USIFE KWANZA MPENZI WANGU.....EPISODE.28.
Baada ya kufanikiwa kusoma na kumaliza masomo yake ya Stashahada ya Uhasibu na Biashara, Deo anasaidiwa na mpenzi wake, Levina kutafuta kazi. Harakati hizo zinawakutanisha na Cleopatra, rafiki wa siku nyingi wa Levina ambaye ni bosi kwenye kampuni ya baba yake.
Katika hali isiyo ya kawaida, Cleopatra anajikuta akivutiwa mno kimapenzi na Deo, na anajiwekea nadhiri ya kumpata. Je, nini kitaendelea?
Vipi shosti, mbona salamu imekuwa ya muda mrefu hivyo? Shemeji yako huyu ujue…” akasema Levina kwa utani, lakini moyoni alikuwa akimaanisha. Mwanamke kwa wivu wewe!” Akasema Cleopatra akimwachia mkono Deo.
Ukweli ambao Cleopatra alishindwa kuuficha mbele ya shoga yake wa siku nyingi Levina, ni kwamba alitokea kumzimikia ghafla Deo, na sasa alitamani kumpindua na kulionja penzi la Deo. Moyoni alijiwekea nadhiri kuwa lazima atafanya chochote kinachowezekana ilimradi ampate Deo.
Mazungumzo yaliendelea wakiwa kwenye bustani ya maua, nyumbani kwa akina Cleopatra, Mbezi Beach na kwa moyo mkunjufu akakubali kumpatia Deo kazi katika kampuni ya baba yake ambayo yeye ndiyo alikuwa bosi.
“Shaka ondoa, kazi umepata Deo, Levina ni mtu wangu tangu kitambo, siwezi kumuangusha,”
“Ahsante sana!” Alijibu Deo kwa furaha akiamini sasa maisha yake yatabadilika.
Mazungumzo ya kawaida yakawa yanaendelea kati ya Levina na Cleopatra. Baada ya kukaa pamoja na kuzungumza mengi, hatimaye muda wa Deo na Levina kuondoka ulifika.
Kama ilivyokuwa wakati wa kusalimiana mara ya kwanza, Cleopatra alijikuta akiganda kwa Deo, hali iliyozidi kumtia hofu Levina.
“Hii ni ‘business card’ yangu, chukua tafadhali,” aliongea Cleopatra wakati akimkabidhi Deo kadi yake ya mawasiliano.
“Namba yako nitachukua kwa Levina kwa ajili ya kukutaarifu siku ya kuja kuripoti kazini.”
“Sawa! Nashukuru sana,” alijibu Deo huku akionesha wazi jinsi alivyofurahi kupata kazi.
“Hee shosti, utanikwaza sasa hivi! Kuagana tu ndiyo mpaka umgande shemejiyo kama ruba! hebu mwachie huko, na wewe ndiyo utakuwa mlinzi wake kazini, ole wako nisikie unamtaka,” alisema kwa utani Levina lakini akionekana kumaanisha kile alichokisema.
Cleopatra alimuachia mkono Deo na wakaanza kuondoka. Akilini mwake, Deo alishahisi kuwa amezimikiwa na bosi wake mtarajiwa, lakini kwa jinsi alivyokuwa anampenda Levina, alijiapiza kuwa kamwe hawezi kumsaliti.
“Deo mpenzi, unaenda kuanza kazi, na sasa kila mtu anakusifia kuwa wewe ni ‘handsome’, tafadhali usije ukanisaliti mpenzi wangu,” alilalama Levina huku akimkumbatia Deo kimahaba.
“Siwezi honey, amini nakwambia.”
***
Siku chache baadaye Deo aliitwa kwa ajili ya kufanyiwa usaili (Interview) ambapo alikidhi vigezo vyote. Kesho yake akaanza kazi akiwa kama mhasibu kwenye kampuni ya baba yake Cleopatra ya Planet-link Enterprises, ambayo Cleopatra ndiyo alikuwa msimamizi wa shughuli zote (bosi).
Kama alivyokuwa amejiapiza tangu siku ya kwanza anakutana na Deo, alimuweka kwenye kitengo cha uhasibu, hali iliyowafanya wawili hao kuwa karibu muda mwingi wawapo kazini.
“Nitakufundisha kazi mpaka utakapozoea vizuri, usisite kuniuliza chochote kinachokusumbua na nitakupa msaada unaouhitaji,” alisema Cleopatra wakati akimkaribisha Deo ofisini.
Tofauti na alivyokuwa mwanzo, Deo wa sasa hakuwa tena yule ‘shamba boy’. Alikuwa akionekana ‘smart’ muda wote, huku ‘u-handsome’ aliojaaliwa na Mungu ukichanua na kuwachanganya wanawake wengi, Cleopatra akiwa mmoja wapo.
Kwa kadri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga, Cleopatra alizidisha vituko kwa Deo, akimtega kwa kila namna ili anase kwenye himaya yake.
“Leo naomba tutoke wote nikakupe ‘lunch’!” Cleopatra alimwambia Deo.
“Sawa, hakuna shida! Ngoja nimalizie kazi kidogo ‘then’ tutatoka.”
Wakiwa kupata ‘lunch’, Cleopatra alikuwa akimchombeza Deo kwa maneno ya uchokozi huku akimsisitiza kuwa asije kumwambia Levina kuwa wametoka pamoja.
“Namjua shoga yangu, Levina. Ana wivu sana akimpenda mtu, kwa hiyo tafadhali usije kumwambia kitu.”
“Lakini mi naona hakuna tatizo lolote akijua, si tumetoka ‘lunch’ ya kawaida, hata mwenyewe angekuwepo tungejumuika pamoja.”
“Ni kweli Deo, lakini sitaki kukorofishana na Levina.”
“Poa nimekuelewa!”
“Nikwambie kitu Deo, ‘You are soo handsome!’ (Wewe ni mzuri sana).
Deo hakujibu kitu zaidi ya kutabasamu kwa haya, hakuzoea kusifiwa maishani mwake.
Baada ya kumaliza kupata chakula cha mchana, walirudi kazini na kuendelea na shughuli za kawaida, kila mtu akiwajibika sehemu yake.
Siku zilizidi kusonga ambapo Deo na Cleopatra wakazidi kuwa jirani.
Ilifika mahali ikawa bila kumuona Deo, Cleopatra hawezi kwenda kupata chakula cha mchana peke yake. Akaanza mazoea ya kumpelekea zawadi ndogondogo. Urafiki wao ukazidi kushamiri.
“Deo!”
“Naam Bosi!”
Aah! Si nilishakukataza kuniita bosi? Niite jina langu bwana.”
“Im sorry, naam Cleopatra”
“Leo ukimaliza kazi jioni una ratiba gani?”
“Nitamsindikiza Levina kwa shangazi yake Mabibo.”
“Basi kama leo utakuwa taiti, naomba wikiendi hii nikutoe ‘out’.”
“Labda nikamuombe kwanza ruhusa Levina, akikubali sawa.”
“Acha mambo ya kitoto Deo, we unafikiri Levina atakuruhusu kutoka na mimi? Halafu si nilishakwambia mambo yangu na wewe usimwambie? Usiniangushe bwana.”
“Ok basi poa, si Jumamosi eti eeh!”
“Eeh! Nataka nikakupe zawadi nzuri niliyokutunzia kwa siku nyingi,” alijibu Cleopatra kwa kudeka huku akimtazama Deo kwa jicho la huba.”
Hatimaye Jumamosi ikafika, siku ya miadi ambayo Cleopatra na Deo walikubaliana kutoka ‘out’ pamoja.
“Huwa unatumia kinywaji gani? Namaanisha bia gani?”
“Pombe huwa sinywi, labda soda tu.”
“Leo kwa kuwa uko na mimi , naomba unywe japo kidogo uchangamshe akili,” alisema Cleopatra huku akiendesha gari lake kuelekea Kunduchi Wet and Wild Hotel. Mawazoni mwake, alikuwa akipanga mengine, na aliamini ile ndiyo siku yake ya kumfaidi Deo.
Je, nini kitaendelea