Kuna taarifa humu juu ya Tanzania kupewa au kutopewa mkopo na WB wa jumla ya $500M kwa ajili ya kuwezesha shughuli ktk sekta ya elimu nchini
Sababu za kutopewa zinasemwa kuwa ni kauli ya Rais Magufuli ya mwaka 2018 yenye kila dalili za kumbagua Mtoto wa kike kielimu kwa sababu ya kupata mimba na kuzaa
Sambamba na kauli hiyo, sababu nyingine inayosemwa ni Sera ya elimu inayo sapoti kauli hii ya Rais Magufuli kumbagua mtoto wa kike ambaye kwa bahati mbaya hubeba ujauzito wakiwa shuleni na hivyo kukosa fursa hiyo.
Napenda tujiulize swali hili, kuwa, hiki kinachosemwa ni hali halisi kweli hapa nchini kwetu? Kama sivyo, kwanini viongozi hawaelewi hili?
Ninavyofahamu mimi kama nchi, ipo mifumo na fursa kwa kila mtu wa umri wowote na jinsia yoyote kujiendeleza kielimu kadiri ya uwezo wake.
Mathalani Tanzania tunao mfumo wa rasmi wa elimu unaoongozwa na sheria mbalimbali kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu.
Aidha tunao mfumo mwingine wa Elimu ya watu wazima (EWW). Huu una taratibu na sheria zake zinazousimamia. Unamhusisha mtu yeyote ambaye hakupata fursa katika mfumo rasmi kujiendeleza kielimu kupitia njia hii.
Aidha tunao mfumo wa MEMKWA ambao unahusisha watoto wenye umri uliokwisha kuzidi kuanza darasa la kwanza kuwa na madarasa yao maalumu.
Kwa upande mwingine ni kweli kabisa kuwa, zipo sheria na miongozo inayoelekeza kuwa mwanafunzi wa kike wanaopata mimba shuleni (msingi, sekondari na baadhi ya vyuo), anaondolewa shuleni ili akalee mimba na kujifungua. Hili ni la kawaida na naamini liko ktk nchi zote duniani zikiwemo za Ulaya na Amerika.
Basically, huu ni utaratibu wa kawaida wenye nia njema kabisa kwa sbb si afya kimaadili kuwachanganya wanafunzi wajawazito na wasio wajawazito darasa moja.
Na kuondolewa kwa mwanafunzi huyu si kwamba ndiyo anakuwa ameshanyimwa kabisa fursa ya kujiendeleza kielimu. Hili sio kweli kama ambayo nimeeleza hapo juu.
Akishajifungua na kuonesha nia ya kuendelea na masomo, basi anaweza kujiunga na darasa la Elimu ya Watu Wazima (EWW).
Na kiukweli ipo mifano ya watu wengi waliosoma kupitia mifumo hii na wanajivunia elimu yao na maarifa waliyoyapata na wengine wana nafasi nzuri tu maofisini.
Sasa tatizo linaweza kuwa wapi? Kwanini kuna malumbano kati ya serikali na WB juu ya mkopo huu kana kwamba kweli watoto wa kike wanabaguliwa kwenye maswala ya elimu? Mimi nadhani tatizo liko kwenye maeneo haya:
1. Rais John Pombe Magufuli kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya sheria na mifumo ya elimu ktk nchi yake kiasi ambacho anajikuta anatoa kauli ngumu na kavu inayoleta madhara makubwa ndani na nje ya nchi!
2. Katika Wizara ya Elimu, ipo idara/kurugenzi ya Elimu ya Watu Wazima (EWW) na ndivyo ilivyo hadi nchini ktk ngazi ya halmashauri. Kwa nini hawa wasiulimishe umma juu ya jambo hili linalotaka kuelekea kutukosesha mkopo wa fedha za kugharamia sekta ya elimu nchini?
3. Mifumo hii EWW na MEMKWA bado ni dhaifu sana kwa kutopewa kipaumbele kifedha, vifaa, miundombinu hususani majengo na walimu. Serikali ikipata fedha hii ya mkopo na kwa kutumia fedha zake za mapato ya ndani, iifanye mifumo ifanye kazi yake kwa ukamilifu wake ili watu wengi wapate fursa ya kusoma na kujiendeleza kielimu!
4. Viongozi wajue sheria na miongozo mbalimbali katika maeneo yao wanayoyasimamia. Wajiupeshe na kutoa taarifa rasmi kwa matamko ya majukwaani kwenye masuala nyeti pasipo kujiandaa na kuwa na taarifa za kutosha juu ya jambo wanalolitolea tamko.