Bibi alileta chakula pale pale, akaleta kimkeka akakaa, tulianza kushambulia wali uliokua kwenye sinia kubwa, huku bibi akiwa kaniwekea minyama lundo kwenye kibakuli kidogo cha udongo, yaani paja, filigisi na kidali humohumo, dah! Nilikula huku nikijiwazia eee kwa hali hii ntarudi nyumbani kibonge kweli!
Wakati tunamalizia kula bibi akachombeza, unamuwaza mchumba?
Mchumba tena? Hapana bibi, nawaza ya fisi kuiba mbuzi mapema tu hii, nilimjibu,
Wewe unashangaa hivyo tu? Wanatokeaga hata mchana wanabeba wanacho kitaka, hivyo kuwa na amani ni mambo ya kawaida tu huku na utayazoea, alisema bibi,
Hodi hapa, ilisikika sauti ya kiume, karibuu, aliitikia bibi,
Babu yako huyo amerudi! Nilinyanyuka na kumpokea bab baiskeli aliyokuwa anasukuma, huku kwenye karia amefunga karai na mbuzi dume kwa ndani yake!
Oooh! Umefika mzee mwenzangu? Karibu sana babu, alinichangamkia mzee bhuhabi,
Asante babu nshakaribia,
Basi nilifungua karai na kumtoa yule mbuzi dume aliyehasiwa (maksai) mzito na amenona sana.