Hali ya mambo imezidi chukua sura mpya barani Afrika, ikiwa ni miaka kadhaa tokea ilipohamishia makao yake makuu katika mji wa Laayoune huko Sahara Magharibi ili kuakisi dhima ya Umoja wa afrika ya mapambano dhidi ya Uonevu, kutokea mji wa Adis Ababa nchini Ethiopia.
Hatua hii ya kuhamishiwa makao yake makuu mjini humo ilifuatia vita na ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu uliofanywa na serikali ya Ethiopia dhidi ya Watigray, na hivyo kunajisi uamuzi wa Afrika kuweka makao yake mjini humo.
Huko katika jiji la Mbabane, kitovu cha demokrasia barani afrika baada ya kuanguka kwa utawala wa kifalme wa karne nyingi wa Mswati, ambaye kwa sasa yadaiwa yuko uhamishoni nchini Afrika Kusini, kimemalizika kikao cha ghafla kilichowakutanisha wakuu wa nchi na serikali za Afrika Huru. Kikao hicho kilichoketi katika jengo jipya la Bunge la nchi hiyo, lilojengwa kwa michango ya wanachama wa vyama vyote vya siasa vya nchi hiyo, na kuliita jumba la Demokrasia, kilikuwa na agenda moja tu; MGOGORO KATI YA UKRAINE NA RUSSIA.
Kikao hicho ambacho kiliongozwa chini ya Uenyekiti wake Bi Aminata Mousa Rais wa Mali ambaye alichaguliwa kwa ushindi wa kishindo kufuatia miaka mingi ya utawala wa kijeshi; kilikuwa kikisubiriwa kwa shauku sehemu zote duniani, kwani kingetoa uelekeo mpya juu ya mgogoro huo. Wachambuzi wa siasa za kimataiafa wanasema kuwa, kutokana na nafasi yake kwenye biashara, rasilimali, ukubwa wa eneo lake, na mahali ilipo, bara la Afrika lina kauli yenye nguvu juu ya mgogoro huo na siasa za kimataiafa kwa ujumla.
Mfano, yadaiwa mwezi uliopita Rais wa Marekani, Bwana Alexander Ford, akiwa katikati ya mkutano wa Wakuu wa nchi za Amerika alisitisha hotuba yake muhimu juu ya sera za Marekani katika mkataba wa NAFTA na kusafiri ghafla kwenda nchini Zaire kuonana na Rais Bizimungu Kayizirege kufuatia hatua ya nchi hiyo kutishia kufuta leseni ya uchimbaji wa madini aina ya Cobalt kwa kampuni ya Texas Mineral Corporations, kutokana na mgodi huo kutiririsha maji yenye sumu na kuathiri wanazaire na mifugo inayozunguka mgodi huo. Madini haya ni muhimu kwa nchi ya Marekani kwani ndio hutumika kutengeneza Simu za kisasa duniani, huku Marekani ikiwa ni mmoja wa wanufaika wake wakubwa. Kwa mujibu wa jarida la Economic Times, Hatua hiyo yaelezwa ingeweza athiri karibu asilimia 10 ya pato la ndani la Marekani, na kutengeneza mgogoro mkubwa wa ajira na hivyo kutishia kukiondoa madarakani chama cha Reps, kinachokabiliwa na Upinzani mkubwa kutoka chama cha Dems.
Msemaji wa Secretariat ya Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Huru, Bi Ummul Kheir, amewaeleza wanahabari kuwa Kikao hicho kimefikia maadhimio yafuatayo.
1. Kimezipa Onyo nchi za Urusi na Ukraine kuwa zisijaribu kamwe kurusha hata kisu, kwani maisha ya wanadamu popote pale duniani, ni jukumu la Umoja wa Afrika Huru kuyalinda.
2. Imeitaka nchi ya Marekani kuacha Mara moja kuziuzia silaha nchi ya Ukraine.
3. Imeziwekea vikwazo Kampuni na wakurugenzi wake wakuu wa Kampuni za Silaha za Lockheed Martin na Raytheon vya kuuza silaha zake barani Afrika. Katika azimio hili, UAH umesema nchi yoyote ya afrika itakayo bainika kukiuka basi itatengwa na Umoja huo. Hatua hii ni kali zaidi, kwani nchi inayotengwa, hushindwa kabisa kufanya biashara kwani njia za kimataiafa zinazoingia nchini humo hufungwa. Hatua hii iliwahi itokea Rwanda pale ilipokiuka azimio la Umoja wa Afrika Huru, la kuitaka kuacha kufadhili waasi huko Zaire na kutokutii. Mizigo yote ya Rwanda ilikwama bandari za Dar Es Salaam, Nairobi, Beira, Durban, na kupelekea hali ngumu ya maisha na hatimaye maandamano yaliyomng'oa madarakani Rais Petro Kangema aliyetawala kwa miaka takribani 20.
4. Imeitaka Mara moja jumuiya ya NATO kuvunjwa kwani ilikwisha majukumu yake mwaka 1991 pale Usoviet ilipokufa. Ikitoa ufafanuzi juu ya jambo hili, UAH umesema kuwa kitendo cha NATO kuendelea kujitanua ndio chanzo cha mgogoro huu. Imeonya kuwa nchi yoyote ya Ulaya itayopuuzia azimio hili, basi kampuni zake zinazofaya biashara na Afrika Huru pamoja na Balozi za nchi hizo, zijiandae kufungasha virago.
Umoja huo umesema unafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea huko Ukraine na ikiliarifua jeshi la utayari la Afrika huru (Africa Standby Force) na Vikosi vya uokoaji kuwa tayari kutoa huduma itakapohitajika.
Gazeti letu lilifanya mazungumzo na mchambuzi wa siasa za kimataiafa bwana Henry Konrad, na kwanza kumuuliza ameyapokea vipi maazimio hayo ya UAH.
Konrad: Kwanza sijashangazwa, kwa miaka kadhaa sasa, bara la afrika limechukua nafasi ya uongozi kwenye siasa za dunia, na imedhihirisha kuwa inaweza kusimamia misingi yake ya kiutu. Na kwa kweli imetumia kile ambacho mataifa yote makubwa duniani yamekuwa yakikitumia, KETE YA KIBIASHARA NA JIOGRAFIA.
Gazeti letu: Je unadhani azimio la kuifuta NATO linawezekana?
Konrad: Kwanza ni kweli NATO haikupaswa kuendelea kuwepo kwa sababu ilianzishwa ili kuidhibiti Soviet [USSR], ambayo haipo tena kwa takribani miaka 20. Pili, Marekani na Ulaya hawana budi kuisikiliza UAH imetaka nini, kwanini biashara zake, rasilimali zake inategemea kwa zaidi ya barani Afrika, na ujio wa mataifa makubwa kibiashara kama China, Uturuki, Brazil inaifanya EU na US wawe na Uoga kwenye kupingana na Afrika.
Gazeti letu: Unadhani hiki kilichofanywa na UAH kina maana gani kwa siasa za dunia.
Konrad: Kwa miaka mingi afrika ilikuwa imejisahau, sasa hivi imejitambua na kujua nafasi yake duniani. Afrika ina 16% ya watu duniani, huku ikiwa na idadi kubwa zaidi ya Vijana, 30% ya madini, 12% ya mafuta, 8% ya gesi asili iko barani Afrika, Afrika inazungukwa na bahari mbili— na Atlantic [inayounganisha Marekani, Brazil na Afrika], na India [inayoungaisha Afrika na Asia i.e China, Korea, Japan, India] kibiashara. Hivyo ni bara lenye kushikiria kete muhimu kwenye siasa za duniani. Ni dhahiri kuwa, Africa ni mdau muhimu, na sina shaka sasa inapswa kuwa na kiti kwenye Baraza la Kudumu la Usalama la Umoja wa Mataifa, na Mashirika baadhi ya umoja wa mataifa yawe na makao yake barani Afrika.