Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Uchunguzi umebaini kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2022, mtuhumiwa anadaiwa kughushi nyaraka na sahihi za wanafamilia wa marehemu kwa lengo la kujipatia umiliki wa eneo la ardhi lililopo Mtaa wa Kizani, Geza Ulole, Wilaya ya Kigamboni. Eneo hilo lilinunuliwa mwaka 2008 kwa kiasi cha shilingi milioni sitini na kuachwa kama urithi kwa watoto wa marehemu.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi, mtuhumiwa alitumia mwanya wa kuaminiwa na familia ya marehemu kuandaa nyaraka za uwakilishi (Power of Attorney) kwa njia isiyo halali. Nyaraka hizo zilidaiwa kutumika kupima eneo hilo na kuligawa katika viwanja tisa, ambavyo baadaye vilikuwa vikiuzwa kwa watu mbalimbali kwa kutumia majina na sahihi za kughushi za wanafamilia. Aidha, uchunguzi umebaini kuwa katika baadhi ya viwanja hivyo, mtuhumiwa alijiorodhesha mwenyewe kama mmiliki halali.
Kutokana na ushahidi uliokusanywa na kufanyiwa uchambuzi wa kitaalamu, TAKUKURU imefungua kesi ya jinai namba CC/26097/2025 dhidi ya Askofu Renatus Joseph Nyalali, ambayo imefunguliwa rasmi tarehe 28 Oktoba 2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
TAKUKURU inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, na itaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vyote vya rushwa, udanganyifu na uhalifu wa aina yoyote bila kuzingatia hadhi au nafasi ya mhusika, kwa lengo la kulinda maslahi ya umma na misingi ya haki.
UFATILIAJI WA MATUMIZI YA FEDHA ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
TAKUKURU Mkoa wa Temeke ilifuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi 04 ya maendeleo yenye thamani ya Shs 36,532,990,529 katika sekta ya elimu,afya na ujenzi inayotekelezwa na Manispaa ya temeke na Kigamboni. Miradi 02 ilikutwa na dosari na ushauri uliotolewa umeanishwa kama inavyoonekana kwenye kiambatisho Na 1.
UELIMISHAJI UMMA
Katika kipindi tajwa elimu kwa umma imetolewa kwa wananchi 404,804 kupitia Mikutano 12,maonesho 04, Semina 35 na Uimarishaji klabu za wapinga rushwa 11 katika shule shule za msingi,sekondari na vyuo na imefanya vipindi vya redio na Televisheni 12 na mifano ya mada zilizotolewa na mafanikio yameambatishwa katika kiambatisho Na 03.
UCHUNGUZI NA MASHTAKA
Kwa kipindi tajwa, TAKUKURU mkoa wa Temeke imeweza kufanya yafuatayo, tumepokea malalamiko 48 kutoka katika idara mbalimbali ambapo malalamiko 22 yanahusu rushwa na 26 yasiyohusu rushwa.
Kesi 02 zilifunguliwa Mahakamani na kesi 02 Jamhuri imeshinda na hivyo kufanya jumla ya kesi 08 zinaendelea mahakamani.
4. MIKAKATI YA JANUARI – MACHI 2026
Katika kuendelea kutekeleza majukumu yake, TAKUKURU Mkoa wa Temeke imejipanga kutekeleza mikakati ifuatayo katika robo ya Januari hadi Machi 2026:
Kuandaa na kutekeleza bonanza kubwa la wanafunzi wa shule za sekondari wanaoshiriki katika klabu za wapinga rushwa zilizopo Wilaya ya Temeke, likijumuisha michezo, nyimbo, mashairi, maigizo na mada mahsusi kwa lengo la kuimarisha uelewa na ushiriki wa vijana katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika vikao kati ya TAKUKURU na wadau, hususan yale yanayolenga kuziba mianya ya rushwa iliyobainika kupitia uchambuzi wa mifumo, ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Kuimarisha shughuli za uchunguzi kwa kutoa kipaumbele cha juu kwa malalamiko yote yanayohusu rushwa, kwa kuzingatia mwenendo wa takwimu za vipindi vilivyopita. Mkakati huu utalenga kuongeza kasi na ubora wa uchunguzi, kukamilisha mashauri kwa wakati na kuhakikisha kesi zenye ushahidi wa kutosha zinafikishwa Mahakamani.
5. WITO
Ndugu wananchi wa Wilaya za Temeke na Kigamboni, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza kwa dhati kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa. Vita hii si ya taasisi moja pekee, bali ni jukumu la kila mmoja wetu. Ni kwa mshikamano, ujasiri na uwajibikaji wa pamoja ndipo tutaweza kujenga Tanzania yenye haki, uadilifu na maendeleo ya kweli, Tanzania isiyokuwa na rushwa.
Aidha, nawatoa wito kwa wananchi wote kujiepusha kabisa na vitendo vya rushwa kwa namna yoyote ile, na kuchukua hatua za kijasiri kwa kutoa taarifa pale wanapobaini dalili za rushwa katika maeneo yao. Serikali imeweka mifumo salama ya kupokea taarifa, ikiwemo Ofisi za TAKUKURU zilizo karibu na wananchi pamoja na namba ya simu 113, ambayo ni bure na inapatikana muda wote.
Ushiriki wenu ni silaha muhimu katika mapambano haya, na kwa pamoja tunaweza na tutashinda vita dhidi ya rushwa.
Inawasilishwa na
Holle Makungu,
Mkuu wa TAKUKURU (M) TEMEKE.