Manventure
Member
- Jul 16, 2021
- 10
- 4
TANZANIA IWE NA VYAMA VYA SIASA VICHACHE ILI KUIMARISHA TAIFA.
Mfumo wa vyama vingi vya siasa unaboresha demokrasia ya nchi kwa kuifanya Serikali chini ya chama tawala iliyopo madarakani kutimiza majukumu kwa ufasaha na uangalizi zaidi. Nchini Tanzania mfumo wa vyama vingi vya siasa ulianza mwaka 1992, ambapo kabla ilikuwa ni chama kimoja yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mpaka sasa Tanzania kuna vyama vya siasa zaidi ya ishirini. Na kila uchaguzi mkuu Serikali hutenga ruzuku kwa ajili ya vyama vitakavyo shiriki shughuli nzima ya uchaguzi.
Tukiangazia kazi kuu za vyama vya siasa ni pamoja na;
1. Kushawishi watu kushiriki shughuli za maendeleo.
2. Kutoa na kupitisha wagombea wa nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi. Viongozi ambao wataitumikia Serikali na wananchi wake.
3. Kutoa elimu ya siasa, demokrasia na umoja kwa taifa.
4. Kuikosoa na kutoa mapendekezo kwa chama tawala. Katika utendaji chama tawala kitapokosea vyama pinzani vina haki ya kukosoa chama tawala.
Maoni yangu mfumo wa vyama vingi hamna ulazima wa kuwa na idadi kubwa ya vyama. Hata kuwa na vyama viwili hata vinne bado itafahamika kama mfumo wa vyama vingi. Tanzania inaweza kubaki na vyama vichache vitavyoleta ushindani kweli na kupunguza gharama nyingi kwa Serikali, wanachama na wananchi kiujumla.
Tanzania kama taifa linalozidi kukua siku hata siku linatakiwa kuwa na vyama vya siasa chini ya kumi, hata ikiwa vitano tu vinatosha pia. Haya ni maoni yangu tu.
FAIDA YA KUWA NA VYAMA VICHACHE VYA SIASA.
1. Gharama za uendeshaji wakati wa uchaguzi zinapungua.
Serikali hutenga ruzuku kwa kila chama kinachoshiriki uchaguzi mkuu. Mfano, uchaguzi mkuu mwaka 2020 CCM ilipata Tsh bilioni 1.33, CHADEMA Tsh milioni 109.68, ACT-Wazalendo Tsh milioni 14, CUF Tsh milioni 5.7, NCCR-Mageuzi Tsh 316,937. Democratic Party Tsh 63,387.
Mfano tungekuwa na vyama viwili fedha takribani milioni 40 zingetumika kwenye shughuli nyingine. Kwa kuwa Tanzania hatujafikia mafanikio makubwa, tunapaswa kupunguza gharama ili kuendana na hali ya taifa kiuchumi. Njia mojawapo ni kuwa na vyama vya siasa vichache.
2. Taifa linakuwa na sera chache ambazo hazitoleta mkanganyiko kwa wananchi.
Mfano kuwa na vyama zaidi ya ishirini ina maana kila chama kina sera zake kwa wananchi. Wengine wanaweza kuwa na sera za viwanda zaidi, wengine kilimo, wengine utalii, wengine usawa kijinsia na mifano mingi zaidi. Sasa ni mwananchi gani anaweza kufuata sera zaidi ya ishirini ili kuwa mzalendo wa taifa. Lakini kama tukiwa na vyama viwili, vitatu hata vitano ni rahisi mwananchi kuchagua aegemee upande gani ambao utakuwa mtetezi kwake na kuchangia maendeleo yake na taifa zima.
3. Vinapunguza mgawanyiko ndani ya jamii na kuongeza umoja.
Ijapokuwa wengine husema vyama vichache huzalisha makundi machache yenye nguvu zaidi kuliko vyama vingi ambavyo kunakuwa na vikundi vidogo vidogo vingi. Lakini ni rahisi sana kushawishi na kuyaunganisha makundi machache kuchapa kazi kama vile ujenzi wa shule au hospitali. Vikundi vingi na vidogo vidogo ni kazi kwa sababu hadi kuunganisha nguvu kazi inachukua muda mrefu. Vivyo hivyo hata katika siasa kuwa na vyama vya siasa vichache ni rahisi sana kutekeleza sera na mipango ya nchi kuliko vyama vingi ambavyo inachukua muda mrefu kwa sera na mipango kukubaliwa au kuafikiwa na kila mmoja.
4. Ni ishara ya umoja ndani ya jamii.
Vyama vichache vinaashilia watu wake wameridhia na kukubali uwepo wa hivyo vyama pekee. Hivyo watu wake watapendana, pale serikali itapokosea itaweza kukosolewa kwa urahisi zaidi. Lakini vyama kuwa vingi inaweza kuwa ishara ya makundi kadhaa kutoelewana katika jamii na kupelekea kujitenga na kutengeneza chama au kundi jingine. Mtazamo ni kama Taifa tutakuwa na vyama vya siasa vichache pia umoja utakuwa imara zaidi kwa sababu hakuna atayejitenga au kuunda taifa lake. Kila jamii ina kasoro ila ni muhimu kufanyia kazi kasoro hizo.
Maoni.
Yapo mataifa mengi duniani ambayo yanatumia mfumo wa demokrasia pamoja na kuwa na vyama vya siasa vichache. Mfano mzuri ni baba wa demokrasia yaani Marekani kuna vyama vikuu viwili ngazi ya taifa. Mataifa mengine ni pamoja na;
Ujerumani – vyama vikuu viwili (2), vyama vidogo vitatu (3).
Australia – vyama vya siasa vitatu (3).
China – chama tawala cha CPC pamoja na vyama vingine nane (8).
Vivyo hivyo Tanzania tunaweza kuwa na vyama vya siasa vichache na bado taifa likatambullika kama mfuasi wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Marejeo
https://www.orpp.go.tz/pages-subvention
https://www.bbc.com/habari-59567666
Upvote
2