Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 28,297
- 68,017
- Thread starter
- #61
Naomba unitag ukitaka kuendelea
Sawa Mkuu
Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Naomba unitag ukitaka kuendelea
Mambo ni moto ila hujatuambia nini kilimpata mr Kibadeni baada ya kutoka hospitali. Lakini pia hatujui Mwanamuziki amefikaje marekani.
[emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787]Mkuu kwani saa 7mchana haijafika mbona mpaka Sasa kimya?
Sawa MkuuShukran Mkuu,, nyongeza, mapema basi kabla hatujatoka mezani
Duh aisee inasikitisha sana [emoji26]Kaburi la mwanamuziki ( Episode 07)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300
EPISODE 07
ILIPOISHIA
Mkuu alinitazama kisha akamtazama Mr. Kibadeni aliyekuwa amelala pale kitandani akiwa hajitambui, kitanda kimoja kikiwa hakina mtu. Ghafla mlango ukafunguliwa, tukageuka kutazama, walikuwa manesi wawili wakiwa wanasukuma kigari cha wagonjwa juu kile kitanda alilala Kijana mmoja mwenye umri kama wa miaka ishirini na nane hivi akiwa amejeruhiwa kama kibaka aliyechapika akachakaa, alafu nyuma ya wale manesi alikuwepo mwanamke mmoja aliyevalia kwa kujitanda, alikuwa mweupe kama mwenye asili ya kisomali hivi, wakaingiza wakamtoa yule mgonjwa waliyemleta, wakamuweka kwenye kile kitanda kilichokuwa pale ndani.
Wakatusalimu kisha wakaendelea nashughuli zao za kitabibu za kumuosha vidonda, nilikuja kujua yule mwanamke mweupe alikuwa akiitwa Zuleikha baada ya kuwasikia wale manesi wakimuita mara kwa mara.
********
ENDELEA
JENGO LA TANZANIA GOT TALENT – TGT, DSM.
“Kipaji ni zawadi ya maisha, kuna kipaji asili ambacho mtu anazaliwa nacho, na kipo kipaji cha kujifunza ambacho mtu hajazaliwa nacho, hatuwezi kusema kipi ni bora lakini mwenye juhudi huyo kazi zake zitaleta matokeo katika maisha yake na jamii inayomzunguka. TGT Ipo kwa ajili ya kukuza vipaji vya vijana wa nchi yetu, tumezunguka karibu mikoa yote kwa ajili ya kuwafikia wale wote waliobahatika kukutana nasi, ninyi ni sehemu tuu ya vijana wenye bahati kuwa hapa, lakini hamkuwa hapa kwa sababu ya bahati isipokuwa tumeona kitu ndani yenu, niliposema “wenye bahati” nilimaanisha ni kwa sababu mmepatikana kati ya wengi, kumaanisha sio ninyi pekee yenu wenye vipaji, hata ninyi mnajua, kweli sio kweli?” akauliza yule mwanamke.
“ Kweli!” Wote tukaitikia kwa sauti zilizopoa. Ulikuwa ukumbi wenye viti vilivyotosha watu zaidi ya mia moja hivi, mwanamke yule akaendelea,
“ Tutaanza shindano letu ambalo litaenda kwa muundo wa mchujo, kila mmoja wenu baada yaku-perform atapewa hukumu palepale kutoka kwa majaji, watakaobaki ndio watapewa nafasi ya kufundishwa na waalimu maalumu tuliowaanda, nawasihi mfikapo kwenye jukwaa muwe watulivu, msiogope, sisi ni watu kama watu wengine, jitahidini kuchagua nyimbo nzuri ambazo ni maarufu kwa watu wengi watakaokuwawanasikiliza, chagua wimbo ambao unaweza Key zake, kuweni wachangamfu na onyesheni uhusika mnapokuwa mnaimba, kama mtazingatia haya nafikiri litakuwa shindano gumu kuamua kwa majaji, haya shindano linaanza;” Yule mwanamke akaongea.
Nilimuona yule Mwanamke mrembo niliyemuona siku zile leo hakuvaa lile gauni jeusi lililomshika vyema kama siku ile, isipokuwa alikuwa kava kivazi Fulani cha kisanii kilichompendeza sana, nilifurahi kumuona tena mahali pale. Sijui kilichonifanya kila saa nimtazame ni kitu gani, labda ni kwa sababu alikuwa ni mzuri sana, tena sana. Siku ile kidogo nilikuwa nimevaa nikapendeza tofauti na siku ya kwanza, kuishi kwa Riadi kulinisaidia kupata mavazi mazuri yanayoendana na wakati. Hivyo iliniongezea kujiamini. Nikamsogelea yule mwanamke mrembo;
“ Mambo Pisikali!” Nikamsalimia, akageuka, nikamuona akishangaa alafu akatabasamu.
“ Kumbe nawe upo?” Akasema,
“ Nikuulize wewe, mimi ni mwanamuziki, wataachaje kwa mfano kunichagua ikiwa wanapenda muziki mzuri!” Nikasema, basi tukacheka, tukaendelea kupiga stori za hapa na pale kusogeza muda tukisubiri kuitwa, wengine wakiendelea kuitwa, nilikuja kujua jina lake, anaitwa Neema, alikuwa mzuri sana Neema, hisia za mapenzi zilianza kuchipua tena tangu ziliposinyaa siku alipoondoka Alice kwenda kusoma nje ya nchi, leo kwa mara nyingine nilihisi mapenzi yakibisha hodi katika mlango wa moyo wangu, yalikuwa yakibisha kwa nguvu sana ilikuwa ni hiyari niyakubalie yaingie ima niyakatalie yauvunje mlango wa moyo wangu, lakini ningewezaje kumkataa Neema Moyoni mwangu kwa uzuri ule wa ajabu aliokuwa nao, niliapa kumkaribisha katika kisiwa cha mapenzi, tukizungukwa na bahari ya upendo, hivyo ndivyo ilivyokuwa,
Neema alitangulia kuitwa, baada ya dakika kshaa akatoka, ajabu aliyefuatia kuitwa ilikuwa ni mimi, sikutegemea kama tungeitwa kwa kufuatana hivyo, hiyo kwangu niliichukulia kama dalili njema katika safari yangu ya mapenzi.
Ukumbi ulikuwa ni uleule wa ile siku, nikasimama wima, nikawasalimia kisha wakanipa ruhusa niendelee kufanya kilichonipeleka, nikaimba beti moja wala sikumaliza wakanikatisha, na kunisifia kuwa ninajua kuimba, wakaniambia nitaendelea, nikatoka nikamkuta Neema akiwa ananisubiri palepale nilipomuacha kwani nilikuwa nimemuachia Begi langu na vitu vyangu. Wote tulikuwa tumechaguliwa kwenda hatua iliyokuwa inafuata, ambayo washirika tuliopita tulikuwa hamsini hivi, tukapongezana kisha yule mwanamke aliyekuwa anaongea mwanzo akawaruhusu wale walioshindwa waondoke, walipoondoka tukabaki tulioshinda katika hatua ile tukiwa tumetulia tunasubiri maelekezo ya yule Mwanamke ambaye mpaka muda ule hatukuwa tunajua jina lake,
“ Habari za mchana, hongereni kwa kufikia hatua hii, hongereni kwa kuchaguliwa, sasa kuanzia wiki ijayo tutaanza shindano letu Mubashara kwenye vyombo vya habari, hivyo kila mmoja wenu itampasa awe amejiandaa, wapo waalimu watakaowasaidia kuwafundisha mambo kadhaa ili kuwafanya muwe wakali zaidi, karibuni waalimu” Yule mwanamke akasema, alikuwa anaongea kwa bashasha sana huku kila wakati akiachia tabasamu lake na kufanya mwanya wake uonekane, aliijua sana kazi yake ya utangazaji na ushehereshaji. Wakatokea waalimu watano ambao walipita mbele baada ya kukaribishwa, yule mwanamke akawatambulisha kwa majina, kisha akawapa kila mmoja wao watu kumi wa kuwa-coach, yaani kila mwalimu akapewa watu kumi wa kuwafundisha,
Nilitamani mimi na Neema tupangiwe mwalimu mmoja lakini hiyo haikutokea, tulipangiwa waalimu tofauti, mimi nilipangiwa Mzee mmoja mwenye Rasta apendaye kuvaa kofia la rangi ya bendera ya Nchi ya Ethiopia, huku Neema akipangiwa Kijana mmoja mwenye Draid awe ndiye mwalimu wake. Baada ya zoezi la kugawiwa waalimu, tuliambiwa tutafika kesho asubuhi kwa ajili ya mazoezi kila siku, nikamuita Neema kisha tukawa tunatoka kuelekea nyumbani,
“ Nilitamani tungefundishwa na Mwalimu mmoja” Neema akasema, maneno yake yalinifanya nitabasamu “Kumbe naye anafikiri kama mimi” Nikawaza, kisha nikasema;
“ Kwa nini unasema hivyo Neema?”
“ Basi tuu! Kwani wewe haukupenda tuwe pamoja?’ Akasema akinitazama,
“ Tena nilitamani niwe mwalimu wako!”
“ Mwalimu wangu!” Akasema kwa kushangaa huku akiachia kicheko
“ Ndio! Mwalimu wako wa Muziki” Nikasema, nikimtania,
“ You can’t be Sirius”
“ Sawa kama hutaki niwe mwalimu wako, lakini mimi ningekufaa sana” Nikasema.
“ Sasa utakuwaje mwalimu wakati nawe upo kwenye mashindano, si utanifundisha mashudu ili ushinde wewe” akasema,
“ Hahaha! Neema Bhana, embu tuachane na hayo, hivi unaishi wapi?”
“ Nani Mimi! Mimi naishi Goba” Neema akasema huku tukiwa tumeshafika kituo cha Daladala,
‘ Unaishi na nani?” nikasema
“ Ninaishi na Kaka yangu” Akajibu, nikawa nimekaa kimya kuogopa kuuliza swali jingine, nilijua kuwa wanawake mara nyingi hawapendi maswali mengi, hawapendi kuulizwa ulizwa, hasa ikiwa ni siku ya kwanza.
“ Nawe unaishi wapi? Akaniuliza, lakini kabla hajajibu tayari gari zinazopita Goba ziliwakuwa zimewasili, hivyo akaondoka kabla sijampa jibu. Huo ulikuwa mwanzo mpya wa penzi tamu na mtoto Neema..
Nilirudi nyumbani nikamkuta Riadi amekaa na shemeji wakiangalia kipindi Fulani kwenye Luninga, walikuwa wamekaa mbalimbali, tayari nilikuwa nimeshajua jinsi familia ile ilivyo hivyo hilo halikunishangaza, kwani shemeji alikuwa akipenda sana kumzingua Riadi, kama sio kununa, basi kulalamika kiufupi shemeji alikuwa na Gubu sana, hata hivyo sikujua hayo yote yalitokana na mimi, nilifuata msemo usemao; Ya ngoswe muachie ngoswe. Kwa maana pilipili nisiyoila kwa nini iniwashe.
“ Vipi Gibson kumeendaje huko?” Riadi akaniuliza nikiwa nimeingia na kukaa kwenye sofa.
“ Nashukuru sana, mambo yanakwenda vile nilivyopanga, tayari nimepita kwenye hatua hii, na wiki ijayo tunaanza kuonekana kwenye Luninga, mtaniona hapa” Nikasema nikiwa nimefurahi, nilishindwa kujizuia kwakweli.
“ Acha utani Gibson” Riadi akasema, nikampa ishara kumuambia iko hivyo. Akasema;
“ Usiniambie utakuwa maarufu!”
“ Hahah! Nitakuwa mwanamuziki mkubwa mashuhuri sana” Nikasema
“ Mmmh! Jipe moyo utashinda!” Shemeji akasema huku akibetua mdomo wake. Wote tukamtazama alafu nikasema;
“ Shemeji! Najua huniamini, lakini nakuhakikishia nitashinda na nitakuwa mtu maarufu katika muziki”
“ Wewe hata mshindi wa tatu hauwezi kufika, acha kutuona watoto hapa” Shemeji akasema.
“ Mke wangu mbona unakuwa hivyo, badala umpe moyo wewe unamkatisha tamaa” Riadi akasema,
“ Sio namkatisha tamaa, Gibson kuimba bado sana, huo ndio ukweli, mpe mtu ukweli hata kama utamchoma”
“ Sikiliza shemeji, niahidi kama nitaingia hata Top 3, Utanipa zawadi gani?” Nikamuuliza shemeji.
“ Wewe huwezi ingia hiyo top 3…” shemeji akasema,
“ Jibu swali utampa zawadi gani?” Riadi akaingilia mazungumzo, hapo kukatokea ukimya huku watu wote tukimtazama shemeji.
“ Haya sema wewe, kama utaingia Three unataka nikupe nini? Mimi chochote ukiombacho nitakupa” Shemeji akasema huku akanitazama, lakini kauli ya chochote atanipa ikamtia wivu Riadi, niliuona uso wa Riadi ukibadilika na kuwa na hasira zilizojificha, wivu ulikuwa karibu sana.
“ Sawa shemeji, mimi naomba nisitaje siku ya leo, subiri siku nikishinda nitarudi hapa mbele ya shemeji kukuomba kitu cha kunipa” nikasema, mjadala ukafungwa.
Usiku uliingia, kitandani nilikuwa namuwaza muda wote Neema, ni kweli alifanikiwa kuuteka moyo wangu, mapigo yangu ya moyo yalitaja jina lake kila yalipokuwa yanapiga, nilitamani kesho ifike ili nikutane naye tena, sijui kwa nini nilisahau kuomba namba zake, nilijilaumu. Usingizi ukanipitia nikalala,
Kesho yake tulikuwa kwenye mazoezi ya muziki, tulifundishwa soft skills katika muziki, tulifundishwa namna ya kuwasilisha muziki jukwaani, pia tulifunishwa namna ya kuutiisha mwili na kuonyesha hisia wakati tunatumbuuza, tulifundishwa namna ya kuangalia hadhira na kuvuta usikivu wao tuwapo jukwaani, kwa kweli sikupata nafasi ya kukutana na Neema, siku ile ikapita, Siku iliyofuata mambo yalikuwa kama siku ya kwanza, sikukutana na Neema, waalimu walituambia masomo ni mengi na muda ni mchache hivyo hata muda wa mapumziko haukuwepo, alafu chakusikitisha zaidi ni kuwa muda wetu wa kutoka tulikuwa tunapishana kwani kila mmoja alikuwa kwenye darasa lake na mwalimu wake.
Siku zote za mafunzo sikupata nafasi ya kuzungumza na Neema, kwa kweli zilikuwa siku ngumu sana kwangu. Siku ya shindano lilikuwa imewadia, niliwaandaa Riadi na shemej wanitazame kwenye luninga, pia nilimpa mama taarifa kuwa anaweza kwenda kwenye luninga za majirani ili aweze kunitazama.
Muda wa kutumbuiza ulikuwa umefika, tuliketi kwenye ukumbi uleule wa mwanzo kabla hatujaingia kwenye ukumbi mkuu wa shindano, tofauti nasiku zingine, ukumbi wa pale mapokezi siku ya leo kuliwekwa Luninga kubwa ambayo ilikuwa inaonyesha matukio yaliyokuwa yanaendelea kwenye ukumbi mkuu, hivyo kila mshiriki aliyeenda kutumbuiza tuklimuona Kupitia luninga ya pale ukumbi wa mapokezi, wakaenda washiriki kama ishirini hivi kisha akatajwa Neema, nikamuona Neema akigeuka kunitazama nikampa ishara ya kuwa tupo pamoja na kumpa moyo kuwa atashinda, Neema alikuwa amevalia kigauni kifupi kilichochanua kama mwamvuli, na kitopu juu kilichomkaa vyema, nywele zake alikuwa kazisuka rasta katika mtindo wenye kuvutia sana, chini akiwa kavaa viatu virefu vilivyozidi kumfanya mrembo maradufu.
Neema aliimba, sauti yake kali inayobembeabembea iliwafanya majaji watulie tulii ungedhani wapo kwenye ukumbi wakimuangalia muimbaji mahiri wa kimataifa, hata sisi tuliokuwa washiriki tulikubali kuwa Neema alikuwa anakipaji kikubwa cha uimbaji, akamaliza, kisha akaruhusiwa kuondoka. Akarudi kwenye ukumbi wa mazoezi na moja kwa moja alikuja pale nilipokuwa nimekaa, nikamkumbatia, huku nikimpongeza na kumpa moyo kuwa amefanya vizuri. Nilijisikia fahari kukumbatiana na Neema mbele za watu, niliona baadhi ya washiriki wakinionea wivu.
Wakapanda wengine kama kumi hivi, kwa kweli kuna kijana na msichana mmoja ambao walinitisha, walikuwa wakiimba kama Majini waimbaji, sauti zao zilifanana na uzuri wa maporomoko ya maji yaliyokatika mpangilio mzuri wa sauti, zilikuwa sauti za kustaajabisha sana, sikuwahi kufikiri kuwa kuna watu wanajua kuimba kiasi kile. Moyoni nilianza kuona wasiwasi, nilikumbuka kauli za shemeji kuwa kwenye kuimba mimi bado sana. Hata hivyo nilijipa moyo, “ siwezi kujikatisha tamaa mwenyewe, nitaonyesha uwezo wangu wa juu kuliko nilivyowahi kuuonyesha” Nikawaza. Nikiwa nawaza namba yangu ikatajwa nikaenda huku Neema akijaribu kunitia moyo kuwa nisiwe na hofu nitafanya vizuri. Alioniongezea tumaini na kujiamini.
Nikasimama mbele kwenye jukwaa, nikijua mama yangu kijijini ananiangalia, ndugu zangu, rafiki niliosoma nao pamoja na familia ya Riadi inanitazama, “lazima niionyeshe dunia uwezo” Nikawaza. Nikaimba kwa sauti mvurugano zikiwa zimepangika kwa ustadi wa hali ya juu sana, niliimba huku nikionyesha vitendo na hisia kali sana, nikawaona majaji wakitasamu huku wakiwa na nyuso za kushangazwa na vile nilivyokuwa ninaimba, sasa nikapandisha Key ikawa ya juu lakini sio juu kabisa, ulikuwa wimbo wa hisia kali, mwishowe nikamaliza. Nikapigiwa makofi, kisha nikatoka, baada ya washiriki wote kutumbuiza, muda wa mchujo ulikuwa umefika, walipaswa washiriki ishirini na tano waendelee na mashindano na waliobakia ishirini na tano wage mashindano, kila kundi la mwalimu mmoja walipaswa wapungue watu watano, mchujo ukaanza, nataka kukuambia hakuna kitu kigumu kama matokeo na mchujo, hata kama umefanya vizuri lakini kura ndizo huamua hivyo huwezijua watu walivyokusikiliza walikuonaje, hivyo hakuna anayejiamini kwenye mashindano hasa ya kupigiwa Kura.
Nyuso za washiriki niliziona zikiwa na wasiwasi mkubwa, ni kama kila mmoja alikuwa akiomba kimoyomoyo, Neema alikaa pembeni yangu akiwa amekunja mikono yake kwenye kidevu huku kila mara akifunika uso na kuuchia, kwa bahati nzuri tulipita katika hatua ile, watu ishirini na tano tungeendelea kuchuana katika hatua iliyofuata, ambayo ilikuwa siku wiki iliyofuata.
Sikutaka kufanya tena uzembe kama mwanzo, nikachukua namba za simu za Neema, kisha kila mmoja akarejea makwao. Nilimkuta Riadi na Shemeji wakinisubiri kwa hamu, ilikuwa jioni hivi wakiwa wameandaa vinywaji na pombe za gharama,
“ Gibson umenishangaza sana, kumbe tupo na muimbaji mkubwa hapa” Riadi akasema, Nikawa kimya nikiwa nimetabasamu, hakuna kitu kizuri kama kuona kipaji chako kinaanza kueleweka na watu.
“ Bado hajanishawishi, ila anajaribu jaribu” Shemeji akasema,
“ Wewe kalia hapo na roho mbaya yako” Riadi akasema,
“ Nani anaroho mbaya, nani?”
“ Tusigombane, tunywe tufurahi, haya tugonge cheers” Nikasema, ili kuzuia ugomvi uliokuwa unataka kuanza. Basi tukanywa na kufurahia, Nikaondoka kwenda kulala nikiwaacha wao wakiendelea kunywa pombe, mimi nilikunywa kidogo, sikuwa mzoefu sana wa kunywa pombe.
Kesho yake tuliendelea na mazoezi, sikuwa na haja ya kuonana na Neema kule TGT kwani tayari nilikuwa na namba zake, hivyo kabla hatujafika tulikuwa tunazungumza kwenye simu, na tukitoka halikadhalika, moja ya kanuni tulizoambiwa siku za mwanzoni ni kujiepusha na mapenzi baina ya washiriki wakati shindano linaendelea, hiyo ilituzuia tusionane mara kwa mara pale TGT.
Shindano la hatua ya pili liliwadia, kila mshiriki alikuwa amejiandaa kikamilifu, na mafunzo tuliyopatiwa yalizidi kutunoa na kutufanya tuwe wakali zaidi, Nilikuja kujua yule kijana aliyeimba kama Jini alikuwa akiitwa Stelin Kaboga, na yule msichana nilimtambua kwa jina Moja, nalo ni Semeni. Washiriki hawa nilitokea kuwapa tahadhari kubwa kutokana na uimbaji wao, walikuwa wakiimba sana, hasa huyu kijana Stelini ndio nilimuona kama mwiba.
Washiriki kumi walipoitwa ndipo akaitwa Neema, aliimba leo kwa kawaida sana ingawaje aliimba vizuri, ila nikilinganisha na waimbaji waliopita kiukweli niliingiwa na wasiwasi huenda Neema akaishia hatua hii, alipomaliza akatoka kisha akatajwa Semeni, baada ya kumpokea Neema tukawa tumetulia tukimtazama Semeni Kupitia Luninga akiwa anajiandaa kuimba, washiriki wote mule ukumbini ni kama tulishamuelewa uimbaji wake hivyo tulikuwa tupo tayari kumsikiliza, semeni akaimba, kudadadeki! Alikuwa anaimba kama Jinni la kike lenye sauti ya kinubi mdomoni mwake, sikujua alikuwa akifanyaje mdomo na koo lake mpaka sauti iwe kwa mtindo ule, lakini masikio yangu yalijua sauti ile ilikuwa nzuri sana, aliimba kuna wakati akawa kama anataka kutufanya tusinzie kwa sauti yake, nikamtazama Neema, nikaona hofu usoni mwake, nikanong’ona sikioni mwake; “ Akiimba kama Jinni wewe imba kama Malaika, akiimba kama mtoto wa Lusifa, wewe imba kama mtoto wa Jibril” akanitazama kisha nikamkumbatia alafu nikasema; Utamshinda Semeni” akaniangalia kisha akaniuliza “ Kweli” Nikatingisha kichwa “ndio” Semeni akamaliza,
Nikaitwa mimi kabla hajaitwa Stelin jambo ambalo sikulifurahia, nilitaka Stelin atangulie kama hatua iliyopita ili nipitie kwenye mapungufu yake, lakini sikujali sana, nikamuaga Neema kisha nikaingia katika ukumbi wa mashindano, nikaona nyuso za majaji zikinitazama kwa shauku kana kwamba zinaniambia unamuona aliyetoka, nami nikawatazama kwa namna ya kuwaambia; subirini muone. Nikaimba nikiwa nimetulia, siku ya leo niliimba pasipo kutumia sauti zisizo za kawaida, niliimba kama mwimbaji mkongwe wa miaka ya ukoloni, hawakuwahi kusikia ladha za nyimbo za wakati huo, nilichokifanya ni kuvuta hisia za wakati wa nyuma, kuzirudisha hisia miaka mia iliyopita, kisha nikaimba katika hisia hizo katika uwepo wa zama hizi, muimbaji ni lazima ajue kuimba kwa namna zote, awe na uwezo wa kuimba katika nyakati zote, iwe zilizopita, zilizopo au nyakati zijazo, hii itamfanya azidi kuishi milele dawamu. Hicho ndicho nilikifanya siku ile, watu walihisi wapo katika miaka mia iliyopita katika uwepo wa zama za leo, hiyo nilifanikiwa nilipokamata marimba na kuyapiga huku nikiimba kwa sauti ya kale yenye mvuto wa kipekee, nani mwingine angeweza kufanya kama mimi, kwa kweli hata wao hawakujua kama jambo lile lingeweza kutukia.
Nilimaliza, wakanipigia makofi, kisha aliyefuata alikuwa ni Stelin, kufululiza kwetu kulimaanisha ushindani baridi uliotangazwa kwa siri katika halaiki ya wenye masikio. Stelin akapanda jukwaani akiwa anajiamini haswa, alikuwa kashika Gitaa lenye nyuzi sita, akaiseti maiki vizuri kisha akatoa heshima kwa majaji, nikawaona majaji nao wakimrudishia hisani ya tabasamu, huyo Stelin aliimba siku ile ungedhani ndio Fainali, alizichana nyuzi za lile gitaa kama mwendawazimu, sauti iliyotoka katika Gitaa haikuwa ya kawaida, ilikuwa sauti ya ajabu yenye kustaajabisha, labda hujui ninasema nini ndugu msomaji kama hujawahi kuona gitaa likitoa sauti za kupendeza alafu muimbaji wake aimbe kwa sauti kuu yenye ukali wa kuyavutia masikio. Stelin alimaliza, akiwaacha washiriki wengine wakijiona hawajui kuimba,
“ Stelin anaimba sana” Neema akaniambia, Nilijisikia wivu lakini kabla sijamjibu akaongezea,
“ Ila wewe unaimba zaidi yake, nafikiri ninyi ndio mtakuwa washindani katika tuzo ya mashindano haya”: Nikamtazama Neema, kisha nikasema,
“ Haya ni mashindano Mpenzi, kila siku watu wanabadilika, huwezi kusema hivyo mapema yote hii, bado washiriki ni wengi Neema”
“ Haijalishi wawe wengi kiasi gani, Stelin na Gibson ndio mtakuwa mnawania Tuzo hii, sasa najuta kwa nini sikubali uwe Mwalimu wangu wa muziki” Neema akasema,
“Huna haja ya kujuta Neema, bado nafasi ingali ipo” Nikasema,
“ Muda uliobaki ni mchache, kama ningeanza tangu siku ile uliyonambia, leo hii hapa ningekuwa mbali sana, unaimba kama malaika Gabriel” Akacheka akiwa ananitazama.
“ Niite Jibril bhana ndio linaswaga mdomoni, hata wewe ni mtoto wa Jibrl” Nikasema, tukacheka sana, muda wa mchujo ukafika, Neema alikuwa kwenye Dangerzone aluipata kura chache lakini zilimuwezesha kuendelea hatua iliyofuata, tulibaki washiriki kumi na mbili. Sasa tuliingia kwenye nusu robo fainali ambayo ingefanyika wiki iliyofuata.
Nilirudi nyumbani nikiwa na mipango tofauti ya kukabiliana na Stelin, nisingejiongopea kuwa Stelin alikuwa mwiba katika koo langu, uimbaji wa Stelin kwa mshiriki yoyote wa mashindano yale mwenye nia ya kutwaa ubingwa ni lazima ungemnyima usingizi.
Wiki ile nilibahatika kwenda alipokuwa akiishi Neema maeneo ya Goba, zilikuwa nyumba mbili kubwa, nyumba ya kwanza ikikuwa ya Ghorofa mbili, ile ya pili ilikuwa nyumba ya kawaida tuu. Kaka yake Neema ni kama niliwahi kumuona siku za nyuma lakini sikuwa nakumbuka ni lini na wapi niliona sura kama ile, alikuwa mrefu wa kati, maji ya kunde mwenye mwili uliojengeka vizuri, kama utamuangalia sana unaweza kugundua ni Polisi au anafanya kazi za namna hiyo kama uanajeshi, au afisa usalama wa taifa.
“ Kaka, huyu ndiye yule kijana niliyekuambia atakuja, anaitwa Gibson, maarufu kama Jibril mwanamuziki” Neema akasema akiwa anacheka.
“ Karibu sana Gibson, nimefurahia sana kuonana na wewe, nimekuwa nikikuona kwenye Luninga, unaimba sana mwamba” Kaka yake Neema akasema,
“ Nashukuru sana Broo” Nikasema,
“ sawa mimi ngoja niwaache nitaenda mjini, Neema mzingatie sana kama siku zote, uwe makini” Kakaake Neema akasema, akiwa anatoka.
“ Sawa kaka, nitamuangalia” Neema akajibu, nikawa najiuliza atamuangalia nani, yaani alimaanisha nani hasa, anamaanisha aniangalie mimi au kuna mtu mwingine, lakini sikuwa na majibu.
Tukafanya mazoezi ya kuimba lakini kila mara Neema alikuwa akiniaga akiniacha pale kwenye nyumba ya ghorofa na kushuka kule nyumba ya chini, siku za mwanzoni nilikuwa naona kawaida lakini kadiri siku zilivyokuwa zinaenda nikwa nataka kujua ni kwa nini Neema alikuwa akiniaga kila saa alafu anaenda nyumba ya chini kule. Nikakumbuka msemo usemao, usimchungeze sana bata hautamla, nikaacha kufuatilia jambo hilo.
Robo fainali ilikuwa imewadia, walikuwepo washiriki kumi na mbili, shindano lilianza Nikiwa wakwanza kutumbuiza, nilijua kuwa kila mtu alikuwa amejiandaa na wote tulikuwa wazuri na wenye vipaji vikubwa, sikutaka kufanya kosa lolote hata liwe dogo vipi, nikamuaga Neema, nikapanda jukwaani, kabla sijaruhusiwa kuimba, mbele ya luninga ya ukumbi wa mashindano tukaonyeshwa jinsi watu mtaani walivyokuwa wanafuatilia shindano lile la Tanzania Got Talent, wengine walikuwa kwenye Bar wakinywa pombe, wengine kwenye vibanda umiza, wengine majumbani mwao, kwa kweli nilijihisi ndoto yangu inaenda kutimia, huo ulikuwa ujumbe kuwa ninatakiwa nionyeshe ulimwengu mimi ndiye Jibril wa dunia. Muimbaji pekee ambaye hakuna kama mimi, baada ya matangazo kumalizika nikaruhusiwa kuimba,
Siku ya leo niliimba nyimbo za mtindo aliokuwa anautumia Stelin, lengo ni kuwaonyesha watu kuwa ninauwezo mkubwa wa kuimba wimbo wa aina yoyote katika mtindo wowote, niliimba kama kwaya ya majini yanayoozesha binti yao, ndani ya dakika tatu nilikuwa nimemaliza nikiwaacha wasikilizaji na watazamaji wakiwa na kiu kali ya kunisikiliza, walitaka niendelee kuimba lakini isingewezekana, nikashuka, wakafuata watu wawili ndipo akaja Stelin, naye akaimba kwa mtindo wa kikoloni akivuta hisia zilizopita miaka mia nyuma, akivuta hisia za wafu waliokufa miaka hiyo, nilichokikubali kwa Stelin ni kuwa alikuwa na uwezo wa kuunganisha sauti mbilimbili bila kukata pumzi, sasa ilikuwa vita ya dhahiri baina yangu na Stelin. Tulimaliza, wakatoka sita tukabaki sita tuliongia nusu fainali, Neema naye alikuwa miongoni mwa walioimba vizuri hivyo akabaki.
Nilirudi nyumbani, nikijua hatua niliyofikia ni nzuri na ambayo ndoto yangu nilikuwa nikiiona angani kama mwezi mwangavu, mazoezi ya pumzi na kutoa sauti zenye mikia mirefu kama mijusi ya msitu wa amazon, unajua kuimba kuna mambo mengi, hasa kuimba kwenye majukwaa ya mashindano ukiwa mubashara, licha ya kuimba sauti nzuri lakini ni lazima uonyeshe uwezo wa hali ya juu ambao wengine hawana, ndio maana mazoezi ya pumzi na sauti zenye mikia ya mjusi ilikuwa muhimu kujifua nazo, kisha kuunganisha sauti mbilimbili kwa wakati mmoja bila kukata pumzi, wakati nikiwa nafanya mazoezi mwenyewe nilipokea simu kutoka namba nisiyoijua, aliyekuwa akiongea ni mwanamke mwenye sauti kavu yenye mamlaka,
‘ Habari Gibson” akasema yule mwanamke
“ Salama, tafadhali nani mwenzangu” nikauliza
“ Mbona unanifahamu?”
“ Nakufahamu? Kivipi! Mbona mimi sikufahamu?” Nikasema nikiwa nashangaa
“ Ni kweli utakuwa hunifahamu, lakini ulikuwa unatafuta kujua jina langu” akasema,
“ Jina lako! Mimi nilitaka kukujua wewe?” Nikauliza
“ Binadamu hamchelewi kusahau, tena akishapata mafanikio binadamu ni mwepesi kusahau”
“Embu niambie nani mwenzangu, nina kazi nyingi za kufanya” Nikasema nikiwa nimekasirika.
“ Gibson! Mimi ni yule niliyekusaidia usipigwe siku ile Kule Nato Night Club, nikamtuma kijana mmoja hivi akakusaidia, mimi ni yuleyule niliyekusaidia usichomwe moto pale manzese, nikamtuma yule mwanaume kama chizi akakusaidia, je hujanijua mimi ni nani?” Akasema, maneno yake yaliifanya akili yangu ikose utulivu, kwa kweli nilifurahi sana kusikia sauti ya mtu aliyenisaidia, aliyeokoa maisha yangu na kugharamia matibabu yangu kwenye ile hospitali kubwa ya kisasa inayomilikiwa na waingereza, Nikiwa nimetulia nikiwa siamini akaendelea kuongea,
“ Sasa umenijua mimi ni nani, sio?”
“ Ndio mama, Ahsante sana Mama.” Nikasema kwa adabu.
“ Niite Aunt hivyo tuu. Ninaombi moja hapa, nataka unisaidie”
:” Mimi nikusaidie? Mimi ni kijana masikini sina uwezo wa kukusaidia Mama” Nikasema, akanikatisha,
“ Nimesema niite Aunt”
“ Ooh Sorry!”
“ Kila binadamu anauwezo wa kusaidia hata kama ni masikini, kila mtu ananamna yake ya kusaidia” Akanyamaza, ni kama alikuwa akitafakari jambo,
“sawa Aunt nipo tayari kukusaidia”
“ Haya ingia WhatsApp nimekutumia Audio ya nini nataka unisaidie” Simu ikakatika, nikaingia WhatsApp nikaisikiliza ile audio,
Siku ya Nusu Fainali ikafika, tukiwa washiriki sita hapo wangetakiwa watoke watatu alafu waingie fainali washiriki watatu, siku hiyo sikuwa nafuraha kabisa, kila mtu alikuwa akinishangaa, Neema kila mara alikuwa akiniuliza ni kwa nini sina furaha lakini sikumpa majibu yaliyoeleweka, tuliimba lakini siku ile niliimba chini ya kiwango kitu ambacho watu wengi walikishangaa, tayari ushindani ulikuwa mkubwa kati yangu na Stelin hivyo kitendo cha mimi kuboronga ni kumtengenezea njia Stelin.
Nilitoka katika hatua ya Nusu fainali huku nikimuacha Neema akiinga Fainali akichuana na Stelin, na Semeni. Hivyo ndivyo ilivyokuwa,
ITAENDELEA KESHO MCHANA
KITABU CHA "WAKALA WA SIRI" KIPO TAYARI WALIOWEKA ODA ZAO WATAKUWA WA KWANZA KUPEWA ODA ZAO
Naomba unitag ukitaka kuendelea
Okay shukraniTayari
KABURI LA MWANAMUZIKI (EPISODE 08)
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300
Episode 08
ILIPOISHIA
Siku ya Nusu Fainali ikafika, tukiwa washiriki sita hapo wangetakiwa watoke watatu alafu waingie fainali washiriki watatu, siku hiyo sikuwa nafuraha kabisa, kila mtu alikuwa akinishangaa, Neema kila mara alikuwa akiniuliza ni kwa nini sina furaha lakini sikumpa majibu yaliyoeleweka, tuliimba lakini siku ile niliimba chini ya kiwango kitu ambacho watu wengi walikishangaa, tayari ushindani ulikuwa mkubwa kati yangu na Stelin hivyo kitendo cha mimi kuboronga ni kumtengenezea njia Stelin.
Nilitoka katika hatua ya Nusu fainali huku nikimuacha Neema akiingia Fainali akichuana na Stelin, na Semeni. Hivyo ndivyo ilivyokuwa,
ENDELEA
Katika maisha sio kila mara unaweza kupata kile ukitakacho hata kama unauwezo wa kukipata, Kuna wakati unaweza jikuta ukipoteza haki yako tena kwa hiyari yako mwenyewe, nilitamani kushinda tuzo ya TGT lakini kwa makusudi kabisa nilijifelisha, wengi walitaka kujua sababu ya mimi kuimba chini ya kiwango lakini hiyo ilikuwa siri yangu ambayo niliapa sitaitoa mpaka nitakapoingia kaburini.
Fainali ilipangwa siku saba zilizofuata, Neema aliomba nimsaidie kumfundisha, sikuweza kumkatalia, nilitaka nimfundishe ikiwezekana aweze kuwa mshindi, basi ikawa kila nilipokuwa namaliza kazi pale nyumbani kwa Riadi nikawa naenda Goba nyumbani kwa kina Neema kumfundisha,
“ Gibson! Unajua mpaka leo bado najiuliza ilikuwaje! Neema akasema, nikiwa nimefika kwao tayari kuanza mazoezi.
“ Bado sijakuelewa, unazungumzia nini?” Nikasema. Nikiwa ninakipanga kinanda kwa ajili ya kuanza mazoezi, Kaka yake alimnunulia Neema Kinanda kwa ajili ya kufanyia mazoezi, alikuwa akimpenda sana.
“ Ilikuwaje ukaimba kwa namna ile siku ile, unajua mpaka leo umeacha watu wengi na maswali” Akasema.
“ Hamna! Nilikuambia siku hazifanani Neema, kwenye mashindano kuna mambo mengi, lolote linaweza kutokea, na yeyote anaweza kushinda, wakati wewe unafanya mazoezi hapa usidhani kila mtu yupo kama wewe, wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji, wengine wanatumia nguvu ya pesa basi ilimradi kila mmoja anatumia nafasi yake ili ajihakikishie ushindi” Nikasema,
“ Inawezekana! Haya tuanze mazoezi” Akasema, kisha tukaanza kufanya mazoezi ya kuimba nilimpisha tizi la maana mpaka mwenye akahisi mwili kuisha maji, baada ya mazoezi akaenda kuoga kisha akaniaga kuwa anakuja kama ilivyodesturi yake, nikawa nimebaki pale chumbani kwake nikiwa napiga Kinanda, lakini wakati ninapiga kinanda nikajikuta akili yangu ikinishawishi nimfuatilie Neema, nikatoka nikiwa nanyata nikiwa na taadhari, sikutaka anikamate. Nikatokea upande wa sebeluni, kisha nikafungua mlango wa sebeluni alafu nikatoka kwa nje, jua lilikuwa bado linanguvu yapata majira ya saa kumi na moja jioni, nikasonga mpaka kwenye ile nyumba isiyo ya ghorofa ambayo niliamini Neema ndio kaingia, nilienda nikijificha ili niisionekane, nyumba ilikuwa na madirisha yenye vioo, nikakuta viatu vya Neema Pale mlangoni, nikashika kitasa na kukitekenya polepole bila ya kutoa sauti, mlango ukafunguka, nikapokelewa na Sebule kubwa nzuri yenye samani za kisasi, chini likiwepo Zulia la manyoya, hapakuwa na mtu, nikasonga nikiwa nashangaa shangaa baadhi ya picha zilizokuwa kwenye kuta za ile sebule, nikaifuata korido nikiwa nanyata lakini kabla sijafika mbali nikasikia sauti za watu wakizungumza, sauti moja niliitambua ilikuwa ya Neema, sauti ya pili ilikuwa ya mwanaume, nikasogea kwenye ule mlango zilipokuwa zinatokea zile sauti.
“ Hiyo haiwezekani, lazima kuna mtu kamshinikiza atoke kwenye mashindano, Neema Mwanangu usiwe mwepesi kuona mambo vile yanavyoonekana, hii ni dunia, inamambo mengi, kuishinda dunia itakupasa uwe na macho ya kuona vilivyojificha, kutazama visivyotaka kutazamwa, Niamini lazima kutakuwa na mchezo amefanyiwa rafiki yako, kaa naye amuulize kuna jambo anakuficha” Yule mwanaume alisema, nilimsikia akiongea kwa sauti kavu inayokwaruza, nilihisi kuchanganyikiwa, “huyu mwanaume angekuwa ni nani, mbona hisia zake zinakaribiana na ukweli” niliwaza.
“ Binafsi nimesikitika sana, ngoja nitamuuliza” Neema akasema, mimi bado nikiwa nasikiliza mlangoni, nikapata wazo la kuchungulia kwenye kile kitundu cha kitasa, nikainama na kusogeza jicho langu kwenye tundu la kile kitasa, lakini sikuambulia kuona chochote, ndani yake kulikuwa na funguo.
“ Nitaongea na kaka yako afuatilie ni kwa nini Gibson ameshindwa kwa makusudi, nini kipo nyuma ya pazia” Yule mwanaume akasema,
“ Haina haja, wala haitasaidia kitu, Gibson tayari ameshatoka, hata tukifuatilia haitabadili jambo lolote” Neema Akasema, hapo pakatokea ukimya kwa kitambo ulionitisha kidogo, kisha Neema akasema;
“ Acha nirudi kwa Gibson, atakuwa ananisubiri, nisijempa wasiwasi akaanza kunitafuta mwishowe akaja huku” Niliposikia hivyo nikarudi upesi kwenye ile nyumba ya ghorofa chumbani kwa Neema, alinikuta nikiwa naendelea kupiga Kinanda asijue kuwa nilikuwa namfuatilia, alipofika tukapiga stori mbili tatu, tuka-kiss mwishowe tukaagana.
Siku ya Fainali ikafika, ukumbi ulikuwa umebadilishwa, fainali ilifanyika katika ukumbi mwingine tofauti na ule wa awali, Mbali na Majaji kama ilivyokawaida siku ya leo kulikuwa na wageni mbalimbali akiwemo Waziri wa sanaa, utamaduni na Michezo, huyu alikuwa mgeni Rasmi, wageni wengine wa kiserikali pamoja na wadhamini wa Shindano lile, siti za upande wa mashabiki zilikuwa zimejazwa watu waliokuwa tayari kushuhudia fainali hiyo ya kusisimua, walikuwepo pia ndugu na wazazi wa washiriki walioingia Fainali, itoshe kusema kuwa ukumbi ulikua umesheheni. Nami nilikuwa miongoni mwa watu tuliohudhuria siku ile, nilishangaa kumuona Richard katika tukio lile, mwanzoni nilipomuona nilidhani nimemfananisha lakini nikapata uhakika pale alipotambulishwa na MC kwa kutumia majina niliyomjua nayo.
Richard alikuwa amebadilika sana, hakuwa yule Richard wa kipindi kile tukiwa kijijini niliyesoma naye, huyu wa sasa alikuwa ni Richard mtanashati aliyezalia Suti ya kijivu na tai iliyomkaa vyema, nywele zake zilikuwa zimechanwa vizuri kabisa, mkononi akiwa na saa nzuri ya gharama, nilishangaa alipotambulishwa kama Naibu waziri wa sanaa, utamaduni na michezo. Nilikumbuka dharau na kejeli zake kuhusu watu wasiopenda shule, nilikumbuka pia jinsi alivyokuwa akiponda muziki na wanafunzi tuliokuwa tunajihusisha na muziki. Yote hayo niliyakumbuka.
Mimi nilikuwa nyuma kabisa ya ukumbi ambapo kulikuwa na sehemu ya kutokea, huku tulikaa washiriki wote wa shindano la TGT, nilikuwa nimekaa karibu na Neema nikiwa nampa moyo na kumkumbusha mambo ya muhimu ya kuzingatia ili afanye vizuri jukwaani, nilikuwa na wasiwasi lakini sikumshinda Neema, yeye alikuwa amezidi, alikuwa akihisi miguu kulegea, shindano lilikuwa lipo mbioni kuanza, nikampa Neema Maji ya kunywa ili kupunguza Pressure, Wakwanza kutajwa alikuwa ni Semeni, kabla hajatokea, Video iliyojaza ukuta mzima wa jukwaa ilimuonyesha Semeni tangu akiimba siku ya kwanza mpaka nusu fainali, uimbaji wake ulikuwa wa kufurahisha ingawaje nusu fainali aliimba chini ya kiwango lakini hiyo haikumaanisha apuuzwe, kisha Mc akatangaza; “ Now Lady and Gentlemen, mabibi na Mabwana jukwaani anayepanda ndiye Semeni” Ukumbi mzima unalipuka kwa shangwe huku jukwaa likitoka moshi na kufanya watu wasilione vizuri jukwaa, kisha Semeni akiwa kavaa kiguo cha ajabu cha kisanii kilichoacha mapaja yake wazi kwa sehemu kubwa, huku akiwa amevaa viatu vyeusi vilivyofunika kuanzia mguu wake mpaka juu kidogo ya mapaja, usoni akiwa kavaa barakoa ya kidizaini iliyoziba macho yake tuu, pua na mdomo vikiwa wazi.
Akachomoza polepole akitembea kilimbwende kama paka mwenye maringo, kila alivyokuwa akisogea kuja katikati ya jukwaa ndivyo tulivyozidi kumuona vizuri moshi ukiwa unapotea polepole mpaka pale tulipomuona vizuri moshi ukiwa umeisha, Semeni akawa anaimba polepole kwa madoido huku akikatika, kisha akainama na kushika chini akawa anatembea kwa miguu na mikono huku uso wake wenye barakoa ukitazama upande wa hadhira, kwa kweli alikuwa amejiandaa, alikuwa akiimba huku akijipinda na kujipindua, akikata maumo na mwili, sauti yake akainyanyua huku akiamka pale chini, kisha akawa anaimba kwa sauti ya juu sana, Hakika alikuwa amedhamiria kuchukua tuzo, Nikamgeukia Neema, naye akanigeukia tukawa tunatazamana, niliuona wasiwasi wa Neema machoni pangu, nikataka kusema kitu lakini akaniziba mdomo.
Alipomaliza kuimba Semeni akajitambulisha kisha akaomba kura kwa watu, watu walimshangilia sana ungedhani mshindi amepatikana, kama mtu anamoyo mwepesi basi asingeweza kuendelea na mashindano, Ratiba iliyofuata ni Kikundi cha wachekeshaji wa Stand up Comedy kiliitwa kuburidisha watu, wakati hayo yakiendelea Neema alienda kujiandaa, walipomaliza wale wachekeshaji program yao, aliyekuwa akifuata ni Neema, kama ilivyokuwa kwa Semeni, Video iliyomuonyesha Neema ilijaza ukuta wote wa jukwaa la kutumbuiza, Neema alionekana akiimba tokea siku ya kwanza mpaka Nusu Fainali, kisha MC akatangaza kumkaribisha Neema, hapohapo Ukuta na sakafu ya jukwaa ikabadilika na kuwa na picha ya mawingu meupe yaliyochanganyika kidogo na rangi samawi, kisha jua likiwa linatoa mwanga mwangavu, Neema akajitokea akiwa kavaa vazi jeupe pee alafu kwa juu kwenye mabega kwenye nyuma kwenye mgongo kiliwa limedizainiwa kama mabawa ya malaika yenye kuwaka taa yakiwa yanapiga piga kwa madoido kadiri alivyotaka Neema, alikuwa kapendeza sana kuliko mwanamke yeyote niliyewahi kumshuhudia katika maisha yangu, pengine siku ile nilidhani sitakuja kushuhudia tena mwanamke atakayemfikia Neema,
Kisha akaanza kuimba, siku ile Neema aliimba kwa kiwango cha juu kabisa ambacho hata mimi sikutegemea. Aliimba zaidi ya Semeni, kila mara watu walikuwa wakisimama na kumshangilia, wala usingedhani watu walewale ndio walimshangilia mshiriki aliyepita, ndivyo binadamu walivyo, leo watamshangilia huyu na akija mwingine watamshangilia ikiwa tuu atafanya vizuri lakini jambo moja la kutambua ni kuwa, kura hazihusiani na kushangiliwa au kupigiwa makofi, kura wakati mwingine hutokana na mapenzi ya ndani ya mshabiki. Neema akamaliza, kisha nikaitwa kutumbuiza, nilivalia joho jeusi linaloburuzika kwa nyuma, usoni nilivaa barakoa yenye mapembe kwenye pembe za ya kichwa changu, siku ile nilitaka kuonyesha kuwa hakuna mwimbaji mwingine kwa watoto wa adamu isipokuwa mimi Gibson, ukuta wa jukwaa na sakafu yake vilikuwa na rangi ya kuzimu, yaani giza na mwanga hafifu na ukungu unapanda, makaburi machache na kaburi moja lilikuwa na ndege aitwaye Bundi, instrumental iliyokuwa ikipiga ilikuwa yenye kusisimua, nikatokea nikiwa kama naanguka kutoka mbinguni, kisha kwenye Ukuta pakaandikwa “ The Last Song Of Lucifer In Heaven” chini yake “ Wimbo wa mwisho wa Lusifa akiwa Mbinguni” ndio jina la wimbo niliouimba siku ile nikitumbuiza, na hiivi ndivyo nilivyouimba;
“ Mahali hapa sikutaka, niutwae utukufu wangu,
Uhuru wa nafsi kuupata, mlango uliowazi tangu,
Niondokane na haya mashaka, nizifurahie siku zangu,
OOOH! Lololo! Ninayo haraka, Naifuata ndoto yangu,
Lelelele! Yeyeye! Nataka takasika, mimi lusifa Mkuu,
Niimbe kwenye vilindi, sauti yangu ipae juu ya vilele vya milima,
Nipige zeze nalo Gitaa, kuliinua jina langu kuu,
Yote yapendezayo, yote mazuri ya kuvutia,
Yote yenye ladha, matamu nayo machungu,
Yote fanya ikiwa utayapenda,
Nitaondoka paradiso, kuufuata uhuru wangu,
Nitatengwa na wote, kuupigania uhuru wa wengi,
Uhuru ni mapenzi, upendo wa dhati hauna mipaka,
Kama unaupendo, imba nami wimbo huu,
Paradiso ipo moyoni, kwenye nafsi yenye uhuru,
Malaika imbeni wote, uhuru kuutetea
Majini pigeni Zeze, chezeni na kutetema,
Makerubi pigeni mbawa, tikiseni vyenu vichwa,
Binadamu wapi mbinja, vigelegele na nderemo,
Yeyeyeye! Yayayaya! Naondoka Paradiso”
Biti la wimbo linaendelea nikiwa nimepandisha sauti juu zaidi kuliko hapo awali,
“ Hatutadumu milele, milele! Milele! Milele!
Hakika tutaondoka! Wala hatutoonekana tena, tena! Tenayayaya!
Tucheze, Tufurahi, Tusiogope kuzifurahia siku zetu”
Kisha wakatokea washiriki wengine waliovalia majoho meupe, walikuwa ni washiriki wa shindano la TGT ambao tulikuwa tumeuandaa wimbo wa pamoja, ilikuwa kwaya kubwa sana, tukio lile lilikuwa la kihistoria, liliibua hisia za kusisimu kwa watazamaji,
Kisha tukaanza kunesa nesa, tukienda upande huu na upande, wala usingedhani waimbaji tulikuwa ni binadamu, sauti zilizotoka hapo zilikuwa zenye kushangaza, ilikuwa ya ajabu, wimbo niliutunga mwenyewe, ulikuwa ni wimbo wa maajabu ambao niliutunga, nikizileta fikra za zamani,
Nikasimama mbele ya wanakwaya wenzangu, mimi pekee nikiwa nimevaa joho jeusi wengine wakiwa wamevaa majoho meusi, nikasema;
“ Hii ni kwaya ya mwisho ya waliofukuzwa mbinguni, tumeimba kwaya hii kwa sababu kutuowa kwa kwaya hii ndio kulileta muziki duniani, aina zote za nyimbo na ushairi zilizopo duniani zililetwa na kwaya iliyofukuzwa duniani, zipo aina nyingi za muziki, lakini kwaya ya waimbaji waliomba na Lusifa ilikuwa na waimbaji elfu tatu, na kila mwimbaji ni aina ya muziki unaojitosheleza, sisi sio hao waliofukuzwa, isipokuwa hii ni sanaa tuu, tupo mbele yenu kuiwasilisha” Tukainamisha vichwa vyetu kisha kukatokea giza kuu baada taa za jukwaa kuzimwa, kisha likapulizwa baragumu, alafu zikafuata ngoma zenye msisimko, kisha ikawa inawaka taa moja moja kuanzia ile yenye mwanga hafifu zilizoko kwenye kingo za ukumbi, kila ilipowaka taa moja kufuata nyingine ndivyo tulianza kudhihirishwa, kisha taa Fulani ikawa inammulika mwana kwaya mmoja mmoja aliyekuwa akiimba, kisha kwa pamoja tukalipuka kwa sauti kuu tukiimba;
“ Katikati ya njia panda, ya kifo na uzima,
Katikati ya Daraja, la kuzimu na dunia,
Katikati ya shingo, ya uzazi na utasa,
Katikati ya Mpaka, wa Jehanamu na paradiso,
Yalayawa! Yalawaya! Huko ndipo tutasimama,
Kwenye njia kuu ya maisha, huko tutaishi,
Katikati ya kitovu, cha mama na mtoto,
Katikati ya kitovu, cha chemichemi ya maji,
Katikati ya kitovu, cha wema na ubaya
Katikati ya kitovu, cha imani na mashaka,
Cha!Cha! chacha! Kitovu cha uhai tutakimiliki”
Tulimaliza kuimba watu wakatushangilia, ulikuwa wimbo wa kushangaza ulioifanya hadhira kujiuliza maswali mengi, baada ya sisi kuwasilisha, aliyekuwa amebakia na Stelin, yeye kitendo cha kupanda pale jukwaani watu walimshangilia sana hata kabla hajaimba, kama binadamu nilijikuta nikiona wivu, wakati Stelin anaimba simu yangu iliingia ujumbe, nikausoma, “ Hongera sana Gibson, umeimba vizuri sana, nakuomba uje ukumbi wa mazoezi huku, utanikuta” Ujumbe ule ulikuwa unatoka kwenye namba ya yule mwanamke, mapigo ya moyo yakaanza kudunda kwa wasiwasi, kabla sijafikiri sana, ukaingia ujumbe mwingine, “ Nakusubiri, njoo tafadhali” nikainuka nikaenda ukumbi wa mazoezi nilipoelekezwa,
Nikamuona mwanamke wa makamo aliyekuwa amenipa kisogo, alikuwa kavaa mavazi meusi, wigi na kofia kubwa la mviringo la kimalkia, nilimkaribia nikiwa nyuma yake, kisha akageuka, nilikutana na sura ya mwanamke wa makamo aliyevalia miwani usoni,
“ Nakushukuru kwa kukubali ombi langu, nimefurahishwa na uelewa wako, wewe ni mjanja sana Gibson, kama usingenisikiliza ungekuwa umefeli mtihani mdogo ambao ungekugharimu maisha, usijali kwa kukosa hizi tuzo, ila kama nilivyokuambia mwanzoni utakuwa mwanamuziki mkubwa, hilo si ndilo unalotaka?” Yule mwanamke ambaye alipenda nimuite Aunt alisema akiwa na uso ulioharibiwa vibaya na vipodozi. Sikujuwa nimjibu kitu gani, akaendelea,
“ Semeni ni binti yangu, anapenda sana muziki, hizi tuzo kwake ni muhimu sana, ilikuwa lazima nikutishe wewe ili wabaki wale watatu, najua Atashinda, Neema hawezi kumshinda Semeni”
“ Vipi kuhusu Stelin?” Nikamuuliza,
“ Hilo limeshaisha, mshindi ni Semeni, kama ulikuwa hujui Semeni na Stelini ni mtu na mpenzi wake, mpaka hujaelewa nini kitatokea?” akasema,
“ Na vipi kama watu wakijua kuwa shindano liliharibiwa na wewe?” Nikauliza,
“ Hakuna atakayejua, labda wewe utoe hiyo siri, unakumbuka nilichokuambia endapo utatoboa siri?” akaniuliza, nikabaki kumtazama nikiwa nakumbuka maneno yake kwenye ile audio.
“ Sidhani kama upo tayari kumpoteza Neema, najua unampenda lakini pia sidhani kama upo tayari kuyaingiza maisha yako hatarini” Akasema, hapo akawa ananitazama, nikawa namuangalia kisha nikaangalia chini nikiwa natafakari kwa hofu,
“ Sikia usiwaze sana kijana mzuri, kuwa mjanja, tuachane na hayo, enhee!” Akasema,
“ Nahitaji mzigo wangu,” Nikasema,
“ Usijali, siku zote mimi ni mwaminifu kwa watu waaminifu kama wewe Gibson, ila ni mshenzi kuliko washenzi kwa watu wasaliti, kwa kazi uliyoifanya nitakuongezea dau nono” Akasema,
“ Tayari nilishafungua akaunti unaweza kwenda kuziweka” nikasema nikiwa nimevuta pumzi ndefu,
“ Sio niende kukuwekea, hapa ninapiga simu Benki wanakuingizia muda huuhuu” akasema, akatoa simu yake kisha akatoa maelekezo kwa mtu aliyekuwa akiongea naye kwenye simu, kisha akakata.
“ Unaweza kuangalia kwenye simu yako, muda mfupi itaingia pesa, utafurahi nakuahidi” Akasema, kisha akaniaga kwa kuhofia kuwa tumekaa muda mrefu na mtu yeyote angeweza kutuona, lakini wakati tunaondoka kuna mtu nilimuona akichungulia ingawaje sikumuona vizuri, nilitaka kumwambia Aunt lakini nikajizuia. Sikujua alikuwa ni nani, na alikuwa pale kwa muda kiasi gani, lakini hiyo haikunitia wasiwasi,
Nikarejea ukumbini, ulikuwa muda wa tuzo kutolewa, kila mara nilikuwa nikiangalia simu yangu kuona kama nitapata taarifa ya muamala uliongizwa kwenye akaunti yangu ya benki, aliyeshinda alikuwa ni Semeni, watu walibaki wameduwaa wakiwa hawaamini, wengi wao walitarajia angeshinda Stelin lakini haikuwa hivyo, niliwasikia watu wakilaumu sana waandaji wa tuzo kwa kusema kuwa wamempendelea Semeni, mitandaoni huko ndio palichafuka, tuzo za TGT zilipondwa vikali sana, hata hivyo hakuna kilichobalika, Neema alishika nafasi ya tatu, tena alipewa na Richard ambaye ni Naibu waziri, nilikumbuka vita yangu na Richard tukiwa tunasoma tukimgombania Alice, sasa naona vita hii alitaka kuihamishia kwa Neema baada ya kuniona nimepanda naye kuchukua zawadi, mbele ya macho yangu alimnong’oneza maneno Fulani ambayo sikuyasikia, nilijisikia uchungu sana lakini kwa vile alikuwa ni mheshimiwa nikashindwa kufanya lolote.
Baada ya tukio kuisha, Kaka yake Neema alituchukua na kutupeleka kwenye Hotel kubwa ya nyota tano kufurahia ushindi, tukiwa tunatoka, Richard alitufuata tena akamuita Neema na kujifanya anampongeza, kisha nikamuona akimpa simu, Neema akaipokea akaandika Namba zake kisha akamrudishia, nikiwa bado ninashangaa hasira zikiwa nimenikaba kooni, Nikamsikia Richard akiniita;
‘ Gibson! Kwema ndugu yangu” Nikamsogelea
“ Kwema, vipi!” Nikasema bila uchangamfu,
“ Naona umepambana mpaka umefika level hii, ngoja tuone” Akasema,
“ Huu ndio mwanzo tuu, hakuna wa kunizuia” Nikasema,
“ Ndio maana ukaimba nyimbo ya Lusifa, hahahah! “ akacheka kwa dharau huku akimuangalia mtu aliyekuwa akimuita, nafikiri alikuwa ni dereva wake.
“ Alice anakuja wiki ijayo, lakini kabla hajaja nataka nikupe maumivu kidogo, nataka nimchukue Neema kwa hii wiki ili ujisikie vile nilivyojisikia kipindi kile ulivyonichukulia Alice wangu” Akasema, akiwa ananitazama kwa macho ya hasira iliyojificha, Nikatabasamu bila ya kumjibu kitu, nikaondoka kwenda kwenye gari walipokuwa wananisubiri Neema na Kaka yake..
*****************
ITAENDELEA KESHO MCHANA.
Jipatie nakala ya Kitabu cha mlio wa risasi harusini Kwa Tsh 13,000/=
Namba
0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel
Tayari
Mwanangu anachelewa mno aiseeMkuu weekend hii, tuwekee