Sitosahau yaliyonipata kijijini Kwamsisi

SEHEMU YA 12

Nilikurupuka na kuingia ndani kuitafuta ile barua, niliikuta chumbani kwangu mezani. Hii barua niliiokota jana hapa chini ya mlango na kuingia nayo ndani kwangu ingawa sikuisoma. Haikuwa na clue yoyote zaidi ya kuandikwa tu jina langu juu ya bahasha, nilianza kuichana bahasha nikitaka kuifungua ile barua, yule kijana aliniwahi akaibetua kisha akaikunja kwa haraka na kunitazama kwa macho makali kama ya mwewe.

"Mwalimu, hii hukupaswa kuifungua na kuisoma ni mtego umetegewa!" aliniambia.

"Umejuaje kama ni mtego?" nilimhoji.

"Nilijua kwa sababu ni azimio la kikao cha wachawi, hawajui kama ninashirikiana na wewe ila nilikwambia uifungue ili nione kama umesha iva kiulinzi binafsi, yaani kutambua hatari inayo kukabili na kuiepuka. Unaonekana bado haujakomaa kiutambuzi wa hatari." yule kijana alitaka kujua kama yale madawa niliyopewa kule katika mji wa ajabu yameanza kunisaidia.

Nilijitazama mwilini na kujiona nimekuwa mtu wa tofauti, ni kama nilikuwa na nguvu fulani lakini sikuweza kuziruhusu nguvu hizo ziweze kufanya kazi katika mwili wangu. Nilimuaga yule kijana naye akaondoka.

Usiku huu nikiwa nimelala kwenye chumba changu nilihisi nikifanya mapenzi na mwanamke mrembo, tulikuwa tumekumbatiana huku tukipeana mahaba mtomoto pale kitandani. Sikuelewa ilikuwaje nilishtuka usingizini na kutazama nikiwa nimejichafua mwilini nilimwona yule mwanamke akipotelea mlangoni. Nilishtuka!

Mwanzo niliihisi harufu nzuri ya marashi pamoja na upepo mwanana ukinipuliza. Nilikuwa nimemkumbatia msichana mrembo ambaye sikumjua kwa jina, alikuwa ni mweupe kama theluji na mwenye nywele ndefu alikaa juu yangu huku mimi nikiwa chini tukipeana mahaba motomoto. Nilizidiwa na mahaba nikashindwa kuongea kitu nilibaki nikigugumia tu, nilimtazama sura yake iliyokuwa iking'aa sana na macho yake yaliyowaka kama kijinga cha moto. Akapanua kinywa chake, nilishtuka nilipoona yale meno mawili yaliyokuwa marefu mithili ya yale ya mnyama dubu.

"Soka nakupenda, mimi naitwa Maimuna nadhani unanikumbuka ila nahitaji kufanya agano na wewe endapo ukinikubali."

"Agano gani?!" nilihoji huku nikishangaa kwakuwa tayari amesha nishurutisha na sasa ninashiriki naye ngono bila ridhaa yangu, wala yeye hakunijibu alizidi kunikumbatia kimahaba!

Nilishtuka usingizini nikamwona yule kiumbe akitokomea mlangoni na kupotea. Nilijipapasa kwenye sehemu zangu za siri, ni kweli nilikuwa nimejilowesha! Kumbe nilifanya mapenzi na yule jini sikuamini niliogopa sana. Kuanzia siku hiyo niliingia rasmi kwenye mahusiano na yule jini Maimuna, nilimsahau kabisa Sitti na nilimchukia sana, hata nilipokutana naye kazini ni mara chache nilikuwa nikimsalimia ilikuwa tukikutana tunapishana kama vile hatujaonana, kila mtu akiendelea na hamsini zake.

****

Siku hii usiku wa manane, tulikuwa tumejipanga kwenye mstari mrefu sana vilisikika vingoma vya asili watu wote tulikuwa tupo nusu uchi. Tulitembea taratibu kueleke kwenye msitu mnene nikiwa na yule mwanafunzi mchawi aliyeitwa Kondo. Kwa mbele alitangulia bibi kizee kisha tukafuata sisi na vijana wengine wawili. Kwa nyuma yetu walikuwepo watu walioonekana kuchoka na kukata tamaa ya maisha wanaume kwa wananwake. Wanaume wote walikuwa vifua wazi huku wametwishwa mizigo mizito ya mafurushi kichwani mwao, hao walikuwa wamedhoofu na kukondeana mno.

Wanawake walikuwa wamevaa kaniki viunoni mwao na waliacha vifua vyao wazi, matiti yao yaliyotepeta yalikuwa yamelala vifuani mwao, pia wao walibebeshwa mizigo mizito vichwani mwao walikuwa wamechoka na waliongea maneno yasiyo eleweka huku macho yao yakibubujisha machozi. Nilikuja kugundua kuwa kumbe walikuwa wamekatwa ndimi zao na ndio maana walishindwa kuongea kwa lugha iliyo eleweka, walikuwa ni misukule. Bada ya hawa watu kwa nyuma walifuatia wazee waliokuwa ni wakongwe kwenye kazi hii ya kuwanga usiku.

Tulitembea kwenye msitu mnene tukaingia kwenye eneo lililokuwa na miti mikubwa sana hapo yule kiongozi wetu akasimama, alikuwa ni bibi kizee na alishikilia mwenge mkononi mwake uliokuwa ukiwaka na kuangaza kwa sehemu kubwa ya eneo hilo. Aliuzunguka mti mmoja mnene na mrefu sana wenye kamba kamba na matawi manene yaliyofunika kivuli kwa eneo kubwa. Mti ule ulisemekana kuwa na umri wa zaidi ya miaka elfu moja, ni mti uliokuwa na maajabu ya kipekee sana.

Baada ya kufika hapo yule kikongwe aliuzunguka ule mti, na sisi wote tukauzunguka ule mti na kutengeneza duara kubwa, tulisimama na kukaa kimya kwa dakika kadhaa. Ndipo yule kiongozi aliyekuwa ni bibi kizee sana, alikuwa ni wana-Kingalu mjane wa mzee Kingalu, alisimama mbele yetu karibia na shina la ule mti kisha akakaa chini taratibu, na sisi sote tukakaa chini kwenye majani, alitoa sauti yake na kupiga ukelele mkali sana kama wa kilio cha kuomba msaada mara tukasikia mitetemo.

Tulisikia upepo ukivuma na matawi ya mti ule yalipishana na kutoa ukelele, ni ishara kwamba tumepokelewa kwenye himaya ile. Niliitwa na yule bibi kwa ishara nikasogea mbele na ile hirizi alikuwa ameiweka kwenye chungu cheusi kilichokuwa na maji meusi sana kwani nakumbuka nilimkabidhi ile hirizi ya Simba siku kadhaa zilizopita. Aliongea maneno kwa lugha ya Kizigua.

"Enyi mizimu ya ukoo wa mzee Kingalu na mizimu yote ya wazee wa zamani tunamkabidhi huyu kijana mikononi mwenu mumpe ulinzi kwa kuwa anakwenda kuirithi ile hirizi iliyokuwa chini ya milki ya mzee Kingalu. Nimemchagua yeye kwakuwa ndiye aliyeonekana kufaa kati ya wengi na hivyo leo atatawazwa rasmi kuwa mrithi wa hirizi hii ya Simba."

Alichukua kile chungu na kisha nikiwa nimepiga magoti nilipanua kinywa changu wazi, ile hirizi ilikuwa imechanganywa kwenye kile chungu pamoja na zile dawa nyingine nililishwa kwa njia ya kumiminiwa mdomoni huku watu wengine wakishangilia kwa kupiga ngoma na makelele. Wale misukule walikuwa wamekaa kimya tu kana kwamba hawaelewi chochote kinacho endelea. Nilikuja kuelewa baadaye kwamba wale misukule hutumika kama wabebaji wa mizigo ama wafanyaji kazi ngumu katika misafara yote ya wachawi.

Nilisimama nikiwa ninaunguruma kama Simba nilijitupa huku na huko kwa sababu nilijisikia vibaya na mawenge mawenge, nilitamani hata kujiua kwa jinsi nilivyojisikia walinishika huku na huku huku wakiniongelea maneno yao ya kilugha.

"Ewe kiumbe uliyemuingia huyu kijana, sema unataka nini tukupe walakini usimtoke huyu haya ndio makazi yako mapya tuliyokupa tunaomba ukae humu na utastarehe kwa raha utakazo zipata."

Nilitoa sauti ya kukoroma haikuwa sauti yangu, "Sawa nimekubali ila kwa kafara ya damu kinyume na hapo nitamuuwa huyu kijana."

Walichukua mbuzi dume wakamchinja na kumwaga damu kila sehemu. Mbuzi ni alama ya shetani na mimi nilikuwa nimemvaa shetani kwahiyo nilitulia lakini kumbe niliingia kwenye ndoto, kwenye lile shimo alitokea kiumbe wa ajabu alikuwa ni kiumbe aliyekuwa na kichwa cha beberu na pembe mbili ndefu, niligwaya!

"Wewe ni nani?" nilimhoji, hakunijibu alizidi kunisogelea. Alikuwa na mikono ya binadamu na miguu mirefu yenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili, mwili wake wote ulijaa manyoya.

ITAENDELEA...
 
Hatari sana
 
Hahaaa, hata mi sikuwa najua kama inaendelea.
 
Kuna watu ni wabishi sana,Kuna mwanafamilia kwetu ni mchngaji lakini ana mganga wake anaemtibu na kumuweka sawa,ananambiaga dada hakuna watu tunarogwa kama wachungaji,kwaio msibishe sana jamani,ushirikina upo,na sio kila anaemtaja Mungu kasimama na imani,wengine kanisanin na misikitini ni sehemu ya kutafuta ridhki tu kama wewe inavyoamka kwenda kibaruani
 
Anayeroga ni huyo huyo....asiwachafue wengine
 
....
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…