Date::8/21/2008
Spika Sitta ampa tahadhari Rais Kikwete kuhusu wahujumu uchumi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Samuel Sitta, amemkumbusha Rais Kikwete kuwa wahujumu uchumi hawastahili kuneemeka kwa madai ya haki za binadamu.
Na Ramadhani Semtawa
Mwananchi
WAKATI Rais Jakaya Kikwete, akionyesha huruma kwa watuhumiwa ufisadi wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), Spika wa Bunge Samuel Sitta, amemkumbusha kuwa ni makosa kusimamia haki za binadamu kwa wahujumu uchumi.
Spika alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya hotuba ya Rais Kikwete bungeni, ambayo pamoja na mambo mengine iliwapa ahueni mafisadi wa EPA kwa kuwaongezea muda wa kuzilipa hadi Oktoba 31, mwaka huu.
Baada ya hotuba ya rais, Spika alimtaka kuongeza ukali kidogo katika masuala ya rushwa na ufisadi na kwamba Bunge litasaidia kuiweka nchi sawa.
"Hongera sana mheshimiwa Rais, umetoa hotuba nzuri, tumesikia, kuna mambo ya msingi, kuna hili la utawala bora, ukiongeza ukali kidogo basi sisi wabunge tutakusaidia. Lakini, wakati mwingine haya mambo ya kuweka visingizio vya haki za binadamu kwa wahujumu uchumi, yanakwamisha maendeleo ya nchi," alisema Sitta huku Rais akitabasamu.
Spika Sitta alifafanua kwamba, wakati mwingine kushindwa kushughulikia wahujumu uchumi kwa kisingizio cha haki za binadamu hurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Alisema nchi za Asia Mashariki zimeweza kupiga hatua kutokana na kuwa makini katika masuala ya rushwa na kwamba kama zingeendekeza visingizio hivyo zisingefanikiwa.
Spika Sitta ambaye chini ya uongozi wake, Bunge limetoa maamuzi mazito dhidi ya uhujumu uchumi, ikiwemo mkataba wa umeme wa dharura kwa Kampuni ya Richmond, alisema kuwapo kwa ufisadi katika Mfuko wa Uagizaji Bidhaa nchini (ICF) ni ishara kwamba zinahitajika juhudi za kusafisha nchi.
Alisema hivi sasa mwananchi wa kawaida hawezi kuelewa akisikia eti wahujumu uchumi mabilionea hawakamatwi kwani kuwakamata ni vigumu.