TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 34
Na Steve B.S.M
Prado kubwa nyeusi isiyokuwa na plate number ilikuja na kusimama kando ya barabara, akatoka mwanaume mrefu, mbavu nene, amevalia miwani yenye glasi nyeupe, nywele kazilaza nyuma, mwili kauvesha suti kali rangi yake nyeusi ti, kuanzia shati mpaka tai yake vyote ni rangi nyeusi.
Bwana huyo mwenye asili ya uchina, kwa mwonekano wa macho yake, alikuwa anatafuna kijiti cha kuchokonolea meno yake madogomadogo huku sura ameikunja. Mwili wake mnene ulivyoshuka kwenye gari chombo hicho kilihema kwa kuutua mzigo, kikanyanyuka maradufu kikikaa katika mazingira yake halisi, alitengenezea koti lake akipandisha mabega kisha akaufuata uchochoro nyuma yake akifuatwa na vijana wawili, nao walivalia suti nyeusi lakini mashati yao yalikuwa meupe kwa rangi, vijana hao walipokuwa karibu na bwana huyu walionekana kama watoto kwa maumbo yao madogo.
Walitembea kidogo tu wakajikuta katika sehemu ile ambapo dhahma ilitokea muda si mrefu, eneo ambalo Mitchelle aliwamaliza wanaume kadhaa ndani ya muda usiozidi dakika moja, hapo wakasimama na kutazama maafa kwa macho ya hasidi, bwana yule mnene mwenye miraba minne akachuchumaa kumtazama kwa ukaribu mmoja wa mabwana wale ambao sasa wameshakuwa wafu, akamgeuza kwa mkono mmoja, maiti ikabinuka kama bua la muhindi, akaikagua aking'atang'ata kijiti chake mdomoni alafu akasimama na kupiga simu, kabla haijapokelewa akatokea bwana mmoja kutoka kwenye ile gari ilowaleta wale mabwana watano kuja kumvamia Mitchelle, bwana huyo alikuwa amevalia kombati jeusi lakini hakuwa na kinyago kama wale wenzake walouawa, bila shaka alikuwa ni dereva, hata mahali alipotokea katika gari hili palieleza hilo, uso wake umeparamiwa na hofu na punde tu alipotoka kwenye gari alimkimbilia bwana yule wa miraba minne na kumweleza namna gani walivyoangamizwa,
"Ilikuwa upesi sana! Hatukuwa na namna yoyote ya kujitetea ..." Wakati huo bwana yule mnene alikuwa anangojea simu ipokelewe, kidogo ikapokelewa, akaeleza yaliyojiri, sauti ya kwenye simu ikamuuliza,
"Kuna aliyebakia?"
Bwana yule wa miraba minne akamtazama bwana yule aliyemkuta katika eneo hili kisha akajibu hakuna aliyebakia, bwana yule aliyebakia akatahamaki kusikia hivyo, hofu ikampara mara mbili yake, akataka kujaribu kuongea lakini bwana yule wa miraba minne akamkatiza kwa kumwonyeshea kidole basi akanyamaza upesi.
"Inabidi twende kwenye mpango namba mbili," bwana wa kwenye simu alizungumza na kuagiza, "tekelezeni mpango huo sasa, lazima tufanikishe hili, hii ni nafasi yetu ya dhahabu." Alafu simu ikakata, bwana huyo mnene akairejesha simu yake mfukoni alafu akachomoa bunduki yake aliyoichomeka nyuma ya kiuno akamwonyeshea bwana huyu aliyebakia, akasema,
"Umesikia? Hamna aliyebaki!"
Kisha akamfyatulia risasi na kumwacha bwana huyo katika dimbwi zito la damu, risasi ilipenya na kutoboa fuvu lake kisha ikasambaratisha kabisa ubongo wake, akalala mfu.
***
"Karibu sana, madam," mwanaume aliyevalia suti nyekundu alimkarimu Mitchelle kwa tabasamu mwanana, mwanaume huyo alikuwa ni miongoni mwa wanaume lukuki waliokuwapo hapa kwaajili ya kuwakaribisha wageni, ukumbi ulikuwa unawakawaka kwa mataa ya rangi mbalimbali, waalikwa na wageni rasmi tayari wameanza kujisogeza wakiingia kila upande.
"Ahsante sana!" Mitchelle alimjibu bwana huyo huki akitabasamu kwa mbali kisha akaufuata mlango mmoja wa ukumbi huu, kulikuwa na milango mitano na kila mmojawapo ukiwa na mfumo mkali wa ulinzi, walisimama hapo wanaume waliovalia suti na vifaa vya mawasiliano masikioni, miongoni mwao walikuwapo wanaume walioshikilia vyombo maalum vya ku-scan wanaokatiza hapa, hapo kama una kifaa chochote chenye kutia walakini wa kiusalama basi vifaa hivyo vingelia ukazuiwa na walinzi.
Kama ilivyo kwa wengine, Mitchelle alikaguliwa mkoba wake kisha na yeye pia, hakukuwa na chaajabu hapa, alikatiza mlangoni lakini kabla hajaendelea ndani zaidi alitakiwa kupachika mikono yake miwili katika skrini fulani iliyounganishwa na mtambo wa utambuzi, hakutegemea hili, alisimama hapo akiitazama mashine hii mlinzi akamsihi afanye upesi,
"Weka mikono yako kwaajili ya 'fingerprint', ma'm."
Mitchelle hakuwa na namna, akajipachika mikono na mtambo ule ukasoma mikono yake, uliscan juu mpaka chini kisha chini mpaka juu, hamna kilichosoma, ikaendelea tena kuscan lakini hamna taarifa ilokuja, iliishia kuwasha taa nyekundu na kuandika 'unknown', yaani isiyofahamika, mlinzi akasogea karibu, akatazama, akagusagusa mashine hiyo na kumtaka Mitchelle arudie tena zoezi hilo, akafanya hivyo lakini bado hamna kitu kilichosoma, alama zake za vidole hazikuwa zinatambulika kabisa.
"Samahani sana, madam," akasema mlinzi, "nadhani itakuwa tatizo la mtandao," kisha akatabasamu kidogo kwa haya, "usijali, wewe nenda, hizi taarifa zimenakiliwa, mtandao utakapokuwa imara basi tutapata kuzitunza." Mitchelle akashukuru na kwenda zake, kwa mwendo wake wa madaha aliingia ukumbini na kunyookea moja kwa moja mahali maalum palipoandaliwa kwaajili ya watu waliokuwa wanauza mali zao katika mnada huu, alifika hapo kwa maelekezo ya 'ushers' waliokuwamo humu, kwa kibali alichokuwa nacho akaketi hapo na kukunja nne kiustaarabu akiusoma mchezo, kidogo tu, hazikupita hata sekunde kumi akaja mhudumu, alikuwa amevalia shati jeupe na 'bow tie' nyeusi kuendana na suruali yake ya kitambaa, mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea 'tray' yenye glasi kadhaa za vinywaji, akamuuliza Mitchelle nini angependa kutumia.
"Naomba whisky, tafadhali," Mitchelle aliagiza, mhudumu akamchagulia glasi mojawapo na kumpatia akisema, "karibu."
Mitchelle alitazama akaona 'tattoo' ndogo chini ya kiganja cha mhudumu huyu, ilikuwa ni picha ya ndege aina ya tai akiwa ameachama mbawa zake, hakujali sana, akabeba glasi yake na kuiweka mezani, hakutaka kuipeleka kinywani upesi, hakuwa na kiu kiasi hiko.
Kadiri muda ulivyoenda ndivyo na watu walivyokuwa wanazidi kuingia katika ukumbi huu, kama dakika ishirini mbele kukawa kumejaa pomoni, kila mtu amekaa katika nafasi yake, wanunuaji katika mahali pao na wauzaji pia vilevile, wahudumu wakawa 'busy' kwelikweli kuhudumia umati huu, wanazurura huku na kule wakibebelea trey zao za vinywaji, walinzi nao hawakuwa nyuma, walikuwa wanakatiza huku na kule kuhakikisha usalama upo.
Ukitazama kwa harakaharaka tu, haikuhitaji jicho la umakini, ukumbi ulikuwa umefurika watu wa kariba na asili tofautitofauti, wazungu walikuwapo hapa, waarabu, wahindi, wachina na hata watu wenye asili ya Afrika, watu hao kwa hadhi zao kubwa walikuwepo hapa kufanya biashara kubwa, kitambo kidogo bwana 'auctioneer', yaani mwendesha mnada akaingia akiwa amebebelea kipaza sauti, alikuwa ni bwana mmoja mfupi, amevalia suti ya kijani, nywele kazitengeneza vema na mwendo wake ni wa kitaaluma, akasalimu na pasipo kupoteza muda mnada ukaanza, mali ya kwanza iliweekwa sokoni watu wenye kuipenda wakaweka madau yao.
Kila kitu kilikuwa kinaonekana kwenye skrini kubwa ilokuwapo jukwaani, bidhaa inayonadiwa na pia mnadi mwenyewe hivyo kila mtu alikuwa na uwezo wa kuona kila kinachoendelea pasipo kujali yupo kona gani ya ukumbi, ikafuatia bidhaa ya pili, ikiwa inanadiwa mhudumu akamfuata Mitchelle baada ya kuona glasi yake ni tupu, alikuwa ni bwana mwingine sio yule aliyemhudumia hapo mwanzo, bwana huyu alikuwa na sura nyembamba yenye janja ndani yake, mwingi wa tabasamu na ushapu, hakuuliza, moja kwa moja akatoa glasi na kumpatia Mitchelle, Mitchelle akaipokea na kushukuru kwa tabasamu, mhudumu akaenda zake.
Kabla Mitchelle hajaweka kinywaji hiko mdomoni alipata kuhisi harufu yake, akatambua ilikuwa ni whisky, kidogo akasita, mhudumu yule alifahamu vipi kuwa anakunywa whisky kati ya vinywaji vyote vilivyokuwapo katika trey? Alijiuliza, aligeuka kutazama kando yake, mhudumu mwingine alikuwa anakatiza, akamwita kwa kichwa, mhudumu akasogea kumskiza, akamwagiza kinywaji bila kusema cha aina gani, wakati huo alikuwa ameficha glasi yake ya mwanzo alopewa, mhudumu akampatia glasi ya whisky, alimtazama mkono wake wa kuume akaona 'tattoo' ileile alokuwa nayo mhudumu wa kwanza, mchoro wa tai aliyeachia mbawa zake, hapa akapata walakini, lakini zaidi kilichompatia mawazo ni saa ya mhudumu huyo, saa hiyo ilikuwa katika mtindo wa 'stopwatch' ikihesabu dakika kushuka chini, kwa muda alotazama zilikuwa zimebakia dakika kumi na tano tu dakika hizo zikwishe.
Akatazama saa yake ya mkononi, akatazama ratiba ya mnada na kubaini baada ya dakika kumi na tano zifuatazo itakuwa ni zamu ya bidhaa yake kuwa sokoni kwaajili ya mnada, upesi akanyanyuka aende maliwatoni, alitembea kwa mwendo wa wastani, mwendo usoleta mashaka, alipotoka tu eneo lenye watu wengi kushika eneo tulivu akafungua pochi yake na kuchukua kitu humo, kitu alichokifichama na kiganja chake, alipoingia tu maliwatoni akafuata sinki na kutema kinywaji kilichomo mdomoni mwake kisha akakigusa na kijifaa kidogo cha chuma, kile kifaa alichokitoa kwenye pochi yake, mara kifaa hiko kikatoa sauti ndogo 'beep-beep, upesi akakirejesha katika pochi yake alafu akachana gauni lake kwa chini kutengeneza mpasuo mpaka pajani.
Alishatambua hamna usalama hapa, huu wote ulikuwa ni mtego, hakuelewa kwasababu gani lakini kwa mambo aloyaona na kuyakokotoa, hapa hapakuwa na usalama kuwapo, kuna kitu kikubwa kilikuwa kinafuatia, akahamishia mkoba wake mkono wa kuume alafu akaufuata mlango wa choo.
Kule ukumbini mhudumu mmoja alimfuata mwenzake akamnong'oneza sikioni,
"Hayupo."
Mwenzake akatupa macho yake kwenye kiti alichokuwa ameketi Mitchelle, kilikuwa kitupu, akatembea upesi kwenda hapo, alipofika akatazama chini akaona glasi zote za whisky alizoletewa mwanamke huyo, glasi hizo bado zilikuwa na kinywaji pomoni, ina maana hazikunyweka, upesi akatoa taarifa kwakupitia kifaa chake cha mawasiliano sikioni, wanaume wawili wa jeshi hili la wahudumu wakaelekea chooni haraka, walitazama chooni lakini hawakumwona mtu, wakafuata korido kusaka huku na kule, kidogo wakakutana na mwili wa mwenzao upo chini unavuja damu!
Mwili huo ulikuwa na majeraha kadha wa kadha ya kukatwakatwa na kitu cha ncha kali, na tukio halikutokea muda mrefu kwani bwana huyo aliyekatwa ndo' alikuwa akiishilia hapa, anarukaruka kama kuku aliyekatwa shingo.
"Code red!" Bwana akasema na kifaa chake cha mawasiliano, "Code red!" Akarudia tena kutoa taarifa wakiongeza mwendo kukimbia, kidogo wakapata taarifa kwamba kuna tukio limetokea katika ofisi ya mnada, haikupita muda wakawa wamefika huko, walikuta watu watatu wameuawa, wakapewa na taarifa kuwa mzigo wa Mitchelle ulishachukuliwa akiondoka pia na mizigo mingine ya thamani, mitatu kwa ujumla, na habari mbaya ni kwamba mwanamke huyo bado hakuwa amepatikana.
Mitchelle, akiwa amebebelea mizigo miwili mkononi, alitoka nje ya ukumbi huu kwa kupitia mlango wa dharura ya moto, alitembea kwa haraka akielekea kaskazini mwa ukumbi lakini kabla hajafika mbali simu yake ikaita kwenye mkoba, akajibana mahali apate kuitazama, namba mpya, akapokea na kuiweka sikioni,
"Boss," sauti ilisema kwenye simu, maramoja akaitambua sauti hiyo ni ya Jennifer, mwanamke anayemfanyia kazi nyumbani kule Marekani, akapigwa na butwaa, "Jennifer?"
"Ndio, ni mimi, boss."
Mara ikaongea sauti ya kiume, "ukitaka mwanamke huyu awe salama, rejea ukumbini."
"Wewe ni nani?" Mitchelle akafoka, kabla hajajibiwa akaisikia tena sauti nyingine ya kiume, mara hii aliitambua kuwa ya Dr. Lambert, akazidi kuduwaa.
"Utarudi, ama?" Sauti ngeni ikauliza, Mitchelle akajikuta akipatwa na kigugumizi cha kinywa.
****