Maelfu wakubali mvua iwanyeshee kumsikiliza Kabwe Dar
*Asema mkataba ulisainiwa Hotelini London
Michael Matemanga, RCT na Boniface Meena
MAELFU ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam jana walijitokeza katika mapokezi na maandamano ya kumpokea Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe, aliyesimamishwa ubunge hadi Januari mwakani. Maandamano hayo, ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka kambi ya upinzani, yalianzia eneo la Ubungo, baada ya Zitto Kabwe kuwasili akitokea mjini Dodoma. Maandamano hayo yalipitia barabara ya Morogoro na kuishia katika viwanja vya Jangwani ambako Kabwe alihutubia wananchi na kufafanua juu ya kile kilichotokea bungeni baada ya kuwasilisha hoja yake binafsi na baadaye kusimamishwa.
Katika hotuba yake kwa wananchi hao waliokusanyika Jangwani, Kabwe alisema iwapo mkataba wa madini wa mradi wa Buzwagi ungesainiwa nchini Uingereza ndani ya ubalozi wa Tanzania nchini humo, kusingekuwepo na tatizo. Alisema iwapo Kamati Teule ya Bunge aliyoomba iundwe kuchunguza mkataba huo uliosainiwa jijini London ingeundwa, ingegundua kuwa mkataba huo ulisainiwa hotelini.
"Niwaambieni tu ndugu zangu, hiki ni kitu ambacho sikukisema hapo mwanzo lakini kama kamati ingeundwa ingegundua kuwa mkataba huo ulisainiwa hotelini na hoteli yenyewe inaitwa hoteli ya Churchill iliyoko jijini London," alisema Kabwe. Alisema wakati Waziri Nazir Karamagi anasaini mkataba huo, Rais alikuwa hajui kama waziri wake alikwenda huko kusaini mkataba kinyume na maelekezo yake.
"Tukumbuke kuwa rais aliwahi kutangaza kuwa serikali itapitia mikataba yote ya madini, Mei mosi mwaka 2006 wakati wa sikukuu ya wafanyakazi na alikumbushia suala hilo, tarehe 17 mwezi Julai mwaka huo huo wakati Waziri wa Nishati na Madini wakati huo akiwa Dk Ibrahim Msabaha, ambaye alitangaza azma ya serikali kusitisha kusainiwa kwa mikataba ya madini na rais alipokuwa Afrika Kusini mwezi Februari 6 mwaka huu, huku akisema mikataba inaendelea kupitiwa, sasa hili inakuwaje?" alihoji Kabwe.
Alisema kutokana na hilo, wakati umefika kusimama kidete kuhakikisha rasilimali za Watanzania zinalindwa ili kuondokana na umasikini uliokithiri, huku akimtaka Kikwete kuangalia nyumbani kwake kwani kumeingiliwa na watu ambao hawajui kujenga nchi zaidi ya kushibisha matumbo yao.
"Rais aisafishe serikali yake mara moja ili ifanye kazi kwa maslahi ya wananchi, kwani wasaidizi wake wanamkosesha imani na Watanzania," alisema Kabwe. Kabwe alimaliza kwa kusema kuwa, mamlaka yote ya dola yapo mikononi mwa wananchi na Bunge ni wawakilishi wao tu, hivyo imani ikikosekana bungeni ni hatari kubwa na wajibu uko mikononi mwa wananchi.
Naye Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Wilbroad Slaa, ambaye alipanda jukwaani baada ya Kabwe kumaliza kuhutubia, alielezea suala la yeye kuamua kuichomoa bungeni hoja yake kuhusu ubadhilifu katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na kuikabidhi kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kuifanya kuwa hoja ya kisiasa isiyopelekwa tena bungeni.