THE MODERN WAR
(vita ya kisasa)
Sehemu ya.............17
Mtunzi: saul david
WhatsApp: 0756862047
17-(USIKU WA CHATTING)
ILIPOISHIA...16
Sehemu iliyopita tulifanikiwa kujua chimbuko la virusi vya COBOS namna vilivyotoka Mexico mpaka vikaingia nchini. Namna marehemu Jenerali Phillipo Kasebele alivyopambana na baadae kuuwawa kikatili na mtoto wake wa kumzaa, Tino.
Simulizi yetu iliishia wakati Godwin amemuua Big' akidhani kuwa ni Annah asijue Annah alihamishiwa chumba kingine tofauti na sasa yuko chini ya uangalizi mkali wa Inspekta Aron mwenyewe.
Je, nini kitafuata?
SASA ENDELEA....
Ikiwa ni majira ya saa 8 usiku Inspekta Aron alikuwa amekaa kwenye moja ya viti vilivyokuwa nje ya chumba alicholazwa Annah ndani ya hospitali ya Mountenia. Alikuwa amechoka sana huku usingizi ukionekana kumuelemea lakini hakutaka kukubali kuyafumba macho yake hata sekunde moja. Kumlinda Annah ilikuwa ni kipaombele chake cha kwanza siku hiyo.
Akiwa anahangaika kupambana na usingizi huo kumbe kwa muda mrefu Annah alikuwa ameinuka kutoka kitandani akawa amesimama nyuma ya mlango wa kioo akimtazama Inspekta Aron namna alivyokuwa akihangaika pale nje kwa ajili yake.
Annah aliitumia nafasi hiyo kumkagua Inspekta Aron kwa muda mrefu sana, akajikuta anawaza mengi kumuhusu kaka huyo ambaye hakujua kama kuna mtu amesimama kwa muda mrefu anamtazama.
"Amechoka, anapambana kwa ajili ya usalama wangu, ameyaokoa maisha yangu na sasa yupo hapa ananilinda dhidi ya maadui" aliwaza Annah, mawazo yake yakampeleka mbali sana akakumbuka siku moja aliwahi kuambiwa maneno fulani na marehemu mama yake
"Mwanangu wewe bado ni msichana mdogo, usiyapaparikie mapenzi utaharibikiwa mapema. Unatakiwa utulie uchague mwanaume ambaye ni sahihi kwako, siku moja mimi na baba yako hatutokuwepo kila kitu tunachokifanya kwako sasa hivi kama kukupenda, kukujali na kukulinda atatakiwa kufanya huyo mwanaume ambaye utamchagua hivyo kuwa makini"
Sauti hii ya mama yake ilijirudia kichwani kwa Annah
"Mmeondoka mapema mama mmeondoka hata kabla sijamjua mtu atakayeyafanya hayo yote kwa ajili yangu" Alisema Annah machozi yakimlenga kwa mara nyingine.
Mara alishtuka kumuona Inspekta Aron liyekuwa ameanza kusinzia pale kwenye kiti alikurupuka ghafula baada ya kutaka kudondoka.
Inspekta Aron alifikicha macho yake yaliyojaa usingizi kisha akatazama huku na huku kuhakikisha usalama na hapo ndipo macho yake yalipogongana na macho ya Annah aliyekuwa kwenye mlango wa chumba chake anamtazama
Walitazamana kwa sekunde kadhaa kisha Annah akatazama pembeni kwa aibu za kike kike huku akitabasamu. Inspekta Aron naye alipata aibu kiasi baada ya kubaini kumbe alikuwa anasinzia mbele ya mrembo huyo.
"Wewe" Inspekta Aron aliita kwa sauti ya chini wakati huo Annah alikuwa akifungua mlango akatoka na kutembea taratibu hadi pale alipokuwa Inspekta Aron.
"Nambie afande"
"Mbona hujalala"
"Sijapata usingizi, nilitaka kutoka nje nitembee tembee kupunguza mawazo ndio nikakuona hapa"
"Aah! wewe mwanamke utembee uende wapi sasa usiku huu?"
"Kwani ni saa ngapi?" aliuliza annah huku akikaa kwenye kiti pembeni ya Inspekta Aron
"Ni saa tisa kasoro usiku"
"Mda hata hauendi jamani, sasa na wewe kwa nini haujalala?"
"Mimi nipo hapa, nakulinda"
"Ahahah unanilinda au unasinzia?" Alisema Annah, kwa mara ya kwanza Inspekta Aron akaliona tabasamu la mwanamke huyo aliyekuwa na huzuni kwa muda mrefu
"Angalau amecheka, mh! ni mrembo kumbe"Aliwaza Inspekta Aron
"Umesema?" Aliuliza Annah
"Nini kwani nimeongea?"
"Ndio kwamba nimesikia vibaya"
"Huenda, mbona mimi sijasema kitu" Alisema Inspekta Aron huku akimtazama Annah usoni wakatazamana tena kisha wakatabasamu kwa pamoja, lakini mara lile tabasamu likapotea ghafula kwenye uso wa Annah.
"Nini! Unawaza nini?" Aliuliza Aron
"Hamna niko sawa.. Aron, unaitwa Aron si ndio?"
"Yeah Aron Phillipo Kasebele"
Alijibu Aron kisha kukawa kimya tena, baadae Annah akavunja ukimya, akawa anazungumza kwa uchungu...
"Najaribu kuwaza tu ni jinsi gani maisha yangu yamebadilika ghafula, kweli hakuna aijuae kesho yake, ni siku chache tu nilikuwa naishi kwa furaha mimi na wazazi wangu wote wawili lakini kila kitu kikabadilika ghafula tangu siku ile ya Birthday yangu. Najuta kwa nini nilitaka tufanye ile part kwenye ule mgahawa, mwisho tukajikuta tunashuhudia mauaji ya kutisha. Yule Osward aliua mtu mbele ya macho yetu bila huruma akakimbia, baadae akaanza kuua watu walioshuhudia tukio lile mmoja baada ya mwingine, licha ya kukamatwa lakini bado watu wake wakaendelea kuua ili tu kufuta ushahidi, na hatimaye zamu yetu ikafika, wakamuua baba wakamuua na mama pia, mimi nikanusurika na sasa najua wananisaka kwa udi na uvumba kuhakikisha nakufa,najua ndio maana uko hapa Inspekta Aron, maisha yangu yamebadilika nimekuwa kama.....aaah jamani" Annah aliongea kwa uchungu akashindwa kumalizia sentensi yake, akaanza kulia kwa uchungu sana.
Inspekta Aron alijikuta anaanza umpya kumbembeleza Annah anyamaze, hakika maisha ya binti huyo yalikuwa ya kuumiza sana.
"Usijali Annah hiyo yote ni mipango ya mungu, kila kitu kitakuwa sawa hakuna baya litakalokukuta HAKUNA MTU ATAKAYEKUGUSA KABLA HAJANIGUSA MIMI" Aron aliongea kwa kumaanisha, maneno hayo yalikuwa ni faraja kubwa kwa Annah, akajikuta anamkumbatia Inspekta Aron kwa nguvu.
Walikumbatiana kwa zaidi ya dakika mbili, hapo Inspekta Aron akamtoa Annah taratibu huku akimpiga piga mgongoni
"Usiniachiee.." Alisema Annah kwa sauti iliyojaa mchoko. Inspekta Aron akamlaza kwenye kifua chake huku akiuzunguusha mkono wake nyuma ya mgongo wa Annah, akamshika vizuri.
Haukupita mda Annah akawa amepitiwa na usingizi akalala. Taratibu Inspekta Aron akamlaza kwenye miguu yake kisha akachukua shuka alilokujanalo akamfunika.
Inspekta Aron aliinamisha uso wake akawa anamtazama Annah kwa macho yenye huruma na upendo mwingi. Akawa anashikashika nywele ndefu za binti huyo na wakati mwingine akiugusa uso wake, alikuwa ni mrembo haswa.
Hapo Inspekta Aron aliikumbuka simu yake, akachukua kutoka mfukoni kisha akatazama saa, ilikuwa ni saa kumi kasoro usiku.
Inspekta Aron alifungua uwanja wa meseji kwenye simu yake akakuta kuna jumbe 14 ambazao hazijasomwa na zote kutoka kwa Najma mtoto wa Waziri Dokta Gondwe. Aron alifungua pia upande wa mtandao wa WhatsApp huko akakuta ametumiwa picha na yule rafiki yake ambaye ni askari magereza, zilikuwa ni picha zikimuonyesha Big na Osward wakati ule wakifanya mazungumzo pale gerezani.
Inspekta Aron alizitazama picha zile kwa makini kisha akausogeza karibu uso wa Big', alihisi ni kama mtu huyo alimuona mahali lakini hakukumbuka ni wapi, ni kweli Inspekta Aron alimuona Big' kwa mbali wakati ule akiwa amembeba Najma na kumuingiza kwenye gari lakini kwa bahati mbaya akawa hakumbuki.
***********
{TANGAZO:- Epuka matapeli simulizi hii imetungwa na SAUL DAVID simu 0756862047, Tafadhali usinunue kwa mtu mwingine tofauti }
******-*-
Inspekta Aron aliamua kuachana na picha hizo akiamini kabisa mchoko aliokuwanao ndio sababu hasa ya kumfanya asahau ni wapi alimuona Big' ambaye kwa sasa tunajua ni marehemu mwili wake ukiwa kwenye chumba ambacho Annah alikuwa amelazwa awali.
Inspekta Aron alirudi kwenye uwanja wa meseji akafungua na kuaanza kusoma zile jumbe 14 kutoka kwa Najma moja baada ya mwingine.
,,, Habari za mida,,,,,
,,,,,,Mambo,,,,,,,
,,,,,,Aron umelala?,,,,,,
,,,,,,Sorry naweza kupiga simu,,,,,,
,,,,,,,Aron Dokta wangu mguu umeanza kuuma sasa nafanyaje, nitumie dawa ipi kati ya hizi?,,,,,,
,,,,,,,Aron mwenzio naumia,,,,,,
,,,,,Sijapata usingizi hadi sasa,,,,,
,,,,,Hlw,,,,,,
,,,,,,,Aron,,,,,,
,,,,,,,Ee jaman huyo mkeo si akuache kidogo,,,,,,
,,,,,,Aron naumwa serious,,,,,,
,,,,,Hlw hadi sasa saa 7 sijapata usingizi Aron mguu unauma sana,,,,,
,,,,,,We mwanaume,,,,,,
,,,,,,,Mmh,,,,,,,
Inspekta Aron alijikuta anatabasamu mara baada ya kumalizia kuzisoma meseji hizo kutoka kwa pisi kali mtoto wa Waziri wa afya Dokta Gondwe.
,,,,,,,,,Pole, samahan nilikua bize kidogo si unajua hizi kazi zetu nitakupigia asubuh pumzika,,,,,,
Aron alijibu huku akimtazama Annah ambaye alikuwa akijigeuza kwenye miguu yake, akagundua shingo ilikuwa imeanza kukuuama baada ya kulala kwa muda mrefu kwenye miguu yake. Aron akaweka simu pembeni akavua koti lake kisha akamuinua Annah taratibu akaweka lile koti juu ya miguu yake kisha akamlaza tena.
Alipoichukua simu yake akakutana meseji mbili zilizoingia mfurulizo kutoka kwa Najma.
,,,,Eeh pole mwaya,,,,,,,
,,,,,Mguu unauma sana Aron au nimeumia sana?,,,,,,
"Duh hajalala huyu mwanamke" Alisema Inspekta Aron na hapo akajikuta anaanza kuchati na Najma. Ikawa ni mwendo wa meseji mfurulizo kila mmoja akionekana kufurahia kuchat na mwenzake. Wakati huo wote Annah alikuwa amelala kwenye miguu ya Inspekta Aron.
[emoji294][emoji294][emoji294]
Hatimaye kukapambazuka ikafika asubuhi ya siku ambayo ilikuwa ikisubiwa kwa hamu, siku ambayo hakuna aliyejua itaisha vipi si Dokta Gondwe si Tino si Sultana wala si Shadow ilikuwa ni siku yenye kitendawili kizito ni nani atabaki na vimelea vya V-COBOS.
ITAENDELEA....