Mchumi Dr Blasius Kahyoza amechambua uhitaji na umuhimu wa katiba mpya kwa kigezo cha uchumi, mambo muhimu katika mtazamo wake ni;
Moja, Hoja ya gharama kubwa kutengeneza katiba mpya ni ukosefu wa uelewa kwa sababu wanaosema hivyo hawatazami faida kubwa za mbeleni za jinsi katiba mpya itakayotoa uhuru mkubwa wa haki za kiuchumi itakavyongeza pato la nchi kama sio kwao kwa watoto wao na vizazi vijavyo. Hivyo hakuna gharama yoyote inayoweza kuwa kigezo cha kuikaata katiba mpya kwa sababu faida zinazidi gharama yoyote.
Mbili, Si rahisi kwa uchumi wa nchi yetu kuwa imara na endelevu bila katiba mpya iliyo imara kwa sababu misingi ya uchumi huwa inategemea sana miondombinu ya kujitawala ambayo huwa inasimikwa na katiba. Anasema ukiacha nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta historia inaonyesha wazi nchi nyingine zote zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo kwa haraka zilitanguliwa na mageuzi makubwa ya miondombinu ya tawala zao kupita Katiba.
Tatu, Wanaosema tujenge kwanza uchumi kisha katiba ije baadaye wanasahau taifa hili limeujenga uchumi huo wanaouzungumzia kwa miaka 60 sasa na limefanya kila kitu isipokuwa kubadilisha katiba ili kufikia hayo maendeleo makubwa linalotamani kuyafikia.
Dkt. Kahyoza anauliza Kama tumefanya kila jambo tulillofikiri ni muhimu kupata maendeleo makubwa na bado imeshindikana busara za kawaida si zingesema tufanye jambo lingine ambalo hatujawahi kulijaribu pamoja na kuzungumzwa sana na wengi amabalo ni kufanya mageuzi makubwa ya miondombinu ya utawala wetu kwa kubadilisha katiba yetu?