BigTall
JF-Expert Member
- Mar 9, 2022
- 706
- 1,716
Wasira amesema chama hicho hakikatai kukosolewa, lakini kinachohitaji ni ukosoaji wenye hoja unaolenga kuonesha mapungufu ili yafanyiwe kazi, badala ya kutumia mitandao ya kijamii kutoa matusi dhidi ya viongozi.
Akizungumzia kauli za mwanasiasa Godbless Lema, Wasira amesema amekubaliana na hoja aliyoitoa kuhusu baadhi ya wanaharakati walioko nje ya nchi, akieleza kuwa Januari 25, 2025, wanaharakati hao walishiriki katika uchaguzi wa CHADEMA kwa lengo la kumuondoa Freeman Mbowe na kumuweka Tundu Lissu.
Wasira amesema kwa mujibu wa maelezo ya Lema, baada ya kufanikisha mabadiliko hayo, baadhi ya wanaharakati hao walianza kujiingiza katika uendeshaji wa chama hicho kwa kutoa maelekezo na amri kwa viongozi wake.
“Tunataka wanaharakati wa hoja, si wanaharakati wa kutukana. Wanatusaidia pale wanapotuambia mmefanya makosa haya na haya, sisi hatukatai kukosolewa,” amesema Wasira.
Aidha, Wasira amesema hata kama mtu ni mpinzani au adui wa kisiasa, anapozungumza jambo la kweli anapaswa kusikilizwa, akieleza kuwa hoja za Lema kuhusu uhusiano wa wanaharakati hao na CHADEMA zinapaswa kuzingatiwa.
Kuhusu msimamo wa CCM kwa CHADEMA, Wasira amesema chama chake hakina ugomvi na chama hicho cha upinzani, lakini kinataka kifanye siasa kwa kuzingatia sheria na misingi ya ustaarabu.
Soma Pia; Wasira: Serikali yetu ni halali kwa sababu imechaguliwa na wananchi
Ameongeza kuwa miongoni mwa masharti yaliyoelezwa katika mjadala wa mazungumzo ni suala la Tundu Lissu, ambalo amesema liko mahakamani, hivyo Serikali haiwezi kuingilia mwenendo wa mahakama, pamoja na pendekezo la kuhusisha mpatanishi kutoka nje ya nchi.