WEST SIDE NIGGAS.
Kaika miaka ambayo nchi ya Siera Leon ilikuwa kwenye vita kali ya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1991 kuliibuka kikundi hatari nchini humo ambacho kilijulikana kama WEST SIDE BOYS (muda mwingine wakijulikana pia kama West Side Niggaz au West Side Junglers) ambao walikuwa na makao makuu yao katika kijiji cha Magbeni na Gberi Bana karibu kabisa na mto maarufu wa Rokel.
Kikundi hiki mwanzoni kilianza kama sehemu ya wapiganaji wa kikosi cha Armed Forces Revolutionary Coucil ambao walikuwa wanaunga mkono wapiganaji wa Revolutionary United Front kuipinga na ili kuing’oa serikali ambayo ilikuwa madarakani.
Wapiganaji wengi wa kikundi hiki cha West Side Boys walikuwa-recruited tangu utotoni kwa wazazi wao kuwawa na wao kutekwa na baadae kufanywa kuwa wapiganaji watiifu wa kikundi hiki.
Kwa kiwango kikubwa kikundi hiki kiliundwa na vijana wenye umri wa kati nah ii ilipelekea kikundi hiki licha ya kujihusisha na mapigano ya kijeshi lakini kilikuwa kinajinasibu na kujiendesha kwa tamaduni za kimarekani za muziki wa kufokafoka (rap) na tamaduni za hip-hop.
Labda nikiwa mahususi zaidi, kikundi hiki kilimuhusudu mno mwanamuziki wa rap Tupac Shakur pamoja na mtazamo wa ‘Kigangstaa’ ambao huwa anaudhihirsha kwenye muziki wake. Hii ndio sababu ya chaguzi ya jina la kikundi hiki ambao rasmi kabisa wao wenyewe walikuwa wanajiita ‘West Side Niggaz’ lakini kutokana na sababu za kimaadili kufanya vyombo vya habari kushindwa kutumia neno ‘Niggaz’ ndipo vyombo vya habari vikaondoa neno ‘Niggaz’ na kuweka ‘Boys’.
kikundi hiki kilikuwa kinajuliakana kwa umaarufu wake wa ukatili uliopitiliza ambao hasa unaaminika ulitokana na historia ya wapiganaji wake namna ambavyo walipatikana ambapo nilieleza awali kuwa wengi wao waliingizwa kwenye kikundi hiki tangu utotoni baada ya kutekwa kutoka kwenye familia zao. Jambo la msingi ambalo tunapaswa kulifahamu ni kwamba hawakutekwa tu hivi hivi na kuchukuliwa na kisha kuingizwa kundini, bali ilikuwa inafahamika wazi kwamba, watu wa kikundi hiki wakivamia kijiji kwa lengo la kuchukua watoto wa kiume mateka, kabla ya kuondoka nao walikuwa wanawalazimisha kuua familia zao kwa ukatili mkubwa.
Hii ilifanywa na viongozi wa kikundi hiki ili kuwapandikizia roho ya ukatili watoto hawa na kuua kiini cha ubinadamu wao na kuwafanya wajione na kutenda kama ‘wanyama’. Lengo lao hili lilitimia kwani kuna muda wakati wa vita hii ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leon kikundi cha ‘West Side Boys’ kiliibuka na kuwa moja ya vikundi vya wapiganaji ambavyo vilikuwa vinaogopwa zaidi.
Licha ya kuwa vitani na kufanya ukatili wa kila aina lakini wanachama wa kikundi hiki hawakuwa nyuma katika ‘kula maisha’ kwani walifahamika kuishi maisha ya ‘kigangstaa’ kama ambavyo wanaona kwenye muziki wa hip-hop wa kimagharibi. Walijulikana sana kwa kutumia sana bangi, cocaine, pombe na muda mwingine kuvaa mavazi ya kimagharibi mno licha ya kuwa vitani.
Silaha zao nyingi walipata kwa kubadilishana na almasi ambazo zilikuwa zinapatikana katika njia tata sana vitani mpaka kufikia wakati zikaitwa jina la ‘blood diamonds’. Magari yao karibia yote waliyokuwa wanayatumia kwa usafiri mengi walikuwa wameyateka kutoka kwenye misafara ya misaada ya chakula ya UN.
Sasa basi,
Kama ambavyo nimeeleza kuwa kikundi hiki cha West Side Boys mwanzoni kilikuwa kinaendeshwa na waasi wa Revolutionary United Front ambao walikuwa wanapambana ili kuiondoa serikali madarakani, lakini kuna muda baadae waligeuka na kuanza kupigana upande wa serikali, yaani baadae walipigana dhidi ya mabosi wao wa Revolutionary United Front.
WAPIGANAJI WA "WEST SIDE BOYS"
Baada ya nchi kuanza kutulia katika miaka ya mwanzoni mwa 2000, vikundi vyote vya wapiganaji vilipewa ‘ofa’ ya kuingizwa rasmi katika jeshi la nchi. Vikundi vingi vilipokea ofa hii kwa mikono miwili lakini wapiganaji wa West Side Boys walikataa ofa hii na kuendelea na harakati zao za msituni kutokea katika makao makuu yao ya kijiji cha Magbeni na Gberi Bana.
Ikumbukwe kwamba katika vita hii, nchi ya Uingereza ilikuwa inaunga mkono serikali kwa kipindi chote cha maiaka 11 ya vita hii ya wenyewe kwa wenyewe.
Mwezi May mwaka 2000 kikosi maalumu cha wanajeshi wa Uingereza kiliingia nchini Sierra Leon kwa lengo moja kuu la kutekeleza operesheni malumu la kusaidia kuondoa nje ya nchi hiyo raia wa Uingereza na wa nchi za jumuiya ya madola ambao bado walikuwa nchini humo. Zoezi hili lilipewa jina la ‘Operation Palliser’. Wanajeshi ambao walikuwa wamepewa jukumu hili walikuwa na amri ya kutojihusisha na mapambano yoyote ya kijeshi bali waelekeze nguvu zao kwenye kusaidia raia wa uingereza na nchi za jumuiya ya madola kuondoka nchini humo, kwa lugha nyingine hii ilikuwa ni ‘non-combat operation’.
Kama sehemu ya mkakati wao wa uokozi kikosi hiki cha jeshi la uingereza viliweka chini ya himaya yake mji wa Freetown na uwanja wa ndege wa Lungi, ambao ndio kiwanja kikuuu cha ndege nchini Sierra Leon. Baada ya hapo liliendeshwa zoezi maridhawa la kuwaondoa nchini humo raian wote wa nchi za jumuiya ya madola ambao walikuwa tayari kwa hiari yao kuondoka nchini humo.
Baada ya Oparesheni Palliser kukamilika kikosi kile cha awali kiliondoka nchini Sierra Leon na kisha kuingizwa kikosi kingine kidogo kilichojulikana kama STTT (Short Term Training Team) ambacho kazi yake kuu waliyopewa ilikuwa ni kulisuka upya kimafunzo jeshi la Sierra Leon.
Kikosi hiki cha STTT kiliundwa na batalioni ya pili ya The Royal Anglian Regiment ambao ilipofika mwezi July mwaka huo 2000 walipumzishwa na nafasi yao kuchukuliwa na batalioni ya kwanza ya The Royal Irish Regiment (1 R IRISH) ambao sasa wao ndio walifanya kazi nchini Sierra Leon kama STTT.
Shughuli za kulifunda jeshi la Sierra Leon ikaendelea kwa mafanikio makubwa na kwa muda wote huu kikosi hiki kipya cha STTT kilikuwa salama kabisa nchini humo.
Lakini ilipofika siku ya tarehe 25 August mwaka 2000 msafara wa magari ya kijeshi ya STTT ulitoka kambini kwao eneo la Waterloo na kuelekea eneo linaloitwa Masiaka kuwatembelea walinda amani kutoka nchi ya Jordan ambao walijumuishwa katika kikosi maalumu cha Umoja wa Mtaifa ambacho kilikuwa nchini humo kikijulikana kama *UNAMSIL*.
Ulipofika muda wa chakula cha mchana wakiwa huko Masiaka walipata taarifa kuwa hatimaye kikundi cha West Side Boys wamekubali ombi la serikali la kuweka silaha chini na kujisalimisha.
Taarifa hii ya kijeshi ilikua imetolewa pasipo usahihi wa asilimia mia. Tofauti kabisa na taarifa hii kueleza kuwa West Side Boys wamekubali kuweka silaha chini, lakini uhalisia ulikuwa ni kwamba kuna wapiganaji wapatao kama 200 tu kutoka kikundi cha West Side Boys ndio ambao walikuwa wamekimbia kikundi chao na kwenda kujisalimisha kwa majeshi ya serikali, lakini kikundi chenyewe halisi bado kilikuwa na wapiganaji wapatao 400 ambao bado walibakia kuendeleza harakati zao.
Taarifa hii ilikuwa ni ya kutia moyo mno kutokana na Group la vijana hawa wa West Side Boys kusumbua mno vichwa vya majeshi ya serikali pamoja na vikosi vingine ambavyo vilikuwemo nchini Sierra Leon. Kama ilivyo Ada ya wanajeshi wote wanapopokea taarifa hii inakuwa kana kwamba hakuna haja ya kusubiri zaidi mpaka pale ambapo watahakikisha kama ni kweli walichokisikia kilikuwa ni sahihi na labda ndani ya Mwezi huu jeshi la nchi hiyo litakuwa limepiga hatua kubwa na labda hatimaye Simulizi za kutisha za vijana wa West Side Boys hawatazisikia tena.
Kwa hiyo ulipofika muda wa kurejea kambini kwao Waterloo, kamanda wa msafara huu wa kikosi hiki cha STTT (1R IRISH) alishauri kuwa wajiridhishe kuhsu taarifa hiyo ya vijana na West Side Boys kuweka silaha chini.
WEST SIDE BOYS
Sasa basi, ukiwa unatoka eneo la Masiaka kwenda Wasterloo au Waterloo kwenda Masiaka, maeneo fulani ya kati kati kuna barabara inachepuka kulekea kwenye kijiji cha Magbeni ambacho kama nilivyoeleza awali kuwa kilikuwa kinatumiwa na West Side Boys kama makao makuu yao.
Kwa hiyo, Meja Alan Marshall, kamanda wa msafara akaamuru kuwa wachepuke kufuata barabara hiyo mpaka kijijini Mgbeni ili kuthibitisha taarifa ambayo walikuwa wameipata kuwa vijana hao walikuwa wameweka silaha chini.
Msafara ukashika kasi kukaribia kabisa kijiji cha Mgbeni. Lakini wakiwa wamebakiza kama kilomita mbili tu kuingia kwenye kijiji hicho walishangaa ghafla tu mbele yao imetokeza gari aina ya Bedford ambayo imefungwa mizinga ya kudungua ndege imewaziba njia mbele yao. Kufumba na kufumbua kila upande… nyuma, mbele… kushoto, kulia… walikuwa wamezungukwa na mamia ya wapiganaji wa West Side Boys wakiwa wamewanyooshea bunduki.
Msafara wao (STTT) ulikuwa na wanajeshi 11 tu, lakini vijana hawa wa West Side Boys ambao walijitokeza ghafla walikuwa si chini ya 150 au 200. Kwa maana hiyo ilikuwa dhahiri kabisa hawakutakiwa kuanzisha mapambano ya risasi kwani ndani ya sekunde kadhaa tu wangeuwawa. Hivyo basi hawakuthubutu hata kuinui silaha zao na kuwanyooshea ‘vichaa’ hawa wa West Side Boys ili walau waonekane hawakuwa na nia mbaya yeyote ile.
Baada ya kuwekwa chini ya ulinzi, walinyang’anywa silaha zote pamoja na magari yao ya kijeshi aina ya Land Rover zenye ‘Wimik’ (Weapons Mount Installation Kit (Tazama picha)) na kisha wakaongozwa kwa miguu kutoka pale walipokamatwa na kuvuka mto Rokel na kuingia kijiji cha Gberi Bana ambako ndiko kwenye makazi ya kiongozi wa kikundi hiki, mwanajeshi mwenye mbwembwe na ukatili usiomithilika, ‘Brigedia’ Foday Kallay.
Baada ya wanajeshi hawa mateka wa STTT kufikishwa tu mbele yake, kitu cha kwanza ambacho ‘Brigedia’ Faday Kallay alikifanya ni kuinua simu na kupiga London, serikali ya Uingereza.
Simu ilivyopokelewa… Brigedia Faday Kallay hakutaka salamu au kujieleza sana… moja kwa moja akaelekea kwenye hoja zake.
“this is brigadier Foday Kallay…get a piece of peper and a pen.!” Kallay alijieleza kwa lafudhi yake mbovu ya kiafrica cha magharibi.
“what for?” aliyepokea simu akamuuliza.
“I want you to write down a list of my demands.!!” Brigedia Faday Kallay akongea kwa kujiamini.
“demands for what.!?” Aliyepokea simu aliuliza kwa mshangao zaidi.
“…I have eleven of your soldiers… and if you don’t comply to my demands they are going to be dead in 48 hours.!” Brigedia Fadaya Kallay aliongea kwa sauti thabiti na kujiamini kabisa.
Japokuwa kwa kiasi fulani vita ya wenyewe kwa wenyewe hapa nchini Sierra Leon ilikuwa inaishia ishia… lakini kwa upande wa nchi ya Uingereza, siku hii ya August 5, 2000 walikuwa kana kwamba wanaingia upya kwenye ‘vita’ ya kwao na kikundi cha West Side Boys.
Jambo baya zaidi vijana hawa walikuwa hawaogopi kifo… ilikuwa ni kana kwamba nafsi zao zilikuwa tayari ziko kuzimu na ni miili tupu ilikuwa inatembea… hivyo kama Uingereza ilitaka kuwapata tena wanajeshi wake wakiwa bado hai… basi walipaswa kupiga kila hatua kuanzia sasa kwa umakini na weledi uliotukuka.
Baada ya serikali ya uingereza kupokea taarifa juu ya kutekwa kwa wanajeshi wake wa kikosi cha STTT jambo la kwanza kabisa ambalo walilifanya ilikuwa ni kutuma timu ya 'negotiators' kwenda nchini Sierra Leon.
Vichwani mwao walikiwa wakiamini kuwa walikuwa wanaweza kuwashaiwshi vijana wa West Side Boys kwa kuwapa vitu vya anasa ili wawaachie wanajeshi wao.
Timu hii ya negotiators iliongozwa na Luteni Kanali Simon Fordham ambaye ndiye alikuwa kamanda mkuu wa kikosi cha 1R IRISH (STTT) kilichopo nchini Sierra Leon.
Pamoja naye alikuwa na wasaidizi kadhaa ambao ni 'professional negotiators' kutoka Metropolitan Police nchini Uingereza.
Licha ya tukio hili kutoka ndani ya ardhi Sierra Leon, lakini Rais Ahmad Kabbah wa nchi alitoa ruhusu yote ya Uingereza wenyewe kuendesha juhudi za kuokoa wanajeshi wao kutokana na suala dhahiri kuwa Sierra Leon hawakuwa na weledi wa kutosha kwa namna yoyoye ile kufanikisha shughuli hiyo.
Kwa hiyo timu hii ya negotiators ikiongozwa na Luteni Kanali Simon Fordham walifanya mawasiliano na uongozi wa West Side Boys ili kuanza mazungumzo. Vijana hao walishikilia msimamo wao wa kutowaachia wanajeshi kwa madai kuwa waliwachokoza kwa makusudi kwa kuingia kwenye himaya yao kijiji cha Mgbeni.
Baada ya mazunguzo marefu sana hatimaye walikukubaliana makutano yao ya kwanza yawe siki ya August 29, 2000 nje kidogo ya kijiji cha Mgbeni kwenye barabara inayochepuka kwenda njia kuu ya Waterloo.
Katika mkutano wao huu wa kwanza upande wa Uingereza uliongozwa na Luteni Kanali Simon Fordham na uoande wa West Side Boys uliongozwa na kiongozi wao mkuu 'Brigedia' Foday Kallay.
Walipokutana, Fordham aliweka msimamo kuwa hawezi kuongea kitu chochote na Kallay mpaka pale ambapo atapewa uhakika kuwa Wanajeshi waliotekwa bado walikuwa hai.
Walibishana kwa muda wa dakika nyingi sana ambapo Brigedoa Foday Kallay akisisitiza kuwa wanajeshi waliotekwa wako hai lakini Luteni Kanali Simon Fordham aliendelea kusisitiza kuwa hawezi kuamini maneni tupu, anataka uthibitisho halisi.
Ili kuepusha mazungumzo yasivunjike, Kallay aliamuru wanajeshi wawili waliotekwa waletwe kutoka kijijini Mgbeni mpaka hapa kikaoni.
Ndani ya dakika chache tu, wapiganaji wake waliwaleta mateka wawili hapo kikoni, kiongozi wa ule msafara uliotekwa ambaye aliitwa Meja Allan Marshall na mwanajeshi mwingine Kapteni Flaherty.
Ukweli ni kwamba negotiators hawa walikuwa wanajua kuwa wanajeshi wao waliotekwa walikuwa hai kabla hata ya kufika hapa, lakini walikiwa na lengo la siri ndani ya akili zao kutaka waletwe hapa wawaone kwa macho yao.
Walipokuwa wakisalimiana na wenzao baada ya kuletwa hapo kikaoni, walipokuwa wanapeana mikono kwa ustadi mkubwa na weledi wa kijeshi Luteni Kanali Simon Fordham alimpa kikaratasi kwa siri Kapteni Flaherty. Karatasi hii ilikuwa ni ramani ya kijiji chote na majengo ya kijiji cha Gberi Bana ambacho mateka hao 11 wa kijeshi walikuwa wanashikiliwa.
Kikao kiliendelea na hoja kuu mezani ilikuwa ni kusikiliza 'demands' za West Side Boys wanazotaka kutimizwa ili waweze kuwaachia mateka wa kijeshi walionao.
Orodha yao ilikuwa ni ndefu kweli kweli, kana kwamba matatizo yao yote walikuwa wanataka yaishe kulitia tukio hili. Katika uhalisia wa kawaida ilikuwa ni kama haiwezekani kutimiza matakwa yao yote japokuwa serikali ya Uingereza mwanzoni walikuwa na dhamira nzuri ya kumaliza suala hilo mezani.
Licha ya orodha ya wavitakavyo kuwa ndefu sana, lakini vitu vyenye uzito zaidi vilikuwa ni hivi vifiatavyo;
1. Kupatiwa vifaa vya mawasiliano, hasa simu za satelaiti.
2. Madawa ya matibabu
3. Wapatiwe kinga ya kisheria kuwazuia serikali kuwashitaki wakiamua kuweka mitutu chini.
4. Kufanywa marekebisho kwenye mkataba wa Lome (Lóme Peace Accord)…. Mkataba juu ulisainiwa mwaka 1999 kati ya serikali ya Rais Ahmad Tejan Kabbah na kiongozi wa RFU Bw. Foday Sankoh.
5. Kuachiwa kwa mateka wote wa kikundi cha West Side Boys waliopo kwenye jela za serikali.
6. Kupewa scholarship kwa kiongozi wa juu wa West Side Boys waliokuwa wanataka kwenda kusoma chuo kikuu nchini Uingereza.
Matakwa haya yalikuwa ni ya kiwendawazimu… lakini ndicho ambacho West Side Boys walikuwa wanakitaka ili waweze kuwaachia mateka waliokuwa nao.
Kikao cha pili kilifanyika siku ya tarehe 31 August.
Katika kikaoni hiki upande wa Uingereza walitimiza matakwa mawili ya West Side Boys… waliwasilisha simu za satelaiti pamoja na madawa ya matibabu.
Kutokana na kutimiza matakwa hayo mawili, West Side Boys walikubali kuwaachia wanajeshi watano kati ya wale 11.
Matakwa haya mawili ya West Side Boys yalikuwa yanatekelezeka tofauti na yale mengine, na ndio maana Uingereza walianza nayo. Yale matakwa mengine yaliyosalia kiuhalisia yalikuwa hayatekelezeki au kama yangetekelezwa basi yangeleta mgogoro mkubwa kuliko ambavyo mgogoro waliokuwa wanataka kuumaliza.
Kwa hiyo ilikuwa dhahiri kabisa kwamba jambo mbadala lilikuwa linahitajika kufanyika.
Uzuri ni kwamba kikundi cha West Side Boys wenyewe walikuwa wamefanyaakosa mawili bila kujijua.
Kosa la kwanza lilikuwa ni mateka wale watano ambao waliwaachia. Walikuwa hawajua kuwa kwenye kile kikao cha kwanza walikabidhiwa kwa siri kikaratasi cha eneo lote ambalo walikuwa wameshikiliwa. Kwa hiyo mpaka siku hii walipokuwa wanaachiwa walikuwa wamekusanya intelijensia ya kutosha kuhusu kijiji cha Gberi Bana.
Kosa la pili, lilitokana na haiba ya ujivuni wa viongozi wa West Side Boys. Walipokabidhiwa tu simu za upepo moja kwa moja waliporejea makao makuu yao walipiga simu kwenda kituo cha habari cha BBC na kufanya mahojiano LIVE kujigamba na kusisitiza kuhusu demands zao zilizosalia.
Kitu ambacho hawakukijua ni kwamba jeshi la Uingereza lilikuwa linafuatilia mawasiliano haya na kufanya 'triangulation' ili kujua kwa ufasaha zaidi simu ilikuwa inapigwa kutoka wapi.
Mateka wale wa kijeshi walioachiwa siku hiyo hiyo haraka sana walisafirishwa kwa chopa mpaka kwenye meli ya kijeshi ya RFA Sir Percivale ambayo ilikuwa pwani ya Africa magharibi ili kwenda kuwasilisha intelijensia waliyo nayo kuhusu kijiji ch a Gberi Bana kwa makamanda wa kijeshi waliokuwa kwenye meli hiyo kutoka Uingereza.
Matakwa ya West Side Boys yalikuwa hayatekelezeki. Jambo mbadala la haraka lilikuwa linatakiwa kufanyika.
Kabla sijaendelea mbali sana, nieleze kidogo kuhusu SAS na 1 PARA vitengo vya weledi ambavyo vililengwa na jeshi la Uingereza kutumika katika oparesheni ya uokozi wa wanajeshi waliotekwa na wapiganaji wa West Side Boys.
SPECIAL AIR SERVICES (SAS)
SAS ni kitendo maalumu cha weledi cha jeshi la Uingereza. Kitengo hiki kiliundwa mwaka 1941 kikiwa kama ‘regiment’ na baadae mwaka 1950 kilibadilishwa kuwa ‘corps’.
Nieleze kidogo hii tofauti ya regiment na corp katika mifumo ya kijeshi.
Katika mfumo wa vitengo vya kijeshi, ‘category’ ya vitengo/kikosi na namna kinavyopewa jina inategemea na kazi ya weledi pamoja na idadi ya wanajeshi kwenye kitengo?kikosi hicho.
Kwa mfano;
FIERTEAM – Inakuwa na watu 3 mpaka 4 na kiongozi wao mara nyingi huwa ni Koplo.
SQUAD – Inakuwa na watu 8 mpaka 12 na kiongozi wao huwa ni Sajenti.
PLATOON – Huwa na watu 15 mpaka 30 na kiongozi wao huwa ni Luteni.
COMPANY – Huwa na watu 8 mpaka 150 na kiongozi wao huwa ni Kapteni au Meja.
BATTALION – Huwa na watu 300 mpaka 800 na kiongozi wao huwa ni Luteni Kanali.
BRIGADE (REGIMENT) – Huwa na watu 2000 mpaka 4000 na huongozwa na Kanali au Brigedia Jerenerali.
DIVISION – Huwa na watu 10,000 mpaka 15,000 na huongozwa Meja Jenerali.
CORPS – Huwa na watu 20,000 mpaka 40,00 huongozwa na Luteni Jenerali
JESHI (FIELD ARMY) – Huwa na watu 80,000 na kuendelea na huongozwa na Jenerali.
KIKUNDI CHA MAJESHI (ARMY GROUP) – Inaundwa na Majeshi (field Army niliyotaja hapo juu) mawili au zaidi. Huongozwa na Field Marshal au Jenerali wa nyota Tano.
REGION/THEATER – Huu ni Mkusanyiko wa ‘Army Groups’ (nilizotaja hapo juu) Nne au zaidi. Huongozwa na Jenerali mwenye nyota Sita au Amiri Jeshi Mkuu (Mara nyingi huwa ni Mkuu wa Nchi).
NB: Idadi ya wanajeshi kwenye vitengo hutegemea na mifumo ya kijeshi na utartibu wa nchi husika japo karibia nchi zote duniani hutumia mfumo huu katika kutambua/kutoa majina kwa vikundi/vikosi vyake na viongozi wa vikosi/vikundi hivyo.
Kwa hiyo ninaposema kuwa SAS iliundwa mwaka 1941 kama ‘regiment’ na mwaka 1950 ilifanywa kuwa ‘corps’ naamini kuwa unanielewa kwa ufasaha kabisa.
Mizizi ya SAS unaweza kuipata kuanzia mwaka 1941 na kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Lakini mwaka 1947 iliundwa upya kama sehemu ya Territorial Army na kupewa jina la 21st Special Air Services Regiment (Artists Rifles).
SAS hupata watu wake kutoka katika vitengo vingine vya jeshi la Uingereza na mara nyingi huchukua wanajeshi ambao wana mafunzo ya ukomando tayari au ‘Airborne Foce’.
Kazi kubwa ya SAS ni kufanya ‘Covert Reconnaissance’ (hii ni kufanya ushushus wa eneo maalumu (mara nyingi eneo la adui vitani) na kupata kujua jografia ya eneo la adui, na namna aduai alivyojipanga). Pia SAS hufanya couter-terrorism, mashambulizi ya weledi dhidi ya adui (direct action) na uokoaji wa mateka.
SAS ilijipatia umaarufu mkubwa mwaka 1980 katika tukio la uokoaji wa mateka kutoka kwenye ubalozi wa Iran, tukio ambalo lilirekodiwa na kuirushwa kwenye runinga.
Nitaongelea kuhusu hili tukio huko mbeleni kwenye nfululizo huu huu wa makala ya Operesheni za kijasusi zilizofanikiwa zaidi.
1 PARA
1st Battalion, Parachute Regiment (1PARA) ni sehemu ya Kitengo cha usaidizi kwa vikosi vya weledi wa majeshi ya Uingereza (Special Forces Support Group – SFSG).
1PARA mizizi yake inaweza kupatikana kuanzia miaka ya 1940 kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambapo kikosi maalumu cha No. 2 Commando chenye ukubwa wa batalioni kilipewa mafunzo maalumu ya parashuti katika kambi ya kijeshi ya Cambria maeneo ya Perham Down, karibu na Tidworth, Hants.
Kikosi hiki kilikuwa na ‘troops’ nne – A, B, C na D. baadae kikaongezewa mpaka kufikia troops 11. Baadae makomando hawa wa kitengo hiki wote walibadilishiwa majukumu na kupelekwa SAS huku jeshi likitengeneza kikosi kingine kipya cha No. 2 Commando.
Baada ya kikosi hiki kipya kuundwa muda mchache baadae kilisukwa upya na kupewa jukumu jipya na jina jipya la 1st Parachute Battalion.
Tangu kipindi hicho mpaka sasa 1 PARA imekuwa na jukumu kuu la kufanya usaidizi maalumu katika oparesheni za kijeshi zinazohusisha vikosi vya weledi kwenye oparesheni maalumu.
Hii ndio sababu ya 1 PARA katika mifumo ya kijeshi kuwekwa kwenye ‘category’ ya Special Opareations Light Infatry ikiwa na maana ya kwamba… kwenye miaka ya zamani kabisa kwenye medani za kivita, light Infatry walikuwa ni wanajeshi wa miguu wenye kubeba silaha nyepesi ambao walikuwa wanatumika kama ‘chambo’ kabla ya wanajeshi wenye silaha nzito kuanza mashambulizi. Lakini katika ulimwengu wa kisasa. Light Infatry imeboreka zaidi na kuwa ni wanajeshi ambao katika medani za kivita weledi wao mkubwa ni katika kasi na mnyumbuko wa haraka wa uendeshaji wa majukumu yao pasipo kutegemea zaidi silaha nzito. Na mara nyingi Light Infatry inakwenda sambamba na ukomando na matumizi ya Parashuti.
TURUDI KWENYE OPERATION BARRAS…
Nilikuwa najaribu kueleza ni kwanini jeshi la Uingereza liliamua kutumia SAS ikisaidiwa na 1 PARA kutekeleza oparesheni ya uokoaji wa mataeka wa kijeshi walichukuliwa na wapiganaji wa West Side Boys nchini Sierra Leon. Na nimeeleza kuwa sababu kuu ya kuamua kuwajumuisha 1 PARA ni kutokana na makao makuu ya West Side Boys kuwepo kwenye vijiji viwili tofauti ambavyo vimegawanywa kwa mto (kijiji cha Mgbeni na Gberi Bana).
Kwa hiyo,
Jeshi la Uingereza lilitoa maagizo kwa makao makuu ya 1 PARA kuandaa kikosi maalumu ambacho kitashiriki katika oparesheni hii ambayo ilikuwa inapangwa. Kiongozi mkuu wa batalioni hii ya 1 PARA akateua kikundi maaumu cha A COMPANY kinachoongozwa Meja Matthew Lowe, ambacho kwa wakati huo kilikuwa kwenye mazoezi nchi Jamaica. Japokuwa makomando karibia wote wa kikundi hiki cha A Company walikuwa ni wapya jeshini lakini viongozi wa 1 PARA waliamua kuwapa jukumu hili kwa kuzingatia kuwa wanajeshi wapya ambao ndio kwanza wametoka mafunzoni morali yao inakuwa iko juu sana. Walichokifanya ilikuwa ni kuwaongezea makomando wachache wenye uzoefu ili kuhakikisha kuwa uzoefu wa medani ya vita haikosekani ndani ya kikundi hiki cha A Company ambao walikuwa wanatarajiwa kupelekwa huko Sirrea Leon.
Baada ya hapo siku ya August 31, A Company walirudishwa kutoka Jamaica mpaka Uingereza na moja kwa moja kupelekwa kwenye kijiji kinachitwa South Cerney nchini Uingereza. Mpaka muda huu hakuna commando yeyote ambaye alikuwa anajua ni nini kinaendelea. Wote waliambiwa kuwa wamepelekwa kijijini hapo kwa ajili ya kufanya mafunzo maalumu ya kijejeshi yajulikanayo kama “readiness to move”. Mtu pekee ambaye alikuwa anajua kwa nini wako hapo alikuwa ni kiongozi wao Meja Matthew Lowe.
Kesho yake jioni baada ya kuwasili kijijini hapo, makomando wote waliitwa na simu zao za mikononi kukusanywa na kuzimwa. Baada ya hapa ndio walielezwa lengo hasa la kurudishwa kutoka Jamaica mpaka Uingereza.
Wakati huo huo…
Kule nchini Siera Leon wale makomando wa SAS waliopandikizwa kwenye timu ya negotiators walikuwa pia wameanza kufanya covert reconnaissance ya hali ya juu zaidi. Walikuwa wanajitahidi kuingia maeneo ya karibu na vijiji vya Mgbeni na Gberi Bana nyakati za usiku ili kusoma namna ya ulinzi ulivyo kwenye hayo makoa makuu ya West Side Boys, silaha walizonazo pamoja na nguvu yao ya idadi ya wapiganaji.
Baadae kitengo kingine maalumu cha jeshi la Uingerreza cha weledi wa majini kijulikanacho kama Special Boat service kilifanikiwa kupitisha kwa siri kubwa boti ndogo ya kijeshi kwenye mto Rokel ambao unatenganisha kijiji cha Mgbeni na Gberi Bana. Boti hii ilikuwa imepakia makoamndo wanne wa SAS ambapo boti ilipopita wao waliruka, makomando wawili kila upande mmoja wa mto.
Makomando hawa nao kazi yao ilikuwa ni kukusanya taarifa nyeti zaidi kuhusu West Side Boys pamoja na kutambua sehemu ambazo helikopta za kijeshi zinaweza kutua.
Ulifika muda ambapo Uingereza ilikuwa imepata Intelijensia ya kutosha kuhusu wapiganaji wa West Side Boys na kilichobakia kilikuwa ni utekelezaji tu wa Oparesheni. Lakini changamoto kubwa ilikuwa ni vyombo vya habari.
Media zote ulimwenguni na hasa hasa vyombo vya habari vya Uingereza na Marekani vilikuwa vimeanza kuripoti juu ya ‘mining’ono’ kuhusu jeshi la Uingereza kufanya Oparesheni ya uokozi. Hili lilikuwa ni suala baya mno kwani kama habari hii ingeendelea kuripotiwa na kuaminika kwenye jamii, basi West Side Boys wangeweza kuua mateka wote ambao walikuwa nao.
Hivyo basi jeshi la Uingereza lilikuwa linajitahidi kwa kila namna kuficha mno mwenendo wao na kutoonesha dalili yoyote kwamba walikuwa wanataka kufanya Operesheni ya Uokozi. Hii iliwafanya iwawie vigumu sana kuingiza A Company ya 1 PARA nchini Sierra Leon kutokana na vyombo vya habari kufuatilia nyendo zote na kuzingatia kwamba hata ndani ya jeshi kulikuwa na watu wanaovujisha habari.
Kwa hiyo chaguo la kwanza lilikuwa ni ‘kulaunch’ shambulio kutokea Uingereza. Yaani siku ambayo operesheni itatekelezwa basi makomando watokee moja kwa moja nchini Uingereza na kuelekea vijiji vya Mgbeni na Gberi Bana nchini Sierra Leon. Lakini hii pia ilikuwa na changamoto yake. Ingeachukua takribani masaa 14 kulaunch operesheni kutokea Uingereza mapaka Mgbeni na Gberi Bana. Kijeshi hii ilikuwa ni ‘risk’ kubwa sana kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa wa West Side Boys Kushitukia mchezo wote kabla haujafanikiwa. Lakini pia safari ya masaa 14 ingewachosha sana makomando na ufanisi wao kwenye operesheni ungepungua sana.
Kwa kuzingatia hili, timu yote ya A Company ilisafirishwa mpaka Dakar nchini Senegal ili kuwe na urahisi wa kulaunch operesheni kutokea hapo kwa sababu nchi hiyo inapakana na Sierra Leon.
Pia ili kupunguza urasimu, balozi wa Uingereza nchini Sierra Leon ambaye alikuwa mjini Freetown, Bw. Alan Jones alipewa mamlaka yote ya kuamuru na kutoa kibali juu ya operesheni hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu. Pia Brigedia David Richards ambaye alikuwa ni kamanda wa vikosi vyote vya Uingereza ambavyo vilikuwa nchini Sierra Leon alipewa mamlaka yote ya kijeshi na kuwa na kauli ya mwisho ya kijeshi kuhusu operesheni hiyo.
Changamoto pekee ambayo walikuwa wamebakiwa nayo ilikuwa ni namna gani wataingiza nchini Sierra Leon makomando wa A Company kutoka 1 PARA pamoja na makomando wengine wa SAS pasio vyombo vya habari kugundua na pasipo kuvuja habari hiyo kutoka ndani ya jeshi.?
Katika hali kama hii ndipo ambapo suala la ‘uhuru’ wa kuripoti kila habari unaonekana kama ni ‘upuuzi’ kwa baadhi ya watu. Media zilikuwa zinataka stori na kila mtu akitaka kuwa wakwanza kuripoti habri hiyo bila kuzingatia ni kwa namna walikuwa wanakuwa kikwazo katika kuokoa maisha ya wale wanajeshi waliotekwa.
Upande wa pili wa mpaka, ndani ya Sierra Leon timu ya negotiators walikuwa wanaendelea ‘kununua muda’ kwa kuendeleza na kurefusha maongezi na West Side Boys ili kuwafanya waone kuwa Uingereza bado ilikuwa na nia ya kumaliza suala hilo mezani kwa maongezi.
Siku zilikuwa zimeyoyoma haswa… uvumilivu wa West Side Boys ulikuwa umeisha… walikuwa wanataka masharti yao yatekelezwe mara moja bila kuchelewa tena hata siku moja. Kadiri dakika zilivyyokuwa zinaenda mbele, ndivyo ambavyo wanajeshi mateka walikuwa wanakikaribia kifo cha kikatili mikononi mwa West Side Boys…
Lakini Brigedia David Richards alijiapiza kuwa kamwe hawawezi kupiga magoti na kuwaramba miguu West Isde Boys… Yaani ni kama waswahili tunavyosema, “inyeshe mvua au liwake jua” watawarudisha salama nyumbani kwa familia zao wanajeshi wao wote waliotekwa na watawashikisha adabu West Side Boys na watajutia kuvuka mpaka wa kuwagusa wanajeshi wa Uingereza.!!
Operation Barras ilikuwa imewiva!!
Mkakati wa oparesheni ambao Uingereza walikuwa nao kichwani ulikuwa kama ifuatavyo;
Walilenga A Company ya 1 PARA ifanye uvamizi katika kijiji cha Mgbeni wakati ambao timu ya SAS itafanya uvamizi katka kijiji cha Gberi Bana upande wa pili wa mto.
Lengo kuu la A Company kupewa jukumu la kuvamia kijiji cha Mgbeni lilikuwa ni kuharibu silaha zote za West Side Boys ambazo zingeweza kutumika kuvuruga Oparesheni. Kumbuka kwamba kama ambavyo nimeeleza kuwa makao makuu ya wapiganaji hawa yako kwenye vijiji hivi viwili ambavyo vinatenganishwa na mto.
Kijiji cha Mgbeni ndicho ambacho kilikuwa kinatumika kama ‘kambi kuu’ ya wapiganaji hawa na ndipo hapo haswa ambapo silaha zao nyingi na vifaa vya kijeshi walikuwa wanavitunza. Kijiji cha Gberi Bana ng’ambo ya mto kilikuwa kinatumika kwa lengo kuu la kwanza kama makazi ya kiongozi wao Foday Kallay na makamanda wake wakuu.
Lakini pia jukumu kuu la pili ambapo A Company walilengwa kupewa lilikuwa ni kuwadhibiti wapiganaji wa West Side Boys wasiweze kuvuka mto mpaka kijiji cha pili cha wakati ambapo SAS watakuwa wanafanya uokozi wa mateka ambao wamehifadhiwa huko. Lakini pia jukumu la tatu ambalo walipewa lilikuwa ni kuokoa magari yote ya kijeshi ambayo yalitekwa pamja na wanajeshi wao wale 11.
Lakini changamoto ya pili ilikuwa ni mbinu ambayo watatumia kuingia kwenye vijiji hivi vya Mgbeni na Gberi Bana. Kulikuwa na mapendekezo kadhaa.
i. Overland Approach: ilifikiriwa kwamba makomando hawa wanaweza kuingia kijijini hapo moja kwa moja kwa kutumia gari za kijeshi. Japokuwa mbinu hii ilikuwa ni nzuri na ya uhalisia zaidi, lakini hasara yake ilikuwa ni kwamba, haikuwa rahisi kuingia kwenye vijiji hivi bila kushitukiwa mapema kabla hata ya kufika kijijini Mgbeni kutokana na West Side Boys kuweka vizuizi vingi kwenye barabara yote ambayo inaelekea kijijini Mgbeni.
ii. Water-borne Insertion: pia ilifikiriwa kwamba makomando hawa wangeweza kuingizwa kinyemela kwenye vijiji vyote viwili kwa kutumia njia ya maji kama ambavyo wale makomando wanne walivyopenyezwa kwa boti za SBS (Special Boat Services) kwa ajili ya kufanya reconnaissance . Njia hii ilikuwa ni murua lakini changamoto yake ilikuwa ni kwamba, mto Rokel ulikuwa na mchanga mwingi kwa hiyo isingewezekana kupita kwa kutumia boti kubwa. Lakini pia mto huu ulikuwa na mkondo unaoenda kasi sana. Sababu hizi zote zilimaanisha kwamba kulikuwa na uwezekano wa kutumia boti ndogo pekee, kwa maana ya kwamba ilikuwa inabidi kupeleka makomando wachache wachache kwa awamu. Hii haikuwa salama sana kwani ilikuwa inatoa mwanya kwa West Side Boys kushitukia ambacho kilikuwa kinaendelea kwenye mto Rokel.
iii. mwishoni ikaamuliwa kuwa njia bora zaidi itakuwa ni kutumia helikopta za kijeshi aina ya Chinook kutoka kitengo cha No. 7 Squadron cha jeshi la anga ambazo zilikuwa hapo hapo nchini Sierra Leon tangu kipindi cha Oparesheni Palliser ambayo nilieleza mwanzoni, raia wan chi za jumuiya ya madola walivyokuwa wanahamishwa kutoka nchini Sierra Leon kwenda makwao.
KUINGIA NCHINI SIERRA LEON
Katika sehemu iliyopita nilieleza ugumu ambao jeshi lilikuwa linaupata kuingiza makomando nchini Sierra Leon pasipo yeyote kung’amua kutokana na vyombo vya habari kufuatilia kila hatua ambayo jeshi la Uingereza walikuwa wanaichukua na pia ndani ya jeshi kwenyewe kulikuwa na maafisa mabao walikuwa wanavujisha habari kwa vyombo vya habari.
Ili kufanikiwa kwa oparesheni hii ilikuwa ni muhimu sana kwa wapiganaji wa West Side Boys waendelee kuamini kuwa Uingereza ilikuwa bado na nia ya kumaliza mzozo huu kwa mazungumzo. Kwa hiyo ulikuwa unachukuliwa umakini wa kupitiliza kuhakikisha kuwa hakukuwa na yeyote ambaye angeling’amua pindi makomando wa SAS na 1 PARA wangeingizwa nchini Sierra Leon.
Kwa hiyo ambacho Uingereza ilifanya ni kuingiza kikosi fulani cha makomando nchini Senegal na vyombo vyote vya habari walielekeza akili yao katika kufuatilia nyendo za kikosi hiki ambacho kilipelekwa Dakar.
Kutokana na vyombo vyote vya habari kuelekeza akili zao katika kufuatilia nyendo za kikosi hiki cha makomando pale Dakar, hii ilitoa mwanya kwa jeshi la Uingereza kupenyeza kwa siri kikosi cha makomando wa D Squadron ya 22 SAS bila chombo chochote kile cha habari kufahamu. Kwa mtindo huu huu pia jeshi la Uingereza liliingiza makomando wapatao 130 wa A Company katika vikundi vidogo vidogo.
Baada ya vikosi hivi viwili vya makomando kuingia nchini Sierra Leon kwa siri kubwa bila yeyote asiyehusika kufahamu, waliweka kambi katika eneo la Hasting, takribani kilomita 50 kusini mwa mji mkuu wa Freetown.
Wakiwa hapa, maandalizi muhimu ya mwisho mwisho yalifanyika kwa weledi mkubwa zaidi. Nia hapa ambapo walifanya mazoezi ya hatua ya mwisho kwa kutumia risasi halisi. Kwa kuwa tayari walikuwa na jiografia yote ya vijiji vya Mgbeni na Gberi Bana, kwa hiyo hapa hapa walipokuwa wameweka kambi na kufanya amzoezi ya maandalizi… kulitengenezwa vijiji vya kufanana kabisa na vile vya Mgbeni na Gberi Bana pamoja na mpangilio wa nyuma wa kufanana kabisa na jinsi zilivyo kule Mgbeni na Gberi Bana.
Wakiwa hapa Hasting wakifanya mazoezi ndipo ambapo waligundua kuwa walikuwa na changamoto nyingine ambayo hii hawakuwa na uwezo wa kuidhibiti kwa namna yoyote ile. Hali ya hewa.
Hali ya hewa ilikuwa ya joto mno kushinda hali ambayo walikuwa wameizoea nchini Uingereza.
Uzuri ni kwamba walau kidogo makomando wa SAS walikuwa na uwezo wa kuhimili hali yoyote ya hewa kutikana na mafunzo adhimu ya miaka kadhaa wanayopitia na moja ya mambo wanayofundwa ni namna ya kuhimili hali tofauti za hewa. Lakini makomando wa 1 PARA hawana mafunzo makubwa juu ya hili na makamanda wa Oparesheni walikuwa wanahofia wanajeshi wanaweza kuchemka (heat exhaustion) na hivyo kuathiri ufanisi wa oparesheni yote.
Hivyo basi uamuzi wa kwanza ambao makamanda wa oparesheni waliuchukua ni kutoa maagizo kwamba siku ya oparesheni, makomando wa A Company ya 1 PARA watabeba silaha na vichache kuliko ambavyo ilikuwa imepangwa awali. Yaani kwamba watabeba bunduki, risasi za akiba, maji na bandeji chache na dawa za kutibu majeraha. Walichokuwa wanakiona ni kwamba kama makomando wa 1 PARA watabeba begi za vita, silaha nzito na vitu vinginevyo watachoka mapema kuzingatia kiwango cha juu cha joto kilichopo.
Mwanzoni wazo hili liliungwa mkono, lakini baada ya kutafakari sana ulionekana umuhimu wa A Company kubeba kila kitu ambacho kilipangwa awali wawe nacho wakati wa utekelezaji wa oparesheni.
Baada ya kufanya uchunguzi wa kina zaidi kuhusu eneo ambalo wataenda kufanya oparesheni waikja kung’amua kwamba muda wa asubuhi hali ya hew inakuwa na baridi ya kuridhisha sana maeneo yote yanayozunguka mto Rokel ikiwemo vijiji vya Mgbeni na Gberi Bana. Kwa hiyo baada ya makamanda wote kujadiliana kwa kina walikubaliana kuwa badala ya kupunguza silaha na vifaa ambavyo vitabebwa na makomando wa A Company, badala yake oparesheni itekelezwe asubuhi sana mapema muda ambao hali ya hewa inakuwa ni ya kuridhisha zaidi, kwa maana ya kwamba joto linakuwa chini kabisa.
Siku zilipokuwa zinakaribia kwa ajili ya utekelezaji wa oparesheni, Mkurugenzi wa Vikosi vya Jeshi vya Weledi (Director of Special Forces), Brigedia John Holmes aliwasili kwa siri kubwa mjini Freetown akiwa ameambatana na Commanding officer wa 22 SAS, commanding officer wa D Squadron na maafisa watatu wa Jeshi la Anga la Uingereza kitengo za Technical Communications.
DSF, Brigedia John Holmes alifikia nyumba iitwayo Seaview, iliyoko karibu kabisa na makao makuu ya jeshi la Uingereza hapo mjini Freetown.
Tukumbuke kwenye sehemu iliyopita nilieleza kuhusu makomando wanne wa SAS ambao walipenyezwa kwa siri kwa kutumia boti ya SBS kupitia mto Rokel, makomando wawili kila upande wa mto. Makomando hawa muda wote huu mapaka sasa bado walikuwa bado msituni pembezoni mwa vijiji vya Mgbeni na Gberi Bana wakiendelea kufuatilia nyendo zote za wapiganaji wa West Side Boys. Nyendo zote hizi walizokuwa wanazichunguza walikuwa wanawasiliana na wenzao na kuwapa taarifa.
Kwa hiyo DSF, Brigedia John Holmes alipowasili Freetown moja kwa moja akafanya kikao kwa njia ya mawasiliano ya kimtandao kati yake, wale makomando wa SAS msituni, makamanda wa SAS na 1 PARA amabo wanafanya maandalizi kule Hasting pamoja na COBRA. Lengo la kikao hiki ni kufanya tathimini kama kuliwa na utayari na uhalisia wa kutoa ruhusa ya kufanyika kwa oaparesheni.
COBRA ni nini?
Japokuwa kwa uhalisi wake inapswa kuitwa COBR lakini watu wamezoea kuita COBRA. Cabinet Office Briefing Room.
Hii nieleze kwa kifupi sana… kama kutakuwa na ulazima wa kuiandikia basi nitapokea maoni.
Hizi ni sehemu za siri sana ambazo vinafanyika vikao vya siri mno vya kamati mahususi kwa ajili ya kukabiliana na suala fualni la kiusalama la kitaifa au kimataifa dhidi ya nchi ya Uingereza.
Muundo wa kamati inayokutana mahali hapa inategemea na tishio husika la kiusalama… yaani kwamba kamati inayokutana inabadilika kutokana na tishio ambalo Uingereza wanakabilina nalo. Yaani kwamba wahudhuriaji ni wale ambao watakuwa na ‘input’ fulani kuhusu hatua stahiki ambazo zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na suala husika ambalo linakuwa linajadiliwa. Lakini mara zote kikao cha kamati hii kinakuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza au Waziri wa ngazi ya juu muandamizi.
Kwa hiyo ninaposema DSF, Brigedia John Holmes kwenye kikao chake kwa kutumia mawasiliano ya kimtandao pia walikuwepo COBRA hiki ndicho ambachi nina maanisha.
Wakati huo huo…
Timu ya negotiators walikuwa wanaendelea ‘kuwapoteza maboya’ West Side Boys na kuwafanya wajiamini kupitiliza. Labda ni kutokana na matumizi yaliyopitiliza ya mihadarati au labda ni haiba yao tu ya ujivuni na kujiamini kupitiliza… West Side Boys walikuwa wanongeza masharti kila uchwao.
Kwa mfano, siku ya Septemba 9… moja ya viongozi wa West Side Boys liyejiita “Kanali Cambodia” alitoa sharti jipya la kiwendawazimu kabisa safari hii. Alisema kwamba ili waweze kuwaachia wanajeshi 6 wa Uingereza walikuwa wanataka kuundwa kwa serikali mpya ya Sierra Leon ambayo nao watakuwa sehemu ya serikali hiyo.
Kwa namna yoyote ilesharti hili lilikuwa halitekelezeki. Hii ilikuwa inadhihirisha wazi kabisa kwamba hakukuwa na namna ambayo suala hili litaishia mezani kutokana na tabia ya ujivuni na haiba ya kuishi nje ya uhalisia ambayo West Side Boys walikuwa wanaionyesha.
Pia…
Wale makomando wanne wa SAS amabo walikuwa misituni karibu na vijiji Mgbeni na Gberi Bana ambao walikuwa wanafuatilia nyendo za West Side Boys waliripoti kwamba hawajawaona wanajeshi wao 6 waliotekwa kwa muda wa siku nne zilizopita.
Pia walisema kuwa walikuwa wanaona kama vile kuna nyendo zinazoashiria West SIDe Boys walikuwa wanataka kuhama kutoka kwenye vijiji hivyo na kuingia ndani zaidi ya msitu na kama hili litatokea basi wanaweza kuua wanajeshi hao mateka au kuwahamisha sehemu za ndani kabisa ya msitu ambako itakuwa vigumu zaidi kufanya uokozi.
Baada ya taarifa zote hizi mbili… ilikuwa dhahiri kwamba oparesheni ilikuwa inatakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo.
COBRA wakamshinikiza Waziri mkuu wa kipindi hicho, Tony Blair kuhusu umuhimu wa Oparesheni hiyo kufanyika haraka iwezekanavyo na Tony Blair akatoa kibali kwa oparesheni kufanyika.
DSF, Brigedia John Holmes pia alifanya mazungumzo na Rais wa Sierra Leon Ahmad Kabbah na kupata kibali kutoka kwake juu ya opareshini hiyo. Kisha kwa kushirikiana na Army Legal Corps akafanya mazungumzo na viongozi wa juu wa jeshi la Sierra Leon na kupewa Baraka zao.
Baada ya oparesheni kupata ‘go ahead’ kutoka kila sehemu stahiki, Luteni Kanali Fordham yule ambaye alikuwa anaongoza timu ya negotiators alimpigia simu kiongozi wa West Side Boys, ‘Brigedia’ Foday Kallay na kumueleza kuwa wako tayari kutekeleza masharti yao lakini kabla ya kufanya hivyo alikuwa anataka uhakika kama wanajeshi wao wote sita wako hai.
Foday bila kuelewa mtego ambao alikuwa amewekewa… akaweka kwenye simu wanajeshi wote sita wanaowashikilia mateka wakamsalimia Luteni Kanali Fordham mmoja mmoja.
Wasiwasi walioupata baa ya makomando wa SAS walioko kule msituni kutowaona wanajeshi wao waliotekwa kwa siku nne na kudhani labda wameshauwawa ulikuwa umesawazishwa. Watu wao walikuwa hai… lakini hawatakuwa hai kwa muda mrefu kama hawatafanya kitu upesi…
DSF, Brigedia John Holmes akatoa idhini ya mwisho kwa vikopsi vya 22 SAS na A company ya 1 PARA… kwamba siku ya tarehe 10 alfajiri sana kabla hata jua kuonesha dalili ya kuchomoza wanapswa kutekeleza oparesheni.
Kwenye medani ya vita wanasema… ”MISSION IS A GO!!”
Kijijini Mgbeni
Chinook ya tatu iliruka moja kwa moja mpaka kijijini Mgbeni ikiwa imebeba nusu ya makomando wa A Company ya 1 PARA.
Helikopta ilitua nje kidogo ya kijiji mahala ambapo palipendekezwa na ile Observation Team ya SAS.
Katika mapendekezo yao kuhusu hii ‘landing zote’ walieleza kwamba sehemu hii licha ya kiwa ndio bora zaidi kwa ajili ya kutua lakini ina hali fulani hivi kama vile matope matope.
Kwa bahati mbaya sana walikuwa wameshindwa kukadiria ni kiasi gani cha matope kilikuwa katika eneo hili. Hii ilisababisha baada ya makomando wa A Company kushuka sehemu hii kwa mtindo ule ule wa ‘fast roping’ kujikuta wako ndani ya tope linalofika karibia na kifua na kuwafanya washindwe kuondoka kwa haraka kutoka eneo hili.
Idadi kubwa ya makomando walijivuta na kutoka ndani ya tope na kuanza kuelekea kijijini, lakini makomando wachache ambao walipewa jukumu la kulinda eneo hili la kutua iliwalazimu wabakie ndani ya tope.
Chinook ilipokuwa inarejea mara ya pili ili kuleta nusu ya pili ya makomando wa ACompany ilishitukizwa kwa kushambuliwa kwa risasi mfululizo kutoka kwa wapiganaji wa West Side Boys. Ili lazimu helicopter nyungine Lynx Attack Helikopta ipite kijijini Mgbeni kufanya ‘strafing’ kama ambavyo ilifanywa kule Gberi Bana.
Strafing ilifanyika mpaka walipohakikisha kuwa hakukuwa na mfululizo wowote wa risasi kutoka kwa wapiganajivwa West Side Boys ndipo ambapo Chinook ilirudi tena sehemu ile yenye tope na kushusha nusu ya pili ya makomando.
Baada ya nusu hii ya pili kutua ardhini kwa mtindo ule ule wa fast roping na kuungana na nusu ile ya kwanza moja kwa moja kwa haraka wakaanza kuingia kijijini Mgbeni.
Bahati mbaya nyingine ikatokea. Kuna mfululizo wa mabomu yalikuwa yanarushwa kutoka kwenye helicopter ile ambayo ilikuwa inafanya ‘strafing’ mara ya kwanza, safari hii ikifanya hivyo ili kuzuia wapiganaji wa West Side Boys wasitoe upinzani mkubwa kwa makomando wa A Company. Bahati mbaya sana moja ya mabomu ambayo yalikuwa yanaelekezwa upande wa Were Side Boys lilitua karibu kabisa na makomando wa A Company waliokuwa wanaingia kijijini Mgbeni kwa kasi na kusababisha makomando saba kujeruhiwa akiwepo Mathews Lowe, kamanda wao.
Tukumbuke kuwa kule kijijini Gberi Bana ambako makomando wa SAS walikuwa wametua muda mchache nyuma nako kulikuwa na majeruhi, komando Bradley Tinnions alikiwa amedunguliwa mara tu baada ya kutua ardhini kutoka kwenye Chinook.
Kwa kulikuwa na Chinook nyingine ambayo ilikuwa inarandaranda mahususi kabisa kwa ajili ya kutua muda wowote kuchukua mateka kama wakifanikiwa kuokolewa.
Ilibidi wawasiliane na hii Chinook ili iweze kutua na kuchukua majeruhi haraka ili oparesheni iweze kuendelea.
Baada ya majeruhi kuondolewa, akiwemo kamanda wao Matthew Lowe, oparesheni kijijini Mgbeni iliendelea ikiwa chini ya komando Danny Matthews ambaye ndiye walikuwa 2IC (Second In Command).
Baada ya majeruhi kuondolewa, 2IC Matthews aliwagawanya makomando wote katika platoons ambazo kila moja walikuwa na jukumu la kushambulia jengo mahususi kama ambavyo walikuwa wamefanya mazoezi kwenye kijiji walichokitengeneza Hastings kufanana kabisa na hiki cha Mgbeni.
Ndani ya dakika chache walifanikiwa kuliteka jengo la silaha la wapiganaji wa West Side Boys. Baada ya hapo kila platoon iliendelea kushambulia jengo lao mahususi ambapo walikuwa wamepangiwa.
Kila mpiganaji wa West Side Boys ambaye alijisalimisha aliwekwa chini ya ulinzi na kufungwa kamba. Wale wote ambao walileta upinzani au kutaka kupambana walitandikwa risasi bila huruma.
Baada ya kuhakikisha kuwa ‘wamesafisha’ majengo yote na hakuna tishio, makomando wachache walielekea kwenye msitu wa karibu kuwasaka wapiganaji ambao walikuwa wamekimbilia huko.
Wale waliosalia hapa walikaa katika mtindo ambao walikuwa kana kwamba wamezunguka kijiji chote ili kujihami na shambulio lolote kutoka nje.
Baada ya kukamata na kuua wapiganaji wote wa West Side Boys ambao walikiwa wamejificha msituni, makomando wa A Company walipanda ‘viazi’ (mabomu ya ardhini) kuzunguka eneo lote la kuingilia kijijini hapo.
Mpaka kufika majira ya saa mbili asubuhi, A Company walikuwa wameikiweka kijiji cha Mbeni mikononi mwao na kilikuwa salama.
Majira haya ya saa mbili asubuhi walianza hatua ya pili ya oparesheni yao.
Kwanza walichoma moto majengo yote na kuharibi silaha zote za West Side Boys pamoja na magari yao.
Tukumbuke kuwa siku ile ambapo wale wanajeshi wa Uingereza walitekwa, walitekwa pamoja na gari zao Land Rover za kijeshi (tazama Picha). A Company walipewa jukumu la kuhalikisha kuwa gari hizi nazo zinaokolewa na kurejeshwa kwenye jeshi la uingereza.
Kwa hiyo land rover hizi, zilifungwa kwamba katika mtindo maalumu na kisha ikapigwa simu zije kubebwa na Chinook (tazama Picha).
Baada ya zoezi lote kijijini Mgbeni kukamilika, makomando wa mwisho waliondoka hapo mnamo majira ya saa nane mchana.
Kijijini Gberi Bana
Makomando wa SAS walifanikiwa kumpandisha kwenye Chinook mwenzao Bradley Tinnions salama kabisa bila na moja kwa moja akapelekwa kwenye meli ya kijeshi iliyoko katika pwani ya afrika magharibi.
Tofauti na matarajio, makomando wa SAS walipoanza tu kushambulia kijiji cha Gberi Bana wapiganaji wengi wa West Side Boys walijisalimisha akiwemo kiongozi wao Foday Kallay.
Mara moja wakati wakomando wachache wakiwaweka chini ya ulinzi wapiganaji walijisalimisha na kuwafunga kamba na huku wakiwatandika risasi wale ambao walikuwa wanajaribu kukimbilia msituni, makomando wengine kwa haraka walielekea kwenye jengo ambalo mateka wanajeshi wa Uingereza walikuwa wanashikiliwa na kuwaondoa mara moja.
Luteni Musa Bangura alikuwa amewekwa mahala pengine peke yake. Walimkuta amefunikwa kwenye shimo ambalo lilikuwa linatumiwa na West Side Boys kumwaga mikojo na kinyesi.
Alikuwa amedhoofu afya yake kupitiliza na alikuwa ana majeraha mwili mzima kutokana na baadae kubainika kuwa West Side Boys walikuwa na desturi ya kumtoa shimoni na kumpa mateso kila baada ya siku kadhaa.
Mara moja Chinook iliwasili kuwachukua wale wanajeshi sita waliotekwa pamoja na luteni Bangura na kupelekwa kwenye hospitali ya dharura ya kijeshi iliyoko kwenye meli ya kijeshi bahari ya afrika magharibi.
Wale mateka raia wa Sierra Leon nao pia waliokolewa lakini wao jeshi walitumia tahadhari ya ziada katika kuwaokoa. Makomando wa SAS walikuwa wanahisi labda kulikuwa na uwezekano wa baadhi ya wapiganaji wa West Side Boys kujichanganya na raia mateka ili kujinusuru wasiuwawe. Kwa hiyo raia wote ambao walikuwa hapa kijiji cha Gberi Bana nao walifungwa kamba mikononi na kuwekwa chini ya ulinzi mkali na kusafirishwa kwa Chinook mpaka kwenye kambi ya wanajeshi wa nchi ya Jordna waliomo nchini humu kama sehemu ya majeshi ya umoja wa Mataifa kulinda amani mchini Sierra Leon (UNAMSIL).
Lengo la kuwapeleka hapa ni kuwafanyia mahojiano ya kina mmoja mmoja ili kuhakikisha kuwa hakuna wapiganaji wa West Side Boys ambao walikuwa wamejichanganya humu.
Baada ya hapa, makomando wa SAS walifanya kama kile ambacho kilifanywa kule kijijini Mgbeni na A Company. Walifanya msako msituni na kukamata wapiganaji wote wa West Side Boys ambao walikuwa wamekimbilia huko. Walijisalimisha walifungwa kamba mikononi na kurudishwa kijijini, na wale ambao walileta upinzani walitandikwa risasi.
Kisha wapiganaji wote wa West Side Boys nao wakasafirishwa kwa Chinook wakiwa chini ya ulinzi mkali kutoka hapa Kijijini Gberi Bana mpaka kambi ya UNAMSIL ya wanajeshi wa Jordan.