Tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha 7.9 limepiga katikati mwa Uturuki na Kaskazini-Magharibi mwa Syria siku ya Jumatatu, na kuua maelfu ya watu na kujeruhi mamia wakati majengo yakiporomoka
Uokoaji wa walionusurika kwenye vifusi katika eneo hilo lenye theluji unaendelea.
Shirika la maafa la Uturuki limesema watu 76 wameuawa, na 440 wamejeruhiwa, wakati mamlaka ilipotawanya timu za uokoaji na kusambaza ndege katika eneo karibu na mji wa Kahramanmaras, huku ikitangaza "kiwango cha 4 ya uokoaji" inayotaka usaidizi wa kimataifa.
Vyombo vya habari vya serikali ya Syria vimesema kuwa idadi kubwa ya majengo yameporomoka katika jimbo la Aleppo, huku chanzo cha habari katika utumishi wa umma cha Hama kikisema kuwa majengo pia yameporomoka huko.
UPDATES
Vifo zaidi ya 100 upande wa Uturuki, 39 Upande wa Syria huku watu wengi wakiwa bado chini ya vifusi.
Italia yaonya kuwa tsunami yaweza tokea kutokana na tetemeko hilo
UPDATE: WALIOFARIKI KWA TETEMEKO LA ARDHI UTURUKI NA SYRIA WAFIKIA 1500
Wakati shughuli za Uokoaji zikiendelea baada ya kutokea Tetemeko lenye kipimo cha Richa 7.8, zoezi hilo linaanza kukabiliwa na ugumu kutokana na Mamia ya Watu kunaswa kwenye vifusi
Zaidi ya watu 5000 wamejeruhiwa na wengine bado hawajulikani walipo na wana hali gani. Nchi za Cyprus, Misri na maeneo ya Lebanon yamepata Mtikisiko kutokana na Tetemeko hilo.
---
UPDATE: IDADI YA WALIOFARIKI KWA TETEMEKO LA ARDHI UTURUKI YAFIKIA WATU 1,800
Vifo zaidi vinazidi kuripotiwa kufuatia Tetemeko la ukubwa wa Richa 7.8 kuzipiga Uturuki na Syria usiku wa kuamkia Februari 6, 2023 na kuporomosha mamia ya Majengo wakati watu wakiwa wamelala
Idara ya Dharula Nchini Uturuki imeomba msaada kwa Jumuiya za Kimataifa baada ya kutokea Matetemeko mengine mawili yenye kipimo cha 7.5. Uingereza tayari imetuma Wataalamu 76 wa Utafutaji na Uokoaji.
UPDATE: Zaidi ya watu 2,300 wamepoteza maisha huku waokoaji wakiendelea kutafuta manusura
Zaidi ya watu 2,300 wamepoteza maisha huku waokoaji wakiendelea kutafuta manusura kutoka chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka kutokana na Tetemeko kubwa la ardhi lililozikumba Uturuki na Syria leo Februari 6, 2023 na kuacha majeruhi zaidi ya 10,000 na wengine wakiwa hawana makazi.
Staa wa zamani wa Chelsea na Newcastle za England Christian Atsu (31) Raia wa Ghana ambaye kwa sasa anacheza Hatayspor ya Uturuki amekwama kwenye kifusi cha jengo lililoanguka baada ya tetemeko la ardhi.
Harakati za kumuokoa Atsu zinaendelea lakini kwenye tetemeko hilo lililotokea leo nchini Uturuki mitandao mbalimbali imeripoti kuwa watu zaidi ya 1400 wamefariki Dunia.
Atsu ambaye alijiunga na Chelsea 2013 na kuishia kutolewa kwa mkopo Newcastle na Everton, alikuwa sehemu ya mchezo wa Ligi Kuu Uturuki jana kati ya timu yake ya Hatayspor dhidi ya Kasimpasa ambapo aliisaidia kupata ushindi wa 1-0 akifunga goli dakika ya 90+
UPDATE: Matetemeko mengi madogo 100 yatokea baada ya lile kubwa
Takriban matetemeko 100 yenye ukubwa wa 4.0 au zaidi yametokea tangu tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 7.8 lilipotokea Kusini mwa Uturuki Jumatatu asubuhi saa za huko, kulingana na Utafiti wa Jiolojia wa Kituo cha Marekani.
Kadiri muda kutoka kwa tetemeko la ardhi la asili unavyoongezeka, frequency na ukubwa wa matetemeko ya baadaye hupungua.
Hata hivyo, matetemeko ya kipimo cha 5.0 hadi 6.0 bado inaweza kutokea nchini humo na kuleta hatari ya uharibifu zaidi. Hii inaleta tishio kwa zoezi la uokozi linaloendelea na kwa timu za uokoaji na manusura.
UPDATE: WALIOFARIKI KWA TETEMEKO LA ARDHI UTURUKI, SYRIA NI ZAIDI YA WATU 4,300
Ripoti za idadi ya waliofariki inaendelea kuongezeka kufuatia Tetemeko la Ardhi la ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Richa, kuzipiga Uturuki na Syria usiku wa kuamkia Februari 6, 2023.
Watu 2,921 wameripotiwa kufariki Nchini Uturuki huku zaidi ya 15,000 wakijeruhiwa, upande wa Syria imeripotiwa waliofariki ni watu 1,444; ikifanya jumla ya vifo kufikia 4,365, inaelezwa idadi inatarajiwa kuongezeka.
Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol amesema Nchi yake itatuma timu ya waokoaji na vifaa vya matibabu ya dharura Nchini Uturuki ili kusaidia uokoaji unaoendelea.