Zitto aanza na Malima
na Asha Bani
ADAM Malima, amekuwa mbunge wa kwanza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kurushiwa makombora ya hoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliyesimamishwa, Kabwe Zitto.
Malima alifikwa na kishindo hicho cha Zitto usiku wa kuamkia jana, wakati wa kipindi cha televisheni cha Je, Tutafika? Kinachoendeshwa na mwanahabari mkongwe na wa siku nyingi, Makwaia wa Kuhenga.
Akizungumza katika kipindi hicho cha mahojiano, Zitto alieleza kushangazwa kwake na kauli aliyoitoa Malima bungeni wiki iliyopita wakati akichangia hoja binafsi ambayo ilihitimishwa kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kusimamishwa ubunge kwa miezi mitano.
Malima katika mchango wake huo wa Jumanne ya wiki iliyopita, alimsifu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwa uamuzi wake kuweka mbele masilahi ya taifa kwa kusaini mkataba wa uchimbaji madini wa Buzwagi na Kampuni ya Barrick Tanzania.
Mbali ya hilo, Malima alimtaka Karamagi kutumia kasi yake hiyo hiyo kusaini mkataba wa uchimbaji wa gesi katika Jimbo lake la Mkuranga iwapo atapatikana mwekezaji mwingine wa aina ya Barrick.
Akizungumza katika kipindi hicho cha televisheni, Zitto alianza kwa kuhoji hoja hiyo ya Malima iwapo aliitoa kwa niaba ya wananchi wa Mkuranga au kwa niaba yake mwenyewe.
Mbunge huyo ambaye sasa amejijengea umaarufu mkubwa tangu asimamishwe na Bunge, alimtaka Malima na Watanzania kutambua kuwa mikataba ya aina hiyo imekuwa na atthari kubwa kwa uchumi wa taifa.
Akitoa mfano, Zitto alieleza kushangazwa kwake na makubaliano yaliyomo katika mkataba mmoja wa kutafuta mafuta katika maeneo mawili ya Tanzania, kule Mkuranga anakotoka Malima na Kigoma, kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Alisema chini ya mikataba hiyo miwili, serikali na wawekezaji hao wanaotafuta mafuta kutoka Ireland wamekubaliana kugawana mapato yatakayotokana na mafuta yatakayopatikana kwa uwiano wa asilimia 30 (zitakazokwenda serikalini) na 70 zitakazochukuliwa na mwekezaji huyo.
Zitto alisema jambo la ajabu ni kwamba kampuni hiyo hiyo ya uwekezaji, imeingia mkataba kama huo wa kutafuta mafuta nchini Kongo, ambako mgawanyo wa mapato yakakayopatikana ni asilimia 45 (kwa serikali) na 55 kwa mwekezaji.
Mbunge huyo kijana alieleza kushangazwa na Malima aliye tayari kuona mikataba mibovu ya namna hii inayoliibia taifa hata kwa kulinganishwa na mataifa mengine jirani ikisainiwa kwa kasi.
Mashambulizi hayo ya Zitto yanakuja siku chache tu baada yeye mwenyewe kuorodhesha majina ya wabunge 10 ambao atahakikisha anawashitaki kwa wapiga kura wao, akiwamo Malima, ambao walikuwa mstari wa mbele kumshambulia bungeni hata kufikia hatua ya Bunge kumsimamisha.
Aidha, Zitto aliwaeleza watazamaji wa televisheni hiyo kuwa, kamati ya kupitia mikataba ya Wizara ya Nishati na Madini ilikataa pendekezo la Karamagi la kusainiwa kwa mkataba wa Buzwagi, kabla waziri huyo hajafikia hatua ya kulazimisha kukubaliwa kwa matakwa yake.
Akijibu hoja hizo za Zitto ambazo zilikuwa na mwelekeo mmoja na zile zilizotolewa na Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Malima alisema mara nyingi wataalamu hulazimika kusaini mikataba katika mazingira magumu.
Pasipo kufafanua kuhusu hoja ya Zitto ya mgawanyo wa mapato katika mikataba hiyo, Malima alisema historia ya nchi za Ulaya kuzikandamiza nchi maskini ndiyo msingi wa kuwapo kwa uonevu wa namna hiyo.
Zitto kwa upande wake alipinga mtazamo huo wa Malima akisema viongozi wetu wamekuwa wakiingia mikataba, wakiweka mbele masilahi yao binafsi na kusahau yale ya wananchi, na akatoa mfano wa mkataba wa Buzwagi.
Alisema kuwa, mbali ya ufisadi kukithiri katika mikataba ya madini, Watanzania tumekuwa na tatizo la kutokuwa na uzalendo katika kuzilinda rasilimali zetu.
Zitto alisema ni jambo la kushangaza kwa serikali na wananchi kukaa kimya wakati mchanga wa madini ukisafirishwa nje ya nchi, kwa madai kuwa hapa nchini hakuna teknolojia ya kutosha ya kupata dhahabu kutoka katika mchanga huo.
Alisema wakati tukiambiwa hivyo, ni ajabu kwamba, vijana wanaoishi maeneo ya migodini hudandia katika malori yanayosafirisha mchanga huo kwenda nje na kuchota vifusi hivyo na kwenda navyo mitoni wanakosafisha na kupata dhahabu wanayoiuza.
Kwa hilo nashangaa kuona vijana wa Kahama huamua kupanda juu ya makontena hayo wakiwa na vikalai na kuanza kuuchota na kuumwaga chini baada ya hapo wanaenda kuchuja na kutenganisha na kupata dhahabu, sasa hiyo teknolojia ambayo Serikali inadai hatuna ni ipi? alihoji Zitto.
Naye Mbunge wa Karatu, Dk.Willibrod Slaa (Chadema), ametoa mwezi mmoja kwa serikali kuanza kufuatilia kile alichokiita ubadhirifu ndani ya Benki Kuu (BoT), kabla hajafikia hatua ya kulazimika kuwataja kwa majina wahusika wote katika kashfa hiyo.
Alisema anatarajia kutangaza majina hayo ya vigogo wanaomiliki makampuni ambayo yamekuwa yakifuja fedha za walipa kodi kupitia BoT, Septemba 15 mwaka huu, katika viwanja vya Jangwani.
Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, Dar es Salaam, aliouitisha ili kutoa maelezo ya ziada kuhusu ubadhirifu ndani ya BoT.
Alisema tuhuma za msingi za ubadhirifu ndani ya BoT, ambazo wananchi wanatakiwa kuzijua ni tuhuma ya benki hiyo kulipa deni la Meremeta Co. Ltd sh bilioni 155 kinyume cha utaratibu.
Dk. Slaa, alisema kwa muda wa miaka minne sasa wabunge wa kambi ya upinzani wamekuwa wakiihoji serikali iwaeleze Meremeta ni mali ya nani na imeandikishwa wapi, mahesabu ya kampuni hiyo yanatolewa kwa nani na taifa linafaidika nini kutokana na kampuni hiyo ambayo imekabidhiwa mgodi wa dhahabu wa Buhemba, mkoani Mara.
Alisema pamoja na kuihoji serikali miaka yote hiyo, imeshindwa kutoa majibu ya kuridhisha, licha ya kusema kampuni hiyo ni kampuni ya Serikali na inaendeshwa na JWTZ kwa lengo la kukisaidia kikosi cha Nyumbu.
Alisema utafiti wake umebaini kwamba Meremeta Co. Ltd, ni kampuni ya serikali, iliandikishwa Uingereza kwa hati ya usajili namba 3424504, kama ilivyotolewa London na Ofisi ya Msajili wa Makampuni, Agosti 19 mwaka 1997.
Oktoba 3 mwaka 1997, kampuni hiyo ilipata hati ya kutimiza masharti namba 32755. Alisema utafiti huo unaonyesha kuwa Tanzania ina hisa 50 katika kampuni hiyo na hisa nyingine ni za kampuni ya Afrika Kusini iitwayo Triennex Co. Ltd yenye hisa 50 pia.
Alisema uchunguzi wa ziada unaonyesha kampuni mbili zaidi zina hisa moja moja, nazo ni London Law Society Ltd (hisa 1) na London Law Secretarial Service Ltd yenye hisa moja.
Wananchi hapa kuna utata mkubwa, Meremeta ni ya nani? Meremeta ina hisa ngapi? Kama Meremeta imeandikishwa kama kampuni ya kigeni Tanzania ni kwanini imepewa fedha za walipa kodi wa nchi hii?
Alisema Watanzania lazima wafahamishwe, kampuni hiyo ilipata faida au hasara kiasi gani, na kwamba taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini inaeleza kuwa mwaka 2006/7 imepata tani 2.7 za dhahabu.
Mapato haya yameenda wapi? Utata huu unaelezwa vipi iwapo serikali inaeleza kuwa Kampuni ya Meremeta imefilisiwa na shughuli zake kuchukuliwa na TANGOLD Ltd? alisema.
Tuhuma ya pili ya ubadhirifu ndani ya BoT kwa mujibu wa utafiti wake ni kuhusu Kampuni ya TANGOLD na kwamba Bunge mara kadhaa limeelezwa kuwa kampuni hiyo ni mali ya serikali kwa asilimia 100.
Hata hivyo alisema utafiti wake umeonyesha ni kampuni ya kigeni iliyoandikishwa kwa mara ya kwanza nchini Mauritius Aprili 8 mwaka 2005, na kupata hati ya kutimiza masharti namba 55661 ya Februari 2000 hapa nchini.
Mbunge huyo alisema Memorandum and Article of Association ya kampuni hiyo haionyeshi popote kuwa ni mali ya serikali wala kuwa na uhusiano na serikali.
Tuhuma ya tatu ni BoT kulipa fedha kwa Kampuni binafsi ya Mwananchi Gold Co. Ltd, alisema kampuni hiyo imeandikishwa nchini kama kampuni binafsi katika mwaka wa fedha wa 2004/2005 na 2006/2007, kampuni hiyo imelipwa na BoT jumla ya dola za Marekani zipatazo 5,512,398.55.
Taarifa za ukaguzi zinaonyesha kuwa hadi Desemba 21, kampuni hiyo ilikuwa imelimbikiza riba ya dola za Marekani 62,847.91, sawa na sh 78,753,459. Hii ni kwa sababu kampuni hiyo ilitakiwa kulipa deni lake ndani ya miezi sita na hadi tarehe hiyo ya ukaguzi, yaani miezi 18 baadaye, ilikuwa haijalipa hata senti moja.
Isitoshe deni la dola za Marekani 2,807,920, ilionekana kwa taarifa ya ukaguzi kudhaminiwa kwa dhahabu ghafi iliyonunuliwa kwa fedha hizo za mkopo. Yaani Watanzania tumekaangwa kwa mafuta yetu, alisema Dk. Slaa.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za BRELA, Benki Kuu ina hisa 500 katika kampuni hiyo na NDC ina hisa 375, Kampuni ya Mwananchi Trust Company Ltd ina hisa 1,123 na Chimera Co. Ltd ina hisa 500.
Alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo ya BRELA, kampuni hiyo ilisajiliwa kwa hati namba 44962 ya Desemba 12, 2002 kama kampuni binafsi na kwa maana hiyo hairuhusiwi kuchukua fedha kutoka kwa umma.
Dk. Slaa alisema uchunguzi wake huo ana imani nao, kwa kuwa umejengwa kwa msingi wa nyaraka za BRELA na Idara ya Usalama wa Taifa.
Aliwatahadharisha watu wanaosema nyaraka mbalimbali zinazoibuliwa ni feki, kwani kuna chombo kimoja ndani ya Jeshi la Polisi chenye mamlaka ya kuthibitisha nyaraka hizo ni feki au la.