Kukithiri ufisadi:Mzee Msuya avunja ukimya
Habari Zinazoshabihiana
Kingunge avunja ukimya kukosa Kamati Kuu CCM 11.11.2007 [Soma]
'Watakaojihusisha na rushwa ya ngono sasa kukiona' 20.01.2007 [Soma]
Mama Karume avunja ukimya,awashukia wanasiasa wenye tamaa 06.04.2008 [Soma]
*Ataka wahusika waburutwe kortini
*Asema hata vigogo wasionewe haya
*Amkumbusha JK mbinu za Nyerere
*Akerwa na mjadala wa Zanzibar nchi
Na Hassan Abbas
WAZIRI Mkuu wa zamani na Makamu wa Kwanza wa Rais, Mzee Cleopa David Msuya amelazimika kutoka katika maisha yake ya ustaafu na kuvunja ukimya akilithibitishia Majira Jumapili kuwa anakerwa kuona hakuna hatua za haraka zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa rushwa na ufisadi nchini.
Mzee Msuya aliyepata kuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tofauti akifanyakazi katika wadhifa huo na Marais, Julius Nyerere na baadaye Ally Hassan Mwinyi kabla ya kustaafu siasa Oktoba 29, 2000 alisema bila taifa kuchukua hatua za haraka dhidi ya matatizo yaliyopo, nchi itaelemewa.
Moja ya mijadala mikubwa iliyoligubika Taifa hivi sasa ni juu ya hatua walizochukuliwa watuhumiwa wa ufisadi uliofanyika kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambako kiasi cha sh. bilioni 133 ziliibwa.
Akizungumza kwa hisia na kuonesha wazi kupata wasiwasi juu ya hatma ya taifa hili aliloshiriki kulijenga akifanyakazi tangu siku za mwanzo za uhuru, Mzee Msuya katika mahojiano hayo maalum yaliyofanyika nyumbani kwake Upanga, Dar es Salaam katikati mwa wiki hii, amesisitiza staili hiyo lazima iachwe, kama nchi inataka kupiga hatua.
"Kuna mijadala mingi sana inaendelea kwa sasa, haya ya watumishi wa umma kuhusishwa na rushwa ni sehemu tu ya matatizo tuliyonayo, lakini kubwa zaidi ni kwamba inachukua muda mrefu sana mambo haya kushughulikiwa," alisema.
Mjadala mwingine uliolitikisa taifa ni ule wa zabuni ya kufua umeme wa dharura iliyopewa kampuni ya Richmond ambayo baadaye ilibainika haikuwa na uwezo wa kitaalamu wala fedha na kuibua kashfa nzito iliyosababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa.
Akizungumza bila kutaja kashfa yoyote moja kwa moja,Mzee Msuya alisisitiza kuwa zipo mbinu rahisi za kupambana na wala rushwa Serikalini. "Katika utawala bora kuna utawala wa sheria, huu ukitumika ipasavyo haki itaonekana inatendeka.
"Utawala wa sheria ukifuatwa unasaidia uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma. Mfumo huu utasaidia kupambana na wala rushwa hata kama ni vigogo. Kama mimi Msuya ninatuhuma za rushwa ichunguzwe na kisha nipelekwe mahakamani ukweli ukajulikane, " alisema na kuongeza:
"Lakini mnapojenga staili ya uongozi ambapo kila jambo linaibuka na watu wana tuhumiana hakuna hatua zinazochukuliwa, mijadala inaendelea tu mitaani, hatuwezi kujenga taifa, niseme wazi sioni mustakabali mwema huko baadaye."
Alipotakiwa kueleza uzoefu wake wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere katika kushughulikia kashfa nzito, Mzee Msuya alisema Mwalimu hakuruhusu wala rushwa kutamba wala kuendekeza mijadala.
"Linapoibuka suala zito la kitaifa, kuna wakati Mwalimu alikuwa akiunda tume kimya kimya kuchunguza. Baada ya kupata ukweli alikuwa akitafuta siku ya kulizungumzia suala hilo na kutangaza hatua alizochukua kisha analiambia taifa kuwa mjadala huo umekwisha watu waendelee kuchapa kazi.
"Kwa staili hii Taifa wakati wa Mwalimu lilikuwa haliingii katika mijadala isiyokuwa na tija kama inavyoonekana sasa," alisisitiza.
Akizungumzia mjadala wa Zanzibar kuwa nchi, Mzee Msuya alisema huo ni mfano mwingine wa mijadala ambayo imekuwa ikimsikitisha.
"Kama nilivyosema awali, mjadala wa Zanzibar nao umeonesha ni kwa kiwango gani taifa letu linakwenda kubaya. Ukitazama watu walivyokuwa wakitumia nguvu katika mjadala huo unashangaa.
"Mjadala huo haukuwa na tija yoyote kwa taifa kwa sababu mwaka 1964 mtu yeyote mwenye akili timamu anafahamu kuwa ziliungana nchi mbili zenye mamlaka kamili na kuzaliwa nchi moja Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar na baadaye ikaja kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Wanaodai Zanzibar ni nchi waseme bayana wanachokitaka kuliko kujificha katika mjadala huo. Kwa nini hawasemi kuwa Tanganyika nayo ni nchi. Kwa mtazamo wangu mjadala huu umeonesha tatizo kuu la kitaifa tulilonalo kwa sababu tulijadili suala lililo wazi-Zanzibar kama Tanganyika zote si nchi," alisema mwanasiasa huyo ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo la Mwanga, Kilimanjaro.
Alisema analiombea dua taifa lipate viongozi bora watakaoendelea kulinda misingi iliyowekwa na waasisi na watakaokuwa makini katika kupambana na changamoto zinazojitokeza.
Wasifu wa Mzee Msuya
*Januari 4, 1931: Alizaliwa Chomvu, Usangi wilayani Mwanga, Kilimanjaro.
*1952-1955:Chuo Kikuu cha Makerere (baada ya kufaulu kutoka sekondari ya wavulana Tabora) alikotunukiwa Shahada ya Sanaa akibobea katika Historia, Sayansi za Siasa na Jiografia.
*Januari 11, 1959: Alifunga ndoa na Bibi Rhoda Christopher ambaye kwa sasa ni marehemu.
Nyadhifa za kisiasa
*1964-1972-Alikuwa Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali ikiwemo Maendeleo ya Jamii,Ardhi na Makazi,Uchumi na Mipango na Wizara ya Fedha.
*1972-2000-Alikuwa Mbunge wa Mwanga kwa vipindi tofauti ambapo pia alipata kuwa Waziri katika wizara za Fedha (1972-1975), Viwanda (1975-1980), Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (1980-1983) ambapo aliushika tena wadhifa huo chini ya Serikali ya Awamu ya Pili kuanzia Desemba 1994 hadi Novemba 1995.
*Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 alikuwa mmoja wa wagombea watatu wa Urais kupitia CCM waliongia hatua ya mwisho akiwa na Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa aliyeshinda.
Mzee Msuya pia alikuwa mwanachama wa TANU na baadaye kuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa CCM.
Kwa sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na anajishughulisha na shughuli binafsi za biashara, kilimo na ushauri.
Source: Majira
Kasheshe, nadhani kama wazee wengi wastaafu hivi ndio wanavyoona hapo juu naona rais wetu kuna mahali amepotoka.