Na Boniface Meena
Mwananchi
Jan/9/2010
RAIS Jakaya Kikwete ameingilia kati sakata lililoibua mjadala mkubwa mwaka jana la mradi wa vitambulisho vya taifa kwa kuagiza lishughulikiwe kwa haraka.
Kitendo cha Rais Kikwete kuingilia suala hilo kimetuliza kwa muda mzuka wa mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo, ambaye katika Bunge la mwaka jana alimpa miezi sita Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kushughulikia suala hilo nyeti.
Shellukindo aliiambia Mwananchi kuwa uamuzi wa Kikwete umemfanya aamue kutowasilisha tena hoja binafsi ya kutokuwa na imani na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye mbunge huyo alidai kuwa ndiye anayekwamisha mradi huo mkubwa wa vitambulisho vya taifa unaotarajiwa kuligharimu taifa takribani dola 160 milioni za Kimarekani.
Hata hivyo, Shellukindo alisema uamuzi wake wa kuwasilisha hoja hiyo utabaki palepale endapo agizo hilo la rais halitatekelezwa ipasavyo.
Mwaka jana, Shellukindo alidai kuwa alipanga kuwasilisha hoja hiyo, lakini Waziri Masha alimuwahi kwa kuahidi kuwa mradi wa vitambulisho ungeisha mwaka jana na hivyo kuamua kumpa miezi sita kukamilisha mradi huo, la sivyo ataendelea na hoja yake.
Kwa mahesabu ya haraka, Shellukindo alitakiwa kuwasilisha hoja hiyo katika Bunge la mwanzoni mwa mwaka huu.
Lakini jana, Shellukindo aliibuka na hoja mpya wakati alipoeleza kuwa ameamua kusitisha msimamo wake huo kwa muda baada ya rais kuingilia kati.
"Hilo suala nimekuwa nikilifuatilia na wakati wa kamati za Bunge tuliambiwa rais ameagiza suala hilo la vitambulisho vya taifa lifanyiwe kazi haraka," alisema Shellukindo.
"Nimefuatilia mwenyewe NIDA na wizarani na nimeona kazi inaendelea vizuri, lakini kama kutakuwa na kitu kimeenda tofauti, msimamo wangu utabaki palepale," alisema mbunge huyo machachari.
Alisema uchunguzi wake umebaini kuwa baada ya Rais Kikwete kutoa agizo hilo, mchakato wa vitambulisho vya taifa unaendelea vizuri na zabuni zinaendelea kushughulikiwa.
Masha anatuhumiwa kuchelewesha mradi huo kutokana na kudaiwa kuingilia mchakato wa zabuni kwa kuhoji sababu za kampuni ya Sagem Securite kuachwa kwenye hatua za awali na tuhuma kwamba kampuni ya ushauri wa kitaalamu ya Gotham International kupewa tena katika mazingira tata.
Kitendo cha Masha kinaelezewa kuwa ni kukiuka taratibu za Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.
Masha ameshakana tuhuma zote na pia kueleza kuwa alichofanya ni kutaka malalamiko ya kampuni zilizokuwa kwenye zabuni yasikilizwe.
Gotham International nayo ilijitokeza na kujitetea kwamba haikupendelewa wala kupata kazi hiyo katika mazingira tata.
Katika mahojiano na gazeti hili mjini Dodoma, Shellukindo ambaye alihoji ni lini mradi huo utakamilika, alisema hana tatizo na Waziri Masha, lakini msukumo wake mkubwa unalenga kuona mradi huo nyeti unakamilika.
Shellukindo alisema wakati huo mjini Dodoma kuwa Waziri Masha hawezi kukwepa lawama kwamba anakwamisha mradi huo, kwani hana sababu za msingi kuingilia mchakato wake wakati Sheria ya Manunuzi ya Umma haimtambui.
Kwa mujibu wa Shellukindo, kutokana na kuwa waziri mwenye dhamana, Masha hakupaswa kuingilia mchakato huo hasa baada ya kupitishwa na Baraza la Mawaziri, badala yake alitakiwa kupata maelezo kutoka kwa katibu mkuu wa wizara ambaye ndiye mwenyekiti wa mchakato.
Shellukindo alidai kuwa mgogoro unaogubika mchakato wa vitambulisho ni wa kimaslahi na kumtuhumu Waziri Masha kuwa angependa mzabuni aliyepatikana na kupitishwa na Baraza la Mawaziri, Gotham asifanye kazi hiyo.
"Yeye anasema haridhiki na Gotham wakati amepitishwa na baraza la mawaziri. Kuna hasara nyingi ambayo taifa linaweza kupata kwa kumuondoa Gotham: Anaweza kuweka kizuizi cha mradi huo mahakamani, kujitoa katika mikataba mingine yote na kuomba fidia kwa usumbufu," alieleza Shellukindo.