Ni vizuri kutafuta suluhisho la kufikirisha juu ya hili suala kubwa. Lakini ni muhimu sana kufahamu vizuri "machinga" ni nani hasa.
Kiuhalisia hawa "machinga" ni watu wanaotaka uhuru mkubwa sana wa kufanya biashara nje ya mifumo na taratibu zilizowekwa kisheria. Ni sekta isiyo rasmi kweli kweli. Wahusika wanataka waingie na kutoka katika biashara hiyo bila taratibu wala vibali rasmi, wafanye biashara popote panapopitika na wakati wowote bila udhibiti (kandokando ya barabara, katikati ya magari barbarani, katika njia za waenda kwa miguu, pembeni ya majengo, mbele ya maduka, nje ya masoko rasmi, n.k.). Wengi ni wahamaji hamaji (hawkers). Wanafuata penye wateja wengi kutegemeana na wakati wa siku. Wakizigundua hizo "hot spots", watajazana kama kama nzige hadi kumiminikia pasipostahili (barabarani, kwenye mifereji ya maji machafu na kuziba vituo vya mabasi na njia za waenda kwa miguu).
Sasa hii lugha ya kutafutiwa maeneo ya mazuri ya biashara kwa wamachinga haina maana. Hawawezi kuelewa wala kukubali. Hawako tayari kukalishwa sehemu moja muda mrefu huku wanasikia biashara imechanganya mahali kwingine. Na kwa vile wanaishi kwa kauli ya serikali iliyowaruhusu kufanya biashara bila kubughdhiwa na wameshaambiwa wao ni muhimu sana kama wapiga kura (fallacy), basi hawako tayari kuambiwa wasichotaka. Wako tayari kwa mapambano.