Simulizi ya kusisimua: Kaburi la Mwanamuziki

Simulizi ya kusisimua: Kaburi la Mwanamuziki

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
28,297
Reaction score
68,017
Simulizi: Kaburi la Mwanamuziki
Mtunzi: Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

Sehemu ya 1


“Kazi yangu bila shaka kila mmoja wenu atakuwa ameifanya vizuri, nilifurahishwa na Richard, yeye aliimaliza tangu jana akaniletea Daftari lake, amefanya vizuri sana. Richard! Tafadhali njoo uchukue Daftari lako” Mwalimu wa Hesabu akasema. Richard akatoka, akaenda kuchukua Daftari lake wanafunzi wote tukimtazama, wengine wakimuonea donge, wengine wakimuona kama kiherehere huku wengine tukiwa hatujali lolote. Kisha mwalimu wa Hesabu akaendelea kusema;

“ Richard amekuwa akifanya vizuri tangu mkiwa kidato cha kwanza, sijui ninyi mnashindwaje na Richard, miaka ijayo Richard atakuja kuwa mtu muhimu sana ndani ya nchi hii. Sijui atakuwa Mchumi! Labda atakuwa Daktari bingwa! Huenda akawa Injinia mkubwa sana hapa nchini. Ati Richard unandoto ya kuwa nani hapo baadaye” Mwalimu wa Hesabu akasema, macho yake yakimtazama Richard huku akitabsamu. Richard naye kwa aibu akatabasamu huku akimtazama Mwalimu wa Hesabu, kisha akajibu;

“ Ningetamani niwe Daktari hilo lisingenishinda, masomao ya fizikia, kemia na Bilojia wote mnajua hayanishindi, labda ningesema niwe Injinia nako nisingeshindwa Mwalimu, Hesabu na Fizikia sijivunii lakini najitahidi kwa kiwango cha wanafunzi bora katika nchi hii. Hata ningesema niwe Mwanasheria, kote ninamudu, lakini yote hayo siyataki, nataka kile ambacho wengi hukitafuta, kile ambacho wengi wamekikosa ndicho ninataka kukisomea, nataka niwe mtaalamu wa mambo ya Fedha, nataka jambo lolote lihusulo Fedha lisinipite, ndoto yangu kubwa ni kuwa mtaalamu wa mambo ya fedha, ukiniita mchumi ni sawa, ukiniita mhasibu pia ni sawa, nataka nikiita fedha initii, nikiikagua inihofie, hiyo ndoto yangu kubwa Mwalimu” Richard alijibu, Darasa lote lilimsikiliza, majibu yake licha ya kuwa na matambo lakini yalionyesha kiburi cha ndani, majivuno ya akili alizojaliwa.

Mwalimu wa Hesabu alituamuru tumpongeze Richard kwa kupiga makofi, rafiki zake walipiga makofi kwa nguvu wakishangilia, wakati washindani wake wakipiga makofi ya kivivu, sisi Back benchers tulikuwa bora liende, tulikuwa tukisukuma tuu siku ziende, kwa kweli hatukuwahi kumuonea wivu yeyote kwa habari za masomo. Hata hivyo ilikuwa ni kero waalimu walipokuwa wakiingia kutufundisha, chanzo cha kero ilikuwa maneno ya baadhi ya waalimu kutudhalilisha sisi tuliokuwa hatufanyi vizuri kwenye masomo, walitukera kadiri ya uwezo wao, wenye mdomo walitumia maneno makali, wenye hasira walituchapa na kutupa adhabau kali. Mambo hayo yalinifanya nizidi kuichukia shule. Kama sio Mama yangu kunilazimisha kusoma basi ningekuwa nimeacha shule siku nyingi, huenda hata kidato cha nne nisingefika. Nilimuonea huruma mama, na hiyo huruma ndio iliyonifanya nivumilie kero za waalimu wa ile shule nikamaliza elimu ya upili.

” Natamani wote mngekuwa kama Richard au Alice, elimu ni ufunguo wa maisha, oneni wazazi wenu wanahangaika kwa umasikini kutokana na kuwa na elimu duni, ndio maana wamewaleta ninyi shuleni mpate elimu msipate shida kama wao wanavyopata lakini ninyi baadhi yenu hamuelewi lolote mkiambiwa, mnacheza na muda wenu, muda hauchezewi, mtoto mdogo unaharakia nini kwenye mapenzi, unaharakia nini mambo ya Starehe, juzi nilikutana na Kabali akitoka Bar akiwa kalewa. Kabali unajua ulinisikitisha sana” Mwalimu wa Hesabu alisema, macho yake yakimkabili Kabali aliyekaa nyuma kabisa.

Nisamehe mwalimu, Lakini mara mojamoja sio mbaya kushtua ubongo” Kabali akajibu.

Hahahahahahah!” Wote wanacheka kasoro Mwalimu aliyebaki anamtazama Kabali huku akitingisha kichwa kwa kumsikitikia.

Anyaway! Shauri yako. Kila mmoja aweke. Daftari la Mathematics juu ya dawati, alafu afungue mahali alipofanyia kazi niliyoitoa jana” Mwalimu wa hesabu akaagiza, jambo hilo likawa linafanyika, mimi ndio nilikuwa namalizia kuhamisha kazi ya Alice aliyoifanya kwenye Daftari langu, Mwalimu alikuwa anaanzia kusahisha madaftari ya wanafunzi waliokaa mbele, mara kwa mara nilimuona Alice akigeuka nyuma kunitazama, nami nilikuwa nikimpa ishara yakuwa namalizia. Alice akawa ananipa ishara nifanye hima, baada ya kujibu maswali matatu kati ya matano, nikaona isiwe kesi, nikamrudishia Alice Daftari yake kwa kulifaulisha kwa dawati lililofuata kwenda mbele mpaka lilipofika kwa Alice.

Sikuwa najua hesabu kusema ukweli, tangu naanza shule niliishi kwa kuibia ibia ilimradi nisiwe wa mwisho darasani, sasa yalibaki maswali mawili kati ya matano, nitayafanyaje, unajua hesabu za kidato cha nne sio za jumlisha wala kutoa, bora hata zingekuwa za Desimali ningejaribu lakini zilikuwa hesabu ngumu zenye alama nyingi, sikuwa naelewa chochote. Nikaandika andika namba za uongo uongo ilimradi kurasa za daftari langu lijae, nikajaza majibu na kuyapigia mstari kwa usafi wote labda nilifikiri mwalimu angenionea huruma hata kama nimekosea jibu basi angenipa vimaksi vya usafi katika kazi. Lakini kumbe jibu la uongo ni uongo tuu hata kama likirembwa na kupambwa.

Mwalimu akanifikia, akachukua Daftari langu, akasahihisha swali la kwanza mpaka la tatu, alipofika swali la nne, aka-stop, nikaanza kuhisi mwili ukilegea, nilihofia asijejua nimeibia kwa mtu. Akanipa alama ya kosa, swali la tano likamshtua,

Iweje upate swali la kwanza na lapili alafu ukose swali la tano? Ati wanafunzi hiyo inawezakana?” Akauliza!

Haiwezekani!” Wakajibu wanafunzi wote mpaka yule jirani yangu niliyekaa naye wakati naye hana anachojua kwenye hisabati.

Wewe utakuwa umeibia tuu! Ndio maana nikashangaa tangu lini Gibson umekuwa na akili za kukokotoa milinganyo kama hii. Embu ona!” Mwalimu akawa anaanza kupekua daftari langu katika kurasa zingine zisizohusiana na kazi ya leo. Kiukweli nilikereka, nilihisi naenda kuumbuka.

“ Heeh! Hii nini! Gibson! Hiki ni kitu gani kwenye daftari langu la Hisabati?” Sauti ya mwalimu ikafanya darasa zima kugeuka na kutazama kilichokuwa kinaendelea, mwalimu akapita mbele akiwa kabeba daftari langu, kisha alipofika mbele kabisa ya darasa ulipo ubao, akaniita nami niende mbele. Nilipofika akaniambia nipige magoti chini. Kwa aibu uso wangu nikiukwepesha na nyuso za wanafunzi wenzangu nikawa naangalia chini nikiwa nimepiga magoti,

“ Kwa hiyo ukaona Daftari langu ndilo la kuandikia huu upuuzi wako, Gibson! Mara ngapi umekanywa na mama yako kujihusisha na Muziki? Mara ngapi! Muziki ni uhuni, hufanywa na watu wajinga, wapuuzi na wasio na haya, au unataka kukata kata mauno kama hivi! Eeh! Hivi na hivi! Ndio unataka?” Darasa zima linacheka baada ya mwalimu kukata mauno.

Lakini mwalimu hata muziki nao ni kazi tuu kama zilivyokazi zingine, napenda sana kuimba Mwalimu!”

“ KELELE!”

“ Unaongea utopolo gani hapa! Muziki! Muziki! Muziki! Upuuzi mtupu! Haya kwa hiyo kupenda kwako muziki ndio ukaona utumie daftari la hisabati kuandika mautopolo yako ya muziki! Hukuona masomo mengine mpaka uandikie kwenye daftari la hisabati? Unadharau HISABATI! Hahahaha! Unajua waalimu wa hisabati wapo wangapi kwenye hii nchi? Unaelewa? Hisabati ni somo lenye heshima, ambalo watu wenye akili za juu ndio hulimudu sio watu kama wewe”
Mwalimu akasema, muda huu hasira zilikuwa zimeikaribia kabisa sura yake.

Nisamehe mwalimu!” Nikasema. Mikono yangu nikiwa nimeiweka kifuani kama ishara ya kuomba radhi.

Leo nitakuchapa bakora mpaka akili ikukae sawa! Haya shika chini mjinga wewe!” Sikuwa na namna nikashika chini, viboko sita vikatua katika makalio yangu, vilikuwa viboko vichungu sana vilivyoyatia maumivu makalio yangu. Nilimuona Alice akilengwa lengwa na machozi, moyoni nilijihisi kuumia sana kuuona uso wa Alice katika hali ile.

Mwalimu alimaliza kufundisha, hatimaye akatoka;

Kila baada ya Lunch ilikuwa mara nyingi waalimu hawaingii darasani. Hivyo muda huo niliutumia kufanya mazoezi ya kuimba, nilikuwa nikienda uwanjani kufanya mazoezi ya sauti, nilizipa mazoezi ala za sauti kama vile ulimi, mdomo, koo na hata Glota. Nilipanua mdomo kuhakikisha sauti yangu inatoka vizuri. Nilifanya mazoezi ya pumzi bila kuchoka kuhakikisha sauti yangu haikati pindi nikiimba sauti ya juu sana.

Kuna wakati nilikuwa nakaa kwenye vivuli ya miti sehemu tulivu, ili kupata tungo nzuri. Nilikuwa nikitunga tungo nzuri za mashairi na kuyarekodi katika kidaftari maalumu. Kivuli na upepo mwanana hutuliza akili, Huibua ubunifu na shauku ya fikra ya kutunga vitu vipya katika sanaa.

“ Labda ni kweli sina akili za masomo ya darasani, ufaulu wangu ni duni. Njia pekee iliyobaki ni kutumia kipaji changu cha kuimba, hakika nitakilinda kipaji change, nitailinda sauti yangu, nitalinda ala za sauti. Lakini Ala za sauti nzuri bila fikra thabiti zenye ubunifu hazitanisaidia kitu, nitalinda fikra zangu kwa kulinda vivuli vya miti ya dunia….” Nikawaza mwenyewe lakini mara Alice akatokea jambo ambalo lilikatisha mawazo yangu.

“ Gibson! Nimekutafuta sana! Nimezunguka uwanjani nikakukosa, nikaenda kwenye yale madarasa mapya pia sikukuona, hapo nikajua sehemu yako ya mwisho ni huku kwenye huu mti wa Mzambarau” Alice akasema.

“ Umekuwa mahiri wa kujua mizunguko yangu eeh! Haya je usingenikuta kwenye huu mti wa mzambarau ungedhani nimeenda wapi?”

“ Bila shaka ningedhani umeshaondoka kwenda nyumbani” Akajibu. Tukacheka wote sana. Alice alipenda kutembea akiwa na juisi ya kopo pamoja na Ubuyu wa rangi nyekundu. Tukala pale ubuyu tukipiga stori. Mara kimya kikafuata, nikamuona Alice akiangalia mbele kwa mbali kidogo, alikuwa kama anawaza mbali la kuhuzunisha. Alinishtua na kunipa hofu.

“ Kuna nini Alice! Unawaza nini?” Nilimuuliza. Alice akanigeukia akanitazama.

“ Mtihani wa mwisho umekaribia sana, sidhani kama mpenzi wangu umejiandaa vya kutosha! Nina wasiwasi sana juu yako Gibson” Alice akasema.

Nikamtazama bila kusema kitu, sikujua nimwambie jambo gani, Alice alikuwa ananijali licha ya kuwa nilikuwa natoka familia masikini, nikiwa naufaulu mdogo mno.

Mimi nafikiri ungeyaweka mambo mengine pembeni kwanza ujikite kwenye kusoma, kisha baad ya kumaliza mitihani yetu ya mwisho ndio uurudie muziki. Unaonaje Gibson?” Alice akasema.

Niache muziki! Alice umechanganyikiwa? Hivi unajua muziki unamaana gani kwenye maisha yangu? Alice! Uliwahi kujiuliza muziki kwangu ni nini? Labda hujawahi kufikiria jambo hili. Acha nikujuze; Muziki kwangu ni maisha, muziki kwangu ndiye mkombozi, wakati madaktari wakitumia taalamu zao kutibu watu, mimi Gibson nitautumia muziki kutibu hisia za watu zilizopondeka, wakati waalimu kama mwalimu wa hesabati wakielimisha watu ingawaje wanatunyanyasa siye tusiye na uwezo darasani, mimi Gibson nitatumia muziki kuelimisha jamii na taifa langu. Alice bado hujaelewa muziki kwangu nini? Bila shaka umeelewa! Haya bado utaniambia niuache muziki?” Nilizungumza nikimtazama Alice kwa macho yaliyojawa na usongo.

“ Lakini Gibson, sijamaanisha uache muziki moja kwa moja, nimemaanisha upumzike kipindi hiki ili tujiandae kwa pamoja kwenye mitihani yetu hii ya mwisho, kisha utaendelea na muziki wako, Gibson unajua mimi ndiye shabiki wako namba moja..”

“ Alice! Naomba tuachane na hayo, tuzungumze mambo mengine!” Baada ya Alice kuniona nimebaki kuwa na msimamo wangu, akaniacha. Niliona jinsi alivyoumia nikaona nijifanye nimekubaliana naye kishingo upande.

**************

“ Kesho ndio nitapiga hatua yangu ya kwanza katika muziki, lazima niwaonyeshe watu kuwa nina kipaji kikubwa, ikiwa ni hatua ya kwanza itanipasa niipige kwa kishindo ambacho kitatikisa vikwazo vyote vilivyombele yangu. Ngoja niendelee mazoezi” nikawaza, alafu nikachukua moja ya kidaftari nilichoandika nyimbo zangu. Nikaanza kuperuzi katika kidaftari kile.

“ Huu! Hapana! Nitaingia na huu! Utafuata huu! Alafu nitamalizia na huu!” Punde nikakatishwa na Alice aliyekuwa ameiingia akiwa na mfuko. Akanikumbatia kwa nguvu, kisha akanibusu!

“ Vipi maandalizi yanaendeleaje?” Akaniuliza, akiwa anachukua stuli, akakaa na kuweka chini mfuko aliokuja nao.

“ Kama unavyoona, nataka kesho mji mzima utikisike, nitaishangaza dunia Alice” Nikasema nikimtazama Alice,

“ Sijui kwa nini hawajatupa nafasi tuimbe walau nyimbo nne!” Nikasema lakini Alice akanikatisha.

“ Gibson mpenzi! Kesho watumbuizaji watakuwa wengi mno, zitakuwepo shule tatu kubwa za kanda hii. Wameona muda utakuwa mdogo, hata hizo nyimbo tatu mlizoambiwa mnaweza msiziimbe, Hivyo unapaswa ujiandae kwa lolote.” Alice akasema.

“ Hata wakisema niimbe moja, kesho nitawafunika wote, kesho ni siku yangu ya furaha. Alice kesho jiandae kufurahia kusikia sauti ya mpenzi wako, kesho utajivunia mimi” Nikasema.

“ Hata sasa najivunia wewe Gibson, mimi siku zote nitajivunia wewe, ila usijiamini sana Mpenzi, kujiamini ni kuzuri lakini isipitilize” Alice akasema, akanyanyuka kisha akatoa nguo kwenye ule mfuko aliokuja nao,

“ Embu vaa hizi tuone!” Akanipa suruali ya jeansi nyeusi hivi na T-shirt nyeupe yenye picha yenye Skull and bones kwa mbele, alafu nyuma yalikuwepo maandishi “ GIBSON ft ALICE”. Nikavaa. Kisha akatoa miwani nyeusi akanipa nivae, nikavaa. Hapo nikamuona Alice akitabasamu kama aliyefurahishwa na muonekano wangu mpya, alafu akatoa Viatu dizaini ya Supra akanipa nikavaa, kisha akaniambia nivae na kofia. Nikamwambia anisubiri niende chumbani kwa mama nikajiangalie kwenye kioo kikubwa. Nikamuacha!

Nilikuwa nimependeza sana, nilifanana kwa ukaribu na wanamuziki wa kimataifa wanaotumbuiza kwenye majukwaa ya kimataifa, baada ya kuridhishwa na muonekano wangu, nikarudi chumbani kwangu,

“ Sasa itabidi uende saluni ukazitengeneze nywele zako vizuri” Alice akasema, akatoa elfu mbili akanikabidhi za kunyolea. Kisha akaniambia nijaribu kutumbuiza mbele yake.

Nikashika kalamu kama maiki na kuisogeza mdomoni. Nikaachia sauti nyepesi na laini nikiupiga wimbo wa mwisho nitakaouimba kesho. Alice akajikuta anatoa machozi, nilifanikiwa kuzigusa hisia zake kikamilifu.

“ Waaaoh! Umeimba vizuri sana. Natamani kesho uimbe kama ulivyoimba leo?” Alice akasema.

“ Usijali mpenzi!Kesho utajionea mwanaume uliyenaye niwa namna gani. Nimekuahidi kuwa siku ya kesho ndio siku utakayojivunia tangu unijue” Nikasema,

Kisha tukaachana, mimi nikienda kunyoa na kuziweka nywele sawa, wakati Alice akirudi kwao. Hiyo ilikuwa saa moja ya jioni hivi.

Itaendelea
 
KABURI LA MWANAMUZIKI ( Sehemu ya 2)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

ILIPOISHIA

Nikashika kalamu kama maiki na kuisogeza mdomoni. Nikaachia sauti nyepesi na laini nikiupiga wimbo wa mwisho nitakaouimba kesho. Alice akajikuta anatoa machozi, nilifanikiwa kuzigusa hisia zake kikamilifu.
“ Waaaoh! Umeimba vizuri sana. Natamani kesho uimbe kama ulivyoimba leo?” Alice akasema.
“ Usijali mpenzi!Kesho utajionea mwanaume uliyenaye niwa namna gani. Nimekuahidi kuwa siku ya kesho ndio siku utakayojivunia tangu unijue” Nikasema,
Kisha tukaachana, mimi nikienda kunyoa na kuziweka nywele sawa, wakati Alice akirudi kwao. Hiyo ilikuwa saa moja ya jioni hivi.


ENDELEA
Alice akiwa anarudi nyumbani njiani akakutana na Richard.

“ Mambo Alice”

“ Poa Rich! Unatoka nyumbani kwetu?” Alice akajibu.

“ Nimefika kwenu nikaambiwa umetoka, umetoka wapi huku?” Richard akasema, macho yake yakimsahili Alice.

“ Nimetoka Saluni kutengeneza nywele, umesahau kesho tukio kubwa kwetu?” Alice alisema, akasogea pembeni kidogo ya barabara kupisha wenye vyombo vya usafiri kupita.

“ Embu toa hiko kilemba nione” Richard akasema, Alice akautoa mtandio alioufanya kilemba kwenye kichwa chake.

“ Umependeza sana Alice, siku zote nakikuambia wewe ni mzuri sijui kwa nini hunielewe, wewe ni pisikali!” Richard alikuwa akizungumza kwa kuchombeza kuufurahisha moyo wa Alice.

“ Mhhh! Yakweli hayo! Mimi naonaga ni Swaga zenu wanaume kutulaghai sisi wanawake” Alice akajibu, aibu ya usichana ikizingira uso wake.

“ Kesho itafaa kama tutakuwa pamoja, nataka tukae sehemu moja, nataka kesho shule nzima wajue wewe ni mpenzi wangu, hatuna haja ya kujificha tena, siku zenyewe zimeisha Alice, wiki ijayo tutaingia kwenye mitihani ya mwisho kabisa, kisha tutaiaga ile shule. Umenielewa?” Richard akasema huku akimtazama Alice.

“ Rich bhana unachekesha kweli! Sisi bado ni vijana wadogo, hatuwezi kuweka wazi kila kitu, watu watatuona hatuna maadili, labda tuwe karibu kama mtu na rafiki yake wa kawaida tuu lakini sio hayo mambo ya mapenzi” Alice alimjibu Rich.

“ Sawa! Nikuombe jambo!” Rich analifuata sikio la Alice kisha ananong’ona maneno Fulani ambayo wawili hao ndio wanayajua. Kisha wanaagana, Alice alikuwa tayari kachelewa nyumba ikiwa inakaribia saa mbili za usiku ambapo kwa mtoto wa kike hapaswi kuwa nje.



**************************

Ukumbi maalum wa shule ulikuwa umepambwa kwa namna ya kuvutia sana. Mapambo ya kisasa yanayopendeza kwa macho yaliufanya ukumbi ule kukonga nyoyo za wote ambao walihudhuria. Wazazi waliketi sehemu zao, wanafunzi wa vidato vingine waliketi sehemu walizokuwa wameandaliwa, Jukwaani palirembwa kuliko sehemu zote za ukumbi, hapo walikuwa wamekaa safu ya wageni maalum, mgeni rasmi, walimu wakuu na wasaidizi washule tatu zilizoamua kufanya tukio hili pamoja, na wakuu wa bodi ya shule. Upande wa kushoto chini kidogo ya jukwaa ilikuwepo mitambo maalum ya kuhakikisha sauti inawafikia vilivyo waliohudhuria tukio hilo. Vijana wawili walikuwa DJ “Disk Jockey” (tamka Diski jokii) katika tukio hili la kuvutia, masikio walikuwa wameweka Wireless Headphone aina iitwayo AIAIAI TMA-1 Headphones ambayo ilikutumia Bluetooth. Dj alikuwa akibadilisha badilisha muziki kulingana na matukio yaliyokuwa yakiendelea mule ukumbini. Upande wa kulia chini ya jukwaa palikuwa na viti vingi vilivyokuwa wazi, hiyo ilikuwa sehemu maalum ya wahitimu wa kidato cha nne ambao ndio walikuwa wakisubiriwa waingie ili sherehe hiyo ianze. Mshehereshaji (Master of ceremonies, MC) alikuwa amesimama mbele ya jukwaa nyuma yake ikiwemo meza kuu. Alikuwa kapendeza sana, MC akamuamuru DJ Awaingize ukumbini Wahitimu kwa muziki mzuri, Dj akaachia Track kali iliyofanya ukumbi mzima kulipuka kwa shangwe, wanafunzi wa vidato vingine walishangilia baada ya kutuona wahitimu tukiingia ukumbini tukicheza kwa mitindo mbalimbali kufuatia mdundo wa muziki. Lilikuwa tukio la kuvutia lililomasha hisia ya wazazi na wageni waalikwa.

Shule yetu tulivalia suruali nyeusi, mashati meupe, pamoja na makoti ya suti yenye rangi nyekundu, na tai fupi za mfano wa maua, wasichana wa shule yetu walivalia sketi nyeusi, mashati ya mikono mirefu yenye rangi nyeupe, shingoni wakiwa na skafu nyekundu zilizowapendeza sana. Kiukweli shule yetu kati ya zile tatu ndio tuliyokuwa tumependeza sana.

Nikamuona Alice akicheza kwa maringo ya kike, alipendeza sana, sikuwahi kumuona Alice katika namna ile. Nywele zake alizitengeneza kwa namna ya pekee iliyovutia sana. Uso wake aliuremba kwa Makeup iliyozidi kuuchomoza uzuri wake kama mbalamwezi. “Alice! Natamani zama zirudi nyuma” Nikatafakari.

Hata hivyo zama siku zote zikipita zimepita, wala haziwezi kurudi tena, zinapita kama moshi, nazo zapotea mawinguni mithili ya ukungu wakati wa jua kuchumoza. Nani awezaye kuuzuiwa wakati, hata kama wakati ungezuiwa usiende, bado usingetaka kusimama pasipo kujongea, kama ukiuzuia usiende mbele basi ungeota mbawa kama ndege na kupaa mbali hata asiwepo wa kuufikia. Huo ndio wakati na mambo yake.

Alice akageuka, hapo tukatazama uso kwa macho, moyo wangu siusemei, mapigo yalipiga na kutoa sauti ambayo iliiambia akili yangu; wewe ni wangu Alice, miliki ya moyo wangu, nakupenda sana Alice” Hivyo ndivyo moyo wangu ulivyoiambia akili yangu. Huku macho yangu yakitazama sura ya mrembo aliyechakaza vibaya hisia zangu, hapo nikamuona Alice akiachia tabasamu jepesi na kufanya uso wake uchanue kama ua la waridi. Nilihisi kupoteza muhimili, kidogo nipoteze step za muziki uliokuwa ukipigwa tukicheza kulikabili jukwaa la mbele kabisa ambalo hapo tungesimama. Alice aliumong,onya moyo wangu ukamong’onyeka. Hapo macho yangu yakashtuka mara yalipohama na kugongana na uso wa Richard aliyekuwa akinitazama kwa jicho la husda, chuki yake ikiwa inakaribia kumshinda, kadiri macho yake yalivyopepesa akiwa ananitazama ndivyo nilivyoweza kuziona hasira zake kwangu.

Akanitazama kwa macho ya maongeo, macho yake yalikuwa kama yananiambia; “wewe ni mjinga tuu, Alice ni halali ya watu wenye akili kama Richard, sio wewe mpuuzi ambaye hujitambui, shule imekushinda” Nami nikiwa nacheza bado tunasonga kuelekea jukwaani muziki ukipiga nikamkazia macho ya maongeo, nikijaribu kutoa taarifa kwenye uso wangu ambao bila shaka Richard angeupate ujumbe niliokusudia, kisha nikawaza hivi nikiwa namtatazama; “ Mapenzi hutua popote kwenye maua mazuri, haijalishi ua litakuwa ni ua la waridi au ua la mti wa miiba, kipepeo hufuata maua mazuri haangalii uchakavu wa mti wala kipepeo hatizami aina ya mti, bali hutazama uzuri wa maua yenyewe. Alice ni kipepeo aliyeyaona maua ya moyo wangu ni mazuri, ndio maana akavutiwa na mimi. Richard unaweza kujiona waridi lakini kipepeo akayaona maua yako hayavutii akatuama kwenye ua lilobebwa na mti usiohehimika”

Tulikuwa tumefika jukwaani bado muziki ukitusindikiza, ukumbi mzima ukitushangilia kwa makofi na vigelegele, Kila mmoja wetu tuliokuwa tunahitimu tulijawa na hisia nzuri zenye furaha. Tukapanda jukwaani tukajipanga kama ilivyokusudiwa, wasichana wakiwa mbele yetu nasi tukiwa nyuma yao. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, tulikuwa walinzi wa wasichana wetu, tuliwaweka mbele ili wapambe mbele yetu kama maua, waangaze mbele kwani wao ni kama nuru. Basi tukapiga Guu chini na kutoa kishindo kikuu, DJ akazima muziki kukawa kimya nasi tukiwa tumeweka mguu sawa. Ulikuwa ni muda wa kuimba wimbo wa taifa, ukumbi mzima ukasimama, wala hakuonekana yeyote ambaye alikuwa amekaa siku ile. Ulikuwa ni wimbo wa heshima wa kuliombea taifa kwa Mungu. Ingekuwa ni utovu wa nidhamu endapo angetokea yeyote mkaidi. Huyo angepewa adhabu kali mno kwa kulidharau taifa lake.

Tukaimba wimbo wa taifa kwa kufuatisha Kinanda kilichokuwa kikipigwa na moja ya wanafunzi. Wakati tunaimba wimbo wa taifa nikamuona Mama yangu akiimba kwa hisia kali sana. “ Dumisha uhuru na umoja, wake kwa waume na watoto, Mungu ibariki…” Kipande hiko nikamuona mama akiyahamisha macho yake mpaka yalipofika kwenye usawa wangu. Tukatazama! Uso kwa macho. Tukiendelea kuimba midomo yetu ikicheza cheza kufuatana na maneno ya wimbo wa taifa. Hapo akili yangu ikapaa katika mkondo wa mawazo. Nilikumbuka harakati za mama yangu kila siku za kujishughulisha na kupika mgahawa, ilikuwa kazi ngumu sana kutokana na mtaji wake kuwa mdogo, vifaa vya upishi alivyokuwa anavitumia vilikuwa duni, moshi wa kuni uliharibu na kufubaza muonekano wake. Tulikuwa na maisha magumu sana. Kama usingeelewa nikisemacho basi Gauni na kilemba alichokivaa mama yangu kingekufanya unielewe. Lilikuwa gauni kuukuu la mtumba ambalo hata mtoto mdogo angejua ni gauni la bei nafuu kabisa, kilemba kilikuwa kimetoka nyuzinyuzi kwa uchakavu, pengine asingevaa kilemba angeonekana na mvuto zaidi, lakini nilimuelewa mama yangu, nywele zake kiasili zilikuwa nzuri, nzito na ndefu lakini alishindwa kuzihudumia. Hivyo kilemba ndicho kilichokuwa msaada mkubwa kwake. Hayo yote yalinifanya nilengwe lengwe na machozi bado nikiwa namtazama mama yangu huku wimbo wa taifa ukimalizika. Tulimaliza kuimba na nikamuona mama yangu akitabasamu huku akiungana na wengine kupiga makofi. Yalikuwa makofi makuu kutoka kwa mama yangu kipenzi, alikuwa akinipongeza kwa hatua niliyoifikia. Kwake aliyaita mafanikio makubwa baada ya msoto wa miaka minne ya kulipa ada, leo Gibson nilikuwa nahitimu.

Tukaimba wimbo wa shule kisha tukaimba nyimbo nyingine moja tuliyoitunga kwaajili ya mahafali. Baadaye tukarudi kwenye siti zetu tulizoandaliwa. Tukiwa tumekaa nikashtushwa na mwanafunzi mmoja niliyekaa naye jirani, alinipa kitu mfano wa biskuti muundo wa vileja. Nikamshukuru nikawa natafuna naye akitafuna tukiwa tunaendelea kusikiliza propgramu zilizokuwa zinaendelea, hiyo ni majira ya saa tano asubuhi. Mara kwa mara nilimuona Alice akigeuka nyuma kunitazama, kila tulipotazama tukawa tunatabasamu jambo ambalo Richard lilikuwa halimfurahishi. Nami nilikuwa namfanyia makusudi ili nimuumize kutokana na tabia yake ya majivuno na kiburi. Lakini Richard hakuonekana kunijali sana, macho yake ni kana kwamba yalikuwa yakinambia subiri uone. Baada ya program kadhaa kupita sasa ilikuwa ni wakati wa kutumbuiza kidogo kabla ya mgeni rasmi kuzungumza na kutoa zawadi.

Zamu yangu ilikuwa imekaribia, sikatai kuwa kuna wakati hofu ilikuwa ikiniingia, kusimama mbele za watu ni jambo kubwa sana. Kuna wakatai nikawa nafikiri hivi nikishindwa itakuwaje, hii ndio ilikuwa siku yangu ya kwanza kusimama mbele ya umati mkubwa kama ule, watu zaidi ya elfu tano walikuwa pale, mji mzima ni kama ulikuwa umehamia pale shuleni. Ghafla nikahisi tumbo kama linauma hivi, nikajua labda ni wasiwasi lakini mbona sikuwa na hofu kwa kiwango kikubwa. Alianza kutumbuiza Mwanamuziki mwanafunzi wa shule nyingine kati ya zile mbili, Watu walimshangilia sana, kiukweli alikuwa anajua kuimba mno, mashairi yake yalisimama, vina na mizani alivizingatia, ingawaje wimbo wake wa pili ulikuwa katika mtindo wa kisasa usiozingatia kanuni za ushairi lakini ulifanya mpaka baadhi ya wageni waalikuwa kusimama na kwenda mbele kumtunza kwa kumpa pesa. Hii ilizidi kunipa hofu kuwa yule jamaa simuwezi.

Nikamuona Alice akinigeukia kunitazama, uso wake ulijawa na wasiwasi kwa kile kilichokuwa kinaendelea pale jukwaani, yule mwanafunzi aliimba sana, tena sana. Nikatabasamu, Alice naye akatabamu kunitia moyo. Yule mwanafunzi akamaliza kuimba nyimbo zake tatu, ukumbi wote ulipiga makofi kwa nguvu nyingi huku watu wakishangilia. Sasa ilikuwa zamu ya Mtumbuizaji wa pili kutoka shule ya pili, tumbo lilizidi kuuma, nilihisi kama nataka kuharisha, nikatoka kwenda nje, wanafunzi wenzangu wakijua ninatoka kwenda kujiandaa kutumbuiza baada ya yule mwanamuziki mwanafunzi wa pili kumaliza ili nipande, lakini kiukweli nilikuwa naumwa na tumbo mno. Wakati natoka Alice alinitazama, nafikiri aliuona uso wangu ukiwa katika hali isiyo ya kawaida. Baada ya mimi kufika nje nikashtushwa na sauti ya Alice nyuma yangu aliyekuwa akinifuata.

“ Vipi Gibson upo sawa! Mbona unashika tumbo huku umekunja sura” Alice akaniuliza, wasiwasi ukishindwa kujificha katika uso wake.

“ Tumbo linauma sana Alice!”

“ Oooh! Pole Gibson! Sasa utaweza kuimba kweli?” Akaniuliza.

“ Sina uhakika! Uuwi! Linakata! Mamaaa yangu” Nikalalama.

“ Gibson! Gibson embu kaa hapa kwanza” Alice akasema akiwa huku akikivuta kiti cha plastic kilichokuwa pale pembeni.

“ Ngoja nimuite mwalimu wa sanaa na michezo.” Alice akaondoka, akaniacha nikiwa nimeinama nimeshika tumbo langu. Nilihisi kama matumbo yanakatikakatika. Punde Alice alirudi akiwa na mwalimu wa sana na michezo. Nikapewa dawa nikanywa, nilisikia ndani ya ukumbi mtumbuizaji wa mwisho akiwa anamalizia wimbo wake watatu. Sikujua aliimbaje lakini shangwe niliyoisikia ilikuwa ni kubwa maradufu ya ile shangwe ya mtumbuizaji wa kwanza. Hii ikanifanya nijue kuwa huyu wa pili atakuwa aliimba vizuri zaidi kuliko yule mtumbuizaji wa kwanza.

“ Gibson! Utaweza au tutoe udhuru kuwa hautatumbuiza, maana wewe ndiye unasubiriwa huko ndani” Mwalimu wa sanaa na michezo akasema.

“ Sina uhakika! Nahisi nitashindwa, tumbo bado linauma sana” Nikasema lakini Alice akanikatisha.

“ Usiseme hivyo Gibson!. Jikaze bhana! Unajua siku ya leo jinsi ilivyomuhimu kwetu, hasa kwa sanaa yako ya muziki. Jikaze Mpenzi” Alice alisema akinibembeleza.

“ Hapana! Siwezi Alice! Nipelekeni tuu hospitalini”

“ Jamani kama anaumwa apelekewe Hospitalini, maisha ni muhimu kuliko muziki..” Sauti ya Richard kutokea nyuma yao ikasema. Wakageuka kumtazama, name nikafumbua macho yangu na kuuinua uso wangu kumtazama Richard.

“ Hapana! Sidhani kama kuna ulazima wa kupelekwa hospitalini, tumeshampa dawa, atakaa tuu sawa. Gibson naomba unisikilize! Dakika kumi utakuwa sawa, leo lazima uonyeshe kipaji chako” Alice akasema.

“ Lakini muda haupo wa kumsubiri, huko ndani hamumsikii MC akimuita? Hizo dakika kumi uongozi wa shule hautakuwa tayari kusubiri na kuharibu ratiba zingine. Kwanza uimbaji sio ratiba muhimu” Richard alisema.

“ Uimbaji sio muhimu kwako Rich, Lakini kwa Gibson ni jambo la maana kuliko kitu chochote”

“ I’m sorry Alice, labda hujanielewa. Uimbaji ni muhimu lakini katika Ratiba ya leo sio muhimu kihivyo. Mimi najua uimbaji ni muhimu zaidi kwa watu kama kina Gibson lakini sisi wenye akili za darasani sio muhimu. Hata kama itakuuma lakini huo ndio ukweli” Richard akasema. Uso wake akiukunja na kuukunjua kwa dharau na kiburi.

“ Itabidi tuka-cancel ratiba yako ya kuimba, kama mpaka sasa hali sio nzuri, basi hatuna namna tena” Mwalimu wa sanaa na michezo alisema.

“ Leo ninataka nionyeshe umuhimu wa muziki mbele ya watu wote. Nitaimba!” Nikasema. Nikanyanyuka huku nikimtazama Richard, uso wake ulipigwa na mshangao, hakupendezwa na maneno yangu. Nikalifuata sikio la Alice kisha nikamnong’oneza jambo. Richard aliyatega masikio yake kama panya ili aambulie chochote lakini hakusikia lolote. Jambo hilo likazidisha hasira yake, akaondoka.

Ukumbi ulikuwa kimya watu wakiangaza macho yao huku na huku kwa kushangaa sintofahamu ya mtumbuizaji wa tatu kuchelewa. Nikamsikia MC akiniharakisha nifanye upesi kwani muda ulikuwa haupo upande wetu. Alice akaingia ukumbini akiniacha nje, akapitia kwa DJ akampa Flash, kisha akapanda jukwaani akiwa amebeba Maiki. Ukumbi ulikuwa kimya, watu wote walikuwa wanamtazama Alice, wengine walijua ndiye mtumbuizaji watatu lakini wanafunzi wa shule yetu hilo hawakuliafiki kwani Alice tangu wamjue hakuwahi kujihushisha na masuala ya muziki achilia mbali nyimbo. Alice akawasabahi.

“ Kwa heshima na taadhima nimuombe mama yangu apite Mbele” Alice akasema. Watu wote wakageuka huku na huku kuangalia mwanamke atakayesimama ambaye ndiye wangejua kuwa ni mama yake na Alice. Mama Alice aliyekuwa kavaa vizuri Gauni la heshima, kichwani kukiwa na nywele zilizosukwa katika mtindo wa kisasa kabisa, masikioni alikuwa amevaa herein zilizokuwa zinang’aa na kumfanya azidi kuvutia. Mama alice akatembea kwa maringo mkononi akiwa ameshika Gitaa akilipiga katika namna ambayo watu wengi pale ukumbini wasingeweza kuamini. Mama Alice alizichana nyuzi za gitaa kama hataki lakini watu walitaka kusikia sauti iliyokuwa ikitoka. Watu wakawa wanampigia makofi yeye akipanda jukwaani. Mpaka alipomfikia Alice.

“ Piga kelele kwa mamaake!” MC akabwagiza.

“ Weeweeeeeee!” Wanafunzi wote wakalipuka kwa shangwe.

Mama Alice akakabidhi Lile Gitaa kwa Alice, akaondoka huku MC akimuamuru DJ amsindikize Mama Alice kwa Muziki mzuri unaomfaa mama wa dizaini yake. Muziki ukapigwa, Mama Alice akashuka huku anacheza kwa madoido ungedhani ni mbobezi wa masuala ya matamasha ya muziki. Alice akaiseti Maiki kwenye stend yake usawa wa nyuzi za Gitaa, kisha akaanza kuzichana nyuzi za ile gitaa, ukumbi mzima ulikuwa kimya kusikiliza sauti laini na tamu ajabu iliyozalishwa na nyuzi zilizokuwa zinachanwa na Alice. Hakuna aliyekuwa akijua kuwa Alice ni mpigaji mzuri wa Gitaa isipokuwa Mama yake, Alice pamoja na Gibson.

Kabla hawajaisha kushangaa, nikatokea nikiwa nimevalia nguo nilizoletewa jana na Alice, haikuwa rahisi kunitofautisha na wasanii wakubwa kwa jinsi nilivyokuwa nimependeza, miwani nyeusi iliyouweka uso wangu nyuma, tisheti nyeupe yenye fuvu kwa mbele, nyuma yakiwepo maandishi “Gibson Ft Alice” Yakiwa katika Face Font ya Algerian yakiwa yamekolezwa, na jinsi nyeusi iliyonikaa vyema, chini kabisa nikiwa na viatu vya namna ya supra nyeupe. Nilipendeza mno mpaka mwenyewe nikawa najiona hivyo. Nikapanda jukwaani nikiimba sauti ndogo laini iliyofanya ukumbi wote uwe kimya ukitusikiliza na kututazama pale jukwaani; Niliimba kwa hisia sana, nilijua sanaa ya muziki inahitaji kutiisha viungo vya mwili kwa kila ukifanyacho jukwaani. Uso wangu niliulegeza nikiwa nimefumba macho yangu kwa upole, mdomo wangu nilikuwa nikiufumbua na kuufumba nikiumba maneno, huku uso nikiukunja kwa kama mtu ninayesikia maumivu makali, kuna wakati nilikuwa nikiyafumbua macho yangu nikiwatazama watu ukumbini waliokuwa wakinisikiliza na kuniangalia, niliziona hisia zao jinsi nilivyozifunga na kamba ya muziki, sasa nilikuwa nikiziburuta vile nilivyokuwa nataka.

Nikawaona baadhi ya wanawake wakilengwa lengwa na machozi, wengine walikuwa wakilia. Kuna wakati nikawa natazamana na Alice ambaye naye alipiga nyuzi za gitaa kwa hisia, akipandisha Key uso wake aliukunja sana kadiri alivyozipandisha key, na alipokuwa akizishusha key akawa anaulegeza uso wake polepole mpaka unarudi katika hali ya kawaida na kuyafumbua macho yake, kisha akatabasamu. Nilimsifu sana kwa kupiga Gitaa. Baada ya wimbo huo kuisha watu wakapiga makofi mazito huku wengine wakitaka tuendelee wote, Alice akainama kwenye heshima kisha akashuka akiwa anasindikizwa na shangwe.

Nikaimba wimbo wa pili nikiwa peke yangu, nikifuata instrumental niliyoiweka kwenye Flash aliyopewa DJ, nikaimba nikizichezesha ala za sauti zangu vizuri na kuzioanisha na ala za muziki zilizokuwa zikipiga kutoka kwenye Flash. Watu walikuwa wanaona kama wapo kwenye tukio bora kabisa la muziki. Hatimaye nikaimba wimbo wa mwisho, huu ndio ulifunga kazi. Moja ya kipande cha wimbo ule kilikuwa;

“ Kiburudisho kilichokamilli,

Kitakasacho, Roho na akili,

Kigusacho, Hisia na yetu miili,

Taa ya macho, fahamu zetu kuhimili,

Tangu jana hata kesho, leo kimewasili,

Hakina mwanzo wala mwisho, Kuishi yake asili.

Nini kitu gani hicho, nimetega kitendawili”

Melody ya wimbo huo ilikuwa ya kusisimua sana, maneno yake yalikuwa kama methali, niliimba kama mhenga katika jukwaa la kisasa kabisa la zama za kileo. Kilichowafanya watu waufurahie wimbo huo ni mdundo pamoja na melody yake, wengi walinisifu, sasa nilifika beti la tatu nikawa naimba nikimtazama Alice aliyekuwa kaa sehemu yake ya wahitimu.

“ Ninafuraha moyoni! Wakwangu wewe wakwangu!

Ujapo uendapo maishani! Mwingine hakika sioni!

Oooh! Mamaa! Honey wangu oo honey! (My bebe)

Wakwangu ooh wakwangu! No body can take us apart!

Umejenga kiota moyoni, in the morning till kali night!

I hug you! Kiss you mdomoni, naji-feel ile Tight!

Ooh! Bebee! Njoo kubembelezee! Uji-feel right nut!

Burudiko kamili, latoka kwako kipenzi mamaa1

Don’t feel shy, tutapaaa ka-njiwa in sky, so how and why!

Ku-feeel shy, kaa nami mtasha, nikupe penzi nainai!

Usitishwe na wapiga mbizi, hasira zao za mkizi!

Miye wako maimai, kwetu siye watachizi!

Tutawachoma na letu penzi, watekee nyoyo zao zishike masizi!

Burudiko kamili! I love you forever until (mwaaaah!)

Hisia kali nikaziona katika uso wa Alice, wimbo huo alijua moja kwa moja ninamuimbia yeye, kuna wakati alikuwa anashindwa kujizuia, akawa anasimama na kupiga vigelegele jambo ambalo Richard hakulipenda. Kiitikio ndicho kilichoubeba wimbo wa mwisho, kile kiitikio mardadi kabisa. Makundi ya watu yaliinuka na kuja kunitunza kwa kunipa pesa kadiri walivyojaliwa. Niliiamba kama mtu niliyeingiwa na jinni muongoza kwaya. Hatimaye nikamaliza, mama yangu akaja kunilaki akisindikizwa na Alice, alikuwa akilia kwa furaha, akanikumbatia. Nilihisi joto la mama na kuyasikia mapigo ya moyo wake.

“ Nakupenda mama” Nikasema! Mama hakuniitia, akaniachia kisha akanitazama usoni akiwa kashika mashavu yangu, alafu akanibusu pajini mwangu. Hivyo ndivyo siku ile ilivyokuwa. Siku ambayo safari yangu ya muziki ilianza.

Itaendelea,,,
 
KABURI LA MWANAMUZIKI (Sehemu ya 03)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

ILIPOISHI
A.,,
Niliiamba kama mtu niliyeingiwa na jinni muongoza kwaya. Hatimaye nikamaliza, mama yangu akaja kunilaki akisindikizwa na Alice, alikuwa akilia kwa furaha, akanikumbatia. Nilihisi joto la mama na kuyasikia mapigo ya moyo wake.
“ Nakupenda mama” Nikasema! Mama hakuniitia, akaniachia kisha akanitazama usoni akiwa kashika mashavu yangu, alafu akanibusu pajini mwangu. Hivyo ndivyo siku ile ilivyokuwa. Siku ambayo safari yangu ya muziki ilianza.


ENDELEA
Siku ile Richard alijipatia utukufu na heshima, alipewa tuzo nne za masomo aliyoyafaulu kwa kiwango cha Grade A, Richard alifaulu kwa ufaulu wa juu katika Fizikia, Kemia, Hisabati na Jiografia, watu wengi walimsifia sana siku ile. Kila alipokuwa akipanda kuchukua tuzo alikuwa akitembea kwa matambo na mara zote alikuwa akinitazama pale alipokuwa akikabidhiwa tuzo na Mgeni Rasmi. Macho na sura yake vilinipa ujumbe; Hivi ndivyo watu hupewa heshima, na huu ndio mwanzo tuu Gibson, subiri uone” ujumbe huo akausindikiza na tabasamu la kifedhuli macho yake yakiwa yananitazama. Kwenye tuzo ya nne Richard aliomba upendeleo kwa MC; apewe maiki kwani anajambo anataka kuzungumza. Mgeni Rasmi akamuamuru MC amruhusu tuu, ukumbi mzima ulikaa kimya ukisubiri jambo ambalo Richard alitaka kulisema. Mwenyewe nilikuwa najiuliza; Richard anataka kuzungumza jambo gani. Sikujua ni kwa nini nilijawa shauku ya kutaka kujua anachotaka kukizungumza Richard.

“ Ndugu Mgeni Rasmi, Ndugu waalimu wakuu, ndugu waalimu pamoja na wafanyakazi wengine wa shule; ndugu wazazi na wageni waalikwa, ndugu wanafunzi wadogo zangu tunaowaacha, ndugu wahitimu wenzangu, Habarini za leo?(ukumbi wote unaitikia) Kutokana na muda kuwa mdogo na nimeibia tuu nafasi hii, nawashukuru sana! Tena sana nyote mliotufanya tuwe hivi tulivyo; hatua niliyoifikia ni kwa msaada wenu pamoja na juhudi zangu katika kuelewa lengo la kuwapo shuleni. Elimu tumeipigania, na siku zote elimu ni kama jembe kwa mkulima ambalo kamwe haliwezi kumtupa. Ukiipigania elimu nayo itakupigania; mifano ya walioipigania elimu ipo na maisha yao ni mfano bora kwetu, kama sio elimu hata Mgeni Rasmi leo hii huenda asingekuwa mbele yetu” Richard anageuka kumtazama Mgeni Rasmi ambaye alikuwa anatabasamu na kumuonyesha ishara ya kukubaliana na maneno yake. Alafu akaendelea kusema;

“ Ndio maana wazazi wetu tunaowapenda walijitoa kikamilifu, wakajinyima kwa ajili yetu ili sisi tusome. Lakini inasikitisha miongoni mwetu kushindwa kutambua juhudi za makusudi zilizofanywa na wazazi wetu. Wengine walikuwa wakicheza na shule bila kujali kuwa shule ni kitu cha thamani kuliko dhahabu; Wapo waliojiingiza kama mambo yaliyokwisha kudharauliwa tangu enzi na enzi, mambo ya aibu katika jamii yetu. Mtu kujiingiza katika Muziki usio na maana yoyote, mtanisamehe wazazi wangu, ikiwa mtafanya hivyo niruhusuni niwaulize swali moja, mnaniruhusu?” Richard akauliza, ukumbi mzima ukaitikia “Uliza”

“ Ni nani kati yenu anatamani mtoto wake siku moja awe mwanamuziki?” Ukumbi mzima ukawa kimya ukimtazama Richard.

“ Unaona! Hata wazazi wenyewe hataki watoto wao kujiingiza kwenye masuala ya muziki. Hii ni kutokana na mambo yafanywayo na wanamuziki; Nani asiyejua matusi yaimbwayo na wanamuziki, labda hamyajui matusi kwani nafahamu wengine hata huo muziki hamuusikilizi, lakini je tabia za wanamuziki si zinajulikana, kuvaa vibaya kwao ndio akili, kutumia madawa ya kulevya kwao ndio ujanja, kuharibu miili yao kwa kujichora chora na kujitoboa toboa kama watu waliochanganyikiwa! Inasikitisha sana! Nisitake kuwamalizia muda wenu. Nashukuru kwa kunisikiliza, na nisameheni ikiwa nimekosea” Richard alimaliza kuongea ukumbi mzima ukampigia makofi isipokuwa mimi na Alice.

“ Haya wale walioandaliwa kumvisha mataji Richard mnaweza kupita mbele upesi, hatuna muda wa kutosha” MC akasema na jambo hilo likawa linafanyika. Alipita Mama mzazi wa Richard na Dada yake mkubwa wakiwa wamebeba maboksi ya zawadi yaliyopambwa vizuri kabisa. Muziki laini mzuri ukapiga kuwakaribisha jukwaani, Richard naye alikuwa akicheza kufuatana na mdundo wa muziki., Nikamuona Richard akimtazama Alice kwa macho ya maswali lakini Alice hakuwa anatazama jukwaani. Akavalishwa mashela uso wake ukiwa hauna furaha. Jambo hilo likanifanya nijiulize kulikoni, mbona Richard kabadilika mara hii! Picha zikachukuliwa.

“ Tabasamu basi kidogo Richard, picha zitoke vizuri” Mc alisema kwa kuchombeza, ukumbi ukilipuka kwa vicheko. Baadaye Richard na ndugu zake wakashuka, lakini uso wa Richard haukuwa ule nilioujua. Alikuwa kakasirika sana! Sikuelewa maana yake. Alice akaitwa jukwaani, yeye akapewa tuzo moja kwa kuongoza somo la Bayolojia. Alikuwa msichana pekee kati ya wanafunzi waliopewa tuzo za akademiki. Hii ilimfanya apewe nafasi ya kuzungumza na kuacha somo kwa wanafunzi watakaobaki.

“ Mimi sina mengi ya kusema ndugu zangu, mengi yamesemwa, mimi zaidi ya kuwashukuru kwa kweli sioni chakusema. Lakini nikilazimika itanibidi tuu niseme” Alice aliongea sauti nyepesi laini ya kisichana; akiwa mwingi wa aibu ungedhani sio yule aliyekuwa anatumbuiza na Gitaa muda uliopita.

“Itakupasa useme jambo lolote Alice” Mkuu wa shule yetu akamuamuru.

“ Inashangaza sana! Pengine mimi ndio sielewi! Nitaomba nieleweshwe!” Alice anakaa kimya kwa kitambo kidogo kisha anautazama ukumbi wote ambao nao unamtazama.

“ Nani hakufurahia tulivyokuwa tunaingia tukiwa tunacheza? Mlifurahia watoto wenu tulivyokuwa tunaingia ukumbini, si ndio! Nawahakikishia ingekuwa ni kazi ngumu kwenu kufurahi tulipokuwa tunaingia tukicheza bila ya mapigo ya muziki. Mapigo ya mziki yalikuwa kichocheo kikubwa cha furaha yetu katika tukio hili. Programu karibu zote zilizokuwa zinaendelea hapa zilitiliwa msumari na muziki, hata baadhi ya wapokea tuzo za akademiki walipandishwa na muziki na kusindikizwa na muziki. Alafu kuna mtu anasema muziki ni uhuni! Anasema muziki haufai! Ajabu sana hii! Kama ungekuwa haufai basi usingekuwepo humu ndani, na hata yeye asingetaka upigwe wakati anapokea tuzo.” Anameza matee kisha anaongea kwa sauti ya chini bado akiwa kashika maiki;

“ Haifurahishi kubagua kazi na kuzidharau kazi za watu wengine, haipendezi kuziona fani zingine hazifai. Huo hauwezi kuwa uungwana, iwe muziki, iwe uinjinia, iwe utabibu, au pengine uanasheria zote ni fani zinazoisaidia jamii. Tena zinategemeana. Kwa vile nimepewa nafasi hii kutoa ushauri kwa wadogo zangu, basi nawaomba muipate elimu ya kweli ambayo haidharau na kubagua fani au kazi zingine” Alice akanyamaza kisha nikayaona macho yake yakizunguka polepole mpaka yalipotuama kwenye macho yangu, tulitazama kwa kitambo tukiwa kama watu tunaotafakari jambo Fulani, kisha nikatabasamu, naye Alice akanijibu kwa tabasamu lake zuri. Ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na makofi. Wakwanza kuinuka nilimuona Mwalimu mkuu wa shule ya pili akisimama, kisha akafuata waalimu wengine, kisha mkuu wa shule yetu na mkuu wa shule ya pili, alafu nikaona watu wote waliokuwa kwenye meza kuu wakisimama huku wakipiga makofi yao.

Kwa mwitikio mkubwa wazazi nao wakasimama, Mimi nilikuwa nikigeuka huku na huku kuangalia kila kundi lililokuwa linainuka, nilishangazwa sana, hisia za mageuzi nikaziona zikimea polepole, hapo nikashangaa mwanafunzi aliyekaa jirani yangu upande wa kushoto akisimama, niligeuka na kumtazama, kisha akafuata kusimama mwanafunzi jirani aliyekuwa upande wa kulia, alafu nikashangaa nikiwa bado nimekaa wanafunzi mmoja mmoja wakisimama mpaka walipomalizika nikabaki peke angu nikiwa nimekaa. “Hii maana yake nini” Nikajiuliza. Bado nilikuwa nikigeuka geuka kuangalia yaliyokuwa yanatokea, ni mpaka nilipopeleka uso wangu mbele lilipo jukwaa, tukagongana uso na Alice aliyekuwa akinitazama kwa uso wa hisia kali machozi yakiwa yanamlenga lenga; Hapo nami polepole nikasimama tukiwa tunatazamana, kisha nikaanza kupiga makofi polepole nikitazama na Alice ambaye alikuwa akiniangalia akiwa kasimama mguu sawa. Nikamuona Alice naye akianza kupiga makofi huku akinitazama, hatimaye wote nyuso zetu zikakunjuka na tabasamu likachomoza katika sura zetu. Ukumbi mzima ulirindima makofi na shangwe.

Alice aliongea maneno ambayo mpaka leo hii nayakumbuka, yalikuwa ufunguo wa faraja katika safari yangu ya muziki. Kumbe wapo wachache waliokuwa wanaelewa kile nilichokuwa ninakihitaji katika maisha yangu. Alice aliiona ndoto niliyokuwa naifukuzia. Ndoto ya kuwa mwanamuziki mkubwa mwenye mafanikio.

Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa siku zile, katika hatua yangu ya kwanza niliyoikanyaga katika msitu wa muziki.

*************************

Hata safari iwe ngumu vipi kamwe usikate tamaa. Safari ya mafanikio inaweza isiwe rahisi, wengi hushindwa na kukata tamaa njiani. Lakini siku zote mvumilivu hula mbivu, uvumilivu unahitaji uwe na moyo mkuu, matumaini yasiyokauka katika chemichemi ya moyo, kila ukianguka katika safari amka, songambele, usiumizwe kwa kujikwaa na kuanguka, umia ikiwa utaiacha ndoto yako ipotee. Safari yangu ya maisha ilianza kabla sijaanza, sisemi iliniacha na kuniacha nyuma nikiitazama ndoto yangu ikiwa mbele yangu ikiwa inayoyoma. Ila nataka kusema ndoto ni kama mawingu mepesi angani ambayo hupeperushwa na upepo na kama usipokuwa makini huweza kuyeyuka na mahali pake kusionekane.

Nikapokelewa na Rafiki yangu aitwaye Ibrapapa ambaye nilipenda kumuita Ibra. Ilikuwa Dar es salaam nikitokea kijijini. Niliambiwa ili nifaniikiwe kwenye muziki ingenipasa nifunge safari nije Dar, ndio maana nikajikusanya kwa vihela vidogo nilivyokuwa navyo nikaja Dar. Ibrapapa baada ya kuhitimu shule alikuja Dar kuyaanza maisha, yeye alifikia kwa Baba yake mdogo, Aliniacha Kijijini mimi nikiwa sina mbele wa nyuma, sikuwa na ndugu yeyote aliyekuwa akiishi Dar, Matokeo yangu ya shule hayakutoka vizuri, hata hivyo niliyatarajia hivyo sikuumia sana. Lakini nisingejiongopea kuwa nilichoshwa na kukaa nyumbani miaka miwili ikiwa imepita tangu nilipomaliza shule, ilikuwa miaka migumu sana. Wale waliofaulu waliendelea na shule kwa kwenda shule za mbali zilizo nje ya kijiji chetu na wengine mbali zaidi ya mkoa tuliokuwa tunaishi. Wengine walipelekewa na wazazi wao Veta, huku wengine wakipelekwa vyuo vya kati. Sisi masikini tulibaki nyumbani, tungeenda wapi sasa, shule tumeshindwa, pesa hatuna, labda pesa zingetupeleka mbali mahali ambapo shule ingeshindwa, lakini umasikini tangu lini umpeleke mtu mbali, labda mbali kwenda nyuma ya nyumba yetu na kujivinjari na vijiwe vya mtaani, unajua wakati nasoma sikuwa naliona jua kama linachoma, lakini tangu nilipomaliza shule na kuambulia matokeo mabaya niliona jua kama lina visa na mimi. Jua lilikuwa linachoma jamani! Nikienda shamba kulima nikimsaidia mama yangu, jua halikutuonea huruma hata kidogo. Hapo ndipo nilipata wazo la kwenda mjini, labda ungefikiri ninaenda mjini kulikimbia jua la kijiji chetu, wala ungekuwa haujakosea. Nilichoshwa, nilipaushwa mpaka nikafubaa, wala usingenikumbuka kama hukuniona kwa miaka miwili.

Ibra alipopokelewa na Baba yake mdogo, akatafutiwa kazi pale Kariakoo ya kutoa vitu nje ya duka na kuwapa wateja mizigo. Kazi yake hiyo ndiyo iliyomfanya ndani ya miaka miwili kujitegemea na kuwa na Ghetto lake la kuishi kama kijana mdogo tuu. Nilimuona Ibra kama kijana mwenye bahati sana kwani mambo yake yalikuwa yanamuendea kirahisi. Hata hivyo nilisahau kuwa maisha huwa na milima na bonde, kuna kupanda na kushuka, lakini pia kuna tambarare, maisha huweza kuja mambo yake magumu sana ambayo mtu kama angepewa nafasi achague basi asingechagua mambo hayo mabaya. Lakini maisha yapo mambo mtu huweza kujichagulia yakamfaa au yasimfae lakini yapo mambo katika maisha kamwe huwezi kuyaamua; yanatokea tuu upende usipende! Yakufae au yasikufae!

“ Gibson! Baba yangu mdogo alipatwa na mkosi mkubwa kuliko yote, mauti ilimjia kwa ghafla kama mwivi. Tukamzika! Hapo ndipo maisha yangu yalipotetereka, Mama mdogo akanifukuza kazi kwenye maduka ya kariakoo, kama nisingekuwa na akiba sijui ingekuwaje, labda leo hii ningekuwa nimerudi kijijini. Zamani sikuwa naamini misemo ya wahenga, lakini tukio la kufukuzwa dukani likanifanya nianze kuamini baadhi ya misemo; mathalani msemo usemao; Akiba haiozi. Kwa kweli akiba yangu haikuoza, ilinifaa katika dhiki ile. Nikaichukua nikaongezea kodi, kisha pesa iliyobaki nikawa naipigia mahesabu niifanyie nini. Kama ujuavyo pesa isiyozalisha ni kama mshumaa uwakao moto. Huisha kwa upesi. Kuchelewa sana kutoa maamuzi ya nini nifanye cha kuzalisha kungeliweza kuimaliza akiba yangu. Hii ingenisokomeza zaidi katika dhiki. Pesa yenyewe ya akiba unafikiri ilikuwa nyingi basi, ilikuwa pesa ndogo tuu, hivyo kuisha ingeisha muda wowote kama nisingekuwa najibana” Ibra alimeza mate, kisha akanitazama,

“ siku moja nikiwa napita barabarani huko, nikaona watu wakiwa wameweka biashara zao pembeni ya barabara, zilikuwa biashara zenye mtaji mdogo kabisa usiofika hata laki moja. Niliwaona wauza viatu vya kike, wauza barafu, pamoja na wauza matunda, nikawa nawadadisi kuona kama nami ningeweza kufanya moja ya biashara zile. Wengi maneno yao yalinikatisha tamaa. Wapo waliosema biashara hailipi, wengine wakanambia askari wa jiji huwakatili sana na kuziharibu biashara zao. Lakini nikawa najiuliza ikiwa maneno hayo ni kweli ninayoweza kuyaamini iweje wao wanaendelea kufanya kitu kigumu. Nikasema nitajaribu kuuza matunda, ndio nikaanzisha kile kibanda cha matunda ukionacho pale” Ibra alisema. Moyoni nilimuona kama mtu aliyenizidi maarifa, nilimtazama sasa kama mwalimu mahiri ambaye ninaweza kujifunza kutoka kwake. Sikutegemea kusikia maneno kama yale kutoka kwa Ibrapapa, unajua zamani nilikuwa namchukulia poa, nilikuwa namuona kama mtu mwenye uwezo mdogo wa kufikiri, lakini kumbe maisha huweza kumbadilisha, yupo mtu mwerevu maisha yakamgeuza mjinga wa mwisho, lakini yupo mtu mjinga lakini maisha yakamgeuza mwerevu wa juu kabisa. Basi jambo hilo kama hukuliona kwa mtu, mimi nililiona kwa Ibrapapa, maisha yalimbadilisha.

“ Nilienda kwa seremala nikamwambia anitengenezee meza pana itakayofaa kuwekea biashara ya matunda, seremala akaiunda meza nzuri niliyoipenda sana, nikanunua na mwamvuli kunikinga na jua pamoja na Mvua, Ilikuwa ile miamvuli mikubwa sio hii midogo ya kubeba mkononi. Nikaenda sokoni kununua matunda kwani kule ni bei rahisi, nikanunua matikiti maji, machungwa, matango, ndizi, siku ya kwanza nilichukua mzigo mdogo kama kianzio. Unajua ukitaka kuanza lazima uanze polepole ili kuepuka hasara, pia ili usome mwenendo wa biashara na wateja wako. Siku ya kwanza na yapili biashara haikufanya vizuri, niliwaona watu wakipita wakiwa wananishangaa, nilichukizwa mno, walikuwa wakitazama kama mtu ninayefanya kitu cha ajabu, labda ni kutokana na kuwa eneo lile hapakuwa na wafanyabiashara wengine, mimi nilichoangalia ni njia ipitishayo watu wengi, pia nilipachagua pale kwa sababu ni karibu na hapa ninapoishi, sikuhitajika kupanda gari ambapo hiyo niliihesabu kama gharama” Ibra akainuka akaenda kwenye ndoo ambayo juu yake kilikuwepo Kikombe, akachota maji kisha akanywa kwa mkupuo. Alafu akarudi na kuketi akiwa na kikombe mkononi,

“ Samahani! Koo lilikuwa limekauka” Akasema,

“ Usijali! Enhee! Ikawaje?” Nikamuuliza.

“ Baada ya miezi miwili nikaanza kupata wateja, wakawa wamenizoea, siku zote biashara ni watu, na watu ndio pesa, kadiri unavyopata watu ndivyo unavyopata pesa, kujulikana na watu wengi hupelekea pesa kukufuata, lakini katika kujulikana uaminifu ni jambo muhimu zaidi, kisha lugha nzuri kwa watu, labda hicho ndicho kilifanya nianze kupata riziki yangu”

“ Nikaamua kupaboresha pale, nikanunua mabati na mbao, wakatengeneza vile ulivyopaona, hiyo ni baada ya miezi nane tangu nianze biashara, unaweza ona rahisi lakini wahenga wanasema utamu wa ngoma ingia uicheze. Sikutishi! Ila najaribu kukuelewesha rafiki yangu. Nikaweka na Mabenchi ya mbao, kisha nikaweka na Deli la kuhifadhia maji ya baridi. Nilijifunza kuwa watu wa nchi hii hasa wa huku mjini hupenda kukaa kwenye vijiwe, nilipochunguza nikajua kuwa wengi huaga makwao kuwa wanaenda kazini lakini ungedhani ni kweli”

“ Kumbe wanaenda wapi?” Nikamuuliza.

“ Huishia kwenye vijiwe wakivizia mishetown za hapa na pale, kwa kulijua hilo, ndipo niliweka bao ili wakija wacheze pale nikijua wakikaa muda mrefu watasikia kiu au njaa na kuninunuza bidhaa zangu. Mbinu hiyo ilizaa matunda. Sipati kikubwa lakini walau kinanisaidia kwa mahitaji madogo madogo” Ibra akamaliza kusimulia, akaniaga kuwa anaenda sokoni atarudi baadaye. Nikamsihi niende naye lakini akanikatalia katakata, akidai mimi bado ni mgeni, nipumzike tuu, akaniambia siku ya jumapili atanipeleka kunitembeza maeneo muhimu katika jiji la Dar es salaam. Akatoka.

Hakikuwa chumba kikubwa sana, ila kilitosha kitanda cha tano kwa sita, sofa la watu wawili, kimeza kidogo, palikuwa na Redio iliyokuwa juu ya stuli, beseni lililokuwa na vyombo na masufuria mawili, jiko la gesi, pamoja na ndoo kadhaa, moja ikiwa ni ndoo ya maji ya kunywa, juu ilikuwepo chandarua iliyokuwa inaning’inia, Dirisha moja lilokuwa limefunguliwa pazia ili hewa ipite, udogo wa dirisha lile ulifanya kile chumba kisiwe na nuru ya kutosha, hewa ikiwa haienei vyakutosha, ndio maana chini ya lile kulikuwa na Feni iliyokuwa muda wote inazunguka tangu nifike kwa Ibrapapa. Kulikuwa na joto licha ya Feni kujitahidi kulikabili.

Nikajilaza nikiwa namsikiliza mzungumzaji aliyekuwa akizungumza kwenye Redio. Mzungumzaji hakunishawishi kuendelea kumsikiliza, nikahamisha stesheni mpaka nilipoikuta stesheni inayopiga muziki, nikaacha hapo. Redio ilikuwa faraja kwangu, iliondoa upweke uliokuwa unaniandama, nilitamani ningeondoka pamoja na Ibra. Lakini ndio hivyo tena, nimekuwa kuku mgeni ninayepaswa kufungiwa kwanza ndani mpaka nitakapozoea mazingira.

Hapo mawazo yakanijia na kunifanya niwe kama sipo; “Nahangaika kwa ajili yenu, lakini wewe hujali! Alafu wewe ndiye kaka mkubwa, Gibson hivi ni lini utanionea huruma mama yako, tazama nguo nilizozivaa, angalia mikono yangu, sivai vizuri ili ninyi msome, najibana kwa ajili yenu lakini wewe hujali, unafundisha nini mdogo wako? Gibson shule ni muhimu sana, soma kwanza umalize, muziki utafanya baada ya kumaliza shule mwanangu, tafadhali Gibson jaribu kunielewa hata kidogo” Nilikumbuka maneno ya mama, yalikuwa maneno ambayo yaliufarakanisha moyo wangu. Nilihisi kujilaumu.

Labda kama ningemsikiliza mama yangu sasa hivi nisingekuwa hapa, huenda nikuwa kidato cha sita au chuo mwaka wa kwanza, na hizi taabu ningekuwa nimeziepuka, lakini ukaidi wangu unanigharimu, nimeamini asiyesikia la mkuu huvunjika Guu!

Lakini nikakumbuka; Hakuna njia rahisi, ingawaje zipo njia ngumu sana. Kwa nini nisingechagua njia ya kawaida ya kusoma, nilifikiri kusoma haikuwa njia ngumu wala haikuwa njia rahisi, kunakili vitu kwenye kitabu ukavihamishia kwenye ubongo kisha kuvirejesha tena kwenye karatasi niliiona kama njia ya kawaida kuliko njia niliyoichagua, hiyo ndio nilidhani inaitwa elimu ambayo waliyoipata huringa nayo. Hata hivyo sikufikiri kama elimu ni ubunifu katika kukabiliana na kutatua matatizo ya mtu binafsi na jamii yake.

Jioni ilipofika Ibra alikuja na mboga tukapika, tukala kisha tukalala. Ikawa usiku siku ya kwanza kulala katika jiji la Dar es salaam.

********************

Msururu wa watahiniwa ulikuwa umejipanga katika Jengo la TGT, nami nilikuwa mmoja wao wa watahiniwa niliokuja kufanya usaili katika shindano lile. Nikiwa na nguo zangu ambazo zilikuwa hazivutii kivile niliketi nyuma kabisa. Hapo nikawa natathmini watahiniwa wenzangu waliokuwa mule ukumbini katika jengo la TGT. Nikaona watahaniwa wakiume waliovalia mavazi mazuri yenye kupendeza sana, nyusoni wakiwa wameficha macho yao na miwani nyeusi zenye miundo ya namna za kushangaza, nikakumbuka siku ile niliyokuwa natumbuiza siku ile ya mahafali yangu ya kuhitimu kidato cha nne. Walipendeza sana. Nikafikiri kuwa kama Alice angekuwepo huenda nami ningekuwa miongoni mwa watahiniwa ambao tungekuwa gumzo kwa kupendeza, watu wakitutazama kwa shauku. Lakini leo nipo pekee yangu baada ya miaka mingi kupita, nimevaa marapu rapu, nimejikunyata na kujificha wala sitaki kujitokeza mithili ya kunguni. Hata ningebanwa na haja ndogo nisingekubali kutoka kwenda chooni, nilisikia aibu sana na mavazi yale.

Labda hunielewi, pengine wewe hujawahi kuwa katika hali ya ufukara, hujawahi kuvaa nguo kama marapurapu wakati wengine wakiwa wamevaa nguo zilizowapendeza. Nilivaa viatu ambavyo nyuzi zake zingeachia muda wowote, nilikuwa nikizinyenyekea nikitembea kwa staha kuzibembeleza zinivumilie zisijekuachia, vilikuwa vimechakaa. Tisheti niliyoivaa ndio ileile aliyoninunulia Alice, ilikuwa imepauka mno, usingeikumbuka wala kudhani ilikuwa ya rangi nyeupe, ilikuwa inakaribia rangi ya maziwa, yale maandishi ya Gibson Ft Alice yaliyokuwa yamemeguka meguka, nami nilikuwa nimevaa miwani, wala usingedhani kuwa niliyekaa pale nilikuwa mwanamuziki labda ungenidhani ni mchekeshaji wa kizamani na wala nisingekulaumu kama ungefikiri hivyo.

Kipaza sauti kilikwaruza kwaruza, watu wote tukakaa kimya, kisha sauti nyepesi laini ya kike tukaisikia kutoka katika kile kipaza sauti.

“ Tunawakaribisha wote katika ukumbi wa TGT, muda mfupi ujao zoezi litaanza, kabla zoezi halijaanza, watapita watu watakaowapatia namba ambazo hizo ndizo zitawatambulisha, utaitwa kwa namba utakayopewa. Karibuni sana! Jisikieni huru” Ile sauti ikaacha kusema, na mara moja zoezi la kupewa namba likaanza, ndani ya dakika kumi watu wote tuliokuwa pale ukumbini tulikuwa tumepewa namba.

Tukaanza kuitwa mmoja baada ya mwingine, nikiwa nasubiri zamu yangu, macho yangu yalipendezwa na mwanamke mmoja ambaye alikuwa amevalia gauni jeusi refu lilishika mwili wake vyema na kuachia upande wa chini kwenye miguu, alikuwa na umbo ambalo ninashindwa kulielezea, kiuno chake kilikuwa chembamba, hips na makalio yakichomoza ungedhani ni kituu maji, maziwa yake yalikuwa ya wastani, alikuwa anasura nzuri sana ninashindwa kueleza, rangi yake ilikuwa ya maji ya kunde inayoteleza. Kwa kweli sikuwa kuona mwanamke mzuri kama yule tangu kuzaliwa mpaka hivi leo, yule mwanamke akiwa umbali uleule akageuza shingo yake na hapo tukatazamana, kwa aibu kubwa nikakwepesha macho yangu. Uzuri wake haukustahili kuangaliwa na mwanaume fukara kama mimi, hivyo ndivyo nilidhani. Nilimuona kama malaika aliyenitazama mmi niliyemuovu, utukufu wake sikuustahimili.

Polepole nikayapeleka tena macho yangu kuona kama bado ananiangalia, nikashtuka tena kumuona bado alikuwa ananitazama, nikakwepesha tena, yule mwanamke kuona hivyo akawa anacheka akiwa anauziba mdomo wake na mkono wake, alikuwa na meno meupe yaliyopangika kisawasawa. Bado ingenichukua muda kuyaona mapungufu yake, hata sijui ingechukua muda gani ili niyabaini mapungufu yake, alikuwa mzuri sana.

ITAENDELEA,,,,,
 
KABURI LA MWANAMUZIKI ( Sehemu ya 04)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

SEHEMU YA 04
ILIPOISHIA

Kwa kweli sikuwa kuona mwanamke mzuri kama yule tangu kuzaliwa mpaka hivi leo, yule mwanamke akiwa umbali uleule akageuza shingo yake na hapo tukatazamana, kwa aibu kubwa nikakwepesha macho yangu. Uzuri wake haukustahili kuangaliwa na mwanaume fukara kama mimi, hivyo ndivyo nilidhani. Nilimuona kama malaika aliyenitazama mmi niliyemuovu, utukufu wake sikuustahimili.
Polepole nikayapeleka tena macho yangu kuona kama bado ananiangalia, nikashtuka tena kumuona bado alikuwa ananitazama, nikakwepesha tena, yule mwanamke kuona hivyo akawa anacheka akiwa anauziba mdomo wake na mkono wake, alikuwa na meno meupe yaliyopangika kisawasawa. Bado ingenichukua muda kuyaona mapungufu yake, hata sijui ingechukua muda gani ili niyabaini mapungufu yake, alikuwa mzuri sana.

ENDELEA
Ikawa ananifanyia makusudi, nikimtazama ananiangalia, nami nikawa nakwepesha macho yangu hivyohivyo ikawa kama mchezo, punde nikasikia namba yangu ikitajwa, upesi nikajiweka sawa kisha nikazipiga hatua zangu kusonga kumfuata Mwanaume mmoja aliyevalia suti nyeusi iliyomkaa vyema, Yule mwanaume akiwa ameshika faili lenye karatasi nyeupe akaniuliza kuthibitisha mimi ndiye mwenye namba aliyoitaja, baada ya kumjibu akafungua mlango akiniambia nimfute, nikamfuata nyumanyuma kama mkia wa mjusi. Tuliifuaata korido mpaka tulipokatisha kulia ambapo tulikabiliwa na lango lenye kibao kilichoandikwa TANZANIA GOT TALENT mbele ya maandishi ukifuatia mwaka wa shindano lile.

Tanzania Got Talent (TGT) lilikuwa shindano kubwa lililokuwa likifanyika mara moja kwa mwaka kwa lengo la kutafuta vijana wenye vipaji, lilikuwa shindano kubwa sana ambalo kwa kweli tangu kuanzishwa kwake limeibua vipaji vingi mno, Kupitia shindano hili wapo wasanii wakubwa wa muziki wamekuwa mashuhuri baada ya kuibuliwa na TGT, mbali na muziki pia TGT imeibua vipaji vya kucheza, kuigiza, kuchora, ususi, uchongaji na sanaa zingine. Siku ya leo name nilikuwa moja wa watahiniwa ambao tutashiriki katika shindano la TGT, hii kwangu niliihesabu kama hatua ya pili kuipiga katika muziki baada ya ile hatua ya kwanza niliyoipiga siku ile niliyotumbuiza kwenye mahafali ya kidato cha nne.

Yale mashindano kwangu yalikuwa ni muhimu sana katika safari yangu ya muziki, shindano hili kama nitafanikiwa kushiriki litaniibua na kunitangaza, litakuza jina langu. Pambano hili nililiona kama pambano langu la mwisho la kuyapigania maisha yangu, kuipigania ndoto yangu. Yale yote niliyoyawaza nikiwa mdogo leo ndio itakuwa mwanzo wa kutimia ikiwa nitasahiliwa na kufanikiwa kuwa mshiriki, lakini kama nisipochaguliwa basi ndoto zangu zingekuwa zimeishia hapo. Unaweza kugundua kuwa nafasi hii kwangu ilikuwa ni muhimu kwa kiasi gani.

“ Utaingia lango hili, ukishaingia utaangalia chini utakuta michoro inayokuelekeza njia ya kwenda na wapi pakusimama kwenye jukwaa, haya kila la kheri” Yule mwanaume alinipa maelekezo, kisha akanifungulia mlango nikaingia yeye nikimuacha, chini nilipokelewa na mchoro wa mshale ulionielekeza ninyooshe mbele, nikatembea nikiwa ndani ya mistari miwili ya rangi nyeupe iliyochorwa kwa chini, hatua kumi nikauona mchoro wa mshale mwingine ukiwa umekata kushoto, nikaufuata nikiwa bado ninafuata ile mistari miwili ambayo ilikuwa kama barabara ya kuifuata, nilipokatisha nilipokelewa na jukwaa kubwa mbele kabisa ya jukwaa upande wa kulia nikawaona watu wanne wakiwa wamekaa kwenye viti mbele yao ikiwepo meza kubwa ya kisasa, watu wale walikuwa wakinitazama kwa macho ya kunisahili, ukumbi wote ulikuwa umepoa kwa kiyoyozi kilichokuwa kinapuliza, ulikuwa ukumbi wa kisasa kabisa wenye kila sababu ya kulinganishwa na kumbi zenye mvuto za kufanyia maonyesho ya sanaa. Nikatembea mpaka ile mistari miwili iliyokama barabara ilipounganika na mchoro wa duara alafu katkati ya lile duara niliona mchoro wa katuni yenye umbile la binadamu ikiwa imesimama. Nikajua kuwa hapo ndipo ninapaswa kusimama, nikasimama, nikainama kama sehemu ya kutoa heshima, namba niliyopewa nikiwa nimeibandika kifuani kwenye tisheti.

Wale watu wanne ambao niliwatambua kama Majaji ya shindano lile;wawili walikuwa wanawake, wawili walikuwa wanaume. Juu ya meza mbele ya kila jaji kulikuwepo na kibao kilichoandikwa jina lake, hata hivyo sikuwa na muda wa kuyasoma majina yao, Pembeni ya vile vibao vyenye majina yao kulikuwa na vijitabu Fulani, madaftari na karatasi, kalamu zilikuwa juu ya meza.

Baada ya kujitambulisha moja ya wale majaji akasema;

“ Karibu sana Ndugu Gibson, hili ni shindano kubwa katika nchi yetu ambalo limesaidia vijana wengi, ninaamini kama utaonyesha uwezo mkubwa siku ya leo basi utashriiki katika shindano hili. Siku ya leo watahiniwa ni wengi kama ulivyowaona huko nje, wanahitajika washiriki hamsini tuu watakaoshiriki, bila shaka umejiandaa, utaonyesha sanaa gani ndugu Gibson?”

“ Nitaimba, mimi ni mwanamuziki” Nilijibu nikijiweka sawa.

“ Vizuri! Utaimba wimbo wako au wimbo wa msanii mwingine?” Yule mwanaume Jaji akaniuliza.

“ Nitaimba wimbo wa msanii mwingine”

“ Kwa nini usiimbe wimbo wako, au haukusema wewe ni mwanamuziki? “ Jaji wa kike akanikatisha na kunitupia swali.

“ Leo nitaimba nyimbo za msanii mwingine ambao unajulikana na watu wengi, kisha siku nyingine nitaimba nyimbo zangu” Nikajibu nikiwa nimetulia.

“Sawa! Jukwaa ni lako, kila la kheri” Yule jaji mwanaume akasema, nafikiri huyu ndiye alikuwa Jaji kiongozi. Nikainama kwa heshima, kisha nikachukua maiki. Nikafumba macho kuituliza akili, kuimba kuna hitaji akili iliyotulia, ili kuweza kuamuru viungo vya mwili vile inavyotakiwa, nikaanza kuimba wimbo wa mwimbaji mashuhuri wa uingereza, nilihakikisha sauti yangu haiiachi pumzi, mazoezi ya pumzi yalinisaidia sana kuimba Key za juu katika wimbo ule, sekunde kumi na tano nikayafumbua macho yangu polepole nikiimba kwa uhakika, alafu nikaanza kuuchanganya wimbo nikitembea kwenye jukwaa kama msanii aliyebobea, jukwaa nililitawala vilivyo, kuna wakati nikawa ninaimba huku nikiwatazama majaji ambao niliwaona kila mmoja wao akiwa ananitazama kwa shauku kubwa. Niliwapa ambacho walikuwa hawajakitarajia, niliwashangaza kwa namna nilivyokuwa naimba huku nikiimba. Kama nisipofanya vizuri siku hii ya kwanza, sifikiriii kama kuna siku nyingine ya kufanya vizuri zaidi ya siku ya kwanza kwani nyota njema huonekana asubuhi. Siku ya kwanza ninaifananishaga na siku ya mwisho.

Nikapandisha sauti yangu katika Key za juu kabisa nikiwa nimekuja uso kwa hisia kali mno, polepole nikapiga magoti yangu bado sauti yangu ikiwa juu, nikiwa nimekunja uso niliwatazama majaji ambao nao niliwaona wakiwa wamekuja sura zao kwa hisia wakifuatia sauti yangu. Nilizipandisha juu hisia zao, haya yalikuwa mafanikio niliyokuwa nimeyasubiri kwa dakika tatu nilizokuwa pale jukwaani. Nikayafumba macho yangu na kuishusha Key ya wimbo; nikamaliza. Hapo nikashtushwa na sauti za makofi kutoka kwa wale majaji, nikayafumbua macho yangu ambapo nikawaona wakiwa wamesimama bado wakiwa wanapiga makofi. Kila mmoja wao alinipongeza, akinisifia jinsi nilivyokuwa na kipaji kikubwa. Walinambia kama nitaendelea vile basi ninaweza kuwa mshindi wa shindalo lile.

Nikadhani huenda njia yangu ingekuwa rahisi kulingana na majibu yao lakini haikuwa kama nilivyotarajia.

Nikatoka, wakaniambia watanipigia simu kama nitakuwa nimefaulu kushiriki katika shindano lile. Nikatoka nikiwa nimejawa na matumaini makubwa, nilipofika kule kwenyeb ukumbi wa watahiniwa nikakutana yule mwanamke Mzuri asiye na mfano, nikamsalimia lakini kabla sijazungumza naye saa namba yake ikatajwa kuwa naye aende kwenye usahili. Kwa kweli sikutaka kupoteza nafasi kwa yule mrembo, upesiupesi nikaomba kalamu nikamuandikia namba yangu ya simu kisha nikampa ile karatasi yenye namba, nikamtakia kila la kheri, tukaagana yeye akiingia kwenye ukumbi wa usahili mimi nikarudi nyumbani.

*****************

Hakuna asiyechoka, hakuna atakayekuvumilia mpaka mwisho, ikiwa wewe mwenyewe kuna muda unaweza kujichoka sembesu mtu mwingine. Hata hivyo wewe pekee ndiye unaweza kujivumilia hata uwe na madhaifu gani, wewe ndiye unaweza kujijali na kujipenda. Ndivyo ilivyokuwa kwangu, Ibra akanichoka, lakini hata mimi nilikuwa tayari nimechoka kukaa kwake, kama ingekuwa ni amri yangu basi ningekuwa nimeshaondoka kwa Ibra, sisemi kumsema vibaya; nitaonekena sina shukrani. Msaada alionipa ibra ulikuwa mkubwa sana. Ibra alichonichosha nacho ni tabia yake ya kurudi akiwa amelewa pombe chakari, lakini atanichoshaje ilhali pale ni kwake, hilo nalo neno. Basi niseme mimi ndiye niliyemchosha hata ninyi mtaweza kunielewa. Pengine nilimnyima uhuru wa kutumia Ghetoo lake vile atakavyo, Ibra alikuwa akija na wanawake kila mara, jambo ambalo kwangu lilikuwa kama ujumbe wa akufukuzaye hakwambii toka.

Kwa vile nilikuwa nikimsaidia kuuza matunda nilijiwekea akiba ndogo ya pesa nikiwa ninampango wa kuondoka pale kwa Ibra na kujiteegemea, lakini kabla sijafanikiwa kufika mbali katika akiba yangu, Ibra siku moja aliniweka kikao, akaniambia;

“ Gibson Rafiki yangu, ninaomba unisamehe sana, usije ukadhani ninakufukuza hapa kwangu, wewe wenyewe unajua sisi ni marafiki wakubwa tulioshibana, lakini maisha wakati mwingine huja na mambo ambayo hatujayatarajia, wiki hii nitakuomba ujiandae uhame hapa, kuna mdada nimempa ujauzito, wazazi wake wamemfukuza kwao, hivi hapa ninavyoongea huyu shemeji yako yupo kwa rafiki yake, lakini kama unavyojua wanawake hawawezi kaa pamoja muda mrefu pasipo magomvi, wamegombana, hivyo nitamleta hapa, hatuwezi ishi wote watatu chumba kimoja Gibson” Maneno ya Ibra yalinipa mawazo sana, sasa nitaenda wapi, akiba yangu yenyewe ilikuwa haitoshi hata kodi ya miezi miwili kwa chumba cha kawaida.

Niliingia katika mawazo, niliiona shida iliyokuwa inakuja mbele yangu. Sikujua hata nitaikabili vipi. Basi zikapita siku tatu baada ya Ibra kuniambia mambo hayo, siku ya nne Ibra alirudi usiku wa saa tano akiwa na mwanamke mmoja, baada ya kukaribishwa Ibra akanitambulisha kwa yule mwanamke, ndiye yule aliyekuwa anamimba yake. Sikuwa na jinsi nilifungasha virago vyangu, sikuwa na vitu vingi, nilikuwa na begi moja la mgongoni ambalo lilikuwa na nguo chache sana.

Ibra akanisindikiza usiku ule mbalamwezi likitumulika, wote tulikuwa kimya, mimi nilikuwa nafikiri nini kinafuata baada ya yale; Ibra akasema;

“ Sasa unaenda wapi ndugu yangu?”

“ Mimi mwenyewe sijui ninakoelekea, lakini usijali kadiri ninavyotembea nitaupate uelekeo” Nikamjibu hasiria zikiwa zimenikaba kooni. Angewezaje kuniuliza swali la namna ile, yeye kama hakujua ninakoelekea kwa nini anitoe usiku ule, alafu swali lile haikuwa muda wake, labda angeniuliza kabla hajamleta huyo mwanamke wake. Lakini hasira zangu zilikuwa sawa na bure tuu. Ibra hakuwa na kosa lolote, yeye alishanisaidia vyakutosha licha ya kuwa sio ndugu yangu, wala hatuna ukaribu wa kinasaba, nimekaa kwake miezi sita, huo ungehesabika msaada mkubwa sana, lakini kama ujuavyo sisi wanadamu hatuna shukrani hata kwa mambo madogo, huwezi amini nilimchukia Ibra. Ninaweza kusema, siku ile Ibra aliipanda mbegu ya chuki katika moyo wangu ambayo sikujua angekuja kuivuna lini. Embu tuone!

Nikaagana na Ibrapapa baada ya kuita bodaboda, nikapanda na kuondoka mbele ya uso wa Ibra akiwa ananisindikiza kwa macho, nikiyoyoma na kupotea katika barabara.

“ Boss unaeelekea wapi?” Bodaboda akaniuliza.

“ Nipeleke kwenye Night Club ilikuwa karibu na eneo hili, hakikisha iwe inakesha usiku kucha hiyo Club” Nikasema, upepo ukinipiga usoni.

“ Sawa Boss haina shida, nitakupeleka NATO NIGHT CLUB, Kuna watoto wakali sana pale” Bodaboda alisema, mimi sikumzingatia sana, kichwa kilikuwa kinamengi sana ambayo sijui kama ningeweza kuyamaliza kuyawaza, nilikuwa loaded. Tukafika, nikamlipa Bodaboda, akaondoka na kuniacha na begi langu mgongoni.

Nato Night Club kulikuwa kumechangamka sana, wala usingedhani ni saa sita za usiku jinsi watu walivyokuwa wamefurika, kwa nje nilipokelewa na wadada warembo waliovalia sare za kuvutia mno, sketi zao fupi zilizoacha wazi mapaja yao makubwa na laini yanayomeremeta kama bilauri ilikuwa kichocheo kikubwa wa wanaume wengi, niseme kuwa kitendo cha kufika tuu eneo la ile club kilinipunguzia mizigo yangu iliyokuwa kichwani, kuwaona wanawake wa Club ile kulifuta kwa muda kumbukumbu za matatizo yangu. Bado nilikuwa nje nikiwa nafanya ukaguzi wa eneo lile, juu lilikuwepo bango kubwa linalowakawaka rangi tofautitofauti, maandishi “NATO NIGHT CLUB” Yalisomeka katika bango lile yalizidi kuleta mvuto wa kipekee kwa kila aliyepita barabara hiyo na kuitazama Club hiyo. Wadada watatu wakanilaki wakinishika mikono kunikaribisha katika Club yao, ukarimu wao ulivuka mipaka, uliziteka hisia zangu na kunifariji, leo mimi fukara ninakaribishwa kwa heshima zote na wanawake warembo kama wale, kumbe nilikuwa najidanganya, na kama ningelijua jambo hili mapema huenda nisingekubali kupewa hehima kama ile. Sikujua ni muda gani begi langu liliondolewa mgongoni mwangu mpaka nilipokuwa nimeketi kwenye kiti ndani ya Club nikiwa nimesimamiwa na mhudumu aliyevalia sare tofauti na wale wanawake wa mapokezi kule nje.

“ Samahani kaka, karibu sana Kwenye Club yetu, hii ni Menu yetu unaweza kuipitia alafu useme nikuletee nini” Yule Dada Mhudumu mwenye sura ya upole na macho yaliyoficha ujanja kwa ndani kabisa alisema akinitazama. Sauti yake ilizingatia sheria na kanuni za uhudumu kwa mteja, ilikuwa sauti tulivu iliyobeba ukarimu, kujali na ushawishi ambao mteja yeyote asingeweza kuleta ukaidi.

Nikasoma ile Menu kisha nikaagiza Pombe ya bei nafuu. Yule Mhudumu akaondoka, hapo nikapata wasaa mzuri wa kuweza kusahili watu waliokuwa mule ndani. Watu wengi mle ndani walikuwa Vijana ambao walikuwa wamekaa makundi makundi wakiwa wamezunguka meza zilizosheheni pombe za namna mbalimbali, wapo waliokuwa wakicheza kufuatia muziki uliokuwa ukipiga, sauti ya muziki ilikuwa juu mno, kusikilizana isingewezekana labda kwa kuongea kwa sauti ya juu, niliwaona pia wadada warembo waliovalia nguo fupi mno ambazo ziliacha sehemu kubwa ya miili yao, Nikangalia upande wa mbele kabisa ilipo kaunta, nikaona Wanaume sita wakiwa wamekaa kwenye stuli ndefu huku wakiwa wamesimamiwa na wanawake kila mmoja wao. Nilivutiwa na Mrembo mmoja aliyekuwa amebeba Mtungi wenye mrija aliokuwa akiuvuta, ilikuwa ni Shisha, kilichonivutia kwa mrembo huyu ni vile alivyokuwa akiutoa moshi huku akicheza muziki kama mtumbuizaji aliyepandwa na Majini. Niliacha kumtazama mrembo yule pale mhudumu alipokuwa ameweka kwenye meza pombe niliyokuwa nimemuagiza.

“ Naomba pesa!” Yule mhudumu akasema akinitazama kwa macho yake ya upole akijitahidi kuficha ujanja ambao niliuona ukiwa umejificha.

Hapo ndipo nilipogundua begi langu halipomgongoni, nilikuwa kama nimepagawa, niligeuka huku na huku, mara niiname chini ya meza kuangalia kama ningeliona Begi, Yule mhudumu alikuwa akinishangaa tuu,

“ Kaka Vipi! Mbona sikuelewi?” Yule Dada mhudumu akaniuliza.

“ Umenionea Begi langu hapa?” Nikamuuliza yule Mhudumu akiwa ananishangaa.

“ Begi! Begi gani?” akahamaki,

“ Nilikuja na Begi hapa Dada..”

“ Samahani kaka, usitake kuniharibia siku, naomba hela niende nikahudumie wateja wengine”

“Kweli! Nimekuja na begi hapa, ndipo hela nilipoziweka” Nikasema huku nikijua tayari nimelizwa.

“ Begi lako halinihusu, ninachotaka pesa yangu. Usiniletee michezo ya mjini hapa, watu kama nyie mimi sio mgeni” Yule Mhudumu akasema, ile sura yake ya upole haikuwepo tena, macho ya ukali yalishaanza kunawiri usoni mwake.

“ Itakuwa wale wadada, washenzi sana! Ngoja niwafuate” Nikasema nikitaka kuondoka.

“ Weeeh! Kaka! Kaka! Usitake nikufanyie fujo hapa, lipa pesa kwanza ndio uende kwa hao Malaya wa hapo nje, wewe kwani mgeni hapa jijini. Mwanaume mzima unakuwa kama mpuuzi, unaibiwaje kijinga na hao Malaya hapo nje. Embu nipe pesa yangu usinipotezee muda wangu” Sasa yule mhudumu sauti yake ilikuwa juu, haikuzingatia tena sheria wala kanuni za kuhudumia wateja.

“Nimekamatika!” Nikawaza nikawa nimeishika kiuno; uso wangu nikiwa nimeuelekeza chini. Yule dada mhudumu akawa ananitathmini akinitazama.

“ Kaka, unanipa pesa au hunipi?” Akaniuliza.

“ Dada yangu, nashindwa hata nikujibuje, pesa niliyokuwa nayo ilikuwa kwenye begi, kama wameliiba hilo begi mimi sijui itakuwaje, hapa nilipo sina hata mia, Dada yangu naomba unisaidie”

“Koma! mimi sio Dada yako, unataka nikatwe kwenye mshahara wangu kisa ushamba wako. Security! Security!” Yule Dada akasema akiwa anaita kwa sauti kubwa, watu waliokuwa karibu wakageuka kututazama, niliwasikia wengine wakisema; hawa ndio matapeli wa mjini. Wengine nikawasikia wakisema; Mwanaume unapenda kula bata alafu huna pesa, utaolewa. Sikuona hata mtu mmoja aliyenionea huruma. Security walikuwa wamefika, walikuwa wanaume wawili wenye miili iliyojengeka haswa, walivalia tisheti nyeusi zilizowashika vizuri, mikono yao ilikuwa na mishipa mingi ya ukakamavu na hii ikanifanya nione wale wanaume walizingatia ratiba za mazoezi.Wakia na sura mbaya zilizovishwa miwani nyeusi wakanikamata na kuanza kuniburuta msobemsobe wakinipiga mitama, nilikuwa nikipiga makelele kutokana na maumivu niliyokuwa nayapata. Watu wakawa wameacha kunywa wakinishangaa nikiwa natolewa nikipigwa.

“ Niacheni nyie! Acheni kunipiga! Mnanipiga nini? Pombe yenu hata sijanywa mnanipiga! Mnanionea tuu bure!” Nilikuwa nikipiga kelele, baadhi ya walevi walikuwa wakicheka, wengine wakanimwagia pombe basi mambo ilimradi yanikere.

“Huyu hatujampa chai ya kutosha ndio maana anaongea ongea, ongeza sukari kwenye chai mpaka ashindwe kutunga sentensi” Nikasikia mwanaume akisema. Na hapo nikashtukia ngumi ya tumbo na mateke mfululizo ya tumbo, sasa hapo nikashindwa hata kutoa sauti, kila nilipokuwa nikijaribu kutoa sauti nje, sauti ilikuwa haitoki.

Wakanitoa nje ya Club, hapo wakawa wananichapa na mikanda!

“ Muacheni!” Sauti ya kijana mmoja nikaisikia ikisema. Wale wanaume wakaacha kunipiga kisha wakageuka kumtazama aliyesema waniache.

“ Inatosha sasa! Anadaiwa kiasi gani” Yule kijana akauliza. Wale wanaume walikuwa hawajui hata nadaiwa shilingi ngapi, akaitwa yule mhudumu. Akasema kiasi ninachodaiwa. Akalipa kisha akawaamuru waniache niondoke Wale wanaume wakaniacha wakaingia zao ndani ya Club. Pale nje kama nilivyopakuta bado wale wanawake warembo walionipokea walikuwepo wengi lakini sikuwa naweza kuwakumbuka wale wadada watatu walionipokea wakati nilipofika.

“ Haya Amka! Amka uende nyumbani” Yule kijana akasema,

“ Ahsante sana ndugu yangu, wangeniua hawa washamba” Nikasema.

“ Amka uondoke” Akasema huku akinisaidia kunivuta nisimame. Niliposimama nikawa najiweka sawa, nilikuwa nimelowa yale mapombe waliyonimwagia kule ndani ya Club.

“ Kwa nini umenisaidia?” Nikamuuliza yule kijana.

“ Sio mimi niliyokusaidia” Akanijibu akitabasamu.

“ Sio wewe? Kivipi sasa?:” Nikauliza kwa kushangazwa na jibu lake.

“ Ningekuwa mimi ndiye nimekusaidia ndio ungeniuliza kwa nini nimekusaidia, lakini sio mimi niliyekusaidia” Akanijibu akinitazama. Tukakaa kimya nikitafakari majibu ya yule kijana, hapo nikakumbuka nina kisimu cha batani, nikakitoa mfukoni nikatazama saa, ilikuwa saa nane za usiku. Sauti ya yule kijana ikanikatisha nikiwa naangalia simu,

“ Hata sijui aliyekusaidia amekusaidia kwa sababu gani?”

“ Ni nani huyo? Tafadhali niambie” Nikamuuliza nikiwa nashauku.

Lakini yule kijana hakuniambia aliyenisaidia ni nani, akaniamuru niondoke niende nyumbani, akaondoka nikiwa namuita;

“ Wewe! Ndugu yangu! Mbona unaondoka sasa, tafadhali niambie nani aliyenisaidia, niambie ndugu yangu, wewee! Usinifanyie hivyo” Niliongea nikiwa namfuata nyumanyuma yule kijana, mpaka tulipofika kwenye gari nyeusi la kifahari, yule kijana akafungua mlango wa nyuma wa lile gari akaingia, akafunga mlango, nikainama kwenye kioo cha lile gari nikimuita;

“ Wewe! Tafadhali! Nambie hata jina lako basi!, niambie unaitwa nani” Niliongea lakini gari likaondoka nikawa nalikimbia mpaka liliponizidi kasi, likayoyoma na kupotelea kwenye kona, likiniacha nikiwa nimesimama nalisindikiza kwa macho uso wangu ukiwa umehamanika.

ITAENDELEA
 
KABURI LA MWANAMUZIKI ( Sehemu ya 05)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

Sehemu ya 05
ILIPOISHIA

“ Wewe! Ndugu yangu! Mbona unaondoka sasa, tafadhali niambie nani aliyenisaidia, niambie ndugu yangu, wewee! Usinifanyie hivyo” Niliongea nikiwa namfuata nyumanyuma yule kijana, mpaka tulipofika kwenye gari nyeusi la kifahari, yule kijana akafungua mlango wa nyuma wa lile gari akaingia, akafunga mlango, nikainama kwenye kioo cha lile gari nikimuita;
“ Wewe! Tafadhali! Nambie hata jina lako basi!, niambie unaitwa nani” Niliongea lakini gari likaondoka nikawa nalikimbia mpaka liliponizidi kasi, likayoyoma na kupotelea kwenye kona, likiniacha nikiwa nimesimama nalisindikiza kwa macho uso wangu ukiwa umehamanika.

ENDELEA
“Nimesaidiwa na nisiyemjua, nimeokolewa na nisiyemfahamu, amenisaidia wala hakutaka nimjue jina lake, katikati ya mabaradhuli amenitetea, usiku wenye giza ameiokoa nafsi yangu” Nilikuwa nikiwaza nikiwa nimesimama kama mlingoti, nikiwa naangalie uelekeo wa lile gari lilipotokomea. Nikaondoka eneo lile nikiwa sina hata sumni mfukoni, wapi nilikuwa naenda, hata mimi sikuwa nafahamu. Nilikuwa kama kikaragosi kinachopelekwa na upepo, ambacho hakijui hatma yake. Simu yangu ya batani iliniambia ni saa tisa za usiku, yakiwa yamesalia masaa matatu tuu alfajiri ifike.

Nikatembea kandokando ya njia mpaka nilipofika Manzese Darajani, nikawaona vijana wa hirimu kama yangu wakiwa wametandika maboksi chini ya lile daraja wakiwa wamelala, hawakujali baridi wala mbu waliokuwa wakiwauma, walilala fofofo kwa starehe wala usingedhani walikuwa wamelala nje. Nikapanda juu ya lile Daraja, nikakutana pia na watu wengine wakiwa wamelala kwa raha au kwa shida zao, hiyo wala haikunihusu, mbele kidogo mwisho wa daraja kwa juu kwenye ngazi ya kwanza ya kushukia niliona mtu akiwa amekaa anavuta sigara, nikapiga hatua polepole kumfuata mtu yule, alikuwa ni mwanaume wa makamo hivi, aliyevalia nguo zilizochafuka sana, nywele zake zilikuwa chafu zinazonuka uvundo, zilikuwa varuvaru zimevurugika, mashavu yake yalifunikwa na ndevu zilizokuwa zinatisha sana, nilifikiri ni kichaa, hofu ikawa imeniingia, ipo hofu ya uchizi, chizi wanautisho wao Fulani ambao kwao ni ulinzi. Nikatembea polepole kama mtu nisiyetaka kumshtua, bado yule mwanaume niliyemtambua kama chizi alikuwa akivuta Sigara huku akiyatazama magari machache yaliyokuwa yakipita chini ya lile daraja.

Nikampita pale alipokuwa amekaa nikiwa nateremka kwenye ngazi za lile Daraja, yule mtu ambaye akanishtua na sauti yake wakati nikiwa nashuka;

“ Oya! Vipi Mwanangu! Unapita wala hatusalimiani usiku wote huu?’ Yule mwanaume chizi akaniongelesha. Nikasimama nikiwa nimempa mgongo nisijue nimjibu nini.

“ Huo sio uungwana ndugu yangu, salamu ni kitu kidogo lakini kinaweza kukupa heshima, salamu wakati mwingine inaweza kuwa chanzo cha msaada wako ikiwa utapata shida, mwanangu umeniangusha sana” Yule mtu chizi akasema, nikageuka kumtazama, macho yetu yakawa yanatazamana, yule mtu akaiweka sigara yake mdomoni akavuta pafu ndefu kisha akaninyooshea mkono kunipa ile sigara, nikapiga hatua kupanda juu kama ngazi mbili ili nimfikie, alafu nikaichukua ile sigara na kuvuta pafu mbili, alafu nikawa naisikilizia ile sigara namna ilivyokuwa inaingia kwenye mwili wangu, uso wangu nikiwa nimeangalia nyota za angani, kisha nikavuta pafu la tatu kabla sijakaa karibu ya yule mwanaume chizi. Nilipoketi nikamtazama yule mwanaume, sasa niliweza kuuona uso wake kwa ukaribu zaidi, alikuwa na macho mekundu, ngozi yake ya uso ikiwa haina rutuba, mdomo wake ulikuwa kwa ndani ukiwa umeficha na ndevu nyingi ambazo zilikuwa zimeanza kuwa za kijivu kutokana na mvi.

“ Unatoka wapi na unaenda wapi mwanangu?” Yule mwanaume akasema, akitoa sigara nyingine na kuipachika mdomoni, akaiwasha. Nikawa nipo kimya bila ya kumjibu, nikiyaangalia magari machache yaliyokuwa yakienda na mengine yakirudi yakipita chini ya daraja.

“ Oya! Mshikaji! Hutaki kunijibu?’ Akasema.

“ Nikijibu nini? Sababu ya hii sigara yako ndio umeona imekupa haki ya kuniuliza maswali! Haya shika, nimetoka wapi, ninaenda wapi or whatever itakusaidia nini wewe kichaa” Nilimjibu kwa hasira, mtu akiwa kwenye msongo wa mawazo mara nyingi hataki usumbufu wowote, maswali kwa mtu mwenye matatizo ni usumbufu na kero ambayo haivumiliki. Hivyo maswali yake yalinichefua sana, nikaamka nikitaka kuondoka pale.

“ Oya mwanangu, kwa hiyo umemaindi sio! Kausha basi” Yule chizi akasema, mimi sikumsikiliza nikaanza kupiga hatua nikishuka kwenye zile ngazi za lile daraja.

“ Oya! Mshikaji wangu, Yaani unasepa kisa mambo madogo, kama vipi Baridi! Unafikiri nitakubembeleza, huo si uchoko!” Yule chizi nilimsikia akiongea mimi nikiwa tayari chini ya daraja nikiwa ninaondoka kwenda nisikokujua, Nikaiacha Morogoro road na kuzama katika vichochoro vya manzese, nikatembea mpaka nilipohisi kuchoka, hali ya hewa ilibadilika; mawingu mepesi yalitawala anga, punde manyunyu yakaanza kudondoka, nikatembea mpaka nilipoona yanaongezeka ndipo nikajificha katika kivaranda kwenye moja ya nyumba za eneo lile. Simu yangu iliniambia ni saa kumi na dakika ishirini. Yalibaki masaa machache kukuche.

“ Ni siku nyingi zimepita tangu niende kufanya usahili katika mashindano ya Tanzania Got Talent, mpaka hivi leo hawajanipigia simu, sijui nini kimetokea, labda sikuchagulia, inamaana kuna watu wenye vipaji kunishinda, haiwezekani, sijaona mtu wa kunishinda kwenye muziki, pakikucha nitaende mpaka kwenye jengo la TGT nikawaulize kulikoni, mmh1 Lakini waliniambia watanipigia, kama nitaenda wanaweza kuniona kama msumbufu, acha nisubiri” Nikawaza mpaka pale usingizi uliponichukua pasipo ya mimi kujua.

*********************************************

Nilikurupuka kama kondoo aliyeshtushwa na sauti ya mbwa, nikaamka nikiwa natetemeka, nilikuwa chapachapa baada ya kumwagiwa maji na mwanamke wa makamu aliyevalia Dera.

“ Wewe kibaka tokaa hapa kwangu, ondoka nisije kukuitia mwizi, ninyi ndio waizi wenyewe, aliyekuambia hapa ni nyumba ya kulala wageni ni nani, huna kwenu mjaa laana wee! Ondoka haraka” Yule mama aliongea kama chiriku, alafu akanipiga na ile ndoo ya maji aliyokuwa ameishika, niliumia.

“ Hawa ndio wezi wenyewe, Mama Nasra jana kachaniwa nyavu ya dirisha lake akaibiwa simu yake, itakuwa ni huyuhuyu mpuzi” Kijana mmoja akatokea akiwa anasema, akanifuata na kuanza kunipiga makofi na ngumi za kichwa.

“Mimi sio mwizi jamani, tafadhalini msinipige, mimi sio mwizi” Nikawa napiga makelele nikilia. Yule kijana hakunisikiliza, aliendelea kunipiga, nikaona nikiendelea kubaki pale nitakufa, nikamsukuma yule kijana akapepesuka na kabla hajaanguka nikampiga na ile ndoo kisha nikatoka nduki nikikimbia kama kiberenge, yule kijana akisaidiwa na yule mama wakawa wameniungia huku wakipiga kelele za mwizi, nikazidisha mwendo lakini kwenye vile vichochoro zile sauti ya mwizi zikawa zinawaleta watu kunizuia wakinipiga makofi wengine vibao, mbao na wengine wakinirushia, sikuanguka mpaka nilipopigwa jiwe la mgongoni lililokuwa limenipata vyema, nikiwa nimeanguka pale chini wale watu waliokuwa wakinimbikiza walinifikia, hapakuwa mbali na barabara kuu ya morogoro road, walinipiga wakanipiga nikapigika mpaka nikachakaa.

“ Mimi sio mwizi! Sio mwizi mimi jamani! Msiniue tafadhali!” Nilikuwa nasema damu zikiwa tayari zimeanza kunitoka puani na mdomoni, nguvu za mwili zilikuwa zimeniisha, hata wangeniacha wala nisingeweza kuinuka. Hapo kichwa nikaanza kukiona kizito, macho yakiwa yanaona ukungu ukungu, kisha kumbukumbu za harakaharaka zikaanza kupita katika kichwa change nikiwa nasikia kwa mbali; tumchomeni! Achomwe moto huyu.

Nikamuona Alice akiwa yupo na Gitaa akiwa kavaa nguo nyeupe pee kama malaika, nguo zile nyeupe zilikuwa zinapepea kama zinapeperushwa na upepo akiwa juu ya kilima, akiwa anapiga Gitaa lake, ulikuwa ni wimbo aliozoea kuniimbia tukiwa wawili kule kijijini; Alice akazichanganya nyuzi za gitaa kisha akaanza kuimba;

“ Pamoja na wewe! Niwapo na wewe

Usiniache mwenyewe, usiende mwenyewe,

Njoo unichukue, kwako nikakae,

Mapenzi unimiminie, wala usiyabakize,

Nipe honey nijilie, kwa huba niyameze”

Wimbo huo ulikatisha baada ya kuhisi kitu chenye ncha kali kikipenya katika mguu wangu, ilikuwa bisibisi niliyokuwa nimechomwa, akili yangu ikarejea eneo lile nikawaona watu tayari wakiwa wamebeba tairi, wakinitazama kwa macho ya chuki; mwanaume mmoja akaja akiwa na lile tairi na kunivisha kwenye shingo, nilikuwa nimelewa kwa kipigo, nafikiri walikuwa wakisubiri petrol iliyokuwa imeagizwa ili wanilipue. “ Gibson wakati wako umefika, Sali sala zako za mwisho, muda mfupi ujao roho yako itakuwa angani ikiuacha mwili duniani ukiwa unateketea kwa moto mpaka majivu” Akili yangu ili ikaniambia, nikiwa napumua kwa taabu damu zikitoka puani mdomoni.

Nikamkumbuka mama yangu niliyemuacha kijijini, hapo machozi yakawa yananitoka nikawa ninalia pasipo kutoa sauti huku kwikwi ikinitingisha;

“ Maa ma! Maaama! Mimi sio mwizi” Nikasema kwa taabu sauti ikiwa inakwama kwama kisha nikasema kimoyomoyo “Mimi ni mwanamuziki” hapo nikayafumbua macho yangu kwa taabu nikiwaona wale watu wakiwa wamenizunguka, wale ambao hawajaridhika bado waliendelea kunirushia mawe kwa hasira. Hawakuniona nikiiba, hawanijui, ndio kwanza leo ni siku ya kwanza wananiona, lakini wananiita mwizi, mwizi wa nini, nimewaibia nini hawa watu, kwa nini wanaroho mbaya kiasi hiki. Labda ni kweli waliwahi kuibiwa vitu vya thamani, wakaharibiwa mali zao, lakini sio mimi niliyefanya hayo. Au Gibson ninafanana na wezi” Nilikuwa nikiwaza, hapo nikamuona kijana asiyefikisha miaka ishirini aliyenyoa kiduku akiwa anakuja mikononi amebeba kidumu cha lita tano kilichojaa mafuta ya taa. Nikayasikia mapigo yangu ya moyo yakifufuka na kupiga kwa nguvu sana, nilijawa na hofu ya kifo, muda wangu wa kuishi duniani ulikuwa umekwisha, sasa zilisalia sekunde chache tuu.

Matumaini ya kuishi yalitoweka, nikakata tamaa, wala sikutegemea tena muujiza wowote muda ule. Ilikuwa asubuhi mbaya katika maisha yangu, asubuhi ambayo kifo kilikuwa kinadai roho yangu. Yule kijana aliyebeba kidumu cha mafuta ya taa akanisogelea, mimi ningali namtazama kwa macho ya huruma, nikimsihi pasipo kutoa sauti asinichome, anionee huruma, mimi sio mwizi. Yule kijana akawa ananitazama kwa macho yake makavu yenye chuki, akakinyanyua kile kidumu mpaka kwenye kifua chake huku bado akinitazama, nikakata tamaa ya mwisho kabisa ambayo ilikuwa akiba yangu nilipouona mkono wa yule kijana ukikizungusha kile kifuniko cha kidumu kilichobeba mafuta ya taa, niliona mikono ikizungusha kifuniko kana kwamba inazungusha macho yangu. Akanitupia kile kifuniko kichwani, kisha akaanza kunimwagia yale mafuta ya taa, nilihangaika, silisumbuka kwa maumivu niliyokuwa nayapata, yale mafuta yaligusa majeraha waliyokuwa wamenipiga wale watu, sasa nilikuwa mfu niliyehai nikisubiri mtoa roho apulize kipenga cha kupokelewa kuzimu.

Yule kijana akatoa Kiberiti, wakati huu watu walikuwa kimya wakitoa macho kwa kile kilichokuwa kinaenda kutokea, hakuna aliyekuwa akinirushia tena mawe, wote walitulia na mtu mmoja tuu ndiye aliyekuwa akiendesha ibada hiyo haramu kwa mtu asiye na hatia, yule kijana kabla hajatoa njiti, sauti kali kutoka nyuma yake ikasikika ikisema;

“ Achaaaa! Usimchome! Sio mwizi huyo!” Yule mtu aliyesema hivyo akamvamia yule kijana aliyetaka kunichoma na kumpokonya kiberiti, kisha wakaparangana, Askari akatokea, watu wakatawanyika kila mmoja akikimbia kutotaka kutoa ushahidi. Mimi nilikuwa pale chini nikiwa nimechoka macho nikiwa nimeyafumba, yule mwanaume akaja kulitoa lile tairi kisha akaniita;

“Oya! Mwanangu! Amka! Amka Mshikaji wangu” Ilikuwa ni sauti niliyoisikia ikiniita kama inatoka ndotoni. Ilikuwa kama sauti ninayoifahamu lakini sikuwa naikumbuka vizuri. Nikayafumbua macho yangu, nilishtushwa nilipokutana na uso wa yule mwanaume chizi niliyeonana naye usiku pale Manzese Darajani. Nikauona uso wa yule mwanaume ukitabasamu, mdomo ukiwa umejificha ndani ya ndevu nyingi sana zenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na kijivu. Lile tabasamu nikaliona likiyeyuka katika macho yangu polepole likifunikwa na ukungu, na hapo nikaona giza kuu. Nikapoteza fahamu.

***********************

Nikiwa nimelala nyumbani, nilimsikia mama yangu akiniaga kuwa anatangulia shamba, akaniambia nisichelewe kumpelekea mbegu kwani ulikuwa ni msimu wa kupanda mahindi. Mama akatoka akaniacha nimelala nikiwa namsikia mtu akiwa anazungumza kwenye Redio iliyokuwa pale chumbani kwangu. Palikuwa na giza la alfajiri yapata saa kumi namoja hivi, nikasikia adhana ya waislam, baada ya adhana kuishi nikamsikia yule mtu kwenye Redio akizungumza;

“Shindano la Tanzania Got Talent linatarajiwa kuanza wiki mbili zijazo, ambalo washiriki wote walioomba watachuana mpaka mshindi atakapopatikana, washiriki wa shindano hilo majina yao yamebandikwa katika ubao wa matangazo katika jengo la TGT, pia majina yamebandikwa katika tovuti ya Tanzania Got Talent, kesho Gazeti la Burudani litachapisha majina hayo. Watahiniwa wote mlioomba mupitie sehemu zilizotajwa hapo kuona kama mmechaguliwa. Yule mtu kwenye Redio akaacha kuzungumza lakini kwa mbali nikasikia mtu akibisha hodi kwenye mlango,

“Hodi! Hodi! Hodi!” Ilikuwa sauti ya kike. Nikawa naiitikia, alafu nikamwambia afungue tuu mlango, Nilishtushwa na yule niliyemuona mlangoni, alikuwa ni yule mwanamke niliyemuona siku ile ya usahili wa watahiniwa wa shindano wa TGT, hapo nikashtuka , fahamu zikanirejea, nilijikuta nipo kitandani nikiwa nimefungwa Ndipu mkononi, kilikuwa chumba ambacho nikajua ilikuwa wodi ya wagonjwa, vilikuwepo vitanda vitatu, kimoja kikiwa hakina mtu, viwili vikiwa na watu ambao ni mimi na mgonjwa mwingine.

Punde akaingia Muuguzi aliyevalia nguo nyeupe za kazi akiwa kaongozana na Dada mmoja hivi, Muuguzi alivyoniona akatabasamu, kisha akaweka vifaa Fulani ambavyo sikuwa nimeviangalia vizuri. Yule Dada aliyekuja naye pia akatabasamu.

“ Unaendeleaje Kijana?” Muuguzi alinisalimia. Nikamjibu. Kisha nikamuuliza;

“Umepita muda gani?”

“ Siku nne tuu Kijana” Akanijibu huku akimpigia simu mtu Fulani. Kisha akaongeza;

“Ulikuja ukiwa na hali mbaya sana, ulikuwa haujitambui, hatukutegemea kama ungeamka, kwa kweli unabahati sana”

Nikawa namtazama nikijaribu kukumbuka mara ya mwisho nini kilitokea. Nikakumbuka Kuwa mara ya mwisho nilikuwa kwenye hatihati ya kuuawa kwa kuchomwa moto na wale watu wenye hasira kali zakijinga kule Manzese.

“ Yule Mwanaume chizi Yuko wapi?” Nikamuuliza Muuguzi baada ya kumkumbuka Yule chizi aliyenisaidia nisichomwe moto.

“ Hilo sio la muhimu Kaka, subiri kwanza upone” Muuguzi alijibu akigeuka nyuma ulipomlango baada ya kusikia ukifunguliwa.

“ Nilikuwa nipo njiani nakuja ndio maana sijapokea simu yako” Daktari wa kike aliyevalia koti la kidaktari(Clinical Jacket).

“ Oooh! Mungu Mkubwa kumbe ameamka! Unajisikiaje Kaka mzuri” Daktari akasema kwa sauti ya ukarimu huku akiitoa Stethoscope kwenye shingo yake na kuanza kupima mapigo yangu ya moyo, kisha akapima na presha.

“Nahisi maumivu tuu ya mgongo” Nikamjibu akiendelea kunipima.

“ Vizuri utakuwa tuu sawa, mumpe chakula alafu baadaye nitakuja kumpa dawa” Daktari akasema kisha akatoka akituacha pale wodini.

“ Habari yako Kaka. Nimekuletea chakula” Yule dada aliyekuja na muuguzi akanisabahi.

“ Salama tuu dada yangu, ahsante kwa kuniletea chakula” Nikajibu.

“ Mimi ngoja niwaache, nikahudumie wagonjwa wengine, nitarudi baada ya nusu saa” Muuguzi alituaga akaondoka. Pale wodini tulikuwa watatu, mimi, yule dada aliyekuja na muuguzi, na mgonjwa mwingine aliyekuwa kalala kwenye ktitanda cha mwisho, alikuwa kalala kama mtu aliyekufa.

“ Kula polepole, enhee! Kula kaka mzuri! Vizuri” Yule dada alikuwa akinilisha kwa kunibembeleza kama mtoto, nilifarijika sana. Lakini nikajiuliza dada yule alikuwa ni nani, mbona ananihudumia wakati mimi sio ndugu yake, nikataka kumuuliza lakini kabla sijafanya hivyo akasema;

“ Ninaitwa Zuleikha! Huna haja ya kujiuliza mimi ni nani?” Nikashangaa sana, alijuaje kuwa nataka kumuuliza jina lake. Nikatabasamu, alafu nikamtazama akiwa amenishikia kijiko karibu na mdomo akinitazama usoni, naye akatabsamu. Alikuwa na sura nyeupe yenye nyusi nyinyingi hivi, kama sio ugonjwa wangu basi nilimfananisha kama mtu mwenye asili ya kisomali. Alikuwa mweupe kama chotara, ingawaje sikuwa na uhakika kwani alikuwa kava ushungi kichwani.

“Kwa nini uko hapa?” Nikamuuliza. Yeye akanijibu.

“ Kwa sababu unaumwa, usingekuwa unaumwa mimi nisingekuwa hapa”

Nikashangaa sana. Kisha nikasema;

“Yule mwanaume chizi yupo wapi, yeye ndiye aliyekuambia nipo hapa?”

“ Kula kwanza Kaka, acha maswali mengi, umesikia mpendwa” Yule Dada akasema kwa sauti nyororo iliyokuwa ikipenya katika vizio vya masikio yangu mpaka ndani kabisa ya moyo. Akanilisha kijiko kingine, nikawa natafuna ukimya ukiwa umetamalaki kwa kitambo, alikuwa akinitazama bandeji zangu nilizokuwa nimefungwa kichwani, alinitazama kwa macho ya huruma sana, nikawa nawaza, huyu mwananmke ni nani, kwa kweli nilikuwa na shauku ya kumjua vizuri, jina lake moja halikuniridhisha, nilitaka kujua anaishi wapi, ameolewa, je anawatoto, na kwa nini anatumia muda wake na mimi pale.

“ Kwa nini unanihudumia wakati hunijui wala mimi sikujui?” Nikamuuliza.

“ Usijali, kula kwanza nitakuambia kila kitu” Akanijibu akiendelea kunipa chakula. Nikala mpaka nilipohisi kutosheka, akatabasamu na kunipongeza kwa kula.

“ Wewe jina lako unaitwa nani?” Akaniuliza.

“ Ninaitwa Gibson, nawe unaitwa nani? Nikamtupia swali.

“ Hahah! Gibson si nilikuambia naitwa Zuleikha, mara moja hii umesahau”

“ Aaah! Kweli ulinambia unaitwa Zuleikha, nisamehe ndugu yangu” Nikasema.

“Usijali, bado unaumwa sio kosa lako” Akasema alafu akacheka name nikajikuta nikicheka lakini misuli ya paji la uso ikawa inauma, nikakunja sura kutokana na maumivu.

“OOhhh! Sorry, tafadhali pumzika kwanza, sawa!” Zuleikha alisema akinilaza polepole kwenye mto wa kitanda. Dakatari akaja akanipa dawa nikanywa. Zuleikha akaniaga akaondoka.Nilitamani kumzuia ili anijibu maswali yangu lakini akili yangu ilinionya.

Nikiwa mpweke kitandani nikiwa nimebaki na yule mgonjwa ambaye tangu nizinduke mpaka muda huu alikuwa hajaamka nikamkumbuka Yule mwanaume chizi aliyeokoa maisha yangu, nilikumbuka jinsi nilivyomzodoa ile siku usiku kwa majibu yangu ya shombo, kwa kweli nilijisikia vibaya, nilijilaumu kwa kitendo nilichomfanyia yule mwanaume chizi, kumbe mtu anaweza kuwa masikini na fukara, na pengine akawa kama kichaa lakini akawa na roho nzuri kuliko hata matajiri na watu wenye akili. Yule chizi ni kweli alikuwa mchafu anayenuka lakini tabia yake ilikuwa njema sana.

Nikakumbuka tabasamu lake siku ya mwisho alivyonikumbatia baada ya kunitoa lile tairi, lilikuwa tabasamu la kichaa lililobebea wokovu wa maisha yangu, tabasamu imara ambalo liliniokoa na mikono ya kaburi.

Usingizi ulinipitia, nikalala nikiziacha shida za dunia zikiwa macho zikinitazama kwa wivu mkali. Shida za dunia hazikutaka kunipumzisha, hazikupenda kuniona ninalala usingizi mtamu, zilitaka muda wote zinione nikisulubika na kulia machozi.

Siku nyingine ilifika, leo Zuleikha aliingia akiwa kava ushungi na baluzi ndefu iliyopasuka upande huu na upande huu, pamoja na suruali nyeusi inayovutika, alikuwa kapendeza sana. Marashi yake yaliongeza sehemu ya ahueni yangu, yalikuwa marashi yanayonukia harufu nzuri sana. Zuleikha alinichangamkia, siku hii mazoea yakiwa yameongezeka kidogo tofauti na jana. Alinipa chakula, nikala nikashiba. Tukapiga stori lakini kila nilipokuwa naingizia mada za kutaka kumjua alikuwa akichomeka mada zingine. Siku ile nayo ikaisha. Nikaachwa mwenyuewe.

Mgonjwa yule bado alikuwa kalala tangu jana nilipozinuduka, nikawa najiuliza huyu atakuwa anasumbuliwa na nini kwani. Nikamtazama nikiwa nimeegema kwenye mto, nikamuona alikuwa ni mwanaume wa makamo mwenye upara, alikuwa kayafumba macho yake huku yakitoa majimaji kama machozi. Punde Muuguzi aliingia akiwa amebeba dawa za jioni, akaniwekea pale, akazibangua kisha akanipa nikameza. Nikamuona muuguzi akimtazama yule mgonjwa mwingine, muuguzi akapiga hatua kumuendea yule mgonjwa. Hapo nikawa makini kutazama anaenda kufanya nini, nikamuona akichukua kitambaa na kumfuta yale majimaji yaliyokuwa yanamtoka yule mgonjwa.

“Hii siku ya sita hatingishiki, hafumbui macho, wala haongei” Muuguzi aliongea akiwa anatoka, kimoyomoyo nikasema siku sita duuuh! Giza likaingia usiku ukatamalaki, nikalala. Usiku wa manane nilishtushwa na kelele za mtu anayekohoa, alikuwa akikohoa mno. Nikaamka na kuketi, nikamuona yule mgonjwa aliyekuwa amezimia kwa siku sita akiwa anakohoa na kutoa mdomoni kitu kama mapovu. Nikawa napiga makelele kwa hofu nikiita Dokta! Dokta! Muuguzi! Njooni haraka huku! Yule mtu alizidisha kukohoa huku mapovu yakimtoka, kitambo kidogo nikamuona akilegea na akawa anapunguza kukohoa polepole, mwishowe akawa kimya kama mwanzo. Nikawa nimeamka nimekaa nikiwa namkodolea macho kwa hofu ya kujua amekufa, punde Muuguzi wa zamu aliingia akiwa mbiombio akamfuata, dakatri naye akafuatia, wakampima, kisha daktari akamuambia muuguzi wamuhamishe wodi upesi, lakini kabla hawajafanya lolote yule mtu akaanza kukoho tena kwa nguvu, nilishtuka kidogo nikimbie. Nikama nilishuhudia maiti ikifufuka.

ITAENDELEA

Simulizi ya Kusisimua ya kijasusi 'MLIO WA RISASI HARUSINI" Inapatikana; Softcopy Tsh 3,000 Kitabu Tsh 10,000/= Itumwe na pesa ya kutolea.

0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
 
Shukrani Sana mkuu bado nakufuatulia nikiwa viunga vya Lubumbashi Congo mkuu one love
 
KABURI LA MWANAMUZIKI ( Sehemu ya 06)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

Sehemu ya 06

ILIPOISHIA

Nikaamka na kuketi, nikamuona yule mgonjwa aliyekuwa amezimia kwa siku sita akiwa anakohoa na kutoa mdomoni kitu kama mapovu. Nikawa napiga makelele kwa hofu nikiita Dokta! Dokta! Muuguzi! Njooni haraka huku! Yule mtu alizidisha kukohoa huku mapovu yakimtoka, kitambo kidogo nikamuona akilegea na akawa anapunguza kukohoa polepole, mwishowe akawa kimya kama mwanzo. Nikawa nimeamka nimekaa nikiwa namkodolea macho kwa hofu ya kujua amekufa, punde Muuguzi wa zamu aliingia akiwa mbiombio akamfuata, dakatri naye akafuatia, wakampima, kisha daktari akamuambia muuguzi wamuhamishe wodi upesi, lakini kabla hawajafanya lolote yule mtu akaanza kukoho tena kwa nguvu, nilishtuka kidogo nikimbie. Nikama nilishuhudia maiti ikifufuka.


ENDELEA
Akawa anapumua kwa kukoroma, hali yake ilizidi kuwa mbaya, nilihisi labda vile ndio alikuwa akiiaga dunia. Wakamuweka mpira puani wa kupumulia, hapo akapoa polepole kisha akatulia mpira wa kupumulia ukiwa puani mwake, alikuwa anashindwa kupumua, kama isingekuwa vifaa vya kisasa vilivyokuwa mule wodini basi mgonjwa yule angekuwa ameshakufa.

**************************

Siku saba zilipita tangu nipate fahamu, hali yangu ilikuwa imeimarika, niliweza kutembea na kuzunguka zunguka mule wodini, Zuleikha alikuwa akija kila ifikapo muda wa kuona wagonjwa. Nilikuwa nimeshazoeana naye, siku ile Zuleikha akaja akiwa kapendeza sana kuliko siku zingine, alikuwa anafuraha sana.

“ Gibson, hali yako sasa hivi imetengemaa, unanuru na nguvu kabisa kama mtu mwenye afya, nafikiri hivi karibuni utaruhusiwa kutoka hapa hospitalini” Zuleikha alisema akiwa ananitazama.

“ Ni kweli, ninajisikia nina nguvu, yale maumivu ya kichwani, na mgongoni sasa hivi siyasikii, labda mguu huu kidogo nikitembea ndio nasikia kama unashtuka, unamaumivu kidogo” Nikasema.

“Usijali utakuwa sawa tuu” Zuleikha akasema, wote tukatazama mlangoni ambapo tulimuona Daktari akiingia na watu wawili hivi, wale watu wakatusalimia alafu wakaenda kwa yule mgonjwa niliyekuwa naye wodi moja, Yule mgonjwa Alikuwa amepata walau nafuu, alikuwa akiyafumbua macho yake na kuyageuza huku na huku, pia alikuwa anauwezo wa kujigeuza tofutti na siku zile nilizomkuta akiwa hajitambui. Daktari akawaruhusu wale watu wawili wazungumze na yule mgonjwa, sikujua wanauhusiano na yule mgonjwa. Hata hivyo haikunihusu.

“ Habari Gibson!” Daktari akanisalimu.

“ Salama kabisa Dokta! Najihisi ahueni” Nikajibu.

“ Pole na hongera sana, kama hali itaendelea hivi kesho tutakuruhusu, naamini hali yako itazidi kuimarika” Daktaria alisema akinitazama nami nikimuangalia uso wake uliokuwa nyuma ya miwani yenye kioo kinachoonyesha macho yake. Akaongeza;

“ Umepata nafuu mapema kutokana na kuwa wewe sio mvivu wa kula, chakula ni dawa nzuri sana ambayo humfanya mgonjwa kupona mapema, ukizingatia kula chakula kizuri chenye mlo kamili na kunywa maji mengi, unapunguza makali ya ugonjwa,. Pia unajitengenezea mazingira ya kupona haraka”

Nilimtazama Daktari akiwa anazungumza huku nikiwa natabasamu, nilikumbuka maneno ya mama yangu aliyowahi kuniambia; Chakula ni dawa. Pia mama yangu alikuwa akiupenda msemo usemao; Mwili haujengwi na matofali kama nyumba, bali unajengwa kwa chakula. Mama yangu hakuwa na elimu kubwa lakini alikuwa na maarifa ya msingi ambayo kwa sehemu Fulani iliweza kunisaidia. Muda wa kuona wagonjwa uliisha, Zuleikha akaniaga, akaondoka na kuniacha mule wodini, nikabaki na yule mgonjwa mtu mzima mwenye upaa ambaye alikuwa akinitazama bila ya kusema chochote. Nilitamani nimuulize lakini akili yangu ilinionya, mwisho tukawa tunatazamana kama majogoo, yeye akiwa kalala kitanda chake, name nikiwa nimelala katika changu. Usingizi ukanipitia wala sikujua ulinichukua saa ngapi.

Nikiwa nimelala usiku nikahisi kitu kikinikaba shingoni, nikawa najitahidi kujitetea lakini nikawa siwezi, mwili wangu ulikuwa hauna nguvu, nikawa najaribu kupiga kelele lakini sauti yangu ikawa haitoki, nikijaribu kufumbua macho siwezi, nikahisi huenda ndio ninakufa, nikajitahidi lakini sikufua dafu, nikawa napiga kelele kimoyomoyo “Mamaa! Mamaa! Mamaa! Hapo kile kitu kilichokuwa kimenikaba shingoni kikaachia; nikaamka nikiwa napumua kwa pupa kama mtu niliyekosa pumzi kwa kuzama ndani ya maji. Sijui ilikuwa ni jinamizi au nini, lakini niliwahi kumsikia mwalimu wa biolojia akisema kuwa mtu akishiba sana chakula cha usiku kuna uwezekano chakula kikapanda usiku akiwa amelala na kumfanya ashindwe kupumua, wengine pia husema hali hiyo husababishwa na utumbo kujikunja, basi kila mtu kulingana na uelewa wake, mimi hayo mambo sikuwa na utaalamu nayo. Mimi nilikuwa mtaalamu wa muziki, mwanamuziki mwenye kipaji cha juu kabisa.

Nikiwa nimejipumzisha pale kitandani, bado pakiwa usiku,taa za pale wodini zikiendelea kukimulika chumba chetu, macho yangu yaliona jambo la kustaajabisha, niliona kitasa cha mlango wa mule wodini kikicheza cheza kama mtu akikichezea. Nikawa nakiangalia nikitarajia mlango ufunguliwe. Bado nilikuwa nimejilaza kitandani, nikaona kitasa kikicheza zaidi hali iliyonifanya niingiwe na wasiwasi kutaka kujua ni nani anafanya vile. Punde mlango ukafunguliwa, ukafunguka robo yake, hapo nikawa macho zaidi kumuona atakayeingia, lakini hakuingia yeyote, chakushangaza nikaona kitasa kikicheza cheza tena, nikayasikia mapigo yangu yakipiga kwa nguvu kwa hofu, mwili wangu ukasisimuka; ule mlango ukarudi polepole mpaka ulipojifunga kama awali. Hii maana yake nini. Nikawa najiuliza kimoyo moyo.

Nikageuka kumtazama yule mgonjwa mwenzangu tuliyekuwa wote mule wodini, nikamuona akiwa akiwa amelala Fofofo. Nikakumbuka kile kitu kikiwa kinanikaba kooni, alafu nikahusisha na kitasa cha mlango kucheza, alafu mlango kufunguliwa na kufungwa. Nikahisi kuna jambo la hatari linataka kutokea, sikujua ni jambo gani lakini hisia zangu zilinitaka niamini kuwa litakuwa jambo baya sana. Ghafla nikiwa nawaza mlango ukafunguka, akajitokeza mwanaume mrefu aliyevalia koti jeupe la kidaktari, usoni akiwa kava barakoa iliyoficha uso wake, ikiwa imetobolewa sehemu ya kwenye macho tuu. Moyo ukapiga kwa kite! Miguu yangu ikawa inatetemeka huku nikiziona nguvu zangu zikiyeyuka, Yule mwanaume mrefu aliyeingia mikono yake alikuwa amevaa Gloves za kitambaa yenye rangi nyeusi, mkono mmoja akiwa kashika bastola, na hiyo ndio iliongeza woga wangu. Nikafumba macho yangu upesi kabla ya yeye kuniangalia, nikasikia akiurudishia ule mlango, alafu nikasikia akipiga hatua twaa! Twaa! Kisha nikawa sizisikii tena, jambo ambalo liliongeza wasiwasi moyoni wangu uliochanganyika na shauku ya kutaka kufumbua macho nimuangalie anafanya nini, nikataka kufumbua macho lakini ile nakaribia kufanya hivyo, nikasikia hatua nyingine Twaa! Hapo nikaghairi huku nikijiambia; Gibson tulia, acha kiherehere, macho yako yatakuponza.

Nilijua shetani siku zote hapendi akifanya mambo yake mabaya pawe na shahidi, watu wabaya hupenda kujionyesha wakifanya mema mbele za watu, lakini wakifanya mabaya hawapendi wajulikane wala hawapendi awepo shahidi. Ikiwa utakuwa shahidi wa mtu mbaya basi usalama wako upo hatarini. Nikamsikia yule mtu akitembea kunifuata nilipolala, hapo mapigo yangu yakaongeza kasi zaidi huku pumzi yangu ikitaka kunishinda kuidhibiti, ilinipasa kuidhibiti kwa ajili ya usalama wa roho yangu.

Yule Mwanaume akanikaribia, akawa amesimama pembeni ya kitanda changu, nikajifanya nimelala fofofo, nikachomoza kasauti kamkoromo kwa mbali kumshawishi aone niko mbali na ulimwengu. Yule mtu akaniweka mkono wake juu ya uso wangu akiupunga mkono wake kwenye uso wangu ili aone kama macho yangu yatacheza ajue nipo macho, nami nikazikaza hisia zangu nikiwa nimeiweka mboni ya macho yangu giza kuidanganya hakuna chochote juu ya uso wangu. Yule mwanaume akaridhishwa na hali aliyonikuta nayo akaamini nilikuwa nimelala sijitambui. Akaondoka nikawa namsikia akitembea kuelekea kwenye kitanda cha yule mgonjwa mwengine. Nikayafumbua macho yangu polepole, nikamuona akiwa amenipa mgongo akikaribia kitanda cha yule mgonjwa, akasimama; alafu akawa anamtazama yule mgonjwa kama anayemdadisi, alimtazama kwa sekunde kadhaa kisha akainyanyua bastola yake na kumuwekea kichwani yule mgonjwa. Kidogo nipige yowe! Niliogopa mno, kwa nini anataka kumpiga, mgonjwa wa watu anayapigania maisha yake yeye anakuja kuyakatilia mbali. Nikamuona akiwa anaishusha ile bastola kutoka kichwani alafu akaiweka mdomoni mwa yule mgonjwa, akaitambaza mpaka kilipo kifua alafu akaishusha zaidi mpaka tumboni, kila alivyokuwa akiitambaza ile bastola mwilini mwa yule mgonjwa aliniongezea presha. Sijui akahisi jambo gani, nikamuona akiinyanyua ile bastola alafu kwa upesi akanielekezea mimi, hapo kwa upesi sana nikayafumba macho yangu kabla macho yake hayajatua kwenye macho yangu, lilikuwa ni tukio lililonifanya nihisi roho inatoka. Niliogopa mno. Yule mwanaume alipoona nimelala akageuza macho yake kwa yule mgonjwa, nikamsikia akimuamsha yule mgonjwa;

“ Kibadeni! Mr. Kibadeni! Amka! Amka wee mpuuzi”

“ Amka! Sitakuua ukiwa ukiwa umelala! Nataka nikuue ukinitazama! Amka Basi!” Yule mwanaume nilimsikia akisema, hapo nikayafumbua tena macho yangu. Nikamuona Yule mgonjwa ambaye sasa nilimtambua kwa jina la Mr. Kibadeni baada ya Yule mwanaume kulitaja jina lake. Mr. Kibadeni akayafumbua macho yake, alishtushwa baada ya kumuona yule mwanaume aliyeuficha uso wake na barakoa nyeusi iliyotobolewa matundu mawili ili macho yake yaweze kuona.

“ Hahahaa! Umeshtuka! Ulidhani ukiwa na roho ya paka ndio utatukimbia, raundi hii hautatoka salama katika mikono yangu, ninaenda kukuua muda mfupi ujao” Yule mwanaume alikuwa akiongea kwa kejeli na jeuri akimtisha Mr. Kibadeni. Nikamuona Kibadeni akiwa anamtolea tuu macho akiwa bado amehamaki, nikawa najiuliza; kwani kibadeni kafanya nini,na yule mwanaume ni nani. Lakini hakuna aliyekuwepo kwa ajili ya kujibu maswali yangu.

“ Tulikuambia ukawa mkaidi, ukajifanya kiherehere! Haya ndio matokeo ya watu wakaidi kama wewe. Unaacha familia yako kwa ajili ya mambo ya kipuuzi! Ulifikiri utasifiwa! Hahahah!” Yule alicheka kwa sauti, nilishtuka kweli. Kicheko chake kilikuwa kicheko cha mauti, wala hakikufanana na kicheko cha furaha

“ Ila Mzee unaroho ngumu sana, tulijua umekufa kwa yale yote tuliyokufanyia, ila leo hautoki, nitakuua, ni mpaka niikabidhi roho yako kwenye mamlaka husika za kuzimu, maana ile siku tulikutelekeza tuu njiani ukatoroka! Hahaha! Leo hautoroki ng’oo” Yule mwanaume akasema alafu akatazama kule nilipo, nikafumba macho yangu upesi. Nikamsikia akiendelea kusema;

“ Nilitaka kukuua na hii chuma ukiwa umelala, nikaona utaniona nilikuogopa alafu utakufa kwa amani pasipo maumivu, ufe bila maumivu! Hilo kwangu sikutaka litokee, huwa nampenda mtu akifa mikononi mwangu afe kwa uchungu, roho yake niitoe polepole kwa maumivu makali, na ndio maana nikakuamsha ili unisaidia ndugu Kibadeni” Nikamuona Mr. Kibadeni akikunja uso wake kama mtu anayetaka kusema jambo Fulani, nikayaona machozi yakimlenga lenga, masikini Kibadeni alikuwa anatia huruma sana.

“Nimekuja na zawadi yako nzuri. Bila shaka utaipenda! Mr. Kibadeni, zungumza basi” Yule mwanaume alisema, kisha akaingiza mkono kwenye mfuko wa lile koti la kidaktari alilokuwa amelivaa.Nikamuona Mr. Kibadeni akiyagueza macho yake kuangalia mikono ya yule mwanaume, alitaka kuona zawadi aliyokuwa ameletewa na yule mwanaume. Sikutarajia kama ingekuwa zawadi ya maana, anfikiri hata Kibadeni alifikiri kama mimi. Wote tukawa tunautazama mkono wa yule mwanaume ukitoka mfukoni. Hisia za wasiwasi ziliongezeka, yule mwanaume akatoa sindano na kichupa cheusi. Kisha akamuonyesha Mr. Kibadeni huku akicheka.

“ Hii ni zawadi yangu niliyokuchagulia kabla haujafa, imetoka mbali kwa ajili yako Mr. Kibadeni, pia ni zawadi yenye gharama kubwa Mzee wangu. Hautanishukuru hata kwa hili” Yule mwanaume akawa anaongea huku akiinyonya dawa na ile sindano. Alipomaliza, akaiinua ile sindano juu iliyojaa dawa. Kisha akamtazama Mr. Kibadeni,

“ Lakini nitakulaumu sana Kibadeni, NO! sio makosa yako, aliyekuleta ndiye mwenye makosa, hivi kweli hapa ndio kakuficha, kama ningekuwa huyo aliyekuleta basi ningekupeleka nje ya nchi, nikakufichie huko, upate matibabu mpaka utakapopona” Yule mwanaume alisema akijaribu kutafakari. Niliuona uso wa Mr. Kibadeni ukiwa na hofu kubwa mno, nilitaka niende kumsaidia lakini kila nilipoutazama mwili wa yule mwanaume, roho yangu ilisita. Lilikuwa pande la mtu ambalo kulikabili ingenipaswa niwe na ujuzi wa mapigano.

“ Nafikiri tumepiga stori za kutosha Mr. Kibadeni, kama unalolote lakusema huu ndio muda wako, dakika chache zijazo hii dawa itakuwa ikipita katika mishipa yako ya damu kwa maumivu makali mpaka itakapoifyonza roho yako yote. Unachakusema?” Yule mwanaume akalisema. Lakini Mr. Kibadeni hakujibu lolote, aliishia kutoa machozi.

Yule mwanaume akaiunganisha ile sindano na lile Dripu alilokuwa ametunfikiwa Mr. Kibadeni, kisha akaichanganya ile sumu na maji ya Dripu, baada ya hapo akaliweka Dripu vizuri, kisha akaangalia saa yake ya mkononi, akatabasamu, akasema;

“ Huu ni muda mzuri kabisa, Saa tisa za usiku, saa kumi kamili utaingia kuzimu, utakuwa umewahi sana Mr. Kibadeni” Nilijikuta nikiwa na hasira sana baada ya yule mwanaume kuongea hivyo. Alikuwa ni muuaji mwenye barakoa, mwenye sauti nzito kiasi, macho yake yalikuwa makali licha ya kuwa yamezingirwa na barakoa, lakini pamoja na hasira zangu wala sikuthubutu kumtetea Kibadeni. Nilikuwa nashuhudia kifo cha kibadeni kwa macho yangu.

Yule mwanaume akatoa simu katika mfuko wa suruali, akabonyeza bonyeza kisha ikawa inaita, baadaye akaiweka sikioni;

“Hallo Mkuu! Kazi imekwisha, haikuwa ngumu sana, hapa ndio nimeshamalizana naye, eeh! Hakuwa pekeake, Huyu mwingine amelala tuu” yule mwanaume akaongea na simu kisha akageuka kunitazama, nikafumba macho yangu upesi kabla hajaniona, nilijua aliyekuwa anazungumziwa ni mimi. Mapigo yangu ya moyo yalianza tena kupiga kwa nguvu. Ilikuwa zamu yangu sasa.

“ Huyu bado kalala Mkuu! Ndio nina uhakika Mkuu! Haina shida Mkuu, au unataka naye tumuue Mkuu? Si ndio hapo Boss, huyu hajatufanya chochote, labda angeniona ndio ningemuua. Sawa Mkuu, mimi ndio natoka hivyo, sawa” Yule mwanaume akamaliza kuongea na simu, mimi bado nilikuwa nimefumba macho yangu nikimsikiliza, sikutaka kuyafumbua macho yangu, niliogopa kufanya mistake moja ambaye ingegharimu macho yangu. Pakawa kimya kwa kitambo, nikawa najiuliza yule mwanaume atakuwa anafanya nini, huku nikijionya nisiyafumbue macho yangu. Nilikumbuka maneno ya yule mwanaume aliyomwambia Kibadeni kuwa kiherehere chake ndicho kimemponza, nikajiambia nitulize kiherehere changu cha macho, umbea usijeukaniponza.

“ Kwa kheri Mr. Kibadeni” Yule Mwanaume alisema, nikasikia akipiga hatua kuufuata mlango wa kile chumba, mlango ukafunguliwa kisha ukafungwa, nikafumbua macho upesi, alikuwa katoka, nikamtazama Mr. Kibadeni ambaye alikuwa bado ameuangalia mlango, hapo akageuza macho yake mpaka tulipotazamana, moyo wangu ukapiga kwa kite, niliogopa sana nilipouona uso wake. Ulikuwa uso uliokata tamaa, nikataka kuinuka lakini kabla sijafanya hivyo nikashtushwa na mlango ukifunguliwa, hapo nikajilaza haraka nikayafumba macho, yule mwanaume akatembea upesi mpaka kwa kwenye kitanda cha Mr. Kibadeni, nikayafumbua macho yangu, nikamuona akiwa anaichukua ile sindano na chupa aliyokuwa kaisahau pale kwenye kimeza kilichokuwa pembeni ya kitanda alicholazwa Mr. Kibadeni, kisha akamtazama Kibadeni, akaondoka.

Nikanyanyuka upesi, nikatembea kwa kunyata mpaka mlangoni, nikasikilizia, nikashika kitasa cha mlango nikakitekenya polepole, nikafungua mlango, nikapokelewa na korido n, nikautoa uso wangu polepole, nikachungulia kushoto sikuona mtu isipokuwa korido ndefu yenye milango huku na huku, nikaridhishwa, nikageuka upande wa kulika, hapo nikapokelewa na mlango wa lifti uliokuwa umefungwa, lakini pembeni kukiwa na kioo kinachoonyesha namba na mshale mwekundu ulioelekea chini huku zile namba zikibadilika kwa kupungua, “kumi na sita, kumi na tano, kumi na nne, kumi na tatu’ nilikuwa nikizisoma kimoyo moyo zile namba, nikajua yule mwanaume alikuwa akishuka na ile lifti. Nikarudi upesi wodini mpaka nilipofikia kitanda cha Kibadeni, nikamtazama kibadeni aliyekuwa ananiangalia kwa uso wa kuhitaji msaada.

“ Nitakusaidia mzee wangu, wala usijali, hautakufa, nitakusaidia” Nikamwambia.

Kisha nikauchukua ule mpira wa Dripu nikauvuta na kuutenganisha na lile dripu, maji ya ndripu na ile sumu ikawa haiendi katika mishipa ya Kibadeni. Yule mzee nikamuona akimeza fundo kubwa la mate, nikajua koo lake lilikuwa limekauka na alikuwa anahisi kiu, nikarudi kwenye kitanda changu, nikachukua chupa ya maji iliyokuwa kwenye kimeza kilichokuwa kwenye kitanda change, nikampelekea na kumnywesha, masikini kibadeni, aliyabwia maji gudugudu kama mtu aliyekuwa na kiu ya jangwani. Huenda ile sumu tayari ilikuwa imemuingia kidogo mwilini na ilikuwa imekausha koo lake, lakini hapana, itakuwa na wasiwasi wa kifo ndio ulikuwa umelikausha koo lake.

Baada ya kutosheka, nikaenda ukutani kulikuwa na Simu iliyopachikwa ukutani, nikaichukua, hapo nikasoma kwa juu kuliandikwa namba, nikazinukuu zile namba kwa kubonyeza batani zilizokuwa kwenye keyboard ya ile simu kama ya mezani, kisha nikaipigia, simu ikaita bila ya mafanikio, ilikuwa haipokelewi, nikapiga zaidi na zaidi bila ya mafanikio.

“ Sasa waliiweka ya nini hapa, mtu akipatwa na shida hapa si anakufa kizembe” Nikawaza. Kisha nikatoka pale ndani, nikawa nachechemea nikifuata upande wa mkono wa kushoto, nikawa nasoma maandishi yaliyoandikwa kwenye vibao vilivyokuwa juu ya mlango, mpaka nilipofika kwenye kibao kilichoandikwa “ONLY STAFFS” Nikabisha hodi, palikuwa kimya, nikatekenya kitasa nikazama ndani, nilimkuta Muuguzi akiwa kalala fofofo kwenye meza, pembeni yake ilikuwepo simu janja, nikajua alikuwa akichati. Alikuwa hoi sana. Nikamuamsha, masikini! Nilimuona akibabaika kwa mawenge ya usingizi, baada ya kuamka nikamuelezea kuwa Yule mgonjwa niliyekuwa naye wodi moja kazidiwa. Tukaondoka mbiombio, tukafika.

Ikabidi nidanganye kuwa Dripu lilikuwa limetoka, sasa akawa anataka kulirudishia, nikawa namzuia, Muuguzi akawa anashangaa kwa nini namzuia. Mimi nikawa naogopa kumueleza kuwa kuna mtu alikuja mule ndani akaitia ile dripu sumu. Kwani sikuwa na ushahidi, na mgonjwa mwenyewe alikuwa haongei wala hawezi kuchezesha uso wake kuashiria jambo kwa kukubali au kukataa, labda Kibadeni angekuwa anauwezo wa kuzungumza au kutoa ishara basi angenisaidia kutoa ushahidi. Lakini ndio hivyo tena.

Yule Muuguzi akawa hanielewi, akawa ananizuia, tukagombana tukiwa tunashikana na kuvutana kila alipotaka kuiunganisha, kwa kweli sikuwa na jinsi, nilimnyang’anya yule muuguzi lile dripu na kulikanyaga pale chini likapasuka na kurusha maji na ile sumu pale sakafuni. Kibadeni alikuwa akitutaza,ma tukifanya yote hayo. Hiyo nayo ilikuwa ni shida kubwa wala sitaki kukumbuka, ilikuwa shida baada ya shida, haijaisha shida hii inaingia shida nyingine, Yule muuguzi akapiga kelele huku akikimbilia ukutani, nikamuona akibonyeza kitufe kitufe Fulani ambacho nilielewa anatoa taarifa ya kuomba msaada kuna hatari imetokea. Hazikuzidi dakika tano mlango wa ile wodi ilifunguliwa wakaingia wanaume watatu waliovalia sare za Ulinzi wakiwa na silaha zao za moto, muuguzi akawaamuru wanikamate, nikiwa nahangaika kujitetea nikiwasihi waniache nieleze, wala hawakunipa nafasi, wala hawakutaka kujua nataka kusema nini, walimsikiliza Muuguzi labda kwa vile anahaki kunishinda, lakini wakati mwingine ukweli huweza kupishana na haki katika macho ya watu.

Nikamuona Kibadeni akijitahidi kutoa ishara lakini hazikuwa na maana yoyote, ni kama alitaka kunisaidia na kuwaelezea wale walinzi kilichotokea, lakini hakuna aliyeliona jambo hilo nikachukuliwa msobe msobe kama mhalifu,

“ Sikilizeni! Naombeni mnisikilize nyie! Mimi sio mtu mbaya, nilikuwa namuokoa yule mzee, sikuwa na nia mbaya” Nikawa naongea ongea tukiwa tayari tumeingia kwenye lifti tukishuka chini. Wale walinzi wala hawakuwa na muda wa kusikiliza maneno yangu. Ndivyo ilivyokuwa siku ile.

ITAENDELEA

Simulizi ya Kusisimua ya kijasusi 'MLIO WA RISASI HARUSINI" Inapatikana; Softcopy Tsh 3,000 Kitabu Tsh 10,000/= Itumwe na pesa ya kutolea.

0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
 
1648549982193.png


Kila siku saa saba mchana, simulizi hii itakuwa ikirushwa hewani.

Toa maoni yako, yatazingatiwa
 
KABURI LA MWANAMUZIKI ( Sehemu ya 07)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

SEHEMU YA 07

ILIPOISHIA....

Nikamuona Kibadeni akijitahidi kutoa ishara lakini hazikuwa na maana yoyote, ni kama alitaka kunisaidia na kuwaelezea wale walinzi kilichotokea, lakini hakuna aliyeliona jambo hilo nikachukuliwa msobe msobe kama mhalifu,
“ Sikilizeni! Naombeni mnisikilize nyie! Mimi sio mtu mbaya, nilikuwa namuokoa yule mzee, sikuwa na nia mbaya” Nikawa naongea ongea tukiwa tayari tumeingia kwenye lifti tukishuka chini. Wale walinzi wala hawakuwa na muda wa kusikiliza maneno yangu. Ndivyo ilivyokuwa siku ile.

ENDELEA

Asubuhi ilinikuta nikiwa kituo cha polisi kwenye kachumba kadogo hivi, baridi ilizitekenya mbavu zangu, ngozi ilikuwa imeota vipele vidogovidogo vya baridi, nilikuwa nipo kifua wazi, shati nililokuwa nimelivaa nilivuliwa na wale walinzi walivyokuwa wakinileta kitu hicho; Kosa langu ni nini, kipi nimeikosea dunia mpaka yanipate mambo yote haya; labda ninalipia makosa ya wazazi wangu, lakini ni makosa gani hayo; nimechoka! Nimechoka kuishi, maisha gani haya, likitoka hili linaingia jingine” nilikuwa nikiwaza.

Nikakumbuka usiku wa jana jinsi yule mtu alivyokuwa akizungumza na Mzee Kibadeni, kichwa kikajawa na maswali mengi yasiyo na majibu; Mzee Kibadeni ni nani, Kwa nini yule mwanaume alitaka kumuua. “ Kwa nini nami nilimuokoa, hiki sasa ni kiherehere, ona sasa yananipata haya, kama nisingemsaidia Mr. Kibadeni huenda muda huu nisingekuwa kwenye hiki chumba” Bado nilikuwa nikiwaza nikijilaumu kwa kujihusisha na mambo yasiyonihusu, lakini nikakumbuka hata mimi kuna mtu alijihusisha na mimi, akaniokoa nisichomwe moto, taswira ya yule mwanaume chizi ikanijia, kisha nikasema; hata mimi kuna mtu alijihusisha na mimi, na ndio maana leo hii nipo hai. Kama nisipojihusisha na maisha ya wengine wakati wa matatizo yao, basi hata mimi ipo siku watu hawatajihusisha na mimi katika matatizo yangu. Nilijifunza maisha yanahitaji kujihusisha na shida za watu wengine, kukimbia shida za watu wengine ni kuzikimbilia shida zako na asiwepo wa kukusaidia. Nikakumbuka yule kijana aliyeniokoa kule kwenye ile Club ya Nato Night Club, “Yule naye alijihusisha na matatizo yangu” Nikawaza, huku nikijifariji kuwa sina haja ya kujilaumu.

“Itakuwa mama amenitafuta sana, itakuwa anawasiwasi mwingi kwani ni wiki mbili sasa zimepita sijawasiliana naye. Masikini Mama yangu yupo katika kipindi kigumu sana, hajui mtoto wake nina hali gani, pia huenda atakuwa ameikumbuka sauti yangu” Nilikuwa nikiwaza, machozi yanilenga lenga, nikawa nayazuia yasitoke.

“Mama sikuja mjini kumdhuru yeyote, nilikuja kwa ajili ya kila mtu katika jamii na taifa letu. Nilikuwa naitafuta funguo ya mageuzi kwa ajili yetu, kuzikonga nyoyo za watu, kuzifungua chemichemi za furaha kwa waliokata tumaini, muziki katika siasa utakaowaunganisha viongozi wakubwa wa nchi na wananchi masikini, muziki katika utamaduni utakaolinda mila, desturi na miiko ya jamii zetu, lakini hayo yote je? Imekuwaje niko hapa! Mama hata mimi sijui” Niliongea kwa sauti ya chini nikiwa peke yangu kama mlokole aliyekuwa anasali. Nikaanza Kulia, kwikwi ikaifanya sauti yangu iwe na kitetemeshi;

“ Siwezi kuishia hapa! Siwezi! Sitakata tamaa. Nitatoka humu tuu!” Nikasema.

“ Acha kujidanganya bwana mdogo, hapa huwezi kutoka, vijana wengi kama wewe wakijaga humu sero siku ya kwanza huwa na matumaini makubwa kama yako, lakini kadiri siku ziendavyo mahabusu huyageuza matumaini yao na kuwa moshi mchungu katika macho yao, baadaye ukiwaona utawakuta wakilia tuu, nataka nikuambie Bwana mdogo, kesi inayokukabili inaweza kukufanya utumikie gerezani nusu ya maisha yako yaliyobakia” Askari yule akasema, aliyetokea kwenye mlango wa chuma uliokuwa na sehemu iliyotosha sisi kuonana.

“ Nusu ya maisha yangu! Askari unajua unachokisema” Nikasema, nikawa nalisogelea lile geti ambapo Askari alikuwa amesimama upande wa pili tukitenganishwa na lile geti.

“ Nina miaka kumi na tano kwenye kazi ya uaskari, nimewaona watu wa namna mbalimbali wakiingia chumba hiki, niliwaona wenye hatia wakifungwa wakitokea chumba hikihiki, lakini pia niliwaona wenye hatia wakiachiwa huru licha ya kuwa na makosa; hiyo inaweza isikuumize sana, ngoja nikuambie bwana mdogo, gereza liliwekwa kwa ajili ya watu wa aina mbili; yakwanza, watu wenye makosa ambao walishindwa kujitetea mbele ya sheria na kuzidiwa nguvu na vielezo vya ushahidi mahakamani, kundi hili lisipokuwa na pesa basi kesi huisha mapema zaidi, lakini ikiwa mshtakiwa atakuwa na pesa anaweza kujinasua na ikaonekana hana hatia. Upo bwana mdogo” Yule Askari alisema, akiwa anakipiga kirungu chake kwenye kiganja cha mkono wake. Nikawa namtazama kwa hasira, nikakumbuka sio yeye aliyenileta pale. Nikamuuliza;

“ Aina ya pili ni watu wa aina gani?”

“ Watu kama wewe, mnaojiona hamna hatia, huenda wakati mwingine hamna hatia, lakini nani atajali. Makosa yenu ni kuingilia maisha ya watu wengine, kujiingiza katika kumi na nane za wakubwa, hiyo huwafanya muwe katika kachumba kama haka, mwishowe mtapelekwa gerezani mkajifunze kufuata mambo yanayowahusu” Yule askari alisema, akiwa ananitazama kwa macho ya kunionea huruma alafu tabasamu la dhihaka likajichora katika sura yake; akashika lile geti, nami nikamsogelea;

“ Sijaingilia maisha ya yeyote yule, nipo hapa kwa sababu ya kulinda maisha ya mtu, hilo ndilo kosa! Nakuuliza hilo ndilo kosa, nijibu..”

“ Sio kazi yangu kujua jambo Fulani ni kosa au sio kosa, mimi nimekukuta humu ndani, nilikuwa najaribu kukueleza uzoefu wangu katika kazi hii, alafu bwana mdogo, unajua unachekesha sana! Nani alikuweka kulinda maisha ya watu wengine! Wewe sio Askari, tangu lini chokoraa akawa mlinda maisha ya watu” Yule Askari alisema kwa dharau.

“ Wewe mpuuzi! Nani chokoraa! Mpuuzi wewe! Fungua geti nikufundishe adabu, fungua sasa mbona unaogopa” Hasira zikanipanda nikawa nafoka nikilipigapiga lile geti, Askari akasogea kidogo nikawa najaribu kupitisha mikono yangu lakini sikuwa namfikia, akanyanyua kirungu chake ili anipige nacho nikarudisha haraka mikono ndani. Kile kirungu kikakata upepo. “Mpuuzi sana wewe” Nikasema.

Yule askari akaondoka. Nikarudi mpaka kwenye kona ya kile chumba na kukaa chini kwa kujikunyata, nilikuwa nimechoshwa na kile chumba, maneno ya yule askari niliyapuuza. Nilimuona kama mtu aliyetaka kunikebehi na kunikera ili nijisikie vibaya, kabla sijafikiria vizuri tazama nikaona kwenye lile geti Askari wawili waliokuwa ndani ya sare zao, nikaamka himahima, wale askari wakalifungua geti lile kisha mmoja akaja kunichukua maelezo yangu, nikaeleza jinsi ilivyokuwa, nikawauliza;

“ Kwa nini mnanichukua maelezo haya”

“ Hizi ni taratibu za kisheria ambazo polisi tunazifuata, maelezo haya yatatumika mahakamani”

“ Mahakamani! Kwa nini maelezo yangu yatumike mahakamani?Mimi sihusiani lolote na mahakama” Nikasema nikiwa nimeshtushwa na maelezo ya wale Askari.

“ Kijana embu tulia, kesho utapelekwa mahakamani…”

“ Hapana! Sio kweli! Mimi nimefanya nini mpaka nipelekwe mahakamani, lipi kosa langu” Nikasema.

“ Sikiliza kijana, unashtakiwa kwa makosa mawili, moja, kumpiga muuguzi wa hospitali, kosa la pili, kuharibu mali ya hospitali..” Yule Askari Polisi alisema akiirudisha kalamu kwenye mfuko wa shati lake.

“ Uongo! Sijampiga yule Muuguzi, wala hata sijamgusa, sijaharibu mali zozote za hospitali, kweli nawaambieni” Nilisema nikiwa najaribu kuwashawishi.

“ Kesho mahakamani utaeleza hayo, sawa kijana, sisi kazi yetu imeishia hapa” Yule Askari polisi akainuka kisha wakafunga lile geti kunifungia kwenye kile chumba, nikawa nawaita nikiwabembeleza;

“ Kaka Polisi!, Ndugu zangu, tafadhali msiniache humu mwenyewe, nitoeni humu, nyie! Embu nitoeni humu mimi sijafanya lolote naapia kwa jina la mama yangu mzazi” Wale askari wala hawakunisikiliza, wakafunga geti kisha wakaondoka. Nililia sana siku ile. Sikuwa na makosa yoyote iweje nifanyiwe vile. Sikuwahi kumfanyia jambo lolote baya katika maisha yangu, kila nilichofanya nilikifanya kwa wema, leo hii wema wangu umeniponza.

Saa hazikuganda, njaa ilibisha hodi tumboni mwangu, ilikuwa tayari ni saa nne za asubuhi. Kama ningekuwa hospitalini ule ndio ungekuwa muda wa Zuleikha kuniletea chai, lakini sasa sikuwa hospitali, nilikuwa sero ndani ya kuta nne.

Punde akaja yule Askari wa mwanzo kabisa, akanitazama name nikawa namtazama, alinidadisi kwa kuniangalia kuanzia juu ya uso akashuka mpaka chini kwenye miguu, alafu akanitazama tena usoni;

“ Bwana mdogo, hakuna ndugu yeyote anayejua upo hapa akuletee chakula, hapa usije ukadhani tutakupa chakula bwana mdogo” Yule Askari akasema, ni kama alikuwa ananionea huruma ingawaje hakutaka kukubaliana na huruma iliyokuwa ikiushawishi moyo wake.

“ Hata nikiwa na njaa, nikifa kwa kukosa chakula hiyo haikuhusu, sawa! Achana na mimi, Fanya mambo yako!” Nikamjibu.

“Hahahah! Unaleta ujeuri huku bwana mdogo, labda hukuwahi kuambiwa kuwa huku ni shule ya watu wenye tabia kama yako, watu wajeuri, wakaidi, wenye kiburi kama chako hapa hufunzwa adabu, NIkushauri kitu bwana mdogo?” akasema akijifanya ni mtu muhimu kwenye jamii, pengine alitaka kunionyesha anaijua kazi yake. Nikamkatiza;

“ Sihitaji ushauri wako! Mnanifungia humu ndani ili mnipe ushauri sio, niliwaambia nataka ushauri, embu nitoeni humu bhana!”

“ Sikiliza kijana, nakupa onyo kwa mara ya mwisho, kiburi chako huku sio sehemu yake, utajikuta katika hali ngumu sana, unafikiri nakuonea wivu wewe kuwa hapa, hahahah! Mimi nilitaka nikushauri jambo litakalokusaidia lakini kiburi chako kimenifanya nighairi, maana hata nikikuambia bado utakaidi, mtu mwenye kiburi na jeuri siku zote huwa mkaidi. Acha nikuache humu, njaa haikukupata vizuri” Yule askari polisi akatoka, nikakimbilia kwenye lile geti, nikalishika nikimchungulia akiwa anapotelea kwenye korido.

Ni kweli nilikuwa nina njaa lakini sikutaka kumuomba shetani chakula, niliwaona wale askari kama mashetani walionifungia kwenye chumba cha mateso. Niliamini kuwa shetani haombwi chakula kwani kamwe hawezi kukupa, nani asiyejua shetani anapenda watu wakiteseka na wakifa polepole kwa maumivu makali, na kama shetani akikupa chakula basi ujue kina sumu. Hivyo ndivyo nilivyojua, lakini nani awezaye kuishinda njaa, sikuwa kumjua wala sikuwahi kuambiwa, wala kusikia mahali popote kuwa kuna mtu aliyewahi kuishinda njaa. Njaa inauma jamani, inatesa sana, njaa haiwezi kukupa nafasi ya kufikiri vizuri, njaa hulegeza mwili na kumfanya mtu aishiwe na nguvu, labda hiyo haitoshi, njaa ikaona pamoja na mateso yote hayo, mtu anaweza pata upenyo wa kuikimbia kwa kulala usingizi, njaa ikafunga njia ya mwanadamu kupata usingizi, ili iendelee kumtesa pasipo kumuachia mapumziko, lakini kwa kujua kuwa wapo wanadamu wakorofi ambao watajitutumua wapate usingizi, njaa ikaona iweke ndoto za kutisha pindi watu hao wakipata usingizi. Basi mtu alalapo akiwa ananjaa ataota ndoto mbaya za kutisha mpaka ataamka mwenyewe. Hiyo ndio njaa ambayo wengi waliwaombea maadui zao.

Hivi leo nami nilikuwa katika njia ambayo sikuwa najua ni njia ya njaa, sikuwahi kujua kuwa Gerezani njaa ni jambo la kawaida, ni moja ya mkondo wa njaa. Ilianza kidogo kidogo, nikawa napiga miayo, kisha ikatulia kidogo, alafu nikawa najinyoosha kama paka aliyelala muda mrefu, kisha njaa ikaongezeka zaidi na zaidi mpaka kuharibu mifumo ya akili, sasa sikuwa na uwezo wa kufikiri jambo la maana, na kama nikifikiri jambo la maana basi siwezi kulifikiria jambo hilo mpaka mwisho. Mwenye njaa hawezi kufikiri la maana.

Ikafika mchana nikawa nimejilaza kwenye kona ya kile chumba, nikamkumbuka Zuleikha, “Zuleikha mbona haji kuniona huku jamani, au labda hajui nimeletwa Gereza gani, lakini lazima angeambiwa nilipopelekwa, sasa mbona haji. Zuleikha njoo tafadhali, nina kufa na njaa” niliwaza, nikiwa nimelala pale chini nikiwa hoi taaban, nikipumua kwa taabu sana.

“ Wewe Dogo! Hahah! Njaa ya siku moja unalegea hivyo kama Mlenda! Sasa maisha ya Jela utayaweza kweli wewe” Nikaisikia sauti ya yule Askari, nikaugeuza uso wangu polepole, nikamtazama, nilimuona akiwa kabeba kibakuli kichojaa ugali mdogo wenye maharage, nikainuka na kuketi, kisha nikawa namtazama. Naye akawa ananiangalia, akacheka alafu akainama na kuingiza ile bakuli yenye ugali na maharage ndani ya geti akakisukuma, nikaamka, na kukifuata kile chakula, nikakibeba, kisha nikamtazama yule askari usoni, akaniashiria nile pasipo kusema, nikala upesiupesi kama mtu niliyefikiri nimepewa muda wa sekunde kumi niwe nimekimaliza, lakini ni kwa sababu nilikuwa na njaa sana.

Nilipomaliza, nikajinyoosha kuivukuza njaa iliyokuwa imejificha katika misuli yangu, alafu nikasimama, angalau sasa nilikuwa nimepata nguvu. Nikamrudishia yule Askari kile kibakuli. Nikamtazama pasipo kusema lolote, ningewezaje kumshukuru mtu niliyemuona kama shetani hata kama amenisaidia chakula, yule Askari polisi akachukua ile bakuli akaondoka bila ya kusema jambo lolote. Hiyo ilikuwa saa tisa mchana.

Jioni ilipofika, wakaja maaskari wawili, hawa walikuwa wamevaa sare ya rangi ya ugoro, walikuwa Askari polisi, kisha akaja na yule Askari niliyekuwa tayari nimemzoea, yule aliyeniletea chakula, akanikabidhi kwa wale Askari magereza alafu akasema;

“ Bwana mdogo zingatia niliyokuambia, usije ukaleta ukaidi, kiburi na jeuri yako huko uendako, utajutia, haya kila la kheri bwana mdogo” Yule Askari akasema, alikuwa akitabasamu kwa mbali niliiona huruma iliyokuwa imejificha, nilitaka kuamini anahuruma lakini nikalipinga wazo hilo.

Nilikuwa nimefungwa pingu sasa, labda nilikuwa nimekamilisha vigezo vya kuitwa mhalifu. Walinipelekea mbiombio wakiwa wamenishika tanganyikajeki, nilitaka kusema jambo lakini akili yangu ikanionya, nilikumbuka maneno ya Yule Askari ambaye sikutaka kuamini alikuwa ni mtu mwema. Tulizifuata korido za majengo yale, kisha tukashuka chini tukawa tunatembea kwenye barabara ya vumbi yenye safu ya maua upande huu na upande huu, ilikuwa ni wakati wa jua kupunga, jioni kabisa vivuli vikiwa ni virefu, nililitazama jua kwa huzuni nyingi, nalo jua lilikuwa likimulika uso wangu na miale isiyo na nguvu, ilikuwa ni miale pekee iliyonipa tumaini, ingawaje maisha yangu yalikuwa yanazama gizani lakini miale ya jua yenye matumaini bado ilikuwa ikinimulika.

Wakanikokota mpaka tulipofika kwenye chumba kimoja hivi ambacho hakikuwa kimesiribwa na saruji, mlango wa chumba kile ulikuwa chakavu lakini imara, moja ya wale askari akafungua mlango wa kile chumba ambacho kilikuwa hakifurahishi machoni. Wakanifungua mbingu, Askari mmoja akiwa ameshika bunduki Kisha wakanikokota mpaka mlangoni, na kunisokomeza ndani kwa kunisukuma, nikapepesuka mpaka nilipoangukia ndani, alafu wakafunga mlango, hapo nikapokelewa na giza zito, sikuona kitu tena, giza lilizidi uwezo wa mboni za macho yangu, ni mpaka dakika moja ilipoisha ndipo nilipo gundua kwa juu kabisa kulikuwa na matundu matano yaliyokuwa yanapitisha mwanga na hewa, yalikuwa matundu yenye upana kama kitako cha chupa ya bia na yalikuwa juu kabisa mahali ambapo hakuna mtu angeweza kufika pasipo kutumia ngazi. Awali hali ya mule ndani niliifurahia kutokana na kuwa nilitoka kwenye chumba nilichokuwa nasikia baridi, sasa chumba kile kilikuwa na joto kwa sababu ya kukosa madirisha makubwa zaidi ya yale matundu, lakini baada ya nusu saa kupita ndio nilipoona kasheshe la joto la mule ndani, jamani kulikuwa na joto, nilikuwa natoa jasho ungedhani muoka mikate ya kienyeji.

Zile nusu saa tangu niingie zilinifanya nione nuru hafifu mule ndani, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo giza lilivyokuwa linazidi, hatimaye kukawa giza kabisa, nikajua kuwa Jua limezama na usiku ulikuwa umeingia. Kulikuwa kimya sana mule ndani, giza lake lilikosa mfano nakuambia, nikatembea kutafuta sehemu ya kulala, nikapapasa papasa mpaka nilipougusa ukuta, hapo nikakaa nikiwa nimeugemea, mawazo mengi yalinifuata mpaka kwenye giza, mpaka kwenye shimo mawazo hayakuniacha. Yalijuaje nipo wapi kila nilikoenda hata mimi sikuwa najua, lakini mawazo ni nafsi ya mtu ya ndani ambayo humfuata mtu popote alipo, nafsi ni kama kivuli cha mwili ambao ni nafsi ya nje, ambacho huongozana popote kama mapacha waliofanana.

Kama niliandikiwa matatizo nilitamani aliyeyaandika matatizo yale awe ameyaandika na kalamu ya mkaa, ili aweze kuyafuta, nilichoshwa na matatizo yaliyokuwa yananiandama katika maisha yangu, labda kwangu maana ya maisha ilikuwa matatizo, nani ajuaye. Sakafu ya kile chumba licha ya kuwa nilikuwa siioni kwa macho lakini ngozi yangu ilinijulisha kuwa ilikuwa sakafu yenye changarawe na cementi ya kuzugia tuu, zile changarawe zilikuwa zikinikera sana, zilikuwa zikinichoma choma, zilininyima raha, lakini nikakumbuka pale ni Sero sikupelekwa mule ili nipate raha. “Bado sijahukumiwa nafanyiwa haya, nalazwa mahali penye mateso namna hii, vipi nikihukumiwa?” Nikawaza.

Baada ya muda mrefu kupita nikiwa katikati ya giza la kile chumba, usingizi ukiwa umenisaliti kwa kunimbia licha ya kujitahidi kuuita nikiubembeleza, nikaona isiwe tabu; kichwani nikajikuta nikipata wimbo nisioujua, yalikuwa maneno ambayo niliyaimba mdomoni huku sauti za mdundo zikiwa kichwani mwangu, na hivi ndivyo nilivyokuwa nikiuimba wimbo ule siku ile;

“ Ninaishi maisha ya kupendelewa, kwa nguvu nisiyoiona ninaishi

Katikati ya giza tumaini limejificha ndani yangu,

Mimi ni waajabu, hata haya yanipate nitafika safari yangu,

Ooooh! Maajabu! Katikati ya giza upo mwangaza ndani yangu,

Hata yote yaishe, dunia nayo ipite, sitaiacha ndoyo yangu,

Kwenye giza nako nitaimba, wote wapate nuru

Hata kwenye njia yenye miiba, nitaimba nikicheza,

Adui wakinizingira kama hizi kuta nne, nitaimba katkati yao,

Furaha yangu haipo nje, kamwe haiwezi kuwa kati yao

Ipo ndani ya kifua changu, kamwe hawatoweza kuichukua,

Sauti kutoka gizani, Gibson leo ninaimba”

Nikawa natabasamu katikati ya giza wala hakuna ambaye angeliona tabasamu langu, moyo wangu ukajawa na furaha, nilijihisi nguvu mpya ikitokea ndani, labda muziki ulikuwa na nguvu za ziada nilizokuwa bado sijazigundua. Hatimaye nikapitiwa na usingizi, nikalala nikiliacha giza likinifuka kama shuka, nikisubiri ndoto ndani ya gereza, labda ningejua ningeota nini lakini sikuwa nafahamu, ningeambiwa nichague ndoto ambayo ningeiota siku ile wala nisingeweza kwani vile tuu nilivyokuwa naishi niliiona kama ndoto mbaya ambayo nilitaka ikate, niamke lakini haikuwa ndoto, ni kweli nilikuwa sero kwenye chumba chenye giza nene lililochanganyika na hewa nzito, joto likiukumbatia mwili wangu.

********************************

Nikaamka, bado kulikuwa na giza nene, sikujua ni usiku au ni mchana, lakini nilikumbuka habari za yale matundu matano katika chumba kile, nikatazama juu, bado yaliyoa mwanga hafifu mno, nikajua kulikuwa hakujakucha, kilichoniamsha ni lile joto, nashindwa kulieleza joto la kile chumba, ila nataka kukuambia kulikuwa na joto la kufa mtu.

Nikasikia kwa mbali Jimbi akiwika, nafikiri alikuwa ndiye Jimbi wa kwanza kuwika kwa siku ile, hii ilimaanisha siku mpya imeingia, alfajiri i karibu. Sauti ya jimbi huwa ni nzuri na yenye kuvutia, tena inaleta nguvu ya matumaini kwa mtu aliyeteseka usiku mzima, sauti ya Jimbi iliwajulisha wale wote waliokuwa wakiteseka usiku mzima kuwa Asubuhi imekaribia, mwisho wa machungu umekaribia, mateso na huzuni yameisha kama usiku ule ulivyoisha. Ndivyo nami nilivyoichukulia ile sauti ya yule jimbi aliyewika; baada ya kusota usiku mzima na mateso ya kile chumba sasa asubuhi i mlangoni. Niliwahi kuambiwa na Mama yangu kuwa jimbi huwika kwa sababu maalum; sababu ya kwanza jimbi hulia kutoa ishara ya kutenganisha masaa kwa masaa, kisha hulia kutenganisha siku moja na ile inayofuata. Kabla ya ujio wa teknolojia ya saa, jimbi alikuwa ni kiumbe muhimu wa kujulisha nyakati za masaa na mianzo na miisho ya siku. Lakini mbali na kujulisha watu muda, jimbi pia huwika kama sehemu ya kutamba kwenye ufalme wake, kutangaza kuwa mtawala wa eneo Fulani ni lakwake, ikiwa jimbi atawika sehemu ambayo sio mtawala basi ingemaanisha vita kwa mtawala anayetawala eneo hilo.

Asubuhi ikafika, nuru ikawa inaongezeka polepole kadiri palivyokuwa pakipambazuka, hata hivyo nuru haikunifanya nione vizuri mule ndani. Nilichoka kukaa sehemu moja, nikaamka na kuanza kutembeatembea mule ndani, ghafla macho yangu yalishtushwa na kitu kama kifurushi kilichokuwa upande wa pili wa kile chumba, kitakuwa ni kitu gani, nikawa najiuliza huku nikipiga hatua polepole kwa tahadhari, nilipokuwa nakikaribia macho yangu yalichora taswira ya umbo la mtu aliyekuwa amelala pale. Nikamsogelea, alikuwa ni mwanaume aliyekuwa amelala, nikainama alafu nikamshika kwenye bega nikaanza kumtingisha,

“ Wewe! Wewe! Amka kumekucha!’ Niliita kwa kunong’ona nikiwa namtingisha. Yule mtu akaamka na kunigeukia.

“Wewe nani!” Yule mwanaume akasema,

“ Mimi mwenzako kwenye hiki chumba” Nikajibu.

“ Sina mwenzangu, niambie wewe nani?”

“ Mimi ni Mwanamuziki..” Nikasema, akaamka kwa hamaki akaniuliza;

“ Mwanamuziki!” tukawa tunatazamana akiwa ananingalia kwa kuyakaza macho yake ili anione vizuri kutokana na giza la chumba kile.

“ Mwanamuziki gani?” Akaongeza.

“ Hahahaa! Kwani kuna muziki gani, unaniuliza kwa sababu hujawahi kunisikia kwenye Redio wala kuniona kwenye luninga?” Nikasema nikiwa najenga urafiki.

“ Afadhali umeongea mwenyewe, labda uniambie mwanamuziki wa Gereza” Yule mwanaume akasema, hapo nikacheka sana, alafu akaendelea;

“ Unafanya nini huku gerezani?”

“ Nimeletwa niwaimbie wafungwa na mahabusu” Nikamjibu nikiwa natania.

“ Itakuwa ajabu sana, kwa hiyo leo ndio umekuja kuniimbia? Hii program imeanza lini, nimekuwa mzoefu wa magereza mbalimbali hapa nchini lakini jambo hili nimelionea kwenye gereza hili tuu” Yule mwanaume akasema, kumbe mtu yule alikuwa mzoefu wa magereza. Itakuwa ni mtu mkorofi sana, nilikuwa nawaza.

“ Mbona umekaa kimya mwanamuziki?” akanitupia swali, nikashtuka kama niliyekuwa sipo pale kutokana na mawazo.

“ Nipo sana, nilifika jana, nitakuwa hapa kwa muda kidogo, nitahakikisha wafungwa wote mnasikia muziki wangu, nitahakikisha mahabusu wote mnaisikiliza dhima ya muziki wangu, baada ya sheria kuwahukumu burudani itawafaraji na kuwapa tumaini” Nikasema, yule mtu akawa ananiangalia kuyapima maneno yangu, yalikuwa kama yanamuingia,

“ Nitawaimbia nyimbo kulingana na hali zenu, ila wimbo wangu wa kwanza ninautarajia kuimba utakuwa ule usemao “HUJACHELEWA KUWA HURU” wimbo huu ni maalumu kwa kila mmoja wetu humu gerezani” nikakatishwa na kicheko ya yule mwanaume;

“Hahhahah! Mwanamuziki! Unasema sijachelewa kuwa huru, hahahah!ningetamani nichelewe kuwa huru lakini ilishindakana, kwangu huu ndio uhuru, humu ndani ninaweza kufanya lolote, uhuru wa gereza ni kama uhuru wa kaburi tuu, labda useme unataka uhuru gani”

Punde lango la kile chumba likafunguliwa, sote tukageuza shingo zetu kuuangalia, jina langu likatajwa, nikaambiwa nitoke nje; nikamgeukia yule mwanaume, akawa ananitazama, kisha akawaangalia wale Askari, nikaamka, nikawafuata wale askari pale mlangoni, nikwa pale mlangoni nikamsikia yule mwanaume akisema;

“ Hujachelewa kuwa huru” Nikamtazama alafu nikatabasamu, kisha nikaondoka na wale askari magereza tukimuacha yule mwanaume akiwa amefungiwa kwenye kile chumba.

Nikavalishwa shati kubwa kubwa ambalo sikujua wamelitoa wapi, wakanipakiza ndani ya gari safari ya mahakamani ikaanza. Haikuchukua muda tukafika, hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika mahakamani, katika maisha yangu sikuwahi kufikiria siku moja nitapelekwa mahakamani kushtaki au kushtakiwa, lakini maisha huweza kukupitisha katika njia ambayo kamwe hukuwahi kuidhania, leo hii nilikuwa miongoni mwa washtakiwa katika mahakama ile.

Ukumbi wa mahakama haukuwa na watu wengi, niliwaona watu wakiwa wamekaa kwenye viti kama wasikiliza kesi, sikuwahi kufikiri kuwa kuna watu hufunga safari kabisa kutoka nyumbani kwenda mahakamani kusikiliza kesi hata isiyowahusu, siku ile nikaona watu wa namna hiyo, nikawaona pia wanafunzi wa sheria ambao walikuwa wamekaa kuisikiliza kesi yangu ili kupata uzoefu, wengine walikuwa wanasheria waliokwishapewa kibali wakiwa tu mule ndani kutafuta wateja ambao ni washtakiwa wasio na mawakili.. Punde aliingia yule muuguzi aliyeniletea matatizo yote yale, koo lilikauka kwa hasira iliyosababishwa na kumuona yule muuguzi, aligeuza uso wake akanitazama, nikajikuta nikitupa tusi zito kimoyo moyo nikiwa namtazama, naye alikuwa ananitazama kwa chuki. Nikajiuliza, kwa kipi nilichokuwa nimemfanyia mpaka anitazama kwa macho ya namna ile. Askari magereza walikuwa beneti na mimi bila kuniachia nafasi, punde Hakimu aliingia, wote wakasimama, hakimu akatembea mpaka mahali pake, akatuamuru tuketi baada ya yeye kukaa. Wale askari magereza wakanipeleka sehemu niliyokuwa nimeandaliwa, wakaniamrisha nikae, nami nikakaa.

Kesi ikaanza kusikilizwa, nilisomewa mashtaka, nikayakataa. Yule Muuguzi akawa anatoa ushahidi wake akiwa anahojiwa na wakili ambaye sikuwa najua ni wakili wake au vipi. Baada ya kujieleza, akatoa lile dripu ambalo nililikanyaga, hicho ni kielelezo kuwa niliharibu mali za hospitali lakini pia akaongeza kuwa nilikuwa nahatarisha usalama wa mgonjwa aliyekuwa ametundikiwa hilo Dripu, yule muuguzi akaambiwa athibitishe kuwa nilimpiga lakini alishindwa, akawa anatoa maneno matupu pasipo ushahidi. Basi kwa sababu kwenye maelezo yangu niliyochukuliwa kule mahabusu niliandika kuwa, nilikanyaga lile dripu likapasuka, mahakama ikanikuta na kesi ya kujibu kwa kuharibu mali za ile hospitali na hukaribu dawa na maji yaliyokuwa kwenye Dripu. Kesi ikahairishwa mpaka kesho asubuhi. Hakimu akatoka, nikarejeshwa tena Mahabusu.

ITAENDELEA; KILA SIKU SAA SABA MCHANA

Simulizi ya Kusisimua ya kijasusi 'MLIO WA RISASI HARUSINI" Inapatikana; Softcopy Tsh 3,000 Kitabu Tsh 10,000/= Itumwe na pesa ya kutolea.

0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
 
KABURI LA MWANAMUZKI (Sehemu ya 08)
Mtunzi: Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

Sehemu ya 08

ILIPOISHIA

Kesi ikaanza kusikilizwa, nilisomewa mashtaka, nikayakataa. Yule Muuguzi akawa anatoa ushahidi wake akiwa anahojiwa na wakili ambaye sikuwa najua ni wakili wake au vipi. Baada ya kujieleza, akatoa lile dripu ambalo nililikanyaga, hicho ni kielelezo kuwa niliharibu mali za hospitali lakini pia akaongeza kuwa nilikuwa nahatarisha usalama wa mgonjwa aliyekuwa ametundikiwa hilo Dripu, yule muuguzi akaambiwa athibitishe kuwa nilimpiga lakini alishindwa, akawa anatoa maneno matupu pasipo ushahidi. Basi kwa sababu kwenye maelezo yangu niliyochukuliwa kule mahabusu niliandika kuwa, nilikanyaga lile dripu likapasuka, mahakama ikanikuta na kesi ya kujibu kwa kuharibu mali za ile hospitali na hukaribu dawa na maji yaliyokuwa kwenye Dripu. Kesi ikahairishwa mpaka kesho asubuhi. Hakimu akatoka, nikarejeshwa tena Mahabusu.

ENDELEA
Tulihamishwa kwenye kile chumba cha giza na kupelekwa chumba kingine kilichokuwa na mahabusu wengine wapatao kama kumi na saba hivi, wafungwa wengi walikuwa wametokeo katika familia masikini, wenye umri kati ya miaka kumi na nane mpaka arobaini hivi, sura zao zilikuwa dhaifu zilizofubaa kwa kukosa lishe, athari za kutumia madawa ya kulevya zikiwa dhahiri katika nyuso zao. Walikuwa na macho mekundu na midomo iliyopauka ikiwa imepasuka pasuka, “ misokoto ya bangi hii” nikawaza.

“ Oya Mkali! Baridi!” Msela mmoja akanijia, akanisabahi. Nikamtazama kwa macho ya udadisi, alikuwa anameno yaliyoharibika kwa kuvuta sigara, uso wake ulikuwa na makovu mengi, hii ilinifanya nimuone kama mtu hatari aliyezoea vipigo; kama sio kibaka huyu nina uhakika ni kaka jambazi’ nikawaza nikiwa namuangalia.

“ Mkali unaleta dharau sio? Hii maskani ya masela, unaonekana mtoto wa mama, tutakufunza adabu humu” Yule msela alisema, akanisogelea macho yake akiwa kayatoa nje, kwa nilivyokuwa nimemsoma; alikuwa ananivizia anipige pigo la kushtukiza, nami sikuwa mjinga kiasi hiko, nikawa nimeigundua hila yake. Nikawa narudi nyuma nikiwa natazama naye. Nikarudi nyumanyuma mpaka mgongo wangu ulipogusa ukuta, nilikuwa nimefikia ukingo hivyo sikuweza kurudi nyuma tena, yule msela akatabasamu, hapo nikahisi kitu kikipanda kama nataka kupita, alikuwa na kinywa kilichojaa meno machafu yaliyokuwa na rangi kama yameoza, kingo za midomo yake zilikuwa na uteute mweupe, alikuwa anatia kinyaa sana.

“ Vipi! Unaogopa? Hahaha! Nataka nikufundishe kidogo michezo ya huku, nikupe shule ndogo tuu ambayo itakufaa sana, baada ya hapo utakuwa mtu mzuri sana” Yule msela akasema akiwa tayari kanikaribia kabisa, uso wake ulikuwa sentimita chache kutoka kwenye uso wangu. Harufu mbaya ilizitekenya pua zangu na kufanya uso wangu ukijikunje kwa kinyaa, nilikuwa nikimtazama kwa hofu. Lakini nikakumbuka mimi ni mwanaume, siwezi kuwa dhaifu kiasi hicho, ni lazima nipambane kama mwanaume.

“ Ondoka hapa!Mimi sio mtoto wa mama kama macho yako yanavyokudanganya, nitakuharibia mshikaji wangu” Nilisema nikiwa navuta pumzi fupifupi kuchochea ujasiri wangu. Tayari watu walikuwa wameanza kutusogelea kushuhudia ugomvi ule,

“ Leo nitakung’oa meno kama nilivyomng’oa yule ngedere pale, naye siku ya kwanza alikuwa kama wewe” Akasema akiwa amegeuka kumuangalia kijana mmoja aliyekuwa pembeni, nami nikageuka kumtazama kijana yule ambaye alikuwa akijitahidi kufumba mdomo wake ili nisiyaone mapengo yake, lakini alikuwa amechelewa, niliona uwazi mkubwa katika safu ya meno yake ya juu, uwazi ule ulikuwa ni upungufu wa meno mawili hivi.

“ Yule nilimtoa meno mawili, leo nitakutoa meno matatu na kukutoboa jicho lako hilo uwe chongo” Yule msela akasema, kisha akanipiga ngumi ya tumbo, nikagugumia maumivu nikiwa nimelishika tumbo langu, nilihisi kutapika, kisha akanipiga kisukusuku cha mgongoni, nikaangukia magoti, nikawa kama nimempigia magoti nikiwa nimeukunja mgongo wangu, yalikuwa mapigo mawili yaliyonitia wazimu, watu wakaanza kushangilia wakimsifu yule msela kama mungu mtu, akanishika kwenye shingo na kuninyanyua juu kunisimamisha, akanigandamiza kwenye ukuta akiwa anazidi kuikaba shingo yangu kwenye koo, nikawa nakosa hewa kichwa change nikiwa nimekielekeza juu kwenye pembe Fulani hivi, pumzi ilikuwa ikipungua kadiri alivyokuwa akikaza mkono kunikaba; lazima nifanye kitu, siwezi kufa kibwege” nikawaza nikiwa nimetoa macho, nikaushika ule mkono wa yule msela nikijaribu kuutoa shingoni, lakini mpango wangu uligonga mwamba, yule mtu alikuwa na mikono migumu kama chuma, alafu alikuwa na nguvu sana. Nikapata wazo, bila kupoteza muda nikalitekeleza, hapo nikamsikia yule msela akiachia yowe “ Uwiii!” Nilikuwa nimepiga kigoti cha kwenye makende yake, lilikuwa pigo murua lilipompata vyema kabisa, akaniachia akiwa amesogea nyuma kidogo, mikono yake akiwa ameshika kwenye korodani zake akiwa analia kwa uchungu.

Wale watu waliokuwa wakishangalia wakapunguza kidogo kushangilia, kukawa na sauti ndogondogo za hamaki, sikutaka kupoteza muda, nikamsogelea na kumuongezea kipigo kingine kwa kumpiga katafunua ambayo ilifanikiwa kuunyanyua uso wake na kumrusha kwa nyuma, nikawasikia wale mahabusu wengine wakitoa sauti; Haaah! Ni kama walikuwa hawaamini. Nilijua vyema uwezo wangu, sikuwa mzuri kwenye kupigana, sikuwa najua ngumi vizuri hivyo nafasi niliyoipata ilinpasa niitumie vizuri. Nikamfuata pale chini yule msela, nikampiga teke la tumbo alafu bila kumchelewesha nikamuongeza teke la mdomoni lililofanya jino lake moja kutoka na kuruka hewani, yule msela alikuwa akipiga kelele kuomba msaada lakini nikawatahadharisha wale mahabusu wasiingilie, na endapo angeingilia mtu basi ningemfanya jambo baya zaidi, wale mahabusu wakanitii, nikamshika yule Msela, nikampiga ngumi mfululizo za uso mpaka alipochakaa, nikamuacha, alafu nikasimama nikiwa nahema kwa pupa nikiwa nipo hoi kwa kuchoka, nikapiga hatua moja moja za kupepesuka, wale mahabusu wakawa wananipisha wakiniogopa.

“ Nilimuambia mwenzenu asinikadirie kisa ananiona sina mwili wenye ukakakmavu. Nilimtahadharisha mbele yenu, Mimi sio Bondia!” Nikapumua nikiangalia huku na huku kisha nikaendelea;

“ Wala mimi sio komando, mimi sio mwanajeshi, tena sio mhuni kama huyu mpuuzi hapa” Nikamfuata na kumtemea mate, yule msela aliyekuwa akiugulia maumivu huku damu zikiwa zinamtoka puani na mdomoni, alikuwa anakoroma pale chini.

“ Mimi ni mwanamuziki, mtoa burudani, mfariji wa waliokata tamaa, nililetwa humu gerezani kuwaimbia, hata ninyi mnayo haki ya kuimbiwa nyimbo nzuri, nikiwa kama mwanamuziki, nitalifanya jambo hilo mbele ya macho yenu, hamtaki kuburudika?” Nikawauliza huku nikiwatazama; wote kama mtu mmoja wakanijibu kwa sauti ya chini, “tunataka” sijui kama walijibu kwa kupenda au labda kwa sababu ya woga baada ya kumpiga yule msela mtata.

“ Sawa! Mkae sasa, kaeni hapo, kila mmoja wenu akae sehemu yake, ili niweze kuimba hapa” Nikasema, wale mahabusu kila mmoja wao akachukua sehemu yake, watatu walikaa katikati pembeni ya alipokuwa amelala yule msela niliyempiga kipigo heavy, wawili walisogea na kuketi kwenye ukuta, mmoja alikuwa ameketi kwenye konda ya kile chumba, wawili walikuwa wamechuchumaa kwenye kona nyingine ya kile chumba, watatu waliamua kusimama karibu na lango la kuingilia lililokuwa limefungwa, chumba kile hakikuwa na giza wala hakikuwa na mwanga mwingi,

“ Hatujui tulipotoka, hatujui tunakoenda,

Hapa ndani tumefika, bila shaka hatukupenda,

Huenda wapo walotaka, tabia njema ilipowashinda,

Tuishi kama kaka, humu ndani tutashinda.

Kujuana ni kutaka, ikiwa wote tutapenda,

Niite Gibson ukitaka, mwanamuziki ninayewindwa,

Lako jina talitaka, nikilijua talilinda.

Tuishi kama Kaka, humu ndani tutashinda.

Eyeeh! Hatujuani! Hatujuaaani! Ooh! Lakini siye ni ndugu!

Ooyeeye! Hatufanani! Hatuufanani! Eeh! Ila siye ni wamoja”

Wimbo huo niliuimba kwa kutunga palepale, nikaziona nyuso za wale mahabusu zikiwa na tabasamu, walikuwa wameupenda ule wimbo wakawa wanapiga makofi na kutengeneza mdundo Fulani huku wakianza kuimba sehemu ya kipande katika wimbo niliokuwa nimeuimba;

‘ Hatufanani! Hatufanani! Oooh! Ila siye ni wamojaaa( huku wakipiga makofi)” nikaongeza mstari nikiamba;

“ Tuupendane! Tuupendane! Kama watoto wa mama mmojaaa” nilipomaliza kuimba nao wakawa wanaimba, Yule msela niliyempiga akainuka naye akawa anaimba sauti yake ikiwa mbaya huku uso wake ukiwa umechakaa sana, kisha akasimama akajikokota mpaka pale nilipokuwa nimesimama, wale mahabusu wakanyamaza wakawa wanatutazama na yule msela, walikuwa wanatazama atafanya nini; Yule Msela akasema; Tuishi kama kaka, humu ndani tutashinda” kisha akanikumbatia kwa nguvu nyingi akiwa analia sana. Kitendo cha kunikumbatia kiliwafanya wale mahabusu wengine wapige makofi huku wakishangilia, ulikuwa mwanzo mpya ndani ya gereza lile. Kisha yule msela akaniachia, akawageukia wale mahabusu wengine mimi akiwa kanipa mgongo, akanyosha mikono yake miwili kuwapa ishara waache kupiga makofi, na wakae kimya, jambo hilo likafanyika, yule msela akasema;

“Humu ndani kila mtu anamakovu katika mwili wake, kweli au sikweli?” Yule Msela akasema, akiwa anatuuliza. Wote tukamkubalia kwa kichwa.

“ Hakuna binadamu asiye na makovu mwilini mwake, makovu ni alama za yale yaliyotupata katika maisha yetu, hubaki kama alama katika miili yetu kutukumbusha na kututahadharisha kuwa tusirudie makosa, humu ndani nafikiri hakuna mwenye makovu mengi makubwa ya kutisha kama mimi, au yupo? Akauliza. Hapo kila mmoja akawa akawa anamtazama vizuri yule msela ambaye kwa kweli alikuwa na makovu ya kutisha sana katika mwili wake, uso wake ulifichwa na makovu ya kuogofya, pengine hiyo ndio ilifanya wengi wamuogope mule ndani, le hii nami nilichangia sehemu ya historia isiyofutika katika maisha yake kwa kumtoa jino moja katka mdomo wake. Akaendelea kusema;

“ Ninamakovu saba makubwa ya kutisha katika mwili wangu, achaneni na haya madogo madogo, moja” akaanza kuhesabu huku akituonyesha, kovu hili likuwa kwenye ubavu wa kulia chini kidogo ya kwapa. Akavuta shati kwa juu upande wa nyuma ya mgongo na kuwageukia mahabusu, hapa sauti kutoka kwetu mahabusu ikatoka katika vinywa vyetu “Mbili” Baada ya kuona kovu kubwa kwenye mgongo wa yule msela, akashusha shati alafu akapandisha kaptura yake kwenye paja akaonyesha “Tatu” Lilikuwa kovu jeusi lililokuwa kama lengelenge lililokauka, akainamisha kichwa chake, “Nne” Eneo la katikati la kichwa kulikuwa na kovu kubwa lililofanya sehemu ile nywele zisiote. Akanyosha mkono wake tuutazame, tukasema “ Tano” kumbe hakuwa na vidole viwili vya mkono wa kushoto, vilikuwa kama vimekatwa. Akaushusha mkono wake, kisha akatutazama kana kwamba akipima mood yetu kama tumependezwa na stori yake, alipoona shauku yetu akaendelea, akainua kichwa chake ili tuone shingoni kwenye koo, hapo tukaona kovu kubwa, tukasema kwa sauti “Sita”.

“Kila kovu lina historia nzito ya kutisha iliyoathiri maisha yangu, kila kovu limebeba kumbukumbu ya majina ya watu, mambo ya kikatili waliyonifanyia, kama nikisema nielezee mkasa wa kila kovu basi ingenichukua muda mrefu sana kumaliza” Yule akasema, kuna muda alikuwa anapangusa damu zilizokuwa zimeganda kidevuni mwake, nikawa najiuliza mbona alisema anamakovu makubwa saba, lakini katuonyesha makovu sita, nikiwa nafikiri hivyo, mtu mmoja nikamsikia akiuliza;

“Mwamba! Lipo wapi Kovu la Saba?”

“ Kovu la saba, kovu mama! Chanzo kikuu cha makovu yote sita ni kovu hili la saba, kama nisingelipata kovu hili basi haya mengine yasingekuwepo na wala msingeyaona hivi leo, huenda ningekuwa mtu bora mwenye kuheshimiwa sana. Amini wajuba, maisha yanaweza kubadilika ndani ya dakika moja, kile ambacho unadhani hakiwezekani; kinawezekana tena kwa urahisi na mapema zaidi ya ulivyofikiria, fikiria kijana mdogo kabisa kutoka katika jumba la kifahari akiwa anaishi maisha mazuri yenye kutamaniwa na kila binadamu mwenye akili timamu, mwenye kupendwa na kulindwa kama mgodi wa dhahabu, kijana mdogo kutoka katika familia bora iliyokuwa inaheshima sana, maisha yanambadilikia, anakuwa kama malaika aliyefukuzwa peponi akatupwa kuzimu kwenye shimo refu lenye giza na kila aina ya wanyama hatari. Hivi naeleweka” Yule mtu akasema, kwa kweli alikuwa ametuacha, tulikuwa hatumuelewi licha ya kuwa tulikuwa tunajitahidi kumuelewa.

“ Miaka thelasini iliyopita tukio la kutisha lilitokea katika familia yetu, tukio lililobadilisha maisha yangu yakuwa ya mateso na kusikitisha, nakumbuka ilikuwa mida ya saa tatu za usiku, siku ile mama yangu alikuwa ananisomea kitabu kama ilivyodesuri yake, ilikuwa bedtime stori ambayo nilikuwa nasomewa mpaka nitakapolala, siku ile mama alikuwa amefumua nywele zake ndefu alizokuwa kazichana vizuri, mama yangu alikuwa nanywele nzuri sana, nilikuwa mdogo lakini niliweza kulitambua jambo hilo, basi mama akawa ananisomea bedtime stori huku akiwa amenikumbatia kwa upendo, usingizi ukanichukua hata sikujua ulinichukua muda gani, nikalala kama kawaida, lakini ghafla nilishtushwa na sauti ya kelele, nikaamka, nikajikuta mwenyewe kitandani, lakini bado nilikuwa nasikia kelele upande wa pili ambapo ilikuwa ni sebuleni, nikaamka, hapo nilikuwa ninamiaka saba hivi; nikatoka chumbani kwangu, nikawa nazisikia zile kelele zikizidi, nikanyata polepole mpaka nilipokaribia sebule ya nyumba yetu, nikachungulia, moyo wangu ulishtuka sana kwa kile nilichokuwa nimekiona” Yule Msela akameza mate kisha akawa anatutazama kwa zamu. Nikama alijua tunataka kujua nini kilikuwa kimetokea, sasa aliiacha shauku yetu ipande juu zaidi, kisha akaendelea;

“Niliwaona wanaume wawili wakiwa wamevaa barakoa za kuficha nyuso zao, pia walikuwa na wanawake wawili ambao walivalia hijabu kuficha sura zao, wanaume wale walikuwa wamewaweka chini ya ulinzi mama yangu na baba yangu, pia Dada yangu wa pekee naye alikuwa kapigwa vibaya sana na wale wanaume, Dada yangu alikuwa na miaka kumi na tano, kwetu tulikuwa tumezaliwa wawili, mimi na huyo dada yangu, nikamuona baba yangu akiwa anatoka damu akiwa hoi kwa kupigwa, alikuwa amevaa pensi na kaoshi aliyokuwa amezoea kuzivaa kama nguo za kushindia nyumbani, alikuwa kachakaa sana, walikuwa wamempiga sana wakiwa wamemsimamia na bunduki, nilikuwa najiuliza kwa nini watu wale wanawapiga Baba, mama na Dada yangu, nikiwa bado nimejificha, nikajua kuwa wale walikuwa majambazi waliokuwa wakihitaji pesa. Nikamuona moja ya wale wanawake majambazi waliovalia hijabu wakiwa wameficha nyuso zao, akamfuata mama yangu, akamkamata kwa nguvu kwenye nywele na kuanza kuzivuta akimpiga makofi na mateke, mama yangu alikuwa akipiga kelele akiomba msaada, kila baba alipokuwa akitaka kumsaidia wale wanaume walimzuia kwa kumpiga ngumi na mateke, hakuwa na ujanja tena, mama alipigwa sana akawa analia kwa sauti ambayo iliniumiza sana, ninaikumba mpaka hivi leo sauti ile, sauti ya mama yangu kipenzi! Nilimsikia mama akisema; Ninajua aliyewatuma, ninajua! Yule ni shetani!” Mama yangu alisema akiwa anatweta kwa nguvu kama mtu anayekaribia kuishiwa pumzi, kisha nikamuona mama akimtazama baba yangu, alafu akasema; Mume wangu nilikuambia achana naye yule mwanamke, najua haya yote ameyafanya yeye, hukunisikiliza mimi mkeo ukaisikiliza tamaa yako, ona sasa ananiua mimi’ Mama aliongea akiwa anatoa machozi ya uchungu, nikawa najiuliza ni mwanamke gani huyo ambaye mama anamzungumzia, nilitamani kumjua huyo mwanamke, tayari chuki iliuvaa moyo wangu, kwa kweli nilimpenda mama yangu” Yule msela akatutazama, akaniangalia mimi kisha akaniambia “ Hatujuani! Hatujuani!” Ngoja niwajuze mimi ni nani. Akaendelea kusimulia;

“Machozi yaliweka ukungu machoni mwangu, wale wanaume wakamshika Dada yangu wa pekee, Dada Consolatha, wakamuelekezea kwa mama yangu, nilimuona Conso akiwa analia kwa kwikwi akihitaji msaada, nikamuona yule mwanamke aliyekuwa akimpiga mama akitoa bonge la kisu, hapo joto la mwili wangu likapanda, nilihisi hatari kubwa inaenda kutokea, yule mwanamke akamsogelea Conso kisha akawaamuru wale wanaume wamshike miguu na mikono kumdhibiti, wakamdhibiti, nikamuona baba akijaribu kufurukuta ili ajinasue na zile kamba alizokuwa amefungwa lakini hakuweza, aliishia tuu kuita Conso! Conso! Binti yangu Consolata” Walimchinja kikatilia sana dada yangu, mbele ya macho yangu nikiwa nimejificha, nilihisi uchungu kunizidi, nilimpenda Consolatha, ndiye alikuwa dada yangu hasa,” Yule msela alikuwa akisimulia huku akilia, wote hisia za huzuni zilifanikiwa kututongoza, nilikuwa nahisi kama nataka kudondosha machozi lakini nikajikaza, simulizi ya msela ilikuwa inasikitisha mno.

“Mama alikuwa akijipigapiga pale chini huku akilia kwa kutetemeka, nilitaka kujitokeza lakini kwa bahati Baba yangu aliwahi kuniona kabla ya wote, akanizuia nisiende kwa ishara ya uso, nilikuwa nataka nikaidi lakini alinisihi sana, tena sana, yule mwanaume mmoja akamuona Baba kama anatoa ishara akawa anageuka kuona anampa nani ishara, nikawahi kujibanza, almanusura yule mwanaume katili angeniona lakini nilikuwa mwepesi kujificha, nikawa napumua kwa hofu, mapigo yalikuwa yakienda mbio, sijui kama ningeonekana ingekuwaje, nafikiri leo hii ningekuwa mmoja wa wahanga wa tukio lile la kutisha, Nikachungulia tena, natazama nikaona yule mwanamke akimshika mama yangu nywele zake na kumkita kisu cha mbavu, nikataka kupiga kelele lakini ghafla nikazibwa mdomo na mikono Fulani hivi; nikawa najaribu kufurukuta nikijaribu kujitoa katika ile mikono lakini sikufua dafu, nilizidiwa nguvu, basi nikawa nalia kwa uchungu nikiwa nachungulia mama yangu akifa mbele ya mikono ya mwanamke katili alificha uso wake, Baba yangu alikuwa kama amechanganyikiwa, hakujua yale yalikuwa ni kweli au ilikuwa ni ndoto, kisha baada ya Mama yangu kuiga dunia kwa maumivu makali, yule mwanamke akakichomoa kile kisu kwenye mbavu, alafu akakifuta katika nywele za mama yangu” Yule msela akaanza kulia, alilia huku akitetemeka, tulijikuta nasi tumeanza kulia, ulikuwa mkasa wa ajabu sana wenye kuumiza hisia.

Nikawa najiuliza, kwa nini watu wale waamue kuwaua ndugu zake Yule msela, nilitamani kujua sababu ya mambo yote hayo, nikakumbuka habari za Yule mwanaume aliyekuja hospialini kumuua mzee Kibadeni, “Dunia hii kuna watu makatili sana” Nikawaza, nikajifuta machozi, yule msela akaendelea;

“Nilikuwa nikilia sana, nilikuwa najiuliza kwa nini wamuue Mama yangu, amewakosea nini mama yangu mpaka wamuue, lakini labda siyajui mambo yote ya mama, sawa nakubali! Vipi Consolata naye, makosa yake ni yapi, Consolata alikuwa binti mpole mwenye adabu, alikuwa mwenye akili sana, hakuwa na kiburi wala hakuwa nadharau licha ya kuwa anatoka kwenye familia ya kitajiri na Baba yake alikuwa ni Waziri, kosa la Consolata ni nini?” akawa anatutazama alafu akatuuliza sisi kama ndio tuliomuuua Conso “Nawauliza Kosa la Consolata ni lipi, niambie sasa hivi?” hapo hofu ikawa imetuingia, tulihisi huenda msela atakuwa ameanza kuchanganyikiwa, tukawa tunatazamana wenyewe wenyewe kama tunajadili jibu la kumpatia yule msela, kisha msela akapiga chafya, puani akawa anatoa makamasi mepesimepesi, akasema;

“ Sitamsamehe yeyote aliyehusika na mauaji ya Mama yangu, niliapa nitamuua kwa kifo kibaya yeyote aliyehusika na kifo cha dada yangu, Conso. Nilikuwa mdogo sana lakini roho ya mauaji ilinivaa kisawasawa, nikawa natingishwa na kwikwi huku macho yangu yakiwa yamejaa machozi, mashavu yote yakiwa yametepeta kwa machozi, bado nilikuwa nimezibwa mdomo, nikiwa nimeshikiliwa kwa nguvu sana pale mafichoni; Nikamuona yule mwanamke aliyemuua Conso, akamuua na Mama akimfuata Baba pale chini alipokuwa amelala akiwa amefungwa kamba, nikajua sasa ni zamu ya baba kuuawa, nikamuona Baba akiyanyanyua macho yake na kutazama kule nilikokuwa nimejificha, nilijkuta machozi yakizidi kutoka zaidi na zaidi, yule mwanamke muuaji akasema; Umeiangamiza familia yako mwenyewe, ubishi wako ndio umemaliza kila kitu katika maisha yako” Baba alipoisikia ile sauti akatoa macho kisha akaita “ Dora!” Akanyamaza akiwa anatazamana na yule mwanamke muuaji, yule mwanamke akalitoa lile juba lililokuwa limeuficha uso wake, “ Kumbe ni wewe, Dora kwa nini umenifanyia hivi” Nami nikawa nashangaa kumuona yule mwanamke ambaye baba alinifanya nitambue jina lake ni Dora, sikuwahi kumuona, wala sikuwahi kumfahamu, ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kumuona katika maisha. Koo langu lilikauka kwa hasira, nilitamani niwe na uwezo wa kumuulia palepale yule mwanamke, naam ndiye Dora aliyeujeruhi moyo wangu, aliyewaua wazazi wangu na kuniachia kovu kubwa ndani ya moyo wangu, kovu lisiloonekana katika mwili wangu lakini ndilo kovu kubwa kuliko ya yote, lililoacha alama mbaya katika mapito yangu, Dora ndiye mhusika mkubwa katika kovu la moyo wangu, huyo mwanamke ndiye aliyeyabadilisha maisha yangu” Yule msela akameza mate, kisha akapenga makamasi yaliyokuwa yanamsonga puani mwake, alafu akamalizia kuyafuta machozi yake.. Ilikuwa simulizi ambayo ilinifanya nijione sijawahi Kupitia maumivu makali kama yale, sasa ni kama tulikuwa tunataka tujue ilikuwaje,

Lakini Msela ambaye sikuwahi kulifahamu jina lake mpaka siku moja isiyo na jina ilipofika, yule msela akagoma kumalizia stori yake ya kutisha iliyobadili maisha yake. Tulimbeembeleza sana, lakini akakataa, lakini akasema;

“ Hata aliyeniokoa walimuua siku ile, yule dada aliyeuziba mdomo wangu ili nisipige kelele walimuua, walimyonga, kisha wakachoma kila kitu mule ndani pamoja na nyumba, labda mnajiuliza niliokokaje, si ndio” Yule msela akatuuliza akitutazama; lakini kabla hatujamjibu, kengele ikagongwa, ilikuwa ni muda wa kwenda kulala, ilikuwa tayari imefika jioni, tulitamani tuwaambie wale Askari magereza watupe muda walau nusu saa ili Yule msela aimalizie stori yake lakini hatukuruhusiwa. Tukagawanywa, wengine wakabaki mule ndani wengine tukapelekwa katika vyumba vingine vya magereza. Hivyo ndivyo ilivyokuwa siku zile katika mapito yangu nilipokuwa gerezani.

***************************

Kesho haikukawia kucha, kama zilivyokuwa siku nyingine siku ya leo ilikucha kwa namna yake, kulikuwa na hali ya mawingu mazito ambayo yaliashiria mvua kubwa ingenyesha dakika chache zijazo, nikapakizwa ndani ya gari la magereza, safari ya Mahakamani ilianza, tukiwa njiani mvua kubwa ilidondoka, ilikuwa ni mvua ambayo ilinyesha kwa namna ya kuogopesha, ilinyesha ikiwa imechanganyika na upepo mkali sana, magari yalikuwa yamewasha taa, nilichungulia nje ambapo niliona maji yakifurika katika barabara, ile mitaro iliyokuwa pembeni ya barabara ilikuwa imefurika maji, sasa ilikuwa inatapika, takataka nazo zilikuwa zikibebwa, ungesema zimetoka wapi kama sio kwa wakazi wa Dar es salaam wasiowaungwana ambao hutupa hovyo takataka bila kujali usafi wa mazingira, jambo hili lilikuwa hatari kwa afya ndani ya jiji la Dar. Milipuko ya magonjwa kama ugonjwa wa kipindu pindu au kichocho husababishwa kwa sehemu kikubwa na Uchafu. Bado Mvua kubwa ilikuwa inanyesha licha ya kuwa tulikuwa tumesimama kwenye eneo la mahakama tukiwa ndani ya gari. Ilitubidi tusubiri mvua iishe ndipo tushuke.

Nusu saa ilipita, Mvua ikakatika, yakabakia manyunyu tuu yaliyochanganyika na kumbikumbi walikuwa wakiruka ruka huku na huku angani, niliingizwa mahakamani, na muda haukupita hakimu aliingia na kesi ilianza kusikilizwa; Hakimu alinisomea shtaka, akanikumbusha nipo chini ya kiapo cha jana, lakini pia akanikumbusha kuwa tayari ninakesi ya kujibu kwa kosa la kuharibu mali ya hospitali, baada ya hapo hakimu akanipa nafasi ya kujitetea na kama nina ushahidi na mashahidi katika shauri linalonikabili. Nikapelekwa kizimbani, na hapo nikaanza kuzungumza;

“ Ndugu Mheshimiwa Jaji, mbele ya mahakama yako tukufu aliyesimama ni Gibson Alexander, ninaomba kujitetea;” Nikamtazama Hakimu aliyekuwa akiandika, akanitazama na kunipa ishara niendelee.

“ Siku ile sikuwa na nia mbaya ya kuharibu mali za hospitali ambayo kwayo nilikuwa nimelazwa, mimi ni mtu mwema, nilijaribu kuokoa maisha ya mtu aliyekuwa anataka kuuawa, Mwanaume niliyekuwa nimelazwa naye kwenye wodi ile alitaka kuuawa…” Nikasema lakini Hakimu akanikatisha.

“ Subiri mbona unaeleza mambo mapya hapa”

“ Hapana mheshimiwa, naeleza kila kitu kilichotokea siku ile” Nikasema kwa nidhamu.

“ Kwa hiyo unaruhusu maelezo yako yaingie kwenye rekodi ya mahakama?” Akaniuliza,

“ Ndio mheshimiwa” Nikajibu, kisha hakimu akaniamuru niendelee.

“ Mheshimiwa, tukiwa wodini usiku wa maneno aliingia mwanaume mrefu mwenye mwili wa kikakamavu akiwa kava koti la kidaktari akiwa ameficha uso wake na barakoa iliyotobolewa sehemu za macho ili aweze kuona, mtu yule akataka kumua yule mgonjwa, akatoa sindano na kichupa. Akamuamsha mgonjwa mwenzangu kwa kuwa alikuwa amelala, akamtishia na kumsumbua, kisha akamuambia anamuua kwa kifo cha polepole chenye maumivu makali mno, ndipo akaivuta dawa kwenye sindano kutoka kwenye kile kichupa, alafu akaiingiza kwenye Dripu, baada ya yule mwanaume aliyetaka kumuua mgonjwa mwezangu kuondoka, mimi Gibson ndio nikaenda kuichomoa ile Dripu kwa yule mgonjwa mwenzangu, baadaye nikaenda kumuita huyu Muuguzi, lakini nilishindwa kumueleza haya huyu muuguzi, nikawa namkatalia asimuwekee mgonjwa lile Dripu, sikuwa namlaumu kwa kugombana na mimi kwani hakuwa anajua sababu, ndipo nikaamua kulikanyaga pale chini likapasuka, ndipo akawaita walinzi wa pale hospitalini wakanichukua pale na kunipelekea kituo cha polisi, na baadaye korokoroni, nikaja jana na leo ndio nipo hapa Mheshimiwa” Nikasema.

“ Ulijuaje ni muuaji huyo mwanaume wakati alikuwa kava kama Daktari” Wakili wa Muuguzi akaniuliza, nikamjibu.

“Nilijua ni muuaji kwa sababu alikuwa kaficha uso wake na barakoa kama jambazi, madaktari hawafichi nyuso zao kwa namna ile, pili, maneno aliyokuwa anamuambia yule mgonjwa mwenzangu”

“ Huyo mgonjwa mwenzako anaitwa nani” Wakili akaniuliza.

“ Mimi sijui anaitwa nani” Nikajibu

“ Na bado unamuita mgonjwa mwenzako,? Unaposema mgonjwa mwenzako unamaanisha nini?” Akaniuliza. Hapo nikanayamaza kwa kitambo kisha nikajibu;

“ Ni kwa sababu wote tulikuwa wagonjwa tuliolazwa wodi moja” Nikajibu.

“ Inasemekana wewe ni mwizi, ulikoswa koswa kuua kule manzese na ndio sababu ya wewe kulazwa kwenye ile hospitali” Wakili akauliza

“ Mimi sio mwizi, wala sijawahi kuwa mwizi” nikajibu.

“ Haiingii akilini watu watake kukuchoma moto bila sababu za msingi, lazima wewe utakuwa mwizi”

“ Mheshimiwa hakimu, naona ndugu wakili ananivunjia heshima kwa kuniiota mwizi, jambo ambalo nikimwambia athibitishe hataweza” Nikasema nikiwa nimekasirishwa sana.

“ Nawakumbusha hapa ni mahakamani, mnapaswa kuzingatia sheria na kanuni, hakuna mwenye ruhusa kutoa hukumu isipokuwa mahakama, sitavumilia lugha za kuudhi na kutweza utu wa mtu yeyote humu ndani” Hakimu akasema, kisha akaendelea;

“ Mr. Gibson, umeongea maneno matupu lakini hakuna ushahidi wowote zaidi ya maneno yako, vipi unalolote la kuthibitisha maneno yako?”

Nikatafakari, “ninatakiwa niithibitishe mahakama ukweli wa maneno yangu, sasa nitathibitishaje, nikishindwa maneno yangu yataonekana ya kujitungia tuu” nikawaza; alafu nikasema

“ Mhe, Hakimu mimi sina ushahidi wowote maana ile siku tulikuwa mimi, huyu muuguzi na yule mgonjwa mwenzangu. Labda yule mgonjwa aletwe hapa mahakamani maana siku ile alikuwa macho akishuhudia yote yaliyokuwa yanatokea, lakini sina uhakika kama sasa hivi anaongea maana alikuwa hawezi jambo lolote zaidi ya kufumbua na kufumba macho yake, kidogo na kujigeuza” Nikasema;

Hapo nikamuona hakimu akijadili jambo na wazee wa baraza kisha walipomaliza akagonga meza kuwanyamazisha watu waliokuwa wameanza kujadiliana mule ndani kwa kunong’ona.

“ Kesi imehairishwa mpaka kesho, mahakama itakupa ruhusa ya kumleta huyo mgonjwa kama shahidi wa kesi hii” Hakimu akamaliza kuzungumza, akatoka.

Nikarudishwa Sero, nikiwa njiani ndani ya lile gari la magereza, macho yangu yalikuwa nje yakitathmini na kusanifu uharibifu uliofanywa na mvua kubwa iliyonyesha masaa mawili yaliyopita, Barabara za vumbi zilikuwa zimeharibiwa vibaya mno, mmomonyoko wa udongo ulizichakaza zile barabara, nikaona takataka zikiwa zimelundikana barabara, hapakuwa panavutia hata kidogo, tukafika mbele kidogo ambapo barabara ilikuwa juuu, nilishuhudia nyumba zilizokuwa mabondeni nikiwa zimefurika maji, ile mvua ilisababisha mafuriko yaliyoharibu makazi ya waliojenga mabondeni, hapo ikazuka mada mule ndani ya gari baada ya kuwaona watu Fulani kule mabondeni wakiwa juu ya paa za nyumba chini nyumba zao zikiwa zimezingirwa na maji.

“ Hawa watu kila siku wanaambiwa na serikali wasijenge mabondeni, wakiambiwa wahame hawataki, wenyewe wanakuambia mvua ya siku mbili haiwezi kutuamisha kutupeleka maporini, ati wao hawataki kukaa nje mji, wanataka kukaa katikati ya mji” Askari magereza mmoja alisema.

“ Kubanana kote kule, vijumba vimebanana kama meno, hakuna hata njia ya gari kupita” Miwngine akaitikia.

“ Gari! Kwani wanampango wa kuwa na magari, magari sio kwa ajili yao, wao wamerizika na bodaboda, baiskeli na bajaji, wakitaka kwenda mjini watapanda daladala” Yule askari magereza akasema, Tukafika Magereza, tukashushwa kila mmoja akapelekwa chumba chake.

Nikiwa magereza nikakumbuka habari za Mr. Kibadeni, nilitamani kujua hali yake, sijui atakuwa anaendeleaje Mr. Kibadeni’ nilikuwa nawaza. Nikakumbuka kuwa kesho ndio siku ambayo mahakama imenipa idhini ya kumleta shahidi wangu mahakamani, nikaamka, nikasogelea mlango wa kile chumba wa kuingilia, nikawa ninaita; “Afande! Afande! Afande!’ Punde Askari magaereza akatokea, nikamueleza kuwa nahitaji kwenda kumpa taarifa Mgonjwa mwenzangu kuwa anisaidie kesho kuwa shahidi wangu, yule Askari magereza akaondoka akasema nisubiri aende kuuliza utaratibu.

Hazikupita dakika kumi, alirejea akiwa na Askari ambaye hajavaa sare, baada ya kusalimiana, nikakabidhiwa kwa yule askari polisi, kisha akanichukua na kuniingiza katika gari la polisi lililofanana na Teksi kimuundo lakini ubavuni lilikuwa na rangi ya Darkblue na maandishi meupe yaliyosomeka “POLISI” Nikaingizwa ndani nikiwa nimevalishwa pingu, tukatoka pale mpaka tulipofika kwenye ile hospitali, tukaripoti kuwa tumefika kumuona mgonjwa aliyekuwa amelazwa wodi na 118 Ghorofa ya ishirini na moja,

“Nifuateni” Yule mtu wa mapokezi akatuchukua mpaka ghorofa ya tano, akatukabidhi kwa Daktari mmoja mwenye kitambi.

“ Unaitwa nani kijana?” akaniuliza.

“ Naitwa Gibson Alexander” Nikajibu.

“ Umekuja kuonana naye kwa sababu gani?” Akaniuliza akiwa anaandika.

“ Ninataka awe shahidi katika kesi inayonikabili”

“ Kesi! Hawezi! Hali yake sio nzuri” Yule Daktari mwanaume mwenye kitambi akasema akinitazama.

“ Basi nahitaji kuonana naye walau nimuone” Nikasema

“ Sidhani kama itawezekana” Akasema lakini yule Askari polisi akasema

“ Hii ni ruhusa ya mahakama, hata kama hajiwezi tunaweza kumuona angalau tumuone kama yupo kweli, hata tusipoongea naye”

‘ Sawa Afande, basi ngojeni kidogo” Yule Daktari akasema, alikubali sio kwa matakwa yake isipokuwa kwa heshima ya Afande, kama asingekuwa Afande basi asingekubali. Akabonyeza bonyeza simu ya mezani kisha akaweka mkonga wa simu sikioni;

‘ Hello! Kuna watu wanataka kumuona mgonjwa k07, ndio, ni kijana mmoja na Askari polisi, ndio, sidhani kama watakubali, wamekuja na ruhusa ya mahakama, ndio nilijaribu kuwazuia, sawa ngoja niwapandishe, sawa haya” Yule Daktari akamaliza kuaongea na simu akatugeukia kisha akasema; Nifuateni” tunakumfuata yeye akiwa mbele yetu, tukapanda kwenye Lifti, akabonyeza bonyeza namba pale, ile lifti ikaanza kuondoka, hatukujua kama inapanda juu wala hatukujua inashuka chini. “ Ulinzi utakuwa umeimarishwa sasa, hapa haijulikani tunaenda ghorofa ya juu au ya chini, nahisi ni kwa sababu ya Mr. Kibadeni kukoswa koswa kuuawa” nilikuwa nawaza.

Lifti ilisimama, lango likafunguka, tukapokelewa na walinzi wawili waliovalia sare za rangi ya darkblue, kofia, na dirii za ngozi vifuani mwao, mabuti meusi ya kijeshi, mkononi wakiwa na silaha, wale watu walitukagua lakini polisi akatoa kitambulisho chake, wakakikagua kisha wakaturuhusu, tukamfuata yule askari, tukapita kwenye korido ndefu iliyopoa kwa kiyoyozi taa zikiifanya korido ile iwe na nuru.

Tukapita milango miwili mkono wa kushoto, na mmoja mkono wa kulia, kisha tukakatisha kuifuata korido nyingine iliyokuwa mkono wa kulia, tukalakiwa na walinzi wawili tena waliokuwa nje ya mlango uliokuwa unatutazama, tukawasalimia, wakatupitishia kifaa Fulani kwenye miili yetu, baada ya kuona hatuna hatari yoyote wakaturuhusu, tukafunguliwa mlango, hapo tukapokelewa na ukumbi wenye mitambo aina aina ya tekonolojia ya kisasa kabisa, hapo nikawa nashangaa shangaa, tukatembea tukipita baaadhi ya ile mitambo kisha kwa mbele nikaona kitanda cha kisasa kabisa chenye mashuka meupe, eneo lote pale lilijazwa na vitu vyenye rangi nyeupe, juu ya kile kitanda alikuwa amelzwa Mr. Kibadeni, pembeni yake alikuwepo kijana mmoja ambaye alikuwa kafanana sana na Mr. Kibadeni, kulikuwa na kachumba kengine ambako nilikuja kujua ilikuwa maliwatoni. Punde mlango wa kile chumba ambacho ni choo ukafunguka, hapo akatokea Mwanaume mmoja aliyevaa koti la kidaktari, nikajua alikuwa ndiye daktari aliyekuwa akiongea na simu muda ule.

Mr. Kibadeni aliponiona akatabasamu, nami nikatabasamu, akayapeleka macho yake katika mikono yangu iliyokuwa imefungwa pingu, akasikitika sana.

“ Gibson!” Akaniita nikaitika kwa kushtuka sikujua kama anajua jina langu.

“ Mbona unashtuka, hahaha! Jina lako nilisikia kwa yule msichana aliyekuwa anakutunza”

“ Nani! Zuleikha?” Nikauliza kwa shauku.

“ Ndio Zuleikha, alishangaa alipokukosa pale, mimi sikuwa na uwezo wa kuzungumza, alafu baadaye nilihamishwa kutokana na ishu za kiusalama”

“ Kwa hiyo alinitafuta kumbe?” Nikauliza nikiwa natafakari.

“ Ahsante kwa kuyaokoa maisha yangu Gibson, Mwanangu huyu ndiye yule kijana niliyekuwa nakuambia mchana wa leo umtafute mahali kokote umpate, yeye ndiye aliyenisaidia, leo hii ningekuwa nimekufa” Mr. Kibadeni akasema akiwa anatabasamu, nilishangaa kumuona akiwa anaongea, unajua alikuwa kama mtu ambaye angekufa muda wowote.

“ Mzee wangu, mimi sina muda mwingi hapa, huyu niliyekuja naye ni Askari polisi, nimekuja hapa kukuomba kesho uje ili uutoe ushahidi katika kesi yangu” Nikaongea lakini akanikatisha

“ Usijali, nitakuja, hata kama hawataniruhusu mimi nitakuja hivyohivyo” Akajibu, kisha askari polisi akaniambia muda wa kuzungumza umeisha, tukawaaga na kuondoka.

Tumaini la kuwa huru likamea moyoni mwanguy, niliyakumbuka maisha ya uhuru, hata kama sikuwa na maisha mazuri lakini angalau nilikuwa naishi kwa uhuru.

************************

Kesho ikafika, nikapelekwa mahakamani, tukiwa tunamsubiri hakimu aje, niligeuza kichwa changu huku na huku, kuangalia kama Mr. Kibadeni ameletwa kutoa ushahidi lakini sikuweza kumuona, wasiwasi ulianza kuisigina nafsi yangu, kama asipokuja inamaana nitaonekana ni muongo, Mr. Kibadeni ndiye mwenye uwezo wa kuthibitisha maneno yangu ni kweli, kama asipokuja basi mahakama itanitia hatiani. Nilijipa moyo hata kama hisia za kukata tamaa zilinisonga.

Hakimu aliingia, bado Mr. Kibadeni alikuwa hajafika, nilihisi kurukwa na akili, kama sio kuchanganyikiwa nilihisi presha ikipanda. Hakimu aliniamuru nimkaribishe shahidi wangu, nikabaki nimeduwaa nisijue kipi ningesema, sikumuona Mr. Kibadeni, nilikata matumaini, milango ya gereza niliiona ikifunguka.

“ Mheshimiwa hakimu, naomba muda kama nusu saa, hali ya shahidi wangu kama nilivyosema jana kuwa anaumwa, jana nilienda na Askari mpaka hospitalini, akaahidi angekuja leo, ikupendeze Mhe, Hakimu, tusubiri dakika thelasini” Nikasema.

Hakimu akahairisha kesi kwa dakika thelasini, lakini nazo hazikukawia kuisha, lakini Mr. Kibadeni hakutokea, Hakimu akarejea mhakamani,

‘ Shahidi wako yupo wap?’ Hakimu akaniuliza.

Nikawa natazama mlango wa kuingilia kuona kama Mr. Kibadeni angetokea lakini sikumuona mtu yeyote. “Nini kitakuwa kimempata Mr. Kibadeni’ Nikawaza.

“ Kama hakuna shahidi basi mahakama itakuhesabu kama unahatia, na itatoa adhabu kali” Hakimu alisema, sikuwa na jinsi zaidi ya kukabiliana na mwisho wangu, mwisho ndani ya gereza.

“ Mheshimiwa Hakimu, naomba tuu niiachie mahakama, nipo tayari kwa hukumu” Nikasema, hakimu akaandika andika kisha akataka kusema kitu lakini ghafla akatokea mtu mmoja akiingia mlangoni, macho ya watu wote yakaelekea mlango, kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuona shahidi. Nami nikageuka kuufuata mlango alipokuwaanatokea mtu yule, nilishtuka kumuona yule kijana pekeake pasipo Mr. Kibadeni, alikuwa ni yule kijana aliyekuwa amefanana na Mr. Kibadeni.

“ Baba yupo wapi ndugu yangu?” swali likaniponyoka.

Yule kijana akawa ananitazama kisha akamtazama hakimu,

“ Huyu ni nani, Gibson?” Hakimu akaniuliza.

“ Huyu ni mtoto wa Shahidi, alikuwa jana na Shahidi jana nilipoenda kule Hospitali kumuona shahidi” Nikajibu. Hakimu akamtazama Yule kijana, kisha akasema;

“ Baba yako yupo wapi?’

“ Baba yangu, hayupo Amekufa usiku wa kuamkia leo” Yule kijana akasema, kwa kweli maneno yake yalinifanya nichanganyikiwe,

“ Nimekwisha! Nimekwisha mimi!” Nikawa napiga kelele pale mahakamani.

ITAENDELEA; KILA SIKU SAA SABA MCHANA

Simulizi ya Kusisimua ya kijasusi 'MLIO WA RISASI HARUSINI" Inapatikana; Softcopy Tsh 3,000 Kitabu Tsh 10,000/= Itumwe na pesa ya kutolea.

0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
 
Back
Top Bottom