Nimemshuhudia jirani yangu wa kushoto akinyolewa bila maji na mara sijakaa sawa jirani yangu wa kulia naye huyoo yanamkuta, kweli bado sishtuki tu ? Ningekuwa mimi ningejisemea lo, miaka arobaini na zaidi yatosha hakuna haja ya kuzidi kung'ang'ania madaraka. Haraka haraka ningekaa chini na wapinzani wangu na kwa pamoja kupanga namna ya kufanikisha mabadiliko ya utawala kwa amani.
Lakini siyo Gadafi, kwa akili yake hakuna mwingine kama yeye na hata kama itatokea yeye asiwepo kwa sababu yoyote ile, ukoo wake upo na wanaye watano si wapo ? Kwa watu kama Gadafi ambaye hata kuingia madarakani alitumia hila, ni vigumu kwao kufikiria kuwa kuna wazalendo Libya zaidi yake. Hao kina Ben Ali na Mubarak walishindwaje kutumia vyombo vya dola dhidi ya wananchi wao ?
Gadafi angekuwa mjanja angeng'amua mapema kabisa kuwa hawezi kuyazuia mabadiliko kwani muda wake Libya ulikuwa umefika. Nina hakika angefanya la maana kama angeyasikiliza madai na kutilia maanani hoja za Walibya waliochoka na utawala wake. Angefanya hivyo bila kumwaga damu ya watu wasio na hatia, angeweza kujijengea heshima na kubaki shujaa nchini humo.
Kama atakuwa alishajichimbia shimo kama Sadam Hussein, haraka atumbukie humo ajiifiche kama panya na hapo labda ataweza kujiongezea siku chache. Hapa kwetu tofauti ni kuwa badala ya Gadafi tuna CCM na siku zinavyosogea ndivyo wanavyozidi kutumia kila hila kubaki madarakani. Hata hivyo siku zao za kujificha pangoni zinakaribia kwa kasi mpya na ari zaidi mfano wa sikio la kufa.