Taifa Stars imejilaza ICU inapumulia mashine
HAUTAIKUTA hospitali yoyote nchini, lakini Taifa Stars inaumwa sana. inahitaji msaada mkubwa. Ina magonjwa mengi ambayo hayawezi kutibika kirahisi, ni tofauti na wengi wanavyofikiri.
Ugonjwa mkubwa wa Stars unaanzia nje ya uwanja. Nani anaitaka Taifa Stars ya sasa? Hakuna. Mashabiki hawaitaki, wachezaji hawaitaki. Nahisi hata Rais Jakaya Mrisho Kikwete naye haitaki Stars ya sasa. Anashindwa kusema tu.
Duniani kote hakuna mchezaji aliyetajirika kwa kupitia timu yake ya taifa. Hii ni timu ya hiyari. Gurudumu lake linaendeshwa kwa mapenzi kati ya wananchi na mashabiki. Wachezaji wanatajirika kupitia klabu zao.
Lakini wachezaji wa Taifa Stars hawaitaki timu kwa sababu mashabiki hawaitaki timu. Mbrazili mmoja alisafiri zaidi ya kilomita 5,000 katikati ya mwaka 2006 kwa ajili ya kuleta muunganiko huu. Marcio Maximo.
Hata hivyo, kile si kitu cha kujivunia sana. Wachezaji na mashabiki wanapaswa kuungana muda wote linapokuja suala la timu ya taifa. Inachekesha, Maximo alipoondoka na uzalendo ukaondoka.
Katika taifa la dunia ya tatu, ambalo lina ligi ya kawaida tu huku likiwa halina wanasoka wanaotamba Ulaya, uzalendo ndio dawa ya kwanza kumfanya adui apate wakati mgumu anapocheza na nyinyi. Lakini hauwezi kuamini, Wajerumani wanaojua sana soka kwa sasa duniani wana uzalendo zaidi kuliko Watanzania wote.
Ugonjwa wa pili mbaya vilevile ni ule wa Kocha, Mart Nooij. Bado kocha hajatusaidia. Tuliambiwa maneno mengi kwamba TFF mpya ingekuja na kocha wa Kidachi kwa madai kwamba ni mafundi sana wa soka. Ilikuwa sehemu ya kampeni na siasa tu za soka la Tanzania.
Nooij haeleweki hata kidogo. Ndani ya uwanja timu ina mapungufu mengi. Hakuna uwiano mzuri kati ya ushambuliaji na ulinzi. Unabaki kujiuliza tu, anawajua vizuri wachezaji wa Kitanzania? Ni kweli wapo katika viwango vya mfumo anaoutaka?
Hata kama tunahitaji mabao, tena tukiwa katika uwanja wa nyumbani, unawezaje kuwapanga kwa pamoja, Mbwana Samatta, John Bocco, Thomas Ulimwengu na John Bocco? Wote hawa si wakabaji wazuri na hawawezi kurudi nyuma kwa haraka wakati wapinzani wana mpira.
Nyuma yao, Nooij anawapanga Erasto Nyoni na Mwinyi Kazimoto. Katika soka la kisasa, mpinzani anajaza viungo wanne hadi watano, wewe unawaweka Mwinyi na Erasto peke yao, unatagemea nini? Ndio maana Msumbiji walituchafua vibaya pale Uwanja wa Taifa.
Ndio maana kupitia mechi za timu ya taifa, sasa hivi tunaanza kuona mapungufu ya Kevin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro' ingawa katika Yanga hayaonekani sana.
Maximo alikuwa mwoga. Alijaza viungo wengi eneo la katikati kwa sababu alijua udhaifu wetu kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Katikati ya uwanja angeweza kuwapanga Shaaban Nditi, Henry Joseph, Athuman Idd na mbele yao kidogo angecheza Nizar Khalfan.
lisaidia sana kutokana na aina ya wachezaji tulionao Tanzania kwa sasa. Hawawezi kupishana na Cameroon, Ivory Coast, Ghana hata Msumbiji. Lakini Nooij anaichezesha Stars kama vile ni timu kamilifu.
Kim Poulsen alijua soka la kutandaza, lakini bado alikuwa anaweka viungo watatu hadi wanne pale katikati. Vipi Nooij na wachezaji wake wa sasa. Anadhani wapo katika viwango vya Yaya Toure?
Ugonjwa mwingine ambao ni mbaya zaidi kwa Taifa Stars ni ule wa kukosa mwelekeo na malengo. Tunataka kufuzu michuano gani? Kwa kutumia wachezaji gani? Kocha anafahamu tunachotaka?
Kocha aliyepita, Kim Poulsen alikuwa na malengo yake. Kabla ya kuchukua nafasi ya Jan Poulsen yeye ndiye alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana. Alipopanda kuwa kocha mkuu alishawaelewa wachezaji wa timu ya vijana na uwezo wao. Alishawaelewa vema akina Frank Domayo, Simon Msuva, Atupele Green, Issa Rashid, Manyika Peter na wengineo. Alikuwa anatazama mbali kidogo.
Lakini pia alishajua jinsi ya kuwatumia wachezaji wakubwa wa Kitanzania. Stars ilikuwa inacheza pasi fupi fupi na za haraka. Mwelekeo ulionekana. Mwenyewe alijiwekea lengo la kwenda Morocco lakini watu wakamhukumu kwa matokeo ya michuano ya Chalenji huku tukiambiwa kuwa tutaletewa bonge la kocha.
Siioni Msumbiji ambayo ingemuondoa Kim katika michuano hii. Katika mfumo wa kawaida wa Kim, Msumbiji ingeteseka tu na yule kiungo wao mtembeaji, Elias Pelembe Domingues, asingetembea sana kama alivyofanya katika mechi hizi mbili.
Ugonjwa mbaya zaidi ni kwamba Stars ipo ili mradi ipo. Wachezaji waliopo baadhi yao wameanza kuchoka, lakini nani mbadala halisi? Kizazi cha akina Samatta kilitengenezwa, kizazi kijacho nani anakitengeneza? Walahu Simba walijitahidi kututengenezea akina Ramadhani Singano, lakini wako wachache.
Tunahitaji kuiokoa Stars kwa kutibu magonjwa yote hayo hapo juu. Tulitaka kukosea kwa kuanza kutibu mabadiliko ya jina la timu wakati magonjwa hayo juu yameilaza Stars kitandani kwa sasa.
Source :
Taifa Stars imejilaza ICU inapumulia mashine - Soka - mwanaspoti.co.tz