Taasisi 14 zapinga ripoti za Tume za Rais kuhusu Ngorongoro, Loliondo

Taasisi 14 zapinga ripoti za Tume za Rais kuhusu Ngorongoro, Loliondo

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014
photo_2024-08-18_09-45-53.jpg

Mtandao wa asasi za kiraia na watetetezi wa haki za binadamu Tanzania umekosoa matokeo ya ripoti zilizotolewa na tume mbili za Rais zilizoundwa kutathmini masuala ya mgogoro wa ardhi na utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, zikisema tume hizo hazikuzingatia maoni ya wananchi wa Ngorongoro.

Taasisi hizo 14 zimetaka uwazi, ushirikishwaji na utekelezaji wa haki kwa wananchi wanaoshi maeneo ya Loliondo na Ngorongoro.

Machi 12, 2026 Rais Samia Suluhu, alipokea taarifa ya Tume za Rais alizoziunda kutathmini masuala ya mgogoro wa ardhi na utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari wa wakazi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu Chamwino, Dodoma.

Ripoti ya kwanza ilitokana na Tume iliyoundwa na Rais na ikiongozwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Gerald Ndika, ilikuwa ni ya ilikuwa ikifanya tathmini kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Soma pia: Jukwaa la Kutetea Wamasai Lapinga Ripoti za Tume za Rais Kuhusu Ngorongoro

Tume ya pili iliyoongozwa na Katibu Mkuu mstaafu Musa Iyombe, iliangalia utekelezaji wa zoezi la uamaji wa hiari kutoka eneo la hifadhi hiyo.

Katika tamko lao, asasi hizo zimesema ingawa kuundwa kwa tume hizo ni hatua muhimu ya kutafuta suluhu ya kudumu, bado kuna haja ya kuhakikisha mapendekezo yanayowasilishwa yanazingatia maslahi ya wananchi, hususan jamii za wafugaji wanaoathiriwa na migogoro hiyo.

“Tume hizi zimepuuza maoni ya wananchi waliojitokeza kwa wingi mbele yake kutoa maoni juu ya changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka mbalimbali zenye ushahidi. Badala yake zimejikita katika utetezi wa uhifadhi, utalii na uwekezaji na kupuuza mahitaji ya wananchi kiuchumi, kijamii na haki zao za msingi,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Tamko lenyewe

TAARIFA KWA UMMA TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA NA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU RIPOTI ZA TUME ZA TATHMINI YA MIGOGORO YA ARDHI KATIKA TARAFA ZA LOLIONDO NA SALE, PAMOJA NA UTEKELEZAJI WA ZOEZI LA UHAMAJI WA WAFUGAJI KWA HIARI TARAFA YA NGORONGORO​

A. Utangulizi

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu mnamo mwaka 2022 ilitangaza na kuanza kwa operesheni ya zoezi la kuhamisha Wakazi wa tarafa ya Ngorongoro kwenda Msomera Wilayani Handeni katika Mkoa wa Tanga.

Vile vile, ofisi hiyo hiyo iliratibu zoezi hilo sambamba na umegaji wa ardhi ya vijiji 16 na kuanzisha Pori la Akiba Pololeti katika tarafa za Loliondo na Sale. Operesheni hizo ambazo hazikuwa shirikishi, zilikiuka misingi ya utawala bora, haki za ardhi na haki za Binadamu kwa wakazi wa Ngorongoro hasa jamii ya wafugaji.

Wananchi waliwekewa vikwazo vingi vya huduma za kijamii kama vile maji, afya na elimu, kinyume na Katiba na sheria za nchi. Takribani kaya ama wananchi zaidi ya 1,627 walihamishiwa Msomera na maeneo mengine.
Wananchi waliobaki Ngorongoro walipata mateso mbalimbali kama vile kuzuiliwa huduma za kijamii hali iliyopelekea mwezi Agosti 2024 wafugaji waishio katika vijiji 25, Tarafa ya Ngorongoro, kuandamana kwa amani kwa siku tano mfululizo kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhamishwa kutoka katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Kufuatia malalamiko hayo, mnamo tarehe 1 Disemba 2024 Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na wawakilishi wa wananchi kutoka Tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale ambapo alitangaza rasmi uamuzi wa kuunda tume mbili kwaajili ya kufanya tathmini ya changamoto zinazolalamikiwa na wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Rais aliunda tume hizo mbili na zilitangazwa tarehe 23 Disemba 2024, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka. Tume hizo mbili zilitakiwa kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu 3 tu. Hata hivyo Tume ziliwasilisha ripoti zao kwa Mheshimiwa Rais tarehe 12 Machi 2026 takribani zaidi ya miezi 12 tangu walipoanza utekelezaji wa majukumu yake.

Asasi za Kiraia na watetetezi wa haki za binadamu Tanzania, zimekuwa zikifuatilia ukusanyaji wa maoni kwa wananchi kwa kipindi chote Tume zilipokuwa zinafanya kazi.

1 Tume ya tathmini ya migogoro ya ardhi ilitembelea na kukusanya maoni katika baadhi ya Vijiji vya tarafa zote tatu za wilaya ya Ngorongoro ambazo ni Loliondo, Sale na Ngorongoro.

A. Tume iliyokuwa ikifanya tathmini kuhusu utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kutoka eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitembelea na kukusanya maoni ya wananchi katika kata zote za Tarafa ya Ngorongoro pamoja na Msomera, na Saunyi mkoani Tanga na Kitwai B mkoani Manyara. Sisi asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu Tanzania, tunatoa tamko hili lenye maoni yetu kuhusu ripoti za Tume hizi mbili zilizowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais tarehe 12 Machi 2026.

B. Ukusanyaji wa Maoni Kwa mujibu wa ripoti za Tume, zoezi la ukusanyaji maoni lilipata muitikio mkubwa kwa sababu wananchi waliamini kuwa Tume hizo zingekuwa huru kupokea na kuchakata maoni yao ili kutatua changamoto zao ambazo zimedumu kwa miongo mingi. Makundi yaliyofikiwa ni pamoja na wawakilishi wa wanawake, viongozi wa kimila, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, wadau wa utalii na uhifadhi, viongozi wa dini na viongozi wa Serikali.

C. Maoni yetu kuhusu ripoti za Tume

1. Tume hizi zimepuuza maoni ya wananchi waliojitokeza kwa wingi mbele yake kutoa maoni juu ya changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka mbalimbali zenye ushahidi. Ripoti za Tume kwa asilimia kubwa hazijazingatia maoni ya wananchi na badala yake zimejikita katika utetezi wa uhifadhi, utalii na uwekezaji na kupuuza mahitaji ya wananchi kiuchumi, kijamii na haki zao za msingi.

2. Tume ya Migogoro ya Ardhi, imeshindwa kuelewa na kutafsiri sheria za Ardhi, Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori na Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) juu ya Mgogoro unaotokana na mwingiliano wa sheria mbalimbali na kuanzishwa kwa Pori la Akiba la Pololeti. Kwa upande wa tarafa za Loliondo na Sale, tume ya tathmini ya migogoro ya ardhi imeshindwa kujibu hoja ya msingi ya wananchi juu ya haki za ardhi na uhalali wa kuanzishwa kwa Pori la Akiba la Pololeti ambalo kimsingi ni ardhi halali ya vijiji 16 katika eneo hilo lenye kilomita za mraba 1,502, iliyokiuka matakwa ya kisheria kwa kuchukua fursa ya mgongano wa sheria mbalimbali.

3. Tume zimekwepa kupendekeza uwajibikaji na uwajibishwaji. Tume ya tathmini ya zoezi la uhamaji kwa hiari katika eneo la NCA imekiri kuwa zoezi hilo halikuwa shirikishi bali lilikuwa la ushawishi. Vilevile Tume hiyo 2 ilikubali malalamiko ya wananchi ya usitishwaji wa huduma za kijamii tangu 2022, ambazo ni haki za kikatiba kwa kila raia wa Tanzania. Hata hivyo Tume hizo hazijapendekeza hatua stahiki za kisheria na kiutawala za kuchukuliwa dhidi ya watumishi na viongozi wa Serikali wote waliohusika katika upotoshaji na hujuma hiyo ili iwe fundisho kwa wengine. Pia ripoti za Tume zimekuwa kimya kuhusu fidia kwa waathirika hao kupata haki zao zilizoporwa katika maeneo mbalimbali.

4. Tume hazijataja ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Licha ya kupewa taarifa na ushahidi wa maneno na nyaraka mbalimbali na wananchi juu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika. Wananchi waliwasilisha taarifa na nyaraka za matukio ya watu kupigwa, kukamatwa kwa watu na mifugo. Mfano wananchi walikabidhi stakabadhi za malipo ya faini za mifugo zenye thamani ya mamilioni ya fedha waliyotozwa wananchi katika tarafa za Loliondo, Sale na Ngorongoro. Hali hii imewafilisi wananchi.

5. Tume ya Migogoro ya Ardhi imeshindwa kuelewa na kutafsiri Sheria za Ardhi, Sheria za Hifadhi ya Wanyamapori na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) juu ya mgogoro katika vijiji vilivyopo eneo la Ziwa Natron lililopo Tarafa ya Sale. Vijiji vya Engaresero, Pinyinyi, Oldonyosambu na Jema ni vijiji halali vinavyo miliki ardhi za vijiji kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa sheria itakuwa ni hujuma kwa wananchi na ni kinyume cha sheria kuanzisha au kuendelea kuwepo kwa Pori Tengefu katika Ardhi ya vijiji.

6. Hoja ya Tume ya uharibifu wa mazingira ni potofu na haina ushahidi wowote wa kisanyansi au kiikolojia na hivyo haina ukweli wowote. Uharibifu wa mazingira na kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imetajwa kusababishwa na ongezeko la watu, mtawanyiko wa makazi na shughuli za kibinadamu. Tume haijatoa ushahidi wowote wa Kisayansi na Kiikolojia kuthibitisha hoja hiyo badala yake imekuja na maneno yasiyokuwa na ushahidi.

Tume zimekwepa kuelezea juu ya uwepo wa tatizo kubwa la ongezeko wa ujenzi holela wa mahoteli yenye idadi kubwa ya watu kwenye eneo hilo inatishia ikolojia, na barabara zisizofuata taratibu za kiikolojia. Aidha ni vyema ifahamike kuwa Wamaasai wamekuwa wahifadhi wazuri wa mazingira na wanyamapori katika karne zote na ndiyo maana ushahidi unaonyesha wazi kuwa maeneo yao ndiyo pekee yaliyobakia kuwa yenye mvuto kimazingira, kiikolojia na wanyamapori kwa wingi. Pamoja na kupewa ushahidi wa kuona na wa taarifa 3 mbalimbali, ripoti zote hazijatambua jitihada hizo za kimaisha zinazoendelea uhifahi endelevu. Kimsingi jitihada za kiuhifadhi za jamii hizi zinapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa badala ya kuwatengenezea tuhuma ili waweze kuhamishwa katika maeneo yao.

7. Tume imepotosha juu ya hitaji la marekebisho ya sheria ya NCA kwa kushindwa kwa mfumo wa Matumizi Mseto ya Ardhi katika tarafa ya Ngorongoro bila ushahidi wa kisayansi au Kiikolojia. Pendekezo hili linalenga kupora haki ya wananchi kwa kuleta sheria ambayo itawaondolea wananchi haki yao ya ardhi waliyoipata kabla ya uhuru, na kufumbia macho ukweli kwamba wananchi wa Ngorongoro walihamishwa kwa mkataba wa kudumu kupisha kuanzishwa kwa Mbuga ya Taifa ya Serengeti.

Tume inapendekeza Marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na utungaji wa Kanuni. Marekebisho ya sheria ya NCA ni kujipatia njia ya kuhalalisha uhamishaji wa wananchi katika tarafa ya Ngorongoro ili kupisha uhifadhi na uwekezaji wa sekta binafsi kwenye maeneo yao kwa kuwa mfumo wa matumizi mseto ya ardhi imetajwa na Tume kuwa sio endelevu tena ndani ya eneo hilo. Vilevile kanuni zitaongeza vikwazo na masharti zaidi kwa wenyeji katika Tarafa ya Ngorongoro. Kwa miaka kadhaa sasa wananchi wamekuwa na malalamiko juu masharti na vikwazo vya makatazo yanayohusiana na maeneo ya malisho, maeneo yenye chumvi ya mifugo, maji, uingiaji wa malango kutoka nje ya eneo hilo pamoja na maeneo ya kimila ya kuabudu.

8. Tume hazijaeleza na ripoti zimekuwa kimya juu ya serikali kutumia Jeshi katika operesheni hii ya kuhamisha watu toka NCA na uanzishwaji na usimamizi wa Pori la Akiba la Pololeti uliofanywa na vyombo vya kijeshi. Jambo hili ni hatari pale operesheni za kiraia na maisha ya kijamii zinapotekelezwa na vyombo vya kijeshi badala ya vyombo vya kiraia. Hali hii imeleta hofu na kuzua taharuki kwa wananchi kujiona kuwa serikali imewafanya maadui wa kuzuiwa na jeshi.

9. Tume haikuelezea kwa namna yeyote changamoto za uanzishwaji wa Pori la Akiba la Pololeti katika eneo la ardhi ya vijiji 16 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,502 kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Na. 604 ya 2022, ambazo zimesababisha uhaba mkubwa wa malisho na maji, na imepelekea vifo vingi vya mifugo na kuibuka kwa migogoro ya ardhi inayohusiana na malisho baina ya vijiji.

10. Tume ya tathmini ya migogoro ya ardhi imepotosha ukweli juu ya matumizi ya eneo la kilomita za mraba 2,500. Tume imesema eneo hilo 4 halitumiki kwa tija jambo ambalo halina ukweli wowote. Kwa mujibu wa rasimu ya Mpango wa Matumizi ya ardhi ya Wilaya ya Ngorongoro ya mwaka 2023 ardhi iliyobaki kwaajili ya matumizi ya malisho ni asilimia 12.4 pekee katika wilaya nzima, eneo ambalo halitoshelezi kwa malisho ikilinganishwa na idadi ya mifugo katika wilaya hii ya wafugaji.

11. Tume imepotosha kuhusu wajibu na kazi za Asasi za Kiraia katika Wilaya ya Ngorongoro. Pendekezo la Tume ya tathmini ya migogoro ya ardhi kuwa NGOs zilizopo katika Wilaya ya Ngorongoro zifanyiwe tathmini na kuchukuliwa hatua stahiki, ni mwendelezo wa vitisho dhidi ya asasi za kiraia ili zisiendelee kutetea haki za binadamu na haki za ardhi katika wilaya hiyo.

Asasi hizi zinatimiza wajibu wao na zinafuata sheria, kanuni na taratibu za uanzishwaji wake na zimechangia katika maendeleo ya kijamii ya wananchi wa wilaya nzima na kupunguza umaskini kwa wananchi wa Ngorongoro. Tume ina nia ovu ya kuigombanisha Serikali na Asasi za kiraia.

12. Tunakumbusha vilevile kuwa miaka ya 1959 wananchi hawa walihamishwa kwa mkataba wa kudumu kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo mkataba huo unaonyesha kuwa wananchi hawatasumbuliwa tena kutoka NCA.

C. Wito na Mapendekezo yetu

1) Tunamuomba Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atupilie mbali mapendekezo ya Tume hizo kwani hayana nia njema wala tija kwa maisha ya wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kwani yataongeza mgogoro zaidi. Mapendekezo haya yanatetea uwekezaji wa mahoteli na utalii ya sekta binafsi bila kujali haki ya wananachi wanaoishi eneo husika.

2) Tunaomba Mhe. Rais aweke hadharani ripoti za Tume zote mbili ili umma usome kwa mapana kilichaondikwa na Tume hizi.

3) Tunatoa wito kwa Serikali kufuta pori la akiba la Pololeti na kuwarejeshea wananchi wa Tarafa za Loliondo na Sale eneo la ardhi ya vijiji 16 lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,502 ili kumaliza taharuki na mgogoro.

4) Tunatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi wote waliohusika kuhujumu miradi ya wananchi katika Tarafa ya Ngorongoro ikiwemo kuhamisha fedha za miradi kupeleka 5 maeneo mengine na fedha hizo zirudishwe kufidia utekelezaji wa miradi hiyo.

5) Tunapendekeza wote waliohusika katika Operesheni hii kuchukuliwa hatua kwa matumizi mabaya ya fedha za Operesheni takribani shilingi bilioni 212 zilizotengwa kwa zoezi hili na kufaidisha watu wachache.

6) Aidha, tunapendekeza Rais atoe agizo la kuzuia wenyeji wa Tarafa ya Ngorongoro kutobughudhiwa kwa namna yeyote ile, kwa kuwa wana haki zote za kuishi katika ardhi yao na kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria. Ikumbukwe pia kuwa, wananchi hao walilipa gharama kubwa ya kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

7) Serikali kusitisha mpango wake wa kutekeleza mapendekezo ya kufanyia marekebisho ya Sheria ya NCA ambayo itapelekea serikali kugombana na wananchi, kukinzana na sayansi; na kuhalalisha kwa kutumia sheria kandamizi uporaji wa wazi wa haki za binadamu, uvunjifu wa haki za binadamu kwa wakazi wa Ngorongoro unaoendelea kwa miongo kadhaa sasa. Pia kuondoa makazi mseto itadumaza utalii na uendelevu wa uhihadhi wa eneo hilo.

Tamko hili limetolewa na asasi za kiraia na watetezi wa haki za binadamu Tanzania, April 14, 2026

1. Jukwaa la Ardhi Tanzania (TALA)
2. HAKIARDHI
3. Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC)
4. Shirika la Kuinua na Kusaidia Maisha ya Wafugaji (PALISEP)
5. Mtandao wa Mashirika ya Kifugaji (PINGOs Forum),
6. Shirika la Uhifadhi wa Mifumo ya Asili na Jadi (TEST),
7. Ujamaa Community Resource Team (UCRT)
8. Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF)
9. Community Research and Development Services (CORDS)
10. Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
11. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
12. Civic and Legal Aid Organization (CILAO) 6
13. Parakuiyo Pastoralists Indigenous Community Development Organization (PAICODEO)
14. KINNAPA Development Programme 7
 
Hizi Tume zinaundwa ili kusafisha uchafu wa wa teuzi wao, hakuna cha maana watashauri.

Ni mjinga pekee ndio ataamini ile ripoti kwamba sijui binadamu walishajaa kuzidi wanyama
 
Back
Top Bottom