STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA THEMANINI
SONGA NAYO................
“Nadhani kwa sasa tunaweza kuongea kwa heshima, nakuuliza swali rahisi tu unaanza kunipigia makelele. Unahisi kwamba mimi najali lolote kuhusu maisha ya wale watu ambao wamekufa labda? Mimi sijali lolote kuhusu wewe kuwajua hao vijana” alizamisha tena kisu kwenye mfupa lile eneo ambalo risasi imepenya, Ezra alijinyonga nyonga pale alipokuwa lakini hakuwa na la kufanya.
“Nilipata taarifa zake kutoka kwa rafiki yangu wa pili ambaye alimuua”
“Umepataje taarifa zake?”
“Niliunganisha na yule The Future ambaye alikuja kuniokoa ndiye ambaye alinipa maelekezo kuhusu maisha ya Othman na mzee mmoja ambaye ndiye amenipa mwongozo”
“Yeye alimjuaje?”
“Kwa sababu yeye na baba yake wamewahi kuwa marafiki na kufanya kazi pamoja”
“Na kule ulikuwa unaenda wapi?”
“Nilikuwa naenda kumtafuta”
“Ulijuaje kama atakuwepo kule?”
“Kwa sababu ni maelekezo ambayo nimepewa na mzee huyo kwamba atakuwa huko kwa sababu ni nyumbani kwao. Alikuwa anaenda kuangalia kaburi la baba yake”
“Una uhakika na hizi taarifa?”
“Ndiyo”
“Nipe maelezo zaidi juu ya yale ambayo unayajua kuhusu yeye”
“Inaonekana kwamba hawa vijana wapo chini ya Gavin Luca na hayupo mmoja, wapo wengi”
“Kivipi?”
“Walikusanywa vijana wote ambao familia zao ziliuliwa na viongozi wa serikali hivyo wapo kwa ajili ya kulipa kisasi”
“Dhidi ya nani?”
“Viongozi wa serikali”
“Na sababu za wewe kumfuatilia mtu huyu mwisho wake ulitaka uwe nini?”
“Kumpata Gavin”
“Halafu?”
“Nilitegemea jambo hili lingenipa umaarufu na kupata nafasi kubwa ya kuaminika kwa wakubwa”
“Kwahiyo haya unayafanya uli upate cheo?”
“Ndiyo”
“Bwana mdogo huna mambo ya mhimu ya kufanya?”
“Naomba nipe nafasi ya mwisho nitakaa mbali na haya mambo”
“Kwa taarifa ambazo nimefuatilia ni kwamba mara ya kwanza ulipewa onyo na nafasi ya kukaa mbali na haya mambo lakini ulipuuzia leo unahitaji mimi nikupe nafasi nyingine?”
“Zilikuwa ni tamaa tu, naahidi siwezi kurudia tena”
“Bahati mbaya sana mimi sio mtu wa kutoa misamaha kama unahitaji misamaha ulitakiwa kwenda kutubu kanisani” mwanaume huyo aliunguruma akiwa anaitoa picha ya mwanamke, Sarah na kumuonyeshea kijana huyo.
“Unamfahamu huyu mwanamke?”
“Ndiyo”
“Unamfahamuje?”
“Ni mwanajeshi lakini ni moja kati ya wadunguaji hodari kwenye hili taifa ambaye watu wengi wanatamani kuwa kama yeye kwa sababu huwa anatumika kama mfano tukiwa tunafundishwa kulenga shabaha”
“Nadhani umeliewa swali langu”
“Nimesikia kwamba ndiye muuaji wa mke wa raisi”
“Unajua ninakoweza kumpata?”
“Hapana”
“Huyo mzee ambaye unadai ulielekezwa kwake anaitwa nani?”
“Mzee Miraj”
“Nampatia wapi?” ilikuwa ni sauti ya mamlaka hivyo hakuwa na namna zaidi ya kuitii kwa adabu kwani alijua kabisa bwana huyo hakopeshi hivyo alijibu kila ambacho alikuwa anaulizwa tena kwa usahihi kabisa.
“Unajua bwana mdogo ulitakiwa ufuate ushauri wa watu ambao walikuonya kabla. Mimi nafanya kazi na wanasiasa ila naichukia sana siasa, haya maisha ni rahisi kama ukiamua kufuata yanayo kuhusu ila unapo amua kujiingiza kwenye mambo kama haya halafu unajua kabisa una maisha magumu na hakuna mtu hata mmoja ambaye yupo nyuma yako kwa ajili ya kukulinda ni jambo la hatari sana. Maisha yanakupa nafasi moja tu, ukiitumia vibaya basi ujue kabisa kwamba hautaipata nafasi nyingine tena ndo inakuwa imeisha.
Lakini licha ya hayo yote ukajitwika ugwiji na kuhisi wewe ndiye unajua sana, ukajiona kwamba wewe ndiye una tamaa ya kupanda vyeo mwisho wa siku unaenda kufa bila hata kuviona hivyo vyeo vyako ambavyo unavililia. Na watu wenye tamaa tamaa za kipuuzi kama nyie mnatakiwa kufa kwa maumivu ila nakuonea huruma umepata maumivu ya kutosha kwahiyo nitakuua haraka tu” yalikuwa ni maneno ya kutisha bwana huyo akitoa somo dakika za mwisho lakini alimhakikishia mtu wake kwamba ilikuwa ni lazima aweze kumuua, yaani hakukuwa na namna ya kwamba angemuacha hai, hilo ndilo lilikuwa jambo la hatari zaidi.
“Hapana usiniue tafadhali, naahidi nitabadilika kuanzia leo. Sitaweza tena kufanya jambo kama hili kwa mara nyingine tafadhani nipe nafasi ya mwisho”
“Bwana mdogo una maneno ya mwisho labda ya kuongea?”
“Usiniu…….” Hakumsikiliza tena, alimfumua na risasi zote ambazo alikuwa nazo na kutoweka hilo eneo, kazi ambayo ilimpeleka huko ilikuwa imeisha, alitoa maagizo kwa vijana wake kwenda kuutupa huo mwili barabarani ili kila mtu auone lakini hiyo ingekuwa meseji pia kwa wenzake ambao wangetaka kuingia kwenye msala kama wa kwake.
******
Ile video haikutua kwenye mikono ya Bashir tu ambaye aliifanyia kazi. Shirika la kijasusi la nchi pia lilikuwa likifuatilia kwa ukaribu sana taarifa hiyo, hivyo baada ya kuiona video hiyo walikuwa makini kufuatilia kila hatua kuweza kujua ni jambo gani ambalo lilitokea huko mpaka mambo yakaishia kwa namna ile.
Yule ofisa wa polisi Ezra walikuwa wakimjua vizuri sana, alikuwa ni kijana ambaye alikuwa ana maono makubwa kuhusu jeshi la polisi ila alikuwa anaponzwa na kitu kimoja, alikuwa na tamaa isiyo mfano, alitamani kufika mbali kwa muda mfupi jambo ambalo lingemletea matatizo makubwa kwenye maisha yake ila yeye wala hakuonyesha kuwa na wasiwasi juu ya jambo hilo.
Taarifa hizo mtu ambye aliamua kuzifanyia kazi ya haraka alikuwa ni Dayana, mwanadada huyo alijua wenzake wapo kwenye majukumu mengine ya kufanya upelelezi mkali hivyo alitaka kufanya kila namna kuhakikisha kwamba anajua alipo bwana Ezra, kumpata ungekuwa mwanzo mzuri wa kuweza kupata habari na taarifa za tukio ambalo lilikuwa likiendelea. Namna pekee ya kumpata kijana huyo ilikuwa ni kudukua namba yake na jambo hilo alilifanyia akiwa ndani ya kituo kikuu cha Osterbay ambapo ndipo kijana huyo alikuwa akifanyia kazi, alikuwa sambamba na mkuu wa kituo kwa sababu alianza kukusanyia taarifa hapo.
Jambo la kwanza ambalo lilimshangaza ni kuona kijana huyo alikuwa akifanya kazi nje ya maagizo ya mkubwa wake, kesi hizo alizuiliwa kabisa kuzifuatilia lakini hakujali bali aliangalia kile moyo wake unamwambia jambo ambalo lilipelekea kuyapoteza maisha ya watu wawili kipuuzi tu.
Simu yake ilionekana maeneo ya Upanga lakini baada ya muda ikaonekana ipo Mbagala, jambo hilo lilimshtua Dayana ikamlazimu kuingia kwenye gari huku nyuma kukiwa na gari ya polisi kuelekea ndani ya eneo hilo ambako ndiko simu ya kijana huyo ilikuwa inaonekana kuwepo. Saba saba kwa Mpili ndipo simu hiyo ilikuwa imegotea, wakati wanakaribia kufika sehemu hiyo waliona watu wengi wakiwa wamesimama pembezoni mwa barabara, watu walijaa eneo hilo na baada ya kuona gari ya polisi walianza kusogea pembeni kwa ajili ya kuwapisha.
Watu hao walikuwa hapo kwa ajili ya kuushangaa mwili wa mtu ambao ulitupwa eneo hilo, mwili huo ulikuwa umechakaa mno kiasi kwamba ulikuwa unatisha hata kuutazama. Mwili ulikuwa ni wa Ezra Ethan yeye akipenda kujiita Double E, zile ndoto zote ambazo alikuwa nazo, ule umaarufu wote ambao alikuwa anausaka ulikuwa umelala na mwili wake, hakuwa hai tena zaidi ilibaki kuwa historia. Swali la msingi likabaki kwamba ni nani alimuua? Kwenye ile video alionekana mwanaume mmoja akimpa msaada, huyo ndiye ambaye alitakiwa kutafutwa ili kuweza kutoa majibu kamili.
“Alikuja kwangu akiwa kijana mdogo baada ya baba yake kufa, aliniomba niwe mwalimu wake nikafanya hivyo. Nimemkuza kwenye misingi ya kipolisi mpaka anakuwa mkubwa akaja kuipenda kazi hii kwa moyo wake wote, alikuwa kijana mtiifu na kijana ambaye alikuwa na njaa ya mafanikio. Hakuwahi kukubali kushindwa jambo lolote mahali popote ambapo angekuwepo, alijiona kuwa mshindi wa kila jambo ambalo alikuwa analifanya
Wakati namuingiza kwenye idara ya polisi nilijitahidi kumlea kwenye misingi iliyo bora, nilimuonya kuhusu siasa na matokeo yake, kila kitu nilimpa somo kuhusu namna ya kuishi ila huenda nilisahau kumpa somo kubwa zaidi la kuinamisha kichwa chini mbele ya wenye vyeo, hakutakiwa kuwa namna hii anapo jiingiza kwenye mikono ya wanasiasa. Wanasiasa hawapendi watu mashujaa, njaa ya kijana wangu ilimfanya kutokuwa mtu wa kusikiliza jambo lolote kutoka kwa mtu mwingine. Hilo ndilo kosa ambalo nitalijutia mpaka siku naingia kaburini” alikuwa anaongea kwa uchungu mkuu wa kituo baada ya kuukuta mwili wa kijana wake ukiwa umedhalilishwa barabarani watu wakipiga picha na kuchukua video.
“Amekufa akiwa bado mdogo sana, kwa ari ambayo alika nayo kwanini usinge jaribu kumleta kwenye shirika letu huku?” Dayana aliongea akiwa anauzunguka huo mwili na kuangalia makovu ambayo yalikuwepo.
“Kwa sababu aliwahi kukataa kabisa kuhusu hilo. Kama nilivyo kwambia hapo mwanzo kwamba kuna sehemu kama mlezi wake nilifeli, nimemfundisha vitu vingi sana kwenye maisha ila nilisahau jambo ambalo huenda ndilo la msingi zaidi. Nilisahau kumfundisha namna ya kuinamisha kichwa na ndiyo sababu hakutaka kabisa kuwepo sehemu kama ya kwenu hiyo.
Shida kubwa kwake ni moja, alipenda umaarufu, alipenda jina lake liwe linatoka kwenye sehemu ambazo watu wanaona. Nyumbani kwake amejaza nishani kibao kwa sababu ya kuwa mfanyakazi bora, jina lake lilikuwa likitajwa sana kwa sababu alikuwa anafanya kazi kubwa na wenzake wanaona, hiyo ndiyo ilikuwa adhma yake kubwa na ndicho ambacho kilimuua hata baba yake mzazi, nadhani inatembea kwenye damu hii. Kazi yenu ninyi ni kazi kubwa sana na ndio ambao mnahakikisha kama taifa tupo salama kwa masaa ishirini na manne kwa sababu bila taarifa zenu muda wote tupo hatarini lakini nani anajali kuhusu hilo?
Hakuna anayejali kwa sababu kazi kubwa ambayo mnaifanya haiwekwi wazi inabaki kuwa siri, watu wanasubiri tu tatizo litokee ndipo waje kuwalaumu tena kwa kuwatukana, yeye hakupenda hayo maisha kabisa. Alitaka kuwepo sehemu ambayo angeonekana muda wote kwa anacho kifanya kisha ashangiliwe”
80 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.