*SEHEMU YA 13 *
Mazungumzo kati ya mama na mwana hayakufikia muafaka, Romy hakutaka kabisa taasisi yao iendeshwe na mamaake kwani aliijua vyema tabia yake ya ukorofi, hakua na lugha nzuri hata kidogo akiwa na wafanyakazi jambo ambalo huwanyima uhuru wa kufanya kazi , Jee leo akirudi kwenye nafasi yake ya zamani? walipokua katikati ya mabishano Romy aliamua kuondoka kwa hasira na kwenda kujifungia chumbani kwake.
"Mtoto mdogo tu wewe! unataka ushindane na mimi? Unajua tabu nilizopitia hadi kukupata wewe? Heeeh kumbe hunijui wewe sasa subiri! Kati yangu na wewe nani zaidi? " alizungumza mama Romy huku akijiinua kiuvivu kuelekea chumbani kwake.
Mama Romy ambae alizoeleka kwa jina la Madam Ziya alikua ni mama wa miaka 45 , mumewe ambae ni baba wa Romy aliiaga dunia miaka 4 iliyopita baada ya kuugua kwa muda mrefu, ugonjwa uliofanikiwa kuondoa uhai wake haukuwekwa wazi hadi leo hii. Kabla ya umauti kumfika aliamua mali zake zote ziwe chini ya usimamizi wa mtoto wake wa pekee ambae ni Romy na yote ni kutokana na kuona mwenendo mbaya wa tabia za mke wake. Hili ndio jambo ambalo lilimchanganya na kumuudhi mno Madam Ziya.
**********
Ni upweke pekee ambao alikua nao mara tu alipoingia kwenye chumba ambacho mamaake alilazwa, hakuweza kuyazuia machozi yake yasitiririke mashavuni mwake kutokana na uchungu ambao alikuwa akiusikia moyoni mwake. Akiwa kwenye majonzi hayo mazito alishtuka mkono wa mamaake ukiwa umeishika nguo yake , alipojaribu kumtazama kwa mshangao basi alishuhudia tabasamu ambalo lilikua na maumivu ndani yake.
"Mama umenishika!! Larah aliuliza kwa mshangao huku akiutazama mkono wa mamaake ambao bado uliendelea kushikilia nguo yake.
"Larah....." Mama Larah aliita jina la bintie kitendo ambacho kilizidisha mshangao na taharuki kwa bintie.
"Naam mama" Larah aliitika huku akiyafuta machozi ambayo hayakuacha kutiririka , haikujulikana kama yale machozi ni ya furaha au huzuni ambayo alikua nayo awali.
Ingawa ni siku mbili zilipita sauti ya mamaake hakuwa ameisikia masikioni mwake ila kwake ilikua kama mwaka , matumaini yalirejea maana hakutegemea kama mamaake angeweza kurudi kwenye hali yake haraka namna ile , licha ya kwamba sio kama zamani ila aliamini kuwa funika hailingani na wazi alimtazama na kumkumbatia kwa furaha huku asiamini kama hayupo kwenye ndoto.
Aliifurahia mno hiyo hali ila bado matukio ambayo yalitokea siku mbili hizo yalimfanya akose umakini, Larah alijikuta akiomba msamaha kwa mamaake huku machozi yakiwa mashavuni mwake, alichodai yeye ni kusamehewa kwa kutofika kwa wakati hospitalini hapo wakati ambao alihitajika , Mama Larah aligundua hofu ya bintie na namna ambavyo alikuwa akiomba msamaha, kama mzazi aligundua uwepo wa tatizo jengine ila aliamua kunyamaza kama ambavyo yeye alinyamaziwa, alifahamu yote hayo baada ya kuona Larah hakua sawa licha ya kwamba waliamua kusameheana na kuwekana sawa.
"Larah , najua una mengi ya yanakusumbua ila ukiwa tayari kusema basi mamaako nitakusikiliza, hongera pia kwa kazi yako mpya ambayo umefanya, nilitamani siku yako ya kwanza nikupe hongera ila ndio hivyo Mungu kaleta hili , Meddy alinieleza sababu ya kutokuwepo kwako hapa nilipozindukana, nimefurahi mno kuona unapambana kwa ajili yangu mwanangu, mheshimu na umsikilize sana Meddy maana yeye ndie ambae anatumbania" Mama Larah aliongea kwa upole na tabu huku akiwa bado kashikilia mikono ya bintie
Larah siku huyo alilala pembeni ya mamaake, alitamani kumwambia kitu ila alijikuta kushindwa, akiwa pale hakuwa tayari kurudi kabisa nyumbani kwao ila kwa vile hakuruhusiwa kulala hospital basi ulipofika muda ilibidi aondoke.
**********
Siku, wiki na mwezi ulipita Larah akiwa ni muajiriwa rasmi wa Perfect na balozi wa Zuri Fashion, pesa aliyoingiza ni ndefu hali ambayo ilimfanya azidi kupendeza na kuongeza bidii ya kufanya kazi kila uchao, aliamua kupambana lengo ikiwa ni kuipigania afya ya mamaake ambae bado alikuwa akiendelea na matibabu hospitaki lakini pia lengo jengine ilikua ni kuilinda thamani ya utu wake ambayo kuna mtu aliishika mikononi mwake, hilo lilimkosesha raha kila leo na kumfanya abaki kwenye utumwa wa mawazo, alijitahidi kumtafuta aliyemuonyesha video na picha zake chafu ila hakufanikiwa kumpata tena, alimchukia mno Mr.Romy huku akimvua thamani yote ambayo alimpa siku ya kwanza walipokutana.
Kama mvumilivu hula mbivu basi Larah hakuwa miongoni mwao, siku hiyo aliamua kuuvunja ukimya ambao unamtesa, mara tu alipotoka kazini basi alimfata Meddy sehemu ambayo alikua akiishi, alimchagua yeye maana aliogopa kumueleza mamaake jambo zito kama hilo, hakutaka kumzidishia maradhi kabisa.
"Larah mbona umepoa hivyo nini shida? Hilo ni swali ambalo Larah alipigwa nalo mara tu baada ya kufika chumbani kwa kipenzi chake Meddy.
Kilio ilikua ni jibu tosha kwa yale maumivu ambayo anapitia, nafsini mwake alijiona ni mwenye hatia kubwa mno .Dhambi ambayo aliibeba kifuani mwake ilimtesa kiasi cha kukosa ujasiri hata wa kumtazama Meddy usoni mwake. Larah alibaki kulia asijue wapi anaanzia kusimulia. Hata ule mdomo alioutegemea pia ulimsaliti maana ulishindwa kutamka neno na badala yake ulibaki kutetema. Ule ujasiri aliotoka nao kazini kwake basi pia uliyeyuka mithili ya barafu jangwani.
Meddy alijiinua kitandani kwake na kumfuata Larah ambae alikua kwenye kochi, alimsimamisha na kumkumbatia huku akimpiga makofi madogo madogo mgongoni. Kilichofuata hapo ni sauti ya kilio ambacho bila shaka kilionekana wazi kuwa kilivumbikwa muda mrefu .
"Lia Larah lia mamaaa" Meddy alimnong'oneza Larah kwa kuamini kufanya hivyo kunaweza kupunguza hasira za uchungu na maumivu.
Baada ya robo saa kupita Larah alirudi kwenye hali yake ya kawaida na maongezi yalianza, Meddy alitaka kujua kinachomtesa Larah hadi kufikia hatua ya kulia na kuonekana mwenye majonzi, alionyesha wazi kuwa hakupenda kumuona kipenzi chake kwenye hali ile. Ni mara kadhaa alitaka asimuliwe ila hakuwahi kupata nafasi .
Larah aliamua kuitoa siri yake ambayo alihisi kuendelea kukaa nayo itazidi kumuumiza, hakuna tukio hata moja ambalo aliacha kusimulia, kila kitu alikimwaga kwa Meddy akiamini hapo ni sehemu salama na pia angeweza kupata msaaada, kila neno ambalo Larah alitamka basi kwa Meddy ilikua ni kama mwiba wenye ncha kali uliochoma moyoni mwake , maumivu yaliyoshikana na hasira yalionekana usoni mwake na kushindwa kabisa kujizuia hadi kufikia hatua ya kupiga ngumi zisizo idadi kwenye ukuta.
"Larah... uliwezaje kukaa na kitu kikubwa namna hiyo? haki ya Mungu ningejua mapema basi nisingeruhusu ukanyage tena sehemu ile" Meddy aliuliza kwa hasira .
"Meddy, hayo hayana umuhimu tena kwa sasa, kama kulia nimeshalia sana na wala haikusaidia chochote...inatosha kwa sasa , ninachotaka kwa sasa ni kumkomesha Mr.Romy , nataka kumfanyia kitu ambacho hatakaa akisahau kwenye maisha yake yote" Larah aliongea kwa ujasiri huku akijifuta michirizi ya machozi kwenye mashavu yake.
Meddy hakua na sababu ya kupinga kwenye hilo, aliufurahia sana uamuzi wa Larah maana hata yeye hakupenda pia , kukichobaki hapo ilikua ni kupanga mipango ambayo waliamini ingekwenda kumkomesha vilivyo Mr.Romy, watu waliandaa mabomu ya kwenda kumsambaratisha Mr.Romy na taasisi yake ya Perfect Advertising
Siku hiyo Larah aliondoka kwa Meddy akiwa na matumaini makubwa mno, ule moyo wake wa upole na upendo aliuweka pembeni na kujivisha moyo wa kisasi na chuki , aliamini kupitia mipango yao kutampunguzia maumivu kiasi fulani.
********
Mr.Romy na mamaake bado walikua kwenye mgogoro mkubwa , kiukweli madam Ziya hakupenda kabisa Larah kufanya kazi pale na sababu yake kuu ambayo alidai ilikuwa ni elimu na hadhi ya binti huyo, alijiandaa kumuondosha kwa namna yoyote ile bila kujali utendaji wake mzuri wa kazi na kiasi kikubwa alichokiingiza kwenye kampuni
Alipokua chumbani kwake alinyanyua simu yake na kuanza kuitafuta namba ambayo alihisi mmiliki wake angeweza kufikia nae muafaka kwenye mpango wake. Namba ambayo aliipiga haikuchukua sekunde nyingi ilipokelewa.
"Nadhani huu ndio muda wa kukamilisha mpango wetu, hakuna kuchelewesha mambo" sauti ya Madam Ziya ilisikika ikitoa maelekezo kwa njia ya simu........itaendeleaaaaaa
SIMULIZI: LARAH (Sipaswi kulaumiwa)
MTUNZI&MWANDISHI: Talhatmoudy 🥰
FACEBOOK PAGE: Talhat moudy love stories.
WHATSAPP No: 0718927182.
*SEHEMU YA 14 *
Siku mpya iliwasili kwa mara nyingine mtaani Geza , kama kawaida yao hekaheka za kuyapambania maisha yao waliziweka mbele huku zile changamoto wakizichukulia kama ni fursa kwenye safari yao ya utafutaji, huu mtaa ulikosa wasomi tu lakini kwa kuchakarika basi walikua hodari mno.
Larah kama kawaida yake alijiamkia mapema na kutupia mavazi yake ambao yaliendanana na kazi ambayo aliifanya , kwa kipindi hiki alikua anapendeza mno maana anatupia mavazi kutoka ZURI FASHION. Licha ya kwamba alianza kufanikiwa na kuingiza pesa ndefu ila hakuweza kuuacha mtaa wake, hata yale maringo basi pia hakua nayo zaidi anapokutana na watu wa jamii yake, watu ambao anaamini kua wao ndio walimlea na kumpa moyo wa kupambana, naam aliwachukulia kama mashabiki wake wanaojivivunia na kuisapoti kazi yake.
"Nimejitolea kujiboresha na ninazidi kuwa bora kila siku . Sitazuiliwa na majuto au makosa niliofanya zamani kamwe, mimi Larah ninatakiwa kusonga mbele kila siku. Hakika hakuna lisilowezekana kwangu. Mr.Romy ...Nakuja kivingine" alijisemea Larah huku akijiweka sawa kwenye pande lake la kioo chake kikubwa, hakua amenunua chingine licha ya kwamba pesa aliipata, kweli cha kale dhahabu.
Baada ya robo saa kuipoteza kwenye kioo na kujihakikishia muonekano wake haraka sana alitoka nje lengo ikiwa ni kwenda hospitali kumuona mamaake kabla ya kuelekea kazini, njia nzima siku hiyo alikua akitabasamu tofauti na siku za nyuma alipokua na msongo wa mawazo.
***********
Jamani Perfect Advertising ilijua kujitangaza bwana, siku mpya kwao ilianza na neema ya kupokea donge nono kutoka WEA (WOMEN EMPOWERING AGENCY) . Tangazo ambalo walitakiwa kulifanya lilikua linatakiwa kuonyesha ni kwa namna gani mwanamke anaweza kufanya kazi yoyote ile endapo kuna nguvu itawekwa ndani yake ikiwemo ya kuaminiwa.
Mr.Romy aliwaita wakuu wa Department zote na kuwaeleza kazi iliyopo mezani kwao, kwenye kikao hicho waliweza kujadili namna ambavyo wangeweza kuifanya kazi hiyo ambayo ilipangwa kuonyeshwa kwenye kilele cha siku ya Wanawake Duniani. Baada ya majadiliano hayo yaliyochukua masaa matatu watu walitawanyika na kwenda kwenye Department zao kuufikisha ujumbe kwa wajumbe ambao hawakuwepo kwenye mjadala.
Mara tu baada ya kutoka kwenye kikao Mr.Romy alipokea ugeni kwenye ofisi yake, huu ulikuwa ni ugeni ambao alijua kivyovyote ungewasili kutokama na kile kilichotokea kati yao usiku wa jana. Madam Ziya alikaa kwa kutulia kwenye kiti huku huku akitupia macho kila kona ya ofisi ambayo hapo zamani aliitumia yeye .Ni kama vile alikua akitafuta kitu.
"Nadhani ujio wangu umekuja na neema, maana nasikia WEA wamekuja na dili nono, Rommy kijana wangu.... naomba kwenye hili tuwe pamoja maana ninao uzowefu mkubwa na pia hawa watu tulishawahi kufanya nao kazi hapo nyuma " Madam Ziya ambae ni mama Romy alianza mazungumzo ambayo hayakumfurahisha kijana wake hata kidogo.
Mr.Romy alishangazwa na maelezo ya mamaake, alijiuliza wapi mamaake kapata habari hali ya kuwa dili hilo wao wamelipata asubuhi, aliwaza ni jibu gani ambalo angeweza kumpa mamaake bila kumkasirisha na kumfanya aridhike , aliujua vyema moto wake endapo angemkatalia.
Akiwa katikati ya fikra hizo nzito mlango wa ofisi yake uligongwa na mgongaji aliruhusiwa, alieingia ni Siti akiwa kapendeza balaa hiyo siku, muonekano huo ulimfurahisha mno Madam Ziya maana tabasamu lililoiva lilidhihirika usoni mwake.
"Aaah kipenziii.... ndio umenawiri kiasi hiki? Yaani kutokukuona mwaka mmoja tu tayari umekua mzuri namna hii!! Romy hemu mtazame vizuri Siti, Unamuonaje?" Aliuliza Madam Ziya kwa bashasha huku macho yakiwa kwa kijana wake, Siti yeye macho chini akijionea zake aibu ila kwenye nafsi yake alifurahia ile hali.
Romy hakutaka azidi kumvunja moyo mamaake, aliamua kutikisa kichwa kama ishara ya kukubali huku akiachia tabasamu hafifu ambalo halikua na ukweli ndani yake. Siti aliyaweka mafaili kwenye meza na kisha kutoka nje huku akiwaacha mama na mwana waendelee na mazungumzo yao.
"Mwanangu ....Lengo la kuwepo hapa ni kukusaidia kwenye haya majukumu ambayo upo nayo, nina uzowefu wa kutosha na nimefanya kazi kwenye taasisi hii kwa miaka isiyopungua kumi na tano hadi pale babaako alipoamua kukuweka wewe, Romy sikatai wewe kuwa msimamizi ila bado nakuona una ujana mwingi" alizungumza Madam Ziya kwa utulivu kama sio yeye aliyeingia na moto.
"Romy , hodari sio yule anaejua lakini hodari ni yule ambae yuko tayari na hachoki kujifunza kutoka kwa wengine, Romy naomba niwe pembeni yako" Madam Ziya aliendelea kumshawishi kijana wake huku macho yake yakionyesha uzito wa kile anachokizungumza.
"Sawa mama nimekuelewa , ila wafanyakazi wangu sitaki uwaondoe , Mama....sipendi dharau kwa wafanyakazi wangu, tukiwa na tabia zenye kufanana basi siku zote utakuwa pembeni yangu maana mimi bila wewe sio kitu" Mr.Romy alikubali ila hakuacha kumuwekea vikwazo mamaake.
Madam Ziya alifurahia kwenye nafsi yake huku akimuahidi kijana wake kubadilika, hakuacha kumzungumza Siti kwa sifa nzuri na urembo ambao alikua nao , yeye alitaka awe mkwe wake ili familia yao izalishe watoto watakaokua wasomi kama wazazi wao.
"Mama , nitaoa wakati sahihi ukifika, nitaoa endapo yule mtu sahihi ninaemtumainia kwenye maisha yangu akiwa tayari kuwa na mimi" Mr.Romy alijibu kwa upole majibu ambayo yalimshtua mamaake.
"Weeh Romy! Unamaanisha tayari kuna mtu yupo moyoni mwako?"
"Haswaaa!! muda muafaka wa kuonekana ukifika basi utamuona" alijibu tena Mr.Romy majibu yaliyozidi kumuacha kinywa chake Madam Ziya .
Hadi kufikia hapo hakukua tena na swali ambalo mama yule aliuliza, kwa siku hiyo aliondoka huku akitegemea kufanya kazi rasmi siku itakayofata. Baadhi ya wafanyakazi waliomuona akitoka walishusha pumzi zao maana walikua na hofu ya kupoteza kule kilichopo mikononi mwao.
*************
Jua ndio lilikuwa linaelekea kuzama huku mwezi ambao ungewapa nuru Wanageza wakati wa usiku ukijiandaa kuchomoza, Larah aliamua kwenda kwa Meddy lengo ikiwa ni kumpasha habari mpya ambayo ilitokea ofisini kwao, habari hiyo aliamini kua kwa namna moja ama nyingine itatumika kwenye mpango wao ambao waliupanga.
Alifanikiwa kufika kwa Meddy na kumkuta akikorofisha mambo nje ya chumba, harufu ya chakula ndio ilizisumbua tundu zake za pua na kushindwa kujizuia hadi kuanza kukisifia chakula kabla ya kukitia mdomoni.
"Yaani Meddy utakae muoa wewe basi atafaidi mno" Larah alianza mazungumzo huku akikaa kwenye kizingiti cha mlango, hakujali hata nguo yake kuchafuka.
"Aaaah Larah, mke wangu mimi ni wewe hapo" majibu hayo ya Meddy yalimfanya Larah atoe kicheko kwake yeye alijua ni utani ila mwenziwe alionekena kumaanisha.
Baada ya maongezi yaliyojaa matani yaliyosindikiza mapishi hatimae chakula kiliwiva, waliingia chumbani na kuanza kula huku story za utani zikiendelea hadi walipomaliza. Larah aliamua kufunguka kile ambacho kilimpeleka pale jioni ile, aliamua kumwaga kila kitu ambacho kilitokea kwenye taasisi yao kwa siku hiyo, hata ujio wa Madam Ziya pia aliuweka kwenye mazungumzo.
Meddy alionekena kushtuka mno alipolisikia hilo jina, Larah alimshangaa Meddy ambae alionekana kukasirika licha ya kwamba alijitahidi kuzuwia hasira zake zilizojiachia wazi.
"Meddy kwani vipi? Una mfahamu huyu mama? Na mbona unatetemeka hivyo?" Larah alihoji kwa sauti ya wasiwasi huku akimsogelea Meddy ambae alikua kwenye sofa.....itaendeleaaaaaa
SIMULIZI: LARAH (Sipaswi kulaumiwa)
MTUNZI&MWANDISHI: Talhatmoudy 🥰
FACEBOOK PAGE: Talhat moudy love stories.
WHATSAPP No: 0718927182.
*SEHEMU YA 15 *
"Meddy kwani vipi? Una mfahamu huyu mama? Na mbona unatetemeka hivyo?" Larah alihoji kwa sauti ya wasiwasi huku akimsogelea Meddy ambae alikua kwenye sofa.
"Larah, hii dunia ina watu wa ajabu sana tena wenye roho mbaya kiasi ambacho hata shetani mwenyewe anaweza kaa kando akawapisha wao. Larah...simpendi kabisa huyu mama na haitakuja kutokea siku nikampenda" Meddy alizungumza kwa hisia za uchungu mno hali ambayo iliibua maswali kwenye ubongo wa Larah.
Meddy ni kama vile aliiwahi akili ya Larah maana alimzubaisha kwa kumbatio ambalo lilichukua dakika kadhaa, alifanya hivyo akiamini kuwa na yeye hasira zake zitapungua .
"Ndege haimbi kwa sababu ana jibu bali anaimba kwa sababu ana wimbo . Larah ipo siku utajua kwanini namchukia huyu mama ila sio wakati huu, nahisi huu ni muda sahihi wa kufanya kile ambacho wanastahili kufanyiwa , hii familia watu wake ni wa ovyo sana" Meddy alizungumza hayo kwa uchungu uliochanganyika na hasira ambazo alishindwa kuzizuia mbele ya binti mrembo.
Meddy alisogeza hatua zake za miguu hadi kwenye dirisha la chumba chake baada ya kusema maneno ambayo yalizidi kumuweka njia panda Larah. Dakika chache zilipita ikiwa hakuna hata sauti ya sisimizi aliyekatiza, kila mmoja alikuwa akiwaza lake kichwani. Larah alimsogelea Meddy na kumgeuza sura yake ambayo ilielekezwa dirishani, alishtuka sana baada ya kushuhudia uso wa Meddy ukiwa umerowana machozi.Alitumia viganja vyake kuyafuta machozi yaliyotiririka mashavuni mwa Meddy.
" Meddy najua wakati wangu sahihi wa kujua haujafika, lakini kuanzia muda huu na maisha yangu yote nitaitolea nafsi yangu kwa mapambano yoyote yaliyopo mbele yetu, tena zaidi yakiwa yanaihusu ile familia.Meddy nipo mbele yako kukusaidia nitumie uwezavyo basi mimi nitafanya" Larah alizungumza hayo kwa upole maneno ambayo yalirejesha tumaini kwa Meddy maana alitabasamu.
Nguvu ya hisia za mapenzi ilizaliwa kwenye mwili wa Meddy baada ya kumkumbatia Larah kwa mara nyingine, alijikuta anapitia wakati mgumu mno pale alipoyasikia mapigo ya Larah yakidundia kifuani mwake. Hayo pia yalijiyokeza kwa Larah maana na yeye alizipokea hisia hizo kwa mikono miwili huku akitoa ushirikiano, kila mmoja alijikuta akiutalii mwili wa mwenziwe vyema kwa kutumia mikono yake. Mapigo yao kwa muda ule yalibadili muelekeo na kuelekea kwenye bahari ya huba❤️huko walijikuta wakizama na kuanza kupunguza hisia ambazo kila mmoja zilionekana kumzidi.
Licha ya ugeni wake kwenye mchezo huo ila hakutaka kamwe aonekane mbumbumbu, mara yake ya kwanza alivyofanya hakua ameona raha yoyote hivyo kwa wakati huu alitamani kuzijua, Larah alijituma kadri awezavyo ili amridhishe yule ambae alikua juu ya kifua chake, ni kama vile alikua na hasira maana alihakikisha kila kilichomjia akilini anakifanya, yeye ni mtoto wa kike anaachaje kuwa mbunifu. Hatua zote alizipitia hadi kufikia mwisho wa mtanange huo ambao uliisha kila mmoja akiwa hoi.
Meddy alifurahishwa na huo mchezo maana ni siku nyingi mno alitamani itokee, Larah yeye alibaki na aibu pale alipogundua kua Meddy alikua akimtazama kwa matamanio kwenye mwili wake ambao haukua na nguo hata moja.
"Larah , usijisikie vibaya kwa hiki kilichotokea, zote hizi ni hisia ambazo tumeshindwa kudhibiti , nitakupenda siku zote , nitakuheshimu na kukufanya ujione wa thamani ulimwengu huu" kwa sauti yake ya kubembeleza Meddy alichombeza mbele ya Larah ambae alibaki akitabasamu.
Hazikupita hata dakika tatu walijikuta wakiurejea tena mchezo, siku hiyo usiku wote waliutumia kupunguza uzito kwenye miili yao.Kila mmoja alitumia ujuzi wake kumridhisha mwenziwe.
******
Siku mpya ilimkutia Larah kwenye chumba cha kipenzi chake Meddy, wa mwanzo alikua ni yeye kuamka hivyo alipata wasaa mzuri wa kumtazama usoni Meddy ambae bado aliendelea kuuchapa usingizi.
"Siijui asili yako ila unaonekana umepitia magumu mengi huko nyuma, una moyo wa huruma na kujali kwanini nisikutunuku upendo? Meddy chochote unachotaka nitafanya " Larah alizungumza kwa sauti ya chini mno, alipotaka kujiinua alijikuta akivutwa mkono wake na kuangukia kifuani kwa Meddy.
"Larah......NAKUPENDA, kuhusu mimi utanijua kadri siku zinavyosogea" kwa sauti iliyojaa upendo Meddy alijikuta akizungumza maneno machache ambayo yaliisuuza na kuiridhisha nafsi ya Larah.
Walizungumza mengi kuhusu penzi lao jipya , hawakusahau kamwe mpango wao ambao ulikuwa kwenye akili zao. Meddy alimpa maelekezo yote Larah huku akimtaka aweke umakini kwenye utekelezaji. Larah alitimkia nyumbani kwao kwenda kujiandaa huku akimuachia maagizo Meddy kuhusu mamaake.
******
Kila timu ilikua tayari kwenda location kwa ajili ya kushoot kile ambacho walielekezwa , Larah alijikuta akiwa miongoni mwao baada ya yeye kuonekana anafaa zaidi, alifurahi mno na kuona sasa mipango yake inakwenda kukamilika, hakuchoka kumkata jicho lake kali Mr.Romy ambae alikua akiwapa nasaha juu ya kazi hiyo.
Safari yao ya kwanza iliishia kwenye garage kubwa ambayo ilipatikana katikati ya mji, huko Larah alitakiwa avae mavazi ambayo yanaendana na hiyo sehemu, makeup artist walikuwepo hivyo alitengenezwa kama mwanamke ambae ile ni sehemu yake ya kazi, uso na nguo za Larah zilipakwa oil huku akitakiwa alale chini ya uvungu wa gari spanner ikiwa mkononi mwake.
Wapiga picha ndio ambao walikua na kazi ya kumtaka Larah abadilishe position wakati zoezi likiendekea, Mr.Romy alijikuta na yeye akitoa simu yake na kuanza kumpiga picha Larah bila ya wengine kuona , yaani alifanya kwa kuibiaibia maana pale hawakuruhusu picha zipigwe ovyo na watu wengine zaidi ya mpiga picha ambae walienda nae.
Baada ya hapo kumaliza walielekea soko kuu la JIZOLEE huko walimuomba mamantilie mmoja awaazime nguo zake ili waupate ule uhalisia, Larah na huko alijiachia maana ilikua ni sehemu ambayo aliizowea, mpiga picha hakua na kazi kubwa ya kutoa maelekezo maana Larah alionekana kuwa na uzowefu. Mr.Romy na huko pia alijipigia picha zake za wizi bila ya wengine kufahamu.
Jioni iliwafikia wakiwa uwanja wa ndege wakimalizia zoezi lao, siku hiyo Larah alionekana kuchoka mno maana alipitishwa maeneo mengi mno ya kazi, hapo ndio alipoona kua kumbe wanawake wanaweza kufanya kazi sawa na wanaume ikiwa tu kutakua na nguvu ya kuwezeshwa pamoja na kutiwa moyo.
Kama kawaida Mr.Romy alimfuata Larah ambae alikwenda kubadili nguo sehemu ambayo walipewa uwanjani hapo, hakutaka hata kubisha hodi maana alijua asingefunguliwa mlango. Larah alishtuka mno kumuona Mr.rommy mlangoni ikiwa yeye hana nguo yoyote mwilini mwake, alijiziba kwa mikono yake maana nguo zilianguka zote kutokana na mshtuko.
Mr.Romy alijitahidi kukwepesha macho yake ila tayari alichelewa maana aliweza kuuona mwili wa Larah ukiwa bila nguo, hilo lilimkera sana Larah na kujikuta ile chuki dhidi yake ikiongezeka.
"Najua kuwa na hii ni kazi ambayo wanawake inawaingizia kipato ila sikufikiria kama mtaijumuisha, haya camera ipo wapi? " Larah alizungumza kwa hasira maneno ambayo yalimshtua mno Mr.Romy.
"Larah unazungumza nini? Sipo hapa kwa lengo hilo hemu vaa nguo basi tuongee kidogo" Mr.Romy alijibu huku uso wake bado ukiwa pembeni.
"Mmh! usichokijua kwenye mwili wangu ni nini? Hivi unadhani sifahamu mchezo wako unaoendelea kuucheza kwangu?
Maswali ya Larah yalimfanya Mr.Romy ageuke bila ya kutaka , alimsogelea Larah ambae safari hii mwili wake hakua ameuziba hata kwa mikono, mara tu alipomfikia alinyanyua..........itaendeleaaaaaa
SIMULIZI: LARAH (Sipaswi kulaumiwa)
MTUNZI&MWANDISHI: Talhatmoudy 🥰
FACEBOOK PAGE: Talhat moudy love stories.
WHATSAPP No: 0718927182.
*SEHEMU YA 16 *
Maswali ya Larah yalimfanya Mr.Romy ageuke bila ya kutaka , alimsogelea Larah ambae safari hii mwili wake hakua ameuziba hata kwa mikono, mara tu alipomfikia alinyanyua taulo kubwa ambalo lilikua chini na kumfunga Larah mwilini mwake.
Baada ya hapo alishindwa kudhibiti hisia zake na kujikuta akimkumbatia zaidi ya dakika mbili, Larah alijitahidi kujitoa kwenye kumbatio hilo ila ilishindikana maana alishikiliwa kisawasawa.
"Larah...." ilikua ni sauti nzito ya Mr.Romy ambayo ilikwenda kusisimua mwili wa bibie, hakua na ujasiri wa kuitika kwani hisia za utamu na uchungu zilimuandama na kujikuta akiubana kimya.
"Larah...." aliita kwa mara nyingine tena kwa upole baada ya kuona kimya kimezidi, Mr.rommy ni kama alihisi kitu hivyo alijitoa kwenye kumbatio na kuitazama sura ya Larah ikiwa imerowana machozi. Alisikitika mno.
Viganja vyake alivitumia kuyafuta machozi ya binti ambae alikua mbele yake, alimhurumia na kujikuta akimkumbatia kwa mara nyingine tena , ni kama vile alimchochomoa maana Larah alijikuta akilia kwa sauti japo sio kubwa sana. Hisia za mapenzi juu ya boss wake zilimuandama Larah ila alijikuta akimchukia kutokana na unyama ambao alimfanyia.
"Larah....umelia sana, naomba nipe nafasi nijieleze kwako, umekua ukinichukia mno ila mimi......" kabla hajamaliza alichotaka kusema walisikia mlio wa viatu ukikaribia usawa wa chumba walichokua huku jina la Larah likiitwa kwa sauti , haraka sana Mr.Romy alijificha nyuma ya mlango ili atakaeingia asimuone na yeye apate kuchomoka kwa urahisi.
Ni kitendo cha sekunde chache tu Madam Siti kuwa ndani ya chumba na Mr.Romy kupata upenyo wa kutokea nje , kuna kitu Madam Siti alikua anakitafuta maana alizunguka pembe zote za chumba ila hakuna alichokipata, hakika aliisikilizia harufu ya Mr.Romy mwanaume aliyebeba hisia zake.
"Larah....upo sawa? Halafu mbona uso wako umejaa machozi ! Nini shida? Madam Siti aliuliza huku akiusoma vyema uso wa Larah ambae alikua kama aliyepigwa shoti maana hakuelewa nini cha kufanya.
"Weeeh Larah......" aliitwa tena ila wakati huu alishikwa hadi na bega ili hisia zake zirudi.
Ingawa alishtuka ila hakua na muda wa kupoteza, haraka alivuta nguo zake na kuvaaa bila kumsemesha chochote aliyekua mbele yake. Baada ya kumaliza alisogea hadi kwenye dressing na kuvuta pochi yake ili atokomee nje ila alijikuta akizuiliwa kwa kushikwa mkono.
"Unasemaje? Larah aliuliza kwa ukali swali ambalo lilimshangaza Madam Siti, ni kama masikio yake hayakutegemea kusikia kile ambacho kiliulizwa.
"Weeh Larah! Umejisahau unazungumza na nani? Halafu mbona kama ulikua na mtu humu ndani, yupo wapi? Madam Siti alihoji mikono yake bado ikiwa imemshikilia Larah.
Larah ni kama vile alikua akipotezewa muda wake, hakua na muda wa kuendelea kubaki pale kabisa , alijua tu kama angeendelea kuwepo basi ingepelekea kuzuka kwa mjadala mrefu , alijitoa kwa nguvu mikononi mwa madam siti na kujiandaa kuondoka.
"Ukijaribu kuuvuka huo mlango utajua mimi ni nani! Hii kazi utaiona chungu" maneno hayo kutoka kwa madam Siti yalimfanya Larah abaki akiwa kashikilia kitasa cha mlango.
"Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu, hivyo sijali wala nini! Sikuogopi..." Larah alizungumza hivyo tu na kuamua kutokomea nje huku akimuacha madam Siti mdomo wazi asiamini kile alichokisia.
Hakua na muda wa kupoteza, haraka na yeye alikwenda sehemu ambayo walikua wamepaki gari lao, aliwakuta watu wote kwenye gari wakimsibiri yeye tu. Alishangaa kumuona Mr.Romy ndani ya gari lake akiwa katulizana na dereva wake, alimtazama kwa jicho kali huku akijiapia kwenye nafsi yake kua ni lazima awe wake.
*********
Zilikua zimebaki siku mbili tu kueleke kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, Larah alikua na furaha mno maana alitegemea kua kile alichokipanga kinakwenda kukamilika. Hata upande wa afya ya mamaake pia mambo yalikua sio mabaya maana tayari alitoka hospitali na alianza kufanya mambo mengi bila usaidizi wa binti yake.
Mr.Romy yeye bado hakua na amani wala furaha , alijitahidi kuweka ukaribu na Larah ila hakuna alichoambulia zaidi ya maumivu ya kupokea maneno mabaya ambayo yalizidi kumuumiza, hakuvunjika moyo na alijipa imani ya kua siku moja atapata tu nafasi kwenye moyo wa binti huyo na kumueleza kile ambacho kinamtatiza kwenye moyo wake.
Madam Siti na yeye alijitahidi kujipendekeza kwa boss wake ila hakuna alichokipata zaidi ya dharau na onyo kali, hata Madam Ziya ambae ni mama wa Romy na yeye hakua na msaada maana alichoka kumhubiria kijana wake juu ya mahusiano yake na Siti . Chuki kati ya Madam Ziya na Larah ilizidi kuongezeka ila hilo halikumfanya Larah atetereke maana alijua kinachomfanya aendelee kuwa pale.
Muda wote kwenye nafsi yake alikua akitabasamu, aliona kua ule wakati wa yeye kuwa na furaha unakaribia kwa kishindo, alitamani saa zikimbie ili bomu alilolitega liripuke na aliowakusudia waumie kama alivyoumia yeye, siku hiyo aliondoka kazini mapema na kuelekea sehemu ambayo Meddy alipanga.
Walipokeana kwa mabusu motomoto huku kila mmoja akiwa na nyuso ya tabasamu, walipohakikisha kutosheka na kinywaji kisichokata kiu walijisogeza hadi juu ya kitanda na kuanza kutazamana kwa macho ya matamanio.
"Meddy , hakika wewe ni mwalimu bora kwangu! Sio tu kwenye uwanja wa mahaba lakini pia kwenye uwanja wa maisha ambao napaswa kuweka huruma na hisia pembeni ili nipambanie kesho yangu na kile ambacho naamini kitairejesha furaha yangu iliyopotea. Nina furaha kubwa mno leo wacha niimalizie kwako" Larah alizungumza hayo huku akianza kupunguza nguo mwilini mwake.
Meddy alijipigia kofi za ushindi moyoni mwake, hahaaa😁 embe tayari limeiva mbele yake , kisu anacho mkononi , anaanzaje kuacha kulimenya ? siku hiyo mmiliki wa uwanja alikua ni Larah licha ya kuwa yeye alikua mualikwa, alihakikisha hampi Meddy nafasi ya kufurukuta , alimkamata vilivyo kijana wa watu aliyebaki kuweweseka kutokana na huba zito alililopewa. Ujuzi wote ambao aliupata kutoka kwenye mitandao ya kijamiii siku hiyo aliufanyia kazi mwilini kwa Meddy, bwana mdogo alibaki akiugulia maumivu tu ya raha huku akishindwa hata kutikisa ukucha.
Baada ya saa nzima kukatika hatimae mechi iliyokosa washabiki iliisha, Meddy hiyo siku alimtazama Larah bila kummaliza, alichopewa kwa siku hiyo hakutegemea kabisa kama atafanyiwa na Larah binti ambae hapo mwanzo waliishi kama marafiki walioheshimiana na kuoneana aibu.
"Meddy ......nilikuahidi kua nitakufanya ufurahi, nilikuapia kua nitakua kando yako siku zote , sijui huko nyuma uliyopitia na wala sitaki kujua ila naamini huu ni wakati bora kwetu, tuufurahie ushindi wetu ambao siku za karibuni utakwenda kuwaliza wale waliotuumiza" Larah alizungumza hayo huku akivuta pochi yake ambayo ilikua na flash.
Moyo wa Meddy uliripuka kwa furaha ambayo alishindwa kuizuia na kujikuta akimkumbatia Larah kwa nguvu, ni kweli siku ile alikua na furaha ambayo inaonekana aliisubiri sana. Mvua ya mabusu aliishusha kwenye mwili wa mwanamke ambae alikua akitabasamu mbele yake.
Mipango endelevu ilizidi kutengenezwa ili kukamilisha lengo lao, kama ni ng'ombe basi tayari ilibaki sehemu ya mkia tu kuliwa, na aliyetakiwa kukamilisha ni Meddy mwenyewe mwenye mipango yake........itaendeleaaaaaa
SIMULIZI: LARAH (Sipaswi kulaumiwa)
MTUNZI&MWANDISHI: Talhatmoudy 🥰
FACEBOOK PAGE: Talhat moudy love stories.
WHATSAPP No: 0718927182.
SEHEMU YA 17
Tayari siku mpya iliwasili ndani ya mtaa wa Geza, tunawajua jinsi walivyo watu wa mtaa huu, kabla jua halijachomoza wao tayari walitawanyika kwenye pembe nne za dunia kwenda kujitafutia kile ambacho wamekipanga, kupata ama kukosa hayo waliyachukulia kama majaliwa ya Mungu. Larah alimaliza kumuweka sawa mamaake na yeye mwenyewe, alimsogelea na kumkumbatia kama wafanyavyo siku zote.
"Mwanangu, furaha uliyonayo usoni mwako naomba idumu siku zote, nafurahi sana kuona mafanikio yako huku na mimi nikiwa hai, najivunia uwepo wako maana umeweza kuipigania afya yangu. Mheshimu sana Meddy maana yeye ndie ambae kila siku amekua mstari wa mbele kwetu, nakutakia kila la kheri kwenye kazi zako...Mungu awe mbele yako binti yangu" Mama Larah aliongea hayo kwa sauti iliyosheheni furaha.
"Usijali mama, nakuahidi mimi binti yako nitabaki kua mwema kwako na yeyote yule aliyeshiriki kunishika mkono wakati wa dhiki" Larah na yeye aliahidi huku akimimina mabusu usoni kwa mamaake.
Huyu mama na yeye hajui tu kama mwanawe tayari keshazagamuliwa zaidi ya mara tano, huyo Meddy anayemsemea aheshimiwe bintie tayari kafanya mume. Au inawezekana pia huyo mama Larah anaelewa kinachoendelea kati yao lakini tu anajizima data😄
Mguu mosi mguu pili hatimae alizipata hatua ambazo zilimsogeza hadi nje ya nyumba ambayo walipanga, akiwa hapo alibahatika kuona kundi la watu likiwa limeduwaa mbele yake likimtazama , kundi hilo liliongozwa na wapangaji wenziwe, mwanzo alidhani labda ni kwa namna ambavyo amevaa , alijikagua na kujiridhisha kua hakua na kasoro yoyote katika mpangilio wa mavazi yake licha ya kwamba yalikua ya kisasa zaidi, bado kundi lile liliendelea kumpa hofu maana nyuso zao zilionekana kuwa na hasira huku nyingine zikionekana kutibuliwa, hawakuishia hapo tu kundi lile lilionekana likionyeshana jambo kwenye simu zao za kisasa huku mikono yao ikiwa kwenye midomo yao wakionekana kushaangaa kitu..
Alijipa matumaini ya kua pengine mpango wake na Meddy utakua umeshakamilishwaa, alifurahi kwenye moyo wake licha ya kwamba hofu juu ya zile nyuso ilimrejesha nyuma, aliamua kusogeza hatua zake mbele ili kuwakaribia kwa ukaribu zaidi ila alisita baada ya kuona sura ya Meddy ikichomoza mbele yake tena ikiwa haina nuru ya tabasamu hata kidogo, haraka sana alimsogelea kwa hofu maana kengele ya hatari iligonga kichwani mwake.
"Meddy kuna nini mbona sielewi? Kwani umefanikiwa kufanya lile jambo? Na kama umefanya mbona jamii yangu inaonekana kuwa na nyuso zilizokosa tabasamu dhidi yangu?" aliuliza Larah kwa hofu huku akimkokota Meddy pembeni .
"Larah, usijitoe akili ! Hivi umewaza nini kabla ya kuachia huo upuuzi wako?" Meddy aliuliza hayo kwa sauti ya ukali.
"Upuuzi gani Meddy? Nyoosha maelezo usinivuruge na wewe! Kwani si tuliamua pamoja " Larah aliuliza kwa hofu kubwa maana hakua akijua kosa lake.
"Pamoja na nani ? Usiniigizie Larah, mimi ndio nilikua na wewe pale kitandani? tayari video na picha zako za utupu ukiwa kitandani na Romy zinasambaa kwenye mitandao yote ya kijamii, nadhani umefakiwa kuonyesha uhodari wako kama mwanamke kabla ya kilele chako kufika...." Meddy alifoka kwa hasira.
Taarifa hiyo ilimshtua mno Larah, hakutegemea kamwe kama siku yake ambayo aliikaribisha kwa tabasamu inaenda kuangukia kwenye dimbwi la huzuni, moyo ulimuenda kasi na kumfanya akae chini bila kutaka. Aliwaza mengi kwenye akili yake hadi alihisi kuvurugwa.
"Meddy, kweli mimi naweza kufanya hivyo? Huyo atakua Romy tu ........nakuapia" kwa sauti ya kilio Larah alijitetea.
"Romy eeeh....inawezekana ikawa kweli ni yeye maana hata account zako umeamua kumpa yeye adhihirishe mahaba yenu ? Kwanini usingesubiri tumalize tulichokipanga? Umejidhalilisha mno na umenivunja moyo, tayari unaangukia kwenye sifa mbaya na kutupiwa kila aina ya matu...." kabla Meddy hajamaliza maneno yake alishtukia Larah akimalizia kuanguka chini kama mzigo.
Kundi ambalo lilikuwa pembeni yao liliwasogelea kwa ukaribu zaidi, Meddy hakujisumbua kumnyanyua zaidi ya kuondoka bila kutoa msaada wowote , watu ambao walimzunguka walibaki wakichukua picha na video ili wapate kuendeleza story ambayo ilibamba mitandaoni. Wale wasiokua na simu basi waliona ule ulikua ni muda sahihi wa kumtupia Larah matusi na laana kibao.
Kwenye wabaya siku zote na mwema huwa hakosekanani, sote tunamkumbuka shogaake aliyeitwa Niffa, huyu ndie ambae kwa muda ule alikua ni msaada kwake, Niffa alibeba jukumu la kumkokota Larah na kumuingiza chumbani kwao, huko alifanikiwa kumkuta mama Larah akiwa kwenye majonzi mazito, hii ilidhihirisha wazi kuwa masikio yake yaliweza kunasa kelele na maneno ambayo yalikua yakiendelea kutupwa huko nje, alimhurumia bintie huku akimshukuru Niffa kwa wema wake.
**********
Kiti chake kwa siku hiyo alikichukia maana hakua na hamu hata ya kukaa, hasira zilimvaa hadi uso wake uliiva na kuzidisha wekundu kwenye pua yake ndefu, Ngumi zisizo na idadi aliamua kuzibamiza kwenye ukuta wa ofisi yake hali iliyopelekea mikono yake kuanza kuvuja damu, alilia na kujilaumu katika nafsi yake. Kichwani mwake yalizunguka maswali ambayo hakua na uwezo wa kuyajibu maana hakuwa na kumbukumbu ya tukio ambalo linaendelea kutapakaa kwenye mitandao, anaikumbuka vyema siku ambayo aliingia na Larah moja ya hotel kubwa Geza ila hakuwa na kumbukumbu ya yeye kushiriki tendo wala kurikodi tukio lolote, nani alifanya? kwanini video iachiwe siku ile?
"Kwanini Larah! kumbe wewe ni nyoka eeeh? Sikuwahi kufikiria kamwe kama unaweza kufanya upuuzi kama huu! Sawa mimi na wewe hatukua sawa lakini ndio ulipize namna hii tena kuelekea siku muhimu ambayo Geza nzima inatutazama? Nitakutafuta na lazima utalipia kwa hili , nataka nijue nani yupo nyuma yako kwenye hili? " Romy alibwata kwa hasira machozi yakiwa usoni mwake.
Hakika ungemuona basi moyo wa huruma ungekuingia, Romy alijiweka kipembeni na kuinamisha uso wake kwenye mapaja yake akilia kwa hasira, alijuta kumfahamu Larah kwenye maisha yake, alijilaumu kwanini alimuamini kupitiliza . Hakua na habari ya mlango wa ofisi yake kugongwa mfululizo, mamaake aliita kila jina ila hakuna alichoambulia zaidi ya ukimya ambao ulimtia mashaka, uamuzi aliochukua ni kuwaita walinzi ambao walianza kuuvunja mlango.
Ule usemi wa uchungu wa mwana aujuae mzazi ulionekana kwa Madam Ziya, hakujali kabisa mazingira machafu ya ofisi ambayo alikumbana nayo , yeye alimsogelea kijana wake ambae bado alijikunyata huku mikono yake ikiwa imerowana damu, alimkumbatia na kunyanyua pale alipokaa huku akimtaka waondoke eneo lile kuepuka mapaparazi ambao walijaa kutafuta taarifa za undani wa tukio ambalo lilijitokeza .
******
"DEAL DONE" hayo yalikua ni maandishi mekundu makubwa yaliyoonekana kwenye ukuta mkubwa mweupe ambao ulipatikana ndani ya chumba ambacho kilikua na vijana wawili wa kiume. Maandishi hayo yalionekana kuchorwa muda mfupi uliopita maana rangi yake ilionekana kuchuruzika na kufanya michirizi.
"Nadhani mpango huu umekamilika, kinachofuata sasa ni kuendelea kuharibu imani zao kwa kuwaendesha vile ambavyo mimi nataka, nitahakikisha hakuna amani kati yao na jina la kampuni yao linakufa kama ambavyo alikufa baba yangu" maneno yenye hisia zito yalitolewa kinywani kwa sauti iliyojaa hasira huku akimgeukia mwenziwe.
Licha ya sura yake kuonyesha hasira lakini mavazi yake yalionekana wazi kabisa kuwa ni mtu aliyejiweza kiuchumi , muonekano wake kwa wakati ule ulionekana kubadilika kabisa! Naam huyu ndie Meddy 🙄 laiti mngemuona basi mngesema hakua yule Meddy wa Larah 😀 wala Meddy ambae alionekana na Wanageza akiranda ovyo mitaani ila ukweli hauwezi kujificha siku zote. Itawashangaza! ndio yeye kabisa .
SIMULIZI: LARAH (Sipaswi kulaumiwa)
MTUNZI&MWANDISHI: Talhatmoudy 🥰
FACEBOOK PAGE: Talhat moudy love stories.
WHATSAPP No: 0718927182.
SEHEMU YA 18
Licha ya sura yake kuonyesha hasira lakini mavazi yake yalionekana wazi kabisa kuwa ni mtu aliyejiweza kiuchumi , muonekano wake kwa wakati ule ulionekana kubadilika kabisa! Naam huyu ndie Meddy 🙄 laiti mngemuona basi mngesema hakua yule Meddy wa Larah 😀 wala Meddy ambae alionekana na Wanageza akiranda ovyo mitaani ila ukweli hauwezi kujificha siku zote. Itawashangaza! ndio yeye kabisa Meddy mzee wa mipango.
Baada ya kula kiapo ambacho alikua na utayari wa kukitumikia basi aliamua kusogea kwenye meza ya kioo ambayo ilisheheni pombe na vileo mbalimbali, alitoa sigara moja kwenye pakti na kuiwasha huku akianza kuvuta kwa kasi mno kiasi cha kutoa moshi mwingi, alimwita mwenziwe kwa ishara ili wajumuike pamoja , walianza kunywa na kufungua mziki mkubwa ambao uliwavutia kucheza pia. Wataachaje kufurahi ikiwa kile walichokipanga kimetimia.
"Larah....utanisamehe kwenye hili, vigezo vyako ndio vimechangia utumike kwenye mpango huu" Meddy alijisemea kwenye nafsi yake huku akiendelea kulisakata rumba.
********
Masaa matano baadae Larah alionekana bado kajikunyata mapajani kwa mamaake , hakua na shauku ya kutoka nje hata kidogo kutokana na kilichotokea. Kwa vile Niffa tayari aliondoka basi mama na bintie walibaki kuusindikiza ukimya wa huzuni uliotawala chumba chao. Uvumilivu ulimshinda mama mtu na kuanza kuzipapasa nywele nyingi za bintie huku akimwita.
"Larah....unaweza kunieleza kwa kina kinachoendea au utabaki kutiririsha machozi ? Mama Larah aliuliza ila zilipita sekunde bila kujibiwa chochote.
"Kama umefanya kitu kibaya na ukasema ukweli mbele ya mtu au watu basi ni rahisi kupata tena kibali cha umma, Ingawa hio haitawafanya wakuamini tena kama zamani..... kwa sababu tayari umevunja kuta za uaminifu walizojenga juu yako, lakini tayari utakua umeiweka nafsi yako kwenye chumba cha uhuru" Aliongeza Mama Larah maneno ambayo kiasi fulani yalimfanya binti yake ajiinue na kukaa kitako.
Larah alimtazama mama yake usoni kwa dakika zisipungua tano , aliona wazi namna ambavyo kuna kila sababu ya kumueleza, alijipa moyo kua kivyovyote mamaake asingemtupa hata angekua mchafu kiasi gani. Hakukua na haja ya kuendelea kumficha maana kila kitu kulikua wazi licha ya kwamba hakuona. Alianza kumsimulia kila kitu kumhusu Rommy na jinsi alivyotaka kumsaidia kipindi ambacho alilazwa, hakuna tukio ambalo aliacha licha ya kwamba yalimuumiza mno , hata namna alivyoutoa mwili wake kwa Meddy ili alipize kisasi pia alisema. Kiufupi ni kwamba Larah hakuacha hata nukta kwenye usimuliaji wake.
"Mmmh Larah! Mbona umefanya mambo yote hayo bila kunishirikisha? Unadhani utaupata tena uaminifu wa Meddy? Au ndio...."
"Mama....sikua na chaguo jengine zaidi ya Meddy, yeye alionyesha wazi kuchukia ukaribu wangu na Romy, na kama hiyo haitoshi nilimuona kuwa ana uwezo na yeye ni mjanja mjanja, sikujua kama hili lingetokea kabla ya mpango wetu kukamilika " alijieleza Larah.
" Ulichokosea hapo ni kuishi na roho ya kisasi binti yangu, hivi umewaza kuwa kisasi chako kitaumiza wangapi? Haya Meddy huyo tayari hupo nae? Hadhi na utu wako pia vimepotea! Unadhani ni rahisi kujirejesha kua yule Larah aliyekua akiheshimika na kuwa mfano wa kila mtu hapa Geza? Umeyaharibu maisha yako mwanangu " Mama Larah aliongea kwa sauti fulani iliyoonyesha uchungu na hasira.
"Mama....Nitafanya kila niwezalo ili nimkomeshe aliyehusika na upumbavu huu, sitadhalilika peke yangu kwenye hili kabisa" alijitapa Larah huku akijiinua.
"Usijizidishie mambo mwanangu, nguvu za kumuadhibu unazitolea wapi? Ni bora uliache lipite maana mwisho wa siku binadamu watasahau na maisha mengine yataendelea , kwani ilikuwaje huo uchafu ukasambaa mitandaoni"
"Mama, kwenye kulipa kisasi naomba uniache kabisa! sikuwahi kufikiria kutumia simu za kisasa kwa sababu ya mambo kama haya, ila mwisho wa siku ilinilazimu maana biashara itangazwayo ndio itokayo! Huyu ni Romy tu aliyefanya hivi hakuna mtu mwengine, maana ni yeye pekee aliyekua anamiliki video na picha zote " sauti ya Larah alipozungumza hayo ilidhihirisha hasira akizokua nazo.
Mazungumzo kati ya mama na mwana yaliendelea, Larah aliushikilia msimamo wake wa kumkomesha aliyemzunguka licha ya kupokea ushauri mzuri kutoka kwa mamaake. Mwisho wa siku aliamua kufuta machozi yake na kuvaa nguo za kawaida na kuanza kuandaa chakula cha mchana, kwa vile kila kitu kilikua ndani basi wala hakusumbuka kwenda nje.
********
Kikao cha mtu tatu kilifanyika kwenye ukumbi mkubwa uliopambwa na kila aina ya samani, waliokaa kwenye ukumbi huo walionekana kuzama kwenye mjadala mzito wa kuinusuru kampuni yao isiangamie . Rommy ndie ambae sura yake ilionekana kukosa raha kuliko wote ambao walikua sebuleni hapo.
"Nisikilize kijana wangu, nadhani huu sio wakati wa kulaumiwa mtu, kama ni makosa uliyafanya wewe mwenyewe kwa kumuamini mwanamke ambae katokea hukoo mitaani, kila kitu kimeharibika na wale wote ambao walikua wana matangazo yao tayari wamesitisha" Madam Ziya ambae ni mama Romy alizungumza huku na yeye akionekana wazi kuchukizwa.
"Ni kweli Mr.Romy, nadhani tunapaswa kuchukua hatua za haraka kulisafisha jina lako na taasisi yetu ambayo imepakwa matope, nitahakikisha nakua mstari wa mbele kwenye hili kwa sababu mimi ndie niliyemkaribisha Larah na kumuaminisha kila mmoja kwamba yeye ni mzuri na anaweza! Sote tulishuhudia namna ambavyo tuliingiza mapato mengi kupitia yeye...." alisisita Madam Siti akiwatazama waajiri wake watasema nini.
Majadiliano yalikuwa mengi kiasi ambacho hakukua na muafaka mzuri kati yao, Romy kwenye kikao hicho hakuonekana kuwa sawa hata kidogo , kichwani mwake yeye hakuwaza kabisa kuhusu taasisi lakini aliiwazia hadhi yake, aliinuka na kuelekea kwenye maegesho ya gari huku kila mmoja akishangazwa maana kikao kilikua hakijamaliza.
"Mmmh! Siti, huu ni muda sahihi wa kua karibu na Romy ili umteke hisia zake, ukimsafishia jina tu basi naamini utaushinda moyo wake ambao umeweka ugumu siku nyingi kwako. Wewe ndie mkwe ninaekutambua" Madam Ziya alitamba baada ya Romy kuondoka.
Kwa uso wa aibu Siti alionekana kulikubali ombi hilo, yeye mwenyewe aliitaka nafasi hiyo muda mrefu ila hakuwahi kuipata, alijiapiza kumfurahisha kwa namna yoyote ile ili aingizwe kwenye moyo wa Romy kijana tajiri na mtanashati.
Baada ya Siti kuaga, Madam Ziya alionekana akizunguka ukumbini kufikiria jambo, kwenye akili yake aliwaza namna ya kumsaidia kijana wake ili taasisi iliyojengwa muda mrefu isianguke . Hata yeye alijisemea kuwa huo ulikua ni wakati wake wa kujionyesha kuwa yeye ni mama bora ambae anaweza kumpigania mtoto wake kwenye hali ngumu .
******
Giza nene ndilo ambalo lilitawala anga la mji wa Geza, ukubwa wa wingu hilo lililotanda ulikwenda kuwaogopesha wakaazi wa eneo hilo, kwa vile tayari ilikua ni majira ya saa kumi na moja za jioni basi kila mmoja alitaka awahi kujificha nyumbani kwake kabla ya mvua nzito kunyesha, ni muda huo ndio ambao bibie Larah alijiandaa kutoka.
"Mama, usiwe na wasiwasi kabisa kuhusu mimi.Ninachokwenda kukitafuta ni heshima na imani iliyopotezwa dhidi yangu" Larah alimbusu mamaake ambae alibaki tu kumtazama kwa kiulizo.
Larah hakutaka kabisa ngonjera za mamaake, alijua kua kuendelea kumsikiliza mamaake kungeweza kubadilisha maamuzi yake. Kwake kubaki ndani ilikua ni kama kujizidishia matatizo, hakutishwa na giza lilillokua nje bali aliongozwa na moyo wake ambao ulitaka pambano . Kwake yeye lile giza alilichukulia kama ni fursa maana watu wote walikimbilia majumbani mwao. Naam ukisikia vita ya panzi neema kwa kunguru ndio hii..itaendeleaaaaaa