Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) leo imefanya maongezi ya kimkakati na Wadau mbalimbali wakiwemo Sekta Binafsi, Sekta za Umma, Asasi za Kiraia, Taasisi za Dini, Vyombo vya Habari, Viwanda vya Uchapaji na Uchapishaji, Kampuni za Simu, Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri, Wasanii, Madereva wa Vyombo vya Moto na Wananchi kuelezea Kampeni inayotarajiwa kuzinduliwa ya kupunguza ama kutokomeza kabisa rushwa Barabarani.
TAKUKURU imeeleza kuwa Kampeni hiyo imepewa jina la
‘UTATU’ ikimaanisha ni muunganiko wa pande Kuu tatu: TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Wadau
Imedaiwa kuwa lengo kuu la kampeni ni kuzuia rushwa za barabarani ambayo imebainika ni kisababishi kimojawapo cha ajali zinazotokea barabarani; tatizo ambalo limekuwa likikemewa sana na viongozi mbalimbali wa Serikali. Aidha imesema
UTATU huo unatakiwa kuweka mikakati ya pamoja na endelevu ya kutibu tatizo la ajali badala ya kulaumiana na kunyoosheana vidole.
Kampeni hiyo imejiwekea mambo malengo mahususi manne, ikiwa kila lengo linatakiwa kutekelezwa na kila mdau kwa nafasi yake:
- Kudhibiti vitendo vya rushwa miongoni mwa wasimamizi wa sheria za barabarani
- Kuandaa mkakati wa kuzuia vitendo vya rushwa barabarani
- Kushirikisha Umma kuzuia vitendo vya rushwa barabarani
- Matumizi ya TEHAMA kudhibiti vitendo vya rushwa barabarani
Kuhusu matumizi ya TEHAMA kudhibiti vitendo vya rushwa barabarani, TAKUKURU imesema tayari limeanza kutekelezwa kwa kutengeneza mfumo utakaotumika kuchukua matukio ya vitendo vya rushwa kwa kutumia simu ya mkononi (Mobile App).
Mfumo huo (Mobile App) utakaozinduliwa pamoja na Kampeni hii ya UTATU, utapakuliwa kutoka
Play Store au
App Store ya simu ya mkononi kisha mtu ataweza kupiga picha za video, mnato au sauti na kuzituma TAKUKURU.
Baadhi ya Majukumu ya Wadau wa Kampeni hii yametajwa kuwa:
Wasimamizi wa sheria na miundombinu ya Barabara (TANROADS, TARURA, LATRA na wengine)
Wanalo jukumu la kusimamia ubora wa miundombinu na Vyombo vya Usafiri ikiwa ni pamoja na
- Kuboresha sheria, kanuni na miongozo
- Kuboresha miundombinu ya barabara na mizani
- Kusimamia usajili wa Vyombo vya Usafiri
- Kuhakikisha alama za usalama barabrani zinaonekana vizuri
- Kutoa taarifa za vitendo vya rushwa barabarani
Wasanii wa fani mbalimbali
- Wana jukumu la kuhamsisha watumiaji wa barabara kupitia Sanaa zao zinazosisimua na kuburudisha huku ujumbe wao ukisaidia kubadili mitazamo ya watumiaji wa barabara kuacha vitendo vya rushwa
- Wanatarajiwa kutoa michango yao ya kuandaa Sanaa zitakazohusiana na kampeni ya UTATU
AZAKI wao wametajwa kuwa wahamasishaji ambapo majukumu yao yatakuwa:
- Kuhamasisha wananchi kutuma taarifa za vitendo vya rushwa barabarani
- Kuhamasisha wananchi waache uoga wa kutoa taarifa za rushwa
- Kutumia mtandao wao kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
- Kuhamasisha wananchi kuacha kutoa rushwa kwa masimamizi wa sheria za usalama barabarani
Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri ambao majukumu yao ni
- Kusimamia Vyombo vya Usafiri ili kutoruhusu magari mabovu kuingia barabarani
- Kuajiri madereva wenye sifa na kuwalipa vizuri
- Kuacha kutoa Rushwa ili wapate leseni bila kufuata utaratibu
- Kuwachukulia hatua madereva wazembe
- Kuwasimamia madereva kuacha kutoa rushwa kwa wasimamizi wa sheria za usalama barabarani
Wamiliki wa Vyombo vya Habari ni kundi lingine ambalo katika Kampeni hii majukumu yake yamebainishwa kuwa
- Kuelimisha wananchi kupitia Vyombo vyao vya Habari
- Kusaidia kutoa nafasi kwenye Vyombo vya Habari na kurusha matangazo kuhamasisha kampeni
- Kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa
Wamiliki wa Viwanda vya Uchapishaji na Uchapaji wao wataweza kushiriki kwa:
- Kusaidia kuchapa machapisho ya kuhamasisha kampeni
- Kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
Vingozi wa dini wao wana majukumu muhimu ya
- Kufundisha maadili kwa waumini wao ili wasitoe rushwa kwa wasimamizi wa sheria za usalama barabarani
- Kutumia Vyombo vya Habari vinavyomilikiwa na dini zao ili kuhamasisha kampeni
- Kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
Katika mkutano huu, wadau walioshiriki kutoa maoni wamedokeza haya:-
Kwanza, wamesema Rushwa ni mtazamo wa ndani ya Polisi na nje ya Polisi, watu wanaona Polisi ni fursa. Kwenye vitengo vinavyoongoza kwa rushwa ni pamoja na kwenye kutoa leseni, ukaguzi wa barabarani. Polisi walio kwenye Pikipiki maarufu kama
‘tiGO’ na madereva wa magari ya Kirikuu wanaodai kuwa wakipita ni lazima wasimamishwe na kuombwa rushwa
Aidha, wengine wamehoji kwanini TAKUKURU hawapo barabarani? Huku wengine wakisema ni bora adhabu ziongezwe kwenye makosa ya barabarani na adhabu ya fedha iondolewe kabisa.
Wengine wakiwemo Viongozi wa Dini wametoa maoni kuwa hofu ya Mungu ndio suluhisho pekee la tatizo la rushwa kwa wananchi wanaweza kuwaepuka TAKUKURU na Polisi ili wasikamatwe kwenye masuala ya rushwa. Pia, Polisi wakiwa na hofu ya Mungu wanaweza kukataa rushwa na kuwakamata wanaotaka kutoa na hivyo kuzuia rushwa.
Lakini, kuhusu
App TAKUKURU waliyozungumzia wadau wamesihi sana kuwa kunatakiwa kuwe na elimu ya awali itakayotolewa kwa Wananchi kabla ya kuanza kutumia App hiyo na pia kuwapa muda Wananchi kuielewa.
Wametaka pia Makamanda wa Polisi na watumishi waboreshewe maslahi kwa kuwa hiyo inaweza kuwa njia mojawapo ya kuzuia rushwa.