Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 za wanawake, Caster Semenya wa Afrika Kusini Friday, September 11, 2009 10:57 AM
Matokeo ya jinsia ya mwanariadha wa kike wa Afrika Kusini, Caster Semenya yanasemekana yamevuja na yameonyesha kuwa Semenya ana jinsia zote mbili za kike na kiume. Semenya ameingia mafichoni tangia ripoti hizo zilipotolewa. Bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 za wanawake, Caster Semenya ana jinsia zote mbili za kike na kiume yaani kwa kiswahili fasaha huntha au kwa kimombo hermaphrodite.
Kwa mujibu wa gazeti la Sydney Daily Telegraph la Australia, Semenya hana tumbo la uzazi na pia hana ovari (kiungo kinachotoa mayai ya uzazi).
Gazeti hilo limedai kupata data hizo kutoka kwa chanzo chao cha kuaminika ndani ya shirikisho la riadha la dunia IAAF.
Gazeti hilo limedai kuwa Semenya ana makende - viungo vya kiume vinavyozalisha homoni za testosterone ambazo humfanya mwanaume awe na misuli, vinyweleo mwilini na sauti nzito.
Semenya mwenye umri wa miaka 18 inasemekana ameingia mafichoni tangia gazeti hilo lilipotoa taarifa hizo jana.
Gazeti hilo pia lilisema kuwa shirikisho la riadha la dunia IAAF linategemea kumnyang'anya Semenya ubingwa wake na kumpiga marufuku kushiriki mashindano yoyote ya riadha yajayo na kumshauri afanye operesheni kurekebisha hali hiyo kwakuwa ni hatari sana kwa afya yake.
IAFF ilithibitisha kupokea matokeo ya jinsia ya Semenya jana lakini maafisa wake walisema kuwa matokeo hayo hayatawekwa hadharani kwa muda wa wiki mbili mpaka watakapokutana na kuongea na Semenya mwenyewe.
Msemaji wa IAAF, Nick Davies alisema kuwa matokeo hayo yataanikwa hadharani baada ya wataalamu kuyapitia tena na baada ya Semenya mwenyewe kuonyeshwa matokeo hayo.
"Hakuna kitu kitakachotolewa mpaka wataalamu watakapomaliza kuyapitia tena matokeo ya jinsia yake, hatuwezi kusema itachukua muda gani lakini ni ndani ya wiki chache zijazo".
Hata hivyo gazeti hilo lilidai kuwa matokeo hayo tayari yameishavuja na mbali ya kuonyesha Semenya ana jinsia mbili yanaonyesha pia kuwa Semenya ana kiwango kikubwa cha testosterone mara tatu zaidi ya mwanamke wa kawaida.
IAAF itabidi imnyang'anye Semenya ubingwa wa dunia wa mita 800 baada ya matokeo hayo kutangazwa kama yatathibitisha habari hizo kuwa ni za kweli.
Hata hivyo IAAF ilishasema awali kuwa haifikirii kumnyang'anya Semenya tuzo yenyewe ya medali ya dhahabu ambayo alipewa baada ya kunyakua ubingwa huo.
Semenya aliingia mafichoni jana usiku baada ya taarifa za gazeti hilo kutolewa na kuna uwezekano mkubwa hatatokea kwenye mashindano ya riadha ya mita 4000 ya wanawake ambayo yamepangwa kufanyika kesho jijini Pretoria, Afrika Kusini.
http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsId=3059738&&Cat=6