Simulizi ya kusisimua: Kaburi la Mwanamuziki

Simulizi ya kusisimua: Kaburi la Mwanamuziki

KABURI LA MWANAMUZIKI (EPISODE 02)
Mtunzi; Robert Heriel
whatsApp 0693322300

EPISODE 02
ILIPOISHIA

Nilikuwa nimeduwaa nikiwa namtazama akiwa anashuka kwenye ngazi polepole kwa madoido huku akitabasamu na kupiga hatua zake kwa tahadhari kwa mwendo wa catwalk, mara kwa mara alinyanyua mkono wake akizitoa nywele usoni kwa mbwembwe utadhani muigizaji mahiri wa filamu; akili haikunirejea mpaka aliponikaribia na kusimama mbele yangu kama malaika mwema na kujigeuza shaaa, nikasikia harufu ya manukato yake mazuri ajabu, kiukweli shemeji alikuwa mzuri wala sitaki kumsifia tena isijeonekana nilikuwa namtamani.

“OOH! My dear! Umevaa nini hii! Subiri nakuja” Shemeji akasema, kisha akapanda tena juu ghorofani. Hazikupita dakika nyingi akarudi akiwa na fuko lenye nguo ndani yake.

“Hizi nguo hazijavaliwa, Riadi aliletewa na Mwanamke mmoja wa kizungu ambaye kwa kweli ananiudhi sana, nahisi wanatoka naye” Shemeji akasema,

“Unamaana gani kusema hivyo?”

“Gibson, wewe sio mtoto mdogo, embu vaa tuondoke muda umekwenda” Akasema,.

*******

ENDELEA
Ndani ya Gari Shemeji alinifanyia vituko vya kila aina, mapaja yake aliyetumia ipasavyo kunifanyia emotional damage, alinitesa sana shemeji, tulifika maeneo ya mikocheni tukamuacha mtoto pale sehemu ya kuogelea tukimkabidhi kwa wahusika wa mahali pale, shemeji akaniambia; sisi twende kwa wakubwa, sio mbali kutoka hapa” na kweli haikuchukua dakika tano tulisimama eneo jingine palepale mikocheni tukaingiza gari ndani ya geti baada ya kuruhusiwa na walinzi, tuliifuata njia yenye vigae ambayo ilizungukwa na maua huku na huku, tukiwa chini ya vivuli vyenye upepo mwanana, eneo lilikuwa na kagiza kanakotokana na kivuli cha miti mingi na maua ya kuvutia yaliyokuwa eneo lile, tulipita katikati ya jengo lilokuwa mbele yetu tukatokea upande wa pili ambapo tulilakiwa na uwazi mkubwa wenye mwanga, kushoto likiwepo Bwawa kubwa la kisasa la kuogelea, tukapinda kulia kuifuata njia ambapo mbele kulikuwepo na eneo la maegesho ya magari. Baada ya kuegesha gari letu, tukashuka nikiwa nashangaa uzuri wa eneo lile, tulipotoka lile jengo kwa juu yalisomeka maandishi Turkey Resort LL. Kulikuwa pia na Mini-supermarket, mbele kabisa kwenye bwawa niliona vitanda vizuri vya kupumzika, nyuma ya vile vitanda vya kupumzikia kushoto kabisa zilikuwepo meza na viti vya dizaini ya kustaajabisha. Bado nilikuwa nikishangaa, niliona wanawake watatu, wawili wakiwa majini wakiogelea kwa raha zao, mmoja alikuwa kalala kwenye vile vitanda akiwa kava miwani nyeusi, na nguo za kuogelea ambazo kwa sehemu kubwa ziliacha sehemu za mwili wake wazi, akiwa kashikilia Glass yenye Cocktail ya rangi ya waridi.

Shemeji alinishika mkono kama vile mtu na mwenza wake, nilipotaka kupingana na jambo lake akanikazia macho, sikuwa na namna zaidi ya kumkubalia, tulioongozana mpaka kwenye ile supermarket, milango ya vioo yenye sensor ikafunguka yenyewe, tukaingia ndani, tukapokelewa na Kijana mmoja wa kituruki, tukapita moja kwa moja kwenye bidhaa, shemeji akanichagulia bukta nzuri ya kuogelea, kisha baada ya kunichagulia, tukarudi kwa yule kijana wa kituruki, tukalipia, tukatoka, akarudi kwenye gari, mimi akanielekeza niende kwenye chumba Fulani kilichokuwa karibu na maegesho ya magari ili nikabadili nguo, sikuweza kukataa,

Nilirejea nikiwa nipo kifua wazi na bukta mpya niliyonunuliwa na shemeji, ilikuwa bukta ya rangi nyeusi yenye mstari mweupe uliopita kama upinde kutoka upande wa kulia mpaka kushoto, ilikuwa imenishika vyema sana, basi nikasogea kwenye lile bwawa wale wadada wawili wakawa wananitazama kwa kujiiba iba, nikawasalimu, wakaniitikia lakini kwa kuchanganya Kiswahili na kingereza, hapo nikajua walikuwa wadada wakishua, kwani hata muonekano wao uliwatambulisha hivyo, walijaribu kunikarimu huku wakizikung’uta kila mara nywele zao zilizokuwa zimelowa maji. Sikupata muda wa kuzungumza nao sana, shemeji alikuja na kunikumbatia kwa nyuma, kisha akaniachia na kunishika mkono wa kulia, nikageuka bado nikiwa nimemshika na mkono wakulia, macho yangu yalaishutushwa, nilibaki nimetoa macho nikiukodolea mwili wa shemeji, alikuwa kavaa skirtini tamka ‘sketini’ iliyomkaa sawa, sketini ni kijivazi cha kuogelea wanachovaa wanawake ambacho huwafanya kuwa na mvuto wa kimapenzi, kwa juu huwa brazia ya kitambaa alafu chini huwa ni kisketi kifupi kilichoachia na kuyaacha mapaja mazito ya shemeji yakimeremeta. Sketini aliyokuwa amevaa ilikuwa ni rangi ya waridi na ile brazia ilikuwa ya rangi yenye mistari meusi na nyeupe. Alipendeza sana, akaninyanyua mkono wangu na kujizungusha na kufanya kile kiguo kupepea kidogo na kuzidi kuniharibu vibaya hisia zangu.

Tuliingia majini tukawa tunaogelea huku kila mara akinikumbatia, shemeji alichokuwa anakifanya ni kuwaonyesha wale wadada wengine kuwa mimi ni mtu wake, aliona jinsi walivyokuwa wakinitazama na kuna wakati nami nilikuwa najiiba kuwatazama, hii ilipelekea kunifokea kila alipokuwa akiniona, sasa tulikuwa tumeshaogelea vya kutosha, wale wadada walikuwa wamejilaza kama mamba kwenye vile vitanda wakiwa wamevaa kila mmoja miwani, tulitoka majini nikiwa nimechakazwa vibaya kihisia na Shemeji yangu, sitaki kukumbuka kwani ule ulikuwa mwanzo wa kujiingiza katika shimo refu lenye giza, ambalo lilibadilisha maisha yangu.

Tukaenda kupumzika kwenye vile vitanda tukipiga stori, kisha tulipokauka, tukaenda kwenye zile meza na viti na kuagiza chakula kwani tayari ilikuwa imetimia saa sita hivi, ile menu ilikuwa na vyakula vilivyoandikwa kwa lugha nisiyokuwa ninaielewa, kama sio picha zilizokuwemo basi nisingeelewa hata kitu kimoja katika menu ile, niliambulia kuona picha ya nyama ya ng’ombe, kuku pamoja na soseji, picha za matunda pamoja na juisi, bei zake zilinishtua sana, sikuweza kuamini kuwa kulikuwa na chakula cha elfu sabini, na juisi ya elfu thelesini na tano, nikakumbuka kauli ya Riadi kuwa pesa aliyoniachia haitanitosha, sasa nilianza kukubaliana na Riadi; kama matumizi yenyewe ndio yale basi ni kweli milioni moja kwa siku tano sio kitu. Mimi sikula vitu vingi isipokuwa nyama iliyochanganywa sijui na kitu ganai pamoja na juisi ambayo iligharimu kama laki moja na kumi, shemeji yeye alikunywa whisky Glenfiddich 15yrs ambayo iligharimu laki na ishirini yenye kiwango cha pombe asilimia arobaini. Aliagiza na nyama choma tuu zilizotengenezwa vizuri, tulimaliza kula na kuondoka wakati shemeji akiwa ameshaanza kulewa, wakati tunaingia ndani ya gari kwa bahati mbaya niliacha simu yangu kule kwenye vitanda, nikashuka kuifuata, sikuikuta pale kitandani nilipokuwa nimelala, kabla sijapawa nikasikia sauti kutoka nyuma yangu;

“Unaitafuta hii?” Nikageuka nikakutana na moja ya wale wadada waliokuwa wanaogelea bwawani akiwa amenielekezea simu huku akinitazama kwa macho ya upendo wenye Haya,

“Yes, Nashukuru sana” Nikajibu nikiipokea,

“ Usijali, naitwa Daniella” Yule mdada mrembo akasema akiwa ananitazama akiachia tabasamu jepesi la kuomba urafiki.

“ Gibson”

“ Embu nisaidie namba zako hapa” Daniella akasema akinipa simu yake niandike namba zangu, hapo nikageuka nyuma kuangalia kwenye gari kuona kama shemeji ananiona, lakini sikumuona, nikachukua ile simu nikawa naandika namba zangu;

“Unamuogopa mkeo? Akaniuliza, nikiwa naandika namba kwenye simu yake.

“sina mke mimi..” nikajibu nikimkabidhi simu yake.

“Gibson unafanya nini?” Nikamsikia Shemeji akigomba kwa nguvu akiwa kwenye gari.

“ Nakuja shem”

“ Kwa heri tutawasiliana Daniella” Nikasema kwa haraka haraka nikaondoka nikimuacha Daniella akinitazama huku akitabasamu kama mtu aliyefanikisha jambo kubwa.

Tulimpitia mtoto na safari ya kurudi nyumbani ikaanza, shemeji alikuwa amelewa kabisa, alikuwa akipiga piga makelele, huku akitaka niongeze sauti ya muziki kwenye gari, alikuwa akinengua huku akibinua makalio yake alafu kuna wakati anashindwa kujihimili anaangukia kwenye usukani, nilikuwa nikimuondoa kwani alikuwa anahatarisha usalama wetu,

“Embu zimaa! Zima muziki huo, huzikii wewe” akawa anaongea kiulevi. Nikazima, akawa ananilazimisha niimbe;

“Niimbie basi, wewe si mwanamuziki, ile nyimbo yako tamu sana, penzi lako pipi filimbi, nailamba aamu! Aamu!” Akawa anaimba huku akionyesha vile anailamba pipi filimbi huku akinishika kwenye mapaja yangu.

“ Embu acha ujinga wako bhana, huoni kuna mtoto hapa, unafanya nini sasa?” Nilimsukuma na kumchapa kibao kimoja cha adabu.

“Umenipiga sio, unajifanya kidume sio” akatulia akawa anacheua macho yakiwa legelege, mwishowe akapitiwa na usingizi.

Simu yangu ikawa inaita, sauti ambayo ilikuwa kero, ilikuwa namba ngeni kabisa, nikajua huenda atakuwa Daniella, “siwezi kupokea simu ya Daniella nikiwa na shemeji” nikawaza, ikaita mpaka ikakata, kitambo kidogo ikaita tena, sikupokea tena mpaka ikakata, bado tulikuwa njiani tukirudi nyumbani, ikaita tena, kwa kweli nilianza kukereka,

“Pokea simu hiyo” Shemeji aliropoka akiwa kalala, nikamtazama alikuwa amechoka kweli.

“ Mama yako ulimuambia akupigie leo” Shemeji akasema akigeuza uso wake kwangu bila ya kuyafumbua macho yangu, “huenda itakuwa ni mama kweli” nikawaza, kabla sijapokea simu ikakata, nikasubiri tena ili apige lakini nikaona kimya, nikaona niipigie ile namba huku nikiwa nimepunguza sauti ili shemeji asisikie upande wa pili, ile simu ikaita kisha ikapokelewa, hapo nilikuwa nimepunguza mwendo wa gari.

“Hello, ooh! Sorry, amefika mbali, tafadhali muite mama yangu, sawa” nikawa nazungumza na mtu wa kwenye simu, mama alikuwa keshaondoka lakini alikuwa hajafika mbali, mwenye duka alikuwa anamuona, dakika moja mama akapewa simu, nikaweka simu loud,

“ Shikamoo Mama!”

“Marhaba mwanangu, yaani tumeipigia simu yako mpaka tukachoka mwanangu”

“Samahani mama, nilikuwa mbali na simu” nikasema lakini shemeji akaropoka na sauti lake la ulevi “Mbali hiyo kwiyoo” nikawahi kumziba mdomo na mkono,

“Huyo ni nani mwanangu?”

“Enhee! Aah! Achana naye, hapo kuna simu gani mama?”

“ Mwanangu mimi hata najua aina za simu basi, acha nimpe mwenye duka atakuambia”

“Sawa mama” Nikajibu, nikiwa namuachia mdomo shemeji.

“Hello mkuu!” Mwenye duka akasema,

“ ndio kiongozi, hapo kuna simu gani nzuri” nikasema, akawa anataja aina ya simu na bei zake.

“ Anhaa! Hapo si una huduma za uwakala wa pesa? Basi naomba umpe Mama yangu simu nzuri ya smartphone ya laki tatu, alafu unitajie namba za uwakala nikutumie pesa yako” nikasema, shemeji akaropoka; “Mwanaume gani unamnunulia mama yako simu ya laki tatu” nikamziba mdomo tena, “embu tulia bhana, pombe zinakuendesha vibaya wewe” nikasema, nikamuona shemeji akifungua macho yake alafu akaniangalia. Akanitoa mikono yangu mdomoni;

“Hivi Gibson unafikiri mimi ni mlevi nisiyejitambua kama wewe, nimeanza kunywa hizi pombe tangu mdogo, alinifundisha Mama yangu, usidhani zinaweza kuniondolea akili” akanitazama huku akilegeza macho yake, alafu akaendelea,

“Shika simu yangu hii mtumie mama milioni moja hapo ya simu alafu umtumie pesa nyingine ya matumizi”

“Hapana shemeji, nashukuru kwa kutaka kunisaidia ila naomba unisamehe kwa kukataa msaada wako” Nikasema.

“Embu acha ushamba wewe, utakufa masikini shauri yako, hii ni bahati tuu, usione najigonga gonga kwako ukadhani siku zote nitakuwa hivi, embu lete hizo namba za wakala alizokutumia” akachukua simu yangu muda huo kuna meseji iliyokuwa imeingia, akatuma milioni mbili, yule jamaa akapiga simu,

“Boss! Wewe ndio umetuma pesa yote hii?” akaniuliza yule muuza duka kwenye simu.

“Ndio mkuu, shilingi ngapi imefika?” Nikauliza.

“Mkuu, hujui umetuma kiasi gani?”

“Mpe mama simu nzuri ya gharama alfu hiyo pesa itakayobaki mpatie” Shemeji akaropoka.

“ Kwani umetuma shilingi ngapi” Nikamuuliza shemeji.

“Milioni mbili tuu!” Akajibu, Nikapigwa na butwaa, lakini akanizuia nisiseme lolote.

“Kiongozi, mpatie simu isiyozidi milioni moja, alafu hiyo pesa nyingine mpatie”

“Haya nitampatia ya laki saba Mkuu” akajibu.

“ Sawa, mpe mama niongee naye” nikasema huku nikimtazama Shemeji,

“Ndio mama, atakupa hapo simu nzuri pamoja na milioni moja na laki tatu”

“Unasemaje Gibson?” Mama akauliza kwa kustaajabu.

“ Hiyo pesa utaanza kuikarabati nyumba pale ilipodondoka, usiwe na wasiwasi mama”

“Ubarikiwe mwanangu, kwani huko mjini unafanya shughuli gani mwanangu, hii pesa ni nyingi sana”

“Usijali mama, wewe tumia pesa za mwanao, tutawasiliana jioni” simu ikakatika.

‘ Ungemjibu shughuli uifanyayo mjini ni kumfurahisha shemeji yako, hahaha!” Shemeji akasema alafu akaachia kicheko cha kishambenga.

“Hivi kwa nini umetoa pesa yote hiyo?” Nikamuuliza.

“Mwanaume unaogopa kuhongwa na mwanamke, hahah! Unaogopa kuolewa?” shemeji akasema, wala sikumjibu nikawa naendesha gari.

“ Utachagua kuolewa na mwanaume mwenzako au kuolewa na mwanamke ambaye ni mimi, kwanza kuishi tuu kwenye nyumba ya mwanaume mwenzako huoni aibu, huko sio ndio kuolewa kwenyewe, sikiliza Gibson, wewe ni kijana mzuri nawe unastahili maisha mazuti kama aliyonayo Riadi, kuwa chini ya mwanaume mwenzako kama mke wake haipendezi, ni afadhali uwe chini yangu utapata chochote na ninaweza baadaye kukuzawadia mtoto”

“Embu tulia bhana! Mtoto yupo hapa ujue, hivi unamfundisha nini mtoto?” nikamkatisha.

“Mtoto ni wewe usiyeelewa mambo madogo, mwanangu mwenyewe anakushinda akili, si ati Junior?” akageuka siti za nyuma na kumtazama mtoto wake, Kupitia kioo cha gari kilichojuu ya mule ndani nikamuona Junior akitabasamu.

“Mimi sijaolewa na mtu, naomba tuheshimiane, kama huwezi kujiheshimu jaribu kuheshimu wengine” Nikasema,

“Hakuna cha bure Gibson, mtu yeyote mwenye akili anajua kila jambo lazima ulipie, iwe pesa au nguvu au ulipie kwa namna yoyote, hiyo ndio heshima, sijui unaposema unataka uheshimiwe unazungumzia jambo gani, ulitaka nikuambie uongo; mwanamke anaolewa sio kwa sababu ya kuwa yeye ni mwanamke isipokuwa kutokana na kutokuwa na mali, wakati mwingine kutokuwa na akili ya kutosha kumuongoza mwanaume, lakini kama mwanaume hana mali na akili pia naye ataolewa tuu. Lakini kwani lipi baya hapo, hutaki kuolewa na mwanamke mzuri kama mimi Gibson” Akasema, mwanzoni nilijua pombe zilikuwa zimemzidi lakini kumbe haikuwa hivyo, aliweza kuzitawala.

“ Mimi natafuta mali kwa jasho langu, sitaki pesa za kupewa pewa kama mtoto mdogo”

“ Hahah! Wacha weeh! Unafikiri hautazitolea jasho hizo pesa nilizompa mama yako? “ Hapo tukatazamana,

“Gibson! Unabahati sana, mimi sina huruma lakini sijui kwa nini umenigeuza kuwa kama kondoo, wewe ndio mtu wa pili baada ya Mume wangu, Riadi kumuonea huruma, nilitokea kukupenda tangu siku ya kwanza niliyokuona pale getini, ndio maana mpaka sasa hivi tupo pamoja” Akasema.

“Embu acha hizo habari, elewa wewe ni shemeji yangu, na itabaki hivyo siku zote, hakuna kitakachoendelea kati yangu na wewe, sawa” nikasema nikikatisha kwenye Geti la nyumba yetu lililokuwa linateleza polepole, tulikuwa tumefika nyumbani, tukashuka, lakini Shemeji hakuweza kushuka kutokana na pombe,

“ Shuka! Si ulisema pombe umekunywa tangu ukiwa mdogo, mbona hushuki sasa?”

“Nashuka” akashuka lakini akawa anapepesuka kidogo aanguke, nikamdaka, tukawa tunatazamana uso wangu ukiwa juu alafu wake ukiwa chini, akatabasamu, nilisikia mapigo yake ya moyo yakipiga, joto lake lilikuwa nyuzi joto za kulifanya yai la kuku lianguliwe, tukatazamana kwa kitambo mpaka niliposikia sauti ya mtoto;

“ Mama, Baba amekuja” Nilishtuka kusikia mtoto akisema hivyo, nikajinasua mikononi mwa Shemeji yangu, nikihaha kwa kuangalia huku na huku, lakini sikuweza kumuona Riadi, akili yangu ikaniambia tazama juu ya ghorofa, sikuamini niliyemuona, moyo wangu ni kama ulipigwa shoti ya umeme, nilimuona Riadi akiwa juu ghorofani amesimama akiwa ameshika kingo za ghorofa akiwa anatutazama mimi na shemeji, nilihisi kama mtu aliyefumaniwa.

ITAENDELEA

Shukrani Mkuu
 
Gibson ni mti unatoa maua Sana lakini naona hazai matunda [emoji1787][emoji1787][emoji1787] shukran Sana mkuu
 
Kaburi la mwanamuzi (episode 04)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

EPISODE 04
ILIPOISHIA

Nikalala, kwa kweli nilikuwa nimechoka siku ile, nilitaka niipe akili yangu utulivu ili kesho nikianza kazi niwe nautulivu wa akili. Kesho ilipofika asubuhi asubuhi niliingia ndani ya gari yangu, dakika chache nilikuwa nimeifikia barabara ya Bagamoyo nikitokea Goba, nikakata kulia kufuata upande wa Mjini, dakika chache nilijikuta nipo Mwenge kwenye mataa, “ Nitaanzia hii Sinza” Nikakata upande wa kulia kuelekea ubungo, hapo nikawa naangalia huku na huku nikiwa ndani ya gari lakini kwa uzoefu wangu jijini Dar sikutegemea kama ningeona hiyo Carwash, dakika saba hivi nilikuwa nipo kwenye Mzunguko wa barabara wa pale Mlimani City, nikakata kushoto na kupokelewa na Katalunya, nikaifuata ile njia polepole ielekeayo Meeda, hapo nikaona Gereji bubu moja, nikasimamisha gari kisha nikamuita kijana mmoja pale, nikamuuliza anaijua gereji yenye nembo ya kichwa na ng’ombe akasema haijui, akasisitiza jina la hiyo gereji nikajitahidi kumwambia imenitoka, kisha nikamuuliza kuhusu Carwash, pia akasema haijui, Baada ya kuuliza watu watano sita katika mitaa yote ya sinza bila mafanikio muda ukawa umeenda nikaamua kwenda kunywa supu kwani tumbo tayari lilikuwa linadai haki yake.

ENDELEA

Baada ya kupata kifungua kinywa, nikaondoka kuelekea njia ya ubungo nikitokea Sinza Madukani, nikakata mkono wa kulia nikiiacha barabara ya shekilango na kuchukua uelekeo wa Ubungo wa mawasiliano, mbele kidogo nikashtuka nilipoona bango lenye nembo ya kichwa cha ng’ombe alafu chini yale yalisomeka maandishi “ Bull Garage” nilifurahi sana kuiona gereji hii, kwangu nilihesabu kama mafanikio ya mapema kabisa, nikaliegesha gari pembeni ya barabara mbele ya ile gereji kisha nikamuita kijana mmoja aliyekuwa pale akiziba pancha tairi.

“ Habari yako ndugu yangu? Nikamsalimu.

“ Salama kabisa Kaka, karibu sana” akajibu.

“ Ahsanate sana” Nikajibu nikiwa nimetulia nikitazama lile bango kisha nikamtazama usoni yule kijana.

“ Karibu kaka, unahitaji huduma gani, karibu kuwa huru” Yule kijana wa gereji ambaye bila shaka alikuwa fundi akanichangamkia kwa ukarimu sana,

“ Ahsante sana, sijui nitakuwa nimekosea, au nimechanganya!” Nikawa nazungumza mwenyewe, nikiwa natafakari.

“ Umekosea nini Bro! Ulikuwa unahitaji nini?”

‘ Samahani sana Ndugu yangu nilisoma vibaya, nilijua hii ni Bull Carwash, kumbe ni Garage” Nikasema nikiwa namtazama usoni kwa udadisi.

“ Hapana Kaka, hii ni Garage tuu wala sio Carwash, itakuwa umechanganya kama ulivyosema?” akasema. “ Hii sasa kasheshe, nilidhani kazi itakuwa rahisi sana lakini kumbe sivyo” nikawaza.

“ Lakini kaka, kama unahitaji Carwash kwa ajili ya gari yako, kuna ile pale, nayo wanatoa huduma nzuri tuu” Yule kijana fundi akasema akionyesha kujali na kutaka kunisaidia.

“ Nashukuru sana ndugu yangu,” Hapo nikamshukuru nikatia gia na kuondoka mdogomdogo, kabla sijafika mbali nikasikia sauti kutokea nyuma ya gari ikiita;

“ Broo! Kaka! Subiri” Nikamuona yule kijana akilikimbiza gari langu Kupitia vioo vya pembeni vya gari, nikapunguza mwendo, akanifikia, “Kaka, fundi anasema anapajua” na kabla hajamaliza kuzungumza akaja mwanaume mmoja mweusi aliyenyoa kipara, “ Habari Mkuu” akanisalimu,

“Nzuri kaka!” nikajibu.

“ Ulikuwa unataka ni..ni..” akasema, akiwa anasitasita kumalizia.

“ Nilifikiri Gereji yenu ni Carwash ya iitwayo Bull Carwash,” Nikasema.

“ Hii Gereji ns hiyo Carwash uliyoitaja ni kaka na mdogo wake, hii inamilikiwa na mdogo mtu na hiyo Carwash uliyoitaja inamilikiwa na kaka mtu, Bull Garage ziko mbili tuu hapa Dar, nyingine iko Kariakoo ambayo ndio kubwa, sisi hapa ni kama mafundi tuu” Yule mwanaume akasema, kwa kweli nilifurahishwa na namna alivyokuwa anajieleza, alikuwa anaongea hata mambo ambayo sikuwa nahitaji kumuuliza, lakini maelezo yake yalijikita kuielezea zaidi Bull Garage wakati mimi nilikuwa nahitaji kujua habari za Bull Carwash. Nikajikuta nikimuuliza;

“ Kutoka hapa ni Bull Carwash ipi iliyokaribu?”

“ Bull Carwash ipo moja mkuu, kwani kuna nyingine tena unayoijua?” akanitupia swali, kwa kweli swali lake nilijikuta nikipandwa na nyongo, zikulipenda, hata hivyo nilijizuia asigundue chochote kilichokuwa kinaendelea katika akili yangu.

“ Ni kwa sababu umesema Bull Garage zipo nyingi ndio maana nikajua hata Bull Carwash nazo zipo nyingi” Nikasema nikimtazama.

“ Hamna, ipo moja maeneo ya msasani kule, kabla hujafika Msasani macho upande wa kushoto utakuta Kituo cha mafuta ya magari, nyuma ya kituo hicho ndio ipo hiyo Bull Carwash, wala hupotei kwa sababu ipo njiani, alafu mwenye hicho kitu cha mafuta ndiye Baba wa hawa watoto” akasema, kwa kweli maelezo yale niliyafurahia sana, kama ningekuwa na zawadi ningempatia, basi nikawashukuru na kuondoka, safari ya kuelekea Msasani ikaanza,

“Watanzania ni waongeaji sana hii, wanapenda kuongeaongea hata na watu wasiowajua vizuri, hii hufanya kazi kuwa rahisi kwa wapelelezi kupata data muhimu kwa urahisi pasipo hata kutumia nguvu wala pesa, watanzania wanaweza kumuelekeza mtu wasiyemjua mahali popote bila hata ya wasiwasi, wasijue kwa kufanya hivyo inaweza kuwa hatari kwa usalama wa baadhi ya raia, huwezi muelekeza mtu usiyemjua mahali unapopajua, labda umuelekeze ofisi za serikali za mitaa au mjumbe au kituo cha polisi ili akapewe maelekezo. Lakini kutokana na upendo na ukarimu wa watanzania ndio hufanya hivyo pasipo kujua uhatari wa jambo hilo” Nikawa nawaza nikiwa nakatiza eneo la bamaga nikiifuata njia ielekeayo makumbusho.

Haikuchukua nusu saa nilikuwa nimesimama mbele ya kitu cha kujazia mafuta kama nilivyoelekezwa, nikaiona njia ya vumbi iingiayo ndani, nikaifuata, sikutembea hata sekunde kumi nikapokelewa na bango kubwa lililokuwa limeandikwa Bull Carwash yenye nembo ya kichwa cha ng’ombe dume mwenye mapembe. Nikaegesha gari, akaja kijana mmoja aliyevalia overall la rangi ya bluu, nikampa malekezo, nikamuachia funguo ya gari nikaondoka kurudi kwenye kile kitu cha mafuta, Nilipofika nikaona magari kadhaa yakiwa yanajazwa mafuta, wahuduma wa kike na wakiume wa kituo kile wakiendelea na shughuli, sasa nilikuwa nikiangalia mfanyakazi ambaye amekaa kizembe zembe bila ya kazi nimfuate ili nikaongee naye. Nikamuona Dada mmoja aliyekwenye sare ya kazi ya kile kituo akiwa anaurudisha mpira wa kujazia mafuta baada ya kumaliza kujaza gari Fulani lililokuwa linaondoka, kwa upesi nikamfuata,

“Mambo Dada” Nikamsabahi. Akanitazama kwa macho ya udadisi, pasipo kunijibu kitu.

“ Pole na kazi Dada mrembo” Nikaongeza.

“ Ahsante! Ndio majukumu” Akajibu huku akitabasamu. Nilijua kuwa hakuna asiyependa kusifiwa, nilijua kilichomfanaya atabasamu ni vile nilivyomuita Dada Mrembo. Saikolojia ya wanawake inasema kuwa ndio viumbe ambao wanapenda sifa kuliko hata kula. Hilo nilikubaliana nalo.

“ Naitwa Peter, nilikuwa namuulizia Osman” Nikasema.

“ Osman! Kwani karudi kutoka Qatar?” Akaniuliza.

“ Kwa kweli hata mimi sifahamu” Nikasema.

“ Mmmh! Kwani unashida gani naye?” akaniuliza, nikamuangalia kwa kumkazia macho kidogo alafu nikatabasamu.

“ Aha! Sorry usijeniita mbeya bure, haha! Labda ungeenda nyumbani kwake ukaulize, hapa hajafika hii ni wiki ya pili, na anakujaga mara mojamoja” Yule Dada akasema,

“ Mimi ni mfanyabiashara wa vipuri vya magari, nimeelekezwa kwake, aliyenielekeza aliniambia nifike hapa lazima nitampata, sasa kumbe hapa napo anakujaga kwa nadra tena!” Nikasema nikipima ufahamu wa yule dada, nikaona tayari kaingia kwenye nyavu zangu.

“ Sasa kwake itakuwa ni wapi? Nikauliza nikimtazama, hapo nikamuona kijana mmoja aliyevalia sare za kile kituo akija, nikajua huyu anaenda kuniharibia mipango yangu,

“ Mimi sijui, ati Boss anaishi wapi?” Yule Dada akamuuliza yule kijana aliyekuwa ameshafika karibu yetu. Sikupendezwa na ujio wake, wala sikutaka ashirikishwe katika mazungumzo yetu, ni vile nilishindwa kumzuia. Tukasalimiana na yule kijana kisha akaendelea;

“ Unamhitaji Boss?” Akaniuliza

“ Ndio” nikasema, akawa ananidadisi kuanzia juu mpaka chini, sikupenda vile alivyokuwa akinikagua,

“ Mimi nafikiri hata huyu hajui, si unaona anavyoshangaa!”Nikasema, lakini yule kijana mjaza mafuta akanikatisha; “ Unauhakika sipajui” “ kama ungekuwa unapajua usingenishangaa namna hiyo” nikasema.

“ Kwani unashida naye gqni?” Nimeshamueleza huyu Dada ndugu, akamgeukia yule dada, kisha yule dada akawa anamuelezea.

“ Kuna duka kule kariakoo,nila mtoto wake, anauza pia vipuri, boss yeye anahusika zaidi na magari zaidi” akasema,

“ Nimetoka huko kuulizia kipuri Fulani, ndio nimeelekezwa kwa mzee mwenyewe anaweza kuniagizia nje ya nchi” Nikasema.

“ Anhaa! Sawa, nenda mpaka Mbezi beach, ukishapita kituo cha shule, ulizia mtu anayeitwa Osman midevu, hapo utampata” yule kijana akaeleza kwa kina, nikawashukuru nikaondoka. Tayari walikuwa wameshamaliza kuosha gari langu, nikalichukua na safari ya mbezi beach ikaanza.

Muda mchache kupita nilikuwa maeneo ya mbezi shule, ikiwa tayari imetimu saa tisa za mchana, niliingia katika mgahawa mmoja na kupata chakula, baada ya kupato mlo nikatoka nikiwa nimeliacha gari langue neo la mgahawa huo, nikatembea kama dakika kumi hivi nikielekea upande wa bagamoyo, hapo nikakuta kijiwe cha bajaji na bodaboda,

“ Kwema ndugu zangu, poleni na majukumu” Nikawasalimu, wakawa kila mmoja akiidakia salamu yangu na kunishawishi nichukue usafiri wake, nikachukua bodaboda, “Nipeleke kwa Osman Midevu” nikamuambia, akanitajia bei, basi tulipokubaliana safari ya kuelekea kwa osman midevu ikaanza, tuliingia ndani kidogo tukawa tunachochola na baada ya dakika kama saba hivi dereva bodaboda akaniuliza; Unashukia palepale kwa Osman Midevu au?” “ mbele kidogo boss” Nikamjibu. “unaenda kwenye ile shule ya English medium?” akaniuliza, “ Haswaa!” Nikajibu.

“ sasa si ungesema tuu shule ya Little Star” akasema,

“ Aliyenielekeza ndiye alivyonambia hivyo, anasema shule hiyo sio maarufu ukilinganisha na Osman Midevu” Nikasema.

“ Ila kweli, kama dereva sio mzoefu wa huku anaweza asipajue, ila Osman midevu ni maarufu mitaa hii, hili ndilo jumba la huyo Osman midevu ulipopataja, unapajua” akasema, nikajibu; Hapana, nikawa napaangalia tukipapita mpaka pikipiki iliposimama mbele kidogo kama hatua hasmini hivi, tulikuwa tumefika shule ya little star, akaondoka na kuniacha mwenyewe.

Nikasogea mpaka kwenye mti kwenye kivuli, nikawa nafanya usaili katika jumba la Osman ambaye sasa niliongezewa utambulisho wake akiwa anaitwa Osman midevu, mazingira ya eneo lile yalikuwa tulivu yenye nyumba zenye uzio, wakazi wa mtaa huu wengi wao walikuwa na vipato vya juu kutokana na aina ya nyumba za kisasa zilizokuwa eneo lile, kuta na mageti ya gharama zilizidi kunipa ujumbe kuwa wenyeji wa mtaa huo walikuwa vibopa walio ya bahatisha maisha, palikuwa pana utulivu, na mtu mmoja mmoja ndiye ungemuona akitembea. Juu ya uzio wa Osman midevu ulikuwepo ulinzi mkali wa nyaya maalum za umeme. Kupita katika uzio ule ingehitajika akili ya juu zaidi kuliko waliobuni mfumo huo wa ulinzi, ndani yake niliona ghorofa moja iliyochomoza, iliyozingirwa na miti mingi, ni kusema ilikuwa nyumba ya ghorofa ya kisasa kabisa iliyozungukwa na uzio thabiti na kupambwa na miti na maua ya aina yake.

Yakapita magari mawili, kisha watembea kwa miguu kadhaa, nikaona kama wataanza kunitilia shaka, nikaondoka, nilitembea kwa dakika kama tano hivi kwa bahati nzuri ikapita bodaboda, nikaiita kisha nikamuaigiza dereva anipeleke Mbezi shule kituoni, akanifikisha, nikarejea kwenye ule mgahawa kwa mguu kuchukua gari langu, sasa nilisema nitarudi kwa Osman nikiwa na gari, nikarudi kwa osman na kuegesha gari mbali kidogo na geti la nyumba ya Osman. Kutokana na gari langu kuwa na vioo vya tinted ingekuwa sio rahisi kwa mtu kuniona, sasa nilianza kuchora taswira ya Osman, nilimchora kama mwanaume wa makamo, mweupe, mwenye ndevu nyingi, labda na upara hivi, mrefu wa wastani mwenye mwili wa kawaida, hivyo ndivyo nilivyomchora kwenye mawazo yangu, hiyo inaitwa schema tamka skima, ambayo ni kuwa na taswira ya kitu au mahali au mtu ambaye bado hujawahi kuonana naye. Schema katika shughuli za upelelezi hasa kwa mtu ambaye hujawahi kumuona ni muhimu sana ingawaje haupaswi kuipa asilimia miamoja.

Masaa yalikimbia na giza likaingia nikiwa bado nipo palepale, nikiwa nimeliegesha gari huku nikiwa ndani yake, sikumbuki ni muda gani usingizi ulinipitia lakini nilishtushwa na mwanga mkali ulionifanya niamke, lilikuwa ni gari lilokuwa linakuja mbele yangu likiwa linamulika huku likija polepole, nikamuwashia taa na kumpa ishara apunguze mwanga, naye akafanya vivyo hivyo, niliangalia saa yangu ya mkononi ikanipa majibu kuwa ni saa nne na madakika, “ Muda umekimbia sana” Nikawaza. Lile gari lilikuwa limeshanipita, nikamkumbuka Mr. Kibadeni, nikampigia simu;

“ Hello Mkuu, Kwema, wapi, heeh! Usiniambie, haiwezekani, hiyo inawezaje kutokea Mr. Kibadeni? Kwa hiyo kwa sasa upo wapi, sawa nakuja” Nilikata simu na kuwasha garai na kuondoka haraka sana. Taarifa aliyonipa Mr. Kibadeni ilinichanganya sana.

“Hii inawezekana vipi, ndio kwanza tumeingia jana, nani yupo nyuma ya jambo hili” Nikawa nawaza. Dakika chache nilishakuwa nimeipata baraabara ya bagamoyo nikafuata upande wa mwenge, Nikiwa naendesha gari punde simu ikaita tena, alikuwa ni Mr. Kibadeni, nikaweka loud kisha nikamsikia Mr. Kibadeni akiongea akiwa na wasiwasi mwingi.

“ Peter Mirambo, wananifukuza, wananikimbiza Peter wapo nyuma yangu, hapa nakaribia mbezi mwisho nawakimbia”

“ Nipo nyuma yako nakuja, nipo mwenge Kibadeni, endelea kuwazuga nakuja” nikasema nikimpa moyo na kuongeza mwendokasi wa gari nikivunja sheria nyingi za barabarani.

“Sawa Pm, wananifukuza na magari mawili hivi, hapa nashindwa nirudi na njia ipi hakuna U-turn eneo hili” Mr. Kibadeni akasema,

“ Endelea kuendesha hivyohivyo Mkuu, wakazie muda mfupi nitakuwa hapo” nikasema kisha sismu ikakatika. Nikaongeza mwendo nikiitafuta Ubungo mataa, kwakweli ile foleni haikuwa inanifurahisha, niliona kama inanichelewesha kuokoa maisha ya Mr. Kibadeni, kwa jinsi alivyokuwa akiongea Mr. Kibadeni ni wazi kuwa alikuwa kazidiwa, licha ya kuwa ni Jasusi mbobevu mbali na fani yake ya uanasheria na cheo chake cha Ujaji lakini hiyo haikuficha hofu yake dhidi ya wale waliokuwa wakimkimbiza, nilichora picha kuwa huenda wanaomfukuza wakawa watu wenye uwezo wa juu sana. Hilo kwangu lisingeweza kunipa shida lakini kilichonipa mashaka makubwa ni siri ya kutoka ya misheni yetu ya siri ya Operation Tornado, “ Yaani ndio tumefika jana tuu tukitokea Marekani, hata hayajaisha masaa arobaini na nane, hata hatujaianza kazi lakini siri imejulikana” Nikawaza, kwa kweli hii iliniogopesha mno, tena sana kuliko kawaida.

Tayari nilishakuwa ninavuka maeneo ya Kimara Baruti sasa nikitumia barabara ya mwendokasi name nikiwa kasi, nisingeweza kutumia barabara ya kawaida kwani ningepooteza muda mwingi njiani, muda mchache nilikuwa namalizikia Mbezi kwa Msuguri hapo simu ikaita tena, alikuwa ni Mr. Kibadeni, nikapunguza mwendo kidogo, kisha nikaipokea na kuweka loud;

“ Upo wapi Kaka, wananikaribia hawa wajinga” Alisema akiwa mwingi wa wasiwasi.

“ Nipo Kwa Msuguri, Wewe upo wapi?” Nipo huku Tegeta A njia inayoelekea Goba Mpakani Kaka” Akasema, lakini nikasikia kishindo kama gari lake likiwa limegongwa kwa nyuma, nafikiri simu yake ilidondoka, nikawa naita lakini akawa hajibu isipokuwa nikawa nasikia mngurumo wa gari. Hapo nikaongeza mwendo, dakika chache nikakata mkono wa kulia barabara ielekeayo Goba, niliendesha kama mwendawazimu, wakati Fulani kuna madereva tulikosana kosana kugongana nikawa nawasikia wakiniachia matusi lakini wala sikuwa najali, nilichokuwa najali ni maisha ya Mr. Kibadeni, Dakika tatu zilitosha kabisa kunifikisha kwenye barabara ielekeayo Goba Mpakani, nikakata kushoto ambapo kulikuwa na barabara ya vumbi eneo hilo linafahamika kama Kituo kidogo cha daladala kiitwacho Tegeta A,

Ile simu ilikuwa imekatika, nikaendesha zaidi na zaidi hofu ikizidi kunishika huku nikianza kuhisi joto licha ya kiyoyozi kilichokuwa mule ndani ya gari, niliendesha kwa dakika tano hivi mbele yangu nikaliona gari likiwa lipo pembeni ya baarabara, nikasimamisha gari langu mbele ya lile gari, nikashuka nikiwa nimeshika bastola mkononi, eneo lile lilikuwa na nyumba moja moja zilizoachana pakiwa na vichaka na giza likiwa na umiliki kwa sehemu kubwa, lilikuwa gari la Mr. Kibadeni, nikaangaza macho yangu huku na huko lakini sikuweza kuona kitu, nikalisogelea lile gari huku mapigo yangu ya moyo yakienda kasi kadiri nilivyokuwa nalikaribia. Nikashika kitasa cha mlango wa lile gari, nikafungua, hapakuwa na mtu, nikatoa kalamu yangu ambayo pia ilikuwa ni tochi nikamulika kulikagua, sikuona jambo lolote la maana, nikaingia ndani kabisa nikiwa namulika mulika, bado sikuona jambo la maana, nikawa najiuliza; “Kibadeni ametoroka au amekamatwa na hawa mabaradhuli” kwa kweli nilichanganyikiwa, nikatoka nje nikalizunguka lile gari, nikona likiwa limepondeka upande wa ubavu wa kushoto, na taa ya nyuma ikiwa imepasuka, nikamulika mulika chini nikashtuka kuona saa, nikainama kuikota, ilikuwa smartwatch maalum ya kidigitali, nikaibonyeza bonyeza, nikakuta sehemu ya audio ambapo imerekodiwa muda mchache uliopita.

“ Kaka wanakaribia kunidhibiti, ila nimevaa mkanda wa suruali ambao una-gps, hiyo saa utaiunganisha na simu yako Kupitia Bluetooth itakupa uelekeo waliponipeleka” Ilikuwa ni rekodi kutoka kwenye ile saa. Haraka haraka nikarudi ndani ya gari langu nikiwa nimebeba ile saa.

ITAENDELEA KESHO SAA 7mchana
 
Mkuu shukran sana hapa naona Mambo yanogile
 
KABURI LA MWANAMUZIKI (Episode 05)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300

EPISODE 05
ILIPOISHIA

Kibadeni ametoroka au amekamatwa na hawa mabaradhuli” kwa kweli nilichanganyikiwa, nikatoka nje nikalizunguka lile gari, nikona likiwa limepondeka upande wa ubavu wa kushoto, na taa ya nyuma ikiwa imepasuka, nikamulika mulika chini nikashtuka kuona saa, nikainama kuikota, ilikuwa smartwatch maalum ya kidigitali, nikaibonyeza bonyeza, nikakuta sehemu ya audio ambapo imerekodiwa muda mchache uliopita.

“ Kaka wanakaribia kunidhibiti, ila nimevaa mkanda wa suruali ambao una-gps, hiyo saa utaiunganisha na simu yako Kupitia Bluetooth itakupa uelekeo waliponipeleka” Ilikuwa ni rekodi kutoka kwenye ile saa. Haraka haraka nikarudi ndani ya gari langu nikiwa nimebeba ile saa maalumu ya kijasusi.

ENDELEA.....
Nilipoiunganisha kwenye simu, nikabonyeza app maalum ya simu ambayo ingeunganishwa na Gps. Ikawa inazunguka tuu ikitafuta position, punde nikaona kwenye simu yangu ramani kama ya ‘google map’ alafu kuna kiduara cha rangi nyekundu kinatembea polepole kufuata barabara zilizokuwa kwenye ile ramani, nikajua kile kiduara ndicho ninapaswa kukifuata, nikawasha gari kisha nikaiweka ile simu mbele juu ya usukani, nikaondoka nikiwa nimeliacha gari la Mr. Kibadeni pale. Sikuwahi kupita njia ile tangu hivyo niliendesha kwa kasi nikiwa na tahadhari zote, Dakika tano nilikuwa nimeshafika mbali sana lakini kile kiduara kilikuwa mbali zaidi tokea pale nilipokuwa, nilienda nikakuta barabara mbili kama kipanda cha mti, hapo nilitakiwa nichague njia moja, nikaangalia kwenye kile kiduara chekundu kwa upesi nikaanza kuifuata njia hiyo mpaka pale nilipo, hii ni sehemu ya kozi nilizofundisha nikiwa mafunzoni kujifunza ujasusi, unapewa picha yenye Bomba ya maaji, alafu kuna kuwa na ndoo za maji zilizopewa majina labda, B1, B2, B3, B4 kisha chini kuna kuwa na mipira mingi ya maji iliyojifungafunga, unaulizwa je ni ndoo ipi itaijazwa maji, nafikiri ulishawahi kuona michezo ya namna hiyo, hiyo michezo ni chemsha bongo ambazo wengi huziona za kitoto lakini kweenye shughuli za kipelelezi huwaga zinatumika, hivyo ilipasa kujua ni barabara ipi ni sahihi ya kupita ili niweze kuwafikia wakina Kibadeni ambao nawaona kama kiduara chekundu kwenye simu yangu.

Nikachukua barabara ya upande wa kulia, nikatembea, nikawa kama nazunguka kurudi nilipotoka, hii iliniambia kuwa walikuwa wanarudi upande wa Goba, Nikasonga na kusonga mpaka nilipoikuta barabara ya lami, upande wa kulia ingenipeleka mbezi mwisho, upande wa kushoto ingenifikisha Goba mpaka mbezi beach,. Simu yangu ilikuwa inanielekeza kuwa walikuwa wapo Goba wakiitafuta Mbezi njia panda ya Goba, bagamoyo Road, nikaongeza kasi zaidi tayari usiku ulikuwa dhahiri, hivyo msongamano wa magari haukuwa mkubwa sana, hii ilinirahisishia kuchanja mbuga, kila nilipokuwa nasonga ndivyo nilivyokuwa nakikaribia kila kiduara chekundu, nikaona kile kiduara kikikatisha upande kushoto kufuata upande wa bagamoyo, nikaongeza kasi ya gari mpaka niliopishana nao wakawa wanashangaa, kitambo kidogo nikawa nimeifikia njia ya Bagamoyo sasa sikuwa mbali na kile kiduara ingawaje sikuwa naona magari yao. Nafikiri walikuwa hawajui kuna mtu anawafuatilia na hilo kwao wangeliita kosa kubwa, kama wangekuwa wanajua kuna mtu anayewafuatilia basi wasingekuwa wanatembea kwa mwendo wa kawaida kama ule, name ingeniwia vigumu kuwapata, hesabu zangu ziliniambia wapo maeneo ya Tegeta kwa ndevu, punde nikashtuka kuona kile kiduara chekundu kikiwa kimesimama pasipo kutembea, “itakuwa wamefika” nikawaza, “lakini vipi kama wamemshtukia kuwa anakifaa cha kutoa taarifa popote alipo” nikawaza nikiwa na wasiwasi na wazo hili, nikatembea mpaka pale Tegeta kwa ndevu, mahali ambapo kile kiduara kilikuwa kimesimama, bado kulikuwa na watu wachache wakiuza matunda na mishikaki, nikaweka gari pembeni, nikasoma eneo lote nikaona hakuna hatari yoyote, bado simu yangu ilionyesha kile kiduara chekundu kipo eneo lilelile,nikashuka nikaenda kwa muuza matunda, nikachukua kipande cha tikiti, nikawa nakula huku nikimuuliza yule muuza matunda,

“ Umeona gari mbili hapa muda mchache uliopita?”

“ Bro! Hapa magari ni mengi yanapita, si unajua hii ni barabara” Akanijibu, majibu yake yalinifanya nijione nimeuliza swali la kijinga kupata kutokea.

“ Sijui niliwekaje hili swali, anyway nipe machungwa ya elfu tatu, embe la buku, alafu ukate na hili ninalokula” Nikasema, lakini wakati ananiweka hivyo, akakumbuka kitu,

“Bro! Usijekuwa ukawa unazungumzia gari moja lililokuwa limepaki hapa na jingine lilikuwa limepaki pale ulipoegesha gari lako” akasema.

“ Nafikiri ni hayohayo”

“ Tena lile gari la nyuma walitupa mkanda, akauchukua yule mtu wa mishikaki” Muuza matunda akasema, maelezo yake yalinifanya nipaliwe, kitendo cha kusikia mkanda kiliizungua akili yangu, kwa kweli nilipoteza utulivu.

“ Uko wapi huo mkanda?’ Nikauliza.

“ Oya J, ule mkanda upo wapi?” Muuza matunda akasema, Kijana mmoja aliyekuwa anauza mishikaki akauleta ule mkanda, nikatoa noti mbili za elfu tano, nikawapa kila mmoja wao,

“ Wameelekea wapi?’ Nikawauliza,

“ Walinyooka moja kwa moja” Muuza matunda akasema, lakini akakatishwa na J muuza mishkaki.

“ Hamna walikatisha barabara ile pale, alafu walikuwa wamesimama pale kwenye lile duka la vinywaji dakika tano zilizopita wakati wewe ukiongea na huyu”

“ Yalikuwa yanafananaje hayo magari isijekuwa sio yenyewe?” nikamuuliza muuza mishikaki.

“ Moja ni Land Cruisser Vx ya rangi ya kijivu yenye giza, nyingine ilikuwa ni Hilux pickup Nyeusi, zote zilikuwa tinted” Akasema akiwa ananiangalia usoni kama mtu aniulizaye ndio yenyewe, hapa tayari walikuwa na pesa yangu zile elfu tano tano hivyo kivyovyote niliwaona wakiombea yawe ndio yenyewe.

“ Ndio hayohayo” Nikasema,

Kusikia hivyo sikutaka kupoteza muda, nikawaacha na kupanda kwenye gari, nikakatisha na kuifuata njia ya vumbi niliyokuwa nimeelekezwa na wale vijana, niliendesha mwendo wa kawaida kwani ilikuwa ni mtaani, bado walikuwepo wapitanjia mmoja mmoja, baada ya kuendesha kwa dakika tatu, nikapunguza mwendo na kumsimamisha mzee mmoja aliyekuwa anakuja mbele yangu,

“ Samahani Baba yangu, umeona magari mawili, Moja ni Cruisser ya rangi kijivu, na pickup nyeusi?”

“ marhaba mjukuu wangu, hayo magari yamepita muda mfupi tuu uliopita wala hayapo mbali, kwani kuna tatizo?” Akanitupia swali,

“Hakuna, ni wenzangu wameliniacha hapo barabarani alafu mimi mgeni wakaniambia sitapotea” Nikasema, nikiwa ninaondoka polepole, nikiacha yule mzee akiniangalia kwa uso wa kutoridhishwa, “ Mzee punguza umbeya” Nikajisemea kwa sauti ya chini, nikaongeza mwendo lakini kabla sijamaliza dakika moja kwa mbali nikaona taa za magari mawili yakiwa yanaenda uelekeo ninaoenda.

“ watakuwa ndio wenyewe” nikawaza, hapa nikiwa nimeongeza umakini wasijue kuwa kuna mtu anayewafuatilia, tulienda kwa dakika tatu zingine kisha nikawaona wakikatisha upande wa kulia, kadiri tulivyokuwa tunasonga ndivyo tulivyokuwa tunaachana na msongamano wa makazi mengi, sasa tulifika sehemu yenye maeneo mengi ambayo bado yalikuwa hayajajengwa, huku maeneo mengine yakiwa ni mapagala ambayo hayajaisha, hatimaye tulifika kwenye eneo ambalo lilikuwa na ukuta mrefu hivi ambao umejengwa na matofali ya block, urefu wake ulikuwa kama heka moja hivi, nikaona yale magari yakisimama kwenye geti la ule ukuta, kisha ile Crusser ikaingia alafu Hilux pickup ikafuatia, Nikaliingiza gari kwenye vichaka kulihifadhi alafu nikashuka, muda wa kazi ulikuwa umefika. Nikashika mahali ninapoweka bastola yangu, kisha nikaitoa na kuishika mkononi, nikauzunguka ule ukuta, wala haukuwa na ulinzi wowote kwa juu, nikaangaza macho huku na huku; hakuwa na mtu yeyote, nikapanda juu ya ule ukuta kama paka, nikachungulia upande wa ndani nikaona Nyumba kubwa ya vyumba kama vitano hivi, nyuma ya ile nyumba kulikuwa na jengo ambalo ujenzi wake ulikuwa unaendelea, ambalo likikamilika litakuwa la ghorofa, kulikuwa na majani ambayo hayakuwa kwenye mpangilio mzuri hii ni kumaanisha hapkuwa na uangalizi mzuri wa mazingira ya eneo lile, palikuwa rafu rafu, chini kabisa nikaona kama miche ya mahindi ikiwa katika mstari kama robo heka hivi, nikateremka polepole bila kutingisha hata majani kama nyoka, nikasonga kwa tahadhari nikiwa najificha kwenye vichaka, nikaona wakimtoa Mr. Kibadeni kwenye Ile Crusset, wakampiga kwanza ngumi mfululizo pasipokuzungumza naye, Mr. Kibadeni akawa analalamika lakini sauti yake ikawa haitoki vizuri kwa sababu walikuwa wamemziba mdomo na Gundi maalum ya solitepu, walimpita mpaka walipoona amechakaa, wakamuingiza ndani kwenye ile nyumba, nikaangalia kwa umakini tena mazingira ya ile nyumba kwa nje nikaridhishwa, nikatoka kwenye kile kichaka, nikakimbia upesiupesi mpaka kwenye kona ya ukuta wa ile nyumba upande ambao haukuwa na taa, nikasonga upande wa nyuma wa ile nyumba kuona kuna nini, nikakuta mapipa ya maji, mchanga na kokoto nyingi pamoja matofali za lile jengo lililokuwa linaendelea, nako kulikuwa na taa inayoangaza eneo lote la nyuma, kwa bahati nikaona swichi, nikageuka kuangalia nilipotoka sikuona hatari yoyote, nikanyata nyatunyatu! Mpaka kwenye swichi, nikazima kukawa na giza, nikalifuata dirisha, nikachungulia hapakuwa na mtu isipokuwa kitanda na godoro na chandarua iliyokuwa imeandaliwa kwa mtu kulala, nikazunguka upande mwingine wa ubavu wa ile nyumba, hapakuwa na kitu, nikaona dirisha la chumba kingine, nikaligelea, hili lilikuwa muundo wa madirisha ya kuteleza yenye kioo na nyavu, nikaichana ile nyavu kidogo nikapitisha mkono, nikasukuma dirisha, nikazama ndani, nikarudishia kama mwanzoni.

Chumba kilikuwa maboksi na mifuko ya saruji, kulikuwa na vumbi sana, nilitumia kalamu yangu yenye tochi kumulikia, Nikasogelea mlango wa kile chumba, kwa tahadhari nikakigusa kuangalia kama mlango umefungwa, ulikuwa umefungwa, nikatoa funguo Malaya, nikafungua ukafunguka, nikapokelewa na korido alafu kwa mbele kuna mlango mkubwa hivi ambapo kwa mbele niliona Sebule isiyo na vitu vingi, yalikuwapo masofa mawili marefu, zulia alafu kwa mbele kabisa ilikuwepo Luninga, nikajiridhisha papo salama, nikajitokeza na kusimama pale sebuleni, nikapasaili kwa haraka haraka hapakuwa na chochote ukutani isipokuwa saa ya ukutani iliyoniambia ni saa sita kasoro za usiku, kulikuwa na korido upande uleule niliotokea lakini kwa kulia, nikaifuata nikiwa nanyata kwa umakini nikipima mzunguko wa hewa na sauti yoyote ambayo ilikuwa kwenye nyumba ile, nikasikia sauti kwenye mlango uliokuwa upo mbele yangu, ilikuwa sauti ya Kibadeni akilalamika, alikuwa akipigwa na kuteswa, nilipoufikia ule mlango nikakuta umerudishiwa nusu na nusu nyingine upo wapi, nikachungulia, nilimuona Mr. Kibadeni akiwa anapigwa na wale watu, walikuwa wanaume wanne, watatu wakiwa wanaume wenye miili inayostahili kuogopwa, walikuwa wanaume wa miraba minne, mwadubwana, alafu na mwanaume mmoja wa makamo mwenye upara na aliyeacha ndevu za juu ya mdomo kama Adolf Hitler, mwenye rangi ya maji ya kunde,

“ Mkiniua hamtapata lolote kati ya mnayoyaomba kutoka kwangu” Mr. Kibadeni aliongea kwa taabu sana, wakati huu alikuwa kafunguliwa ule gundi mdomoni.

“ Kibadeni hapa utasema ukiwa hai na hata ukiwa mfu utasema, hahahah!” yule mwanaume mwenye upara akacheka. Alafu wale wanaume wengine nao wakacheka. Wakimdhihaki

“ Kama mkiniambia aliyewatuma basi na mimi nitawaambia kila kitu” Mr. Kibadeni akasema, lakini alipigwa ngumi ya tumbo akagugumia kwa maumivu,

“Acha ukaidi, tutakuua sisi, unafikiri hayo masiri yako tunayahitaji sana sisi, hujiulizi tumejuaje umetoka Marekani juzi, unafikiri hatujui, hahahah! Unafikiri kuna siri unayo sisi hatuna?” Yule mzee akasema akimsogelea Kibadeni pale kwenye kile kiti walichokuwa wamemfunga.

“ Sasa kama mnajua kila kitu ni kwa nini mnaniuliza maswali yenu ya kijinga?” Mr. Kibadeni akasema, akiwa anavuja damu kwenye ukingo wa mdomo.

“ Nimeshakuambia Ukaidi hapa utakugharimu na kufupisha maisha yako” Yule mzee akasema huku akitoa Sigara kwenye mfuko wa koti lake, alafu akaiweka mdomoni, nikamuona moja ya wale wanaume wakitoa kiberiti cha gesi na kukiwasha na kuichoma ile sigara mdomoni mwa yule mzee. Yule mzee akavuta pafu mbili, kisha akapuliza moshi wake ukatapakaa chumba kizima.

“ Embu tuambie ulienda na nani marekani, tunajua wewe ulienda lakini hutukujua mliyeenda naye” Yule mzee akasema, akaiweka tena sigara mdomoni akiyapunguza macho yake ukubwa akiwa anavuta pafu ndefu ya sigara, kisha akaiachia alafu akafumba macho yake akiwa anautoa moshi polepole kwenye pua, kisha akatoa pia kwenye mdomo.

“ Mpigeni tena kidogo” kabla hajamaliza kusema wale wanaume wakamshika tena na kuanza kumpiga, walimpiga mpaka pale yule mzee aliposema; “muacheni sasa, rafiki yetu yupo tayari kusema kila kitu. Kwa nini mnampiga?” aliongea kwa kufoka.

“ Kibadeni rafiki yangu, hakuna ambaye anataka kuua hapa, wewe ndiye utaamua tukuue au tukuache, uamuzi ni wako” Yule mzee akasema alafu akamsogelea karibu kibadeni, kibadeni akamtemea mate yaliyochanganyika na damu, kisha akaanza kucheka;

“ hahahah! Rafiki! Mwisho wako umefika, ngoja uone, njia ya mwovu haina mwisho mwema, serikali haipo mbali itakukamata”

“ Serikali? Ipi? Au serikali yako! Hahahah!” Embu sema nani ulienda naye Marekani,?” Yule mzee akasema lakini Kibadeni ni kama aliamua kufa na siri, hakutaka kusema, nikamuona yule mzee akitoa mfukoni simu, kwa jinsi Kibadeni alivyokuwa akiitazama ile simu nikajua itakuwa ni simu yake, wakachukua kifaa Fulani wakapitisha juu ya ile simu ikachora pattern ambazo Kibadeni ndizo anazofungulia simu yake, kile kifaa kilikuwa kina sensor yaku-detect mipanguso ya mara kwa mara katika kioo cha simu. Mapigo ya moyo wangu yakaanza ziara, wasiwasi wa kujulikana uliniingia kwani niliamini kuwa mtu wa mwisho kuwasiliana na Mr.Kibadeni alikuwa ni mimi, kitendo cha yule mzee kuanza kuipekua ile simu kilimaanisha muda mfupi ujao wangenifahamu. Nami sikutaka jambo hilo litokee.

“ Kwa hiyo umeamua kufa Mr. Kibadeni?”

‘ Umri wangu sasa ni miaka hamsini na saba, hata sina mtoto mdogo anayenitegemea, na hata ningekuwa naye wala nisingeogopa kwa ajili ya kulinda siri za nchi” Kibadeni alisema.

“Muueni!” Yule Mzee akaamuru wale vijana.

“ Subiri!” Mr. Kibadeni akaseema, hapo nikamuona yule mzee akimtazama kisha akasema;

“ Vipi unataka kutuambia ukweli, uliyeenda naye Marekani alikuwa nani?”

“ Nilikuwa naombi moja?”

“ Ombi lipi?”

“ Nataka kabla hamjaniua nijue nani aliyewaambia nilienda marekani, hilo tu mkinifanyia nitamwambia Mungu asiwahesabie dhambi hii ya kuniua” Kibadeni akasema, wale watu wakatazamana alafu wakacheka,

“ Muueni huyu anafikiri sisi ni wajukuu zake” Yule Mzee akasema, nikawa nimejiandaa kuvamia nikiwa tayari nimeiandaa bastola yangu kushambulia, lakini kabla sijataka kufanya lolote nilihisi kitu kigumu kikigusa kisogo changu

ITAENDELE KESHO SAA 7mchana
 
Back
Top Bottom