Soo la Zitto: PCB wajitosa
2007-08-24 18:34:19
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Hatimaye lile sakata aliloliibua Mhe. Zitto Kabwe bungeni kuhusiana na mkataba wa madini ya Buzwagi limechukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, TAKUKURU kujitosa katika uchunguzi wa kile kilichotokea.
Kwa mujibu wa taarifa aliyotoa jana kupitia mahojiano ya kwenye kipindi kimoja cha luninga, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw. Edward Hosea amesema hivi sasa wameshaanza mchakato wa kufuatilia suala hilo ili kujua kama kuna rushwa ilitembea.
Mhe. Zitto amekuwa akimshutumu waziwazi Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Naziri Karamagi kwamba alikiuka taratibu na kutaka iundwe tume teule ya kuchunguza sababu za Waziri huyo kusaini mkataba wa madini ya Buzwagi Jijini London Uingereza katika namna ambayo aliielezea kuwa ina utata.
Baada ya suala hilo kuzua gumzo kubwa nchini hasa baada ya hoja ya Mhe. Zitto kutupiliwa mbali bungeni na kisha yeye mwenyewe kusimamishwa kwa tuhuma za kusema uongo Bungeni, TAKUKURU imeamua kutojiweka pembeni na badala yake, Bw. Hosea amesema wameanza kulifuatilia kwa kina.
Bw. Hosea ameweka wazi suala hilo wakati wa mahojiano ya kwenye kipindi cha Tuambie kilichorushwa `live` jana usiku na Televisheni ya Taifa, TVT, Redio Tanzania Dar es Salaam na Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alikuwa akijibu swali la msikilizaji mmoja aliyeuliza kwa njia ya simu kuwa taasisi hiyo inalichukuliaje suala hilo nyeti hasa baada ya kusikia tuhuma zilizotolewa na Mhe. Zitto dhidi ya Waziri Karamagi Bungeni.
Akifafanua zaidi, Bw. Hosea alisema TAKUKURU ina njia mbili kuu ambazo inaweza kuzitumia kufuatilia jambo.
Akasema njia ya kwanza ni ya mbunge mwenyewe au Mtanzania mwingine yeyote kuwasilisha malalamiko na vielelezo muhimu katika taasisi yake.
Lakini akasema njia ya pili ni TAKUKURU yenyewe kujitosa katika jambo lenye maslahi kwa taifa, hasa kutokana na ukweli kuwa nao ni sehemu ya jamii na hivyo imesikia na kufuatilia kila kitu wakati na baada ya mijadala ya Bunge.
``TAKUKURU pia ni sehemu ya Jamii, tumesikia vizuri tuhuma zote tangu kule Bungeni na maoni ya wananchi baada ya vikao vya bunge, tumeona ni wajibu wetu kulifuatilia.... napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa tunalishughulikia suala hili,``akasema Bw. Hosea.
Aidha Bw. Hosea amesema TAKUKURU inapata ubavu wa kuchunguza suala hilo kwa kutumia kifungu cha 16 cha sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa ambayo inaipa taasisi hiyo nguvu ya kufanya hivyo.