Tujikumbushe: Miaka ya 1990 hadi 2000 video za watu kuchinjwa zilienea sana mitandaoni

Tujikumbushe: Miaka ya 1990 hadi 2000 video za watu kuchinjwa zilienea sana mitandaoni

Mhaya

JF-Expert Member
Joined
Aug 20, 2023
Posts
1,831
Reaction score
5,489
Mwisho wa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000, intaneti ilikua jukwaa la video za kutisha za mauaji, ikiwemo vichwa vya watu wa Magharibi kama wazungu na wamarekani vikichinjwa. Video hizi zilitengenezwa na kusambazwa na mashirika ya kigaidi yanayoendesha operesheni katika Mashariki ya Kati, Asia, na maeneo mengine yenye migogoro. Kila kanda ilikuwa na wahusika wake na madhumuni yao ya kutengeneza video hizi za kutisha na za propaganda kuogopesha watu, serikali au mamlaka za kimataifa.

Picha linaanza huko Iraq, baada ya uvamizi wa Marekani mwaka 2003 kumtafuta Saddam Hussein aliyekuwa Rais wa Iraq kwa kipindi hicho. Marekani ilidai kuwa Saddam Hussein alikuwa na uhusiano na Al-Qaeda, kundi la kigaidi liliokuwa nyuma ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, dhidi ya taifa la Marekani.

Saddam Hussein alikamatwa na vikosi vya Marekani mnamo Desemba 13, 2003, wakati wa Operesheni Red Dawn, karibu na mji wake wa nyumbani wa Tikrit, Iraq. Aligundulika akijificha katika pango dogo la chini ya ardhi au wengine wakilipa jina la "shimo la buibui" kwenye shamba lililokuwa katika kijiji cha ad-Dawr. kikundi cha Al-Qaeda nchini Iraq (AQI), chini ya uongozi wa Abu Musab al-Zarqawi, kilianza kuachia video za mauaji ya kikatili kama kuchinja na kupiga risasi watu mbalimbali huku wakirekodiwa.

Waathirika walikuwa mara nyingi wanahabari wa kigeni, wakandarasi, na wafanyakazi wa misaada ya kimataifa. Mmoja wa matukio maarufu yaliyoshitua dunia ilikuwa mauaji ya Nicholas Berg, mkandarasi Mmarekani, mnamo 2004. Matendo haya yalikuwa yamekusudiwa kueneza hofu na kuonyesha upinzani wao dhidi ya uingiliwaji wa kigeni. Watu mbalimbali na viongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda walipelekewa moto na baadhi ya kukamatwa na wengine kukimbia.

Saddam Hussein ni miongoni mwao ya waliosakuliwa kwa udi na uvumba, baada ya kukamatwa mwaka 2003, Saddam Hussein alifunguliwa kesi na Mahakama Maalum ya Iraq kwa makosa dhidi ya binadamu. Alikubaliana na hatia mwaka 2006 kwa Mauaji ya Dujail (1982), ambapo wanaume na wavulana 148 wa Kisuni waliuawa kwa kisasi kutokana na jaribio la kumwua. Alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifo kwa kunyongwa na alitekelezwa hukumu hiyo mnamo Desemba 30, 2006.

Makosa mengine aliyotuhumiwa ni pamoja kuvunja haki za binadamu ikiwemo kuua wa Kurdi zaidi ya 5,000 katika matukio tofauti kwa kutumia silaha ya sumu na nyinginezo hususani katika tukio la kampeni za Anfal (1986-1989) na tukio la shambulio la kemikali la Halabja. Matukio mengine ni kama kuwadumaza wa Shia kupelekea vifo zaidi ya 1,000, kuwanyamazisha wanasiasa kwa kuwauwa au kuwateka. Uvamizi wa nchi za jirani mfano vita ya Iran na Iraq ya mwaka 1980-1988, na uvamizi wa nchi ya Kuwait mwaka 1990. Mambo mengine ni kama rushwa na ukandamizaji.

Ikumbukwe Osama bin Laden ndiye alikuwa kiongozi wa Al-Qaeda, shirika la kigaidi alilolianzisha mwaka 1988 alikishirikiana na viongozi wengine. Al-Qaeda ilijulikana kwa kupanga mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani kwa kuteka ndege zenye abiria na kisha kwenda kuziangusha kwenye ghorofa refu pale Marekani jaribio la kujitoa muhanga, pamoja na mashambulizi mengine mengi duniani. Itikadi ya kikundi hicho inajikita katika tafsiri kali za sheria ya Uislamu, na kinataka kuanzisha dola la Kiislamu kwa kutumia vurugu na ugaidi dhidi ya kile kinachoitwa maadui wa Uislamu, ikiwa ni pamoja na nchi za Magharibi na serikali za Mashariki ya Kati.

Huko Afghanistan, baada ya shambulio la Septemba 11 na uvamizi wa Marekani kutafuta magaidi uliofuata katika nchi za ukanda huo, Taliban na makundi yanayohusiana au kushirikiana katika ugaidi yalianza kuachia video za mauaji kama chombo cha propaganda kuzitisha serikali za Magharibi.

Video hizi mara nyingi zililenga watu wa Magharibi na raia wa Afghanistan wanaoshukiwa kushirikiana na majeshi ya Marekani. Lengo lilikuwa kuogopesha na kuzuia ushirikiano na vikosi vya kimagharibi. Taliban walijulikana kwa kutekeleza hukumu kali za kikatili dhidi ya watu waliovunja sheria za dini, kama vile kuchinja au kupiga mawe watu mpaka kufa.

Hii ilijumuisha kuua mtu kwenye umati wa watu wakitazama au mauaji ya hadhara. Video hizi zilikuwa zikitumika kama njia ya kuonyesha nguvu yao na kudhihirisha maadili yao ya dini yao. Katika miaka ya 1990, kabla ya kuvamiwa na Marekani, Taliban walikuwa wakitumia vyombo vya habari, ikiwemo kurekodi video za kikatili, kuonyesha adhabu za kikatili kwa watu waliokiuka sheria za Kiislamu za Sharia. Baada ya Marekani kuvamia Afghanistan, Taliban na makundi mengine ya kigaidi kama Al-Qaeda walikuwa wakitumia video kurekodi na kusambaza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya majeshi ya Marekani na washirika wao.

Walikuwa pia wakichapisha video mitandaoni za mashambulizi ya kigaidi kama vile shambulio la kambi za kijeshi za Marekani au mashambulizi ya kujitoa muhanga au kijilipua na mabomu. Video hizi zililenga kuonyesha ushindi wa makundi hayo na kuhamasisha wafuasi zaidi kujiunga nao kutokea kila pembe ya Dunia na kupitia pia makundi mbalimbali kama Al-Shabaab ambapo pia mtanzania aliwai kumatwa nchini Kenya akiwa miongoni mwa magaidi wa Al-Shabaab wenye uhusiano na Al-Qaeda. Wakati wa kipindi cha vita, baadhi ya video zilionesha mauaji ya kigeni yaliyofanywa na makundi ya Taliban au Al-Qaeda. Hizi ni pamoja na video za mauaji ya wanahabari wa Magharibi au watekaji nyara raia wa kigeni. Lengo lilikuwa kueneza hofu na kuonyesha upinzani kwa uingiliaji wa Magharibi.

Mfano wa Video maarufu ni ile ya kuchinjwa kwa mwandishi wa habari Mmarekani Daniel Pearl mwaka 2002 huko nchini Pakistan alipokuwa akifanya kazi zake za uandishi wa habari ambapo alitekwa na kisha kuchinjwa na video kupostiwa mtandaoni ikiwa na kichwa cha habari "The Slaughter of the Spy-Journalist, the Jew Daniel Pearl", ambapo Al-Qaeda waliiandika na kutangaza video hiyo kama sehemu ya kuonyesha nguvu zao na ubabe kwa Mmarekani. Al-Qaeda na Pakistan Inter-Service Intelligence (ISI) walihusika moja kwa moja na hayo mauaji, ambapo baadae kiongozi mkuu wa Al-Qaeda, Khalid Sheikh Mohammed (KSM) alikamatwa na kupelekwa Guantanamo na alikiri kushiriki mauaji hayo, mwingine ni mwanamgambo wa Kipakistani Ahmed Omar Saeed Sheikh ambaye nae alitiwa mbaroni.

Huko Chechnya nchini Urusi, wakati wa vita vya Chechen (1994–2009), waasi wa Kiislamu walijulikana kwa kuwaua wanajeshi wa Urusi na mateka wenye uraia kigeni mbele ya kamera. Katika karne ya 18 na 19, Chechnya ilijaribu kupinga uvamizi wa Urusi, lakini ilishindwa na ikajumuishwa katika Milki ya Urusi kwa nguvu. Kuanguka kwa Muungano wa Kisovyeti kulileta nafasi kwa mataifa na maeneo mbalimbali yaliyokuwa yanamilikiwa na umoja wa Kisovieti kudai uhuru ikiwemo Nchi ya Ukraine inayopigwa makombora Leo hii kwa kukiuka mkataba wa Urusi dhidi ya NATO.

Mwaka 1991, Chechnya, chini ya uongozi wa Dzhokhar Dudayev, ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi. Serikali ya Urusi, chini ya Boris Yeltsin, ilikataa kutambua uhuru wa Chechnya, ikidai kuwa ni sehemu muhimu ya Shirikisho la Urusi. Hii ilianzisha mvutano uliosababisha Vita vya Kwanza vya Chechnya. Wachechen ni jamii yenye mila imara na dini ya Kiislamu, huku wakiwa na historia tofauti sana na ile ya Warusi wengi wa Kikristo wa Orthodox. Tofauti hizi za kitamaduni na kidini zilichochea mvutano, na katika kipindi cha machafuko, baadhi ya wanamgambo wa Kiislamu walihamasisha mapambano kama "jihad" dhidi ya Urusi. Katika miaka ya 1990, Chechnya ilijitokeza kama kitovu cha wanamgambo wa Kiislamu.

Vikundi hivi vilikuwa vikipigania kujitenga wao kwa wao, lakini pia vilivutia wapiganaji wa kigeni kutoka mataifa mengine ya Kiislamu. Baada ya Vita vya Kwanza vya Chechnya, Chechnya ilipata uhuru wa muda. Hata hivyo, serikali ya Chechnya ilishindwa kuleta utawala thabiti. Wanamgambo wa Kiislamu na wahalifu walitawala baadhi ya maeneo, na kukawa na utekaji nyara wa raia wa kigeni na mauaji ya kutisha. Abu Musab al-Zarqawi, kiongozi wa mtandao wa Al-Qaeda, na wapiganaji kutoka Afghanistan walihusishwa na wanamgambo wa Chechen.

Wanamgambo wa Chechen pia walihusika katika ukatili mkubwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa hukumu za kikatili kwa wale waliokuwa wakishukiwa kuwa wasaliti au washirika wa Urusi. Video za kutisha za wanajeshi wa Urusi wakiwa wamekatwa vichwa zilianza kusambazwa, zikionyesha ukatili wa wanamgambo hao. Makundi kama Islamic International Brigade yalitumia video hizi kujitangaza na kuonyesha upinzani wao dhidi ya majeshi ya Urusi. Picha hizi za kutisha zilisambazwa sana kwenye intaneti, na kuongeza hofu duniani dhidi ya haya makundi ya kigaidi. Hali hii ilifanya Urusi kuwa na sababu ya kuingilia tena kwa lengo la "kudhibiti ugaidi" wakati wa Vita vya Pili vya Chechnya.

Chechnya ni eneo muhimu kiuchumi, likiwa na matenki ya mafuta na njia za usafirishaji wa mafuta kutoka Asia ya Kati hadi Ulaya. Urusi haikuwa tayari kupoteza udhibiti wa rasilimali hizi, ambayo ilikuwa sababu kubwa ya kutoipa Chechnya uhuru wake. Vikosi vya Urusi vilianza operesheni ya kijeshi mwaka 1994 kwa lengo la kurejesha udhibiti wa Chechnya.

Hii ilisababisha mauaji ya maelfu ya raia. Grozny, mji mkuu wa Chechnya, uligeuzwa kuwa magofu kutokana na mashambulizi makali ya anga na mizinga. Raia wengi walifariki, na mashirika ya haki za binadamu yaliripoti mauaji ya kiholela, ubakaji, na utekaji nyara wa raia wa kawaida. Wanajeshi wa Urusi walifanya operesheni ya kijeshi katika kijiji cha Samashki, ambapo mamia ya raia walipigwa risasi au kuchomwa wakiwa hai. Mwaka 2000, wanamgambo wa Chechen waliteka ukumbi wa michezo, wakidai Urusi ijitoe Chechnya.

Mateka zaidi ya 170 walifariki, wengi kutokana na gesi iliyotumika na vikosi vya Urusi kujaribu kuwaokoa na mwaka 2004 wanamgambo wa Chechen waliteka shule huko Ossetia ya Kaskazini, ambapo zaidi ya watu 330, wakiwemo watoto, walikufa baada ya makabiliano ya kikatili. Mashambulizi ya kigaidi yaliyohusishwa na wanamgambo wa Chechen, kama Shambulio la Moscow Theater (2002) na Shambulio la Shule ya Beslan (2004), yaliimarisha msimamo wa Urusi wa kutokubali uhuru wa Chechnya.

Matukio haya yalitumiwa na Urusi kama sababu ya kupanua operesheni za kijeshi katika mkoa huo. Rais Vladimir Putin alitumia mgogoro wa Chechnya kama njia ya kuimarisha mamlaka yake. Vita vya Chechnya vilimsaidia kujenga picha ya kiongozi mwenye nguvu aliyedhamiria kupambana na ugaidi na kulinda uadilifu wa Urusi na himaya zake.

Huko Pakistan, makundi kama Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP) yalitoa video za mauaji zikilenga wanajeshi wa Pakistan, raia, na mateka wa kigeni. Vitendo hivi vilikuwa na lengo la kueneza hofu na kuonyesha upinzani wao dhidi ya serikali ya Pakistan na washirika wake. Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP), inayojulikana pia kama Pakistani Taliban, ni kikundi cha wanamgambo wa Kiislamu kilichoanzishwa mwaka 2007. Kikundi hiki kiliundwa kwa lengo la kuunganisha makundi mbalimbali ya wanamgambo wa Kiislamu yaliyokuwa yakifanya kazi katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa Pakistan, hasa kwenye mpaka wa Afghanistan. Katika historia yake, TTP imehusika na mauaji ya kutisha, mashambulizi ya kigaidi, na usambazaji wa video za kutisha ili kueneza propaganda zao.

TTP ilianzishwa chini ya uongozi wa Baitullah Mehsud na ilihusisha wanamgambo wengi waliokuwa na uhusiano na Taliban ya Afghanistan. Lengo lao kuu lilikuwa kupinga serikali ya Pakistan, ambayo waliona kama mshirika wa Marekani na maadui wa Uislamu. Ajenda zao zilikuwa kuanzisha sheria za Kiislamu (Sharia) katika Nchi ya Pakistan na kupambana dhidi ya vikosi vya NATO vilivyokuwa Afghanistan baada ya uvamizi wa Marekani mwaka 2001.

TTP walifanya mashambulizi mengi yaliyosababisha vifo vya maelfu ya raia wa kawaida, ikiwa ni pamoja na mabomu kwenye masoko, shule, na nyumba za ibada. Moja ya mashambulizi yao ya kikatili zaidi yalikuwa shambulio la Shule ya Jeshi Peshawar (2014), ambapo wanamgambo wa TTP waliwaua watoto 149, wengi wao wakiwa wanafunzi. Wanamgambo wa TTP walirekodi video za mauaji, mara nyingi wakitumia mbinu za kukata vichwa, kuwapiga risasi, au kuwachoma wahanga wao. Mauaji ya hadharani mara nyingi yalifanywa dhidi ya watu waliowashutumu kwa kushirikiana na serikali ya Pakistan au vikosi vya Marekani. Video za wanamgambo wakikata vichwa vya wanajeshi wa Pakistan.

Mashambulizi ya mabomu yaliyoonyeshwa moja kwa moja, yakionesha magari au majengo yakilipuliwa. Utekelezaji wa adhabu za kikatili kwa watu waliodaiwa kukiuka sheria za Kiislamu, kama vile kupigwa mawe au kuchapwa viboko. Mauaji ya kikatili na video zilileta hali ya hofu nchini Pakistan, hasa katika maeneo ya kaskazini magharibi.

Raia walikimbia maeneo yaliyodhibitiwa na TTP, na miji mingi iliharibiwa kutokana na mashambulizi ya vikosi vya serikali dhidi ya wanamgambo. Serikali ilianzisha operesheni za kijeshi kubwa, kama vile Operesheni Zarb-e-Azb (2014), kuwasambaratisha wanamgambo wa TTP. Hata hivyo, TTP waliendelea kufanya mashambulizi ya kujilipua na utekaji nyara.

TTP iliendelea kushirikiana na vikundi vingine vya kigaidi kama vile Al-Qaeda na ISIS, huku wakipokea msaada wa kifedha na silaha kutoka kwa wanachama wa mtandao wa kigaidi duniani kote.

TTP ilidhoofishwa sana na operesheni za kijeshi za Pakistan, lakini bado imeendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale. Katika miaka ya hivi karibuni, kikundi hiki kimejaribu kurudi kwa nguvu kwa kutumia propaganda mpya na kujiimarisha mpakani mwa Pakistan na Afghanistan.

Hali kama hii ilijitokeza pia kutoka maeneo kama Yemen, Somalia, na Syria, ambapo makundi kama Al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi ya Kiislamu yalikuwa yakifanya kazi. Walitumia video hizi kudai dhamana ya vitendo vyao, kuajiri wafuasi, na kueneza itikadi zao za kidini au kisiasa. Hapo jirani yetu Kenya kasumbuliwa sana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, tukio kubwa ni lile la chuo cha Garissa mashariki ya Kenya ambapo pia kuna mtanzania alikamatwa akishirikiana na kundi hilo la kigaidi

Madhumuni nyuma ya video hizi yalikuwa ya wazi. Kwa makundi haya, video zilikuwa zana za kigaidi na propaganda, kueneza hofu, kupata umakini wa kimataifa, na kuimarisha juhudi za kuajiri wapiganaji wa Jihad. Vilevile, zilikuwa taarifa za kisiasa, aina ya kisasi dhidi ya uchokozi wa Magharibi au uingiliaji katika nchi zenye Waislamu wengi.

Mwanzoni mwa miaka ya 2010, utengenezaji wa video hizi ulifikia viwango vipya na kuongezeka kwa kundi la ISIS (Islamic State of Iraq and Syria) ambalo chimbuko lake ni Al-Qaeda ya Iraq ambapo lilijitenga kutokana na utofauti wa mipango kazi na mitazamo. Kikundi hiki kilileta mbinu za uzalishaji wa video wa kisasa, kutengeneza video ambazo si tu zilikuwa za kikatili, lakini pia zililenga kuongeza athari zake za kisaikolojia katika kutia wasiwasi.

Ilijitangaza kuwa ni serikali inyoongozwa na Khalifah (kiongozi mkuu wa imani ya Kiislamu) mwaka 2014 chini ya uongozi wa Abu Bakr al-Baghdadi na ililenga kuanzisha utawala wa Kiislamu mkali katika eneo kubwa la Mashariki ya Kati. ISIS inafuata sheria kali za Uislamu wa Sunni, na kundi hilo halitambui mipaka ya Nchi, linataka kila mtu afuate sharia za Kiislamu. Udhibiti wake tangu hapo umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kampeni za kijeshi za mialiko ya kimataifa, ikijumuisha vikosi vya Marekani, Urusi, na nchi za ukanda huo kama vile Iraq na Syria.

Juhudi za serikali, mashirika ya habari, na majukwaa ya mitandao ya kijamii zimekuwa zikifanya kazi kupunguza usambazaji wa maudhui haya mtandaoni. Licha ya hayo, video za kipindi hicho ziliacha alama isiyofutika katika mitazamo ya kimataifa kuhusu ugaidi, na kubadilisha namna dunia inavyoelewa malengo na mbinu za makundi ya kigaidi.
 
2003-2025 mambo yashabadilikaaa duniaa inakimbizwaa Kasi Sanaa na new Genz...
 
Back
Top Bottom