Timu za madaktari wa China zimekuwa msaada mkubwa kwa afya ya jamii katika nchi nyingi zinazoendelea, zikiwemo za Afrika. Katika nchi nyingi za Afrika, licha ya changamoto za lugha, madaktari hao wamekuwa msaada mkubwa kwa kuungana na madaktari wazawa katika kutoa elimu ya afya, utambuzi wa wagonjwa, tiba, na mafunzo.
Botswana ni moja ya nchi ambazo zimefaidika sana na timu za madaktari wa China, kwani madaktari hao wamekuwa makini katika kufanya kazi zao, na kutoa suluhisho la kiafya kwa wagonjwa wao. Ikiwa ni baada ya saa mbili kamili asubuhi, sehemu ya nje ya kliniki ya wanawake wajawazito katika Hospitali ya Princess Marina, iliyoko mji mkuu wa Botswana, Gaborone, tayari imejaa wanawake wajawazito wanaosubiri kuonana na madaktari kwa ajili ya ushauri.
Ndani ya chumba cha uchunguzi, Luo Jinying, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika timu ya 17 ya madaktari wa China nchini Botswana, anarekebisha kipimo cha ultrasound, vifaa vinavyofuatilia mtoto aliye tumboni, na vifaa vingine, pamoja na madaktari wengine kadhaa vijana wa huko.
Kama hospitali kubwa zaidi ya umma nchini Botswana, Hospitali ya Princess Marina inapokea wagonjwa wengi wanaopewa rufaa kutoka sehemu mbalimbali za nchi hiyo, na kubeba mzigo mkubwa wa kuwatibu wagonjwa wenye hali mbaya, huku idara ya ukunga na magonjwa ya wanawake ikiwa ni kati ya idara zenye shughuli nyingi zaidi.
Luo, baada ya kuonana na zaidi ya wanawake 30 wajawazito kwa siku nzima, anasema kuonana na wagonjwa ni sehemu ndogo tu ya kazi zao za kila siku, na mara nyingi saa za kliniki zinaendelea hadi saa kumi na moja jioni, na baadaye wanaendelea na zamu za dharura usiku kucha, daima wakiwa tayari kwa uokoaji wa dharura.
Anakumbuka mwanamke mjamzito aliyekuwa anasumbuliwa na kutangulia kwa kiungo mwana pamoja na hali mbaya ya mtoto aliye tumboni, akisema ni moja ya kesi za dharura alizowahi kushughulikia.
Anasema tangu utambuzi hadi kukusanya wafanyakazi wa idara mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya upasuaji, hadi kuzaliwa salama kwa mtoto, mchakato mzima ulichukua dakika saba tu.
Mwitikio wa haraka uliwezeshwa na maboresho katika muda wa kuingilia kati kati ya uamuzi na kujifungua kwa dharura (DDI), ambao ulitimizwa kwa msaada wa timu ya madaktari wa China.
Akitumia uzoefu kutoka nchini China, Luo alishirikiana na mkuu wa idara hiyo, Bayad Hassan, kuanzisha timu ya mwitikio wa haraka, kurahisisha uratibu kati ya wakunga, wataalamu wa dawa za usingizi, idara za huduma za uangalizi wa kina, na idara nyingine, na kuimarisha mafunzo ya dharura kwa wafanyakazi wa zamu ya usiku. Baada ya marekebisho na marudio ya mafunzo, muda wa huduma ya DDI ulipungua hatua kwa hatua na kufikia kati ya dakika 25 na 30, na hivyo kufikia vigezo vilivyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Tangu mwaka 1981, mkoa wa Fujian nchini China umepeleka timu 17 za madaktari, ikiwa ni jumla ya zaidi ya wahudumu 500 wa afya nchini Botswana. Fan Wandong, mkuu wa timu ya madaktari wa China nchini Botswana, anasema mwezi Julai 2024, timu yenye wajumbe 45 ya madaktari wa China iliwasili Botswana na kuanza kufanya kazi katika Hospitali ya Princess Marina iliyoko Gaborone na Hospitali ya Rufaa ya Nyangabgwe iliyoko Francistown, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo.
Katika miaka miwili iliyopita, timu hiyo imetoa zaidi ya ushauri 180,000 wa afya na matibabu, kushiriki katika zaidi ya upasuaji 5,000, kutoa huduma saba za bure za kliniki, na kutoa mafunzo kwa zaidi ya maafisa 1,000 wa afya wa huko.
Fan anasema, msaada wa matibabu sio tu kuwatibu wagonjwa, jambo la muhimu zaidi ni kusaidia kuboresha uwezo wa matibabu wa huko na kuimarisha mfumo wa huduma za afya.