SEHEMU YA 8
Niliamka asubuhi kisha nikachukua mfuko wa nailoni nikaizungusha ile hirizi na kuchimba pale chumbani kwangu na kuifukia. Sakafu ya nyumba yangu ilikuwa ni ya udongo na hivyo ilikuwa rahisi kuchimba kule ndani. Nikakumbuka kwamba nilipewa masaa 48 na hapo tayari nilisha tumia masaa 12 ili niikabidhi ile hirizi kwenye himaya ya Mzee Samasimba kupitia kwa kijana wake Mbwana aliyemteka Sitti kichawi. Siku hii ya jumamosi ilikuwa siku ya tofauti kidogo kwani ilianza na kawingu kamvua za rasharasha na na baadaye jua likawaka, ni siku moja tangu tumzike Mzee Kingalu.
Niliingia bafuni kuoga, nilipotoka hata kabla ya kuingia chumbani nilikutana uso kwa uso na Mganga mkuu. "Kijana jiandae tuondoke!" Nilimtazama usoni hakuwa na maneno mengi na mimi sikuwaza sana niliingia ndani na kuvaa kisha nikatoka nje nilichukua baiskeli yangu kwani naye alikuwa na yakwake. Tukatoka kwenda mpaka Mkata mjini kununua vingira (vifaa vya kiganga) kwa ajili ya shughuli kubwa kwa siku hiyo. Kumrudisha mtu aliyepotea na kumrudisha mtu aliyechukuliwa Msukule.
Tulifika Mkata majira ya saa 6 mchana tukanunua vifaa vinavyo hitajika akiwemo mbuzi dume (beberu), kuku jike mwekundu (koo) pamoja na dawa nyingine za asili hatukutaka kupoteza muda, tulirudi na moja kwa moja tukaingia kilingeni. Tiba ya kwanza ilikuwa ni ya kunitengenneza mimi kimwili, mganga alinifanyia dawa za kunifanya nisionekane katika ulimwengu wa roho yaani nisiweze kabisa kuingia kwenye rada za wachawi wowote wale. "Mwanangu umeshaingia vitani huna budi kujivika mavazi ya chuma," alisema yule Mganga.
Alinichanja chale kwenye viwiko vya mikono, kifuani na miguuni kisha kunipaka dawa iliyokuwa kwenye ile tunguli yake ni dawa iliyotokana na mchanganyiko wa miti zaidi ya saba na viambatanishi vingine vilivyochomwa kwa pamoja na kunuiziwa kisha kuchanganywa na mafuta ya mnyonyo na asali na kuwekwa kwenye tunguli hiyo. Baada ya kazi hiyo aliniambia imebaki kazi moja nayo ni tambiko litakalo fanyika huko porini kwenye mti mkubwa sana nikamuitikia kwani kwa wakati huo tulikuwa na kazi kubwa sana ya kuwaokoa ndugu zetu hao kwahiyo zoezi hili la kunitengeneza tukalisitisha kwa muda.
Tukaingia kwenye kazi rasmi ya kumtafuta mtu aliyepotea/ aliyeibwa kichawi. Utambue kuwa mtu aliyepotea ki mazingira ni tofauti kabisa na mtu aliyechukuliwa msukule hivyo namna ya dawa zake pia huwa ni tofauti. Mganga aliweka maji kwenye chungu na kuyanuizia kisha kuchanganya na dawa kadhaa ikiwemo mzizi wa kata njia, makombe ya hirizi pamoja na mavumba mengine akafunika kwa kutumia kinu. Baada ya muda alipofunua niliweza kuiona sura ya Sitti kwenye kile chungu cha maji, alionekana mwenye huzuni nyingi na kukata tamaa. "Huyu atakuwa amefungiwa huko kwenye eneo la mbali wamemtelekeza kwenye kisima kirefu cha zamani kwahiyo inapaswa kuokolewa," alisema yule mganga baada ya kuangalia kwenye ramli yake.
Nilimueleza Mganga kuhusu kile kitu nilichokipata kutoka kwenye mwili wa marehemu naye akaniambia kwa sasa nikihifadhi kwanza kama nilivyo fanya baadaye kitakuwa na kazi kubwa. "Umefanya jambo jema mwanangu hawa watu haitakiwi uwakubalie kwa kila kitu watakacho kuambia ni lazima ujue namna ya kupambana nao bila hivyo watakuburuza. Baada ya kugundua kwamba Sitti hakufichwa mbali na eneo la kijiji, ilibidi ifanyike dawa maalum ya kuwafunga wasimpeleke mbali zaidi tulikwenda kwenye njia panda usiku wa saa 2 hivi.
Ilikuwa ni jambo gumu kwangu mimi kama mwalimu na heshima zangu kuonekana nikifanya mambo ya kishirikina hadharani, ingawa hakuna aliye nishangaa kwani wanakijiji wa Kwamsisi uchawi kwao ni kama mila, na tiba za asilia hufanywa hadharani bila kificho chochote kwa hiyo ndani ya muda mfupi niliokuwa pale niliweza kuzoea mazingira na maisha ya pale na hivyo kuto kuogopa kufanya shughuli za kiganga hadharani.
Hivyo tukapasua nazi kumi na mbili kwa ajili ya kuvunja mipango yao kisha yule kuku alimchinja na kumuachia achague njia tunayoweza kuifuata. Baada ya yule kuku kuchinjwa alirukaruka na kuangukia kwenye njia ya upande wa mashariki, mganga akiwa ameshikilia vifaa vyake ikiwemo tunguli mbili moja ameivaa shingoni na nyingine ameishikilia mkononi pamoja na mwengo na pembe ndogo alisimama kwenye ile njia kwa dakika kadhaa huku akinuizia maneno akapiga ukelele wa hali ya juu sana na kuita "Sitii njoo, njoo!" kisha akapuliza ile tunguli yake. Kumbe tulifanya makosa kwani kwa kufanya hivyo tungewaamsha wachawi wakajua kumbe tunawafuatilia, walijiandaa vyema kutukabili ila tuliwazidi ujanja.
"Enyi Subiani, enyi Makata, enyi Maimuna njooni sasa mnisaidie kumtafuta kilembwe changu!" Nawaita muje sasa hivi mganga aliwaamrisha majini yake yamuingie basi baada ya muda akapandisha mashetani yake maramoja akaondoka huku akiwa anakimbia nilimfuata nyuma huku nimebeba ule mkoba wenye zana za kazi tulitembea mpaka mashambani, tukaingia kwenye msitu mnene kidogo ndipo tukaisikia sauti ya vilio na maombolezo tulikaa kutazama Sitti alikuwa amewekwa kwenye kisima kirefu jambo la ajabu hawakumuwekea ulinzi wowote, labda walijua kwamba itakuwa ngumu kwa sisi kufika huko.
Nilimulika na tochi kutazama kisimani, kilikuwa kirefu sana na hatukuwa na ngazi yoyote ilibidi nimtupie kamba tuliyokwenda nayo na bila kutarajia Sitti aliweza kuipanda ile kamba na tukaweza kumtoa alilia na kunikumbatia kwa furaha. Mganga alituamuru kuondoka eneo hilo kwani wale wachawi lazima wataanza kutufuatilia kuna taarifa ambayo wamesha ipata. Tulitoka tukapita njia ya tofauti. Tulivyokuwa njiani tukawaona wanakuja kwa kasi huku wakiwa na mienge mikononi mwao tulijificha pembeni ya mbuyu wakapita kuelekea eneo walikokuwa wamemficha Sitti baadaye tukatoka tukikimbia kuelekea nyumbani kwa Mganga.
ITAENDELEA