Viva, Kabwe viva!
Member of Parliament for Kigoma North (CHADEMA), Zitto Zubery Kabwe shakes hands with Dar es Salaam residents who turned up to welcome the MP who has been suspended to attend the parliamentary seatings for four months. Picha kutoka IPPMEDIA.
Deus Bugaywa
MOJA ya misingi ya demokrasia ni pamoja na kuwa na mihimili mitatu ya dola inayofanya kazi moja ya kumhudumia mwananchi, lakini ambayo ni tofauti sana kutoka mhimili hadi mhimili.
Serikali kama moja ya mihimili hiyo ni mtendaji mkuu wa kazi za siku kwa siku za nchi, na Bunge kwa upande wake ni mtunzi wa sheria ambazo zinatafsiriwa na Mahakama ambao ni mhimili mwingine wa dola.
Bunge, lakini kwa kupitia uhalali wake wa kuwa sauti ya wenye nchi, wananchi, kwa serikali yao likapewa heshima ya kusimamia, kudhibiti na kuhoji pale inapobidi juu ya mienendo mbalimbali ya serikali katika mchakato wake wa kutoa huduma kwa jamii, yaani wananchi.
Hivyo basi katika mihimili inayotegemewa kuifuatilia na kuibana serikali katika kila jambo linalotia shaka au kuleta maswali yasiyo na majibu kwa wananchi ni Bunge, kwa kuwa lenyewe ndiyo sauti yao kwa serikali.
Wabunge kwa maana hiyo hawapaswi kwa namna yoyote ile kubembelezana na serikali pale masilahi ya nchi yanapokuwa yanawekwa katika mazingira tata, na kuibua hisia zisizo nzuri miongoni mwa wananchi, kwa kuwa wao wanawajibika moja kwa moja kwa mwananchi.
Kuchaguliwa kwa wabunge kupitia vyama bado hakuondoi jukumu lao la kuwa wasemaji wa wananchi kwa serikali yao, wanapaswa wahoji, wadadisi na wadurusu lolote, popote ili mradi tu jambo hilo lina masilahi ya nchi.
Vile vile serikali inayojiamini kuwa ni mtumishi mwadilifu kwa watu wake wala haina haja wala sababu ya kuhofia Bunge au kuweka mashinikizo ya kuathiri shughuli za Bunge kwa kuwa wanajua walichokifanya ni chema na kwa nia njema na kwa manufaa ya taifa, hawaogopi hoja wa kuulizwa chochote juu ya utendaji wao, wala hawana kitu cha kuficha.
Ukiona serikali inafanya kila linalowezekana kujenga ‘uswahiba' na Bunge kwa gharama ya Bunge kuhama katika wajibu wake wa msingi wa kutetea masilahi ya nchi bila kujali mtoa hoja ni wa chama gani, basi ujue hapo kuna mushikeli na yamkini kuna jambo ambalo linafichwa.
Baadhi ya wabunge wa chama tawala wamenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari wakitamka hadharani kwamba wanazibwa midomo, kwamba linapokuja suala la kujadili hoja mahsusi bungeni kwa maana ya kujadili masuala ya masilahi kwa wananchi na taifa lao, haijalishi wao matatizo hayo yanawahusu na yapo mengi majimboni kwao kiasi gani, wanatakiwa tu waunge mkono hoja ilimradi tu wao ni wa chama tawala na chama ndicho chenye serikali.
Ndiyo maana haikushangaza sana na badala yake iliwaudhi watu wengi, kiasi cha kuwapa tabu kuamini kama mambo haya yanaweza kutendeka Tanzania, pale Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa Zito Kabwe, alipotoa hoja ya kutaka iundwe tume kuchunguza mazingira yaliyopelekea Waziri wa Nishati na Madini kusaini mkataba wakati kukiwa na kauli ya serikali kusitisha utiaji saini wa mikataba mipya wakati hii ya zamani ikiwa inapitiwa na zaidi sana mkataba huo kusainiwa nje ya nchi.
Siku ya mjadala kwa sababu ya majukumu sikupata nafasi ya kuangalia mjadala huo moja kwa moja, lakini namshukuru rafiki yangu mmoja aliyeniambia kama sikuona mjadala huo wa hoja binafsi ya Zito, ilikuwa lazima niuone kwa gharama yoyote ile.
Kwa maelezo yale ya mwanaharakati mwenzangu, nilidhamiria kutimiza azima hiyo, hivyo nililazimika kuangalia marudio usiku saa nne, niliweza kufuatilia mjadala huo mpaka saa saba kama na robo hivi, lazima niseme ukweli usiku huo nilikuwa na usingizi wa mang'amu ng'amu, nilikuwa nashangaa kama kweli nchi hii tumefika hapo.
Nilidhani ni mimi tu, asubuhi tu nikakutana na mama mmoja ambaye katika mazungumzo aliniambia mumewe naye kama mimi alikuwa anafuatilia kikao kila usiku ule, mwenzangu alienda mbali, yeye shinikizo la damu lilipanda na asubuhi hiyo hakuweza hata kwenda kazini kwa ajili ya kutuliza hali iliyosababishwa na mijadala hiyo.
Mpaka kufika mchana wa siku hiyo, nilishapokea simu na ujumbe mfupi mwingi ukihoji ni nini kinafanyika na Tanzania inakwenda wapi, mimi kwa vile kazi ni hii kuujulisha umma hiki na kile, nahisi ujumbe umefika.
Tukirudi kwenye mada nashindwa kupata tafsiri sahihi ya kulidanganya Bunge ni ipi na inatumika wapi na kwa nani, Mheshimiwa Zitto amepewa adhabu na Bunge kwa kosa la kulidanganya Bunge najiuliza sipati jibu, kulidanganya Bunge kunaanzia wapi na kunaishia wapi.
Nakumbuka wakati akichangia mjadala wa bajeti, Mbunge wa Nzenga, Lucas Serelii, alitishia kuzuia bajeti za Wizara ya Miundombinu na Waziri Mkuu kwa kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha uliotangulia huu, wizara hiyo ilisema bungeni katika mwaka wa fedha huo ingeweza kujenga barabara kadhaa jimboni kwake na haikufanya hivyo.
Mheshimiwa huyu alitishia hivyo kwa kuwa aliahidiwa na waziri, lakini hakutimiza ahadi hiyo, ndiyo maana alitishia kuzuia bajeti ya wizara hiyo kwa kuwa alidanganywa na kwa maana hiyo Bunge lote lilidangaywa, na hatukusikia hata harufu ya hoja ya kumwadhibu waziri kwa kuwa kutoa ahadi na kutoitimiza ni uongo.
Wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Waziri Karamagi alibanwa kuhusu ahadi ya wizara yake kupeleka umeme huko Peramiho, kwamba alichoahidi sicho na kwamba yeye alidanganya Bunge na wananchi wa Peramiho, mpaka waziri mkuu walipoingilia kati kuokoa jahazi, hatukuona hata dalili tu ya kumchukulia hatua.
Haya yote tulidhani ni busara za Spika zinatumika kwa kuwa alishasema mwenyewe mapema kwamba Bunge lina kanuni nyingi sana zilizopitwa na wakati na hivyo inapokuwa lazima busara za Spika zingetumika ili kurekebisha hali ya mambo, je, busara za Spika zilikuwa wapi wakati wa hoja ya Mudhihir dhidi ya Zitto?
Hoja iliyotumika kumwadhibu ina uzito gani ukilinganisha na yale yaliyoibuliwa na maelezo ya mtoa hoja tangu wakati akichangia bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini?
Je, si kweli kwamba wengi wa wabunge hata wa CCM hawakujua kwamba mgodi wa Buzwagi umeuzwa, tena kwa mkataba kusaniwa nje ya nchi, asingekuwa Zito na utundu wa udadisi wake si mpaka leo, tungekuwa gizani wakati mali yetu imeuzwa bila wenyewe kuwa na taarifa achilia mbali kujua mkataba wa uuzwaji wake?
Hili busara za Spika hazikuliona mpaka akasimamia kidete kusimamishwa kwa mbunge huyu? Katika hatua nyingi za mjadala huo Spika alisikika akisema kuwa yeye anafuata kanuni tu, je, si huyu huyu aliyetuahidi kutumia busara zake kwa kuwa kanuni nyingi zilikuwa zimepitwa na wakati?
Je, Spika aliona ni vyema sana kutumia busara zake katika kumuepusha na adhabu Mheshimiwa Malima wakati alishasema uongo bungeni, tena uliothibitishwa na tume iliyotumia shilingi milioni 100 za walipa kodi wa nchi hii, lakini busara hizo zikakosekana kwenye suala la Zitto ambalo mbali na uongo wake kutothibitishwa bila kuacha shaka yoyote, lakini pia hoja yake imewafungua macho Watanzania na kuilazimu Wizara ya Nishati na Madini kutoa maelezo ambayo katika hali ya kawaida haikuwa tayari kuyatoa mpaka hoja hiyo ilipoibuliwa?
Je, Waziri Chenge pamoja na ukongwe wake bungeni kwa kuwa mwanasheria wa serikali kwa miaka 10 na zaidi kama mwenyewe alivyosema, tumweke kundi gani anapojenga hoja ya kitoto kwamba Zito anataka kuganga njaa, eti anataka tume iundwe ili apate posho za tume, Spika hakuona kama hili ni tusi na kudhalilishwa kwa mtoa hoja?
Anataka kutwambia nini, kwamba wana CCM wanapounda tume lengo huwa ni kuganga njaa na kupata posho na si kuchunguza kile kilichoundiwa tume? Huenda ndiyo maana haishangazi kuwa tume nyingi zinazoundwa chini ya serikali majibu yake hayawekwi hadharani, pengine Mheshimiwa Chenge alikuwa anatufungua macho.
Hivi katika hili nani alikuwa na nia njema kwa taifa hili, Zitto aliyekuwa anahoji uharaka wa dharura kiasi hicho wa kusaini mkataba wa kuuza mgodi wa dhahabu kama vile ni nyanya mbivu zinazotarajiwa kuanza kuoza kesho au Chenge ambaye, kama mwanasheria mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu aliyehusika moja kwa moja na kutiwa saini kwa mikataba mibovu isiyokuwa na faida na ambayo tunairekebisha sasa?
Lazima ifike mahali tukubali kuweka masilahi ya taifa letu mbele bila kujali sana sisi ni wapenzi au mashabiki wa nani, na tuna kitu kimoja tu kinachoweza kutufikisha hapo, nayo ni kuwa na maadili yenye nidhamu za Kitanzania ambayo ndiyo yatasaidia sana kutuongoza kufikia malengo yetu kama taifa.
Haya yatakuwa kinga ya watu wetu na taifa letu dhidi ya kila aina ya mbinu chafu na unafiki uwao wote, kwa kuwa ni vigumu sana kuwa na katiba inayokidhi mahitaji yetu bila kutumiwa kwa manufaa binafsi na baadhi ya wajanja ambao si haba nchi hii, ni maadili na miiko ya Kitanzania tu ndiyo inaweza kuliokoa taifa hili.
Ukiangalia kwa mapana hoja ya Kabwe ilikuwa imejikita katika muktadha huo kwamba inawezekana kabisa sheria haikatazi au haisemi chochote, lakini tumueleweje waziri wetu anapokwenda kusaini mkataba wa kuuza mgodi wetu, nje ya nchi, na anakuja anakaa kimya kana kwamba Tanzania ni kampuni yake au familia yake anayoiendesha kwa matakwa binafsi?
Wakati huo huo kila mtu anajua uzoefu wetu na sekta ya madini, kila panapoingiwa mkataba serikali hujifanya haisikii, wote tunakumbuka yaliyojiri katika mgodi wa Bulyanhulu wakati wa hatua za awali za ubinafsishaji wake, Tundu Lissu na LEAT wanalielewa vizuri hili, hakuna asiyejua misukosuko ya wananchi wa Mtakuja huko Geita na fidia zao, halafu leo waziri anasaini mkataba wa madini katika mazingira tata tena nje ya ardhi ya Tanzania na hatuambii wenye mali juu ya kuuzwa kwake, anaonekana ‘shujaa na mzalendo halisi' tunaipeleka wapi nchi hii?
Safi sana! CCM kama hiyo ndiyo njia mliyochagua sawa, lakini mwisho wa siku hii ni mali ya Tanzania si ya CCM, mnaweza kuwa nambari wani lakini linapokuja suala la mali za Tanzania hakuna nmbari wani wala ziro, wote kama raia tuna hisa sawa za mali ya nchi hii Muumba aliyopenda iwe ya kila raia wa ndani ya mipaka ya taifa hili, wala msidhani kuna hali ya kudumu katika maisha haya, hakuna kinachodumu isipokuwa mabadiliko.
Zitto aliwaeleza, akinukuu toleo la mwisho la jarida la Cheche kwamba ‘You can ban organizations, you can liquidate people but revolutionary ideas never die' huo ndio ukweli wa maisha kama zilivyo nguvu za uvutano (gravitational force) ukubali au ukate zenye zipo ili kuishi.
Katika hili la kusaini mkataba nje naomba wabunge waliopinga hoja ya kuundwa kamati teule ya Bunge na kuunga mkono hoja ya kufungiwa shughuli za Bunge Mheshimiwa Zitto watueleze, kimaadili ni sawa kwa waziri kufanya alivyofanya?
Yaani, kusaini mkataba mpya wakati kuna tamko la serikali kusitisha utiaji saini wa mikataba ambalo halijatenguliwa na kusaini mkataba nje ya nchi, wanataka kutuambia huo ndio uadilifu wa nidhamu za uongozi wa Kitanzania?
Wakati muasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, anawasilisha hoja bungeni ya kuundwa kwa Jamhuri ya Tanganyika Juni 28, 1968, kwa mujibu wa hansard za kikao hicho kipindi cha kwanza (1st session) anasema hivi kuhusu uadilifu, naomba nimnukuu kwa urefu kwa sababu ya unyeti wa suala hili.
"Kama taifa lisipokuwa na maadili yanayoiwezesha serikali kusema ‘Hatuwezi kufanya hivi, huu si Utanganyika' au watu kusema ‘Hatuwezi kuvumilia hili, huu si Utanganyika'. Kama watu hawana maadili ya namna hiyo haijalishi mnaunda katiba ya namna gani. Watakuwa siku zote ni waathirika wa udikteta.
"Tunachotakiwa kuendelea kufanya ni kujenga maadili ya taifa letu, muda wote kuendelea kujenga maadili ya taifa yatakayomwezesha kiongozi yeyote wa nchi kusema ‘Nina mamlaka ya kufanya hivi kwa mujibu wa katiba, lakini siwezi kufanya kwa kuwa huu si Utanganyika' au watu wa Tanganyika, kama wamefanya kosa kumchangua mwendawazimu kuwa kiongozi wao ambaye ana madaraka kikatiba kufanya XYZ, akitaka kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme ‘Hatukubali hili kutoka kwa mtu yeyote iwe ni kutoka kwa rais au rais kipeo cha pili.'"
Kwanini Mwalimu anasisitiza hili, ni kwa sababu wakati mwingine na hasa kwa mazingira kama yetu, ni vigumu sana kuwa na katiba isiyo na mianya ya kuruhusu watu kufanya lolote wanalotaka. Kinga pekee dhidi ya uhuni wa aina hii ni kuwa na maadili ya taifa ambayo si lazima yawe sheria lakini ambayo kwa akili ya kawaida tu yanatuwezesha kutambua kuwa hili ndiyo na lile siyo.
Ni utetezi dhaifu sana kuanza kutetea uozo ambao uko dhahiri kwa jina tu la kwamba eti katiba au sheria fulani haikatazi au hata haisemi kitu, ni kumkufuru Mwenyezi Mungu kwa kuacha kutumia kwa makusudi akili alizotupa kwa ajili ya kuutiisha ulimwengu.
Na kwa hatua ya Bunge ya kumsimamisha ubunge, naomba nimpongeze Kabwe kwa kuwa kwanza ametudhihirishia tofauti kati ya wabunge wanaodhamiria kuwa wabunge kwa ajili ya ubunge na wale wanaokwenda huko kwa masilahi, kwamba walikutishia posho na nusu mshahara, hongera kwa kuwakumbusha kwamba ubunge si posho au mshahara, ni kutetea masilahi ya nchi na wananchi wake.
Kama mzee Malecela alivyokuita kwamba wewe ni ‘mwiba', hata mimi namuunga mkono, kama wewe ni mtu makini utakosaje kuwa mwiba kwa Bunge ambalo limesahau wajibu wake na kuwa kama kamati ya chama?
Utakosaje kuwa mwiba kama wewe ni mzalendo halisi na mwanaharakati wa ukombozi halisi wa taifa hili katikati ya nchi ambayo hata mwasisi wake alikiri inanuka rushwa?
Wewe ni jasiri na Mtanzania daima, wewe ni tumaini la Tanzania ya leo na ya kesho ndiyo maana sipatia hata kigugumizi kusema VIVA, KABWE VIVA!
Mungu ibariki Tanzania, uilinde dhidi ya unafiki unaoitafuna!
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu; 0754 449 421 au barua pepe:
drbugaywa@yahoo.com