Wataalamu wa kijeshi wanakubali kwamba zaidi ya makosa ya kimkakati ambayo majeshi ya Kirusi yamefanya, jambo la msingi ambalo limewawezesha waukreni kudumisha udhibiti wa anga yao ni utekelezaji wa mbinu ya ubunifu, ambayo inakabiliana na mapungufu na mazingira.
Kwa kuwa na kikosi kidogo cha anga, wamejikita kwenye mashambulizi ya kasi na sio kupelekwa kwa wingi, ambayo imewasaidia kuelekeza rasilimali zao.
"Ingawa ni ndogo zaidi, jeshi la Ukraine ni la kitaaluma na lina silaha nzuri sana. Pia wamepata mafunzo kutoka kwa vikosi vya NATO, ikiwa ni pamoja na Kanada na Marekani," Dorn anabainisha.
Mchambuzi huyo wa masuala ya kijeshi anabainisha kuwa, jambo lingine la msingi ni kwamba, kabla ya mzozo huo kuanza, nchi washirika zilianza kutuma misaada ya kijeshi kwa Ukraine, yakiwemo makombora ya kutoka ardhini hadi angani, ambayo yamesaidia kuizuia Urusi kufikia ukuu wa anga.
Mwanzo wa uvamizi wa Ukraine pia ulisababisha nchi nyingi za Magharibi kutuma msaada wa kijeshi kwa Kyiv, pamoja na mataifa ambayo yamedumisha msimamo wa kutoegemea upande wowote kwa miaka mingi, kama vile Ujerumani.
Uchambuzi wa kijeshi unaonyesha kuwa Waukraine wametumia kimkakati ndege zisizo na rubani za TB-2 za Uturuki na ndege zisizo na rubani za Raven, ambazo hazijatumika tu kwa mashambulio dhidi ya meli za adui, lakini pia kwa vikosi vya ardhini.
Jumatano iliyopita, Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza kuwa nchi yake itatenga dola milioni 800 za msaada wa kijeshi kwa Ukraine, zikiwemo silaha kama vile ndege zisizo na rubani ambazo zinaweza kugeuka kuwa mabomu ya kuruka na silaha za kupambana na ndege zinazoweza kudungua helikopta kutoka angani.
Hata hivyo, udhibiti wa anga pia umekuwa hatua ya mvutano kati ya Ukraine na Magharibi.
Tangu uvamizi huo uanze, hitaji la mara kwa mara la Rais wa Ukraine, Volodimir Zelensky, kwa washirika wake wa Magharibi limekuwa uanzishwaji wa amri ya kufungwa kwa anga juu ya nchi yake, ambayo ingemaanisha kwamba NATO italazimika kuangusha ndege za Urusi zinazovuka anga yao.