Kuna sababu nyingi zinazofanya watu wajiunge na chama fulani (chochote kile au cha siasa), na pia kufanya waondoke. Wengine ni kwa sababu ya maslahi binafsi ikiwemo kipato (fedha), cheo (mfano Ubunge) au umaarufu. Inafaa pia tukubaliane na kutokubaliana, wakati mwingine. Habari hii kutoka Uhuru inasaidia kuelewa hilo kuhusiana na mjadala unaoendelea hapa.
Chadema bado kwafukuta
Na Karume Malembeka, Kigoma
HALI ya kisiasa ndani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa imezidi kuwa mbaya tangu aliyekuwa makamu mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Dk.Walid Amani Kabourou alipojiengua na kujiunga na CCM.
Katika hatua inayoonyesha kudhoofika kwa chama hicho, kimemvua uanachama
mwenyekiti wake wa wilaya ya Kigoma Vijijini, Jeremiah Midaho, kwa
kinachoelezwa kukiuka maadili ya uongozi.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kigoma, Jaffari Kasisiko, aliwaambia
waandishi wa habari mjini hapa kuwa uanachama wa Midaho ulikoma kuanzia
Januari 5, mwaka huu, baada ya uongozi wa mkoa kutangaza suala hilo rasmi.
Kasisiko alisema uamuzi huo wa kumfukuza mwenyekiti huyo wa wilaya,
ulifikiwa na kikao cha kamati ya utendaji ya mkoa ya CHADEMA kilichokutana mjini Kigoma Desemba 28, mwaka jana.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA mkoa alisema Midaho amefukuzwa kwa
mujibu wa Katiba ya chama hicho, kifungu cha 5.4.3 kinachoelezea kukoma
kwa uanachama.
Kasisiko alisema Midaho akiwa mwenyekiti, morari na
utendaji wake ndani ya chama ulishuka kwa kiasi kikubwa, ambapo
mchango aliokuwa akiutoa haukuwepo kabisa, badala yake alianza kuwa
mzigo ndani ya chama.
Alibainisha kuwa awali, kiongozi huyo alikuwa na mchango mkubwa
ndani ya chama akifanya mambo mengine kwa kujitolea fedha zake za
mfukoni, lakini kuanzia Julai, mwaka jana utendaji wa kiongozi huyo
ulipotoka.
Mbali ya kushindwa kushiriki katika kazi za kuhamasisha uhai wa chama
na kwenda kinyume cha maadili ya uongozi, pia kiongozi huyo anadaiwa
kushindwa kuhudhuria mikutano muhimu ya CHADEMA katika ngazi za
mkoa na taifa.
Inaelezwa kuwa kujitoa kwa Dk. Kabourou CHADEMA na kujiunga na CCM, kunaweza kuwa pia kunachangia jambo hilo, kutokana na uswahiba wa karibu walionao watu hao.
Habari za ndani ambazo gazeti hili imezipata zinaeleza kuwa katika
uchaguzi mkuu uliopita, Midaho ambaye alishindwa kwenye kura za maoni za
chama hicho na Zitto Kabwe, alikuwa akipigiwa chapuo na Dk. Kabourou huku
Zitto akiungwa mkono na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.
Suala hilo lilizua mtafaruku baina ya kambi hizo mbili, na inaelezwa kuwa
hata baada ya uchaguzi kumalizika, na Zitto kushinda ubunge katika jimbo la
Kigoma Kaskazini, Midaho alikuwa haambatani na viongozi wenzake.
Habari za duru za kisiasa mkoani hapa zinasema Midaho alionekana kuwa na dalili za kutaka kujiunga na CCM, jambo lililowafanya viongozi wa CHADEMA
waamue kumfukuza, kuliko kupata aibu ya kuondoka kwake akiwa bado kiongozi.
Miongoni mwa nafasi alizowahi kushika Midaho kabla ya kufukuzwa
ni pamoja na ukatibu uenezi wa wilaya Kigoma vijijini, mgombea ubunge
jimbo la Kigoma Kaskazini mwaka 2000, meneja wa kampeni wa Dk. Kabourou katika uchaguzi wa jimbo la Kigoma mjini na mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa CHADEMA.