Hii ndio nguvu mpya, kasi mpya na ari mpya na Maisha bora kwa kila kiongozi wa chama
Mkataba wa Mgodi Buzwagi kumnufaisha zaidi mwekezaji
Na Mwandishi wetu
Mwananchi
SUALA la uwekezaji wa katika mgodi wa madini wa Buzwagi uliopo mkoani Shinyanga linazidi kunyumbulika ambapo imebainika kwamba mkataba kati ya serikali na Kampuni ya Barrick ni wa zaidi ya miaka 50.
Kwa mujibu wa mkataba huo, uliosainiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Nizar Karamagi na Mwakilishi wa Kampuni ya Barrick, Gareth Taylor, Februari mwaka huu London, Uingereza, kampuni ya Barrick itachimba madini katika mgodi huo kwa miaka 25 na kwamba itaongezewa tena miaka mingine 25 baada ya kipindi hicho.
"Waziri atatakiwa kutoa leseni maalum ya uchimbaji kwa kampuni haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kwa kipidi kisichozidi siku 60 tangu kampuni kuwasilisha maombi ya leseni na leseni atakayotoa waziri itakuwa kwa kipindi cha mwanzo cha miaka 25,
"Kampuni itakuwa na uhuru wa kuongezewa muda wa leseni kwa masharti yale yale kwa kipindi kingine cha miaka 25 na endapo kipidi cha nyongeza kitaisha na kampuni akaomba kuongezewa tena, basi kama waziri ataona ni kwa maslahi ya taifa ataweza kutoa kipindi kingine kwa kampuni atakachoona kinafaa," sehemu ya mkataba huo ambayo Mwananchi imeiona inaeleza.
Kwa upande wa mrabaha, mkataba huo unaonyesha kwamba kampuni hiyo imeruhusiwa kuchimba madini mengi zaidi ya dhahabu.
Kifungu hicho cha mkataba kinaeleza kuwa kampuni Barrick kupitia kampuni yake tanzu ya Pagea italipa asimilia tatu ya mrabaha wa madini yote yatakayochimbwa baada ya kuondoa gharama za uzalishaji, isipokuwa katika madini ya almasi ambayo yatalipiwa asilimia tano.
Kuhusu mapato halisi ambayo yanatarajiwa kupatikana kutoka katika mgodi huo, vifungu vya mkataba huo vinaonyesha kuwa nje ya malipo ya mrabaha na kodi ya zuio, serikali ya Tanzania pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kahama ulipo mgodi huo, itakuwa inalipwa jumla ya dola za Marekani 583,980 kwa mwaka.
Baadhi ya kodi ambazo zitalipwa ni pamoja na asilimia tatu ya thamani ya madini baada ya kuondoa gharama za uzalishaji kama mrabaha kwa madini yote yanayochimbwa eneo la Buzwagi.
Pia mkataba huo unaonyesha kwamba kampuni hiyo itakuwa ikilipa ushuru wa stempu kama ulivyoanishwa katika Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 20 ya mwaka 1972, kuanzia tarehe ya kuanza kwa mkataba wa Buzwagi.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa kampuni ya Pangea Minerals kutolipa hata senti tano kwa ushuru wa stempu kwani kifungu cha 5 (1) cha sheria ya ushuru wa stempu kimsema: "Hakuna ushuru wowote utakaolipwa kutokana na waraka wowote uliosainiwa kwa niaba au kwa taarifa ya serikali," ambapo kama kifungu hiki kisingekuwapo, basi serikali ingekuwa na wajibu wa kulipa ushuru huo kuhusiana na waraka huo.
Agosti 14, mwaka huu Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, lililimsimamisha Ubunge, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kujishughulisha na shughuli zozote za Bunge hadi Januari mwakani baada kubainika kuwa alisema uongo kuhusu uwekezaji katika mgodi wa Buzwagi.
Zitto aliwasilisha hoja binafsi akitaka maelezo kuhusu kusainiwa kwa mkataba huo wa mradi wa mgodi wa Buzwagi kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick, wakati serikali bado inafanya durusu ya mikataba.
Spika wa Bunge, Samwel Sitta, alisema Mbunge huyo atasimamishwa kwa vikao viwili hadi Januari mwakani kushiriki shughuli za Bunge kuanzia siku azimio la Bunge lilipopitishwa, yaani jana, zikiwamo zile za Kamati za Bunge.
Zitto alipotakiwa kujibu hoja, alisimamia msimamo wake wa kwanza na akasema yeye ni mwanademokrasia na kwamba angekuwa tayari kwa uamuzi wowote ambao Bunge lingeuchukua.
Akiwasilisha hoja hiyo, Kabwe alilitaka Bunge likubali kuunda kamati hiyo teule ili kuchunguza mwenendo mzima wa kusainiwa kwa mradi huo kulikofanyika jijini London, Uingereza Februari mwaka huu.
Alidai kuwapo kwa ukiukwaji katika baadhi ya taratibu zinazosimamia kuongoza sekta ya madini nchini ikiwemo haraka iliyomfanya Waziri Karamagi ausaini mkataba huo akiwa nje ya nchi bila kusubiri ripoti ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) kuhusiana na mradi huo ambao kwa kawaida hutolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc).
Hata hivyo, baada ya Ziito kusimamishwa ubunge vyama vya upinzania vilianza ziara mikoani kuwaeleza wananchi uonevu aliofanyiwa.
Ziara hiyo imesababisha wapinzania kuibua tuhuma nyingine kubwa kwa baadhi ya viongozi wa serikali kwamba wanahusika na ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma.