Trump anapowashinikiza wamalize vita kwa amani, jamaa wanamwona kama mpuuzi vile.
Bila shaka ile hoja kwamba Trump anachukiwa kwa vile ni mkweli sana, inazidi kuonekana wazi.
Wakati wote amejitahidi kuangalia mbele na kufanya hesabu za mapato na hasara, kisha kufanya hitimisho sahihi.
Washirika wake wa NATO na Ukreni wao kwa vile vita vimeshawaabisha tayari, wako radhi kupitia njia yoyote bila kujali matokeo - alimradi tu wasikubali kwamba wameshashindwa.
Mfano, mtu kama Zelenskyy angeulizwa nini hasa angependa Marekani ifanye kwa sasa dhidi ya Russia, bila shaka atadai Trump azichange na Putin hata kwa kumrushia mabomu ya nyuklia Mosko.
Jamaa hajali kesho yake kwa sasa. Na huo ndio mtazamo wa viongozi wengi wa NATO. Wana hasira, hawana busara; lakini bahati nzuri kabisa hawana uwezo wa kutimiza nia yao ovu.
Marekani ya Trump imeona na kushawishiwa na mambo kadhaa makuu yenye mvuto kwa Putin.
Moja ni ukweli kwamba vita hivi chanzo chake hasa ni Ukreni yeye mwenyewe kwa kuchochewa na viongozi vipofu wa NATO kwa hisani ya utawala wa Marekani katika serikali iliyopita.
Inashangaza kwamba Zelenskyy hivi sasa yuko tayari kufanya maridhiano ya amani, Urusi ikiwa imeshamega 25% ya ardhi yake bora, wakati ambapo angeweza kufanya hivyo kabla ya vita na kuepusha mabalaa haya yote.
Kwa hiyo Ukreni alijitakia majanga kwa kuwasikiliza watawala walafi na wasioona mbali kama akina Boris Johnson.
Leo hii yeye ameigeuka Ukreni aliyoahidi kuipigania hadi mwisho; amejificha salama kwenye upenu fulani wakati nchi hiyo ikisota na kumwaga damu za raia wasiokuwa na hatia.
Jambo la pili ambalo utawala wa Trump umegundua kwa Putin ni kwamba ni mstaarabu na yuko na nia njema - tena kwa pande zote mbili.
Ukweli ni kwamba pamoja na uwezo wa Urusi, yenyewe haijioni kama mbadala wa Marekani bali sehemu ya tawala kubwa duniani.
Inaonekana wazi kwamba wakati ambapo Urusi iko tayari kuishi pamoja na mataifa mengine, wakiwemo mahasimu wa NATO, kwa upande mwingine NATO hasa ingependa kuiona Urusi ikifutika kwenye ramani ya dunia.
Aidha mtazamo chanya wa Putin umethibitika mara nyingi kwa namna anavyoshughulika na Ukreni kwanza kama ndugu na jirani yake, lakini pia kama taifa lenye haki na fursa ya kustawi kwa amani na furaha.
Ukizingatia vikwazo kibao na chokochoko nyingi ambazo Russia imefanyiwa, siyo tu na Ukreni na NATO, bali na Marekani yenyewe, huku Russia ikiwa mstari wa mbele daima kusisitiza maafikiano na kujenga uhusiano mzuri kwa pande zote mbili kwa faida ya vizazi vijavyo, basi kila mwenye jicho lisilo na hasidi hugundua kwamba Putin ameendesha operesheni yake kistaarabu sana.
Hata Marekani yenyewe haiwezi na wala haina uvumilivu kama huo.
Unaweza kukubaliana nami hapa kwa kutazama tu namna Marekani inavyowabagaza na kuwaaibisha viongozi wakuu na muhimu wa Ulaya (washirika wake wa karibu sana) - tena mbele ya kadamnasi la umma wa dunia!
Kwa hiyo, si ajabu Trump amevutiwa sana na msimamo huo na utashi wa Urusi ambao kimsingi ni wenye maslahi kwa wote.
Jambo lingine la tatu ambalo Trump anahusudu kwa Putin na hivyo kuchochea nia yake ya kumwelewa sana jamaa ni kauli yake mwenyewe ya America First.
Kama ambavyo Trump yupo kwa maslahi ya Marekani, basi Putin naye yupo kwa maslahi ya Urusi.
Na chochote kinachojaribu kuingilia ukweli huo, kila mmoja wao hukihesabu kama adui hatari na asiyevumilika dhidi ya ustawi wa taifa lake.
Kama ambavyo Marekani haipendi kumwona adui hatari mlangoni kwake, vilevile Russia haiwezi kuuvumilia upuuzi kama huo.
Kiongozi au mtu yeyote anayejidai kutoona uhalisia huo wa mambo, basi lazima ama ni mpumbavu kupindukia au amejivika unafiki uliokithiri.
Kama nilivyoelezea hapo juu, Trump ni mkweli kwa asimilia nyingi na ndiyo maana ni rahisi kuona kile ambacho swahiba wake Putin anapitia.
Unaweza kusema hawa jamaa ni marafiki, lakini ni kwamba tu mitazamo imefanana na falsafa zao kuhusu nchi zao ziko sambamba.
Jambo la nne ni uthabiti wa Urusi katikati ya mitikasi yote ya kujaribu kudhibitiwa na kuangushwa na washirika hasimu wa NATO.
Marekani ya Trump bila shaka imefanya hesabu zake vizuri na kugundua adui usiyeweza kumshinda, basi jiunge naye - na hilo ni wazo lenye mantiki na akili.
Miaka minne iliyopita tangu vita Ukreni vizuke 2022, ilitosha kabisa kuisambaratisha Urusi na kuifanya iwe dhaifu hohehahe mithili ya Ujerumani wakati wa vita vya dunia.
Mikakati na vikwazo vilivyokusudiwa kufanikisha hilo, kwa masikitiko ama furaha vimewarudia wao wenyewe na kuvuruga uchumi wa nchi zao, huku vikiwang'oa viongozi wengi na hata kutishia machafuko na mapinduzi ndani yao.
Hii ndiyo sababu mojawapo ya Marekani ya Trump kupiga yu-tan, na, pamoja na NATO, kukamia mno madini adimu ya Ukreni katika jitihada za kufidia hasara kiuchumi iliyopata kwenye vita hivi ili kujiliwaza kufuatia kuipoteza Ukreni.
Hizo ni harakati za mwisho za mfa-maji katika kujaribu kuinua hali ya maisha yaliyodorora nchini mwao.
Kituko na jambo baya zaidi, taifa la Ukreni lililoathirika na vita ndilo linashinikizwa kwa ushawishi na vitisho kama sehemu ya kuwaletea suluhisho kiuchumi!
Tunaweza kusema Marekani anaitumia Ukreni kama kifuta jasho chake; anaitumia Ukreni kama kiinua mgongo wa uchumi wake yenyewe!
Katika mazingira haya, huku Urusi uchumi ukizidi kupanda, kwa nini Marekani asijilegeze na kujilengesha tena kwa Putin? Tajiri hanuniwi, ama vipi?
Sababu ya tano kwa nini Trump anaonekana kuegemea upande wa Urusi ni kwamba kwa sehemu kubwa Urusi ni kinara wa ushawishi kwenye uwanja wa teknolojia, masuala ya usalama, biashara na hata ushawishi kijamii.
Nani asiyependa kujisogeza karibu na gwiji la namna hiyo - hata kama huko nyuma mahusiano baina yao hayakuwa na afya?
Ni wazi Marekani ya Trump imekabiliwa na ukweli mchungu wa hali ya kutoepukika kwa Urusi katika nyanja tegemevu za siasa, diplomasia na uchumi wa dunia - vyote hivi vikichagizwa na uwezo wake wa kudumisha amani na usalama madhubuti.
Hii ndiyo kusemaje? Trump anapomshinikiza Zelenskyy amalize vita mara moja, ni kwa vile tayari ana data halisi za kutosha kuhusu Urusi na jinsi ilivyojidhatiti na kujizatiti kulinda maslahi yake kwa gharama yoyote.
Wanaodhani Trump kwa kufanya hivyo anadhihirisha kuwa ni dhaifu na mjinga au wale wanaoeneza propaganda duni kwamba ni kibaraka wa Urusi, bila chembe ya shaka hao wanabwabwaja mambo yaliyo juu ya upeo wao.
Putin ameilazimisha Marekani kumeza dawa yake yenyewe; ni furaha ilioje kwa dunia kuona dawa hiyo ikifanya kazi mujarabu kupitia utawala mpya wa Donald Trump!