watu ambao wanaishi kwenye hilo eneo huwa wanaamini kwamba kuna maisha baada ya kifo.
Watu hawa wanaamini imani za dini tatu, ya kwanza ni Taoism. Hii inaunganishwa moja kwa moja na mwanafalsafa Lao Tzu ambaye mwaka 500 B.c.E aliandika kitabu kikuu cha misingi ya Taoism. Imani hii inaelezea kwamba binadamu na wanyama wanatakiwa kuishi kwa kubalansi uhalisia wa ulimwengu ambapo imani hii inaamini juu ya uhai wa nafsi, yaani nafsi haifi na huwa inaungana na ulimwengu mwingine baada ya mwili kufa.
Imani ya pili ni confusianism ambayo inaamini kwenye kufa pamoja na kuheshimu sheria na imani za jamii na mazingira yake. Imani ya tatu ni Buddism, hawa wanaamini kwenye zile falsafa za kitamaduni na mafundisho yake, ni dini ya nne kwa ukubwa duniani na hawa ndio haswa wale ambao waliitambulisha tahajudi kwenye kuuweka mwili na akili ya mwanadamu sawa, tahajudi hizo zimekuwa msingi wa ulimwengu hususani pale mtu anapokuwa kwenye hali mbaya kiakili au anazongwa na mambo mengi yanayo athiri afya ya akili yake na utulivu.

Kwenye huo mji ndiko ambako alienda kuishi Gavin, aliishi kwenye huo mji wa mizimu akijifunza ustaarabu na maisha kwa ujumla. Huko aliwasoma wanadamu akiwa anaendelea kupewa mafunzo makali baada ya miaka miwili ndipo alikutana na huyo mtu ambaye kwa mara ya kwanza alimpatia nguvu za ajabu baada ya kuhakikisha ameiva mno kwenye dunia ya mapigano lakini iso hivyo tu bali hata namna ya kuyamudu na kuyaishi mazingira, namna ya kuweza kuheshimu taratibu ambazo zimewekwa sehemu fulani na kuziishi, kuishi bila kuonea watu wengine ambao walikuwa hawana hatia na watu wa aina yake hawaruhusiwi kupigana bila sababu kubwa za msingi kama akikutwa anafanya hivyo kuna hatari kubwa ya yeye kuweza kuuawa na viongozi wake.

Huyo mtu alisafiri kutoka mbali kwenda ndani ya eneo hilo ambapo alikuwa anafanya hivyo kila baada ya miaka kadhaa na mwaka huo ambao alienda ni mwaka ambao ndio Gavin alikuwa amemaliza mafunzo yote na kuwa mwanafunzi bora kwenye kila daraja. Wakati huo alikuwa anaweza kupigana na mtu yeyote yule mbele yake lakini hakuwahi kuwa na nguvu za ziada kwenye mwili wake. Liang zu ndiye ambaye alifika ndani ya huo mji wa mizimu pembezoni mwa mapango na maporomoko makubwa ya maji, ndani ya mji huo ndipo kilipokuwepo hicho chuo kidogo cha hayo mafunzo.

Mtu huyo alikuwa mzee sana, ndiye ambaye alikuwa mlinzi wa nguvu za ajabu ambazo zilihifadhiwa kwenye upanga mmoja uliokuwa unalindwa kuliko hata maisha ya wanadamu ambao walikuwa wanaishi kawaida. Upanga huo ulikuwa na nguvu za ajabu ambazo historia yake ilianzia karne ya 16 huko kwa kiumbe kimoja ambacho kiliaminika kuwa shetani. Beigujing, huyu ni shetani ambaye alielezewa vizuri zaidi kwenye riwaya iitwayo JOURNEY TO THE WEST yaani safari ya kwenda magharibi.

Ulikuwa ni mzimu wa kike ambao ulifahamika zaidi kwa jina la white bone spirit. Ulikuwa ni mzimu wa kike ambao baada ya kufa kwa baadae nguvu yake ilichukuliwa na wataalamu wa mambo ya imani za kitamaduni ambapo walikusanya nguvu hizo pamoja na za viumbe wengine hatari ambao walipata kuishi huko china. Lengo kubwa la kuzibeba nguvu hizo ilikuwa ni kuweza kuzitunza kwa ajili ya matumizi mazuri ya baadae ya taifa hilo hususani kama lingeingia kwenye wakati mgumu au kwenye hali ambayo ingelipelekea kuwa kwenye taharuki kubwa.
Lakini kwa bahati mbaya nguvu hizo zilikuja kutua kwenye mkono wa bwana mmoja ambaye alipata kuitwa Yuan ji sheng, bwana huyo alizitumia kwa manufaa yake binafsi na kuulia watu wengi sana kiasi kwamba wahusika wakawa wanajuta kuzipa mwanya wa kuingia kwa mtu mwingine. Walimtafuta bwana huyo na kumuua kisha wakaubeba upanga ambao ndio zilitumika kutunzwa nguvu hizo na kwenda kuuficha mahali pa siri ili usije ukaja kutumika na mtu mwingine wala kutua kwenye mikono ya watu ambao sio sahihi kwa mara nyingine tena.

50 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA MOJA
SONGA NAYO................

Sasa kwa miaka takribani miatano, ule upanga ulikuwa unapita kwenye vizazi mbali mbali ambavyo vilikuwa vinakula kiapo cha kuutunza kuanzia hiyo karne ya kumi na sita mpaka karne ya ishirini na moja ambapo siri hizo zilikuja kuvuja. Ilikuwa ni siri kubwa juu ya ule upanga na nguvu zake ambazo zilikuwa ndani yake, zile nguvu kama mtu ambaye angekuja kuwa nazo angefanikiwa kuzimudu vizuri basi angekuja kuwa msaada na mlinda amani wa ulimwengu ila kama nguvu hizo zingekuja kuingia kwenye mkono wa mtu ambaye siye basi huyo ndiye angekuja kuuvuruga ulimwengu kwa namna ambayo angeitaka yeye mwenyewe.

Sasa ile siri juu ya silaha ile haikubaki kuwa siri tena, kuna watu ambao walizipata habari zake hivyo wakawa wana mpango wa kuweza kuuiba ili waweze kufanya kile ambacho wanakitaka. Yule mzee ambaye ndiye alikuwa mlinzi, umri wake ulizidi kwenda na hakuwahi kuona mtu sahihi wa kuweza kumpa yale madaraka kwa sababu wengi walionekana kuwa na tamaa na kufeli kila mitihani ya imani ambayo alikuwa anawapa ili aweze kuwakabidhi silaha hiyo. Akiwa kwenye hofu kubwa ndipo alipo sikia kwamba kuna mwanafunzi ambaye alikuwa mgeni ndani ya taifa lile aliyekuwa amefauu mafunzo yake yote hivyo alitakiwa kuja kumuona kama kawaida ambavyo alikuwa anataka kuwakagua vijana ambao walikuwa wanafanikiwa kumaliza mafunzo hayo.

Hiyo ndiyo sababu ambayo ilimfanya mzee huyo asafiri maili nyingi mpaka ndani ya eneo hilo kumuona kijana huyo aliyekuwa amepewa taarifa zake. Safari yake ilijumuisha na ule upanga wa siri ambao kwa karne nyingi ulikuwa unalindwa kuhakikisha taifa lao linabaki salama. Ndiyo kwa mara ya kwanza alikutana na mumeo wa ndoa na baba mtoto wako ambaye unamuona hapo dirishani na kukaa nae kujua kama alikuwa ameiva kweli. Alikuwa ni mwanafunzi wa kipekee kabisa kuwahi kumuona, alikaa naye kwa muda ndani ya lile eneo akiwa anamfundisha namna ya kuweza kuzimudu nguvu za asili kwenye mwili wake na namna ya kuweza kuishi nazo bila kuleta madhara kwa watu wengine.

Alimpa onyo juu ya madhara makubwa ya kuweza kuzitumia nguvu hizo kwa matumizi ambayo hayafai kwa wanadamu kwa sababu zilitunzwa ili kuja kuwa na matumizi ya kulilinda taifa lao na kuulinda ulimwengu ila kama angekuja kuzitumia vibaya basi kulikuwa na asilimia nyingi za yeye kuweza kuwa shetani kabisa na asingekuja kurudi kwenye hali ya ubinadamu maisha yake yote.
Baada ya kuwa na uhakika ndipo alifanya maamuzi ya kuziingiza nguvu hizo kwenye mwili wa mumeo na kumkabidhi huo upanga, nguvu hizo ziliingiziwa kwenye upande wake wa ubavu wa kulia ndiyo maana mpaka leo hilo eneo huwa halitakiwi kuguswa na kitu chenye nguvu ama ncha kali kwa sababu ni hatari sana. Norah hii ni siri ambayo nakupa haitakiwi kwenda kwa mtu mwingine yeyote yule kwa sababu hili jambo linaweza kuja kuvuruga amani ya ulimwengu mzima na sio Tanzania tu, siri ya hizi nguvu zake za ajabu tunayo watu watatu tu na wewe sasa unaenda kuwa mtu wa nne.

Maamuzi ya kumpatia nguvu hizi Gavin yalifanywa na mzee huyo baada ya kugundua kwamba Gavin muda mfupi alitakiwa kurudi Tanzania hivyo angekuwa mbali na mizimu ambayo waliamini kwamba ilikuwa inazisimamia nguvu hizo, kwa maana hiyo kama angekuwa mbali basi nguvu yake pia isingekuwa kubwa ukitofautisha kama angekuwa nazo mtu wa karibu. Pili alifanikiwa kwenye mafunzo yote kwa asilimia zote miamoja hivyo hakukuwa na shaka juu ya hilo lakini sababu nyingine kubwa ni kwamba mzee huyo hakutaka nguvu hizo zije kupatikana kwa mtu yeyote wale watu wa huko waje kujua kwamba zilikuwa zimeenda wapi hata kama siku wangefanikiwa kumuua yeye.

Alijua nguvu hizo zingekuja kuwa salama kwenye mwili wa Gavin ambaye alisisitizwa mno na kula viapo vikali juu ya matumizi yake lakini mzee huyo alimpa elimu ya namna ya kuzitumia nguvu hizo kwa asilimia ndogo ila zingekuwa zinazidi kuongezeka nguvu kadri miaka ilivyokuwa inazidi kwenda, hakutakiwa kuzitumia kwa muda mrefu sana tena akiwa na hasira kali kwa sababu yangekuja kutokea mambo makubwa na ya kutisha na ndio ukawa mwanzo wa kukitengenza kiumbe cha kutisha ambacho muda mwingi kimeishi kwenye mikono yangu na mimi ndiye nimemkuza huyu mtoto.

Baada ya pale ndipo ilianza safari ya kurudi Tanzania na baada ya kurudi Tanzania ndipo ulikuwa umeandaliwa mpango mkubwa wa kuuawa kwa familia yake ambayo ilikuwa na maadui kila kona. Ujio wake ulikuja na mambo mengi sana, familia yake iliuawa, pacha wake aliuawa ile hali ilimuathiri kiasi kwamba alishindwa kuweza kuzizuia zile nguvu zake akaanza kuzitumia. Mara ya kwanza aliua watu miamoja tukahisi ni kawaida ataweza kuzimudu lakini kwa mara ya pili aliua watu miambili na hamsini na ilikuwa inaenda kumshinda kabisa hali ya kuhimili kuzimudu zile nguvu hivyo haraka nikaondoka naye na kwenda kuishi pangoni huko maporini ambako tulikaa mwaka mzima baila kuonekana wala kuwasiliana na mtu yeyote yule.

Bahati ilikuwa mbaya mno kwa upande wangu kwa sababu wakati ule narudi, nilikutana na habari nyingine mbaya. Mwanangu wa kumzaa na mume wangu walikuwa wameuawa pembezoni mwa bahari sehemu ambayo nimetumia miaka yangu mingi sana kwenda mara kwa mara. Kwa wakati ule Gavin hali yake ilikuwa imerudi kama kawaida baada ya ule mwaka mmoja na hapo alianza kuwatafuta watu ambao walihusika kwenye mauaji ya zile familia zetu. Jina lake lilikuja kuwa maarufu miongoni mwa baadhi ya watu, lilifahamika hususani kwa wale watu ambao alikuwa anawatafuta.

Wengi walijua yule ndugu yake ndiye alikuwa yeye hivyo walikuwa na uhakika kabisa kwamba wamemmaliza lakini haikuwa hivyo, baadae walijisahau na kustarehe akarudi na kuua mtu mmoja mmoja huku akiwa anamtafuta mtu ambaye alikuwa nyuma yuma ya lile jambo. Hali hiyo ilipelekea yeye kuanza kuwaua wale watu kwa mahesabu kwanza, mwanzoni ilikuwa ni ngumu kumpata hata mmoja kwa namna walivyokuwa makini kwenye ufanyaji wa hayo matukio yao na usiri mkubwa uliokuwa umetawala baina yao.

Walitumia miaka mitano kulisaka jina hilo hususani baada ya kugundua kwamba kuna mtu mwingine alikuwa anajiita Gavin Luca, kwa imani ya walihisi kwamba ni mtu mwingine aliyekuwa anautafuta umaarufu mpaka siku ambayo juzi hapa walimkamata mtu mwingine aliyetengenezwa kama mtego wakihisi ni Gavin mwenyewe, yule mtu ndiye ambae alianza kutupa mrejesho wa wahusika ambao walikuwa wamejificha nyuma ya pazia. Hivyo mpaka unamuona mumeo wakati huu anafanya haya mauaji ujue ni harakati za muda mrefu ila wahusika wameanza kupatikana kwa sasa.
Uzuri ni kwamba hajatumia nguvu zake kwa sasa jambo ambalo linaifanya amani iendelee kuwepo ila hata mimi sijui ni kitu gani kitatokea kama itakuja kutokea akawa hana uwezo wa kuzimudu hizo nguvu zilizopo kwenye mwili wake kwani hata mimi inawezekana nisiwe na uwezo wa kumzuia kufanya kile ambacho atakitaka yeye. Huyo ndiyo mumeo na baba wa mtoto wako Norah na jina lake halisi sio Mike Tores, mwanangu anaitwa GAVIN LucA”.

Norah alikuwa ameganda kama sanamu, hakuwa ameongea neno lolote lile mpaka wakati huo kwa sababu simulizi ambayo alipewa ilikuwa inatisha mno, mtu ambaye alikuwa anazungumziwa kwenye simulizi hiyo hakuamini kama ndiye huyo ambaye yeye alikuwa akilala naye kitanda kimoja.
Gavin hakuwa binadamu wa kawaida kama ambavyo alikuwa anamuona yeye kwenye macho yake, kilikuwa kiumbe cha ajabu na cha kutisha mno. Mwanamke huyo alibaki analia, alikuwa analia kwa sababu ya kuishi na mtu ambaye hakufanikiwa kumjua kwa lolote lile, maisha yake yote yalikuwa ni ya uongo. Lakini pia simulizi ambayo aliipata kuhusu maisha ya familia ya bwana huyo ilimhudhunisha. Hakuhitaji kuongea jambo lolote lile alikubali kuondoka naye hilo eneo kwa ahadi kwamba baada ya kufika huko alitaka yeye na mumewe wakae pekeyao kwa ajili ya kuzungumza jambo hilo kwa sababu hakuwa na uhakika tena kama mwanaume huyo alikuwa hata anampenda.

51 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA HAMSINI NA MBILI
SONGA NAYO................

******
Sarah alikuwa kama amechanganyikiwa, ni kwa muda mfupi tu maisha mambo yalikuwa yanambadilikia. Mama yake hakuwa anamuelewa mpaka wakati huo, walikuwa kwenye mzozo baada ya mama huyo kugundua kwamba mwanae alikuwa amehusika kwenye mauaji ya mke wa raisi wa nchi, kwake jambo hilo aliliona kama baya na hatari kwa familia yake ndiyo maana hakuwa kabisa kwenye hali ya utulivu.
Alihisi mwanae huyo alikuwa akijihusisha na mambo mabaya, kama mama jambo hilo lilimfanya ajisikie vibaya kwa sababu mwisho wa familia yao ulikuwa unaonekana kabisa kuwa mbaya. Ni muda ulikuwa umepita tangu afanikishe kulitekeleza tukio hilo ambalo alilifanya kwa ajili ya familia yake lakini aliishia kupata lawama tu. Ni kawaida muda mwingine kwa mwanadamu kukubali kupokea lawama lakini jambo la mhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba familia ipo salama na ndilo jambo ambalo yeye binafsi alikuwa akilizingatia zaidi.
Alikuwa mpweke mno, alikuwa amekaa karibu na dirisha akiwa anatazama mbalamwezi zilivyokuwa zimeupamba mlima Kilimanjaro, akiwa hapo anavuta sigara yake taratibu kupunguza mawazo ambayo yalikuwa yanamzonga kwenye jumba lake hilo umeme ulikatika ghafla na kurudi, haikuwa kawaida, hata siku moja nyumba yake haikuwahi kukutana na tatizo la namna hiyo hivyo alishtuka kidogo kisha akatulia tena na kuhisi huenda lilikuwa ni wenge lake.
Wakati amekaa tu simu yake ilianza kuita ikabidi aitoe mfukoni ndipo aligundua kwamba ilikuwa inaita, kuita kwa simu hiyo ndiko kulimpa umakini na kumshtua. Simu ilitoka kwa Nick, mwanaume ambaye walikuwa wameanzisha naye mahusiano muda mfupi uliokuwa umepita, haikuwa kawaida kabisa mtu huyo kumtafuta muda kama huo hivyo moja kwa moja aligundua kabisa kwamba hapakuwa sawa, ni lazima kulikuwa na tatizo mahali. Aliipokea simu hiyo.
“Nick kwema?”
“sina imani Sarah, unaweza ukaniambia uko wapi muda huu?”
“Leo sijatoka nipo ndani”
“Upo na familia?”
“Wao wamelala”
“Basi naomba uje unifungulie mara moja” alishtuka baada ya kugundua kwamba bwana huyo alikuwa amefika kwake majira hayo, hakuwa na kumbukumbu kabisa kama kwenye maisha yake kama aliwahi kumuelekeza kwake ni wapi, sasa alipajuaje? Akiwa anajiuliza swali hilo gumu ambalo hakuwa na jibu lake kwa wakati huo aligundua kwamba bado simu ilikuwa hewani hivyo akajichekesha na kuuliza swali.
“Nick umepajuaje nyumbani kwangu?”
“Sarah sio muda wa maswali saivi, nina dharura ya msingi ambayo imenileta hapa tafadhali na unajua kabisa kwamba nisingekuja bila ruhusa maalumu eneo hili” alisita kidogo kisha akakubali kwa sababu alikuwa akimwamini bwana huyo.

Aliiweka sawa silaha yake kiunoni na kuanza kusogea eneo ambalo lilikuwa na mlango wa kuingilia ndani ya jumba lake. Aliufungua kwa tahadhari baada ya kuwasha taa za sebule ambayo ilikuwa kubwa ya kutosha kufanyia mambo mengi ya msingi. Baada ya kuufungua mlango huo alikutana uso kwa uso na bwana yule ambaye usoni alikuwa mkavu kabisa bila wasiwasi wowote ule.
“Nick kuna nini?” aliuliza swali ambalo hakujibiwa, hakujibiwa kiasi kwamba ayeye mwenyewe alianza kupata mashaka kuhusu mtu huyo, alimkagua kuanzia juu mpaka chini, hakuwa na dalili za kwenda kirafiki hilo eneo. Moyoni alipata majibu akiwa amechelewa.
“Nick, na wewe ni miongozi mwao?” akili ilikuja kumrudi baada ya kuhisi kwamba huenda hata huyo jamaa yake alikuwa miongoni mwa wale watu ambao walimletea majanga mazito kwenye maisha yake kiasi kwamba mpaka wakati huo hakuwa na uelekeo sahihi.
“Ulikuwa ni wakati mwema kukufahamu Sarah ila naomba unisamehe kwa sababu sina namna juu ya hili, unatakiwa kufa”
“Whaaaaat?” nani alikwambia unapaswa kuweka imani yako kubwa kwa wanadamu? Itakula kwako, kuna wakati hata nafsi yako mwenyewe haupaswi kuipa imani kubwa kupitiliza. Yule mwanaume ambaye alianza kumpa imani yake na kumzawadia mwili wake, alikuwa miongoni mwa wale washenzi ambao ndio walikuwa wanamletea wakati mgumu kwenye maisha yake. Alibaki ameduwaa asiamini kile kilichokuwa kinaendelea lakini bwana yule hakuonekana kujali kwa lolote lile.

Alianza kujipapasa taratibu kwenye kiuno ili kutoa ile bastola akiwa anarudi nyuma, nani angempa nafasi kama hiyo mdunguaji hatari wa namna hiyo? Alibebwa juu na guu ambalo lilitua kwenye kiuno sehemu ambayo aliihifadhi bastola, wakati anadondokea kwenye sofa moja na bastola yake ikienda upande mwingine aligundua kwamba bwana huyo hakuwa mwenywe bali alikuja na wanaume wengine wa kutosha ndani ya hilo eneo. Walikuwa jumla wanaume sita ambao wote walionekana kuvaa nguo za jeshi.

Alisimama kupambana na mtu wake wakati huo baadhi ya wanaume waliingia kwenye vyumba vingine kufanya ukaguzi. Sarah hakuwa na namna zaidi ya kuyapambania maisha ya familia yake, alidunda kwenye sofa na kutua pale ambapo alikuwepo Nick, mateke yake mfululizo hayakufua dafu baada ya kuishia kwenye mikono ya mwanaume huyo ambaye aligeuka na buti la kichwa ambalo lilimkosa Sarah kichwa likatua kwenye shingo yake kiasi kwamba akayumba mpaka kusimamia mbali.
Wakati anakaa sawa, hakuwa na muda wa kutosha kupumzika kwa sababu mwanaume huyo alikuwa anakuja kwa kuzunguka kwa kasi mpaka alipo mfikia, alijaribu kupangua teke moja ambalo alifanikiwa lakini wakati huo mkono ulitua kwenye ziwa la kulia, alitoa sauti ya kilio kwa mbali, ulimuingia vizuri. Alirudi nyuma kwa kuyumba akaishia kushindiliwa na double kick iliyo mpeleka mpaka ukutani akapasua runinga kubwa ambayo ilikuwepo hapo.
Mwanaume huyo hakuwa na huruma kabisa, alikuwa anapigana na mtoto wa kike kama anapigana na mwanaume mwenzake. Sarah akiwa anavuja damu mdomoni na puani alisikia sauti za kelele, alikuwa mama yake na mdogo wake wakiwa wamebebwa msobe msobe kuletwa karibu na alipokuwepo yeye wakati ule. Jambo lile lilimpa hasira kuona familia yake inafanyiwa huo ukatili mbele yake, akahitaji kunyanyuka huku akiwa anapiga kelele, alikutanishwa na mguu wa uso, damu nyingi zilisambaa kila kona ya lile eneo akiwa anadondokea upande wa pili.
Mama yake alipiga makelele akiwa anaomba mwanae aachwe ila mazingira hayakuwa rafiki wakati ule, nani angemuacha Sarah? Hakuwepo wala hakuwa na msaada. Sarah alijikongoja kuegamia ukuta akiwa anamuomba mama yake msamaha kwa sababu huenda kama sio yeye basi familia hiyo ingekuwa kwenye amani lakini yeye alifanya kila kitu kuwalinda kwa sababu hata kama angegoma kufanya kazi ya watu hao mpaka muda huo familia hiyo ingekuwa imekufa muda mrefu.
“Sarah nasikitika kukwambia hili ukiwa umechelewa kuweza kulielewa, wanadamu tupo tofauti mno, wanadamu muda mwingine hatueleweki hivyo usihadaike na maneno ya mdomoni. Mimi kwako nilikuja kwa lengo maalumu ili niweze kujua kama kuna mambo ya ziada unayajua
Baada ya kujua siri ndogo ambayo ilikuwa kwenye moyo wako mimi ndiye ambaye nilipendekeza jina lako kwa mtu wa kwenda kumuua mke wa raisi kwa sababu ilikuwa ni rahisi kukumudu maana najua kila kitu kuhusu wewe
Hata kukamwatwa kwa familia yako mara ya kwanza ni mimi ambaye nilikuwa nyuma ya kila kitu, nimekuwa nikifanya kazi na hawa watu kwa muda sasa na sijutii kwa sababu napata kila ninacho kihitaji kwa wakati ambao nauhitaji mimi
Shilingi ina pande mbili Sarah, sio kila upande ni wa ushindi, mimi huwa naangalia upande ambao siku zote umeshikilia ushindi na ndiyo namna ambavyo maisha yanatufunza kuweza kuyaishi. Hawa watu wana pesa, wana nguvu kubwa, wana kila kitu hivyo hakuna mtu kwenye taifa hili ambaye anaweza kwenda kinyume nao akaweza kuishi ama kuwepo kwa muda mrefu”
“Kukufupishia maelezo ni kwamba nimekuja hapa kuhakikisha naua familia yako yote, nataka ushuhudie mama yako akifa huku unaangalia, lakini pia mdogo wako ambaye unampenda sana nataka afe ukiwa unamshuhudia pia. Wewe unaonekana kuwa hatari kwa hawa watu kwa sababu kama Gavin alifanikiwa kukuacha hai na kukupatia kiwango kikubwa cha pesa ambacho inabidi niondike nacho muda huu maana yake lazima kuna siku atakuja kukutafuta na unaweza kuja kuwa sababu ya mambo kuharibika

Sehemu ya 52 inafika mwisho.

Shukrani sana mtunzi 👊
 
Back
Top Bottom