SUPASTAA, Neymar ameripotiwa kuzungumza na wakala wake kuhusu ofa zinazoletwa kumhusu yeye ili ang’oke Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu.
Real Madrid imetajwa kwa muda sasa kuhitaji huduma yake, lakini, kwa sasa zimeibuka timu nyingine zinazohitaji saini ya Mbrazili hiyo, Manchester United na Manchester City. Hata hivyo, pesa ndiyo itakayoamua.
Hapa ndipo utakutana na ile methali ya mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama. Man United wanataka kutumia vyanzo mbalimbali vya kipesa kunyakua huduma ya supastaa huyo anayeuguza majeraha ya mguu kwa sasa.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola yupo tayari kuingia vitani kunasa saini ya mchezaji huyo na ametenga Pauni 300 milioni. PSG wenyewe wanaonekana wanachosubiri kwa sasa ni pesa tu. Kama watamuuza kwa Pauni 300 milioni, hapo watakuwa ameingiza faida kubwa sana, zaidi ya Pauni 100 milioni.
Kusikia hivyo, kocha wa Man United, Jose Mourinho naye ameingia vitani kumsajili Neymar na anaamini atamnasa. Mourinho anamhitaji pia Marco Asensio kwenye kikosi chake msimu ujao. Mourinho anaamini katika matumizi ya pesa.
Ripoti zinadai ukiweka pesa kando, Mourinho anataka kumtumia pia Paul Pogba kumnasa Neymar.
Kilichopo ni, Pogba anaweza kupelekwa PSG pamoja na pesa ili Neymar atue Old Trafford.
Ripoti za ndani kabisa kutoka Old Trafford zinadai wadhamini wa timu hiyo, Chevrolet ndiyo watakaofanya mchakato mzima wa kuhakikisha Neymar anazipiga chini Real Madrid na Man City na kutua Man United.
Taarifa zaidi zinadai kwa timu hizo zilizotajwa hapo, Man United pekee ndiyo wenye jeuri ya kumlipa mshahara atakaoutaka Neymar. Kwa sasa Mbrazili huyo anakunja pesa ndefu huko PSG, Pauni 775,477 kwa wiki ukijumlisha bonasi zote. Mshahara pekee haupungui Pauni 600,000 kwa wiki.
Kwa hesabu hizo, si Man City wala Real Madrid wanaonekana kuwa uwezo wa kumudu mshahara wa wiki wa staa huyo zaidi ya Man United tu, ambao kulipa mkwanja mrefu kama mshahara wa wiki si tatizo kwao kama kwa sasa tu wanamlipa Alexis Sanchez zaidi ya Pauni 500,000 kwa wiki.
Kitu kingine Man United wana uhakika, wadhamini wao Chevrolet wanaweza kuweka mkwanja mrefu, huku dili likionekana kukaa vizuri Adidas pia wanaweza kulifurahia kama ilivyofanya kwa staa Pogba, wakati alipotua kwa pesa nyingi Old Trafford.
Man United inalenga kujiboresha zaidi sokoni kuvutia dili za kibiashara, hivyo kuwa na wachezaji mastaa kutawafanya nembo yao kuendelea kutikisa Ulaya na duniani kwa jumla.
Chevrolet ndiyo wadhamini wakuu wa Man United wanaotokea kwenye jezi zao, huku Adidas pia wakimwaga mkwanja mrefu kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Old Trafford. Mourinho alishawahi kumwambia Neymar anamtaka aende Man United ambako atakwenda kumfanya kuwa staa mkubwa na nembo ya timu hiyo kama ilivyo kwa mastaa wenzake Lionel Messi ni Barcelona wakati Cristiano Ronaldo ni Real Madrid.