Kupitia Mawakili Tibe Kenneth Rwakatare, mtoto wa marehemu Mchungaji Dkt. Gertrude Pangalile Rwakatare, Nicholas Mugarura, Mwesigwa Muhingo na David Saire Manoti, wametoa tahadhari kwa umma kutonunua mali zinazodaiwa kumilikiwa na St. Mary’s International Academy Limited pamoja na mali za marehemu, wakisema baadhi yake zipo kwenye migogoro ya kisheria.
Kwa mujibu wa mawakili hao, katika Shauri Dogo la Kibiashara Namba 21127 la mwaka 2026, Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara imetoa amri ya ndogo (Maintenance status quo) ya kuamuru hisa na mali za kampuni zibaki kama zilivyo bila kuuzwa hadi mashauri yatakapoamuliwa Mahakamani“Tunautaarifu umma kwamba wasije wakanunua mali yoyote inayomilikiwa na Kampuni ya St. Mary’s International Academy Limited,” wamesema mawakili hao.
Aidha, wamesema shauri la mirathi ya marehemu linaendelea Mahakama Kuu, Kituo Jumuishi cha Temeke, ambako mahakama imeamuru orodha na mgawanyo wa mali ufanyike upya.“Mtu yeyote asinunue mali yoyote ya Marehemu Mchungaji Daktari Gertrude Pangalile Rwakatare, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwapelekea kupata hasara,” wameonya.
Mawakili hao pia wameeleza madai ya Tibe kwamba aliondolewa katika umiliki wa St. Mary’s International Academy Limited kwa kutumia nyaraka na saini ambazo hakuzitambua, akidai kuwa zilighushiwa.
Pia soma: Mali za urithi na hekaheka zake