Nimefarijika sana kuona maelezo ya Mkataba wa Buzwagi ambao ulipelekea Mh. Zitto kupewa suspension ya miezi mitano ya kutoshiriki kwenye vikao vya Bunge. Ninasubiri kwa hamu jinsi wabunge wa CCM watakavyokutana kwenye kikao kijacho hapo mjini Dodoma kwa ajili ya kuendeleza kijiwe chao cha soga.
Hivi wale wabunge wote wa CCM ambao walisimama kumtetea Karamagi kwa nguvu zote na hatimaye kuunga mkono hoja ya Mh. Mudhihir M. Mudhihir ya kumsimamisha Mh. Zitto, wanajisikiaje pale wanapoona hayo madudu ya kwenye mkataba? Hapa naona kuna bao la pili ya kisigino (la mkono wa Mungu labda), maana sasa ndiyo itadhihirika wazi kwamba ni nani alisema uongo kati ya Mh. Zitto na Mh. Karamagi.
Ninamuonea huruma Mama Makinda ambaye anadai kwamba Zitto alisimamishwa kwa sababu ya kutumia lugha mbaya ambayo haikubaliki Bungeni, lakini hoja yake ilikuwa ya msingi. Swali langu kwa Mama Makinda ni rahisi sana, je, Mh. Zitto alitakiwa atumie lugha gani? Maana alichosema Mh. Zitto ni kwamba Mh. Karamagi alilidanganya Bunge au kuna neno jingine zaidi ya hilo ambalo linam-describe muongo??
Nikitazama kwa mbali ninashawishika kuamini kwamba kitumbua cha mtu fulani kiko mbioni kujaa vumbi na mchanga maana kasi ya kimbunga ni kubwa sana na kitumbua chenyewe kiko wazi kabisa (kimekuwa exposed). Kwa hali ilivyo hata akikifuta namna gani hakiwezi kulika tena labda akakioshe kwa maji na bado hata akiosha na maji utamu na ladha yote ya kitumbua itakuwa imepotea na hakitakuwa kitumbua tena bali ugali wa unga wa mchele!
Nina mashaka kwenye kuvuja huu mkataba kuna mkono wa watu, na lengo likiwa ni kuongeza pressure kwa mfanyabiashara wa sekta binafsi ambaye hapotezi muda wa kusoma mkataba bali anakubali kusaini na kufuta kwa kalam ya wino baadhi ya vipengele vya mkataba ili awahi kutimiza wajibu na asipoteze "opportunity" ya uwekezaji. Hapa naona huu mkataba umevujishwa kwa makusudi kabisa ili NK akose nguvu ya kujitetea kwenye hili na hivyo kulazimika kukubali kuachia ngazi pasipo JK kumwambia wazi kwamba aachie mchuma ili ngoma iendelee kuyeya. Hiyo ndiyo diplomatic way ya jamaa kuondoka kimya kimya bila JK kuonekana mbaya au kamtosa. It was calculated maana JK alisema tangu awali kwamba hakujua kama mkataba ulisainiwa na siyo lazima ajulishwe kila mkataba unaposainiwa, sasa hapo huo msalaba ni wa Karamagi peke yake. Muungwana kajiweka kando na kumwachia ngoma aicheze mwenyewe na ikimshinda basi abwage manyanga.
Ninasubiri kwa hamu sana kuona miniti za kikao cha Kamati ya Ushauri ya Madini, najua nazo zitakuja tu iwapo jamaa ataendelea kuwa mbishi au kung'ang'ania kubaki ofisini. Siku ya kufa nyani miti yote huwa inateleza na hakuna hata kimbilio. Kimbilio pekee lililobaki ni mahakamani ambako nako hatujui kama ataenda kweli au anatikisa kiberiti ili kuona kama kimejaa au kiko pungufu! Kila la heri huko mahakamani maana nahisi hata Jaji atakayesikiliza kesi yake na akakubaliana nae itabidi jamii imshangae kwa hukumu atayotoa!