SEHEMU YA 42
Moja kwa moja nikajitazama kwenye vidole vyangu.
Nikakuta nimevaa pete ileile niliyovalishwa ndotoni.
Nikashtuka sana na kuwatazama watu waliopo chumbani kwangu ambao walikuwa wakipiga makofi na vigelegele, kwa haraka haraka nikaweza kumuona mama, mama Semeni, dada Penina na rafiki yake Fatuma, Lucy, Carlos na watu wengine watatu ambao sikuwafahamu.
Nikainuka pale kitandani nikiwa na hasira sana, nikaenda sebleni nao wakanifata nyuma, nikataka kutoka nje mama akanizuia huku akiniuliza,
"Unataka kwenda wapi mwanangu?"
Nikiongea kwa ukali,
"Mama huu ni udhalilishaji, huwezi kuingiza watu wote hao chumbani kwangu bila ridhaa yangu"
Mama akaongea kama kunipooza hivi,
"Ilikuwa ni surprise mwanangu"
"Surprise gani mtu nafanyiwa wakati nimelala mama? Uliona wapi bhana? Mmenikera sana"
Nikarudi nyuma na kumsogelea Carlos, kwakweli nilikuwa na hasira sana muda huu na sikumuogopa mtu yeyote wala kitu chochote. Nikamuuliza Carlos,
"Toka lini watu wanavishwa pete ya uchumba usingizini? Toka lini? Niambie upesi bhana, umenikera sana. Uchumba gani wa ndotoni"
Nikachukua kidole changu ili kuivua ile pete, nia yangu ni kumtupia nayo Carlos usoni ila ile pete haikuvuka ilikuwa imeng'ang'ania kwenye kidole changu, nikakaa chini huku machozi yakinitoka.
Dada Penina na Fatuma wakajaribu kunipooza, ila walishindwa kwamaana nilikuwa na hasira sana.
Mara gafla watu wote wakatoka pale sebleni na kuniacha mimi na Carlos tu, nadhani Carlos aliwaambia kuwa waondoke tuzungumze.
"Sasa Sabrina kilichokuchukiza ni kipi?"
"Usijifanye hujui Carlos, unajua kila kitu. Uliyoyafanya ndotoni kwangu huyajui wewe?"
"Yapi hayo Sabrina? Sijui chochote"
"Unajua, nimesema unajua tena unikome sitaki kuolewa na wewe, sitaki kuolewa na jini mimi"
Mara gafla nikasikia kicheko cha kutisha, nikaanza kuogopa na sikuwa na pa kujificha au kukimbilia pale sebleni, ikanibidi nikimbilie kwa Carlos aliyeonekana kama mtu kwangu.
Nikamsogelea nae akanikumbatia, nikajikuta nimekuwa mpole gafla na ule ukali wote wa mwanzo umepotea.
Kisha Carlos akanikalisha na kuwaita wale wa nje.
Nilikuwa kimya kabisa yani kama vile sio mimi niliyekuwa nafoka sana muda mfupi uliopita.
Carlos akaanza kutambulisha wale watu watatu ambao siwafahamu,
"Hapo kuna mama, baba na kaka yangu"
Mama alikuwa ameandaa chakula na wote wakajumuika kula kasoro mimi ambaye nilishindwa kula kabisa na kuwaacha wenyewe wale wamalize na wafurahie kitu
ambacho mimi nakichukia.
Walipomaliza kula, wakaongea mawili matatu na kuaga. Mama akauliza wanapokaa wale wazazi wa Carlos, wakamuelekeza ili na sisi tuweze kwenda.
Jioni ya leo nilikaa na kuiangalia ile pete ambapo nilitamani hata nikate kidole niweze kuitoa kwangu maana ilinikera sana ila sikuwa na la kufanya tu.
Muda wa usiku ulipofika napo sikujihisi kula na kuamua kwenda kulala hivyo hivyo.
Nikiwa nimelala, akaja yule kijana wa ndotoni na kusema
"Pole mke wangu mtarajiwa, najua una njaa na unahitaji kula. Nakuletea chakula upendacho."
Akaniletea keki na maziwa na juisi.
Nikajikuta nikila ile keki na maziwa, ila juisi nilikunywa kidogo na kuiacha.
Kisha akaniambia,
"Ulitaka kunitia aibu leo ila ni vizuri niliwahi kukudhibiti maana ungeniumbua kwa wageni wale, bora kwa mama yako na dada yako maana najua jinsi ya kuwaweka"
Nikamsikiliza tu,
"Hivi karibuni nitakuoa ila ndoa yetu haipaswi kuonwa na watu kamavile ila kuna viumbe maalum wa kushuhudia ndoa yetu"
Nikashtuka usingizini na kusema kwa nguvu,
"Viumbe gani hao?"
Sauti ikasikika,
"Ni majini wenzangu, wanaoishi baharini na mapangoni"
Nikaanza kutetemeka kwa uoga, chumbani kwangu kulikuwa na harufu ya marashi iliyotapakaa chumba kizima.
Nilipoangalia pembezoni mwa kitanda changu nikaona sahani yenye punje za keki, pakti ya maziwa na juisi iliyonywewa kidogo, hapo nikashtuka zaidi baada ya kugundua kuwa mambo yote yale ya kula na kila kitu yalifanyika chumbani kwangu, nikainuka ili nikimbie chumba. Sauti ikasikika,
"Unaenda wapi Sabrina?"
Nikazidi kutetemeka, wazo likanijia kuwa nimpigie simu Carlos, nami sikupoteza wakati nikachukua simu na kumpigia akapokea.
"Acha kunitesa Carlos"
"Nakutesaje Sabrina?"
"Unanitisha hadi naogopa kulala"
Nikamsikia Carlos akicheka sana kwenye simu hadi ile simu ikakatika, ila hali ikawa shwari mule ndani.
Sikutaka kulala tena mule ndani, nikatoka na kwenda chumbani kwa mama na kulala pembeni yake hadi kunakucha.
Mama alipoamka alishtuka na kuuliza,
"Umekuja muda gani humu?"
"Muda mrefu tu, ila mama nina ombi moja"
"Lipi hilo?"
"Naomba twende kwa wale watu ambao Carlos aliwaleta na kujifanya kuwa ni ndugu zake"
"Inamaana huwaamini?"
"Ndio siwaamini"
Basi mama akaniambia kuwa hakuna tatizo na kwavile walimuelekeza wanapoishi basi itakuwa vyema kama tukienda leo leo kabla hatujasahau zaidi hayo maelekezo.
Tuliamka na kufanya kazi za hapa na pale kisha kujiandaa kwa hiyo safari ya kuwafata hao ndugu wa Carlos.
Tuliondoka na kufika eneo ambalo tulielekezwa na wale ndugu wa Carlos, tukawapigia simu wakaja kutupokea na kutukaribisha sana.
Tulifika kwao na kuongea ya hapa na pale, nikaenda pembeni na yule ambaye alisema ni kaka wa Carlos.
"Hivi kweli Carlos ni ndugu yako?"
"Ndio ni ndugu yangu kwani vipi?"
"Ni ndugu yako kabisa?"
"Kwanini unamashaka?"
"Unajua anapoishi?"
Akasita kujibu kisha akaondoka bila ya kusema chochote.
Nikarudi tena ndani ambako kulikuwa na hao waliosema ni wazazi wake na mama.
"Samahani naomba niulize"
"Uliza tu"
"Eti nyie ni wazazi wake kabisa na Carlos?"
Mama akanikatisha,
"Ndio maswali gani hayo Sabrina?"
"Mmh mama nauliza tu"
Nikatulia tu huku nikingoja kujibiwa, yule aliyetambulishwa kama mama yake akaguna kwanza na kuanza kunijibu,
"Mmh! Sisi ni kama baba yake na mama yake mdogo"
"Kivipi? Inamaana nyie sio?"
"Hapana, sisi ni ndugu zake"
"Maana mmesema kuwa nyie ni kama, ndiomana nikapatwa na maswali hapa"
"Usijali, Carlos ni mtoto wetu sana. Tangia akiwa mdogo tulikuwa nae"
Mama nae akauliza,
"Kwani nyie ni wenyeji wa wapi?"
"Sisi ni watu wa Kigoma, Carlos amezaliwa hukohuko na kukulia hukohuko"
Kidogo nikajiridhisha ila bado sikuwa na imani nao kwa sana.
Tukaongea mengi na kuaga.
Tulipofika nyumbani tulimkuta dada Penina akiwa ndani na rafiki yake Fatuma, tuliwasalimia kisha Fatuma akaanza kuongea,
"Jamani kweli Carlos ni daktari wa ukweli mama, amenisaidia tatizo langu hata siamini"
"Kwani ulikuwa na tatizo gani?"
"Nilikuwa na tatizo la uzazi mama, yani kila hospitali waliniambia mimi ni mgumba. Kuna mganga nilienda akasema ndugu zangu wamenifunga nisizae, mwingine akasema ni lile jini mahaba lililonivaa kipindi kile ndio lilinifunga nisizae kwakweli nilikata tamaa. Siku ile tumetimuliwa kwa yule mganga mashuhuri sababu ya Sabrina niliumia sana tena sana ila Carlos kanitibia bure kabisa, dawa ile nimekunywa kwa siku moja tu nikaenda kukutana na mwenzangu kama ilivyoandikwa. Si alisema kuwa baada ya siku tatu nitapata majibu, basi leo nimechukua kipimo cha mimba na kujipima, nimekuta nina ujauzito wa siku. Kwakweli nimefurahi sana ndiomana nimekuja kuwaeleza habari hii"
Mama nae akaifurahia sana ile habari,
"Kwakweli bora nimepata mkwe daktari"
Dada Penina akadakia,
"Tena ni daktari wa madaktari"
Wakaendelea kuongea pale nami nikaenda chumbani kwangu kupumzika.
Baada ya muda kidogo nikapigiwa simu na Sam.
"Sabrina, tafadhari naomba tuonane haraka sana"
Nikakubaliana nae, kisha kisha nikatoka chumbani kwangu na kwenda kumuaga mama kuwa natoka mara moja kwani moyo wangu uliniambia kuwa kutokuaga kwangu ndio chanzo cha kutokea Sabrina wawili wawili huko njiani.
"Uwe makini Sabrina, kumbuka wewe ni mchumba wa mtu sasa"
"Usijali mama"
Nikaondoka pale nyumbani na kuelekea mahali ambako nimepanga kukutana na Sam.
Nilifika mapema kabla ya Sam kufika, nikatulia kumngoja afike na haikuchukua muda akawasili.
Akachukua mkono wangu ili kunisalimia ila akarushwa pembeni kama na umeme, akasogea na kuniuliza.
"Umeshika nini mkononi Sabrina?"
Nikamuonyesha kile kidole chenye pete.
Sam akasikitika sana na kusema,
"Umeitoa wapi?"
"Carlos kanivisha"
"Nawe ukakubali?"
"Nilikuwa nimelala Sam, alinivisha nikiwa usingizini"
Sam akazidi kusikitishwa na kile kitu.
"Sasa Sabrina umechukua hatua gani mpaka sasa?"
"Sijafanya chochote ila leo tulienda kwa ndugu wa Carlos"
"Hao ndugu sidhani kama wa kweli, kwanza niambie amekupa pete hiyo kwa misingi ipi?"
Nikaogopa kumwambia Sam kama amenipa kama mchumba wake kwani nilijua Sam atachukia tu.
"Sijui ila amenivisha tu"
"Na bado hatujachelewa Sabrina, nadhani twende leo kwa wale watu"
Nikainuka pale, Sam hakuweza kunishika hata mkono kwani alipigwa na shoti alipojaribu kunishika tena.
Safari ikaendelea ila tulipokuwa njiani nikapotezana na Sam, hata sijui nilipotezana nae vipi ila hakuonekana nikajaribu kumpigia simu hakupatikgna kwahiyo nikaamua kurudi nyumbani tu.
Kufika nyumbani nikamkuta Sam yupo nyumbani kwetu akiongea na mama,
"Huyu mwenzio ni mchumba wa mtu sasa kwahiyo usipende kumfatilia"
"Mchumba wa mtu kivipi?"
"Kwani huelewi maana ya mchumba wa mtu wewe? Ni mke mtarajiwa wa mtu"
"Ni nani huyo mumewe"
"Kumbe hujui, ni....."
Nikaingilia kati na kuleta habari za salamu kisha nikamvuta Sam,
"Umefika muda gani huku?"
"Uliponipotea nikajua lazima utarudi kwenu ndiomana nikaja huku moja kwa moja. Niambie ukweli Sabrina, au Carlos kakuvisha pete ya uchumba?"
"Hapana Sam"
"Niambie ukweli ili nijue jinsi ya kukusaidia"
"Kama ni kweli utanisaidiaje?"
"Niambie kwanza ni kweli au si kweli"
Nikiongea kwa unyonge,
"Ni kweli Sam"
"Kwanini umenificha muda wote Sabrina?"
Mara Carlos akawasili muda huo nyumbani kwetu, akatupita mimi na Sam pale nje bila ya salamu ila alimuangalia Sam kwa jicho kali sana na kuingia ndani.
Mara gafla Sam akaanza kuwashwa, alijikuna sana hadi nikamuonea huruma, akaondoka nyumbani kwetu huku anakimbia nikajaribu kumuita lakini hakugeuka nyuma kuniangalia wala nini, akapotea kabisa maana giza lilishaingia.
Nikarudi ndani kwa masononeko makubwa sana, nikawapita pale sebleni na kwenda chumbani kwangu halafu usingizi ukanipitia, kwenye ndoto nilimuona Sam tu siku ya leo, nilimuona Sam akiteseka na kuhangaika.
Nikashtuka na kusikia harufu ya marashi chumba kizima, sikutaka maajabu ingawa ni usiku sana nikainuka na kwenda kulala chumbani kwa mama.
Nikiwa nimelala tena, nikajiwa ndotoni na yule kijana wa ndotoni akasema,
"Karibia nakuja kukuchukua mke wangu, Carlos na Sam hawatahusika tena"
Nikamshangaa wakati Carlos ni yeye mwenyewe, nikaogopa sana.
Akaendelea kusema,
"Unaogopa nini sasa? Je nikikwambia kuwa muda huu upo chumbani kwako na si chumbani kwa mama yako kama unavyodhani? Na huyo uliyelala nae si mama yako bali ni mimi"
Nikashtuka tena toka usingizini na kuangalia mandhari ya chumba ilikuwa ni chumba changu na harufu ileile ya marashi. Mara gafla nikaguswa mgongoni na kuitwa jina langu.