Sipaswi kulaumiwa

Sipaswi kulaumiwa

SEHEMU YA 22

"Larah..."aliita Mr.Romy kwa upole huku zile hasira zote akiziweka pembeni, Larah mwenyewe alibaki kumtazama.

"Naomba nikwambie kitu...zile chuki na hasira zote ziweke pembeni. Najua nimekosea na sikupaswa kufanya hayo niliyofanya na pia najutia kwa hilo, naomba unisamehe na tuanze upya. Naahidi kukusafisha kama ulivyofanya wewe leo hii, nipo tayari kwa kila kitu Larah " maneno hayo kutoka kwa Mr.Romy yalimfanya Larah afurahie kwenye nafsi yake huku akiona kua kazi kiupande wake imekua nyepesi tofauti na alivyodhani.

Hakuishia hapo tu Mr.Romy alishindwa kustahamili kuona machozi ya Larah yakimwagika mbele yake, alisimama na kumuinua kisha akamkumbatia kwa upendo mkubwa huku akimpigapiga mgongoni kumfariji.

Naam penzi jipya lilizaliwa kati yao, Larah aliamua kujiachia mazima ili aweze kulipiza kisasi chake kirahisi, hadi kufikia hapo kwa kitendo ambacho kiliendelea kati yao basi kilimhakikishia kua Mr.Romy ndie mhusika wa tukio lile na ndio maana kakubali kwa urahisi.

Zile picha na video ambazo zilitumwa kupitia account zake walizifanyia utaratibu na kuzifuta zote, licha ya kwamba watu walikua wanazo. Baada ya hapo Larah alirudi kwenye majukumu yake ya kawaida huku akimuacha boss ofisini kwake, hakuondoka hivi hivi bali alimuaga kwa busu zito ambalo aliamini litazidisha mahaba.

Mara tu baada ya kutoka Mr.Romy alipokea simu kutoka kwa mamaake Madam Ziya, hapo alizopokea ni lawama tu kutokana na kile ambacho alikiona kwenye vyombo vya habari. Madam Ziya hakua tayari kuona mahusiano ya kijana wake na binti wa mtaani ambae ndie aliyepelekea taasisi yao kuyumba. Hakuishia hapo tu baada ya kuona Mr.Romy kashikilia msimamo wake wa kua na Larah basi alimsisitiza amfanyie uchunguzi wa kina kuanzia maisha yake na watu ambao wanamzunguka ili wasije kuangukia tena kwenye mambo makubwa kama yaliyojitokeza.

**********

Jioni ilipotimia Larah alijisogeza maeneo ya kwao akitokea ofisini, njiani alipopita story zilikua ni kumuhusu yeye na kile ambacho alikizungumza asubuhi na kuenea kwenye mitandao ya kijamii , wapo waliompongeza kwa ujasiri wake na pia wapo ambao walimbeza na kumuona kua sio wa thamani tena. Hayo hata hakuyatia akilini alichojali yeye ni furaha ya maisha yake na sio wengine.

Alisogea hadi kwenye chumba chao ambacho walipanga, taratibu huku akiweka sura ya tabasamu aliingia ndani na kukutana na kitu ambacho kiliipoteza furaha yake, kwa mwendo wa haraka alimsogelea mwanamke aliyekaa pembeni ya mamaake wakitia story.

"Niffa naomba utoke" hii kauli kutoka kinywani mwa Larah iliwaacha wazi midomo wale waliokua kando yake.

"Laarah waungwana wakikutana hujuliana hali kwanza!!" Niffa alizungumza kwa upole kama sio yeye ambae alitakiwa kutoka, Mama Larah yeye hakutia neno alibaki kumtazama bintie kwa masikitiko.

"Kuna muda baadhi ya vitu vinakua havina umuhimu wa kuwepo, kiswahili changu nafikiri kinaeleweka sihitaji uwepo wako hapa" Larah alizungumza hayo akionekana wazi hakua kwenye matani.

Niffa alishangazwa na hali hiyo , hata mama yake na yeye alizidi kumshangaa bintie na tabia zake , Niffa alitamani kumtukana ila alijizuia alipogundua uwepo wa mtu anaemheshimu eneo lile. Kwa ukaribu zaidi alimsogelea Larah na kumburuza hadi nje .

"Sipo hapa kwa ajili ya shari , naomba unigaie muda wako kidogo tu" aliomba Niffa huku akiweka sura ya msisitizo

"Hivi hufahamu kuwa muda ni mali? Sipaswi kuongea na watu pale tu ninapokuwa na muda, bali natakiwa kutengeneza muda wa kuongea na watu. Niffa....sikuhitaji na wala sina muda mchafu wa kupoteza na wewe" maneno hayo kutoka kinywani kwa Larah yalimduwaza Niffa na kumfanya asiamini alichosikia. Alipotaka kujiweka vyema ili atoe jibu alimshuhudia Larah akipiga hatua kuuelekea mlango. Kamwe hakutaka hilo litokee hivyo alimuwahi na kumvutia nje kwa mara nyingine.

" Larah....JITAMBUE. Anza kwa kuufahamu utu wako mwenyewe , jitahidi kuwa na mtazamo wa wazi wa utu wako, ikiwa ni pamoja na uwezo, udhaifu, mawazo, imani, misukumo na hisia zako. Larah kujitambua ni raha sana maana kunakupa kuelewa watu wengine, jinsi gani wanakuona wewe, mtazamo wako na majibu yako kwao katika wakati husika. KWAHERI"

Niffa alimaliza kuzungumza na kuanza kupiga hatua kuondoka , Larah uso chini huku maneno mazito kutoka kwa Niffa yakimuelemea. Alitamani hata arejeshe muda nyuma ili amsikilize ila haikuwezekana tena maana wakati sio gari kama linaweza kwenda na kurudi.

Hali ya majuto ilimzidi na kuanza kumvaa, alibaki kizingitini akiilaumu nafsi yake kwa kushindwa kutenga muda wa kumsikiliza rafiki yake. Hakupaswa kamwe kumfikiria kua yeye ndie chanzo cha matatizo yaliyomkumba kwa maana kila kinachotokea basi kilipangwa na Mungu kitokee.

"Kivyovyote vile sipaswi kuwasahau wale walionisaidia na wakasimama nami katika nyakati za shida na nyakati ngumu za majaribu. Niffa wewe ndio chanzo cha yote ila wema wako kwangu bado utaniazibu....hapana sistahili kukumbatia!! Yafaa nikuweke kando na kukukwepa kabisa " Larah alijisemea mwenyewe ni kama vile alichanganikiwa.

Larah aliingia ndani akiwa vilevile mwenye hasira na majuto ndani yake. Aliona aibu kumsogelea hata mamaake hivyo alikaa kando na kisirani chake akisubiri kusomewa mashtaka yake. Siku hiyo mama Larah alijitahidi kudhibiti ulimi wake maana hakusema neno kabisa , alimuacha bintie aendelee na kiburi chake.

************
Siku , wiki na miezi ilipepea kama upepo hadi kufikia miezi mitatu tokea picha na video chafu za Larah na Mr.Romy kuachiwa mtandaoni. Perfect Advertising ilijua kujiinua upya kwa mara nyingine. Larah na wafanya kazi wote waliungana kuitengeneza upya taasisi hiyo. Penzi kati ya Mr.Romy na Larah lilizidi kukuwa huku kila mmoja akiiva kiimani juu ya mwenzie hata zile tofauti ambazo walikua nazo basi zilionekana kufifia, hisia za upendo zilizaliwa na walipendeza sana maana kila sehemu walikua pamoja yaani kiufupi hakuna Larah bila Mr.Romy.

Hili jambo lilimkosesha sana amani Niffa maana kila alipojaribu kuweka ukaribu na watu hao basi ilishindikana. Hakuna aliyetaka kumsikiliza kati yao hata mama Larah pia na yeye alimfukuza Niffa pale alipokwenda kwa lengo la kutaka ukaribu wa mazungumzo. Naam hawa ndio wanadamu ambao siku zote wakipata basi huwasahau hata wale waliokua nao kwenye nyakati ngumu.

Larah aliishi maisha mengine kabisa , alikua ni sio yule Larah wa kulalia uji au wali mkavu. Huyu alikua ni Larah aliyeishi na kuogelea kwenye utajiri. Alihama uswahilini na kuishi ushuwani kulingana na hadhi yake. Hakuna asiyemjua mlimbwende Larah, juhudi na bidii za kufanya matangazo mengi yenye ubora ndio yaliyomfanya kuwa hapo alipo.

Katika chumba cha kifahari chenye kila aina ya mapambo Larah alionekana akiwa kalala fofofo, akiwa kwenye usingizi huo mzito alishtuliwa na mlio wa simu iliyokua kando yake, mlio ule ulimkera na kupelekea kuachia msonyo mkali huku akijinyongoa na kuyafikicha macho yake. Alizidisha hasira pale alipoona jina la aliyepiga simu .

"Huyu nae hajui kupuuzwa? Larah aliropoka huku akiiacha simu ile iite hadi ilipokata.

Hiyo haikua dawa kabisa maana mpigaji aliendelea kupiga simu ile bila kukoma. Kwa hasira aliipokea na kuiweka sikioni kwake huku uso wake ukiwa umewiva. Ni kama aliisusia maana aliacha aliyepiga azungumze alichokusudia huku yeye akiubana kimya.
"Naona unajisahaulisha wewe ni nani kwangu! usisahau ulipotoka na wala usimsahau aliyekurusha hapo ulipo. Nikuone getoni kwangu sasa hivi" sauti ya Meddy ilinguruma kutoka kwenye simu iliyokua sikioni kwa Larah, alichukia ila hakua na namna.....itaendeleaaaaaa
 
SEHEMU YA 23

Naona unajisahaulisha wewe ni nani kwangu! usisahau ulipotoka na wala usimsahau aliyekurusha hapo ulipo. Nikuone getoni kwangu sasa hivi" sauti ya Meddy ilinguruma kutoka kwenye simu iliyokua sikioni kwa Larah, alichukia ila hakua na namna.

Simu ilibaki sikioni mwake ila hakuna aliyezungumza licha ya kwamba ilikua hewani, Larah mwenyewe alipoona sekunde zinakatika aliamua kuikata na kuitupia pembeni ya mto. Kwa mwendo wa uchovu na hasira alielekea bafuni kwake kwa lengo la kujiandaa ilia amfate Meddy.

Nusu saa nzima ilikatika haraka kama barafu juani l, alijihakikishia muonekano wake kupitia kioo kikubwa kilichokua kwenye meza yake kubwa ya vipodozi, naam kipya kinyemi pande la kioo liliachwa uswahili.

Kwa mwendo wake wa madaha alitoka chumbani kwake na kuelekea katika chumba ambacho mamaake analala, huko alikuta chumba cheupe kikimtazama . Alijitahidi kuita ila hakukua na majibu zaidi ya ukimya uliotawala chumba kile, alihamaki na kutafuta usawa wa njia ya jikoni kwa maana alijua angemkuta huko.

"Mamaa, yaani hata afya yako haijatengamaa tayari unajitutumua na kazi!! Kwani dada wa kazi hayupo? Ni mara ngapi lakini mama nakwambia? Alilalamika Larah kwa deko baada ya kumkuta mamaake jikoni akikoroga uji, hili lilionekana wazi kumuudhi na hakupenda maana sura yake aliikunja na ule uzuri wake kupotea kwa muda.

" Larah binti yangu, nimekaa kitandani muda mrefu sana . Umenipambania na wala hukuwahi kukata tamaa kwenye hili , kama saivi nimepata ahuweni kwanini nisikuhudumi? Larah , wacha niitumia nyakati hii kulipiza yale ambayo nilishindwa wakati wewe ulihitaji msaada wangu" Mama Larah alijitetea baada ya kuona bintie kachukizwa.

Larah hakua na neno mbele ya mamaake, alimpenda na kumheshimu sana. Alimfata na kumkumbatia huku akimzawadia na busu zito la shavu . Baada ya hapo alimsaidia kuandaa meza ambayo ilisheheni vitafunwa , uji ulionukia uliletwa na watu walianza kujisevia. Larah hakufunua mdomo wake kumweleza mamaake mpango na usumbufu wa Meddy dhidi yake.
********
Ndani ya PERFECT ADVERTISING AGENCY alionekana Mr.Romy akiwa kasimama usawa wa dirisha akichungulia chini kama kuna kitu aliambiwa kitakatiza hapo. Akiwa kwenye pozi hilo alisikia simu yake ya mezani ikikia, haraka aliipokea na kusikiliza alichoambiwa na Secretary wake. Ingawa sura yake ilijikunja ila hakuweza kubadili ukweli wa kile alichoambiwa.

Alipokata simu tu basi macho yake aliyapeleka hadi kwenye kitasa cha mlango , alikitazama kwa hasira huku akitamani kifunguliwe ili apambane ba huyo aliyeambiwa ataingia. Naam sekunde chache zilitosha kutimiza alichotegemea, Niffa alionekana kutabasamu mara tu alipoingia na bila kusubiri kukaribishwa alikaa kwenye sofa dogo.

"Niffa , najua hujawahi kujua maana ya kupuuzwa na ndio maana unaendelea kuyafatilia maisha yangu ikiwa nina amani? Mr.Romy alianza mazungumzo na kumsogelea kwa ukaribu Niffa.

"Una amani? Amani ipi! Ya kuwekwa kwenye giza? Rommy nakuhurumia sana na baadae yako. Kama leo hii naonekana mwendawazimu na msumbufu kwako basi kuna siku haya yatakurejea wewe, na ubaya wa mambo utakua umechelewa.Hii dunia watu wanaishi kwa akili sana , Wachunguze wanaokuzunguka hii itakupa majibu ya kwanini nimekua nikitaka kukwambia kitu muhimu"

"Kitu gani wewe nambie tu sio kunizungusha"

"Ilikua ni hapo zamani kukwambia hili ila kwa wakati huu unapaswa kuutafuta ukweli mwenyewe. Unajua kwa nini? Nataka usinione mnafiki" Niffa alipomaliza kusema hivyo aliondoka bila kuaga.

Mr.Romy alibaki kwenye mshangao asijue afanye nini, maneno ya Niffa yalimpa viulizo vingi kiasi cha kushindwa kujua wapi aanzie kutafuta majibu. Yeye alipoona hakuna habari mbaya huku penzi lake jipya basi hakuwaza kama kuna wabaya nyuma yake. Kama ni mamaake alishasema na kuchoka hadi kuamua kuwaacha sasa huyu adui alitoka wapi?


Akiwa bado kwenye mawazo alishtuliwa na muito wa simu yake ya mkononi. Kwake ilikua ni namba ngeni lakini aliipokea hivyohivyo na kuiweka sikioni mwake.

"Kuna tangazo langu nimekutumia WhatsApp naomba nisambazie" sauti ya kiume kutoka upande wa pili wa simu ilizungumza na kukata.

Bila kuchelewesha aliwasha mobile data, alipoingia WhatsApp alikutana na namba ngeni ambayo alitoka kuzungumza nayo, namba hiyo ilionyesha kua imetuma mijumbe 3 . Mr.Romy aliifungua na hapo ndipo alipojikuta akikaa kwenye sofa bila kutaka, miguu ilimuisha nguvu na mikono ilibaki kutetema.

Alijikuta akiivua tai yake shingoni bila kutaka, joto ambalo alihisi lilizidi ile AC ambayo ilikuwa ofisini kwake. Video, Audio na picha ambazo alizifungua zilimuacha mdogo wazi na kuanza kumfanya atokwe na jasho jingi. Alipoamua kuzipiga zile namba basi hazikua zikipatikana tena, aligonga meza kwa hasira na kujikuta akitukana ovyo.

Secretary wake alifika mara tu aliposikia kelele zile, ila alichokutana nacho kilimfanya azidi kumuonea huruma boss wake. Akiwa kwenye harakati za kuweka sawa vitu vilivyotupwa ovyo uliingia ugeni ambao hakuna ambae aliutegemea kama ungefika. Mr.Romy alijiinua na kujiweka sawa licha ya kwamba bado alionekana hayupo sawa.

Ugeni ambao ilifika ni wanasheria na washauri wa babake na Mr.Romy, hawa mara nyingi hufika endapo kutatokea changamoto ya mali zao. Mr.Romy aliwakaribisha huku akimtaka Secretary awapishe.

Mazungumzo kati yao yalianza huku mada kuu ikiwa ni yeye kutakiwa kuoa ili aendelee kushikilia madaraka aliyopo lakini pia walifika hapo kwa lengo la kumshauri atoe asilimia ndogo kwa ajili ya mamaake ambae hakua amepata kitu kwenye mgao wa mali.

"Nisikilizeni wazee wangu, kuoa nitaoa muda sio mrefu lakini maamuzi ya babaangu naomba yabaki hivyohivyo na wala haitatokea siku nikayabadilisha, labda iwepo sababu ya kufanya hivyo ila sio kwa hii mliyonipa" Mr.Romy alijibu huku akiwa kawakazia macho .

Hakuna kilichojadiliwa pale kikakubaliwa na Romy labda jambo pa kuoa tu. Watu wale waliondoka wakiwa na hasira huku Romy akijiapiza kuwabadilisha maana aliona wanapoelekea . Hakupumua vyema kwenye kiti watu wawili waliruhusiwa kuingia , hawa walikua wanatoka kwenye taasisi hiyo hiyo kitengo cha usimamizi wa fedha. Walipofika hapo walimkabidhi nyaraka chache Mr.Romy wakitaka azipitie.

Mshtuko mkubwa uliomfika ulimfanya azidi kuchoka, kama kuna siku mbaya kwenye maisha yake basi hiyo aliihesabu ni ya pili baada ya siku ya kifo cha babaake. Alishindwa kuzuia machozi mbele ya wafanyakazi wake. Mapigo ya moyo yalimpanda na kutaka kumuangusha ila hakuwahi kufika chini , wafanyakazi wake walitoa taarifa za kuzima kwa boss wao na taratibu za kumuwahisha hospital zikaanza.

**********

Alionekana ni mwenye majuto huku akiilaumu nafsi yake kwa matendo yake, alilivuta shuka kwa lengo la kufunika sehemu zake ya mwili ambazo zilitoka kutumiwa kwa lisaa lizima. Machozi yaliyojaa maumivu hayakuchoka kutirirka shavuni mwake , alitamani hata kutoka nje akakiri makosa yake lwa mwanaume aliyempenda ila hakua na nafasi tena.

"Larah....utaendelea kulia au utaondoka na mimi? Aliuliza Meddy kwa sauti yake kavu.

"Nakuchukia Meddy sifikirii kufanya lolote na wewe" kwa sauti ya kilio Larah alijibu.

"Hahahaaa , unanichukia? Hivi wewe atakuoenda nani? Romy?? Uliyeshiriki kumuibia kwa lengo kulipa kisasi? Yeye ni mjinga tu kama walivyo wengine na ninamchukia kwenye maisha yangu maana yeye ndie sababu ya yote haya"


"Meddy inatosha sasa!! Kwanini unamchukia namna hiyo mpenzi wangu kwanini? Aliuliza Larah kwa hasira huku akijifunga vizuri .

"Oooh mpenzi wako? Sikuwa najua kama una wapenzi wawili" kwa dharau Meddy alijibu.

"Meddy.... leo nataka kujua kwanini unamchukia Romy? Kwanini unanitumia mimi kutimiza malengo yako? Nataka kujua Meddy...." kabla Larah hajamaliza alisikia simu yake ikiita.......itaendeleaaaaaa
 
SEHEMU YA 24

"Meddy.... leo nataka kujua kwanini unamchukia Romy? Kwanini unanitumia mimi kutimiza malengo yako? Nataka kujua Meddy...." kabla Larah hajamaliza kuuliza alisikia simu yake ikiita, alisogea nakutaka kuichukua ila Meddy aliiwahi.

"My boy" alisoma Meddy jina ambalo lilitokea kwenye simu ya Larah huku akipuuza maswali aliyoulizwa.

"Boy wako anapiga, bila shaka tayari alishagundua tulichofanya . Larah napaswa kuondoka haraka maana kile nilichotaka kimekuwa, kila mtu apambane kivyake. Wewe umelipiza kisasi chako na account yako imeshajaa" Meddy alizungumza hayo huku akiizima kabisa simu ya Larah ambae hakuchoka kumwaga machozi, Larah alijiuliza maswali mengi kumhusu Meddy ila hakukua na jibu sahihi alilopata.

"Najuta kukujua Meddy, umekuja kuyaharibu maisha yangu nyakati ambayo furaha ipo na mimi, siondoki na wewe wacha sheria iamue" Larah alisikitika.

"Ooh kumbe, mimi siwezi kabisa kufungwa kizembe. Nimetumia muda na akili nyingi mno kua hapa , KWAHERI " Meddy alizungumza maneno yaliyomuacha mdomo wazi Larah, alianza kutoka nje huku akimuacha bila kumwambia sababu ya kufanya yote hayo, wakati alipokua anaondoka hakuchukua chochote kutoka ndani.

Larah alilia sana hiyo siku, hakutamani kwenda popote maana aliamini hakuna ambae angemtazama kwa jicho jema kutokana na kile alichofanya . Yeye ndie sababu ya anguko la PERFECT ADVERTISING AGENCY kwa mara nyingine. Alijuta na kujilaumu kwanini hakumuepuka Meddy mapema, ila angefanya nini na alihusika kwa asilimia kubwa kuyabadili maisha yao . Hata hivyo nafsi yake kipindi cha nyuma ilijazwa kisasi na kuziweka kando hisia za upendo ambazo mwisho wa siku zilirudi moyoni na kumuendesha. Aliuona wazi upendo wa Romy kwake na ndio maana ilikua rahisi kupata kila ambacho alitaka.

"Nimeshayaharibu maisha yangu, sitakwenda popote kuikimbia adhabu yangu. Meddy ni mtu mbaya mno. Sitokubali kabisa nifungwe bila kujua sababu ya yeye kufanya yote haya" aliwaza Larah.

*******
Safari ya Romy iliishia mitaa ya uswahilini ambayo walikua wakiishi Larah zamani, huko alijitahidi kuulizia sehemu ambayo Niffa anakaa. Mbele ya pesa kila jambo huwa jepesi maana hakusumbuka kabisa kumpata.

Akiwa ndio kwanza kafika na kujitupa kitandani kwake aliusikia mlango wake ukigongwa kwa fujo. Alitabasamu kama ya kwamba kile alichosikia alikifurahia , alijua tayari mji umeanza kuchangamka hivyo kwa mwendo wake wa madaha aliusogelea mlango na kunyonga kitasa .

"Ooh!! Karibu kwangu Mr.Romy " kwa tabasamu pana Niffa alimkaribisha.

Ni kama hakusikia ukaribisho aliopewa , alibaki mlangoni aliyakagua kwa macho mazingira ya chumba cha bibie Niffa. Licha ya udogo wake lakini kilivutia kutokana na namna ambavyo kilipangwa. Niffa alimpiga kofi dogo begani kama ni njia ya kumshtua .

"Vipi? Naona umekuja kwa fujo lakini umekwama mlangoni unashangaa tu!! " Niffa alizungumza kwa upole huku macho yake akiyagandisha kwa Romy.

Romy alishangazwa na upole wa Niffa , siku hiyo alimtazama kwa jicho lingine kabisa, jicho ambalo liligundua uzuri wa sura na umbo la Niffa . Romy hasira zote ziliyeyuka na kubaki akiwa mpole , hahaaaa kama ni simba basi alishikwa sharubu zake.

"Niffa,naanza kuamini maneno uliyotamka leo asubuhi, naomba kuujua ukweli tafadhali nisaidie" kwa unyenyekevu Romy akiomba huku zile hasira akiziweka kando.

"Una uhakika upo tayari kuupokea ukweli? Swali kutoka kwa Niffa lilikuwa jepesi ila kwa Romy aliona ugumu wa kujibu hivyo alibaki kimya.

"Romy ...... chuki naziweka kando kwa vile niliamua tokea awali kukusaidia , kama na wewe umeshaamua basi nitakusaidia ila sitozungumza chochote hadi pale itakapobidi" Niffa alizungumza.

"Kivipi? Romy aliuliza kwa shauku.

Niffa hakuwa na muda wa kueleza kwa mdomo kwani aliona kufanya hivyo ni kupoteza muda, alisogea kitandani kwake na kubeba pochi yake. Alimtaka Romy wasogee mtaa wa pili tu kutoka kwake , huko aliamini wanaweza kupata chochote ambacho kitawasaidia.

*********

Ulikuwa ni wakati mzuri mno kwao, nyuso zao zilionekana kuwa za furaha tofauti na siku zote. Chumba chao kilipambwa na pesa nyingi hadi nyingine wakawa wanakanyaga. Walifungua mziki na kuanza kucheza huku wakijimwagia zile pesa, walipotosheka walijibwaga kitandani na kuanza kutazamana kwa macho ya matamanio, hisia zao ziliwavuta wafanye kile ambacho wapendanao hukifanya wakiwa faragha, naam hapo ilikua ni mwendo wa kuingiza na kutoa tu hadi saa nzima ilipokatika.

"Meddy, tumeshafurahia vya kutosha, naamini sasa moyo na nafsi yako vimeridhia hivyo naomba usiku wa leo hii tuuhame huu mji maana Mr.Romy hatatuachia kabisa" alizungumza Madam Siti akiwa kifuani kwa Meddy.

"Hata mimi nimeshapanga hilo, naamini sasa bibi yangu atapumzika salama huko alipo, nilimuahidi kuwa nitalipiza kisasi kwa ajili yake. Nimewaangusha wote na sifikirii kama yupo atakaesimama katika anguko hili" kwa furaha na bashaha Meddy alizungumza huku akimzawadia busu la nywele Siti wake.

********
Iliwachukua nusu saa tu kuifikia nyumba aliyokua akiishi Meddy , Niffa mbele Romy nyuma wakisubiri aliyepo ndani afungue, dakika tatu nzima ziliyoyoma hadi mlango kufunguliwa. Larah macho yalimtoka kwa alichokiona , hakutegemea tukio kama lile kwa wakati ule. Mdomo ulibaki kutetema asijue aseme nini, kama ni samaki basi tayari ndoano ya mvuvi ilikua mdomoni mwake.

Hasira za Romy zilionekana waziwazi usoni mwake, alimsogelea Larah ambae na yeye hakuacha kurudi kinyume nyume hadi alipokifikia kitanda, aliinua mkono wake kwa lengo la kumpiga ila hakufanikiwa maana mkono wake ulishikwa na Niffa.

"Utaharibu Romy, au unataka niondoke? Ulisikia wapi ukweli hupatikana kwa kutumia nguvu? Wewe mwanaume bwana unaanzaje kupigana na mwanamke!! Niffa aliongea huku akimshika Romy na kumuweka kando.

"Sipaswi kulaumiwa! Sipaswi kulaumiwa Romy " maneno hayo kutoka kinywani kwa Larah yalisindikizwa na machozi.

"Tulia Larah, huu sio muda wa kulia, lengo la kua hapa ni kutaka ushirikiano na utayari wako kwenye hili, kama kuharibu tayari umeshaharibu " Niffa alizungumza.

"Larah, ukitaka mimi na wewe tuelewane nieleze kila kitu kumhusu Meddy na wala usiache sehemu hata moja , nieleze unavyomfahamu" kwa sauti yake ya upole yenye kumaanisha Mr.Romy alizungumza.

Upendo aliokua nao Larah kwa Romy ulikua ni mkubwa mno, licha ya kwamba hapo mwanzo aliuchanganya na kisasi ambacho hakikumpa faida yoyote zaidi ya hasara na kujikuta akitumika kukamilisha mipango ya watu bila yeye mwenyewe kujua. Aliamua afunguke yote ili apate amani ya nafsi yake ili hata akiwekwa ndani basi amtengenezee mamake mazingira ya kuishi bila uwepo wake........itaendeleaaaaaa
 
SEHEMU YA 25

"Miaka mitano iliyopita mamangu alianza kuugua ugonjwa ambao ulisababisha mimi kukutana na Meddy, yeye ndie ambae alikuwa msaada wetu na kuanzia hapo maisha yetu aliyaendesha yeye kwa kiasi kubwa maana hatukua na ndugu wa upande mwengine. Meddy alihusika kunitafutia kazi sehemu mbalimbali, matibatu na matumizi yetu ya ndani pia yalichangiwa na yeye.... " Larah alimeza mate kidogo huku akijifuta machozi ambayo hayakuacha kumwagika.

"Nilipopata kazi kwenye taasisi yenu nilifurahi mno, maana niliamini zile ndoto ambazo niliziota tayari zimekuja kwenye uhalisia, sikubahatika kumaliza elimu hivyo nilipoona fursa imekuja mbele yangu basi nilijitahidi kuitendea haki. Nilifanikiwa kwenye hilo ila moyo wangu uliingiwa na doa la chuki pale nilipogundua ukatili wako ulionitendea Romy, sikuwa na yoyote wa kumsimulia zaidi ya Meddy ambae na yeye alionekana kuumia mno. Niliteseka asubuhi na jioni kufuta kumbukumbu mbaya ambayo uliniachia ,nilikuona mnyama pale ulipoutumia utu wangu uendelee kukusaidia katika mambo yako....." machozi ya Larah hayakukoma na kumfanya anyamaze kwa muda.

"Moyo wangu ulipanga kulipa kisasi, sikutaka ushauri wa yoyote kwenye hili ila tulichopanga sio ambacho kilitokea , picha zetu mimi na wewe zilivuja kabla ya mpango wetu tuliopanga mimi na Meddy kutimia, hilo pia lilinifanya niamini kwa asilimia zote kua unahusika..."

"Ehee.. mlipanga kufanya nini? Aliuliza Romy.

"Mpango tulioutekeleza saivi ndio ambao tulipanga kuufanya siku ile , licha ya kwamba huu wa saivi aliuboresha yeye mwenyewe Meddy" Larah alieleza.

"Ohoo sasa nimeelewa ni kwanini ulijifanya unanipenda hali ya kwamba mimi ni adui kwako"

Larah alijikuta akipinga hilo swali , alijieleza kua yeye alimpenda Romy tokea siku ya kwanza tu kukutana , kilichopunguza upendo ni kitendo cha kurekodiwa na kuachiwa wazi mitandaoni. Lakini pia alikiri kua upendo wake wa mara pili ulikua wakisasi ambacho mwisho wa siku kilirejesha hisia zake za mapenzi kwa Romy.

"Kama mapenzi yako yalirudi kwangu kwanini hukuwahi kuniweka wazi maisha yako ya nyuma? Kwanini hukutaka na mimi nijieleze kwako kuhusiana na lile tukio? Hivi kwa akili yako unafikiri mimi naweza kufanya upuuzi kama ule? Laiti ungenipa muda nyakati ambazo nakufata basi wala tusingefikia huku" maneno ya Romy yalimfanya Larah azidi kujisikia vibaya na mwenye hatia.

"Isingekua rahisi Romy, Meddy alinishikilia sana nitimize kile nilichomuahidi, alitumia msaada wake kwetu kama njia ya kufanikiwa, nisigeweza kukataa" Larah alijibu kwa upole.

"Larah hayo yote tisa, hivi uliwahi kujiuliza kwanini Meddy alishikilia wewe kulipiza kisasi kwa Romy na sio mtu mwengine" aliuliza Niffa.

"Niliwahi kumsikia akilalamika na kusema anamchukia Madam Ziya lakini sababu ya chuki hizo hakuwahi kuiweka wazi "maneno ya Larah yalimfanya Romy anyanyue shingo yake na kumtazama kwa umakini Larah.

"Larah... usalama wako ni kufunguka ukweli wote, Meddy mlilala pamoja si chini ya mara 10 kwanini ushindwe kugundua hilo? " swali hilo kutoka kwa Romy lilimfanya Larah achoke zaidi, hakuwahi kujua kama Romy anafahamu mahusiano yake na Meddy lakini pia yeye mwenyewe hakufanikiwa kuijua sababu ya Meddy kumchukia Madam Ziya.

Wakati anajiandaa kutoa majibu Niffa alitoa simu yake na kuanza kuwaonyesha picha, video na audio ambazo zilikua ni ushahidi tosha wa mazungumzo ya Madam Siti na Meddy, ushahidi wote huo ulichukuliwa siku na nyakati tofauti. Mr.Romy alijikuta akimtazama Niffa bila kummaliza maana zilikua ni picha zilezile ambazo alitumiwa na namba ngeni asubuhi, hapohapo alitoa simu yake na kupiga simu makao makuu ya Polisi.

Niffa na Larah walijikuta wakiwekwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi, kiupande wa Larah haikumshangaza maana alijua makosa yake ila Niffa yeye alijikuta akimtazama Romy kwa jicho la chuki, hakujua kosa lake ni lipi hivyo alijutia kujiingiza kwenye mambo yasiyomhusu.

**********
Hali ya mchafuko na wizi wa kiasi kikubwa cha fedha kutoka taasisi ya PERFECT ADVERTISING ulianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, hilo pia liimfikia Madam Ziya ambae alikua ukumbini na wanasheria wa kijana wake wakijadili namna ya kumiliki mali, mara tu baada ya kuona taarifa hizo alijitahidi kumpigia simu kijana wake ila haikua ikipokelewa, alimtafuta dereva wa Mr.Romy ambae alitoa maelekezo yote.

Madam Ziya alijikuta akichukia mno maana na yeye alikua mbioni kuzifukuzia hizo mali. Alijikuta akianza kumtilia mashaka Larah maana yeye ndie masikini mwenye roho ya kutotosheka , aliamini kua ukaidi wa kijana wake ndio uliwasukuma huko.

Hakuna aliyemuaga , aliwacha wanasheria na yeye kutokomea nje. Kwa mwendo wake wa haraka alisogea hadi sehemu ambayo wanaweka magari yao, huko alichukua gari moja na Safari ya kituoni ikaanza. Siku hiyo dereva alimuweka kando aliyakanyaga mafuta hadi kibati cha spidi akakimaliza . Ilimchukua dakika kumi na tano tu kufika kituo cha polisi.

Alipiga hatua na kusogea mapokezi, huko alisikilizwa na kuelekezwa usawa ambao kijana wake alikua, alifurahi alipomuona Larah na shosti wake Niffa ila ghafla furaha iliyeyuka baada ya kuiona sura Siti ikigeukia upande aliokua .

"Mama .....umefata nini? Aliuliza Romy huku sura yake akiikunja.

Mamaake ni kama lile swali hakuulizwa yeye, alibaki akiwakagua watu wanne ambao walikua mbele ya Romy na askari, alizidi kumtazama Siti ambae uso wake ulionekana kuchakazwa kwa kipigo.

"Romy umemfanya nini mtoto wa watu? Siti hawezi kufanya hivi! Wahalifu ni hawa wengine" Madam Ziya aliongea hayo huku akimhurumia mno Siti na kuanza kumfutafuta sehemu alizochafuka.

"Hahaaa nani wahalifu? hivi kati yetu kuna mhalifu aliyefikia uhalifu wako? Meddy aliamua kufumbua mdomo kwa kumkandamiza Madam Ziya maswali ambayo kila mmoja yalimpa mshangao isipokua Siti.

"Uhalifu? Wewe mtoto mbona unakosa adabu na aibu" Madam Ziya alijibu huku na yeye akianza kuingiwa na mashaka.

"Sio ajabu hata kidogo maana nitakua nimechukua kutoka kwako" Meddy alifoka huku akionekana wazi kUna jambo alitaka kusema.

"Romy, wacha nikiri kwa kila mtu sababu ya kufanya yote hayo. Najua njia ambayo niliitumia kulipiza haya sio sahihi ila imebidi iwe hivyo, hakukua na wa kunishika mkono mnadhani ningefanya nini..." Meddy alimtizama kwa hasira Madam Ziya ambae na yeye uoga ulianza kumvaa.

"Romy...tafadhali mwanangu usimsikilize.."

"Mwanao? kati yake na mimi Zamedi nani kijana wako" Meddy aliuliza swali ambalo lilikua gumu kwa Madam Ziya, alishtuka kusikia hilo jina.

"Zamedi? Kila mtu alilitaja hilo jina.

" Yeah, ndio mimi . Nimekua mkubwa sasa eeh , hahaaa inashangaza si ndio? Mitaa ilinilea baada ya bibi uliyemtupia ulezi kufariki sababu ikiwa ni wewe. Ulituacha ukiamini kua umasikini utatuua? Kwani ungekubali kuishi kwenye ukweli wako ungepungukiwa nini?" Meddy aliendelea kuuliza maswali mengi mfululizo, kila mmoja alionyesha mshangao kwa kile alichosikia.

Madam Ziya uso ulimshuka, kama ni maji tayari yalimwagwa mchangani anaanzaje kuyazoa! ilibaki na yeye ajitose ili azichezee tope. Alianza kwa kuomba radhi kwa wote waliokua mbele yake, alimsogelea Meddy na kumkagua baadhi ya maeneo.

"Zamedi...wewe kweli ni kijana wangu na hilo ndio jina lako halisi. Wewe ni mtoto wa pekee niliyebahatika kukupata katika ulimwengu huu. Nilikuacha mikononi kwa bibi yako ukiwa na mwaka mmoja tu hii ilikuja pale ambapo Mr.Lami alitaka kuanzisha familia na mimi, nilimdanganya ya kua sikua na mtoto wala ndugu yoyote kwenye ulimwengu huu , hii ilimzidishia huruma juu yangu na kumfanya aanzishe familia na mimi. Changamoto ilikuja baada ya kupita mwaka bila ya kushika ujauzito , hospitali zote tulizunguka kutafuta tatizo ila majibu yalitoka kuwa hakukua na shida kati yetu....." Madam Ziya alishindwa kuendelea na kuanza kujifuta machozi ambayo yalikua mashavuni mwake, alikohoa mfululizoili kuweka koo sawa.

"Mume wangu alinisisitiza niwe na subira ila sikutaka kumsikiliza maana niliamini mwisho wa siku na yeye angechoka na kutafuta mchepuko, hapo ndio niliamua kutengeneza ujauzito feki na hata mtoto nilimnunua, mtoto huyo ni Romy. Romy ambae alikuaj kubeba kila upendo ambao babaake alikua nao juu yangu. Chuki zangu dhidi yake zilianza hadi mume wangu kugundua na ndio maana hakuwahi kuniweka kwenye usimamizi wa mali zake. Hiyo ilikua ni kama adhabu yake kwangu" Madam Ziya aliamalizia simulizi yake hiyo kwa sauti iliyojaa majuto.

"Mama...wewe utabaki kuwa mama kwangu siku zote, mimi haya nilishakusamehe kwa sababu niliyajua zamani hata kama sikua najua kama una mtoto. Baba aliwahi kunieleza kila kitu na hata sababu ya kifo chake basi najua kuwa ni wewe. Kila mmoja wenu atapata hukumu kulingana na makosa yake, Niffa nakutegemea kwenye ushahidi"

"Sipaswi kulaumiwa kwa hili, sikua najua chochote Romy!! tafadhali naomba msamaha wako. Mamaangu ataishije akisikia haya" Larah alizungumza kwa sauti ya kilio.

"Larah , kwenye hili lawama inakuhusu. Nilijiweka karibu sana na wewe ili nikueleze alichokifanya Meddy ule usiku tulipokua hotelini matokeo yake hukunipa nafasi ya kujieleza. Niliwafatilia mwenyewe na kila mlichokua mnakipanga basi mimi nilikua najua, sikutaka kuonyesha utofauti wowote na ndio maana niliwakumbatia ili niendelee kuwajua njama zenu, Larah kuhusu mama nitamhudumia " Meddy alizungumza hayo na kutoka huku akiwaacha watu wake wakiwa chini ya ulinzi.

Tusilolijua ni kwamba Meddy alifatilia mambo yake kimyakimya, aliwaacha wabaya wake wafanye walichodhamiria huku akiweka usalama wake na mali zake chini ya jeshi la polisi na ndio maana ukamatwaji wa Meddy na Siti ulifanyika haraka na kwa urahisi.

Mama Larah aliwekwa wazi kuhusu matukio yaliyojitokeza, alisikitishwa mno na kumuomba sana Romy amsamehe binti yake. Sheria ilichukua hatua dhidi ya wahalifu pale pande zote zilipojitosheleza kwa ushahidi. Larah alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja huku faini ikiwa juu yake. Meddy na Madam Siti kulingana na makosa yao walihukumiwa miaka 10 . Madam Ziya kwa vile alikua na hatia ya kumuua M.r Lami basi alihukumiwa kifungo cha maisha. Niffa aliachiwa huru baada ya kushiriki kikamilifu kutoa ushahidi wake ambao alikua nao.

"Ulimwengu unanihukumu kwa makosa yangu, lakini ningefanya nini ikiwa Meddy alikua ni msaada wa pekee kwenye maisha yetu. SIPASWI KULAUMIWA mimi wala maaangu, hata kama ningejaribu kumsikiliza Romy basi upendo wa Meddy juu yetu usingevunjika, unajua kwa nini? Sitaki kuufanyia kazi msemo wa mema elfu moja hufuta baya la siku moja. Nakupenda Romy na upendo wangu ulikua kwako siku ya kwanza tu kukuona , sijutii usichana wangu kuondolewa na wewe kwa sababu nilikupenda, ugumu wa maisha ndio hutufanya tuchukue maamuzi yasiyofaa kwenye maisha yetu , Naamini mama yupo kwenye mikono salama" . Huo ulikua ni ujumbe ambao Larah aliuacha baada ya kujinyonga akiwa gerezani, asubuhi ilionekana maiti yake ikining'inia huku chini yake kukiwa na maandishi aliyoyaandika kwa kutumia mkaa.

Romy alishangazwa na kusikitikika mno na maamuzi ya Larah, yeye aliacha apewe adhabu ili ajifunze makosa yake na sio kumkomoa. Aliumia mno moyo wake maana bado alikua na hisia za mapenzi dhidi yake. Kibarua cha kumuweka sawa mama Larah alikua nacho maana haikua rahisi, mwisho wa siku alimchukulia mama Larah kama mamaake , alimshirikisha na kuomba ushauri kwenye mambo yake mbalimbali.
MWISHO
 
Back
Top Bottom