Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, David Jumbe, anasimulia kwa kina matukio yaliyomkuta kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, akidai kuwa alipokea vitisho, alifuatwa nyumbani na baadaye kutekwa na watu aliowatuhumu kuwa maafisa wa vyombo vya usalama.
Katika mahojiano haya, Jumbe anaeleza jinsi alivyolazimika kujificha baada ya kupewa taarifa kwamba angepotezwa ndani ya siku tatu, safari yake ya kwenda Kenya, kurejea Tanzania kwa muda mfupi na tukio la Mei 20, 2026 ambalo anasema alitekwa akiwa karibu na nyumbani kwake.
Swali: Kabla ya kufika kwenye tukio la kutekwa, hebu turudi nyuma kidogo. Nini kilitokea kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, 2025?
Jibu: Kuelekea uchaguzi kulikuwa na kamata kamata kubwa ya viongozi na wanachama wa CHADEMA katika maeneo mbalimbali nchini. Watu wengi walikuwa wamejificha kwa sababu hali haikuwa shwari.
Kwa mujibu wa rekodi za chama, kuanzia Oktoba 1 hadi 25, kulikuwa na zaidi ya watu 50 ambao walikuwa viongozi au wanachama wa CHADEMA waliokuwa wameripotiwa kutekwa au kukamatwa na baadhi yao kujulikana walikuwa vituo vya polisi.
Mimi nilikuwa bado nchini. Nilimtembelea Mwenyekiti, Tundu Lissu, gerezani na nikamweleza hali ilivyokuwa. Nilimwambia kwamba viongozi na wanachama wetu walikuwa wanakamatwa sana, wengine wamelazimika kujificha na wengine wamekimbia nchi.
Lissu aliniambia jambo la msingi ni watu kuhakikisha usalama wao. Alisema mapambano tunayafanya tukiwa salama. Kwa hiyo kama usalama wa mtu hauko vizuri, ni bora achukue hatua.
Soma pia: David Djumbe (Msaidizi wa Lissu) atekwa
Mimi niliamua kubaki nchini kwa sababu nilifikiri tukitoka wote na kukimbia wote, inaweza kukatisha tamaa watu wanaoendelea na harakati.
Swali: Baada ya uchaguzi kupita, nini kilitokea?
Jibu: Baada ya uchaguzi na matukio yaliyotokea, watu wengi zaidi walianza kukamatwa, wengine kutekwa na kupotezwa. Kwa hiyo watu wakaanza kutafuta sehemu salama zaidi.
Mimi sikuondoka nchini mpaka mwisho wa Novemba. Novemba 27, 2025 nilipigiwa simu na mtu ambaye simfahamu. Aliniambia ana taarifa ambazo si nzuri kwangu.
Aliniambia watu waliokuwa wakiteka watu walikuwa wananitafuta na kwamba watanipoteza ndani ya siku tatu. Alisema sitamaliza siku tatu.
Alinieleza pia kwamba sikuwa na kesi yoyote iliyokuwa imefunguliwa dhidi yangu. Alisema wanaonitafuta walikuwa wanataka kunifrustrate Mwenyekiti akiwa gerezani na walikuwa wakiamini kwamba kuna mambo ya Tundu Lissu ninayajua ambayo wanataka kuyapata.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wangekamata, kunitesa ili nitoe taarifa hizo, halafu waniue.
Swali: Ulipokea taarifa hiyo kupitia simu ya kawaida au WhatsApp?
Jibu: Ilikuwa simu ya kawaida. Mtu huyo aliniambia ameshanipa taarifa na jukumu langu lilikuwa kuchukua hatua. Alinishauri niondoke.
Niliporudi nyumbani nilimweleza mke wangu. Nilimwambia nimepewa taarifa hiyo na mtu ambaye simjui, lakini siwezi kuipuuza kwa sababu tayari nilikuwa nimeona dalili za kutafutwa.
Swali: Usiku huo kulikuwa na tukio lolote?
Jibu: Usiku wa kuamkia Novemba 28, alarm ya usalama nyumbani kwangu ilitrigger. Mimi na mke wangu tukaamka. Tayari tulikuwa na hofu kwa sababu tulikuwa tumeambiwa inaweza kuwa muda wowote.
Nilitoka chumbani nikiwa nimechukua panga kwa sababu nilikuwa nimejiambia kama watu watakuja kuniteka nyumbani, nitapambana nao.
Nilipochungulia nje nikaona gari limepaki mbele kidogo ya nyumba yangu, taa zikiwa zinawaka. Baada ya muda mfupi watu wakaingia kwenye gari na kuondoka.
Nilihisi kwamba huenda hao ndio waliokuwa wamesababisha alarm. Siku hiyo sikulala tena.
Asubuhi nikaondoka nyumbani pamoja na mke wangu na watoto, tukaenda Bagamoyo.
Swali: Uliwapa taarifa polisi?
Jibu: Sikutoa taarifa polisi wakati huo. Niliwajulisha watu wachache wa karibu. Kulikuwa na askari mmoja wa kituo jirani ambaye nilizungumza naye baadaye.
Nilikuwa nimeamua kujificha zaidi na kujiandaa kuondoka nchini.
Lakini nilipokuwa Bagamoyo, mke wangu alipokwenda kwenye shughuli ya familia, nilipokea ujumbe kutoka kwa mpwa wangu aliyekuwa nyumbani.
Aliniambia kuna watu wamekuja nyumbani wanatafuta mimi. Alisema walikuwa watano na kuna mwingine kwenye gari, na walikuwa na silaha. Walijitambulisha kuwa polisi.
Swali: Walijitambulisha kuwa polisi wa wapi?
Jibu: Mke wangu alipofika nyumbani aliwakuta. Walimwambia wanamtafuta mume wake. Baadaye nilizungumza na mmoja wao kwa simu ya WhatsApp.
Alisema yeye ni polisi kutoka Oysterbay na wametumwa na ZCO kunifuata. Nilimuuliza nina tuhuma gani. Akasema wao hawajui, wameagizwa tu na ZCO na nikifika Oysterbay nitaelezwa.
Nilimuuliza pia kwa nini watu kutoka Oysterbay, Dar es Salaam, wanakuja kunikamata katika eneo la Vikawe, Kibaha, Mkoa wa Pwani, wakati Mkoa wa Pwani una vyombo vyake vya polisi. Hakunipa jibu la swali hilo.
Niliwaambia nitarudi mwenyewe. Wakakubaliana kuondoka na kumwambia mke wangu kuhakikisha nikirudi niende Oysterbay.
Mimi nikaunganisha taarifa nilizokuwa nimepewa kuhusu watu waliokuwa wakitafuta viongozi na wanachama wa CHADEMA na nikaona kwamba huenda hawa ndio wale waliokuwa wananitafuta.
Swali: Baada ya hapo ulifanya nini?
Jibu: Niliona siko salama. Rafiki yangu akaja akachukua watoto na kunichukulia begi. Siku hiyo hiyo nilianza kujificha rasmi na baadaye nikavuka mpaka na kwenda Kenya.
Swali: Ulikaa Kenya kwa muda gani?
Jibu: Takribani miezi sita. Baadaye nilirudi Tanzania kwa muda mfupi kwa sababu ya suala la biashara lililohitaji nifanye kazi halafu niondoke.
Nilifika nyumbani Mei 18. Tarehe 19 nilikuwa bado najificha. Mei 20ndipo tukio la kutekwa lilipotokea.
Swali: Uliporudi Tanzania, ulifanya nini kuhakikisha watu hawajui umefika?
Jibu: Nilijificha. Sikuenda kwenye shughuli za umma. Simu zangu zilikuwa karibu zimezimwa na nilikuwa nawasiliana na watu wachache sana.
Mmoja wa watu niliowasiliana naye alikuwa Allan Macha. Nilikuwa na gari langu lililokuwa limeharibika na yeye alikuwa analisimamia gereji.
Nilimwambia kesho twende gereji pamoja. Asubuhi akanipitia kwa gari yake yenye tinted windows.
Tukaenda gereji na kukaa huko kwa muda. Baadaye nikaenda kukutana na rafiki mwingine wa biashara maeneo ya Ununio.
Tulikuwa tunatafuta sehemu yenye faragha zaidi kwa sababu magari yalikuwa yanaongezeka eneo tulilokuwa tumekaa.
Baadaye mimi na Allan tukaanza kurudi nyumbani.
Swali: Nini kilitokea mlipokaribia nyumbani?
Jibu: Tulipokuwa tumebakiza takribani mita 300 kufika nyumbani, Allan aliniambia kuna magari yanakuja kwa kasi nyuma yetu.
Nikaangalia kwenye side mirror na nikaona kweli magari yanakuja kwa kasi. Nilijaribu kumpisha mmoja apite kwa sababu barabara ilikuwa nyembamba.
Gari hiyo ilipopita mbele yetu, ghafla ikatublock. Nilipojaribu kurudi nyuma, nikakuta kuna kitu pia kimezuia nyuma.
Swali: Ilikuwa gari gani?
Jibu: Ilikuwa Toyota Probox nyeusi. Hiyo ndiyo niliyoiona vizuri ikiwa mbele yetu.
Walishuka watu kwa kasi na kuja kwenye gari yetu. Walianza kufungua milango na kujaribu kututoa.
Mimi na Allan tukaanza kupambana nao na kupiga kelele kwamba ni watekaji. Nilikuwa pia nawauliza kama ni polisi, kwa nini wanakamata kwa namna hiyo.
Watu wakaanza kusogea eneo lile. Bodaboda wawili walikuja karibu.
Swali: Walifanikiwa kukuchukua?
Jibu: Ndiyo. Walinivuta kwa nguvu, wakanishika miguuni na sehemu nyingine za mwili, wakaniwekea pingu na kunipeleka kwenye gari.
Wakanirusha kwenye buti ya gari. Mmoja wao akaniambia nimejifanya mjanja sana na nimekuwa nikirukaruka muda mrefu, lakini sasa wamenikamata na huo ndio mwisho wangu.
Baada ya gari kuanza kuondoka, alianza kunipiga kwa kitako cha bunduki. Alinipiga kwenye miguu, mapaja, mbavu na baadaye kichwani.
Swali: Ulipokuwa ndani ya gari ulikuwa unafikiria nini?
Jibu: Nilikuwa nimefungwa pingu na nimewekwa kwenye buti. Aliponiambia leo ndio mwisho wangu, nilianza kufikiria watu wengine waliokuwa wamepotea.
Nilimkumbuka Ali Kibao, Mdude, Soka na Kipanya, watu ambao nilikuwa nikiwasiliana nao na baadaye walipotea.
Nikajiuliza kama kweli leo ndio mwisho wangu.
Ndani yangu nikapata jibu kwamba hapana, leo sio mwisho wangu. Nilianza kusema kwa sauti, “No! Leo sio mwisho wangu.”
Nilipokuwa nasema hivyo, yule mtu akaendelea kunipiga.
Swali: Kuna wakati uliona matumaini ya kuokoka?
Jibu: Ndiyo. Tulipokuwa tunaelekea barabara kuu, nilisikia mmoja wao akisema kuna bodaboda wanawafuata.
Hilo lilinipa matumaini kwa sababu nilifikiri kama kuna watu wanafuatilia gari, labda nitapata nafasi ya kutoroka.
Wakaendelea kuzungumza kuhusu bodaboda. Walikuwa wakisema wanaongezeka.
Baadaye mmoja wao akamwamuru dereva aendeshe kwa kasi ili kuwapoteza bodaboda.
Swali: Bodaboda waliendelea kuwafuata?
Jibu: Ndiyo. Walikuwa wanaendelea kuongezeka. Baadaye nilisikia amri ya kupiga risasi ili kuwatawanya.
Safari iliendelea na baada ya muda yule aliyekuwa akionekana kama kiongozi wao akaamuru gari lisimame. Akasema hawawezi kuruhusu bodaboda waendelee kuwafuata na wakaamuru washuke na kuwatawanya kwa risasi.
Swali: Hapo ndipo ulipopata nafasi ya kutoroka?
Jibu: Ndiyo. Baada ya kushuka, niligundua tuko Mbweni. Nilitambua eneo kwa sababu nilishawahi kufanya kazi huko mwaka 2017 wakati wa uchaguzi mdogo wa Kata ya Mbweni.
Niliona msitu upande wa kushoto na kulia na nikatambua eneo la usalama.
Wakati wale watu walipokuwa nje ya gari wakipiga risasi kuelekea upande wa bodaboda, niliona hiyo kama nafasi yangu.
Nilijirusha kutoka kwenye buti, nikafungua mlango wa gari na kujiviringisha kuingia msituni.
Swali: Waligundua umeponyoka?
Jibu: Baadaye waligundua. Nilikuwa nimeingia kwenye msitu mnene sana na nilikuwa natambaa kwa sababu huwezi kutembea vizuri ukiwa umesimama.
Nilikuwa sina viatu. Vilitoka wakati wa mapambano.
Nilikuwa bado nimefungwa pingu. Suruali yangu ikanaswa kwenye miiba. Kwa sababu nilikuwa nimefungwa pingu, sikuweza kujinasua vizuri.
Hatimaye nilitoa mkanda, nikavua suruali na kuiacha kwenye miiba. Nikaendelea kutambaa nikiwa nimebaki na boxer.
Soma pia: Msaidizi wa Lissu apatikana baada ya kudaiwa kutekwa akiwa na pingu mkononi pamoja na majeraha
Swali: Ulikaa msituni kwa muda gani?
Jibu: Takribani saa mbili.
Nilikuwa naendelea kusogea huku nyuma nikisikia risasi. Baadaye nikasikia risasi zikielekezwa upande wa msitu na nikahisi wamegundua sipo tena kwenye gari.
Nikaendelea kusogea mpaka nikatokea upande mwingine.
Swali: Baada ya kutoka msituni uliomba msaada wapi?
Jibu: Nilifika eneo lenye nyumba nyingi. Nilifahamu baadhi ya nyumba hizo zilikuwa za watu wenye nafasi kubwa serikalini na watu wa usalama.
Sikutaka kugonga nyumba yoyote kwa sababu niliogopa huenda nikakutana na watu wale wale waliokuwa wananifuatilia.
Niliendelea kutembea mpaka nikafika barabarani na kuona jengo lenye mlinzi.
Nilimkimbilia mlinzi huyo na kumuomba msaada.
Nilikuwa sina viatu, sina suruali, mwili umejaa damu, nimefungwa pingu na kichwani kulikuwa na miiba.
Alitaka kupiga filimbi kwa sababu alishtuka kuniona.
Nilimwambia mimi si mhalifu, nimetekwa na nimetoka kutoroka. Nilimtaja jina langu, David Jumbe, na nikamwambia mimi ni msaidizi wa Tundu Lissu.
Aliposikia jina la Lissu alionekana kunifahamu.
Swali: Mlinzi huyo alikusaidiaje?
Jibu: Kwanza nilimuomba anifungulie pingu. Aliziangalia na kusema pingu hizo si za kawaida.
Alisema si kama zile pingu za polisi ambazo sehemu ya ufunguo inaonekana. Hizi sehemu ya kufungulia ilikuwa haionekani na hivyo ingekuwa vigumu kuzifungua.
Kwa hiyo nikamwambia anisaidie kupiga simu kwa familia yangu.
Akapiga simu kwa mke wangu kwa kutumia simu yake. Nikamwambia nimeokoka na niko Mbweni.
Nikawatumia location. Baada ya takribani dakika 20 na kitu, familia yangu ilifika na kunichukua.
Swali: Kuna taarifa kwamba gari mlilokuwa nalo lilipelekwa Polisi Mbweni. Hilo ni kweli?
Jibu: Ni kweli. Allan aliweza kutoroka na akawasiliana na bodaboda waliokuwa wakitufuata.
Alitoa taarifa kwamba mimi bado nilikuwa kwenye gari na ametekwa, huku yeye akiwa ameweza kutoroka.
Baadaye gari moja liliachwa na polisi wakaichukua na kuipeleka kituo cha Polisi Mbweni.
Allan alienda kuitambua siku iliyofuata. Alikuta laptop yake ndani na pia kiatu changu kimoja.
Kiatu kingine kilipatikana eneo la tukio na kikapelekwa kwa mke wangu.
Swali: Gari hilo lilirudishwa?
Jibu: Kwa maelezo yangu wakati wa mahojiano haya, bado lilikuwa mikononi mwa polisi. Allan alijaribu kulifuatilia kwa wiki nzima lakini alikuwa akiambiwa asubiri.
Pia hakukuwa na faili la kesi nililoelezwa, hakuna mpelelezi aliyewasiliana nami na sijawahi kupewa maelezo kuhusu kinachoendelea.
Hilo ndilo lililonifanya niendelee kuamini kwamba tukio lile lilifanywa na maafisa wa vyombo vya usalama vya Serikali ya Tanzania.
Swali: Polisi walielezaje suala la pingu?
Jibu: Kabla sijawa hadharani kwamba nimefanikiwa kutoroka, polisi walienda kwenye ofisi za chama.
Walisema nimekimbia na pingu. Amani Golugwa (Naibu Katibu mkuu) aliwauliza kama CHADEMA tunajua nimetekwa, wao wamejuaje kwamba nilikuwa nimefungwa pingu na nilitoroka nazo?
Baadaye walifanya mawasiliano na Mambosasa na ikaelezwa kwamba pingu hizo zilipaswa kupelekwa Oysterbay ili nifunguliwe.
Golugwa akauliza: kama polisi hawahusiki na tukio, wamejuaje aina ya pingu nilizofungwa?
Baada ya hapo polisi wakatoa taarifa kwamba hawahusiki na tukio la kutekwa kwangu na kwamba uchunguzi ungeendelea.
Swali: Uliamua kwenda Oysterbay?
Jibu: Pingu zilikuwa zimeniumiza sana. Mikono ilikuwa imevimba na ilikuwa inauma. Nilikuwa nimejaribu kuzifungua kwa njia mbalimbali na hata kutumia grinder lakini haikufanikiwa.
Kwa hiyo sikuwa na option nyingine. Nikaenda Oysterbay. Kulikuwa na vyombo vya habari mbalimbali. Baada ya muda walileta ufunguo na wakafungua zile pingu kwa ufunguo.
Hapo ndipo nilipojiuliza: kama pingu hizo si za polisi, funguo walizipata wapi?
Baada ya kufunguliwa, niliandika maelezo yangu kwa kina, takribani kurasa tisa. Nilipewa PF3 na kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
Lakini sikuambiwa kwamba nina tuhuma yoyote katika kituo cha Oysterbay.
Swali: Baada ya kutoka Oysterbay uliendelea kuishi Tanzania?
Soma pia: Polisi: David Djumbe amepatikana, tunachunguza waliomkamata Bunju
Jibu: Nilikaa nyumbani takribani wiki moja. Wakati huo ndugu na majirani walikuwa wengi nyumbani kwangu, hivyo niliona niko salama.
Lakini kadiri muda ulivyopita, polisi hawakutoa taarifa yoyote na gari liliendelea kushikiliwa.
Mtu mmoja alikuja kuniambia, “Usijiamini. Ondoka, hapa sio salama.”
Baadaye nikaondoka na kurudi Kenya.
Swali: Unaishi Kenya kama mkimbizi?
Jibu: Hapana, sijajiandikisha kama mkimbizi.
Ninaishi kwa kujitegemea. Najua tu kwamba nikiwa Kenya ninaona ni salama zaidi kuliko Tanzania. Lakini hata Kenya sina uhuru wa asilimia 100 kwa sababu nimeona matukio ya watu kutekwa hapa pia.
Kwa hiyo bado siko huru kabisa. Naangalia kama mambo yatabadilika ili nirudi. Kama hayatabadilika, nitaendelea kujificha.
Swali: Familia yako imepata vitisho?
Jibu: Hawajapata vitisho vya moja kwa moja. Lakini unaweza kuhisi kwamba hawako salama kiasi gani.
Hawawezi kuwa huru kama zamani. Hata wao wanaishi kwa tahadhari.
Swali: Hebu tuzungumzie uhusiano wako na Tundu Lissu. Ulikuwa unafanya kazi gani kama msaidizi wake?
Swali: Kwanza Lissu ni rafiki yangu. Tumefahamiana tangu mwaka 2012. Sio ndugu yangu, ingawa tunatoka kabila moja.
Nilijiunga CHADEMA mwaka 2012 na nilianza mchakato wa kuandaa jimbo la Singida Kaskazini kwa uchaguzi wa 2015. Wakati huo Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki.
Nilikuwa na biashara ya vifaa vya kompyuta Dar es Salaam. Nilisaidia ofisi ya CHADEMA Singida kwa kuwapelekea kompyuta, printer na scanner.
Viongozi wa chama walimwomba Lissu aje kupokea vifaa hivyo. Hapo ndipo nilipokutana naye kwa mara ya kwanza.
Baada ya hapo tukawa marafiki. Wakati mwingine nilipokuwa Dodoma nilikuwa nalala kwake. Tulikuwa tunawasiliana mara kwa mara.
Wakati wa uchaguzi wa 2015, niligombea Singida Kaskazini na Lissu alikuwa akigombea tena Singida Mashariki. Pamoja na kuwa alikuwa na majukumu yake, alikuja kunisaidia kampeni.
Swali: Ulianza lini kuwa msaidizi wake rasmi?
Jibu: Majukumu yangu yaliongezeka baadaye, hasa wakati wa maandalizi ya kurejea kwake nchini.
Nilianza kuratibu usalama wake. Niliandaa timu ya walinzi takribani vijana 10 ambao tulikuwa tunawabadilishana kulingana na ratiba.
Niliratibu pia shughuli zake mbalimbali. Aliporudi nchini na kuanza mchakato wa kugombea urais, niliratibu shughuli zake za usalama na shughuli nyingine za kisiasa na kisheria.
Swali: Ulikuwa na jukumu gani wakati wa mchakato wa uteuzi wa mgombea urais?
Jibu: Nilikuwa naratibu shughuli zake zote. Niliongoza msafara, niliratibu usalama wake na shughuli za kujaza fomu na kutafuta wadhamini.
Siku ya mwisho ya kuwasilisha fomu Tume Dodoma, mimi ndiye niliyeenda kuziwasilisha na kushirikiana na maafisa wa Tume kuzihakiki.
Viongozi wengine walikuwa chini. Mimi nilikuwa na maafisa 15 wa Tume tukifanya uhakiki wa majina mpaka karibu saa mbili usiku.
Baada ya Lissu kupitishwa kuwa mgombea rasmi, tuliingia kwenye kampeni. Mimi nilibaki kuwa msaidizi wake na nilikuwa ninasimamia protokali ya kampeni, huku Amani Golugwa akiwa meneja wa kampeni.
Swali: Kwa nini unaamini kazi yako inaweza kuwa sababu ya wewe kulengwa?
Swali: Kwa sababu muda wote Lissu akiwa nchini nilikuwa karibu naye.
Watu waliotaka kumwona au kuwasiliana naye mara nyingi walipitia kwangu. Nilijua ratiba zake na baadhi ya mawasiliano yalipitia kwenye simu yangu.
Kwa hiyo mtu anayekuwa karibu na kiongozi kama Lissu anaweza kuonekana kama daraja.
Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu mipango yake, watu anaokutana nao au mawasiliano yake, wanaweza kudhani msaidizi wake anajua.
Ndiyo maana naamini wale watu waliokuwa wakinitafuta waliona kwamba nikiteswa au nikikamatwa, wanaweza kupata taarifa wanazotaka kuhusu Lissu.
Swali: Kabla ya kuingia kwenye siasa za vyama, ulikuwa pia katika harakati za wanafunzi. Unaweza kueleza historia hiyo?
Jibu: Nilikuwa na historia ya harakati za mabadiliko tangu nikiwa chuoni.
Nilifanya utafiti kuhusu mifumo ya elimu ya juu katika nchi zinazotuzunguka, ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Niliona Tanzania ilikuwa na changamoto katika mfumo huo.
Nilikuwa mwanafunzi DIT na nilianzisha harakati za kudai mabadiliko kwenye mfumo wa elimu ya juu. Pia nilifungua kesi Mahakama Kuu kuhusu utekelezaji wa sheria zinazohusu vyuo vya elimu ya juu.
Baadaye nilianzisha TAHLISO ili kupata nguvu ya kuzungumza kwa niaba ya vyuo mbalimbali.
Wakati huo niliongoza pia harakati za wanafunzi kupinga mitihani ambayo tuliona haikuwa kwa mujibu wa sheria.
Tuligoma na tukafukuzwa chuoni. Lakini tuliendelea na harakati na hatimaye tukadai tupewe vyeti vyetu.
Swali: Uliwahi kuongoza maandamano makubwa ya wanafunzi?
Jibu: Ndiyo. Nikiwa mwenyekiti wa TAHLISO niliratibu maandamano makubwa yaliyofanyika Jangwani mwaka 2004 kuhusu mabadiliko katika bodi ya mikopo.
Nafikiri mpaka leo hayajawahi kutokea maandamano makubwa ya wanafunzi kama yale.
Hizo ndizo harakati nilizokuwa nimezifanya kabla sijaingia kwenye siasa za vyama.
Na jambo la muhimu ni kwamba wakati nafanya harakati hizo, nilikuwa mwanachama wa CCM.