36.-(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika
Katiba hii na ya sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na
mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna
mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika
nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za
idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika
kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika
utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo
zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbali
zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuzi
unaofanywa na Rais.
(3) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (2), masharti
mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya sheria yoyote
inayohusika, mamlaka ya kuwateua watu wengine wote
wasiokuwa viongozi wala watendaji wakuu, kushika nafasi za
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na pia mamalaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka, yatakuwa mikononi
mwa Tume za Utumishi na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na
kupewa madaraka kuhusu nafasi za madaraka kwa mujibu wa
Katiba hii au kwa mujibu wa sheria yoyote inayohusika.
(4) Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa
kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya
watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.