Sipaswi kulaumiwa

Sipaswi kulaumiwa

Mwachiluwi

JF-Expert Member
Joined
Mar 10, 2022
Posts
25,258
Reaction score
48,589
Siku zote changamoto ndio zinatufanya nini tuamue kwenye maisha yetu, kwenye maamuzi hayo tunatakiwa tuwe na umakini wa kutoathiri hisia za wengine. Binadamu tunakosea mno kuishi kwa kukariri, usimhukumu mtu bila kujua chanzo cha kosa! kuuliza sio ujinga na kukaa kimya sio dawa ya kuuwepuka ujinga.

Naam nakukaribisha kwenye kisa hiki cha kusisimua, kisa ambacho nina imani kitakwenda kukuburudisha, kukusisimua na kukufunza mengi.KARIBU.

SEHEMU YA 1

Ni asubuhi tulivu ambayo jua lilianza kutoa mwanga kwa wanamtaa wa Geza, mtaa ambao ulisifika kwa idadi kubwa ya watu ambao hawakuyapatia maisha, ndio hawakuyapatia maisha ila hilo halikuwafanya kukata tamaa ya kuyapambania maisha yao na ndio maana isingekua ajabu alfajiri kukuta umati wa watu kwenye soko lao kuu la JIZOLEE , naam hao ndio Wanageza ambao waliyazowea maisha yao japo kuwa hayakuzoweleka, hadi kufikia saa kumi na mbili za asubuhi kunguru na ndege kadhaa angani walionekana wakirukaruka na kutoa kelele, kelele ambazo bila ya shaka zilikwenda kuwaibua vitandani wale walioendekeza usingizi.

Ndani ya chumba kimoja ambacho kimuonekano kilidhihirisha wakaazi wa humo hali yao ya uchumi ilikua duni , alionekena binti wa miaka 18 akijiangalia kwenye pande la kioo lililokuwa dirishani, alijitahidi kuzisuka nywele zake nyingi ambazo zilimpa shida mpaka kufikia hatua ya kukasirika na kuanza kutafuta kitu kwenye meza ndogo iliyokuwa chumbani humo.

" Laarah , natamani mikono yangu ingekua na nguvu nikakusaidia kuziweka vyema nywele zako ila ndio hivyo... " sauti kutoka nyuma yake iliyojaa maumivu ilimfanya aache kutafuta alichokusudia na kumfuata alietamka maneno yale, hakua mwingine bali ni mamaake aliyekua kitandani.

"Mamaa.....hupaswi kuongea yote hayo, mimi ni mkubwa sasa hivyo kuna mambo napaswa kuyafanya mwenyewe, tena pale nilikuwa natafuta mkasi ili nizipunguze hizi nywele" kwa sauti yake ya upole aliongea huku mikono yake ikiwa kwenye paji la uso ikipapasa chunusi zilizoisumbua sura yake.

Tabasamu mwanana ambalo bila ya shaka lilibeba hisia za maumivu alilionyesha kwa mtoto wake, alimtaka bintie alale kifuani kwake huku taratibu akijaribu kuchana kipande kidogo cha shuka kwa mkono wake wa kushoto, haikushangaza kuchanika maana shuka lenyewe lilikua laini kutokana na uchakavu, alijaribu kuzifunga nywele zile ila mikono illimsaliti kwa wakati huo.

"Mama unafanya nini? Mikono yako haina nguvu tena ya kufunga nywele zote hizii, ndio maana nataka kuzipunguza " alilalamika Larah kwa sauti yake ya upole iliyojaa deko.

"Utapunguza urembo wako binti yangu, naomba uziache!

"Heheee mama... urembo bila pesa? Umasikini wetu ndio unaficha vitu vingi vizuri tunavyofanya, hemu ona leo hii, masikini ukimsaidia ajiwezae basi utaambiwa unajipendekeza , kama hiyo haitoshi basi ukimpenda mwenye vyake pia utashukiwa uchawi au una tamaa ya mali, hivyo mamaangu mimi sijaona faida ya uzuri huu..... " Larah aliongea akionekana kuchukizwa na jinsi ambavyo watu waliwachukulia.

"Mwanangu hao ndio walimwengu na hayo hayapo kwao tu matajiri hata sisi masikini tumejivika hiyo tabia, Imani yangu inanituma ya kwamba utapata mtu sahihi katika maisha yako ambae hatakupenda kwa uzuri wako tu bali pia jinsi mwenyewe ulivyo"

"Mamaaa, ukianza kuuhubiri uzuri wangu najua hutomaliza, sasa mimi ndio hivyo kumekucha wacha niwahi sokoni " maneno hayo yaliambata na mfungo wa nywele zake kwa kutumia kipande kilekile cha shuka ambacho mamaake alichana, ingawa hazikukaa vyema ila alibana.

Alihakikisha anamuacha mamaake katika mazingira mazuri na salama kwa afya yake , kila kitu ambacho kingehitajika wakati yeye akiwa hayupo alimuwekea karibu yake, kwa upendo alimsogelea mamaake na kumbusu kwenye paji la uso na kuondoka kwa kumpungia mkono.

Safari yake aliipa kituo cha kwanza mbele ya chumba cha jirani yao ambae alikuwa akifua, hakuacha kumuachia maagizo mafupi na kuomba kutupiwa macho mamaake hadi pale ambapo angerudi kwenye mihangaiko yake, kwa vile waliishi vyema na majirani zao basi wala hakusumbuka sana, alijuwa mamaake yupo mikono salama.

**********

Nje ya soko kuu la JIZOLEE alikuwepo kijana ambae alionekena kumsubiri mtu kwa muda mrefu, macho yake hayakuacha kuangaza usawa wa njia kuu ambayo vyombo vya usafiri havikuchoka kupita, ghafla kijana yule sura yake ilichanua ua la tabasamu, tabasamu ambalo lilikwenda kuibua hisia za furaha kwa yule ambae alimtunuku, hata hivyo kijana yule hakuweza kustahamili kuwa pale hivyo aliona ni bora amfuate yule ambae alimzawadia tabasamu muda mfupi uliopita.

Kumbatio ndio ilikuwa salamu yao endapo wawili hao wangekutana , hawakujali macho ya watu waliokuwa pembeni mwao ila wao waliziendekeza hisia kufanya kile walichoamini kinawapa furaha, kwao tabasamu ilikuwa silaha kuu wakiamini ndio chaka la kuficha machungu wanayopitia, kwa vile muda ulikuwa umepotea kijana yule alikumbuka kujitoa mbio kwenye kumbatio lile na kuanza kumtazama binti aliyekuwa usoni kwa macho ya kugombeza, Larah alisanuka!

"Samahani sana Meddy , najua imekua kawaida ila unadhani nitafanya nini na ndio hali halisi ya maisha yangu" alijitetea Larah huku akiweka tabasamu zito la ulaghai mbele ya mwanaume yule ambae sura yake aliikunja kwa hasira.

"Tatizo nakuchekea Larah ndio maana unanipa hii adhabu, kamwe matatizo yako yasikufanye ukashindwa kujipangia muda mzuri wa kufanya kazi , heshimu sana kile ambacho kitakufanya uyafute hayo matatizo uliyonayo , hemu nihurumie na unipe moyo mimi ninaekupigania " Meddy aliongea kwa kumgombeza.

"Lakini Meddy na mamaangu ni muhimu pia , hivi unadhani bila yeye ningekuwa hapa leo hii? Mama ana nafasi kubwa mno kuliko haya matatizo ninayopitia, kumbuka mimi ndio kila kitu kwake" Larah alizidi kujitetea.

"Sijakataa hilo, ila unadhani usipofanya kazi utamhudumia vipi! Kula, kodi na dawa utapata wapi?...." aliuliza Meddy ila hakuna jibu alilopewa zaidi ya ukimya.

"Ok...tuachane na hayo, leo hakuna kukaa kwa mama Pili ukanuka masufuria ya ubwabwa , hata vijana wa Geza waliozowea kukutania basi leo hawatakuona, kuna sehemu mpya nakwenda kukupeleka, huko sitaki uzembe Larah! ni mwendo wa kuchapa kazi ili mifuko ivimbe" Meddy alitoa maelekezo.

"Weweeh! kwa maana leo miguu yangu haitosalia ndani ya soko hili la JIZOLEE ? Kwa tabasamu Larah alihoji na kulinyooshea mkono soko lililokuwa mbele yao.

"Kabisaaaa! Ila chonde mama, machachari yako yaweke kando , Larah nareje tena mapepe sitaki, kinachotakiwa ni kazi tu! " aliongea Meddy akionekana kuwa serious.

"Meddy mbona unasisitiza sana hadi nimeanza kuogopa! hii kazi ya safari hii ni kazi gani?" Larah alihoji kwa wasiwasi.

Meddy alisogeza mdomo wake sikioni kwa bibie Larah na kuanza kunong'ona maneno machache ambayo yalikwenda kuibua mshangao kwenye uso wa Larrah, alionekena wazi kushtuka huku wapita njia wakianza kumshangaa kutokana na mshangao aliouonyesha.........itaendeleaaaaaa.
 
SEHEMU YA 2

Kelele za wanunuzi na wapiga debe mbalimbali bado ziliendelea kurindima ndani ya soko la JIZOLEE , kila mmoja alikuwa wa maji kuipambania leo yake , kuna wale waliopishana na magunia ya bidhaa mbalimbali, matusi na lugha za ajabu ndizo ambazo zilitumika na wengi yaani kiufupi soko lilijaa hekaheka.

"Kuna watu wakianza kuyapatia maisha husahau hata walipotoka" alianza kulalamika mamantilie mmoja huku akihangaika kushusha sufuria la maharage jikoni.

"Hheeh usinambie shoga! Kwamba umeachwa tena ? Alihoji mwenziwe ambae alikuwa pembeni akichoma vitumbua.

"Si kile kitoto cha kuitwa Larah, nilikipokea hapa kikiwa kidogo na kukifundisha kazi, leo hii kimetanuka kifua ndio kinaleta dharau? Eti mtu unaletewa taarifa asubuhi kuwa hatofika kazini, hii haki kweli? Mimi kazi zote hizi nitafanya vipi? Mama Pili alinung'unika kwa uchungu na hasira.

"Mmh shoga huruma yako ndio imekuponza. Nilikwambia zamani kuhusu yule mtoto ila uliziba masikio , ona leo yanayokukumba, watoto wengine wanataka mteremko hasa yule ambae damu yake bado inachemka!

"Lakini alikuwa mchapakazi, wewe mwenyewe ulikuwa shuhuda wa wateja kwa namna walivyokuwa wanamiminika kwa sababu yake, ona leo hii moja tu..hata nzi hajapita? Na huyu Meddy sijui kapotelea wapi! alizidi kulalamika mama Pili.

"Meddy wa nini tena?

"Aniletee kifaa kipya, Unadhani bila ya hivyo nitatoboa hapa! Watoto wazuri kama Larah ndio kivutio cha kazi zetu hizi!! Maneno ya mama Pili yalimuacha mdomo wazi mwenzake na mwisho aliishia kushika hamsini zake.

**********

Usafiri wa bodaboda ndio ambao uliwafikisha kwa haraka sehemu waliyokusudia, walishuka na kufanya malipo kama ambavyo walikubaliana na dereva, walianza kuisogeza miguu yao kwenye jengo kubwa la ghorofa mbili lililokuwa kando yao, nje ya jengo hilo kulikua na bango kubwa lenye maandishi yaliyosomeka * PERFECT ADVERTISING AGENCY *

"Meddy una uhakika nitapokelewa na nguo hizi? Alihoji Larah huku hofu ikitawala usoni mwake haswa pale alipoanza kujikagua mavazi yake na kuyashuhudia jinsi yalivyopauka.

"Hemu tulia mrembo wangu, hapa kinachotakiwa ni kazi tu" Meddy alimtoa hofu na kumshika mkono hadi kwenye mlango mkubwa wa kioo ambao ulifunguka wenyewe (automatic)

"Naogopa mwenzio.......sijawahi hata kuwaza kama ipo siku nitaukaribia huu mjengo , sikwambii kuingia humu ndani" Larah alimnong'oneza Meddy huku mikono ikiwa imemshikilia kisawasawa.

Mshangao wa uzuri na ugeni wa jengo lile katu haukumuacha Larah salama, macho yake aliyazungusha kila pembe yakishangaa utundu wa namna jengo lile lilivyopambwa , kila kitu kwakwe alikiona kigeni maana alizowea kusimuliwa au kuona kwenye televisheni tena ya jirani, alijisikia vibaya pale alipoona ni yeye pekee jengo lile alionekena kituko, watu wote ambao alipishana nao walitupia mavazi ya kuvutia na yenye hadhi isipokua yeye tu, alijionea tabu maana hata harufu yao pia haikua ikilingana na yake.

"Habari yako sister ....sisi ni wageni wa Madam Siti " alijitambulisha Meddy mara tu baada ya kufika mapokezi.

"Ahaaa! Kijana unaitwa nani? " aliuliza mhudumu yule bila kuitikia salamu, alimkagua kwa macho Meddy na bibie Larah huku simu ya ofisi ikiwa sikioni.

"Meddy" alijibu kwa kujiamini.

"Mmmh! Larah mimi nitaweza kufanya kazi hapa !! Maana hata salamu inaonekana haina thamani!" alijiuliza kwa sauti ambayo alihisi ni yeye pekee aliisikia ila kumbe ilipenya hadi kwenye masikio ya Meddy ila sio kwa Mtu wa mapokezi.

"Hupaswi kuogopa Larah, hii ni kazi kama ambavyo kazi nyingine zinafanywa, kikubwa ni kuweka imani kuwa utaweza haijalishi changamoto zipi utapitia , unatakiwa kuomba Mungu uvuke salama kwenye kila kizingiti ili mradi lengo kuu lifikiwe,Larrah wewe ni mpambanaji, hodari, mvumilivu, una busara na mwenye akili licha ya kwamba hukutulia darasani" maneno ya Meddy yalimfanya Larah ashtuke kwenye fikra zake na kubaki akimuangalia kwa jicho la kutahayari.

"Ni kweli Meddy napaswa kupambana kwenye hili, siku zote masikini huwa hachagui kazi ilimradi iwe inamlipa walau pesa chache ya mlo wa siku, nina imani nitaweza japo kuwa hii kwangu ni ngeni na inaonekana kuwa ngumu" kwa sauti ya chini Larah aliongea kwa kujiamini maneno ambayo yalikwenda kuibua tabasamu la kijana Meddy akiyekuwa pembeni yake.

"Ndio maana nakupenda Larah wangu" Meddy alimjibu huku akimzawadia kumbatio mwanana.

Wakiwa kwenye kumbatio hilo lililodumu dakika chache walishtuliwa na kikohozi ambacho kiliwafanya waache walichokua wanafanya, mhudumu aliwatazama kwa macho yaliyojaa kejeli na wivu, Meddy alilifahamu hilo ila wala hakua amelitilia maanani.

"Mnaombwa kusubiri pale kwenye bench , madam Siti atafika muda sio mrefu" baada ya kimya kifupi kilichoambatana na mtazamo Mhudumu alitoa maelekezo.

Iliwachukua dakika kumi kumsubiri waliyemfata na hatimae Madam Siti alikua mbele yao , maamkizi baina yao yalichukua nafasi yakiambatana na utambulisho, kiukweli Larah alijisikia amani baada ya kuona Madam Siti ni mcheshi tofauti na alivyodhani, Madam Siti aliwapa maelekezo ya sehemu ambayo wanapaswa kwenda huku akiwa mbele yao kwa hatua kama tano hivi.

Safari yao ilikomea kwenye ofisi ambayo ilitambulishwa kwa kibao kidogo kilichoandikwa CREATIVE DEPARTMENT kikining'inia mlangoni, walipoingia ndani Larah alishangazwa na ukubwa wa ofisi hiyo ambayo iligawiwa sehemu mbalimbali. Sehemu ambayo walisogea wao ilikua mithili ya duka la nguo, watu wasiopungua watano walikuwemo wakiwa na kazi ya kuyapangilia vyema mavazi yaliyokuwepo, Larah alijikuta akifurahia kuwa pale kwani aliamini ile ni sehemu ambayo ingeweza kutimiza kile ambacho alikiota siku zote.

"Larah, nadhani kila kitu Meddy alikueleza, kinachotakiwa hapa ni kazi tu, na endapo kazi hii utaifanya kwa ubora ambao unatakiwa basi itakua ni njia yako ya kuelekea kwenye mafanikio na ukivuruga basi ukumbuke kuwa utakua umeitia hasara kubwa kampuni yetu na kwenye hili basi kampuni haitakufumbia macho" Madam Siti aliongea kwa utulivu huku akiwa makini kumsoma bibie larah.

Tumbo la joto liliombatana na hofu lilianza kumsumbua Larah, maneno ya Madam Siti yalimuogopesha kiasi cha kutaka kuikataa kazi ile, alimtazama Meddy kwa jicho la kwanini ulinileta huku, mwisho aliyafikiria maisha yake na kujikuta akiikubali kazi ile na kuamua kuifanya kwa moyo wake wote.

"Nakuahidi Madam, nitafanya kazi kama vile ambavyo inatakiwa au zaidi ya hapo na wala sitokwenda kinyume na matakwa yenu" maneno yaliyojaa ujasiri yalimtoka Larah .

Madam Siti na Meddy walimfurahia Larah kutokana na maamuzi yake, walijikuta wakimpa moyo na kumuondoa hofu juu ya kazi hiyo, taratibu alielekezwa vitu mbalimbali kwa kila sehemu ambazo zilipatikana kwenye ofisi ile, Larah alipewa mafunzo machache kuhusu tangazo ambalo atalifanya kesho yake na baada ya hapo alitakiwa kuwasili siku inayofuata kwa ajili ya kuanza kazi ambayo ilimpeleka.....itaendeleaaaaaa.
 
SEHEMU YA 3
Usiku ulitia nanga katika mtaa wa Geza, kwa wale waliobarikiwa kupata walichokitafuta mchana kutwa basi ulikua ni muda sahihi wa kukitumia wakiwa pamoja na familia zao, wapo walioamua kuutumia usiku huo kwenda kumbi za starehe, vilabu vya pombe na hata kukaa maskani kupiga soga ambazo zingeusogeza usiku mbele , hata hivyo waliokosa cha kuweka mdomoni usiku huo waliamua kulalia maji huku wakijipa matumaini ya kwamba kesho Mungu angewaona na kuwabariki chochote , hawakukata tamaa.

Licha ya ugumu wa maisha ambao alikuwa akipitia ila hakuwahi kuwaonyesha watu maumivu ya changamoto anazopitia kwenye uso wake, tabasamu ndio ilikuwa silaha pekee ambayo angeishika kuwaadhibu wale ambao walitamani aanguke, siku hiyo silaha hiyo aliiweka chini na kushindwa kabisa kuvumilia kile kinachomtesa moyoni mwake.

"Larah binti yangu una nini? Mbona wa tofauti sana leo! Tokea umerudi kibaruani kwako naona hujachangamka kama siku zote" mamaake alihoji kwa sauti ya upole huku akizidi kumkagua kwa macho bintie aliyekuwa pembeni na sahani ya chakula ambayo aliishika muda mrefu .

Machozi ndio yaliyotoka na kwenda kurowanisha wali ambao ulikatiwa kachumbari, hata mamaake tayari alipata jibu la swali ambalo alimuuliza bintie, ingawa alihitaji maelezo ila hakufanya pupa maana alijua kuwa mpaka bintie akilia basi kuna jambo kubwa linamtatiza akilini mwake na yeye mwenyewe kashindwa kulitatua.

Kufumba na kufumbua tayari Larah alijimwaga kwenye mwili wa mamaake uliokua kitandani, ingawa hakuenea wote ila hilo halikumfanya asijisikie faraja , alijua kukitumia alichojaaliwa, alilia hadi alipohisi kutosheka .

"Mama nimekua mdhaifu sana pale ninapotakiwa kufanya maamuzi hasa ukiwa na wewe unahusika, siwezi kwenda mbali na wewe mama hata iweje, naamini umasikini hautatuua mama si ndio?" Larrah aliamua kufunguka huku macho yake yaliyorowana machozi yakimuangalia mamaake .

"Kuwa muwazi mwanangu, mimi ni mgonjwa wa mwili ila akili na fikra zangu bado zipo sawa, cheo ni dhamana napaswa kukuongoza vyema kabla walimwengu hawajaichukua hii nafasi , Larah endapo machozi yatatoka kwenye nyumba yake na yakaonekana na mtu wa nje hiyo ni ishara kwamba umeshindwa, Larah..... hupaswi kulia mwanangu " Mama Larah aliongea hayo akionekana kuchukizwa na kilio cha bintie, haraka sana Larah alivuta fulana yake na kuyafuta machozi yake kitendo ambacho kiliibua furaha kwa mamaake ingawa hakuionyesha usoni.

"Larah , binadamu hamna kitu mwanangu, leo nipo kesho nitawafata waliotangulia, kuna wakati kwenye maisha tunahitaji kufanya maamuzi hata kama ni mabaya, usiogope kufanya maamuzi kwa sababu maamuzi mazuri ni uzoefu wa maamuzi mabaya unayofanya mara nyingi.” mama Larrah alianza darasa kwa bintie .

" Mama sio kwa hili ! mimi najali utu zaidi, uliwahi kuniambia kuwa masikini si yule tu ambaye hana kitu bali ni yule ambaye anacho lakini anataka zaidi, sitaki kuwa miongoni mwao mama" Larrah alizidi kushikilia msimamo wake.

" Larrah usiishi kwa kukariri, Gari la maskini ni miguu yake mwanangu, kumbuka kuwa maamuzi unayofanya leo ndio yataonyesha kesho utakuwa wapi, itengeneze kesho yako kwa maamuzi unayochukua leo. Maisha yako baada ya miaka kumi, ishirini au hamsini ijayo yanategemea sana maamuzi unayochukua leo, mimi ndio nimeishia hapa mwanangu na haya ni mavuno ya maamuzi yangu niliyoyafanya jana" Mama Larah alizidi kumfunua akili bintie.

"Mama...Meddy kanitafutia kazi nzuri sehemu nyingine ila sifikirii kama ile kampuni ni sahihi kwangu, ukizingatia ni nje kidogo ya mji huu wa Geza, kumbuka wewe ni mgonjwa mama, unataka kuangaliwa kila muda" Larah aliongea kwa hisia za uchungu.

"Fanya maamuzi leo hata kama ni mabaya, ingawa maamuzi yako yanaweza kukupa maumivu au kupoteza faraja yako, kukufanya ukosane na watu lakini ni bora kwa sababu kuna hatua utakuwa umepiga kuelekea kwenye mafanikio yako, Larah mimi ni mgonjwa ndio ila wewe kua mbali na mimi kwa jambo la faida haitaathiri chochote, ninachoshukuru tumeishi vyema na watu hivyo sifikirii kama nitapata tabu sana"

"Ni kweli hii kazi itanilipa tofauti na ilivyokua kwa mama Pili ila nakuwazia wewe mama, ni kweli watu wapo ila binadamu sio watu wa kutabirika hata kidogo, yawezekana akakuonyeshea tabasamu usoni ila moyoni mwake hali ikawa tofauti"

"Larah mwanangu, mimi baraka zote nimekupa ukafanye kazi, naelewa kila kitu mimi hivyo wala sitopata tabu, muhimu unifanyie kile ninachokueleza basi sitashindwa kujisaidia baadhi ya mambo".

"Haya amka mamaangu ukakistiri chakula" Mama Larah alimnong'oneza bintie.

Larah hakua na hamu ya kula kwa muda ule, ni kama vile maneno ya mamaake hakuyasikia maana hapohapo alijitoa mwilini na kusogea pembeni huku akivuta shuka na kujifunika gubigubi.

"Larah... wee Larah, fanya kuamka uje ukistiri chakula kabla hatujakerana" Mama Larah alifoka baada ya kuona bintie kajilaza.

"Kwani chakula si natafuta mimiii!! kuna harasa gani kumwaga? Alijisemea Larah kwenye nafsi yake huku akiendelea kujilaza bila kusema chochote.

"Weeh Larah !! huna huo usingizi naomba uinuke au unaona siwezi kukufanya chochote " Mama Larrah alizidi kufoka maneno yaliyokwenda kumshtua Larrah, hakutegemea kama mamaake angesema vile .

Hapohapo alikifuata chakula na kuanza kula huku hasira ikiwa usoni mwake, mamaake na yeye alimtazama kwa jicho hilohilo la hasira , Larah alikula haraka haraka ili amalize alale.

"Wakati wewe unakula haraka haraka ukiwa na hasira kuna wenzio huko nje hadi muda huu hawajui watakula nini, na hata wangefanikiwa kupata chakula basi wangeweza kufuata utaratibu mzuri wa kula kwa kumshukuru Mungu na kuifurahia neema hiyo" Mama Larah alivunja ukimya, maneno hayo yalimsuta Larah na kujiona mkosefu mbele ya Mungu na mamaake.

"Mamaa, nisamehe kwa kumkaribisha shetani kwenye akili yangu, sikupaswa kufanya yote haya kipenzi changu, nimekosea mno naomba unisamehe mama"

"Hukupaswa kabisa kufanya yote haya , mimi hujanikosea hata kidogo ila kuna Mungu ambae unapaswa kumuomba msamaha unapomkosea, ulikuwa huru na maamuzi yako baada ya kupokea ushauri mzuri kutoka kwangu, Larah kamwe usije ukasahau tulipotoka, USIKU MWEMA " Mama Larrah alimaliza kuzungumza na kujifunika shuka lake huku akiutafuta usingizi.

Nafsi ya Larrah ilibaki kwenye majuto, alijilaumu kwa kitendo chake cha kuonyesha hasira za wazi kwa mamaake ikiwa hakuna kibaya alichofanyiwa, aliilaumu nafsi yake pia kwa kumuingiza kwenye mawazo mabaya ya kususia chakula, alijikuta akikumbuka nyakati ambazo waliishi kwa kushindia uji au maji, chozi lilimtoka.
************
Siku mpya iliwafikia kwa mara nyingine wana mtaa wa Geza, kama kawaida yao hawakusubiri kamwe majogoo waliopewa jukumu la kuwaamsha yafanye kazi yao , kiukweli vitanda vyao viliwachoma! hata kama hawakujua kwa kwenda ila kwao kukaa ndani kusubiri riziki iwafikie ni mwiko. Pirika zilizidi kwa siku hiyo maana watu wengi walikua na shauku ya kuianza wiki kwa kishindo, ilikuwa ni Jumatatu yenye hekaheka, kelele za watoto wasiopenda kwenda shule pia zilisikika kwenye vyumba vya wengi yaani kiufupi Jumatatu ilijulikana kwa mtindo huo.

Baada ya kumaliza kumsafisha mamaake alichukua bakuli la uji na kuanza kumywesha taratibu hadi aliposhiba, alihakikisha anasafisha sehemu ambazo zilichafuka na kumuwekea mazingira rafiki mamaake kwa muda ambao hatokuwepo, kwa vile dakika zilikua zimepotea alijiandaa haraka ili awahi asije akamkera muajiri wake mpya, kabla ya kutoka alimsogelea mamaake na kupiga magoti mbele yake........ITAENDELEAAAAAA

JEE ? UNAJUA LARAH ANATAKA KUFANYA NINI KWA MAMAAKE, KWANINI HAPASWI KULAUMIWA? BADO TUNA SAFARI NDEFU !! USICHOKE KUUNGANA NA MIMI SEHEMU IJAYO.
 
*SEHEMU YA 4 *
Baada ya kumaliza kumsafisha mamaake alichukua bakuli la uji na kuanza kumywesha taratibu hadi akamaliza, alihakikisha anasafisha sehemu ambazo zilichafuka na kumuwekea mazingira rafiki mamaake kwa muda ambao hatokuwepo, kwa vile muda ulikua umepotea alijiandaa haraka ili awahi asije akamkera muajiri wake mpya, kabla ya kutoka alimsogelea mamaake na kupiga magoti mbele yake huku akimtazama.

"Mamaa, najisikia vibaya mno kukuacha mwenyewe muda mrefu" aliongea Larah kwa sauti ya upole yenye huzuni.

"Larah mwanangu, maisha yanatafutwa na siku zote hakuna kupata rahisi, mimi jua limezama ila wewe ndio kwanza lipo utosini mwanangu , ukiacha majirani waliotuzunguka basi jua kuna Mungu ambae hajawahi kumtupa mja wake, nenda mwanangu Mungu atakuongoza kwenye kila hatua yako " Hayo ni maneno ya kutia moyo yaliyotoka kinywani kwa mama Larah.

Larah hakuona sababu ya kuendelea kubaki eneo lile , alimbusu mamaake na kutoka nje huku akimpungia mkono, kama kawaida yake alisogea chumba cha jirani na kugonga mlango , alitoka mama wa makamo akiwa kwenye mavazi ya kupendeza, bila ya shaka alijiandaa kwa safari.

"Shikamoo mama Sindi" alisalimia Larah kwa upole na adabu zote.

"Marahaba...." aliitikia mama yule ambae alikua bize kuufunga mlango wa chumba chake na kufuli.

"Aah...aa...ma....mama Sindi kumbe unaondoka ? Aliuliza Larah kwa kubabaika.

"Ndio kwani vipi? " jibu hilo la mama Sindi lilimshangaza Larah kwani halikutoka kama ambavyo alizowea, kiufupi kulikua na ukali ndani yake.

"Ni...niii...nikajua upo umtupie jicho mamaangu hadi nitakaporudi" ingawa maneno yaligongana ila alijitahidi kutamka.

"Mmh! shogaangu.... mimi leo sipo na kurudi kwangu inawezekana ikawa usiku kabisaa labda umjaribu mama Sikujua" alijibu mama Sindi na kuondoka bila kusubiri neno.

Larah alihisi miguu kumuisha nguvu, kila alipotaka kupiga hatua kukielekea chumba cha mama Sikujua miguu yake ilikua mizito, alimuogopa sana huyo na yote ni kutokana na tabia yake ya umbea na kukuza mambo lakini pia alikua mbabe, alijikokota na kusogea hadi chumba alichoambiwa, mikono yake iliishia hewani ikijishauri kupiga hodi, ghafla mlango ulifunguliwa na mama Sikujua alionekena akiwa kabeba beseni lenye vyombo vichafu.

"Ehee !!mtoto mzuri naona leo umevunja kabati!! Sijui nani unakwenda kumchuna maana sio kwa kupendeza huko, hadi nywele umezichana vyemaa!!haaloooooo" Mama Sikujua alianza kumchambua Larah aliyekua kasimama akijichekesha japo kua maneno yalimuudhi.

"Kuna kazi naenda kuifuatilia , sasa nilikuwa naomba unitazamie mamaangu hadi nikirudi maana mama Sindi hayupo" Larah aliongea kwa upole huku akijifikicha vidole vyake.

"Weeh Larah , unanijua vizuri mimi kushinda ndani siwezi au ndio kunitafutia lawama? Alianza kuropoka mama Sikujua.

"Sio hivyo, ila nitajitahidi kuwahi na kile ambacho nitakipata basi sitoacha kukuzawadia" Larah alizidi kushawishi.

Maneno hayo kutoka kinywani kwa Larah yalikwenda kuibua tabasamu zito kwa mama Sikujua, yaani ni kama vile Larah alicheza na akili ya huyu mama kwani hajawahi kuacha jambo la kulipwa limpite, kiufupi pesa ilikua ni sabuni yake yake ya roho , aaah Larah sisi ni majirani , tena majirani ambao tumeishi vyema na mamaako , sio vyema kumuangalia yeye kwa malipo, mimi nipo... wewe nenda ukirudi utakachojaaliwa utanipa maana ndio navunja safari zangu" Mama Sikujua alijitetea ili asionekane anapenda pesa, anaachaje kukoga sasa ikiwa ni sabuni ya roho😁

Larah alishukuru na kuondoka kuelekea barabarani ambapo angekutana na Meddy kwa ajili ya safari yao, njia nzima alikuwa na shauku ya kuanza kazi kwa nguvu na ari zote, alitembea kila mwendo ili afanane na warembo ambao aliwaona ofisini kwao jana yake.

"Nitahakikisha nakua bora zaidi ya wale wote ambao walifanya nao kazi huko nyuma, baada ya hapo nitakua Larah mpya ndani ya Geza, nitamtibu mamaangu na atainuka tena tuishi kama zamani" Larah hakuacha kuwaza na tabasamu zito likiwa usoni mwake.

Siku hiyo Larah hakupokea malalamiko ya kuchelewa kutoka kwa Meddy maana alifika kama ambavyo walipanga, alisifiwa kwa mabadiliko aliyoyaonyesha kuanzia kujali muda, mpangilio wa mavazi na mwendo . Waliamua kuchukua bodaboda ili wafike haraka .

"Larah, safari yako ya maisha ndio inaanza leo, kama ni mwendo basi hii ndio hatua ya kwanza, elewa ya kwamba utakapofanya kitu ambacho kitairidhisha kampuni hii basi uhakika wa kuajiriwa moja kwa moja upo, wala haitakua kazi ya muda tena " Meddy hakuacha kumpa maneno ya hamasa kipenzi chake mara tu walipoingia kwenye jengo lile.

"Sitakuangusha Meddy, naamini tangazo ambalo nitalifanya leo litakwenda kufungua ukurasa mpya wa maisha yangu, Meddy .....wewe ni mtu muhimu sana kwangu hivyo napaswa kuziunga mkono juhudi zako, SITAKUANGUSHA" Larah aliahidi.

ZURI FASHION ndio ambao waliingia mkataba na PERFECT ADVERTISING AGENCY kwa lengo la kutangaziwa nguo zao mpya mbazo wataziingiza sokoni, waliichagua kampuni hiyo kwa sababu ilikua na ushawishi mkubwa ulioambatana na umaarufu kwenye kufanya matangazo ya biashara mbalimbali, ukiachana na hilo PERFECT ADVERTISING AGENCY walikua na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii hivyo ingekua rahisi watu kuhabarika kupitia wao lakini pia waliwaunga mkono wale wote ambao waliwafanyia matangazo kwa kuwauzia bidhaa zao hapohapo kwenye maduka ya taasisi.

Kwa vile walitaka kubadili muonekano kwa watu basi safari hii bahati ya mtende ilimuangukia Larah , kutokana na akili yake kua nyepesi alifanikiwa kuyashika haraka yale ambayo alitakiwa kufanya kwenye tangazo hilo, ilichukua zaidi ya masaa matatu binti huyo akiandaliwa kimuonekano na kiutendaji.

Ule muda wa Larah kuonekana jukwaani uliwadia, wafanyakazi wengi wa PERFECT ADVERTISING AGENCY walikuwepo kuhakikisha tangazo hilo linafanyika vizuri, kila mtu alikaa kwenye nafasi yake. Watu wa Media na wao hawakua nyuma ili kuleta ubora wa matukio ambayo yatajitokeza, Hata wafanyakazi wa ZURI FASHION baadhi yao walikuwepo ili kushuhudia namna kazi yao inafanywa .Muda mchache mbele jukwaa liliwaka , kila mtu alishangazwa na muonekano wa Larah , nyuso za mshangao ziliwakumba wote ambao walikua ukumbini wasiamini wanachokiona hususan waliomuona jana yake.

Ukumbi ilifunikwa na uzuri wa bibie Larah , uzuri ambao ulichangiwa na aina ya nguo ambayo aliivaa, Larah alitupia nguo fupi ya rangi buluu iliyokoza ambayo iliishia magotini mwake, nguo ilizidi kupendezeshwa na stones ndogo zilizog'aa vyema kifuani kwake , kwa vile mwangaza uliotengenezwa jukwaani hapo ulikua hafifu basi Larah alionekana kuwaka hadi sio poa , kama hiyo haikutosha nguo hiyo iliwekwa manyoya manyoa madogo ya buluu ambayo yalikua mikononi na sehemu ya magoti, kiatu cha juu alichovaa chenye rangi ya Silver ndio kilizidi kumfanya aonekane mithili ya twiga atembeae nyikani, hata pochi ambayo alibeba ilikua ya rangi silver yenye stones za rangi buluu , hemu vuta picha hapo na zile nywele zake ndefu ambazo siku hiyo zilifungwa nyuma kwa mtindo mzuri ikisha zikafungiwa na kibanio chenye ua rangi ya Silver, nyie kumbe maisha ya umasikini yanaficha muonekano wetu eeeh, Larah alimshangaza kila mmoja kwa uzuri wake na jinsi alivyopendeza.

Zowezi halikuishia hapo tu , Larah alibadili muonekano wa mavazi mbalimbali ambayo yataingizwa sokoni na ZURI FASHION. Hata jukwaa lilikua likibadilishwa muonekano kutokana na aina ya nguo ambayo alivaa. Watu wa Media walikua na kazi ya kuhakikisha kuwa wanatoa picha na video ambazo zingekwenda kuwavuta wateja.

Hatimae zoezi lilifika ukingoni, Larah alipokea pongezi kutoka kwa watu mbalimbali , alifurahi mno kuona kazi yake ya kwanza imekwenda vyema huku wengi wao wakiifurahia , alibaki kutabasamu peke yake huku macho yake yakiangaza kila kona ya holi lile kumtafuta Meddy, alimuona Meddy wake akiwa kajitenga kidogo na watu , akiwa anaanza kupiga hatua za kumsogelea ghafla alishtushwa na mguso wa bega, aliigeuza shingo yake na mwili wote nyuma kwa lengo la kumjua aliyemshika.

Mapigo yake yalikwenda kasi baada ya kukutana na sura ya mwanaume ambae alikua akitabasamu, sio tabasamu tu ambalo lilizua taharuki ya mapigo ya moyo wake bali uzuri na usmati wa mwanaume yule pia ulimfanya abaki kwenye mshangao.

"Hongera kwa kazi nzuri Larah" mwanaume huyo aliongea hayo kwa sauti nzito yenye msisimko ambao ulimfanya Larah abaki kumtazama hadi kushindwa kuuona mkono ambao alipewa......itaendeleaaaaaa

Haya mtoto Larah huyo kaona sura tu na sauti basi akili haichaji😄Heheee picha ndio linaanza hivoo, tafadhali usikae mbali ili uwe wa mwanzo kujua kilichoendelea.
 
*SEHEMU YA 5 *

"Hongera kwa kazi nzuri Larah" mwanaume huyo aliongea hayo kwa sauti nzito yenye msisimko ambao ulimfanya Larah abaki kumtazama hadi kushindwa kuuona mkono ambao alipewa.

Bwana yule alipoona mkono wake upo hewani na aliyempa yupo mbali kimawazo basi aliamua kuurejesha kwenye mfuko wake wa suruali, ingawa macho yao yalitazamana ila kiupande wa Larah fikra zake hazikuwa hapo kabisa ni kama alipigwa na shoti ya umeme kwa jinsi alivyoganda.

Katika kuangaza kwake Meddy alifanikiwa kuona walipokuwa , hali aliyowaona nayo ilimshangaza ila hakutaka kuwashtua kamwe. Moyoni mwake alichukia mno huku hasira za wazi zikianza kujichomoza ingawa alijaribu kuzizuia. Kwa vile hakutaka kuchafua hali ya hewa na kukiharibu kibarua cha kipenzi chake basi aliamua kuondoka haraka eneo lile.

Kipaza sauti chenye tangazo la kuwataka watu warudi kwenye nafasi zao ndicho ambacho kilikwenda kuurejesha mfumo wa hisia wa bibie Larah , alishtuka kuona yule ambae alikuwa kwenye mfumo wake wa akili hayupo mbele yake, hata alipotumia macho yake kumtazama Meddy sehemu ambayo alikua awali pia hakumuona, alijilaumu na kujitukana kwenye nafsi yake, akiwa kwenye taharuki hiyo ghafla alisikia jina lake likitajwa.

Kwa vile alitakiwa kukaa kwenye meza maalumu yenye watu wazito, basi alijisogeza kwa mwendo wake wa madaha huku macho yake yakiangaza kila kona kumtafuta Meddy huku akiachana na wazo la kumtafuta mwanaume aliyemfanya azubae.

"Larah .... jaribu kutembea kama kwamba unabusu ardhi na miguu yako" sauti nzito ambayo haikua ngeni kwenye masikio yake ilimfanya atazame mbele yake, macho kwa macho walikutana kwa mara nyengine, hii ni baada ya Larah kujikwaa na kiti ambacho alikalia mwanaume aliyetamka hayo.


"Heeh ni wewe , kwani umenijuaje na unataka nini" aliuliza kwa ukali kidogo huku sauti yake ikiwashtua wachache ambao walikua karibu yao.

Kila mmoja wao mkono ulikua mdomoni kwa mshangao, walibaki wakimtazama Larah kwa macho ya kugombeza ila hawakufanikiwa jambo, Larah alibaki vilevile na hasira zake tena wakati huu hakuchoka kumtazama mwanaume yule ambae aliishia kutabasamu, kama ni mwendo alitembea wa taratibu iweje aambiwe atembee kama anataka kuibusu ardhi? Kwake aliona ni dharau na dhihaka za wazi.

Mwenye kipaza sauti aliwataka watu wote kuweka umakini kwa kile ambacho kinakwenda kuonyeshwa pale na watu wa Media. Wafanayakazi wa kampuni ya ZURI FASHION walikua makini mno kutazama kile ambacho kitaonyeshwa kwenye TV kubwa ambayo ilikuwa mbele ya ukumbi huo. PERFECT ADVERTISING walionyesha uhodari wao wa kutengeneza video na picha mbalimbali ambazo zilionyesha mavazi yaliyokua ndani ya mwili wa bibie Larah, hakika Larah alijiona ni mwenye bahati mno huku akiona wazi kuwa safari yake ya maisha ndio imeanza.

Baada ya mijadala kuhusu tangazo hilo hatimae muda wa kufunga kikao uliwadia, bwana mdogo mwenye sauti yake nzito ndie ambae aliinuka na kutoa utambulisho ambao ulikwenda kumshtua Larah, hakuamini masikio yake hadi pale macho yalivyoshuhudia namna ambavyo watu walikuwa makini kumsikiliza na hata heshima alizopewa wakati anamaliza hutuba yake fupi.

Alijiona ni mkosefu huku akijuta kwanini alikutana na huyu mtu, alikumbuka namna alivyomdharau na kumuona ni mtu baki tu , kumbe jamaa ni mkurugenzi wa PERFECT ADVERTISING AGENCY, taasisi ambayo imempa kazi ya mkataba wa kushiriki kwenye tangazo la nguo kutoka ZURI FASHION.

"Mungu wangu! nimefanya nini mimi? Mmh napaswa kumuomba msamaha kabla Madam Siti hajasikia hii ila nitaanzaje? hata Meddy na yeye akisikia hili atajisikia vibaya mno" Alijiuliza Larah maswali mfululizo huku kile kinachozungumzwa na mkurugenzi asikisikie.

Akiwa kwenye fikra hizo nzito ghafla alishtukia akiguswa bega na mfanyakazi wa PERFECT , alipomuuliza anasemaje basi alionyeshewa kidole mbele kwenye stage sehemu ambayo aliiona sura ambayo ndio ilimfanya awepo kwenye hiyo hali.

"Umeitwa mbele na mkurugenzi" alinong'ona yule mfanyakazi wa kike ambae alikua pembeni yake baada ya kuona Larah hakua ameelewa kitu.

Moyo wa Larah ulishtuka kwa mara nyingine huku kijasho cha meno kikianza kumtoka, aliogopa baada ya kuona kua watu wote kwenye ukumbi ule wamemtolea macho. Alijiinua na kujipa ujasiri wa kuanza kupiga hatua mbele hata kama alikua na uoga ulipitiliza, haki ya Mungu laiti kama haja ndogo ingekua karibu basi ingedhihirika kwenye miguu yake😁.

"Hatimae safari yangu imeishia hapa, mbona nimekoma mimi na mdomo wangu" alijisemea Larah kwenye nafsi yake huku akijikatia tamaa kabisa, uso na sura ilimshuka mithili ya aliyebanwa ugoni.

Alipofika tu kwenye jukwaa alipokelewa na tabasamu zito kutoka kwa Mkurugenzi wao wa PERFECT, hilo lilimshangaza maana matukio ambayo yalitokea baina yao basi isingekua rahisi boss kumuonyesha tabasamu zito mfanyakazi wake ambae kamkosea adabu, yeye alijua kitumbua chake kimeingia mchanga tayari ila hii ilimshangaza mno.

"Hakuna kitu ambacho kimenifurahisha leo hii kama hichi ambacho nakiona, Madam Siti na Wafanyakazi wote munastahili pongezi kwa kutuonyesha kipaji na mtazamo mpya kwenye taasisi yetu, sio hivyo tu naamini hata wenzetu wa ZURI FASHION mumelifurahia hili, jamii inatuamini hivyo kupitia hii kazi mpya naamini itaongeza ufanisi wa kazi zetu ili kufikia lengo" alizungumza mkurugenzi wa PERFECT kwa hisia za furaha huku macho yake yakiwa usoni kwa bibie.

Larah alipokea maneno ya hekima na pongezi kutoka kwa mkurugenzi huyo , hakuamini kabisa kama boss wake angeweza kumsifu , mkurugenzi na yeye alimpa kipaza sauti Larah ili atoe neno la shukurani, Boss aligundua uoga aliokua nao binti wa watu ni hivyo tu alitaka kumkomoa.

"Huyu boss na yeye ana makusudi sasa mimi nakisema nini hapa? Oooh!! Mungu wangu nijaalie mimi nisije nikaropoka ujinga, hii ni mara ya kwanza kwangu" alijisemea Larah kwa hofu kubwa huku akikishika vyema kipaza sauti alichopewa.

Macho yake aliyapeleka moja kwa moja kwa watu ambao walikuwa mbele yao, aliwatazama na kuwazawadia tabasamu mwanana ambalo liliweka umakini wa kusikilizwa, Larah aliiweka hofu pembeni na kujiambia moyoni kwake kua huo ndio wakati sahihi wa kujitangaza , alimkumbuka mama yake aliyelala kitandani kwa zaidi ya miaka mitano, alikumbuka namna ambavyo siku nyingine hufikia hadi hatua ya kulala kwa kula mlo ambao haukukidhi angalau robo ya mwatakwa ya nafsi zao, hakusahau pia namna ambavyo siku nyingine hukosa hata pesa za kununua dawa .

"Nawashukuru sana wote ambao mumeshiriki kwa namna moja ama nyingine kunifanya niwe hapa leo hii, imani yenu kwangu ndio imenifanya leo hii kutimiza hili kiwango mkubwa, hakika PERFECT ADVERTISING na ZURI FASHION mtabaki moyoni mwangu siku zote, nyinyi ndio ambao mumeifungua ndoto yangu ambayo ilifungwa kwenye fundo la umasikini, Sikua najua siku wala muda wa ndoto hii kufunguliwa ...NAWASHUKURU SANA, Nina mengi ya kusema ila naamini hayatafikia kiwango cha shukurani ambacho ninacho juu yenu! AHSANTENI SANA" Larah alitoa maneno yake hayo huku machozi yakimtiririka machoni mwake, hata wale ambao walikua wakimsikiliza pia walijikuta wakimhurumia.

Mkurugenzi wa PERFECT ADVERTISING alijikuta akimtazama Larah kwa jicho la huruma, ila alishangazwa baada ya kumuona Larah akitabasamu hali ya kwamba machozi yapo mashavuni mwake, hilo halikumshangaza yeye tu hata wale waliokua wakimtazama pia walibaki wameduwaa. Sasa sijui kama machozi hayo yalikuwa ni ya furaha ama huzuni kwa kile alichokisema.

Baada ya hapo Larah aliruhusiwa kurudi kwenye nafasi yake, pongezi nyingi zilimshukia huku akiahidiwa kupewa kazi nyingine ambazo zitajitokeza, naam kama kizuri chajiuza basi Larah alinunuliwa maana kila mmoja alipendezwa na utendaji wake wa kazi kwa hiyo siku.

Baada ya wageni wote kuondoka alijitahidi kumtafuta Meddy kwa macho ila hakufanikiwa kabisa, Madam Siti ndie ambae alikutana nae na kumtafutia usafiri ambao moja kwa moja ungemfikisha kwao, naam Mkurugenzi katoa agizo nani wa kupinga😁

********

Larah alifanikiwa kufika kwao salama usalimini , ingawa tayari ilikua jioni ya jua kuzama ila alikua na shauku kubwa mno ya kumsimulia mama yake kile ambacho alikifanya kwa siku hiyo, uso wake ulijaa tabasamu zito pale alipoufikia mlango wao .

Alishtuka mno baada ya kukumbana na hali ambayo hakuitegemea, hakua na hata nguvu ya kupiga hatua kwa kile ambacho anakiona, ni chozi pekee ndio liliifikia sakafu ambayo haikua na kapeti..........itaendeleaaaaaa

Larah sijui kukutana na kitu gani, Meddy na yeye sijui kakimbilia wapi? Twende pamoja kwenye mwendelezo wa simulizi hii.
 
*SEHEMU YA 6 *

Alishtuka mno baada ya kukumbana na hali ambayo hakuitegemea, hakua na hata nguvu ya kupiga hatua kwa kile ambacho anakishuhudia, ni chozi pekee ndio liliifikia sakafu ambayo haikua na kapeti .

"M....Me...Meddy mama kawaje? Aliuliza Larah kwa sauti iliyochanganyika na kilio ndani yake.

"Ndio kama unavyomuona Larah, mimi mwenyewe nimeshangaa kumkuta hivi " alijibu Meddy huku akimtazama kwa masikitiko mama Larah ambae tayari muda huo mdomo wake ulionekana kupinda, alipojitahidi kusema neno basi ilishindikana, kiukweli alisikitisha maana hata alipotaka kuinua mikono yake pia ilionekana kumgomea.

"Mama...mbona nilikuacha mzima? Mama Sikujua yuko wapi? Eti Meddy? Aliuliza Larah mfululizo huku akionekana wazi kuchanganyikiwa.

"Larah hemu tulia kwanza , unajua kama hizo tafrani zako unazozionyesha zinaweza kumzidisha? Meddy alizungumza kwa sauti ya chini ingawa ilikua ya kugombeza.

"Huwezi jua nina uchungu kiasi gani Meddy, nilitaka kukataa hii kazi kwa kuepuka haya mambo, muone mama leo hii mikono yote imekua haina nguvu tena, hata mdomo wake ambao alitumia kunipa faraja na kunipa nasaha basi leo umemsaliti! Sisi ni masikini Meddy ila kwanini Mungu anazidi kutupa mitihani? kwanini kila siku sisi? naumia Meddy!!!!" alilalamika Larah maneno ambayo yalimtoa machozi mamaake .

Ni kama vile Larah alishtuka baada ya kuona hilo, akili yake ilimrudi na kujilaumu kwanini siku hiyo alizungumza maneno ya kumuumiza mamaake tena huku machozi yakiwa mashavuni mwake, ni miaka imepita hakuwahi kumuona mama yake akitoa chozi. Alimsogelea na kumkumbatia palepale kitandani licha ya kwamba yeye hakupata ushirikiano kwenye hilo.

"Mama , nimeshindwa mwanao! Sina ujasiri wa kutoangusha chozi ukiwa kwenye hii hali, ulinambia nifanye maamuzi hata kama yataumiza wengine ila sio kwa hili mamaa! Ona sasa umezidi kuumwa nilipokua mbali na wewe, hata yule ambae nilimuamini na kumuacha pembeni yako basi pia katuumiza mama! Nisamehe mimi mamaangu" Larah alizungumza hayo kwa uchungu huku akiyafuta machozi yake.

"Larah, unajua kuwa lawama hazitasaidia kitu muda huu? Unajichosha tu hapo na kuzidi kumuumiza mama, tunatakiwa tumuwahishe hospitali haraka" alizungumza Meddy kwa hasira akionekana wazi kuchukizwa na maneno ya Larah.


Larah aliona namna ambavyo Meddy alichukia, hakua na cha kufanya zaidi ya kukubali agizo aliopewa, Meddy alimpa nafasi Larah ya kumuandaa mamaake huku yeye akitoka nje kwa lengo la kwenda kutafuta usafiri.

**********

Mkurugenzi wa PERFECT ADVERTISING AGENCY alikua na kibarua cha kurudia kuzitazama video na picha ambazo zilimuonyesha Larah akiwa kwenye mavazi tofauti, mapozi ya Larah ndiyo ambayo yalimfanya azidi kuduwaa na kupelekea kushindwa kutambua uingiaji wa mtu ofisini kwake.

"Mr.Romy .....Mr.Romy ....Mr.Romy..." aliita aliyeingia ila hakuna alichoambulia zaidi ya ukimya uliotanda licha ya kwamba aliyemwita alikua mbele yake.

"Mr.Romy..." aliita tena ila wakati huu alijaribu kugonga na meza kidogo , naam hapo alifanikiwa maana Mr.Romy alionekena kushtuka huku akiifunga haraka laptop yake.

"Ooh Siti tayari umefika...aaa..aah karibu ukae" alizungumza Mr.Romy kwa kusuasua.

Madam Siti halikumshangaza hilo maana tokea muda ambao aliingia alimshuhudia boss wake huyo akiwa hayupo kawaida ila akilini kwake alijiuliza ni kitu gani ambacho kilimpelekea boss wake kuufunga laptop yake haraka.

"Mr.Romy upo sawa kweli? " aliuliza madam Siti huku akikaa kwenye kiti ambacho alikaribishwa.

"Nipo sawa Siti, sema tu nilikua siamini kabisa kama binti mpya angeweza kufanya kazi nzuri kama hii, nataka kumfahamu Larah zaidi " Mr.Romy aliropoka.

"Nilijua tu ungeniuliza kuhusu hili, Mr.Romy kile ambacho umekiona siku ya leo ni maamuzi ambayo tuliyapanga wafanyakazi wote, sisi Creative Department ndio ambao tulipanga kuitafuta sura mpya ambayo italeta mabadiliko kwenye soko letu" alieleza madam Siti kwa ufupi majibu yaliyomfanya Mr.Romy atabasamu ingawa kile alichokitaka hakikujibiwa vyema.

"Wow, hongera kwa hilo madam Siti, hakika umenifanya nijivunie uwepo wako kwenye taasisi yangu, naomba tuondelee kufanya nae kazi maana kuna kitu nakiona ndani yake" alizungumza Mr.Romy huku sura yake ikiwa makini kumtazama Madam Siti.

Mjadala kati yao ulikua ni Larah kujiunga na kampuni yao , walitaka awe mfanyakazi wao wa kudumu ili wapate kufanya nae kazi kwa uhuru kabla taasisi nyingine hazijataka huduma yake, kila kitu kiliandaliwa huku wakiwa na lengo la kumuingizia malipo yake haraka kwenye namba ambayo yeye mwenyewe alielekeza.

**********

Larah na Meddy walikuwa nje eneo ambalo watu hukaa kwa lengo la kusubiri taarifa za jamaa zao ambao wanapata huduma kwenye hospitali ile, ingawa tayari muda ulikua umesoge na mishare ya saa ilisoma saa mbili na nusu za usiku ila hilo halikuwafanya wakate tamaa ya kuwa pale, Larah alikua na kazi ya kujifuta machozi kila sekunde ziliposogea, maumivu aliyoyabeba kifuani mwake aliona wazi yatamshinda. Hapo ndipo alizikumbuka zile nyakati ambazo hukaa na mamaake wakacheka licha ya kwamba walikua na dhiki, alitamani uzima ule mamaake urudi ili waishi kama zamani.

Hata Meddy na yeye alizama kwenye fikra nzito ambazo hakujua wa kugawana nae, ni yeye pekee mwenye uwezo wa kumsaidia Larah ambae ni rafiki yake tokea zamani, kuna muda waliishi kama ndugu na kuna nyakati waliishi kama wapenzi, kwenye huzuni walikua pamoja na kwenye furaha basi wangecheka pamoja, ghafla mlio wa simu iliokua mkononi mwake ulimshtua , aliitazama na kugundua kuwa ni ujumbe mfupi , mara tu alipomaliza kuusoma huo uliingia mwingine ambao aliufungua haraka, alitabasamu na kumtazama Larah huku akiikumbatia simu yake.

" Larah ....." aliita Meddy huku akimgusa begani.

Tabasamu la Meddy lilitoweka baada ya kuishuhudia sura ya Larah imerowana machozi, Lile tabasamu ambalo alizowea kuliona kwenye uso huo basi siku ile lilipeperushwa na wimbi la huzuni, aliinua mikono yake miwili na kuanza kumpangusa machozi ambayo yalitiririka bila mpangilio, ni kama vile alimchomoa maana Larah aliangua kilio kizito na kujitupa kwenye kifua cha Meddy , hakukua na namna bwana mdogo alimuacha mtoto mzuri ayamwage machozi kifuani mwake, walio kando yao ndio waliweza kujionea na kubaki kuwatazama tu.

" Larah, Maisha yamegawanywa katika nyakati kuu TATU, kuna hii ya SASA ambayo ni fupi sana ila nzito kuibeba , ipo ya BAADAE ambayo ni mashaka kwetu kwa maana hatujui kinachofuata na nyakati ya mwisho ni YALIYOPITA ambayo ni ya kweli na yametuachia funzo kubwa" alizungumza Meddy kwa upole baada ya kilio cha Larah kukata.

"Una maana gani Meddy" aliuliza Larah huku akijitoa kwenye kumbatio na kumalizia kupangusa machozi yake kwa mikono.

"Larah, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila ambacho kinatufika kwani huwa kina funzo kubwa mno kwetu, huu ni wakati mgumu kwako lakini unatakiwa ufahamu kuwa utapita na maisha mengine yataendelea, wakati wa sasa ndio wa kuuthamini zaidi kwa maana ndio hubeba nyakati yako ya Baadae, Larah usiwe mtu wa kusikitika ila jitazame sasa una kipi mkononi? Jee! una kithamini? " Meddy alijitahidi kueleza ila bado alimuacha njia panda Larah.

"Bado sijakupata Meddy...." Larah alidadisi tena akionekana kuwa mwenye khofu sana.....itaendeleaaaaaa

Meddy anakusudia kumwambia nini Larah, Mr.Romy ataka Larah asainishwe mkataba wa kuwa mfanyakazi wa kudumu huku akisisitiza alipwe mapema, jee! Kwa hali hii unahisi nini kitatokea sehemu ijayo?
 
Back
Top Bottom